Thailandi
Ripoti ya Kitabu-mwaka 1992
FRANK DEWAR alikuwa mwananchi wa New Zealand naye alifahamiana vema na misiba. Ingawaje alikuwa mmoja wa wale saba waliosafiri katika bahari kuu ya Pasifiki Kusini katika miaka ya katikati ya 1930 wakiwa katika mashua ndogo ya matanga ya meta 16 iliyoitwa Lightbearer. Kwa muda wa miaka sita iliyotangulia, alikuwa ametembea kwa miguu kotekote katika New Zealand na kusafiri juu ya mawimbi ya Australia, Tahiti, na Rarotonga, kimojawapo Visiwa Cook, akiwa na roho ya kimisionari yenye kuwaka. Alikuwa na ujumbe wa kuhubiri. Na lo! jinsi alivyohubiri juu ya Ufalme wa Mungu! Bila kutosheka na kueneza evanjeli katika Pasifiki ya Kusini, alikaza macho yake katika Siberia yenye baridi kali. Kwa hiyo, wakati wa Julai 1936—mwezi wenye joto lenye kutokeza mvuke ukiwa umeloweshwa na mvua ya pepo za monsuni—yeye, akiwa na umri wa miaka 27, alikuwa akifanya nini katika jiji geni la Bangkok, ambako hakujua hata nafsi moja na hakuweza kusema lugha ya huko?
Yeye na wenzake, mapainia wengine sita, au wahubiri wa wakati wote, walikuwa wameombwa na ofisi ya tawi ya Watch Tower Society katika Australia wateue nchi moja katika Mashariki ya Mbali iwe eneo lao la kutolea ushuhuda. Frank alichagua Siamu, inayoitwa sasa Thailandi, akifikiria ndipo mahali palipokaribia Urusi zaidi ya penginepo pote.
Kwa hiyo, kutoka Australia, Lightbearer, wakiwemo ndani mapainia hao saba wajasiri, ilitweka matanga kuelekea Singapore. Baada ya kuhubiri kwa muda katika Singapore na katika Kuala Lumpur, Maleya (ambayo sasa ni sehemu ya Malesia), Frank alipakia mali yake, akanunua tikiti, na akiwa na dola tano mfukoni mwake, akapanda garimoshi lililokuwa likienda Bangkok, ambako aliwasili Julai 22, 1936.
Safari ya garimoshi kwenda Bangkok ilikuwa ndefu na yenye kuchosha, yenye joto na jasho; makao yalikuwa yamesongamana watu, lakini kwa wazi Yehova Mungu alikuwa anamtunza kijana Frank—kwa kuwa kazi kubwa ilikuwa mbele yake. Hata hivyo, Frank siye aliyekuwa wa kwanza kuleta habari njema katika Siamu. Claude Goodman alikuwa ndiye wa kwanza.
Habari njema za Ufalme wa Mungu zilifika Thailandi kwa mara ya kwanza katika 1931, wakati Claude Goodman kutoka Uingereza alipotembelea Bangkok, mji mkuu. Alikuwa ameanza kupainia katika India katika 1929. Baada ya kufanya kazi katika Ceylon (sasa Sri Lanka), Burma (sasa Mianmari), na Maleya, alilazimika kungojea meli huko Penang iliyokuwa ikienda Calcutta, India. Akikomboa wakati huo wenye kufaa, alisafiri kwa garimoshi kwenda Bangkok na kuhubiri nyumba kwa nyumba huko kwa juma moja hivi, akiacha marundo ya vichapo vya Biblia vya Kiingereza kwa watu wenye kupendezwa. Claude hakujua hata kidogo jinsi ambavyo lingekuwa jambo gumu kudumisha kupendezwa miongoni mwa Wathailandi. Wao na nchi yao wakoje?
“Nchi ya Tabasamu”
Je! wewe umepata kusikia habari za “nchi ya tabasamu”? Pengine wewe una paka wa Siamu. Yawezekana umesikia habari za mapacha wa Siamu. Majina hayo yanahusianishwa na Ufalme wa Thailandi, nchi ya ajabu katika Asia ya Kusini-mashariki.
Ikipakana na Mianmari upande wa magharibi, Laos upande wa kaskazini na kaskazini-mashariki, Kambodia (Kampuchea) upande wa mashariki, na Malesia upande wa kusini, Thailandi ina ukubwa kama wa Ufaransa. Wakaaji wayo milioni 56 huonea shangwe halijoto ya kitropiki wakati wote wa mwaka. Ardhi kubwa yenye rutuba, hasa katika nyanda za kati, na hali zinazofaa kabisa kwa ukuzi huifanya ifae sana kwa kukuza mpunga (mchele). Maji yayo ya pwani ya kilometa zaidi ya 2,600 ya Ghuba ya Thailandi na Bahari Andaman, ambayo ni mkono wa Bahari Hindi, yanajaa viumbe hai vya majini.
India na hasa China zimekuwa na uvutano mwingi hapa. India ilieneza imani za Kihindu na Kibuddha toka upande mmoja hadi upande mwingine wa “nchi ya tabasamu” kwa njia ya wafanya biashara wayo. Lakini zaidi ya miaka elfu moja iliyopita, watu wa Thailandi walianza kuenea upande wa kusini kutoka China. Hivyo, wengi wa watu wa Thailandi waweza kufuatia ukoo wao kurudi nyuma mpaka kwa wale waliohama kutoka kusini mwa China.
Tangu 1939 jina rasmi la nchi hii limekuwa Thailandi, kuonyesha upendo wa uhuru walio nao watu wayo. Jinsi gani hivyo? “Thailandi” humaanisha “Nchi ya Walio Huru,” na ingawa nchi nyingi ambazo ni majirani wayo zilifanywa kuwa makoloni wakati wa karne zilizopita, Thailandi ilifaulu kudumisha kujitegemea kwayo kwa kisiasa. Walakini, uhuru wa aina nyingine, haukujulikana katika nchi hiyo kwa muda mrefu, mpaka Goodman na kisha Dewar walipowasili. Acheni tuone jinsi uhuru huo ulivyokua miongoni mwa wananchi wasio Wakristo wanaoishi katika nchi inayopatikana katika ‘sehemu ya mbali zaidi sana ya dunia.’—Mdo. 1:8, NW.
Mahali Palipo Mbali Sana Kidini
Tangu itokee ikiwa taifa katika karne ya 13, Thailandi imekuwa nchi yenye kufuata imani ya Buddha. Asilimia yapata 95 ya wananchi ni Wabudda, asilimia 4 ni Waislamu, na wanaopungua asilimia 1 wanadai kuwa Wakristo. Imani ya Buddha ya Thailandi ni ya tawi la Theravada, au Hinayana, nayo ni vumilivu sana kuelekea imani nyinginezo. Kwa sababu ya ile imani ya kwamba dini zote ni njema, mara nyingi watu wanazoea imani ya Buddha na ya Konfyushio wakati ule ule mmoja. Imani ya kwamba vitu vyote vya asili vina uhai wenye fahamu ingali imeimarika sana. Na imani ya Brahmani imeongezwa juu ya mazoea mengi ya Kibuddha.
Matokeo ya matendo ya wakati uliopita, au Karma, yanakubaliwa katika imani ya Buddha kuwa ndiyo yanayosababisha cheo cha mtu cha uhai wa sasa. Kwa kuwa falsafa ya Buddha haifikirii hata kidogo kuwako kwa mtu mwenye nguvu zipitazo za kibinadamu, hakuna wazo la kwamba kuna kutoa hesabu kwa mtu fulani aliye juu zaidi. Wabuddha wanajitegemea wenyewe ili kupata maarifa na nuru ya elimu. “Bwana Buddha,” kama Wathailandi wanavyomwita kwa kumpa heshima, hakufundisha juu ya Mungu wala hakukana kuwako kwake.
Kwa sababu ya mazingira ya kidini, Thailandi imekuwa kweli kweli mahali palipo mbali sana kwa habari za kweli za Biblia. Wamisionari wa Jumuiya ya Wakristo walianza kuwasili katika Thailandi katika karne za 16 na 17. Ingawa walijaribu kuwafahamisha watu Biblia, hawakuwasaidia ‘kujua kweli itakayowaweka huru.’ (Yn. 8:32) Ili kuipata ilikuwa lazima Wathailandi wangoje mpaka wakati fulani katika karne ya 20—wangojee watu kama Frank Dewar.
Ujumbe wa Uhuru Wafika Thailandi
Ile safari ya garimoshi ya kilometa 1,500 kutoka Kuala Lumpur kwenda Bangkok ilionekana ikichukua wakati mrefu sana kwa Ndugu Dewar. Aliketi wima kwa saa 36 ngumu sana katika behewa la daraja la tatu lililosongamana watu. “Nilikuwa hoi kutokana na majeraha niliyokuwa nimepata kutokana na aksidenti katika Kuala Lumpur miezi michache mapema kidogo,” akasema. “Lakini Yehova, kupitia malaika zake, aliniandalia.”
Kijana mmoja Mthailandi mwenye urafiki, mwana wa aliyekuwa hapo awali balozi Mthailandi kwenye Lile Kao la St. James katika Uingereza alikuwa akisafiri katika garimoshi ilo hilo. Alipopata kujua kusudi la Frank Dewar la kuja Thailandi na kwamba jumla ya pesa zake ni dola tano tu, alimtunza kwa fadhili kwa muda. Kwa njia hiyo, Frank akaweza kujitegemea katika hiyo nchi mpya.
Frank alianza kufanya kazi mara moja akieneza ujumbe wenye msingi wa Biblia wa uhuru wa kiroho, na kwa muda uliobaki wa mwaka huo, alihubiri sana katika sehemu za kibiashara na za makao ya jiji hilo, akikaza fikira kwa wananchi wenye kusema Kiingereza na Kichina. Hakukuwa na vichapo vya Biblia vilivyopatikana bado katika Kithai.
Mapainia Zaidi wa Kigeni Wajiunga
Baadaye, akiwa safarini katika Maleya, Frank alikutana na painia Mjerumani mrefu mwenye uchangamfu, Willy Unglaube, kutoka Königsberg katika Prussia Mashariki, wakati huo ikiwa sehemu ya Ujerumani. Akiwa painia mwenye bidii na mwenye nia ya kujasiria, Willy alikuwa tayari amehubiri katika nchi kadhaa, kutia na Ufaransa, Algeria, na Hispania, na katika kisiwa cha Korsika. Kwenye mkusanyiko katika Lucerne, Uswisi, katika 1936, Joseph F. Rutherford, wakati huo akiwa msimamizi wa Watch Tower Society, alidokeza kwa Willy na mwenzake, Kurt Gruber, kwamba kwa sababu ya vita ya kiraia iliyokuwa inachacha katika Hispania, ingewafaa zaidi wakihubiri mahali penginepo. Walichunguza-chunguza Kitabu cha Mwaka ili waone walikohitajiwa mapainia nao wakachagua Singapore, Maleya, na Thailandi. Hivyo Frank Dewar aliporudi Thailandi mapema katika 1937, Willy Unglaube aliandamana naye. Hata hivyo, Kurt Gruber alibaki Maleya.
Katika 1938 John Edward (Ted) Sewell, painia kijana wa Australia alijiunga na mapainia hawa wawili wenye kufanya kazi kwa bidii katika Thailandi. Ted alikuwa mpya kidogo katika kweli, akiwa amebatizwa kwa muda wa miaka miwili tu. Lakini kwenye kusanyiko katika Sydney katika 1938, wakati Ndugu Rutherford alipowaomba akina ndugu wakatumikie katika nchi za Mashariki ya Mbali, Ted hakusita kufanya uamuzi. Kama ilivyokuwa kwa mapainia wengi wa mapema, mara hiyo akasema: “Mimi hapa, nitume mimi.”—Isa. 6:8.
Katika Septemba 1939, alipokuwa akihubiri katika Penang, Maleya, Kurt Gruber aliambiwa na ofisa wa polisi mwenye urafiki kwamba Uingereza ilikuwa imetangaza vita juu ya Ujerumani na kwamba raia wote wa Ujerumani wanaopatikana katika maeneo ya Uingereza watazuiliwa wakati wa kipindi cha vita. Alimshauri Ndugu Gruber aondoke Maleya mara moja. Kurt aliruka ndani ya gari lake, akapiga mbio kwenda katika makao yake kuchukua mali yake ya kibinafsi na, akisaidiwa na yule ofisa, alipita vituo vya ukaguzi bila matata. Alifaulu kulipia nauli katika meli ya Kichina iliyokuwa ikienda Bangkok, gari lake likiwa limefichwa chini ya rundo la nazi. Shangwe ilikuwa kubwa ya kuwa na mapainia wanne sasa katika lile shamba kubwa katika Thailandi!
Kupainia na Kunguni
Kuhubiri habari njema hakukuwa rahisi kwa vyoyote. Ijapokuwa kwa ujumla Wathailandi ni watu wenye fadhili na wenye ukaribishaji wageni sana, katika enzi hiyo ya kabla ya utalii, ni wachache sana waliokuwa wameonana na watu wa kutoka nje. Kwa hiyo, hawakuelekea kuwa wenye urafiki kwa watu wa kigeni. Kizuizi cha lugha kilifanya tatizo hilo kuwa gumu zaidi, kwa kuwa mapainia hao waliweza kusema Kithai kidogo sana. Vichapo walivyotoa vilikuwa vigeni si katika habari iliyokuwamo tu bali pia katika lugha.
Juu ya yote hayo, vizuizi vilivyosababishwa na mazingira ya kidini na njia ya kufikiri ya watu ilitokeza matatizo zaidi. Wakiwa wanatosheka na dini yao yenye kuvumilia dini nyinginezo na yenye kuwafaa, kwa kawaida Wathailandi hawawi wakitafuta kitu fulani kilicho bora zaidi, wala hawawi na tamaa ya Mesiya alete ukombozi.
Hali huko ziliwataka pia mapainia watosheke na vitu vichache sana vya kimwili na kwamba waendelee wakiwa na vitu vichache zaidi vyenye kufaa kuliko hapo awali. Wakilazimika kujitafutia riziki, mapainia hao wenye kuhama-hama hawangeweza kugharimia makao kama yale watu wengine wa kigeni waliokuwa huko ili kufanya biashara walifurahia kuwa nayo. Alipowasili katika mji mpya, painia alikuwa akikaa katika hoteli isiyo ghali, ambayo katika visa vilivyo vingi, iliendeshwa na Wachina. Frank Dewar akumbuka hivi:
“Kwenye kituo cha reli au kituo cha mwisho cha basi au cha mashua, nilikuwa nikikodi riksho moja kwa ajili yangu mwenyewe na nyingine ichukue vibweta kadhaa vya vitabu. Labda kwa satang 25 (senti 10 [za U.S.] hivi wakati ule), riksho hizo zilikuwa zikinipeleka kwenye hoteli ndogo, ambapo nilikuwa nikimwendea karani na kuhamia humo. Karani alikuwa akinipa taa ndogo yenye kutumia mafuta ya taa na kumwambia mvulana mwenye kutunza vyumba anipeleke chumbani. Mvulana alikuwa akinionyesha chumba kimoja, na kunipa taulo ndogo, na kuniambia kilipo choo na bafu. Mvulana akiisha kuondoka, nilikuwa nikimwaga mafuta yaliyomo ndani ya taa juu ya kitanda kufukuza kunguni chungu nzima, [kisha] nilikuwa nikihakikisha kwamba taa imejazwa mafuta tena, na kuoga, kula, kusoma kidogo, na hatimaye kuingia chini ya wavu wa kuzuia mbu na kutoa jasho mpaka nilalapo usingizi katika chumba hicho kidogo, kisicho na hewa.”
Kusafiri katika siku hizo kulikuwa na tabia yake pia. Akieleza safari ya garimoshi kutoka Bangkok kwenda katika jiji la kaskazini la Chiang Mai, painia mmoja alisema hivi: “[Sisi] tulilazimika kusimama usiku kucha katika jukwaa [la behewa] kwa sababu hakukuwa na inchi moja ya mraba iliyobaki kwa nafasi ya kuketi; isitoshe, hata vijia [vya garimoshi] vilijaa mifuko na vikapu, baadhi yavyo vikiwa na mabata na kuku, na watu walikuwa wanachuchumaa juu ya hivyo pia. Garimoshi lilipoendelea mbele kuelekea kaskazini tulinyunyiziwa maji kwenye kila kituo, kwa kuwa ulikuwa wakati wa sherehe ya kurusha maji, ambayo Wasiami walishangilia sana. Kusafiri katika wilaya za mashambani kunafanywa kwa basi katika majira ya ukame; hayo nayo, tulipata kwamba, sikuzote yalisongamana watu na mifugo. Au nyakati fulani sisi sote tulilazimika kushuka huku mzigo wa mchele ukipandishwa ndani, kisha ilikuwa lazima tupande tena vizuri kadiri tulivyoweza na kutumia kadiri tulivyoweza nafasi iliyopatikana.”
Sala za Kupata Mtafsiri Zajibiwa
Wakati wa miaka hiyo michache ya kwanza, mbegu nyingi za kweli ya Ufalme zilipandwa katika shamba la Thailandi katika mji mkuu na pia katika mikoa. Alipokuwa akifanya kazi kwa miezi minne hivi katika miji ya kaskazini, Ndugu Dewar aliweza kuangusha vitabu na vijitabu 2,491. Wakati wa mwaka wa utumishi wa 1939, hao mapainia watatu waliangusha jumla ya vitabu vilivyojalidiwa 4,067 na vijitabu 14,592 na wakapata maandikisho 113. Hata hivyo, vichapo hivi vyote, vilikuwa ama katika Kiingereza, Kichina, au Kijapani. Hakukuwa vichapo vilivyopatikana bado katika lugha ya wenyeji isipokuwa kijitabu Protection, kilichokuwa kimetafsiriwa katika Kithai na mwanafunzi mmoja kwa kubadilishana na vitabu kadhaa vya Kiingereza.
