Rwanda
RWANDA ni mojawapo ya nchi ndogo zaidi barani Afrika. Pia ni mojawapo ya nchi maridadi sana. Nchi hii inayoitwa Nchi ya Milima Elfu Moja ina milima, misitu, maziwa, na maporomoko ya maji, na vilevile unamna-namna wa mimea na wanyama. Milima mikubwa ya Virunga, iko katika eneo lenye milima lililo katika sehemu ya magharibi inayopakana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongoa na katika sehemu ya kaskazini ya Uganda. Mlima Karisimbi, ambao mara nyingi huwa umefunikwa na theluji, ni mlima wa volkano isiyotenda na ndio mrefu zaidi katika safu hii ya milima. Una urefu wa mita 4,480. Sehemu za chini ya milima hiyo, kuna msitu wa mvua wenye mianzi mingi, ambamo tumbili walio katika hatari ya kutoweka hubembea kwa uhuru kwenye matawi na mizabibu. Ni katika mazingira haya yenye miti mingi ambamo pia mojawapo ya hazina zenye thamani nchini Rwanda inapatikana, yaani, sokwe wa milimani.
Mimea ya kipekee na majani yenye kunawiri huenea hadi fuo za Ziwa Kivu na Msitu wa Nyungwe. Kuna sokwe, kima wa rangi nyeusi na nyeupe, na wanyama wengine zaidi ya 70 katika msitu huo. Kuna spishi 270 hivi za miti na karibu spishi 300 za ndege. Vipepeo wengi na okidi huchangia uzuri wa hifadhi hiyo.
Kutoka katikati mwa Msitu wa Nyungwe, kuna kijito cha maji kinachotiririka kuelekea upande wa mashariki. Hatua kwa hatua vijito na mito mingine hujiunga nacho na hatimaye maji yake hutiririka katika Ziwa Viktoria. Kutoka hapo, maji hayo huteremka kwa nguvu na kwa kasi sana ili kuendelea na safari yake ndefu kuelekea upande wa kaskazini kupitia Ethiopia, Sudan, na mwishowe Misri, ambapo yanaingia katika Bahari ya Mediterania. Mto Nile unaoanza ukiwa kijito katika milima yenye miti mingi ya Afrika ya kati, husafiri umbali wa kilomita 6,825 hivi, na hivyo kuufanya Mto huo kuwa mmoja wa mito mirefu zaidi duniani.
NYAKATI ZENYE TAABU
Hata hivyo, inasikitisha kwamba nchi hiyo ndogo ya Rwanda imepitia jeuri yenye kutisha. Mamia ya maelfu ya wanaume, wanawake, na watoto walichinjwa kikatili katika mauaji mabaya zaidi ya jamii nzima-nzima kuwahi kutokea katika nyakati za kisasa. Visa vya jeuri isiyozuiliwa vilitangazwa duniani pote na kuwafanya wengi kushangazwa na unyama wa mwanadamu kumwelekea mwenzake.—Mhu. 8:9.
Mambo yalikuwaje kwa watumishi waaminifu wa Yehova wakati huo mgumu na katika miaka ya baadaye? Kama vile tu kijito cha maji kutoka Msitu wa Nyungwe kinachoonekana kuwa hakifai kinavyoshinda vizuizi vyote, kutia ndani joto kali la jua, na kuwa mto mkubwa, ndivyo watu wa Yehova nchini Rwanda walivyovumilia mateso na wanaendelea kumtumikia Mungu. Wamevumilia mateso makali na matatizo mengi na kwa njia hiyo, wamewatia moyo akina ndugu na dada zao ulimwenguni pote. Unaposoma habari za Rwanda, utapata masimulizi yenye kugusa moyo ya upendo, imani, na ushikamanifu. Tunatumaini kwamba masimulizi haya yatakutia moyo uthamini hata zaidi uhusiano wako pamoja na Yehova na kuuonea fahari undugu wa Kikristo.