Mapainia waliona uhitaji mkubwa mno wa mtafsiri—mtu aliyekuwa mtumishi wa Yehova aliye wakfu na kubatizwa na ambaye angekuwa na tamaa yenye juhudi ya kufanya kweli zenye thamani kuhusu Yeye na Ufalme Wake zipatikane kwa watu wa Thailandi. Ndugu Unglaube alimwandikia Ndugu Rutherford, akitaarifu kwamba hawakuwa na mtafsiri. Ndugu Rutherford alijibu: “Mimi siko Thailandi; nyinyi mko huko. Iweni na imani katika Yehova na mfanye kazi kwa bidii yenye kuendelea, nanyi mtapata mtafsiri.” Mapainia hao walikuwa na imani nao walistahimili. Yehova hakuwakatisha tamaa.
Wakati wa Desemba 1939, Kurt Gruber na Willy Unglaube walifunga safari kwenda Chiang Mai, ambako walimpata mtafsiri waliyekuwa wakisali wampate—Chomchai Inthaphan. Wakati ule, alikuwa mwalimu mkuu wa Shule ya Wasichana ya Kipresbiteri. Akiwa amesomea Chuo Kikuu cha Manila katika Ufilipino, mwanamke huyo alikuwa ameelimishwa vizuri katika Kithai na Kiingereza. Akiwa pia na upendo wenye kina kwa Mungu na akiwa mwenye bidii kumtumikia, alitambua upesi kwamba yale waliyohubiri mapainia hao wawili ilikuwa ndiyo kweli.
Ujapokuwa upinzani kutoka kwa wamisionari Wapresbiteri na matoleo yenye kushawishi kutoka kwa shule, Chomchai alitoa barua ya kujiuzulu na kuwajulisha kwamba anaacha kanisa.a Alipokuwa angali anafanya kazi shuleni, akiendelea huko mpaka mwisho wa mwaka, alianza kutafsiri kitabu Salvation. Baadaye, wakati ofisi ya tawi ilipoanzishwa katika Bangkok, Chomchai akawa mmoja wa wale washiriki wa kwanza wa familia ya Betheli. Kwa miaka mingi Chomchai alifanya kazi yote ya kutafsiri. Akiwa mpenda paka, alikuja pia na paka wake wa Kisiami kwenye Betheli. Ingawa alipatwa na magonjwa kadhaa yenye kulemaza wakati wa miaka kumi ya mwisho ya maisha yake, yeye aliendelea kuwa mwaminifu katika utumishi wake wa wakfu mpaka kifo chake katika 1981 akiwa na umri wa miaka 73.
Wahubiri wa Kwanza Wenyeji
Yaonekana kwamba kabla ya kufika Chiang Mai katika Desemba 1939, Ndugu Gruber na Unglaube walifanya kazi katika miji ya kaskazini ya Phrae na Nan. Katika Phrae mwuguzi mmoja alipata vijitabu Home and Happiness na Protection naye akampa rafiki yake Buakhieo Nantha, ambaye alikuwa mwuguzi katika Nan, na akamwambia kwamba watu hao wawili wa kigeni wangekuja Nan muda mfupi baadaye. Ingawa Buakhieo alilelewa akiwa Mbuddha, alikuwa amekuwa Mpresbiteri miaka miwili mapema, baada ya kujifunza katika shule ya bweni ya Kipresbiteri na kupata mazoezi ya uuguzi katika hospitali ya kanisa katika Chiang Mai. Alisoma vile vijitabu viwili kwa kupendezwa sana. Kwa hiyo kufikia wakati wale mapainia wawili walipokuja Nan, alikuwa tayari kujifunza Biblia.
Buakhieo alipotumwa Chiang Mai kwa mazoezi zaidi, alikutana na Kurt na Willy kwa mara nyingine tena, ambao kufikia wakati huo walikuwa wakifanya mikutano kwa ukawaida na kikundi cha watu wenye kupendezwa. Chomchai alikuwa amewajulisha mapainia hao kwa mwalimu mkuu wa seminari ya Kipresbiteri, Kham-ai Chaiwan. Baada ya kuzungumza habari juu ya Utatu, moto wa mateso, na nafsi, alitambua kwamba Mashahidi wa Yehova walikuwa wakifundisha kweli aliyokuwa akitafuta. Aliwahurumia Kurt na Willy naye akawaalika waondoke hotelini wahamie katika nyumba yake. Alifanya maendeleo mazuri katika kweli. Alipotiwa chini ya mkazo na mwajiri wake aache kushikamana na kanuni za Biblia, hangeweza kuondoshwa, ijapokuwa hiyo ilimaanisha kupoteza kazi yake na malipo ya uzeeni aliyoahidiwa.
Baada ya miaka minne ya kazi ngumu, jitihada za hao mapainia wanne wa kigeni zilianza kuzaa tunda. Katika 1940 Buakhieo Nantha, Chomchai Inthaphan, Kaeomalun dada wa kimwili wa Chomchai, na Kham-ai Chaiwan na mke wake, Buakhieo, walibatizwa wakiwa Mashahidi wa Yehova wa kwanza wenyeji katika Thailandi.
Kutoka Mtu wa Ukoo Hadi Mtu wa Ukoo
Kama vile wafuasi wa mapema wa Yesu walivyokuwa na hamu ya kuwaambia watu wa ukoo wao habari za kuwa wamempata Mesiya, ndivyo wanafunzi hao wapya hawakusita kuhubiri habari njema kwa familia zao na marafiki wao. (Linganisha Yohana 1:41.) Ndugu Kham-ai alikuwa na mtu wa ukoo, Kham Raksat, ambaye alikuwa mzee wa kanisa katika San Kamphaeng, si mbali na Chiang Mai; kwa kweli, yeye alikuwa amejenga kanisa hilo. Kham, kama Kham-ai, alikuwa mwanamume mwenye moyo mweupe, akitafuta kweli. Aliwaalika Kurt, Chomchai, na dada yake Kaeomalun kwenye kanisa lake wahubiri na kueleza Biblia. Wakikasirishwa na jambo hilo, wamisionari Wapresbiteri waliagiza baadhi ya walimu wawafukuzie mbali Mashahidi hao. Hata hivyo mwenendo huo usio wa Kikristo, ulifanya Kham aazimie hata zaidi kuendelea kujifunza Biblia na Mashahidi. Miaka kadhaa baadaye, kundi lilianzishwa katika San Kamphaeng. Kham akawa mwangalizi msimamizi, naye kwa kuona fahari akaweka kwenye nyumba yake ishara hii, “Jumba la Ufalme la Mashahidi wa Yehova.” Katika miaka ya baadaye washiriki wengi wa familia za Chaiwan na Raksat walikuja katika kweli.
Ilikuwa ni baada ya mazungumzo marefu na yenye kina kwamba Chomchai na Kaeomalun waliweza kumsadikisha mama yao juu ya kweli. Yeye, kama Mashahidi wengine wote wa mapema katika Thailandi, alikuwa Mkristo kwa jina tu, naye alikuwa mtendaji sana katika kanisa la kwao katika Ban Paen, kilometa zapata 30 kusini mwa Chiang Mai. Kuacha kanisa kwake kulitokeza msukosuko fulani katika kijiji. Lakini kuazimia kwake na ujasiri vilikuwa na matokeo mazuri wakati watu kadhaa katika kijiji hicho walipokubali kweli, na baada ya wakati kundi likaundwa.
Kutoka kwa mama ya Chomchai, kweli ilienea kwa familia ya binamu wa Chomchai katika Chom Thong, wilaya moja katika mkoa wa Chiang Mai, ambako kikundi kingine cha Mashahidi kiliundwa baadaye.
Kwa hiyo wale wa kwanza kuitikia ifaavyo kuhubiriwa kwa habari njema katika Thailandi, hasa katika sehemu ya kaskazini ya nchi, ambako kulikuwa na vikundi vya Kiprotestanti katika miji na vijiji kadhaa, walikuwa watu wenye malezi ya Ukristo wa jina tu. Ingechukua wakati fulani bado kabla Mbuddha wa kwanza hajakubali kweli ya Biblia.
Kazi Yaendelea Ijapokuwa Vita ya Ulimwengu ya 2
Kwa kuwa Thailandi ilidumisha kutokuwamo wakati wa sehemu ya kwanza ya Vita ya Ulimwengu ya 2, mapainia wa kigeni na wahubiri wenyeji waliweza kuendelea na kazi yao ya kuhubiri bila kuzuiwa. Wakati Kurt Gruber na Willy Unglaube walipokuwa wakipata mambo hayo yenye kusisimua katika mikoa ya kaskazini, Ted Sewell aliendelea kukaa katika mji mkuu, ambako familia moja ya asili ya Sri Lanka yenye kupendezwa walijiunga naye katika kazi ya kutoa ushuhuda. Katika 1941, wakati Dada Chomchai alipohamia Bangkok, familia hiyo walimpokea kwa fadhili katika makao yao. Pole kwa pole, wengine, sana-sana Wachina, walionyesha kupendezwa, na kundi likaundwa kitengenezo.
Edith Mungsin, sasa akiwa katika miaka yake ya 80, angali akumbuka alivyokutana na kundi katika Bangkok kwa mara ya kwanza: “Nilipata kuona Biblia katika shule ya Kiprotestanti. Baada ya kifo cha baba yetu Mwingereza wakati wa vita ya ulimwengu ya kwanza, dada zangu watatu nami tulitumwa katika shule ya bweni ya Kiprotestanti katika Chiang Mai, ambako tulikuwa na masomo ya Biblia pia. Kwa hiyo nilijifunza habari za historia ya Yesu Kristo tokea utoto, na upendo na heshima yenye kina kirefu kwake vilitia mizizi katika moyo wangu. Hata hivyo, maswali kadhaa juu ya Biblia yalikaa bila kujibiwa, kwa kuwa nilikuwa mwenye haya sana nisiweze kumwuliza mtu yeyote, na sisi wanafunzi tuliwaogopa walimu. Baadaye, niliishi kwa muda mfupi katika Singapore na kisha nikarudi Thailandi katika 1941. Nilipokuwa safarini kwenda Chiang Mai, nilimtembelea Kham-ai Chaiwan pia, ambaye nilijua alikuwa kiongozi miongoni mwa jamii ya Kipresbiteri huko. Kwa kuwa nilikuwa na haraka ya kuchukua garimoshi kwenda Bangkok siku hiyo, ilikuwa vigumu kwake kunitolea ushuhuda. Hata hivyo alinipa vijitabu vitatu na kunihimiza nivisome.
“Katika garimoshi, nilivitoa kwa haraka vile vijitabu na kuvisoma toka jalada hata jalada. Nilisisimuka kwa maelezo ya mafundisho ya Biblia na wakati ule ule nikashuka kwa sababu habari hiyo ilikuwa tofauti sana na vile tulivyokuwa tumefundishwa katika shule. Nikitaka kujua kweli ilikuwa nini, nilitafuta Mashahidi wa Yehova katika Bangkok. Nilipopata mahali pa mikutano yao, ndipo funzo la Biblia lilipokuwa linaendelea. Kwa hiyo niliketi na kujiunga nao. Mmojawapo wa hao 12 waliokusanyika nilimjua vizuri sana—Chomchai, ambaye alikuwa amekuwa mwalimu katika ile shule niliyokuwa nimehudhuria; tulifurahi sana kukutana tena.
“Kwa sababu ya maarifa yangu na uelewevu wa Biblia wenye kuongezeka niliacha kwenda kanisani. Pia niliondoa msalaba shingoni pangu. Wazee wawili wa kanisa walinitembelea nyumbani kwangu wakajaribu kunifanya nirudi kanisani, wakiniambia: ‘Usiwaamini hao mashahidi bandia!’ Niliwaambia, ‘Acheni nijifunze Biblia na kuhakikisha kwanza. Ikiwa Mashahidi wa Yehova wanakosea, nitarudi katika kanisa lenu.’ Hawakurudi kamwe.”
Uvamizi wa Japani Watokeza Magumu
Vita ya Ulimwengu ya 2 ilipoendelea kuchacha nayo Japani ikapanua uvutano wayo katika Asia na maeneo ya Pasifiki, hatimaye Thailandi ilihisi mchomo wa vita. George Powell, Mwaustralia aliyekuwa ametunza bohari la vichapo vya Sosaiti katika Singapore kabla kazi haijapigwa marufuku huko na ambaye wakati huo alihamia Thailandi, hukumbuka jinsi, asubuhi moja katika Desemba 1941, Dada Chomchai alivyokuja akikimbia kuteremka chini ya ngazi, akipaaza sauti, “Imetukia!” Ndiyo, tangazo lilikuwa ndipo tu limetolewa katika redio kwamba Wajapani walikuwa wameanza kupiga miguu kuingia Thailandi. Ingawa majeshi ya Japani hayakuingilia sana maisha ya kila siku ya watu wenyeji, hali za kiuchumi ziliharibika. (Lile daraja lenye sifa mbaya juu ya mto Kwai [Khwae Noi] na ile “njia ya reli ya kifo” vilijengwa na wafungwa wa vita wa kigeni.) Na kukaliwa kwa nchi na serikali ambayo ilikuwa rafiki ya Ujerumani wa Nazi hakika kungekuwa na matokeo mabaya juu ya kazi ya kuhubiri ya Mashahidi.
Katika 1941, baada ya kuwa wametumikia katika Netherlands East Indies (sasa Indonesia), mapainia wawili Wajerumani, Hans Thomas na Wolfhelm Fuchs, walipewa mgawo mpya kwenda katika Thailandi ambayo ilikuwa ingali inadumisha kutokuwamo kwayo. Hata hivyo, baada ya uvamizi wa Japani kuanza, mapainia wote wa kigeni walipatwa na magumu katika kazi yao ya kuhubiri ama kwa sababu walikuwa raia wa nchi ambazo Japani na rafiki yake Ujerumani zilikuwa zikipigana vita nazo au kwa sababu walikuwa raia wa rafiki ya Japani ambayo ilipinga vikali Mashahidi wa Yehova. Katika Japani yenyewe kazi ya Mashahidi ilikuwa tayari imepigwa marufuku kwa miaka kadhaa.
Si siku nyingi baada ya uvamizi, wenye mamlaka Wajapani waliagiza polisi wa Thailandi wakamate George Powell na Ted Sewell na kuwaweka katika kambi ya mateka katika Bangkok kwa muda uliobaki wa vita wa miaka mitatu na miezi minane. Katika 1942 Wajerumani Kurt Gruber, Hans Thomas, na Wolfhelm Fuchs walikamatwa, na vichapo katika bohari vikatwaliwa. Willy Unglaube aliponyoka kukamatwa, kwa kuwa alikuwa sehemu za mashambani wakati ule. Ingawa wenye mamlaka Wajapani walijaribu sana kumpata, aliepa kukamatwa muda wote wa vita.
Kwa sehemu iliyo kubwa, wahubiri wenyeji, waliachwa bila kupatwa na madhara. Hata hivyo, walipohubiri nyumba kwa nyumba, hasa katika Bangkok, polisi Wajapani wenye mavazi ya kiraia waliwafuata-fuata. Mara nyingi, baada ya wahubiri kutoka katika nyumba, wanaume hao walikuwa wakienda ndani na kuhoji-hoji, na nyakati nyingine hata kutisha, wenye nyumba.
Kisa kimoja kilitokea wakati akina Dada Chomchai na Buakhieo walipokuwa wakihubiri katika mji wa kaskazini wa Nan. Polisi walipekua-pekua mikoba yao na kisha wakawapeleka akina dada hao katika kituo cha polisi. Hata mzee wa kanisa mwenyeji, Duangkaeo Jarityonphan, ambaye walikuwa wamekuwa na mazungumzo kadhaa naye, alikamatwa. Chomchai na Buakhieo waliwekwa kizuizini na polisi kwa siku nyingi kabla ya kesi yao kutatuliwa. Yaonekana walikuwa wameshtakiwa kibandia na padri wa Roma Katoliki ambaye hakupenda kutoa ushuhuda kwao kuwa walikuwa waungaji mkono adui wa siri. Ebu tutaje kwamba, Duangkaeo, yule mzee wa kanisa, hatimaye alikuja katika kweli.
Wakatiliwa Mbali—Lakini Watunzwa
Baada ya kukamatwa kwao, wale Wajerumani watatu mapainia walizuiliwa na wanajeshi Wajapani. Mahoji yasiyokoma, pamoja na mapigo ya kikatili, yaliendelea kwa siku tatu usiku na mchana. Maofisa hao waliwaambia watie sahihi taarifa katika Kijapani, ambayo hawangetafsiri. Ndugu walipokataa, ofisa mmoja alipaaza sauti kwa hasira, “Sisi hatujali mnayosema juu ya Ufalme wa mbinguni, lakini hapa duniani Wajapani watatawala!”
Hans Thomas husimulia hivi: “Kwa kuwa sisi hatukuwa Wanazi, ubalozi wa Ujerumani haukutufanyia lolote. Kwa kweli, tuliambiwa, ‘Mwajua vile mngalitendewa katika Ujerumani!’ Mwishowe, baada ya kuwa tumezuiwa na wanajeshi kwa majuma mengi, tuliwaomba wenye mamlaka Wathailandi tafadhali wafanye jambo fulani kwa niaba yetu. Vyovyote iwavyo, tulikuwa tumehamia Thailandi kihalali ili kuendesha kazi yetu ya kimisionari kwa ruhusa ya serikali. Na kwa kuwa hatukuwa tumefanya lolote dhidi ya serikali ya Thailandi, hatukuona sababu kwa nini wenye mamlaka wa kijeshi Wajapani watuweka kizuizini. Kwa kuwa Thailandi ilijulikana kuwa nchi ya watu huru na haikuwa chini ya utawala wa Kijapani kisheria bali ilikuwa tu katika mapatano ya kirafiki na Japani, tuliomba tukabidhiwe kwa wenye mamlaka Wathailandi. Mwishowe ombi letu lilikubaliwa.”
Mapainia hao walipelekwa kwenye ofisi za CID (Central Investigation Department [Makao Makuu ya Idara ya Upelelezi]) katika Bangkok wakawekwa humo. Ndugu wenyeji wangeweza kuwatembelea na kuwapa mahitaji yao ya kila siku yaliyo ya lazima kwa maisha. Walipokuwa kwenye CID, ripoti moja ilipokewa juu ya kesi ya wale dada waliokuwa wamekamatwa katika Nan. Yule ofisa msimamizi alikuwa pia anashughulikia kesi ya wale ndugu Wajerumani. Aliposoma ripoti hiyo kutoka Nan, alisema, “Lo! Chomchai! Mnara wa Mlinzi! Nawajua watu hao. Wao si hatari.” Ujumbe ulipelekwa Nan Mashahidi hao waachiliwe na kesi yao iachwe. Muda mfupi baada ya hapo, Kurt, Hans, na Wolfhelm, waliachiliwa huru pia. Kwa tukio zuri, Ofisa huyo alikuwa amekuja wakati uliopita kwenye nyumba ya akina ndugu katika Bangkok kujifunza Biblia.
Wale mapainia Wajerumani walitunzwa pia katika njia nyingine. Wakiwa wamekatiliwa mbali kabisa na mawasiliano yote na tengenezo la Yehova katika nchi za ng’ambo, walikuwa, kana kwamba, wameachwa peke yao. Wakati ule ule, ilikuwa lazima wawe waangalifu sana ili waepuke kukamatwa na wenye mamlaka Wajapani. Miezi kadhaa kabla ya uvamizi wa Japani, mapainia hao walikuwa wameongoza funzo la Biblia na msimamizi wa kampuni ya Kiswisi ya kuingiza na kutoa bidhaa nchini. Mwanamume huyo mwenye urafiki alikuja sasa kuwasaidia akina ndugu, akawaajiri kazi wawe wauzaji wa bidhaa za kuandikia na kuwalipa kulingana na kiasi cha bidhaa walizouza. Namna hii ya kazi iliwafaa sana. Waliweza si kugharimia mahitaji yao ya kila siku tu bali pia waliweza kuweka akiba ya pesa za kutosha kuchapisha vijitabu nchini ili kuongezea akiba yao ya vichapo iliyokuwa ikipungua sana. Na wakati ilipoonekana kuwa matata yaelekea kutokea katika eneo, sikuzote waliweza kuchomoa bidhaa za kuandikia kutoka ndani ya mikoba yao mikubwa.
Wale mapainia wawili Waaustralia waliokuwa katika kambi ya mateka hata wao ‘hawakuachwa bila msaada.’ (2 Kor. 4:9, HNWW) George Powell asema: “Ndugu zetu waaminifu Wajerumani na akina dada Wathailandi hawakutuacha kamwe bila kutusaidia wakati wa siku hizo zenye mashaka. Tunda waliloleta lilifurahiwa sana sana, lakini badilishano la kitia-moyo pamoja nao lilikuwa jambo lenye kuburudisha hata zaidi ambalo lilifanya maisha zetu zivumilike na zijawe na tumaini.”
Akina ndugu walifanya nini baada ya Japani kukatilia mbali chakula chote cha kiroho baada ya kukalia nchi? Waliendelea kuwa na mikutano ya kawaida, kutia na Funzo la Mnara wa Mlinzi. Wakati haikuwezekana tena kupata matoleo mapya ya Mnara wa Mlinzi, walianza kutumia yale ya awali kidogo, kwa utaratibu wa kinyume-nyume. “Mnara wa Mlinzi wa Novemba 1941, wenye makala ‘Utawala wa Mashetani Waisha,’ ndilo lililokuwa toleo la mwisho tulilopokea,” akumbuka Ndugu Thomas. “Kuanzia na toleo hilo tulijifunza kurudi nyuma mwaka kwa mwaka, tukitumaini kwamba siku moja vita ingekoma nasi tungeweza kuwasiliana na Sosaiti. Zaidi ya miaka minne mirefu ilipita. Tulikuwa tunaendelea kujifunza Mnara wa Mlinzi wa 1936 wakati matoleo mapya ya magazeti yalipoanza kuwasili.”
Kutiwa Nguvu kwa Ajili ya Utendaji wa Baada ya Vita
Katika Novemba 24, 1945, karibu siku ile ile miaka minne baada ya mawasiliano kukatishwa, simu ilipokewa kutoka ofisi ya msimamizi wa Sosaiti katika Brooklyn, U.S.A., ikiwaarifu akina ndugu kwamba kazi ya ulimwenguni pote ya kutoa ushuhuda ilikuwa kubwa sasa kuliko ilivyopata kuwa hapo awali. Baada ya Japani kukubali kushindwa katika Agosti na kisha kuachiliwa kwa Ndugu Powell na Sewell, mipango ilifanywa kuihamisha bohari la vichapo iwe katika mahali penye kufaa zaidi na ambapo palikuwa pakubwa vya kutosha kufanyia mikutano. Kwa msaada wa maofisa Wathailandi, mahali palikodiwa katika Soi Decho, kando ya Silom Road.
Kabla na wakati wa vita, wale mapainia walikuwa na shughuli nyingi wakipanda mbegu za kweli, hivi kwamba sasa kulikuwako kiini cha watu wenye kupendezwa. Hivyo, wakati wa 1946 iliwafaa sana ndugu kupokea vichapo walivyopelekewa Theocratic Aid to Kingdom Publishers, Kitabu cha Mwaka, na Organization Instructions. Mapainia hao walisoma kwa hamu nyingi misaada hiyo yenye thamani sana ili ‘wapate habari ya karibuni zaidi,’ na ili wapitishe habari hiyo mpya kwa washirika wao wenye kupendezwa. Watu kadhaa wapya wenye kupendezwa walikuwa wameanza kuhubiri, lakini bado walihitaji kupata uthamini kamili zaidi wa tengenezo la kitheokrasi.
Mapainia hao walijitumikisha kwa bidii yenye kuendelea katika kueneza habari njema kwa njia ya akiba hii mpya ya vichapo. Hivyo, wakati wa mwaka wa utumishi wa 1946, kikundi hicho cha wahubiri 14 na mapainia waliangusha vitabu na vijitabu 14,183 na wakaanza mafunzo ya Biblia mapya 47. Lo, ni jambo kubwa kama nini lililotimizwa na kikoa hiki kidogo!
Tukio kuu lilifikiwa kwa kuchapwa kwa Mnara wa Mlinzi katika Kisiami (Kithai), kuanzia na toleo la Januari 1, 1947. Ilikuwa chapa ya kila mwezi ya nakala 200 zilizochapwa kwa mashine ya kurudufisha. Ndugu Wathailandi walikuwa wakibubujika kwa shangwe kwa kuwa sasa walikuwa wakipokea chakula kigumu cha kiroho kwa ukawaida katika lugha yao wenyewe. Mkalimani hakuhitajiwa tena katika funzo la Mnara wa Mlinzi.
Ziara ya Kwanza ya Msimamizi
Katika Aprili 1947, aliyekuwa wakati huo msimamizi wa Watch Tower Society, Nathan H. Knorr, na mwandishi wake Milton G. Henschel, akiambatana naye, alifanya ziara yake ya kwanza katika Thailandi. Pindi hiyo ilikuwa tukio kubwa kwa kuwa na kusanyiko la kwanza lililopata kufanywa katika Thailandi. Hotuba ya watu wote, yenye kichwa “Shangwe ya Watu Wote,” ilitolewa kwa wasikilizaji 275 kwenye jumba la Chuo Kikuu cha Chulalongkorn katika Bangkok.
Hotuba hiyo ilipewa utangazji mzuri na vyombo vya habari vya humo nchini. Hata hivyo magazeti mawili ya habari yalimshtaki Ndugu Knorr kuwa aliivunjia heshima dini ya Buddha katika hotuba yake. Habari kama hiyo yenye kuchochea chuki kwa wepesi sana ilitokeza mara moja uchunguzi wa maofisa wa CID. Ulifunua kwamba hakukuwa na taarifa au maelezo yenye kuchukiza yaliyokuwa yamefanywa. Wahariri wa magazeti hayo mawili waliomba radhi hadharani kwa sababu ya kuwapasha raia wa Bangkok habari zenye kosa na kwa sababu ya ukosefu wa haki aliotendwa N. H. Knorr na Watch Tower Society. Magazeti mengine kadhaa ya habari yalichapisha itikio la Sosaiti kwa uchambuzi huo, ikitokeza ushuhuda mkubwa hata zaidi kwa ajili ya kweli kuliko hotuba yenyewe.
Sasa Tawi
Ilikuwa wakati wa ziara ya Ndugu Knorr kwamba mipango ilifanywa ya kupanga kazi vizuri zaidi kitengenezo. Kwa shangwe ya akina ndugu na dada katika bohari la vitabu huko Bangkok, Ndugu Knorr alitangaza kwamba George Powell, akiisha kuhitimu kutoka darasa la nane la Shule ya Biblia ya Gileadi ya Watchtower katika mwaka huo, angerudi Thailandi akiwa mwangalizi wa tawi. Hivyo, Thailandi ikawa tawi katika Septemba 1, 1947.
Upesi baada ya hapo, Kurt Gruber aliwekwa rasmi awe mwangalizi wa mzunguko awe akitembelea yale makundi manne katika Kaskazini na moja katika Bangkok. Ziara hizo zilifanyia maendeleo uthamini wa akina ndugu kwa ajili ya mipango na taratibu za kitheokrasi, kutia ndani maana ya kuripoti wakati uliotumiwa katika kuhubiri. Kama tokeo, jumla ya wahubiri wakati wa mwaka wa utumishi wa 1948 iliruka kutoka 31 kufikia 65.
Kazi ilipewa kichocheo kingine katika Aprili 1948 kwa njia ya kusanyiko la kwanza la mzunguko, lililofanyiwa Chiang Mai. Wazia mshangao na shangwe ya akina ndugu kwenye kusanyiko hilo wakati walipohudhuria Shule ya Huduma ya Kitheokrasi kwa mara ya kwanza kabisa! Wengi wao walikuja kutoka vijiji vya mashambani nao walikuwa na elimu rasmi kidogo sana, lakini tangu sasa na kuendelea wangefaidika kutokana na elimu ya kitheokrasi na mazoezi yanayoandaliwa na tengenezo la Yehova kwa watu wake kila mahali.
Programu ya mkutano wa watu wote iliyokuwa imeanza miaka mitatu iliyopita katika nchi nyingi sasa ilianzishwa katika Thailandi. Hasa katika Bangkok, hotuba za watu wote zilitangazwa kwa vikaratasi na magari yenye vipaaza sauti. Watu walihudhuria mikutano hiyo kwenye Jumba la Ufalme la huko na kwenye shule za watu wote. Wakati mmoja, hotuba ya watu wote ilitolewa kwenye Ushirika wa Kibuddha katika Bangkok. Lilikuwa jambo lisilo la kawaida kuona watawa wa kiume Wabuddha 125, wakiwa wanavalia kanzu zao za rangi ya manjano, wakikaa kwenye safu zilizopangwa kwa utaratibu na kusikiliza kwa makini hotuba juu ya uasilia wa Biblia. Baadaye waliuliza maswali kadhaa. Kitabu cha Mwaka cha 1949 kilitoa maelezo haya kuhusu pindi hiyo: “Wengi wa mapadri hawa wana elimu nzuri na, tofauti na mapadri wa Utawala wa Makasisi Wakatoliki, wao ni wavumilivu sana kuelekea dini nyinginezo, na ni wenye adabu nzuri na wenye heshima.”
Wamisionari wa Gileadi Wafungua Sura Mpya
Katika jitihada ya kuimarisha tengenezo la nchini humo, Sosaiti iliwaalika Ndugu Gruber na Thomas wahudhurie darasa la 15 la Shule ya Gileadi. Kuhitimu kwao kulifanywa wakati wa Ongezeko la Theokrasi Kusanyiko la Kimataifa katika Yankee Stadium, New York, katika Julai 30, 1950. Wakiisha kurudi, walijiunga na wamisionari wengine watano wa Gileadi (bila kuhesabu George Powell) ambao kwa wakati ule ule walikuwa wamewasili—Alfred Laakso kutoka darasa la 7 na Joseph E. Babinski, Donald Burkhart, Gerald (Jerry) Ross, na Darrow Stallard, wote kutoka darasa la 12.
Wakati wa 1951 na 1952, wahitimu zaidi wa Gileadi waliwasili. Miongoni mwao walikuwa Guy Moffatt kutoka Uingereza na Neil Crockett kutoka New Zealand (wote wawili walikuwa wamepewa mgawo kwanza waende Malesia), Esko na Anja Pajasalmi na Elon na Helvi Harteva kutoka Finlandi, na Eva Hiebert na Marguerite Rood kutoka Kanada. Kufikia mwisho wa mwaka wa utumishi wa 1952, jumla ya wamisionari 20 waliozoezwa Gileadi walikuwa wakitumika Thailandi.
Kukiwa na wamisionari wengi sana hivyo wakiwa tayari kusaidia katika kazi, makao ya misionari yalianzishwa katika sehemu mbalimbali za nchi, kutia na Chiang Mai, Nan, na Lampang katika Kaskazini, Nakhon Ratchasima katika sehemu ya kati ya Thailandi, na Nakhon Si Thammarat na Songkhla katika sehemu ya Kusini. (Katika miaka ya karibuni zaidi, wamisionari walipewa migawo pia kwa muda fulani katika Khon Kaen, Ubon Ratchathani, Udon Thani, na Nakhon Sawan.) Makao hayo ya misionari yalipata kuwa ngome za kitheokrasi kwa akina ndugu yakiwa mahali pa kati pa sehemu hizo kwa ajili ya utegemezo na kitia-moyo cha kiroho kilichohitajiwa sana.
Tatizo la Kujifunza Lugha Mpya
Takwa la msingi la kuwa misionari mwenye mafanikio ni kuwa na uwezo wa kuwasiliana na watu katika lugha yao wenyewe—ambalo ni tatizo gumu kushinda kwa wamisionari wengi katika Thailandi. Tatizo la lugha ya Thai si kwamba ina sarufi ngumu yenye kutatiza. Kwa kweli, sarufi ni rahisi, kwa kuwa haina maneno ya kuhangaikia kama vile maneno ya kudhihirisha, ya kutiwa mwishoni mwa shina, ya kuonyesha jinsia ya kiume au kike, kubadili viarifa, yenye kuhitaji mabadiliko ya sarufi, au wingi.
Tofauti na herufi zenye mapambo za Kichina, Kithai kina alfabeti ya sauti, yenye konsonanti 44 na vokali 32 ambazo huunganishwa kufanyiza silabi za sauti. Lakini jambo linalofanya lugha hii kuwa tofauti sana na lugha za Magharibi ni hali yayo ya sauti ambayo inafanana na Kichina. Katika Kithai, kuna namna tano za sauti. Hivyo, ikitegemea ubadilifu wa sauti, neno au silabi yaweza kuwa na maana kadhaa, na nyakati fulani maana zilizo kinyume kabisa. Kwa mfano, “khao” likisemwa kwa sauti ya kuelekea chini humaanisha “mchele”; katika sauti ya chini-chini, humaanisha “habari.” Neno ilo hilo likipewa ubadilifu wa sauti wa kuelekea juu, lamaanisha “-eupe,” na katika sauti ya kawaida, au ya usawa, linakuwa “harufu mbaya sana.” Kwa hiyo misionari aliyekuja karibuni huenda akasema analeta “mchele mzuri (mwema),” “-eupe -zuri,” au “harufu mbaya sana nzuri” badala ya “habari nzuri (njema).”
Kupata ustadi juu ya hali hizo za pekee sana (kutia na sauti za vokali ambazo ni tofauti sana na zile za lugha zilizo nyingi za Magharibi) hutaka mazoezi, saburi, na uendelevu. Na kama vile ilivyo katika lugha nyinginezo, mgeni anaelekea sana kufanya makosa ambayo yaweza kuchekesha sana. Alipokuwa akieleza tofauti kati ya Mashahidi wa Yehova na dini za Jumuiya ya Wakristo, misionari mmoja alitaka kumwambia mwenye nyumba kwamba sisi hatutumii msalaba. Lakini aliyosema kwa kweli ni kwamba sisi hatutumii “suruali.” “Hata wanaume?” mwenye nyumba akashangaa akitaka kujua. “Hata mmoja,” dada akajibu kwa mkazo.
Walio wengi zaidi wa wale mapainia wa kigeni na wale wamisionari wa Gileadi wa mapema walijifunza lugha ile peke yao. Baadaye, Sosaiti ilianzisha njia mpya ili kusaidia wamisionari wajifunze lugha inayosemwa katika migawo yao. Wakifanya kazi ngumu ya kujifunza lugha kwa saa 11 kila siku kwa mwezi wa kwanza, na saa 5 kila siku katika mwezi wa pili, haikuwa kazi ndogo. Hata hivyo wamisionari wamethamini sana mpango huo, kwa kuwa umewasaidia sana kufanya kazi yao ya kuhubiri na kufundisha ifanikiwe sana.
Hawatofautiani Sana na Wenyeji Kama Farangs
Jambo kuu katika ziara ya pili ya Ndugu Knorr katika Aprili 1951 lilikuwa kuanzishwa kwa kazi ya mapainia wa pekee. Akina ndugu na dada wenyeji wenye uwezo walipewa migawo ya kusaidia makundi katika kazi ya kuhubiri na kufungua kazi katika maeneo mapya. Kwa kuwa hawakuhitaji kung’ang’ana na lugha ya wenyeji na kwa kuwa hawakutofautiana sana na wenyeji kama farangs wenye rangi ya ngozi nyeupe zaidi, au watu wa kigeni, mapainia wenyeji wametimiza fungu lenye maana sana katika kueneza ujumbe na kusaidia wapya. Kwa sasa, kuna mapainia wa pekee 70 (zaidi ya asilimia 6 ya jumla ya wahubiri).