JITIHADA ZA AWALI ZA KUHUBIRI NCHINI RWANDA
Ripoti ya kwanza kuhusu kazi ya kuhubiri habari njema nchini Rwanda iliandikwa katika Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova cha 1971 (Kiingereza). Kilisema: “Machi mwaka huu [1970] mapainia wa pekee wawili waliweza kuingia Rwanda na kuanzisha kazi ya kuhubiri katika mji mkuu wa Kigali. Wamepata watu wenye shauku na wanaoitikia ujumbe wa Ufalme, na tayari mtu mmoja anayependezwa ameanza kuhubiri. Mapainia hao tayari wameanzisha mafunzo kumi miongoni mwa watu wachache wanaozungumza Kiswahili. Sasa wanajitahidi sana kujifunza Kinyarwanda ili wawahubirie watu wengi zaidi.”
Mapainia hao wawili waliotajwa katika ripoti hiyo ni Oden Mwaisoba na mke wake, Enea, kutoka Tanzania. Kwa sababu hawakujua Kinyarwanda, walianza kwa kuwatembelea watu wanaozungumza Kiswahili, wengi wao kutoka Kongo au Tanzania. Kufikia Februari 1971, kulikuwa na wahubiri wanne waliokuwa wakiripoti, lakini hakukuwa na machapisho yoyote katika Kinyarwanda, na ni watu wachache tu waliojifunza kweli kwa sababu wahubiri hao hawakujua Kinyarwanda.
Stanley Makumba, mwangalizi wa mzunguko mwenye ujasiri aliyekuwa akitumika nchini Kenya, alizuru Rwanda kwa mara ya kwanza mwaka wa 1974. Akumbuka hivi: “Kulikuwa na magari machache kutoka mpaka wa Uganda na Rwanda, kuingia Ruhengeri, nchini Rwanda. Nililazimika kusimama ndani ya lori lililojaa watu hivi kwamba sikuweza kusogeza miguu yangu. Mke wangu aliketi mbele na dereva. Tulipofika, ilikuwa vigumu mke wangu kunitambua kwani uso na nywele zangu zilijaa vumbi. Nilikuwa na maumivu makali ya mgongo kutokana na safari hiyo hivi kwamba kwa muda wa juma moja kabla ya kusanyiko dogo la mzunguko na hata katika kusanyiko lenyewe, nililazimika kutoa hotuba nikiwa nimeketi. Sikuweza kuwajulisha akina ndugu wakati ningewasili ili kuwatembelea kwa sababu usafiri haukutegemeka!”
MWENYEJI AREJEA
Wakati huo, Gaspard Rwakabubu, ambaye ni Mnyarwanda, alikuwa fundi wa magari katika migodi ya shaba nchini Kongo. Anasema: “Mnamo 1974, nilihudhuria Shule ya Huduma ya Ufalme mjini Kolwezi. Michael Pottage, aliyekuwa mmoja wa walimu, alitaja kwamba ofisi ya tawi ya Kinshasa ilikuwa inatafuta mzee wa kutaniko aliye Mnyarwanda ambaye angependa kurudi nchini kwao kusaidia katika kazi ya kuhubiri. Nikawaza, niende au nisiende? Nikasema kuwa ningezungumza na mke wangu, Melanie.
“Wakati huohuo, mkubwa wangu kazini alikuwa tu amepanga niende Ujerumani kupata mafunzo zaidi. Nilikuwa nimefanya vema kazini na niliongezwa mshahara kwa ukawaida. Hata hivyo, ilituchukua muda mfupi tu kufanya uamuzi. Nikamwambia Ndugu Pottage kwamba tuko tayari kurudi Rwanda. Mkubwa wangu kazini alishangaa. Akaniuliza: ‘Mbona usiwe Shahidi wa Yehova hapa? Kwa nini urudi Rwanda?’ Hata ndugu fulani wasiokuwa na nia mbaya walijaribu kunivunja moyo. Wakaniambia: ‘Una watoto wanne. Soma Luka 14:28-30, uketi chini na ufikirie kwa uzito.’ Hata hivyo, hatukuyumba-yumba.
“Mkubwa wangu kazini alitulipia gharama zote za usafiri wa ndege kurudi Rwanda. Tulipofika Kigali, mnamo Mei 1975, tulikodi nyumba ya matofali yenye sakafu ya udongo, tofauti kabisa na nyumba nzuri tuliyoishi nilipokuwa nikifanya kazi katika kampuni ya migodi na ambayo ilikuwa na kila kitu. Hata hivyo, tulikuwa tumejitayarisha na tuliazimia kabisa kufanikiwa.”