Dada Buakhieo Nantha na Somsri Phanthuphrayun (sasa Darawan) walipewa migawo kuwa mapainia wa pekee wa kwanza, wakatumikie jiji la kusini la Nakhon Si Thammarat. Ndugu Sa-ngat Mungsin, painia mwingine wa pekee, alitumwa katika Chiang Rai, mkoa wa kaskazini zaidi unaopakana na Mianmari. Mapainia wa mapema kidogo walikuwa wameangusha vichapo vingi katika sehemu hizo mbalimbali, na hawa mapainia wa pekee walikuwa na hamu sasa kufanya kazi ya kufuatia na kuanza mafunzo ya Biblia.
Wale dada mapainia wa pekee wawili wa kwanza katika Nakhon Si Thammarat walimkuta Kruamat, mwanamke kijana Mbuddha aliyekuwa na duka lake mwenyewe la kushona nguo. Kwa kuwa yeye hakuwa na tamaa ya kubadili dini yake, ilitaka ziara nyingi pamoja na ushawishi mwingi wa upole ili kumfanya achukue wakati kutoka kazi yake ya kushona ili kuzungumza mafungu machache katika kile kitabu “Let God Be True.” Kupendezwa kwake kulipokwisha kuamshwa, akawa mwanafunzi wa Biblia mwenye bidii, na ujapokuwa upinzani kutoka kwa familia na marafiki wake, alianza kushirikiana na Mashahidi na kisha akaanza kuhubiri habari njema. Upesi baada ya ubatizo wake, akawa painia. Baadaye Dada Kruamat aliolewa na misionari Neil Crockett, na kwa miaka kadhaa walitumikia katika kazi ya mzunguko. Kwa sasa yeye ni painia wa pekee katika kundi moja la Bangkok ambamo Neil hutumikia akiwa mzee.
Msaada Watolewa Vijapokuwa Vitisho vya Kifo
Wakati Ndugu Sa-ngat alipohubiri katika mji wa Mae Sai kwenye mpaka wa Mianmari, alipata kuona jambo ambalo huthibitisha kwamba watu wenye mwelekeo wa kondoo ambao huona njaa ya kweli na uadilifu watapatikana, wajapokaa katika sehemu iliyo peke yake au wajapopingwa. Katika Oktoba 1951 alikutana na mwanamke kijana, Karun Chuthiangtrong, ambaye alizaliwa katika familia ya Kibuddha iliyozoea ibada ya wazazi wa kale waliokufa kulingana na pokeo la Kichina. Mwanamke huyo asimulia malezi yake hivi:
“Nikiwa tineja, nilimwuliza Nyanya mara nyingi tulitoka wapi na jambo linalotukia baada ya kufa. Lakini hadithi za kubuniwa na ng’ano nilizoambiwa katika kujibu maswali yangu hazikuniridhisha mimi. Katika 1945, nilipokuwa na umri wa miaka 19, mtu wa ukoo wangu aliyeishi Chiang Mai alipelekea familia yetu nakala moja ya Agano Jipya ya Kithai. Nilianza kuisoma nami nikapata kuona kwamba iliongea habari za Mungu akiwa ndiye Muumba na juu ya tumaini la uhai wa milele. Nakumbuka kwamba kati ya vichapo ambavyo mtu huyo wa ukoo wetu alitupelekea vilikuwamo vijitabu viwili vya Watchtower Society. Hata hivyo, wakati ule nilielewa kwamba ilikuwako namna moja tu ya dini ya Kikristo.
“Katika 1946 nilibatizwa katika Kanisa la Kipresbiteri. Nikijawa na bidii ya kuambia wengine juu ya ujumbe wa wokovu, nilitaka kuwa mhubiri. Nyakati kadhaa nilipeleka barua za ombi la kukubaliwa katika shule ambazo zilitoa mazoezi kwa wahudumu, katika Thailandi na pia katika nchi jirani ya Mianmari. Lakini kwa njia fulani sikufanikiwa kamwe.”
Wakati Ndugu Sa-ngat alipomtembelea Karun na akaweza kujibu maswali yake kwa wazi na kwa kupatana na akili, Karun alipata kitabu “Let God Be True.” Haikumchukua muda mrefu kutambua mlio wa kweli katika habari njema. Lakini haikuchukua muda mrefu pia upinzani kuanza. “Mara nyingi,” aendelea, “tulipokuwa tunazungumza juu ya Biblia, nyumba yetu ilipigwa kwa mawe, au watu walikuwa wakija na kufanya kelele nyingi nje ili kutusumbua. Siku moja mzee mmoja wa kanisa alikuja pamoja na polisi mmoja, ambaye alikuwa ndugu yake mdogo, na kujaribu kunitisha kuwa ningekamatwa nisipokoma kushirikiana na Mashahidi wa Yehova. Ndugu Sa-ngat alizidi kutishwa kwa kifo na kikundi kijulikanacho kama Mkono Mweusi. Hivyo Sosaiti ikaona inafaa kumhamisha kwa kumpa mgawo kwenda Songkhla upande wa kusini wa Thailandi.” Si muda mrefu baada ya hapo, Ndugu Sa-ngat alipigwa risasi akauawa jioni moja katika 1953; kesi hiyo haikutatuliwa kamwe.
Wakati ule ule, Karun alianza kuhubiri habari njema. Akiwa peke yake sasa na akiwa kilometa 320 kutoka kundi lililokuwa karibu zaidi naye, aliendelea kuhubiri kwa ujasiri, akiwa anatiwa nguvu na ziara za mwangalizi wa mzunguko na kwa kupelekewa vichapo na ofisi ya tawi kwa ukawaida. Kufuatia ubatizo wake katika Novemba 1952, Dada Karun alitumikia akiwa mfanyakazi wa wakati wote kwa miaka zaidi ya 20 na, ijapokuwa misiba angali anahubiri ujumbe wa uhuru wa kweli.
“Jina la Ajabu kwa Mtu wa Mungu”
Wale mapainia wa mapema walitimiza fungu muhimu sana katika kuhakikisha kwamba kazi imeimarishwa katika Thailandi. Wajapokuwa wachache kwa hesabu, walihubiri bila kuchoka katika eneo lao kubwa mno. Ilichukua miaka mingi kabla ya kuona matokeo kwa namna ya wanafunzi wapya. Lakini walivumilia. Walikuwa ‘wameweka mikono yao kwenye plau,’ nao waliendelea bila kuacha.—Lk. 9:62, NW.
Mwishowe, walio wengi wao waliondoka Thailandi wakatumike katika mashamba mengine. Wakiwa na bidii isiyopungua, na upendo kwa Yehova na wanadamu wenzao, walistahimili katika kazi ya utumishi wa wakati wote, baadhi yao mpaka kifo chao, wengine mpaka wakati wa sasa. Baada ya kuwa amepainia kwa miaka zaidi ya 50, Willy Unglaube alisema hivi: “Ninapotazama nyuma, inaonekana kuwa wakati mfupi tu. Kuwa mjumbe wa Yehova ndio utumishi ulio mzuri zaidi ambao mtu angeweza kuwa nao duniani. Bila shaka, lazima mtu awe na imani, imani nyingi, ili kushinda vikwazo vyote. Lakini sikuzote mimi hufikiria Mithali 18:10. Ndiyo, kama singekuwa nimechukua utumishi wa painia, nisingalikuwa na fursa ya kupata kujionea jinsi Yehova huwatunza watumishi wake wakimtegemea. Ninapofikiria unabii kwenye Isaya 2:2, mimi najua kwamba kungali kuna kazi nyingi ya kufanya, nami nataka kuendelea kushiriki kazi hiyo mpaka Yehova asemapo imetosha.” Ndugu Unglaube alikuwa angali anatumikia akiwa painia katika Ujerumani wakati alipomaliza mwendo wake wa kidunia miaka kadhaa iliyopita. Mtu mmoja katika eneo alitaja wakati mmoja kwamba “Unglaube” (linalomaanisha “kutoamini” katika Kijerumani) lilikuwa kweli kweli “jina la ajabu kwa mtu wa Mungu.”
Na namna gani juu ya Frank Dewar, aliyekuwa wa kwanza kukaa na kuhubiri habari njema katika Thailandi? Migawo yake ilimpeleka nchi mbalimbali katika kontinenti ya Asia, kutia Burma, China, na India. Katika 1966 alirudi Thailandi, ambako yeye pamoja na mke Mburma, Lily, wangali wanatumikia wakiwa mapainia wa pekee katika mji wa kaskazini wa Chiang Rai. Mwana wake, Donald, alitumikia akiwa mwangalizi wa mzunguko katika Mianmari na sasa amepewa mgawo wa Betheli katika Yangon (Rangoon).
Wamisionari Wajaribiwa
Ikiwa “Nchi ya Walio Huru,” sikuzote Thailandi imewapa raia zake uhuru wa kidini. Na Wabuddha Wathailandi kwa asili ni wenye uvumilivu kuelekea dini nyinginezo. Kwa hiyo hakujapata kamwe kuwa na uadui au mnyanyaso wa waziwazi wa kiserikali. Mtu angetazamia kwamba, uhuru huo wa kuhubiri habari njema waziwazi bila kuzuiwa, ungesaidia na kuongezea kazi mwendo.
Wakati wa miaka ya 1950 hesabu ya wahubiri ilizidi kuongezeka pole kwa pole. Hata hivyo, wamisionari wengi wa kigeni walikabiliwa na jaribu la aina ya pekee kwao, ambalo baadhi yao walishindwa kuliweza kwa mafanikio. Kaarle Harteva, ndugu mdogo wa Elon Harteva, ambaye alikuwa mhitimu wa darasa la 20 la Gileadi na akiwa misionari wakati wa pindi hiyo, atoa maelezo haya: “Ingawa urafiki wa watu ulifanya mambo kuwa yenye kupendeza, baada ya wakati fulani ulipata kuwa mkazo kwa wamisionari wengi. Urafiki huo ulikuwa, na ungali ni, sehemu ya utamaduni na mara nyingi hufanyiza ukuta mwororo wa ukinzani ambao ni vigumu kushinda. Kwa sababu hiyo, mazungumzo mazito na yenye kina yalikuwa machache na yalipatikana katikati ya vipindi virefu.”
Pia, kwa sababu ya malezi yao ya Kibuddha, subira nyingi ilitakwa ili kusaidia wapya waelewe kikamili kweli za Biblia na kuleta maisha zao katika upatani na viwango vya Yehova. “Njia za ulimwengu wetu mpya zilikuwa tofauti sana,” aendelea Ndugu Harteva, “halafu, malezi ya watu yalikuwa tofauti sana vilevile, yakiwa yameimarishwa sana na dini yenye kuruhusu watu wafanye watakavyo. Akina dada wengi wenye umri mkubwa wakati ule walizoea kutafuna popoo, ambayo ilitia meno yao rangi nyeusi sana kama mpingo. Dada wengine walikuwa wakivuta sigara zao zilizotengenezewa nyumbani zikiwa zimefungwa kwa majani makavu ya migomba ya ndizi zenye urefu wa sentimeta 25 hata walipokuwa wakienda nyumba kwa nyumba. Mtu angeweza kujua walipokuwa kijijini kwa ‘ishara zao za moshi.’ Pia ningali nakumbuka akina ndugu wakivuta sigareti kwenye makusanyiko ya mzunguko.” Bila shaka, baada ya wakati waliacha mazoea hayo yasiyopatana na Maandiko.
Wamisionari kiasi fulani walijaribiwa kwa habari ya uvumilivu wao na upendo wao kwa kazi wakati walipopata kujua kwamba ingewachukua muda mrefu kabla hawajaweza kikweli kusema lugha vizuri vya kutosha ndipo waweze kufundisha na kutoa hotuba. Na baadaye, wakati ongezeko lilipopunguza mwendo na miaka mingi ingepita bila kufanya hata mwanafunzi mmoja mpya, baadhi yao walivunjika moyo.
Hata hivyo, wamisionari wengine walifanya mgawo huo kuwa makao yao. Baada ya miaka 20, 30, au zaidi, wangali wanatimiza wajibu wao mbalimbali wakiwa wamisionari nao wanaweka kielelezo chema.
Baadhi ya wamisionari waliooana walipata watoto nao wakaacha mgawo wao wa misionari kwa sababu hiyo. Kwa kusifika, hesabu fulani kati ya hao wenzi wa ndoa waliamua kuendelea kukaa katika Thailandi, ambako uhitaji wa wahudumu waliokomaa ni mkubwa sana.
Sinema ya Sosaiti, Kifungua-Macho
Kukiwa na uwiano wa mhubiri 1 kwa wakaaji 100,000, Mashahidi wa Yehova katika miaka ya 1950 hawakujulikana sana nchini. Ile sinema yenye kuitwa The New World Society in Action (Sosaiti ya Ulimwengu Mpya Katika Tendo) ilithibitika kuwa msaada mkubwa katika kuwafahamisha watu kuhusu kazi ya Mashahidi wa Yehova. Mashahidi wenyewe walifaidika pia, kwa kuwa sinema hiyo ilifungua macho yao waone mweneo wa ulimwenguni pote wa tengenezo la Yehova, hivyo kuwasukuma wahisi kuwa karibu zaidi nalo. Wakati uliopita, ni wachache wao wangeweza kuona akilini mwao tengenezo lionekalo la Mungu ni kubwa na limeenea kadiri gani na jinsi lifanyavyo utendaji walo mbalimbali kwa ustadi sana.
Esko Pajasalmi alionyesha sinema hiyo sehemu ya kaskazini ya Thailandi na katika Bangkok. Kwa kawaida yeye alitangazaje sinema hiyo? “Mapema katika siku, tulikuwa tukiangika kiambaza cha kuonyeshea sinema katika uwanja wa michezo wa kijiji ambapo wanakijiji wangeweza kukiona kwa urahisi,” akasema. “Kisha tulikuwa tukitembelea shule na kuingia tu katika kila darasa na kufanya tangazo fupi kwa wanafunzi na walimu. Kwa njia hiyo kijiji chote kilipata kujua habari. Baada ya jua kushuka, wachuuzi wakiwa na tamutamu zao za kienyeji—njugu na mandizi yaliyochemshwa kwa mafuta, kupikwa, kuokwa, pamoja na vitafunwaji vingine—walikuwa wakiwasili katika uwanja wa michezo mmoja baada ya mwingine. Walikuwa akiweka tayari maduka yao madogo-madogo na kuyaangazia kwa taa ndogo zenye kutumia mafuta ya taa zilizotengenezwa kwa mikebe mitupu ya maziwa. Upesi, walitujia kutoka pande zote huku wakionekana kama vikundi vya vimulimuli. Lakini sivyo, walikuwa watazamaji wetu wakibeba taa ndogo-ndogo zenye kutumia mafuta ya taa. Walikuja kwa mamia, na mara nyingi kwa maelfu, kutazama sinema yetu.”
Mara nyingi sinema hii ilionyeshwa katika mahali pasipo pa kawaida. Mmojawapo wanachuo mashuhuri Mbuddha katika kaskazini mwa Thailandi, Khun Maha Phon, alijifunza Biblia na Esko kwa wakati fulani, naye alitaka watawa wa kiume na wafuasi Wabuddha waone Sosaiti ya Ulimwengu Mpya ilivyo. “Kwa hiyo tuliionyesha mara kadhaa wakati ambao watawa wengi wa kiume walihudhuria,” akumbuka Ndugu Pajasalmi. “Nyakati nyingine tulikuwa tukionyesha sinema hiyo ndani ya wat [hekalu] lenyewe. Nilikuwa nikiketi mbele ya sanamu ya Buddha iliyokuwa na kimo cha kuanzia meta 6 hadi 8 na kuendesha mitambo, nacho kiambaza kilikuwa kikitandazwa juu ya mlango mkuu, watu wakiwa wameketi sakafuni wakitazama sinema. Lilikuwa jambo la ajabu kuhubiri habari za Yehova na Ufalme wake katika hekalu la Kibuddha.”
Mojayapo heshima bora sana ya hadharani iliyopata kupewa Mashahidi wa Yehova katika Chiang Mai ilitoka kwa mwanachuo uyo huyo, Khun Maha Phon. Ndugu Pajasalmi akumbuka hivi: “Alitualika tutoe hotuba na kuonyesha sinema katika jumba la Buddhist Association, ambamo alitujulisha kwa njia ifuatayo: ‘Huenda mkataka kujua kwa nini mimi, Mbuddha, nimewaalika hawa Mashahidi wa Yehova waonyeshe sinema yao na kutoa hotuba katika jumba hili. Mimi nimejifunza na mmoja wao kwa miezi mingi nami naweza kuwaambia kwamba wao ni tofauti sana na zile dini nyingine zote za Kikristo ambazo tumeona hapa. Wao hufanya kazi kwa bidii katika kuhubiri, nao wanazoea yale wanayohubiri. Hata wanafanya kazi yao wao wenyewe katika makao yao ya misionari. Kama yeyote wenu, baada ya kuona sinema hii, atapata amani katika ujumbe ambao Mashahidi wa Yehova wanahubiri, mimi nitakuwa mwenye furaha sana.’” Kwa hiyo wale waitwao eti Wakristo wenzetu huku wakiwa wenye shughuli sana kushambulia Mashahidi wa Yehova, wale waitwao eti Wabuddha wapagani walionyesha hali ya kuwa wenye kuvumilia sana maoni yanayotofautiana na yao.
Kaarle Harteva alikaza fikira zake katika kuonyesha sinema iyo hiyo katika ile miji mikubwa katika kaskazini-mashariki. “Inashangaza jinsi tulivyofaulu nyakati nyingine,” akataja. “Wakati mmoja, mtambo wetu wa umeme ulishindwa kufanya kazi huku tukiwa katikati ya kuonyesha sinema. Tukitumaini kwamba si wote wa wale zaidi ya elfu waliohudhuria wangeondoka, nilitimua mbio kwa teksi (baiskeli ya magurudumu matatu) niliyokodi nikatafute mtambo mwingine. Kwa mshangao wangu, niliporudi, walikuwapo watu zaidi waliokuwa wakingojea kuona sinema kuliko hapo mwanzoni. Baada ya wonyesho huo, mwenzangu nami tulishindwa kuwapa mkononi kila mmoja trakti katika umati mkubwa kadiri hiyo. Hivyo tulirusha tu trakti hizo hewani. Hakuna hata mojayapo iliyoanguka chini.”
Wonyesho wa peupe mbele ya jumba la mji mkuu wa mkoa katika Kalasin uliweka rekodi ya hudhurio—zaidi ya 4,200 walikuwapo. Maelfu zaidi waliona sinema hiyo ilipoonyeshwa kila siku wakati wa sherehe ya juma zima ya Siku ya Katiba katika Lumpini Park, Bangkok.
‘Tuliongea Kupita Usiku wa Manane’
Katika 1952 Elon Harteva na mke wake, Helvi, walikuwa miongoni mwa kikundi cha kwanza cha wamisionari waliopewa mgawo kwenda Nakhon Ratchasima, mji mkubwa zaidi ya yote katika Thailandi ya kati. Akitumia Nakhon Ratchasima kuwa kituo cha kuendeshea shughuli, Elon alitembelea miji mingine katika eneo hilo la nchi ambalo karibu ni lenye ukame. Katika Khon Kaen alikuta Bw. Seng Buawichai, mhubiri mwenyeji wa Christian and Missionary Alliance.
Tayari akiwa na shaka juu ya fundisho la Utatu, Bw. Seng alikaribisha mazungumzo juu ya habari hiyo. “Tulizidi kuongea kupita usiku wa manane,” akumbuka Elon Harteva. “Na kwenye saa kumi asubuhi iliyofuata, Bw. Seng aliniamsha akaanza kuuliza maswali zaidi. Katika siku hizo nyumba nyingi hazikuwa na taa ya umeme bado. Tukichuchuma chini sakafuni, tulisoma Biblia kwa nuru hafifu ya taa zenye kutumia mafuta ya taa.
“Kwenye ziara iliyofuata, Bw. Seng alikuwa amealika Wakristo wengine kadhaa wa jina tu na kupanga hotuba ya watu wote itolewe katika nyumba yake. Baadhi ya watu waliokuwapo walitoka katika vijiji vilivyokuwa jirani. Kutembelea mmoja wa watu hao wenye kupendezwa kulitaka safari ya kutembea kwa miguu ya kilometa 11 kupitia katika mashamba ya mpunga na msitu. Nilipofika kijijini, nilishangaa kama nini kuona sala [kibanda] kilichojengwa juu ya maboriti kikiwa na umbo kama la mnara wa mlinzi mdogo. Mtu huyo si kwamba tu alikuwa na Biblia bali alikuwa pia magazeti kadhaa ya Mnara wa Mlinzi, ambayo alitumia kuelezea Biblia wageni waliotua wapumzike kwa muda kwenye kibanda hicho wakiwa njiani kwenda kwenye vijiji vingine.”
Baadaye Bw. Seng na mwanamume mwingine kutoka kijiji hicho walipata kubatizwa.
Kuingia Ndani ya Indochina
Kufuata ziara ya tatu ya Ndugu Knorr katika Thailandi, katika Aprili 1956, jitihada zilifanywa za kutuma wamisionari katika nchi zilizokuwa hapo kwanza Indochina ya Ufaransa, yaani, Vietnamu, Kambodia, na Laosi, nao wangekuja chini ya uangalizi wa tawi la Thailandi. Habari njema zilipata kufika eneo hilo la Indochina kwa mara ya kwanza katika 1936, wakati mapainia wawili kutoka Australia walipowasili katika jiji la Saigon (sasa laitwa Jiji la Ho Chi Minh). Mmoja wao, Frank Rice, alisonga mbele na kazi kwa ujasiri mpaka alipokamatwa na askari-jeshi wa vita Wajapani katika 1943 na baadaye akalazimika kuondoka nchini. Wakati wa 1953 na 1954, kazi fulani ya kuhubiri ilifanywa na mtu mwenye kupendezwa, ambaye alipeleka ripoti zake kwenye ofisi ya tawi ya Ufaransa.
Baada ya Vietnamu kuwa jamhuri karibu na mwisho wa 1955, Ndugu Knorr alimwuliza Ndugu Babinski, ambaye wakati huo alikuwa mwangalizi wa tawi katika Thailandi, awasiliane na wenye mamlaka katika Saigon apate ruhusa ili wamisionari wa Watch Tower Society waingie nchini humo. Katika Juni 27, 1957, wahitimu wa Gileadi wa kwanza watano waliwasili Saigon, nayo makao ya misionari ikawekwa chini ya usimamizi wa tawi la Thailandi.
Kazi Yasonga Mbele, Ijapokuwa Vita Katika Vietnamu
Wamisionari waliona kuhubiri nyumba kwa nyumba katika Saigon kuwa jambo lenye kupendeza mno. Kwa ujumla watu waliwapokea kwa fadhili, na vichapo vingi viliangushwa. Wakati wa mwaka kamili wa kwanza wa utumishi, maandikisho karibu 1,200 ya Mnara wa Mlinzi na Amkeni! yalipatikana. Hata hivyo, kidogo kazi ya kufanya wanafunzi iliendelea polepole.
Mwanzoni kazi ya kuhubiri ilifanywa kwa Kifaransa, na mikutano yote iliongozwa kwa Kifaransa. Hiyo ilikuwa lugha ya jamii ya “wenye elimu.” Kama ilivyokuwa katika siku za Yesu, si wengi wa jamii hiyo walikuwa tayari kuwa wanafunzi. Kwa hiyo Sosaiti ilitia wamisionari moyo wajifunze na kutumia lugha ya wenyeji, Kivietnamu. Hiyo ilichukua miaka kadhaa ya kazi ngumu. Lakini mara wamisionari walipokwisha kuwa wenye ufasaha katika lugha ya wenyeji na watu wa kawaida ‘wakawasikia wakisema kwa lugha yao wenyewe,’ wengi walipata kupendezwa.—Mdo. 2:6.
Vile vijitabu “Habari Njema Hizi za Ufalme,” “Tazama! Nayafanya Yote Kuwa Mapya,” na Kuishi Katika Tumaini la Taratibu Mpya Yenye Haki vilitafsiriwa katika Kivietnamu na vikatumiwa kwa wingi sana katika kazi ya funzo la Biblia. Kufikia 1966, wahubiri 11 walikuwa wamejiunga na wale wamisionari 8, kati yao 3 wakiwa wamebatizwa.
Lakini namna gani juu ya ile vita kali ya Vietnamu iliyochacha kwa miaka mingi sana? “Badala ya kuwa na wasiwasi sana juu ya yale yanayoweza kuupata Saigon, sisi twajishughulisha na kazi ya kuhubiri habari njema kwa watu wengi wanaosongamana katika jiji ambao wanahitaji sana ujumbe wa tumaini,” akasema misionari mmoja aliyekuwa akitumikia katika Saigon wakati ule. Ndiyo, wamisionari na ndugu wenyeji walitumia kanuni kwenye Mhubiri 11:4: “Mwenye kuangalia upepo hatapanda [mbegu]; naye ayatazamayo mawingu hatavuna.” Badala ya hivyo, waliendelea ‘kutupa mkate wao juu ya uso wa maji,’ na ‘baada ya siku nyingi waliupata tena.’ (Mhu. 11:1) Wakati wa 1974 katika yale makundi matatu katika Saigon, wahubiri 113 walikuwa wakitumikia bila hofu, hata hivyo kwa uangalifu.
Mara nyingi, kwa wazi mwongozo wa kimalaika na ulinzi vilitolewa, kama katika 1968, muda mfupi kabla ya vita hiyo yenye umwagaji mwingi sana wa damu kuanza wakati wa shambulio la Tet juu ya Vietcong. Wamisionari walihama kutoka makao yao yenye starehe katika eneo la makao wakaenda katika nyumba ndogo katika kisehemu cha Wachina katika sehemu ya chini mjini Saigon. Upesi eneo walimokuwa wakiishi lilikaliwa na Vietcong. Robert Savage, mmoja wa wamisionari, aliandika hivi: “Majeshi ya Vietcong wameshambulia kotekote katika Saigon kwa nguvu kamili. Hali ni kali sana, lakini bado si yenye hatari kwetu. Akina ndugu wamekuwa wema sana. Kwa kuhatarisha maisha zao, wametujia kwa kupitia vijia vya sehemu za nyuma ili kujaribu kutusaidia.”
Baada ya shambulio la Tet, wamisionari na ndugu wenyeji walisonga mbele. Katika 1970 kile kitabu Kweli Iongozayo Kwenye Uzima wa Milele kilitolewa katika Kivietnamu, kikatokeza mafunzo mengi mapya ya Biblia. Kuchapwa kwa Mnara wa Mlinzi katika Kivietnamu katika 1971 kulikuwa kichocheo kingine kikuu kwa kazi. Katika mwaka wa kwanza wa kuchapwa, maandikisho zaidi ya elfu moja yalipatikana kwa chapa ya Kivietnamu. Katika 1973 Vietnamu ilipata kuwa tawi nayo ikaangalia kazi humo mpaka serikali ilipoangushwa katika 1975.
Kambodia Yapokea Ushuhuda
Alipokuwa katika safari yake ya kurudi Saigon katika Juni 1956, Ndugu Babinski alitua katika Phnom Penh, mji mkuu wa Kambodia. Kama alivyokuwa amefanya katika Saigon, alionana na maofisa wa serikali ili kupata ruhusa ya kutuma wamisionari nchini humo. Huko nyuma katika miaka ya mwisho-mwisho ya 1930, mapainia kutoka Saigon walikuwa wametoa ushuhuda fulani katika Phnom Penh. Lakini baada ya juma moja, polisi waliwaambia kwamba hakuna kazi ya kidini iliyoruhusiwa katika ufalme wa Kibuddha isipokuwa kwa ruhusa ya pekee kutoka kwa mfalme. Hata hivyo, mfalme hakutoa ruhusa.
Ndugu Babinski alikutana na waziri wa mambo ya ndani wa serikali ya kifalme ya Kambodia. Ofisa huyo alionekana akipendezwa sana na yale aliyoambiwa na Ndugu Babinski hivi kwamba hakuona sababu kwa nini Mashahidi wa Yehova hawawezi kuendesha utendaji wao katika nchi yake. Baada ya miezi mingi ya kungojea, Sosaiti ilitaarifiwa kwamba serikali haikuwa imefanya uamuzi bado juu ya kutoa vyeti vilivyoombwa. Kwa hiyo, katika Aprili 1958, Ndugu Babinski aliomba apewe heshima ya kuwa na mahoji pamoja na Mwana wa Mfalme, Norodom Sihanouk. Ingawa Ndugu Babinski alipata kuongea tu na karani wa kibinafsi wa huyo mwana wa mfalme naye akaacha baadhi ya vitabu vya Kibiblia apewe mwana wa mfalme, ruhusa ya kuhubiri ilitolewa, na katika Desemba 1958 wamisionari wanne wa kwanza waliingia hatimaye katika Kambodia na wakawa na shangwe ya kuanza kazi yao ya kutoa evanjeli katika Phnom Penh.
Wengi miongoni mwa ile idadi kubwa ya Wachina katika Phnom Penh walisema Kiingereza fulani kuongezea Kichina; na hesabu kubwa kidogo ya Wavietnamu wakaaji walisema Kifaransa na Kivietnamu pia. Hata hivyo idadi iliyo kubwa zaidi ya watu wa kawaida, waliweza kusema Kikambodia tu. Ni wazi kwamba, kulikuwa na tatizo la lugha. Mwanzoni, mikutano iliongozwa kwa Kiingereza, na Wachina wengi kidogo walikuja. Halafu, mikutano ilipangwa katika Kifaransa, na baadhi ya Wavietnamu wakahudhuria. Wamisionari walijaribu kujifunza Kikambodia, na vichapo fulani vilichapwa katika Kikambodia ili kufikia watu wenyeji kwa ujumbe wa Ufalme. Lakini wamisionari walibadilishwa-badilishwa, na hakuna yeyote aliyekaa muda mrefu vya kutosha kuweza kikweli kuwa mwenye ufasaha vya kutosha katika lugha ile. Baadhi ya Wakambodia walijifunza na wakaanza kushirikiana na wamisionari, hivi kwamba katika mwaka mmoja kulikuwako kilele cha wahubiri 13 katika utumishi wa shambani. Kwa wazi kweli haikuwa imegusa mioyo yao kwa kina kirefu vya kutosha, kwa kuwa polepole walio wengi wao waliaacha msimamo wao.
Kwa sababu ya mabadiliko ya serikali katika kupendelea upande mmoja kisiasa, kufikia mapema katika 1965 ilikuwa wazi kwamba Watu wa Magharibi hawakutakwa tena katika Kambodia. Maombi ya vyeti kwa ajili ya Panayotis Kokkinidis, ambaye alikuwa amehitimu katika Gileadi katika 1964, yalikataliwa. (Kwa hiyo alipewa mgawo mpya kwenda Saigon.) George na Carolyn Crawford, wamisionari wawili wa mwisho waliobaki, waliambiwa kwamba vyeti vyao havingefanywa upya vilipokwisha katika Mei 27, 1965. Kwa kupendeza, miaka minne mapema barua rasmi ilikuwa imepelekwa kwa wamisionari, ikiwataarifu kwamba walipaswa kukomesha kazi yao ya kuhubiri waziwazi. Lakini barua hiyo haikupokewa kamwe, wala polisi wa usalama hawakupokea nakala yao ya barua hiyo.
Kwa hiyo akina Crawford wakalazimika kuondoka Kambodia. Shahidi mmoja tu Mvietnamu ndiye aliyebaki, yaani, Ndugu Long. Hata hivyo, baadaye katika 1965, mwanamume mwenye umri mkubwa Mkambodia aliyekuwa amebatizwa wakati wa mojayapo ziara za kawaida za mwangalizi wa mzunguko alijiunga na Ndugu Long. Ndugu huyo alikufa akiwa mwaminifu miaka miwili baadaye. Ndugu Long, ambaye aliendelea akiwa Shahidi pekee mwenyeji kwa ajili ya Yehova katika nchi hiyo, alikwenda Ufaransa kabla ya serikali ya Kambodia kubadilika katika 1975.
Njia za Kitheokrasi Zathibitika Kuwa Zenye Mafanikio Katika Laosi
Nchi ya tatu ya zile zilizokuwa hapo awali French Indochina ambayo imekuwa chini ya tawi la Thailandi ni Laosi. Wakiwa na uhusiano wa karibu na Wathailandi kikabila na kitamaduni, watu wa ufalme huo wa Kibuddha ulio kaskazini-mashariki mwa Thailandi walisikia habari njema kwa mara ya kwanza katika 1958. Katika Desemba wamisionari wawili waliwasili katika mji mkuu, Vientiane. Wanne zaidi walifuata katika Machi 1959. Mwishoni mwa 1960, wahitimu sita wapya wa Gileadi walitumwa Laosi, na kao la pili la misionari likaanzishwa katika Savannakhet.
Kufikia wakati ambao hao wawasili wa 1960 walikuwa wametulia, wale wamisionari wote wa mapema kidogo walikuwa wameondoka nchini kwa sababu moja au nyingine. Hata hivyo, yaonekana, baadhi yao, walitaka kufuata mawazo yao wenyewe badala ya njia za Sosaiti zilizokuwa zimethibitishwa zenye mafanikio kwa kutumiwa kwa wakati mrefu. Katika Januari 1965 mwangalizi wa mzunguko aliripoti kwamba kikundi hicho kilikuwa na mkutano mmoja wa saa moja kila juma. Hivyo, ni maendeleo kidogo sana yaliyofanywa.
Kwa hiyo lilikuwa tukio la wakati ufaao wakati akina Crawford walipopewa mgawo mpya kwenda Vientiane baada ya wao kulazimika kuondoka Kambodia katika Mei 1965. George Crawford hukumbuka hivi: “Baada ya kukaa katika Vientiane siku chache tu, tuliona kwamba kulikuwa na mwelekeo usio wa kawaida kuelekea mikutano na namna inavyopasa kuongozwa. Wengine katika kikundi hicho walikuwa wakifuata wanadamu, na ilionekana kwamba walikuwa wakishirikiana kwa ajili ya pato la vitu vya kimwili. Tulijitahidi kukaza akilini maoni yanayofaa na uthamini kwa tengenezo la Yehova na uhitaji wa kufanya kazi karibu-karibu na ofisi ya tawi katika Bangkok. Kwa msaada wa Ndugu Timothy Bortz, badiliko lilifanywa la kufanya mikutano kwa kupatana na namna na ratiba iliyodokezwa na Sosaiti. Lugha ya Kilao ilianza kutumiwa. Polepole wale waliokuwa wakifuata wanadamu waliacha msimamo wao ijapokuwa jitihada kubwa ya kuwajenga kiroho.”
Ilipokuwa lazima Ndugu na Dada Bortz waache utumishi wa misionari katika Laosi kwa sababu za kiafya, akina Crawford waliachwa peke yao wakiwa wamisionari. “Ilionekana kwetu kama kwamba tulikuwa tukipiga vita ambayo hatungeshinda ili kumaliza mwelekeo usiofaa uliokuwamo miongoni mwa kikundi na katika kujaribu kupata mwanzo mpya,” aendelea Ndugu Crawford. “Lakini upesi wamisionari wanne wapya waliwasili—John na Kathleen Galisheff kutoka Kanada na Margaret Roberts na Sylvia Stratford kutoka Uingereza. Hao walikuwa wafanyakazi wenye ujuzi, wakiwa wamekwisha kutumikia wakiwa mapainia wa pekee katika Quebec na katika Ailandi. Baadaye katika 1967, Terance Olsen kutoka Kanada na Brian Marks kutoka Uingereza waliongezwa kwenye kikundi chetu. Msaada huo wa ziada ulileta tofauti katika kushinda ile mielekeo isiofaa. Sasa watu wengi wenye kupendezwa walifikiwa na wakasaidiwa wafanye maendeleo katika kweli.”