Kwa kuwa mapainia wa pekee kutoka nchi nyinginezo walitumia Kiswahili katika mawasiliano, watu wengi walifikiri kwamba mapainia hao walikuja kufundisha Kiswahili. Maoni hayo yalibadilika Gaspard na familia yake walipowasili kwa kuwa walitumia Biblia ya Kinyarwanda kuwafundisha watu kweli za Ufalme.
Isitoshe, Ndugu Rwakabubu alitafsiri broshua “Habari Njema Hizi za Ufalme” yenye kurasa 32 katika Kinyarwanda. Ilichapishwa mwaka wa 1976 na kusomwa na watu wengi. Watu waliisoma waliposafiri na walipokuwa barabarani. Matumizi ya jina Yehova yaliwachochea wengi kutaka kujua zaidi.
WANYARWANDA WAIKUBALI KWELI
Wakati huo, kulikuwa na wahubiri 11 tu nchini, na wengi wao hawakuwa raia wa Rwanda. Justin Rwagatore alikuwa miongoni mwa Wanyarwanda wa kwanza kujifunza kweli. Alianza kujifunza pamoja na mapainia wa pekee kutoka Tanzania wakitumia Kiswahili kwa sababu hawakujua Kifaransa au Kinyarwanda. Mtu huyo mchangamfu na mwenye urafiki, alibatizwa mwaka wa 1976 na aliishi Save, ambapo mfalme wa Rwanda alikuwa amewaruhusu wamishonari wa Katoliki kujenga misheni mwaka wa 1900. Justin anakumbuka kwamba watu walitaka kujua kile ambacho Biblia inafundisha hasa. Hata hivyo, viongozi wa dini walikuwa wakatili kuelekea Mashahidi wa Yehova na waliwakataza wafuasi wao wasiwasikilize wala kupokea machapisho yao.
Ferdinand Mugarura, ndugu mwenye bidii, alikuwa pia mmoja wa Wanyarwanda wa kwanza kukubali kweli. Mwaka wa 1969, akiwa anaishi mashariki mwa Kongo, alipata nakala ya kitabu Kweli Iongozayo Kwenye Uzima wa Milele katika Kiswahili. Baadaye, alipojua mahali ambapo Mashahidi waliokuwa karibu walipatikana, yeye na wengine wawili walitembea kilomita 80 kila Ijumaa ili wahudhurie mikutano na kujifunza Biblia, na kisha kurudi nyumbani siku ya Jumatatu. Ferdinand alibatizwa mwaka wa 1975, siku ileile ambayo mwanafunzi wake mmoja wa Biblia alibatizwa. Aliwekwa kuwa painia wa pekee nchini Rwanda mnamo 1977 na anakumbuka akiambiwa kwamba mwaka uliotangulia, kusanyiko la mzunguko lilifanywa sebuleni mwa nyumba ya Rwakabubu. Watu 34 walihudhuria na watatu wakabatizwa.
WAMISHONARI WANYIMWA VIBALI VYA KUINGIA NCHINI
Kwa kuwa sikuzote Baraza Linaloongoza linahangaikia shamba la ulimwenguni pote, lilikuwa limewatuma wamishonari nchini Rwanda hapo awali. Mnamo 1969, wahitimu wanne wa darasa la 47 la Shule ya Gileadi walitumwa kutumika huko.
Nicholas Fone akumbuka: “Mwishoni mwa Januari, Ndugu Knorr aliwapa wanafunzi migawo yao. Tulisikia akiwaambia Paul na Marilyn Evans kwamba wametumwa Rwanda. Kisha akaniambia mimi na mke wangu: ‘Nanyi mtaenda pamoja nao!’ Tulifurahi sana, na baada ya mkutano tukaenda kwenye maktaba ya Gileadi na kuchukua ramani kubwa kutafuta Rwanda. Hata hivyo, baadaye tulipata barua inayosema kwamba akina ndugu hawakuweza kupata kibali cha kuturuhusu kuingia Rwanda. Tulitamauka lakini tukakubali mgawo mwingine wa kwenda Kongo pamoja na Paul na Marilyn.”