Miongoni mwao alikuwamo mwanamke mmoja Mlao, Siphanh Lao. Baada ya kujifunza Biblia katika Laosi, alifunga safari kwenda Kanada na United States, ambako alipewa nafasi ya kuajiriwa kazi yenye mshahara mnono lakini yenye kutilika shaka. Yeye asimulia hivi: “Sikuruhusu Shetani anirudishe tena ndani ya ulimwengu kwa kukubali kazi yenye mshahara mnono . . . ambayo ingenifanya nivunje msimamo wangu wa kutokuwamo kwa Kikristo.” Badala ya hivyo, yeye aliamua kurudi Laosi na kubatizwa. Kwa kweli, Siphanh alikuwa ndiye Mlao wa kwanza Mbuddha katika Vientiane kuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova. Kabla ya hapo, watu wengi katika eneo walikuwa wakisema, “Nyinyi hamna Mlao yeyote katika dini yenu.” Hilo lilibadilika sasa. Ndugu mdogo wa Siphanh, Bunhoeng, alifanya maendeleo haraka sana katika kweli na akawa painia wa pekee katika 1972.
Dada Crawford hueleza hivi: “Mimi nakumbuka wakati tulipokuwa ni sisi sita tu kwenye mikutano wakati wa 1965 na 1966. Kwenye kusanyiko la mzunguko letu la kwanza, hatimaye tulikuwa na tisa waliohudhuria kwa ajili ya programu ya Jumamosi jioni, walio wengi wao wakiwa jukwaani kwa maonyesho. Kwa kutofautisha, kwenye kusanyiko la mzunguko katika 1971, tulikuwa na 75 waliohudhuria, na 99 walihudhuria Ukumbusho katika 1974.”
Wakati serikali mpya ilipochukua mamlaka katika Laosi katika sehemu ya mwisho ya 1975, kulikuwako makundi mawili yenye afya yaliyokuwa yakitenda kwa muundo wa kitheokrasi, moja katika Vientiane na jingine katika Savannakhet. Kazi fulani ya kuhubiri ilikuwa imefanywa pia katika mji wa Pakse, sehemu ya mbali ya kusini. Ilikuwa lazima wamisionari wote waondoke Laosi. Hata hivyo, akina Crawford na akina Galisheff wameendelea na utumishi wao wa ushikamanifu katika Thailandi.
Ndugu Franz Aja Thailandi
Acheni sasa turudi kwenye kazi katika Thailandi. Frederick W. Franz, makamu wa msimamizi wa Sosaiti wakati ule, alifanya ziara yake ya kwanza katika Thailandi katika Januari 1957. Hilo lilikuwa tukio kubwa kwa ndugu wenyeji. Hawakuwa wamepata kukutana naye kamwe, ingawa walikuwa wamesikia mengi juu yake. Kusanyiko la siku tatu lilipangwa katika Bangkok lilingane na ziara yake.
Wakati wa mkutano wa pekee pamoja na wamisionari, habari ya kuwa na kichapo chenye kufaa kwa ajili ya idadi ya watu wasio Wakristo lilizungumzwa. Kitabu “Let God Be True” kilikuwa kimekwisha chapwa katika Kithai huko nyuma katika 1949 na kilitumiwa sana katika kazi ya funzo la Biblia. Hata hivyo, kilikazia kukanusha mafundisho yenye kosa ya Jumuiya ya Wakristo, ambayo watu walio wengi Wabuddha hawakufahamiana nayo. Hivyo, ingetamanika kuwa na kitabu ambacho kilieleza tu kweli za mafundisho ya Biblia kwa watu ambao hawakuwa na malezi mengi ya Kimaandiko.
Ndugu Franz hakusema mengi wakati huo. Lakini wakati katika 1958 kile kitabu Kutoka Paradiso Iliyopotea Mpaka Paradiso Iliyopatikana kilipotolewa, loo, jinsi akina ndugu walivyothamini uandalizi huo wa wakati wenye kufaa kutoka kwa tengenezo la Yehova! Kilipopatikana katika lugha ya Thai katika 1961, nakala zaidi ya 50,000 ziligawanywa katika shamba. Kikiwa na vielezi vyake vyenye kupendeza na kikiwa kikubwa, watu walikubali kitabu hicho, hata ingawa mchango wake ulikuwa karibu mshahara wa siku nzima wa mfanya kibarua.
Kuchapa Habari Njema Katika Kithai
Ijapokuwa nakala zilizochapwa katika chapa ya Kithai ya vitabu na magazeti ni chache kwa kulinganisha, sikuzote akina ndugu katika Thailandi wameandaliwa chakula cha kiroho kwa wakati wake kwa lugha yao. Vitabu vikubwa vya Sosaiti vilivyo vingi ambavyo vimejalidiwa vimechapwa katika Kithai. Katika 1952, wakati mwenezo wa gazeti Mnara wa Mlinzi ulipofikia nakala 500, lilianza kuchapwa na kampuni ya kibiashara katika Bangkok. (Tangu Januari 1, 1947, lilikuwa limekuwa likirudufishwa na akina ndugu.) Ndipo, kuanzia na toleo la Oktoba 1, 1971, Mnara wa Mlinzi likawa gazeti la mara mbili kwa mwezi. Na tangu 1978, Amkeni! limekuwa likichapwa kila mwezi. Si kwamba tu hilo lamaanisha chakula zaidi cha kiroho cha namna namna kwa akina ndugu bali pia Amkeni! huvutia zaidi wasomaji Wabuddha.
Iwe nakala maelfu machache au milioni kadhaa za kitabu au gazeti huchapwa, kutafsiriwa, kupanga chapa, kuchunguza ili kusahihisha makosa, na kazi ya picha huchukua karibu kiasi kile kile cha wakati katika lugha yoyote. Hivyo kazi nyingi inafanywa kwenye ofisi ya tawi, ambamo washiriki wa familia ya Betheli wa kudumu 16 na wafanyakazi wasaidizi kadhaa wa tawi wanatumikia kwa sasa mahitaji ya ndugu zao na ya watu wenye kupendezwa kotekote nchini.
Mapainia Wenyeji—Wazoezwa Gileadi
Miongoni mwa wale wanafunzi 103 wa darasa la 31 la Gileadi, ambao shughuli za kuhitimu kwao zilifanywa katika 1958 wakati wa Mapenzi ya Kimungu Kusanyiko la Kimataifa katika Yankee Stadium, New York, lenye kukumbukwa sana, walikuwamo mapainia wawili kutoka Thailandi—Ndugu Bantoeng Chantraboon na Dada Buakhieo Nantha. Ndugu Bantoeng alikuwa amewekwa kuwa mwangalizi wa mzunguko katika 1956. Angali anatumikia akiwa painia wa pekee katika kaskazini mwa Thailandi. Dada Buakhieo alikuwa mmoja wa wale mapainia wa pekee wawili wa kwanza katika Thailandi. Aliendelea kwa bidii katika kazi ya painia wa pekee kwa bidii mpaka kifo chake katika 1986. Dada Somsri Darawan, painia wa pekee mwenzi wa Buakhieo, alikuwa amehitimu kutoka darasa la 20 la Gileadi katika 1953. Kwa miaka mingi amekuwa akisaidia kwa wakati wote katika kazi ya tafsiri kwenye tawi.
Wafanyakazi wengine wa wakati wote wenyeji walipokea mazoezi kwenye Shule ya Gileadi na kisha wakarudi kwenye nchi ya kwao kuendeleza faida za Ufalme. Kikundi cha karibuni zaidi, kiliwasili katika 1979, waliokuwamo wakiwa Asawin Urairat, ambaye sasa yumo katika Halmashauri ya Tawi, na mke wake, Chiwan, pamoja na Sakda Darawan (mwana wa Somsri), ambaye anatumikia akiwa badala ya mwangalizi wa mzunguko, na Dada Srisuphap Vesgosit, ambaye ni misionari kwenye makao ya misionari ya Thon Buri.
Mahali Papya pa Tawi na Uangalizi Mpya
Tangu mwisho wa Vita ya Ulimwengu ya 2, Sosaiti ilikuwa imekodi jengo kwa ajili ya ofisi ya tawi na makao ya misionari kwenye 122 Soi Decho, mahali penye kujulikana sana na wakaaji wengi wa Bangkok. Wakati, katika 1957, mkodishaji alipotaka kuongeza kodi kupita kiasi, Ndugu Knorr aliona wakati ulikuwa umefika wa kununua ardhi na kujenga jengo la tawi. Katika 1959 ardhi yenye kufaa ilipatikana kwenye 69/1 Soi Phasuk, Sukhumwit Road, katika eneo zuri la makao si mbali sana na wilaya ya kibiashara ya jiji.
Kufikia Oktoba 1961 kampuni ya ujenzi iliyopewa kazi iliweza kuanza ujenzi. Lilipomalizika miezi sita baadaye, jengo hilo lenye ghorofa mbili lilitia ndani Jumba la Ufalme na vyumba sita vya kulala. Wafanyakazi wa Betheli, watatu wakati ule, pamoja na wamisionari sita, walifurahi kuhama kutoka kwenye makao ya muda katika Soi Lang Suan na kuingia katika makao mapya yenye starehe.
Muda mfupi kabla ya ujenzi kuanza katika 1961, badiliko la uangalizi wa tawi lilikuwa limetukia. Joseph Babinski, aliyekuwa amechukua mahali pa George Powell katika mgawo huo katika 1950, alilazimika kuacha utumishi wa misionari kwa sababu ya madaraka ya familia. Katika Septemba 1, 1961, Paul Engler alipewa mgawo wa kuwa mwangalizi wa tawi. Akiwa mzaliwa wa Ujerumani, Ndugu Engler alikuja Thailandi baada ya kuhitimu kutoka darasa la 20 la Gileadi. Alitumikia akiwa misionari katika mji wa kaskazini wa Chiang Mai kwa karibu miaka sita kabla ya kuhamia Betheli katika 1959. Waangalizi wote watatu wa tawi—Ndugu Powell, Babinski, na Engler—waliandaa mwelekezo wenye thamani sana kwa kazi ya Ufalme katika Thailandi.
Wakati wa Kupepeta
Wakati wa pindi ya 1945 mpaka 1960, kulikuwako ongezeko ambalo daima lilizidi kuendelea katika hesabu ya wahubiri, zaidi ya asilimia 20 katika miaka fulani. Ndipo, ghafula, hesabu zikashuka. Mwaka wa utumishi wa 1961 ulimalizika kwa upungufu wa asilimia 1. Katika miaka mitatu iliyofuata, mshuko uliongeza mwendo, kufikia asilimia 4, asilimia 5, na asilimia 12 kwa utaratibu uo huo, kabla ya kupunguza mwendo kufikia asilimia 3 katika 1965 na asilimia 1 katika 1966. Kufikia wakati huo, hesabu ya wahubiri ilikuwa imeshuka kufikia 265 kutoka kilele cha 382 katika 1960. Ni jambo gani lilikuwa limetukia?
Kwa kutazama nyuma yaonekana kwamba Shule ya Huduma ya Ufalme iliyoongozwa katika 1961 ilianzisha wakati wa kupepeta. Darrow Stallard, ambaye kufikia wakati huo alikuwa ametumikia akiwa mwangalizi wa mzunguko kwa miaka mingi, aliongoza darasa la shule hiyo katika Chiang Mai na jingine katika Bangkok. Wakati wa mtaala huo, ustahili wa wahubiri wa Ufalme ulipitiwa. Waangalizi wa kundi waliohudhuria mtaala huo, pamoja na baadhi ya mapainia wa pekee na wamisionari, walifanywa watambue kwamba wale ambao hushiriki pamoja na Mashahidi wa Yehova katika utendaji lazima waongoze maisha zinazopatana na matakwa ya Kimaandiko. Nyakati fulani jambo hilo lilikuwa limesahauliwa. Baadhi ya watu wapya wenye kupendezwa walikuwa wameanza utumishi wa shambani kabla ya kustahili Kimaandiko. Wengine walikuwa wamebatizwa hata kabla ya kunyoosha mambo yao ya ndoa.
Shauri lililopokewa kwenye shule hiyo lilipotumiwa, baadhi ya wahubiri walipatikana kuwa hawakustahili tena kuhubiri. Baadhi yao hata hawakutaka kufanya mabadiliko. Kwa hiyo, wakati wa 1962, jumla ya watu 9 walitengwa na ushirika, na wakati wa miaka minne iliyofuata, ilikuwa lazima kutenga na ushirika 25 zaidi—hesabu za juu isivyo kawaida katika Thailandi. Huo ulikuwa wakati wenye kuvunja moyo kwa walio dhaifu zaidi, hiyo ikifanya baadhi yao kuwa wasiotenda. Hata hivyo tukio katika 1963 liliwachangamsha waaminifu.
Kusanyiko Kubwa Zaidi Lililopata Kufanywa
Shangwe kuu ilitawala wakati tangazo liliposikiwa kwamba Bangkok lingetiwa ndani ya “Habari Njema za Milele” makusanyiko yaliyofanywa kuzunguka dunia katika 1963. Sasa kwenye mmojawapo makusanyiko yao wenyewe, akina ndugu katika Thailandi wangeweza kujionea wenyewe mweneo wa kimataifa wa tengenezo la Yehova. Kutayarishia kusanyiko na kufanya mipango iliyohitajiwa kwa wajumbe wa kigeni karibu 600 ilikuwa kazi kweli kweli, kwa kuwa wageni walikuwa na hesabu kubwa kuliko wahubiri nchini kwa uwiano wa 2 kwa 1. Kukiwako 961 katika hudhurio kwa ajili ya hotuba ya watu wote iliyokuwa na kichwa “Wakati Mungu ni Mtawala Juu ya Dunia Yote,” hilo lilikuwa ndilo kusanyiko kubwa zaidi la Mashahidi wa Yehova lililopata kufanywa katika Thailandi.
Kabla ya tukio hilo ni mara chache sana kikundi kikubwa kadiri hiyo cha watalii kilipata kutembelea nchi hiyo. Si ajabu kwamba tukio hilo lilitangazwa kwa wingi sana kwa magazeti ya habari, redio, na televisheni! Kuwasili kwa Ndugu Knorr kulitangazwa kwa TV. Vituo sita vya redio vilitangaza programu za dakika 15 zilizokuwa zimetayarishwa. Magazeti ya habari yasiyopungua kumi yaliripoti habari za kusanyiko na miendo ya wasafiri hao wa kuzunguka ulimwengu. Kichwa kimoja kikubwa cha habari kilitangaza hivi kwa herufi kubwa: “Ndio Uchukuzi Mkubwa wa Hewani Kupita Yote Tangu GI.”
Msaada Kutoka Ufilipino
Katika Desemba 1963, wakati Denton Hopkinson kutoka tawi la Ufilipino katika Manila alipotembelea Thailandi akiwa mwangalizi wa eneo la dunia, aliona uhitaji wa wafanyakazi wenye ujuzi ili kuchochea ndugu wenyeji katika huduma ya shambani. Wakati ule Shule ya Gileadi ilikuwa ikikazia kuzoeza waangalizi, na wamisionari wengine hawakuwa wametumwa nchini kuchukua mahali pa walio wengi wa wamisionari waliokuwa wameondoka Thailandi. Kwa hiyo Ndugu Hopkinson alipendekeza kwamba mapainia wa pekee kutoka Ufilipino watumwe Thailandi kusaidia katika kazi. “Lakini,” alimwambia mwangalizi wa tawi, “tunaweza kuwatumia akina dada peke yao. Tunahitaji ndugu zetu wote sisi wenyewe.” Baadaye, ndugu Wafilipino walitumwa pia.
Pendekezo hilo lilikubaliwa na Sosaiti, na kufikia katikati ya 1964, dada wawili wa kwanza—Rosaura (Rose) Cagungao na Clara dela Cruz—wakawasili. Walipewa mgawo wakiwa mapainia wa pekee wafanye kazi katika lile eneo kubwa mno la mkoa wa Thon Buri, ng’ambo ile nyingine ya Mto Chao Phraya kutoka Bangkok. Mwaka mmoja baadaye waliletwa chini ya mpango wa misionari hata ingawa hawakuwa wamesomea Gileadi. Matukio yenye furaha yalifuata wakati Dada Cagungao alipoolewa na mwangalizi wa tawi, Paulo Engler, na Dada dela Cruz akawa mke wa Diego Elauria, misionari mwingine Mfilipino katika Thailandi.
Ikatukia kwamba, wale wamisionari kutoka Ufilipino walichangamana vizuri sana katika eneo la Asia ya Kusini-mashariki, wakifanana sana na watu wenyeji na kuweza kufanya kazi katika eneo bila kutambulikana sana kama wamisionari Wazungu au Waamerika. Hivyo, kwa muda wa miaka iliyopita, wamisionari zaidi kutoka Ufilipino walitumwa Thailandi na pia katika Vietnamu Kusini, Laosi, na nchi nyinginezo za Asia. Kwa sasa, kuna Wafilipino kumi wanaotumikia wakiwa wamisionari katika Thailandi.
Matatizo ya Kusalimu Bendera
Kazi ilikuwa ndipo tu imeanza kuongeza mwendo tena wakati katika Oktoba 1966 suala la kusalimu bendera lilipotokezwa mbele. Mapema kidogo, katika Novemba 1965, mwana wa mhubiri aliye peke yake alikataa kwa sababu ya dhamiri kushiriki katika sherehe ya bendera. Wakati baba yake alipoeleza jambo hilo kwa njia ambayo kidogo haikuwa ya busara, mkuu wa wilaya na ofisa wa elimu wa sehemu hiyo walitoa ripoti kwa Wizara ya Elimu, na kutia ndani nakala ya kitabu “Let God Be True.” Likiwa kama jibu la barua yenye uharaka sana iliyopelekewa ofisi ya tawi katika Oktoba 31, 1966, mwangalizi wa tawi, Paul Engler, na msaidizi wake, Guy Moffatt, walienda kwenye Idara ya Mambo ya Kidini katika Wizara ya Elimu.