Mnamo 1976, ndugu wengine wawili pamoja na wake zao walitumwa Rwanda baada ya kuhitimu kutoka darasa la 60 la Gileadi. Kwa kuwa waliruhusiwa kuingia Rwanda, wote walihamia nyumba ya kukodi, wakahubiri kwa ujasiri, na kuanza kujifunza Kinyarwanda. Muda wa kukaa nchini ulipoisha baada ya miezi mitatu, Idara ya Uhamiaji ilikataa kuwapa vibali tena, hivyo, wamishonari hao wakatumwa Bukavu, mashariki mwa Kongo.
“WALIFANYA KAZI KWA BIDII”
Katikati ya miaka ya 1970, mapainia wa pekee kutoka Tanzania na Kongo walianza kuondoka Rwanda kwa sababu mbalimbali. Wakati huohuo, akina ndugu Wanyarwanda walianza kufanya upainia na kupanua kazi ya kuhubiri kotekote nchini. Kisha, mnamo 1978, kitabu Kweli na trakti mbili zikatafsiriwa katika Kinyarwanda. Mbali na machapisho hayo, kukawa pia na toleo la kila mwezi la gazeti la Mnara wa Mlinzi. Machapisho hayo yaliwasaidia wengine kujifunza kweli. Mmishonari, Manfred Tonak, alisema hivi kuwahusu mapainia Wanyarwanda: “Walikuwa wenye bidii, na walitenga wakati mwingi kwa ajili ya huduma. Wapya waliiga kielelezo chao.”
Gaspard Niyongira aeleza jinsi habari njema ilivyokuwa ikienea nyakati hizo. “Kufikia wakati nilipobatizwa mwaka wa 1978, viongozi wa kidini walikuwa na wasiwasi sana kuona wengi wakiikubali kweli. Mamia ya watu walihudhuria makusanyiko yetu. Tulipoenda kuhubiri, tulikuwa kama kundi la nzige! Mara nyingi, wahubiri 20 hivi wangeondoka katikati mwa mji wa Kigali na kwenda kuhubiri kwa miguu huko Kanombe, kitongoji kilicho umbali wa kilomita tisa hivi. Baada ya kutua kidogo ili kupata chakula cha mchana, wangeendelea kwa kilomita nyingine saba hadi Masaka na baadaye jioni walirudi Kigali kwa basi. Vikundi mbalimbali vya wahubiri vilifanya hivyo pia katika sehemu nyinginezo. Haishangazi kwamba njia hiyo ya kuhubiri iliwafanya wengi wafikiri kulikuwa na maelfu ya Mashahidi wa Yehova nchini. Kwa sababu hiyo, kukawa na mashtaka mengi dhidi yetu yaliyowachochea wenye mamlaka wasitutambue kisheria.”
Wakiwa na shauku nyingi kwa ajili ya kweli, ndugu nchini Rwanda walitamani kuonja shangwe ya kushirikiana na ndugu zao kutoka nchi mbalimbali. Kwa hiyo, mnamo Desemba 1978, mashahidi 37 hivi kutoka Rwanda, kutia ndani watoto, walisafiri umbali wa kilomita zaidi ya 1,200 kupitia Uganda ili kuhudhuria Kusanyiko la Kimataifa lenye kichwa “Imani Yenye Ushindi,” lililofanyiwa Nairobi, Kenya. Safari hiyo haikuwa rahisi. Usafiri haukutegemeka na mara nyingi magari yaliharibika. Isitoshe, nchi ya Uganda ilikuwa na msukosuko wa kisiasa. Hatimaye wajumbe hao walipofika katika mpaka wa Kenya, maofisa wa mpaka wa Uganda waliwashutumu kuwa wapelelezi, wakawakamata, na kuwapeleka katika makao makuu ya kijeshi mjini Kampala, Uganda. Idi Amin, aliyekuwa rais wa Uganda wakati huo akawahoji. Akiwa ameridhika na majibu yao, aliamuru waachiliwe. Ingawa walikosa programu ya siku ya kwanza ya kusanyiko mjini Nairobi, ndugu hao walifurahi kuona maelfu ya akina ndugu kutoka mataifa mbalimbali wakiwa pamoja kwa amani.