Ndugu hao walimweleza mkurugenzi mkuu wa idara kwamba Mashahidi wa Yehova huheshimu bendera ya nchi yoyote wanamoishi, kwamba wanaonyesha heshima hiyo kwa kutii sheria za nchi hiyo, lakini kwamba huomba ruhusa ya kutoshiriki kufanya tendo la ibada kuelekea mfano. Ibada kama hiyo inapingana na sheria ya Mungu wetu, Yehova. (Mt. 4:10) Hata hivyo, mkuu huyo alisisitiza kwamba taifa liliwekwa mbele ya dini na akashikilia kwamba kusalimu bendera hakuhusiani na ibada ya kidini.
Miezi mitano baadaye, Ndugu Engler aliitwa na CID ili ahojiwe. Jambo hilo lilikuwa limepitishwa kwa Wizara ya Mambo ya Ndani. Kwa muda wa saa nane, zilizochukua siku tatu, Ndugu Engler alimweleza kirefu kapteni wa polisi mwenye kupeleleza msimamo wetu juu ya suala ya kusalimu bendera. Pia alisimulia kwamba nchi nyingi huwavumilia Mashahidi wa Yehova wakati wowote suala hilo linapotokea.
Baada ya kusikiliza kutoa sababu kwa Ndugu Engler kwa makini, kapteni huyo wa polisi aliamua kwamba watoto wa Mashahidi wa Yehova katika Thailandi wanahitaji tu kusimama wakiwa kimya wakati wale wanafunzi wengine wanapofanya sherehe ya kusalimu bendera. Halafu akapelekea wenye mamlaka ya juu zaidi ripoti ili ifikiriwe.
Uamuzi ungekuaje? Katika nyakati zilizopita, sikuzote wakuu wa serikali walikuwa wamekuwa wenye kufuata haki na wenye fadhili kwa Mashahidi wa Yehova. Sala nyingi zilitolewa “kwa ajili ya watu wote; kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka,” ili watu wa Mungu waendelee ‘kuishi maisha ya utulivu na amani,’ waendelee na kazi bila kuzuiwa. (1 Tim. 2:1, 2) Mwaka mmoja hivi baadaye jibu lilifunuliwa kwa njia isiyo ya moja kwa moja.
Siku moja au mbili tu baada ya Ndugu Engler kumaliza mahoji na CID, wamisionari watano wapya waliwasili kutoka Ufilipino. Ingekuwa lazima maombi yao ya kuwa na cheo cha wahamiaji nchini yakubaliwe na CID. Kwa mwaka mzima, hakukuwa na jibu. Kisha, katika Aprili 1968, wamisionari hao waliarifiwa kwamba maombi yao yalikuwa yamekubaliwa. Huo ulikuwa pia wonyesho wa jinsi wenye mamlaka walivyokuwa wameamua juu ya kile kisa cha kusalimu bendera. Lakini hakukuwa kumekuwa na jibu rasmi.
Vichapo Viwili Vyapigwa Marufuku
Mmoja wa wahubiri katika mkoa wa mashambani alipata kuona tangazo likiwa limebandikwa kwenye jengo la mambo ya kijamii. Ilikuwa amri kutoka kwa mkurugenzi mkuu wa Idara ya Polisi ikisema kwamba chapa za Kithai za “Let God Be True” na “Habari Njema Hizi za Ufalme” zilikuwa zimepigwa marufuku katika Ufalme wa Thailandi. Lilikuwa jambo lenye kushtua! Amri hiyo ilikuwa imechapishwa katika Machi 29, 1968, lakini Sosaiti haikuwa imejulishwa. Hata hivyo, kufikia wakati huo kitabu “Let God Be True” tayari kilikuwa hakimo akibani. Nakala zaidi ya 13,000 zilikuwa zimeangushwa wakati wa miaka 16 ya kukitumia. Kwa nini kijitabu “Habari Njema” kipigwe marufuku? Ni jambo gani ambalo lingeweza kufikiriwa kuwa lenye kuchukiza? Zaidi ya hilo, kwa sababu ya urahisi na unyoofu wacho, akina ndugu walipenda sana kutumia kijitabu hicho kuanza mafunzo ya Biblia.
Mkuu ambaye akina ndugu walionana naye alionyesha kusikitika sana alipokuwa akitaja kwamba fungu la maneno lenye kutokeza tatizo hilo ilikuwa sentensi hii: “Ni makosa kwa mwanadamu kujaribu kufanya sanamu ya mfano wa Mungu na kuiabudu.” Alieleza kwamba kwa kuwa Wabuddha hupenda kufanya sanamu ya mfano wa Buddha, huenda wengine wakachukizwa na sentensi hiyo. Wakati Ndugu Engler alipomwambia kwamba kijitabu hicho hakiongei juu ya Buddha hata kidogo bali kinaongea juu ya Yehova Mungu, Muumba, mkuu huyo alijibu, “Basi mwapaswa kusema hivyo.” Hangekataa kama neno “Muumba” lilitumiwa badala ya “Mungu.” “Lakini,” akaongeza, “itawalazimu kubadili jina la kijitabu hicho pia kwa sababu jina hili limekwisha pigwa marufuku sasa.”
Kwa hiyo, tangu wakati huo, jina la kijitabu “Habari Njema” katika Kithai limekuwa Lazima Habari Njema Ihubiriwe.
Eneo Lenye Kuzaa Tunda Katika Kambi ya Wakimbizi
Baada ya mabadiliko ya serikali katika Vietnamu Kusini, Kambodia, na Laosi katika 1975, wakimbizi walimiminika Thailandi—kutia na wengi wa ndugu Walao ambao waliona lazima ya kuondoka katika makao yao. Katika Kituo cha Wakimbizi Walao kilichokuwa karibu na Nong Khai katika kingo za Mto Mekong, kundi lilikuwa limekuwa likitenda kwa wakati fulani, wahubiri 20 na zaidi wakiripoti. Akina ndugu walitumia vizuri wakati wao wakitolea wakimbizi wengine ushuhuda, wengi wao wakiwa hawajapata kamwe kusikia juu ya habari njema katika nchi ya kwao. Hesabu kubwa kidogo ya watu wenye kupendezwa walianza kuhubiri, na kadhaa wakabatizwa walipokuwa katika kambi hiyo.
Mwanamke mmoja Mlao mwenye umri mkubwa, aliyekuwa Mbuddha, alialikwa na mmoja wa wamisionari wa Jumuiya ya Wakristo ahudhurie kanisa katika kambi hiyo. Alikuwa mzoevu wa kutafuna popoo naye alijaribu sana kuacha zoea hilo bila kufanikiwa. Alimtajia misionari huyo tatizo lake, ambaye alijibu, “Usijali. Unaweza kutafuna popoo au kuvuta sigareti na bado uwe Mkristo. Beba tu chombo chako cha kutemea mate uje nacho kanisani.” Kwa kuwa mwanamke huyo mwenye umri mkubwa aliona kutafuna popoo kuwa jambo baya kiadili alifikiri hivi nafsini mwake, “Ikiwa wanakuruhusu kutafuna popoo au kuvuta sigareti, labda wanakuruhusu kusema uongo au kuiba pia.” Kwa hiyo hakwenda kwenye kanisa lao. Si muda mrefu baada ya hapo, mmoja wa dada zetu alionana naye katika utumishi wa shambani. Karibu mara hiyo mwanamke huyo mwenye umri mkubwa akauliza: “Unaweza kutafuna popoo katika dini hii?” Jibu lilipokuwa la, alitambua kwamba Mashahidi ni tofauti, naye akaanza kujifunza Biblia.
Mwanamke huyo akamwambia rafiki yake mwenye umri wa miaka 65 aliyokuwa akijifunza. Bibi huyo, ambaye pia alikuwa mzoevu wa kutafuna popoo, hakuweza kusoma. Kwa hiyo dada yetu na yule mwanamke mwenye umri mkubwa wakamfundisha jinsi ya kusoma na kuandika. Mabibi hao wote wawili wenye kupendezwa wakaanza kuhudhuria mikutano kwa ukawaida. Hata hivyo, ilikuwa vigumu sana kwao kushinda tatizo lao la kutafuna popoo. Haikuwa mpaka walipojifunza ile sura juu ya matumizi ya madawa ya kulevya katika kitabu Amani ya Kweli na Usalama kwamba wakaweza kupata nguvu ya kuacha zoea hilo. Wakati mwangalizi wa mzunguko alipotembelea kundi katika kambi hiyo, walimwambia jinsi walivyojisikia wakiwa safi sasa, na kwa fahari wakafumbua vinywa vyao kwa tabasamu kubwa ili kuonyesha meno yao, ambayo hayakuwa meusi tena. Wote wawili wakabatizwa kambini humo.
Kwa kuwa wale ndugu watatu waliokuwa wakitumikia mmoja akiwa mzee na wale wengine wakiwa watumishi wa huduma wa kundi hilo hawangeweza kuondoka kambini ili kuhudhuria Shule ya Huduma ya Ufalme, shule hiyo ikaja katika kambi. Mwangalizi wa mzunguko aliwatembelea na kujifunza nao mtaala wote.
Mwishowe, ndugu wote kambini walihamishiwa nchi nyinginezo na kupewa makao. Katika mahali kadhaa, vikundi na makundi yenye kusema Kilao yamesitawi kutokana na kikundi hicho hodari cha Mashahidi wakimbizi.
Ukamilifu Wajaribiwa kwa Suala la Damu
Mashahidi wa Yehova hukataa damu kwa sababu za kidini zenye kutegemea Biblia. (Mdo. 15:28, 29) Kwa kuwa matumizi ya damu kwa matibabu ya tiba lingali zoea la kawaida, na katika Thailandi maoni ya daktari hukubaliwa kwa ujumla na wagonjwa bila swali, ndugu wengi wamekabili majaribu makali ya ukamilifu.
Kwa mfano, Araya Tanchakun, painia wa pekee ambaye alikuwa na mimba, alianza kuvuja damu ghafula. Alipimwa akapatikana na hali ambayo kondo la nyuma lilikuwa limeshuka na kufunga njia ya kutokea mtoto. Alipewa mchanganyo wa chumvi, lakini madaktari wakamwambia kwamba ingekuwa lazima kumtia damu ikiwa angeendelea kuvuja damu.
Alimweleza msimamo wake kila daktari aliyekuja kazini. Mmoja wao, aliyesema kwamba aliwajua Mashahidi wa Yehova kutoka Amerika alidokeza kwamba damu itiwe kwa siri, ‘bila kuliambia tengenezo.’ Dada Araya alikazia kwamba uamuzi wake ulikuwa jambo kati yake na Yehova, si na wanadamu. Daktari mwingine alitaja kisa cha watawa wanaume Wabuddha, ambao kwa kawaida hawangeguswa na mwanamke. Lakini wakiwa wagonjwa hospitalini, waweza kuhudumiwa na wauguzi wa kike. “Je, hakuna hali fulani kama hizo katika dini yenu zinazoruhusika?” akauliza. Jibu lilipokuwa la, alionyesha sikitiko kwamba katika Thailandi madaktari hawawezi kupata amri ya mahakama ili kutumia damu. Daktari hakumpa dada tumaini kubwa, hasa kwa kufikiria kwamba wakati wa kuzaa ulikuwa unakaribia. Alipoondoka hospitalini siku chache baadaye, wafanyakazi wa hospitali walimwambia kwamba wangemkubali kurudi ikiwa tu atakubali damu. Hivyo, jaribu lake halikuwa limekwisha.
Phonthipa Teeraphinyo, dada mmoja kutoka kundi jingine, alimjulisha Araya kwa daktari aliyekuwa amemsaidia kuhusiana na suala la damu. Juma moja hivi baadaye, Araya akapata maumivu ya kuzaa na akaanza kuvuja damu tena. Wakati daktari huyo katika ile hospitali ya pili alipoona hali yake dhaifu, alihangaika na kubadili nia yake. Aliambia Araya na mume wake kwamba hata kumpa tu dawa ya kumpoteza fahamu akiwa katika hali hiyo huenda kukamuua. Hata hivyo, waliendelea kusimama imara. Mume wake alimwambia daktari aendelee bila kutumia damu naye angemshukuru hata kama mke wake angekufa. Wakati daktari alipoona kwamba walikuwapo Mashahidi 30 hospitalini waliokuwa wakingojea kwa hangaiko, alivutiwa naye akakubali kufanya upasuaji bila damu ili kumtoa mtoto.
Kila mtu alifurahi na kufarijika wakati Araya alipozaa msichana mwenye afya, mtoto wake wa nane, na yeye mwenyewe alikuwa hajambo. Akijua kwamba hao wenzi wa ndoa walikuwa wahubiri wa wakati wote kwa miaka mingi, na kwa kuvutiwa sana na wonyesho huo wa imani, daktari huyo hata alikataa kukubali malipo yoyote.
‘Nikifa, Msilie’
Majuma machache baada ya Araya kuondoka hospitalini, Phonthipa, yule dada aliyemjulisha kwa daktari huyo mwenye kusaidia, alimtembelea kumshukuru kwa kuheshimu masadikisho yetu ya kidini, na kwa kufanya upasuaji bila damu. Daktari huyo alipata kuona kwamba rangi ya ngozi ya Seri, mwana wa Phonthipa mwenye umri wa miaka tisa, ilionekana kufifia. Uchunguzi wa damu uliofuata ulifunua kwamba alikuwa na ugonjwa wa kupungukiwa damu. Matibabu pekee yaliyojulikana kwa ugonjwa huo, akasema daktari, yalikuwa kutiwa damu.
Seri alitendaje aliposikia hivyo? “Hata kama nitalazimika kufa leo au kesho, mimi sitakubali damu yoyote, hata tone moja,” akamwambia daktari. Si kwamba tu alijua sheria ya Mungu juu ya damu bali alikuwa tayari pia kuitegemeza chini ya hali zote. Aliposikia bila kukusudiwa madaktari wakisema kwamba imani ya mama yake juu ya damu haikuwa ya kiakili, Seri alimtetea, akisema: “Msimlaumu mama yangu! Nyinyi madaktari mnalaumu tu kwa sababu hamjajifunza Neno la Mungu.”
Majuma sita hivi baada ya hali ya Seri kupimwa, alilazwa hospitalini. Alikataa damu kabisa kabisa ujapokuwa mkazo wenye kushawishi kutoka kwa madaktari. Alizidi kuwa dhaifu naye akapewa dawa ya kupunguza maumivu yake. Hata hivyo, muda wote wa kuteseka kwake, Seri alionyesha imani yenye kusifika. Bila kukoma, aliongea juu ya tumaini la kuishi katika Paradiso ya kidunia inayokuja. Katika pindi moja alimwambia mama yake: “Mama, nikifa, mwambie Baba asilie, wala wewe, Mama, usilie, bali iweni wachangamfu kwa sababu tuliweza kupita jaribu la Shetani.” Seri alikufa akiwa mwaminifu, akiachia wengine wachanga kielelezo chema katika kudumisha ukamilifu chini ya jaribu.—Mit. 22:6.
Vijana Wachukua Msimamo kwa Ajili ya Kweli
Katika Thailandi utayari ambao kwa huo vijana wengi hukubali kweli na kuwa wahubiri hutofautiana sana na kutojali kwa watu wazima walio wengi, ambao wanashikamana sana na mapokeo. Ile hali kubwa zaidi ya kuwa na akili zilizofunguka ya kizazi kichanga zaidi imesaidia baadhi yao waanze kujifunza Biblia na kuwa Mashahidi kwa ajili ya Yehova. Wengi wao wanalazimika kupigania sana kweli, kwa kuwa wazazi wao na watu wengine wa ukoo hupinga. Ustahimilivu huo kwa kawaida huwasaidia kuwa wenye nguvu kiroho.
Wahubiri wengi vijana wanatoa ushuhuda mzuri katika shule kwa mwenendo wao mwema na kwa kuchukua msimamo usioridhiana kwa ajili ya ibada ya kweli. Mara moja kwa mwaka, katika siku ya wai khru shule zote hupangia programu ya pekee, yenye kuambatana na sherehe za kidini, ambazo katika hizo wanafunzi hutoa heshima inayokaribia ibada kwa walimu wao. Kwenye shule moja, ndugu watatu vijana walitangulia kumweleza mwalimu mkuu wa shule yao sababu kwa nini wao hawangeweza kushiriki katika programu hiyo na wakaomba waruhusiwe kutoshiriki. Hata hivyo, walitakwa wawepo lakini walipewa fursa ya kuonyesha heshima yao kwa walimu bila kushiriki katika sherehe ya kidini.
Katika siku ya wai khru, hao watatu waliitwa baada ya sherehe kwisha. Walimu wapatao 70 kufika 80 waliketi jukwaani mbele ya wanafunzi zaidi ya elfu moja. Katika hotuba fupi, ndugu zetu walionyesha kwamba Mashahidi wa Yehova hutenganisha jambo la kuonyesha heshima wanayostahili walimu na ibada. Wanaweza na wanapaswa kuonyesha heshima popote na nyakati zote, hata nje ya makao ya shule. Hata hivyo, ibada yao inatolewa kwa Muumba tu, Yehova Mungu. Walimu na wanafunzi wenzi walipenda waliyosikia. Ndugu hao walipomaliza, jumba lilijawa sauti ya kishindo cha kupiga makofi.
Jitihada za Kupata Kutambuliwa na Serikali
Mpaka miaka ya mapema ya 1970, wamisionari walio wengi ambao walipewa mgawo kwenda Thailandi walipewa ukazi wa kudumu. Katika njia nyingine pia, wenye mamlaka walikuwa na maoni yaliyofunguka na wenye kusaidia. Hata hivyo, akina ndugu walipojaribu kupata kuandikishwa kwa Sosaiti au kufanyiza shirika ili ‘kuthibitisha habari njema kisheria,’ wenye mamlaka walijibu kwamba hakuna uhitaji wa jambo hilo. (Flp. 1:7, NW) Mkurugenzi mkuu wa Idara ya Mambo ya Kidini alitaarifu hivi kwa barua katika 1974: “Kwa kuwa shirika hili lina kusudi kuu la kuhubiri na kufundisha dini ya Kikristo, hakuna uhitaji wa kufanyiza shirika. Mwaweza kuendelea na utendaji kulingana na kusudi hilo; hivyo, acheni kufanyiza shirika kwa sasa.”