JITIHADA ZA KUTAKA KUTAMBULIWA KISHERIA
Si kila mtu aliyependezwa na kweli za Biblia pamoja na viwango vizuri vya maadili vinavyofundishwa na Mashahidi. Viongozi wa kidini hasa walikasirika sana kuona watu wengi wakiikubali kweli. Ndugu Rwakabubu akumbuka: “Wengi waliokuwa Wakatoliki, Waprotestanti, na Waadventisti wenye bidii, walituma barua za kujiuzulu kutoka dini za awali. Ndugu mwingine alisema kwamba matokeo ya kazi ya kuhubiri yalikuwa kama moto uliowashwa katika dini. Baada ya muda mfupi, idadi ya waliohudhuria mikutano katika Kutaniko la Kigali iliongezeka hadi zaidi ya 200. Mwanzoni, viongozi wa kidini hawakujishughulisha nasi kwa sababu tulikuwa wachache sana. Hata hivyo, kadiri idadi hiyo ilivyozidi kuongezeka, watu fulani walidai kwamba sisi ni hatari kwa usalama wa nchi. Ni muhimu kutaja pia kwamba karibu wakati huohuo, askofu mkuu wa Kanisa Katoliki nchini Rwanda, Vincent Nsengiyumva, alijiunga na halmashauri ya chama cha kisiasa kilichokuwa kinatawala.
“Kwa sababu kulikuwa na ongezeko la haraka, tulihitaji kutambuliwa kisheria ili tuwe na wamishonari, tujenge Majumba ya Ufalme, na kufanya makusanyiko makubwa. Ofisi ya tawi ya Kenya ilifanya mipango Ernest Heuse kutoka Ubelgiji, awasiliane na mawaziri wa serikali ili kuomba tutambuliwe kisheria, lakini jitihada zake hazikufanikiwa. Baadaye, mwaka wa 1982, ofisi ya tawi ya Kenya, ikatushauri tuwaandikie Waziri wa Haki na Waziri wa Mambo ya Ndani, kuomba tutambuliwe kisheria. Mimi pamoja na mapainia wengine wa pekee wawili tukatia sahihi ombi hilo. Lakini hatukupata majibu yoyote.”
Wakati huohuo, upinzani uliongezeka. Antoine Rugwiza, ndugu mnyamavu na mwenye kuheshimika akumbuka kwamba katika matangazo ya redio ya kitaifa, rais alisema kwamba hatawavumilia wale wanaoidharau “imani ya Wanyarwanda.” Kila mtu alielewa kwamba anarejelea Mashahidi wa Yehova. Muda mfupi baada ya tangazo hilo, ndugu walikatazwa kukusanyika pamoja. Pia, kulikuwa na fununu kwamba watakamatwa. Mara mbili Ndugu Rwakabubu aliamriwa afike mbele ya shirika la usalama wa Serikali ili ahojiwe.
Kisha, mnamo Novemba 1982, Kiala Mwango, akiwa na mke wake, Elaine, alitumwa kutoka Nairobi ili asimamie makusanyiko ya mzunguko yaliyofanywa Butare, Gisenyi, na Kigali. Ndugu Rwakabubu alikuwa mwenyekiti katika makusanyiko hayo. Baada tu ya kusanyiko la Kigali, kwa mara ya tatu aliamriwa afike katika majengo ya serikali yaliyokuwa yanatumiwa na rais. Hata hivyo, wakati huo hakurudi! Katika muda wa siku nne, wale mapainia wengine wa pekee wawili ambao walikuwa wametia sahihi ombi la kutambuliwa kisheria, wakakamatwa. Wote watatu wakafungwa bila mashtaka au fursa ya kujitetea. Baadaye, wengine wakakamatwa pia. Jumba la Ufalme likafungwa, na milango ikatiwa makomeo. Waziri wa Haki akawaandikia wakuu wa wilaya barua ya kuwapiga marufuku Mashahidi wa Yehova.