Mwaka mmoja baadaye, wakati wamisionari wawili wapya walipopeleka fomu za kuomba vyeti vya kuhamia nchini, Sehemu ya Uhamiaji ilitaka barua kutoka kwa Idara ya Mambo ya Kidini ikihakikisha kwamba wenye kuomba vyeti walikuwa wamisionari. Hata hivyo, Idara ya Mambo ya Kidini ilikataa kutoa barua kama hiyo kwa msingi wa kwamba Watch Tower Society haikuwa imeandikishwa katika idara hiyo. Jibu kwa ombi jingine la kuandikishwa lilikuwa kama lile la wakati uliopita.
Bila kuwa na barua kutoka kwa Idara ya Mambo ya Kidini, wamisionari walipewa tu vyeti vya wasiohamia nchini, hiyo ikifanya wahitajiwe kufanya safari nyingi za kutoka nje ya nchi kati ya vipindi vya siku 90. Mwandishi mdogo wa elimu alithibitika kuwa mwenye kusaidia sana alipoendewa kuhusiana na hali hiyo yenye kusumbua. Katika 1980 alimwandikia barua mkuu wa uhamiaji, akitaarifu hivi: “Wizara ya Elimu imefikiria jambo lile na kuamua kwamba kwa kuwa Thailandi ina mwongozo wa kutoa uhuru wa kidini, . . . inafaa kuwapa wamisionari hao muda wa kukaa wa mwaka mmoja.”
Wamisionari hao walipewa muda mwingine wa mwaka kupitia usaidizi wa aliyechukua mahali pa mwandishi mdogo, ambaye alipendekeza kwamba Mashahidi wa Yehova wafanyize shirika chini ya sheria za nchi. Hivyo, katika 1982 Shirika la Kuendeleza Funzo la Biblia lilianzishwa na likaandikishwa, hesabu fulani ya ndugu wenyeji wenye ujuzi wakiwa washiriki wa halmashauri.
Shirika hilo, ambalo ni tengenezo la kitamaduni, linaweza kuwa na uenyeji wa mali, kutia na Majumba ya Ufalme. Hata hivyo, Idara ya Mambo ya Kidini imekataa kufikia sasa kutambua shirika hilo kuwa tengenezo la kidini. Kutambuliwa huko kungewezesha wamisionari wapya kuingia nchini. Ni nini sababu ya kukataa huko? Idara hiyo ina mwongozo wa kushauriana na viongozi wa matengenezo ya Jumuiya ya Wakristo ambayo tayari yametambuliwa katika Thailandi juu ya mambo yanayohusu dini ya Kikristo. Wakati mkutano ulipoitishwa wa kuzungumza ombi la Mashahidi wa Yehova, wakilishi wa matengenezo hayo (kutia na Roma Katoliki, Kanisa la Kristo katika Thailandi, Muungano wa Kikristo na Kimisionari, Baptisti, na Waadventisti wa Siku ya Sabato) walikubaliana kwa umoja kwamba wao ‘hawawezi kutoa kibali kwa Mashahidi Wakristo wa Yehova’ kwa sababu mafundisho na utendaji wa Mashahidi wa Yehova haupatani na wao. Tatizo hilo lingali linabaki.
Mkusanyiko wa Pekee Wachochea Utendaji
“Washika Ukamilifu” Mkusanyiko wa 1985 katika Bangkok ulikuwa wa pekee kwa sababu ulikuwa ndio mkusanyiko wa kwanza uliokuwa wa kimataifa kikweli tangu ule mkusanyiko wa 1963 uliofanywa kuzunguka ulimwengu. Wajumbe wa kigeni wapatao 400 kutoka nchi 18 walikuja Thailandi. Ndugu Lyman A. Swingle aliwakilisha Baraza Linaloongoza.
Sehemu yenye kutokeza ilikuwa utumishi wa shambani katika Ijumaa alasiri, wakati karibu wageni wote, asilimia kubwa yao wakiwa mapainia, walitoka nje pamoja na ndugu na dada zao Wathai nao wakawa karibu kuwazidi hesabu. Jambo hilo, pamoja na ile programu ya wakati ufaao, liliwavutia sana akina ndugu na likathibitika kuwa kichocheo cha kuzidisha utendaji wao kotekote nchini.
Wakati wa miezi iliyofuata mkusanyiko huo, vilele vipya katika wahubiri vilifikiwa. Katika Aprili 1986, hesabu ya mapainia wasaidizi 157 iliwakilisha ongezeko la asilimia 80 kupita kilele cha wakati uliopita. Kundi moja lenye wahubiri 91 lilikuwa na mapainia wasaidizi 48, kutia 6 kati ya wazee 7. Wahubiri 43 waliobaki waliripoti wastani wa saa 20.9 kwa mwezi huo.
“Mdogo” Awa Elfu
Utendaji wa Ufalme usiokatishwa ulianza katika Thailandi katika 1936, wakati Frank Dewar alipowasili Bangkok akiwa painia peke yake. Ilimchukua pamoja na mapainia wengine wageni miaka minne ya kazi ngumu kabla ya wahubiri wa kwanza wenyeji kubatizwa. Mpaka 1960, hesabu ya wahubiri ilizidi kuongezeka kufikia 382, kwa miaka iliyo mingi kwa mwendo wa zaidi ya asilimia 10. Wakati wa miaka ya 1960, kulikuwako upungufu kwa miaka kadhaa, lakini kufikia mwisho wa miaka hiyo ya 1960, hesabu ya wahubiri ilikuwa imerudia kiwango cha 1960. Halafu kukaja miaka ya maongezeko mpaka kufikia asilimia 20, kabla ya mwendo huo kusawazika kwa asilimia ya kati ya 3 na 5 kwa mwaka.
Mwaka baada ya mwaka, akina ndugu walikuwa wakingojea tukio lililokuwa limetumainiwa kwa muda mrefu—kupita alama ya 1,000 katika wahubiri. Ikawa hivyo katika Aprili ya 1988, wakati jumla ya 1,021 waliporipoti. Mwaka wa utumishi wa 1990 ulimalizika kwa ongezeko la asilimia 6 na kilele kisichopata kufikiwa cha 1,148. Kukiwa na mafunzo ya Biblia 1,169 yaliyokuwa yakiongozwa kila mwezi na hudhurio la Ukumbusho la 2,692 katika 1990, kuna uwezekano mzuri wa ukuzi zaidi. Kama ilivyoahidiwa, Yehova ‘anaiongeza mwendo.’—Isa. 60:22, NW.
Kazi ya mzunguko imetimiza fungu la maana katika kuwatia nguvu akina ndugu katika yale makundi 34 na vikundi mbalimbali vilivyo peke yavyo katika sehemu zote za nchi. Tawi limetimiza kwa sehemu uhitaji wa waangalizi wasafirio wenye sifa za ustahili kwa kuwapa migawo ndugu waliozoezwa Gileadi kwenye kazi ya mzunguko na wilaya. Lakini ndugu wenyeji vijana wenye nguvu na bidii, kama vile Phisek Thongsuk, wametumikia kwa miaka kadhaa sasa na ni msaada mkubwa kwa akina ndugu. Emilio Batul, aliyekuwa mwangalizi wa mzunguko kwa miaka 10 katika Ufilipino kabla ya kwenda Thailandi, amekuwa katika kazi ya kusafiri kwa miaka 22.
Kujitayarishia Mpanuko
Ofisi ya tawi ilipohamia kwenye ardhi ya Sosaiti yenyewe kwenye 69/1 Soi Phasuk, Sukhumwit Road, huko nyuma katika 1962, majengo hayo yalitosha na kuzidi. Tangu hapo, wale wafanyakazi 3 wa Betheli wameongezeka wakawa 16. Ardhi iliyopakana na ya Sosaiti yenye jengo la makao na bustani nzuri sana ilikodiwa katika 1985 iandae makao ili eneo la ofisi katika jengo la tawi liweze kupanuliwa. Lakini upesi nafasi hiyo iliyoongezwa ikathibitika kuwa isiyotosha. Baada ya kutafuta-tafuta sana akina ndugu walipata na wakanunua kisehemu cha ardhi katika sehemu iliyo nje tu ya Bangkok kilichokuwa kimesitawishwa karibuni. Ujenzi wa majengo hayo mapya, ambayo yatakuwa makubwa mara tano zaidi ya yale ya sasa, ulianza Februari 1990.
Kama ilivyo katika matawi mengine yote ya Sosaiti, Thailandi imekuwa na Halmashauri ya Tawi tangu 1976. Mwanzoni waliokuwa washiriki wa halmashauri hiyo ni Paul Engler akiwa mratibu, Elon Harteva, na Guy Moffatt. Tangu hapo Elon Harteva amerudi Finlandi. Ndugu Moffatt alikufa katika 1981 baada ya miaka 45 ya utumishi wa wakati wote, alikuwa ametumikia miaka 30 kati ya hiyo akiwa misionari na katika utumishi wa Betheli katika Thailandi. Kwa kuwa alikuwa ametumikia akiwa mwangalizi wa mzunguko na mwangalizi wa wilaya, alijulikana sana na akina ndugu kotekote nchini, naye alipendwa na kuheshimiwa kwa ajili ya kupendezwa kwake na akina ndugu kwa moyo mweupe na bidii yake kwa ajili ya ibada ya kweli. Baada ya kurudi kutoka Shule ya Gileadi katika 1980, Asawin Urairat akawa mshiriki wa kwanza mwenyeji wa Halmashauri ya Tawi. Halmashuri ya sasa yatia ndani pia Ernst Fischer, ambaye alihitimu kutoka Gileadi katika 1972, na Kaarle Harteva.
Kutazama Mbele kwa Uhakika
Ingawa Thailandi ilikuwa imeimarika sana katika mapokeo kwa karne nyingi, ibada ya kweli ya Yehova Mungu imeweka huru watu wengi kutoka utumwa wa dini ya Kibabuloni. Wale wa kwanza kuwa Mashahidi wa Mungu wa kweli katika nchi hiyo walikuwa hapo awali Wakristo wa jina tu. Hata hivyo, sasa, walio wengi ni watu waliokuwa na malezi ya Kibuddha. Kwa mfano, kwenye “Tumaini Lenye Uhai” Mkusanyiko wa Wilaya katika 1980, kati ya wale 36 waliobatizwa 26 walikuwa hapo awali Wabuddha. Ni mmoja tu aliyekuwa hapo awali Mkatoliki, na tisa walikuwa na wazazi wao katika kweli. Kupitia habari njema za Ufalme wa Mungu, watu wengi, kutia na waliokuwa hapo awali Wabuddha, wana taraja la kuingia katika aina ya uhuru ambao hakuna mwanadamu au serikali ya kibinadamu, hata ile ya “Nchi ya Walio Huru,” ingeweza kuleta—uhuru wa kutokamilika, magonjwa, na kifo.—Linganisha Yohana 8:32.
Mashahidi wa Yehova wataendelea kuhubiri habari hizi njema kila mahali. Ni kweli, kungali kuna kazi nyingi ya kufanywa katika Thailandi. Zaidi ya nusu ya ile mikoa 73 ingali ni maeneo yasiyogawiwa mtu. Lakini sisi tuna hakika kwamba kazi itafanywa kwa kadiri ambayo Yehova amekusudia. Nayo itakamilishwa. Mpaka wakati huo, sisi tutaendelea “kusema miongoni mwa mataifa: ‘Yehova mwenyewe amekuwa mfalme,’” na tutajitahidi kusaidia watu wengi kadiri iwezekanavyo wawe huru kikweli.—Zab. 96:10, NW.
[Maelezo ya Chini]
a Katika Thailandi ni desturi kuwaita watu kwa jina lao la kwanza.
[Chati katika ukurasa wa 252]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Thailandi 1,500
1950 89
1960 382
1970 380
1980 735
1990 1,148
Kilele cha Wahubiri
300
1950 14
1960 41
1970 69
1980 114
1990 195
Wast. Mapainia
[Sanduku/Ramani katika ukurasa wa 186]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
MYANMAR (Burma)
Bahari ya Andamani
TAHILANDI
Chiang Rai
Chiang Mai
Nan
Lampang
Nong Khai
Udon Thani
Khon Kaen
Nakhon Ratchasima
Bangkok
Nakhon Si Thammarat
Songkhla
Ghuba ya Thailandi
MALESIA
LAOS
Vientiane
Savabbakhet
KAMBODIA (Kampuchea)
Phnom Penh
VIETNAMU
[Sanduku]
THAILANDI
Mji Mkuu: Bangkok
Lugha Rasmi: Kithailandi
Dini Kubwa: Ubudha (Theravada)
Idadi ya Watu: 55,888,393
Ofisi ya Tawi: Bangkok
[Picha katika ukurasa wa 188]
Frank Dewar alisafiri katika Bahari Kuu ya Pasifiki Kusini akiwa katika mashua ndogo ya matanga ya meta 16 “Lightbearer.” Aliwasili Bangkok katika Julai 1936
[Picha katika ukurasa wa 191]
Mandhari ya Thailandi yenye kutofautiana kutoka Ghuba ya Phangnga, katika upande wa kusini, inayozungukwa na mapango ya milimani na mandhari ya pwani, mpaka eneo la hekalu la Buddha wa Emeraldi katika Bangkok likiwa na kichwa chalo chenye safu tatu cha jitu la hadithi za kubuniwa
[Picha katika ukurasa wa 193]
Willy Unglaube, juu, na Kurt Gruber walihubiri sehemu ya kaskazini ya nchi katika miaka ya mwisho-mwisho ya 1930
[Picha katika ukurasa wa 197]
Chomchai Inthaphan alipata kuwa mtafsiri katika 1941 naye alikuwa katika utumishi wa Betheli tangu 1947 hadi kifo chake katika 1981
[Picha katika ukurasa wa 199]
Buakhieo Nantha, mmojawapo Mashahidi wa kwanza mwenyeji wa nchi, alikuwa mhitimu wa Gileadi, katika darasa la 31
[Picha katika ukurasa wa 202]
George Powell, mwangalizi wa tawi wa kwanza, na Dona, mke wake
[Picha katika ukurasa wa 207]
Thailandi ilipata kuwa tawi katika Septemba 1, 1947. Ofisi ya tawi ya kwanza ilikuwa kwenye 122 Soi Decho, Bangkok
[Picha katika ukurasa wa 209]
Tayari kwa kazi ya kutoa ushuhuda kwa magazeti kwenye kusanyiko la mzunguko la kwanza katika Chiang Mai, Aprili 1948. Mstari wa nyuma upande wa kulia yuko Hans Thomas, painia katika Thailandi tokea 1941 hadi 1954
[Picha katika ukurasa wa 210]
Wamisionari kutoka darasa la 12 la Gileadi. Joseph E. (Bob) Babinski, Gerald (Jerry) Ross, Darrow Stallard, Donald Burkhart
[Picha katika ukurasa wa 214]
Karun Chuthiangtrong. Kiu chake kwa ajili ya kweli kilizimwaje?
[Picha katika ukurasa wa 220]
Seng Buawichai alikuwa na shaka juu ya fundisho la Utatu
[Picha katika ukurasa wa 224]
George na Carolyn Crawford wametumikia wakiwa wamisionari tangu 1963, katika Kambodia, Laosi, na Thailandi
[Picha katika ukurasa wa 227]
Suyi Chinesia, mhubiri wa mapema katika Laosi; Bunhoeng Lao, ndugu ya Siphanh; na Siphanh Lao, Malao wa kwanza Mbuddha kuwa Shahidi katika Vientiane
[Picha katika ukurasa wa 229]
Wamisionari wanahubiri kwa kutumia merikebu katika klong (mifereji) mingi ya Bangkok, 1956
[Picha katika ukurasa wa 230]
Bantoeng Chantraboon, mhitimu wa darasa la 31 la Gileadi, katika 1958, alitumikia akiwa mwangalizi wa mzunguko
[Picha katika ukurasa wa 231]
Somsri Darawan, mmoja wa mapainia wa pekee wa kwanza Wathai, alihitimu kutoka Gileadi katika 1953
[Picha katika ukurasa wa 232]
Ile ofisi ya tawi ya awali palikuwa mahali penye kuju-likana si kwa wamisionari hawa tu bali pia kwa wakaaji wengi wa Bangkok
[Picha katika ukurasa wa 233]
Ofisi ya tawi, 69/1 Soi Phasuk, Sukhumwit Rd., Bangkok. Betheli mpya imeratibiwa imalizike katika 1991
[Picha katika ukurasa wa 235]
Kwenye “Habari Njema za Milele” Kusanyiko la 1963 katika Lumpini Park, Bangkok, walikuwapo wajumbe wa kigeni wengi mara mbili kuliko wahubiri waliokuwa nchini
[Picha katika ukurasa wa 237]
Rosaura Engler (Cagungao) na Clara Elauria (dela Cruz), Wafilipino wawili wa kwanza kutumwa Thailandi watumikie wakiwa wamisionari. Kwa nini Wafilipino wakapewa mgawo kwenda Thailandi?
[Picha katika ukurasa wa 238]
Guy Moffatt alitumikia miaka 30 akiwa misionari na katika utumishi wa Betheli katika Thailandi
[Picha katika ukurasa wa 241]
Mashahidi Walao wakiwa njiani kwenda kuhubiri katika kambi ya wakimbizi. Kulikuwa na wakimbizi 20,000 wa kutembelewa
[Picha katika ukurasa wa 249]
Lyman Swingle wa Baraza Linaloongoza pamoja na mtafsiri wake.Paul Engler kwenye mkusanyiko katika Bangkok katika 1985
[Picha katika ukurasa wa 251]
Halmashauri ya Tawi imetumika kwa jumla ya muunganisho wa miaka 99 katika utumishi wa wakati wote. Kutoka kushoto kwenda kulia, Paulo Engler, Asawin Urairat, Ernst Fischer, na Kaarle Harteva