Hatimaye, mnamo Oktoba 1983, ndugu hao watatu waliotia sahihi maombi ya kutambuliwa kisheria, wakafunguliwa mashtaka. Walishtakiwa kwamba ni walaghai na wadanganyifu—madai ya uwongo na yasiyo na msingi. Mahakama haikutoa shahidi hata mmoja wala stakabadhi yoyote ili kuthibitisha madai yao. Ndugu hao wakahukumiwa miaka miwili gerezani. Wauaji walipoachiliwa kutokana na mpango wa msamaha, ndugu hao waaminifu hawakuachiliwa. Huko Gisenyi, Mashahidi wengine watano walivumilia kifungo cha karibu miaka miwili bila amri halali ya mahakama wala kuhukumiwa.
MAISHA GEREZANI
Maisha yalikuwa magumu gerezani. Wafungwa walipewa chakula cha mhogo na maharagwe mara moja kwa siku. Nyama ililiwa mara moja hivi kwa mwezi. Matandiko yalikuwa na kunguni, lakini kwa sababu ya msongamano, wafungwa wengi walilala sakafuni. Haikuwa rahisi kupata maji. Akina ndugu waliishi pamoja na wahalifu sugu na wajeuri. Mara nyingi walinzi wa gereza walikuwa wakali, ingawa mmoja wao, Jean Fataki, alikuwa mwenye fadhili. Alikubali kujifunza Biblia, hatimaye akabatizwa, na ni painia mwaminifu hadi sasa.
Ndugu Rwakabubu akumbuka: “Tulipokuwa gerezani, askofu huyo alifanya Misa huko gerezani. Aliwaambia wasikilizaji wake wajihadhari na Mashahidi wa Yehova. Baadaye, baadhi ya Wakatoliki waliomsikiliza wakatuuliza ni kwa nini askofu mkuu alisema hivyo, kwa kuwa waliwaona Mashahidi wa Yehova kuwa wenye amani.”
Punde si punde, Roger na Noella Poels wakawasili mjini Kigali kutoka Ubelgiji. Roger alikuwa na kandarasi ya kazi. Wale ndugu watatu walikuwa bado gerezani, hivyo, Roger akaomba kuzungumza na Waziri wa Haki ili amweleze kuhusu imani yetu na kuuliza kwa upole sababu inayofanya serikali iwachukie Mashahidi wa Yehova. Waziri huyo alikatiza mazungumzo kwa kusema: “Bwana Poels, nimekusikiliza vya kutosha! Utarudi kwenu Brussels. Hutaendelea kukaa nchini Rwanda!”
Kwa kuwa wale ndugu watatu waliendelea kuwa imara bila kutishika, walilazimika kukamilisha kifungo chao cha miaka miwili, ingawa katika mwaka wa pili walihamishiwa gereza lililokuwa afadhali kidogo. Wakaachiliwa mnamo Novemba 1984.
MATESO YAZIDI
Upinzani uliendelea. Matangazo ya redio yalisema kwamba Mashahidi wa Yehova si watu wazuri na wana msimamo mkali wa kidini. Kufikia Machi 1986, kukamatwa kukawa jambo la kawaida nchini kote. Miongoni mwa waliokamatwa ni Augustin Murayi, ambaye kwa sababu ya msimamo wake wa kutokuwamo, alifutwa kazi kama mkurugenzi-mkuu katika Wizara ya Elimu ya Msingi na ya Sekondari. Alishambuliwa katika magazeti na hata zaidi katika redio.
Kotekote nchini, ndugu na dada wengine, hata dada wajawazito pamoja na watoto wadogo, walikamatwa. Kuelekea mwishoni mwa 1986, walihamishiwa gereza kuu la Kigali kusubiri mashtaka. Kwa kuwa hawakuimba nyimbo za kitaifa, hawakuvaa beji ya rais, na hawakununua kadi ya chama cha kisiasa, watu walikata kauli kimakosa kwamba Mashahidi wa Yehova walikuwa wapinzani na walitaka kuipindua serikali.
Phocas Hakizumwami asema akitabasamu: “Baadhi ya akina ndugu wa kutaniko lililokuwa Nyabisindu walikuwa wa kwanza kukamatwa. Kwa kuwa tulitazamia kwamba hatimaye sote tungekamatwa, tulitambua kuwa eneo letu la kuhubiri lilikuwa karibu kubadilika kutoka nje ya gereza hadi gerezani. Hivyo, tukaamua kuwa na kampeni kubwa ya kuhubiri eneo letu la ‘nje’ kwanza. Tulihubiri sokoni na kuwaachia watu vitabu na magazeti mengi. Tulimwomba Yehova atusaidie tumalize eneo letu kabla ya kufungwa. Yehova alitusaidia, kwa kuwa tulimaliza eneo letu mnamo Oktoba 1, 1985. Siku saba baadaye tukafungwa.”
Mwaka uliofuata, Palatin Nsanzurwimo na mkewe, Fatuma, walikamatwa na maajenti wa shirika la usalama wa Serikali. Baada ya kuhojiwa kwa saa nane na nyumba yao kupekuliwa sana, walipelekwa gerezani pamoja na watoto wao watatu. Wakiwa njiani kwenda gerezani, ndugu mdogo wa Palatin, aliyekuwa akiwafuata kwa ukaribu, akamchukua mwana wao mwenye umri wa miaka mitano na binti mwenye umri wa miaka minne ili awatunze. Palatin na Fatuma wakafungwa pamoja na mtoto wao mchanga mwenye umri wa miezi 14. Baadaye Fatuma alihamishiwa gereza lingine ambamo alikaa kwa miezi tisa.
Wakati huo, watoto wanne wa Jean Tshiteya walifukuzwa shuleni. Baadaye kidogo, aliporudi nyumbani, alipata mke wake amekamatwa, nyumba yake imepekuliwa, huku watoto wakiachwa peke yao. Muda mfupi baadaye, Ndugu Tshiteya akakamatwa na kutupwa gerezani huko Butare, akajiunga na mke wake na ndugu wengine. Baadaye, Mashahidi wote waliokuwa wamefungwa katika magereza mbalimbali huko Butare wakahamishwa na kupelekwa katika gereza kuu la Kigali. Wakati huo, watoto wa Ndugu Tshiteya walikuwa wakitunzwa na akina ndugu mjini Kigali.
Ndugu Tshiteya akumbuka: “Akina ndugu na dada walipoletwa katika gereza kuu la Kigali kutoka magereza ya maeneo mengine, walisalimiana kwa shangwe, wakisema ‘Komera!’ yaani, ‘Jipe moyo!’ Mlinzi mmoja wa gereza aliposikia salamu hiyo, alisema hivi kwa ukali: ‘Mna wazimu! Watu wanawezaje kujipa moyo gerezani?’”
Licha ya kukamatwa, watu wenye mioyo minyoofu hawakuvunjika moyo, na mara nyingi mateso yalikuwa na matokeo mazuri. Odette Mukandekezi, dada mwenye bidii na mwenye urafiki, alikuwa miongoni mwa waliokamatwa wakati huo. Anaeleza: “Wakati wa mateso, akina ndugu walikamatwa na kupigwa. Siku moja tulimpita msichana mdogo anayeitwa Josephine akichunga ng’ombe. Alikuwa na Biblia na alikuwa amesoma kwamba Wakristo wa mapema walishutumiwa, wakateswa, wakapigwa mijeledi, na kufungwa gerezani. Kwa kuwa alijua kwamba Mashahidi walikuwa wanateswa, alikata kauli kwamba dini yao ni ya kweli, na akaomba afundishwe Biblia. Sasa yeye ni dada aliyebatizwa.”
Wakati wa marufuku, Gaspard Niyongira alikuwa dereva wa lori, na mara nyingi alienda Nairobi, Kenya, kwa sababu ya kazi yake. Alibeba machapisho kisiri kutoka Nairobi na kuyapeleka Rwanda akiwa ameyaficha ndani ya sanduku la pekee lililokuwa ndani ya lori lake. Sanduku hilo lingeweza kubeba makatoni sita ya machapisho. Wakati huohuo, Henry Ssenyonga, kutoka magharibi mwa Uganda, alileta magazeti nchini Rwanda kwa ukawaida akitumia pikipiki yake.
Mikutano ya kutaniko ilifanywa katika vikundi vidogo-vidogo. Ikiwa wenye mamlaka wangekisia kwamba Mashahidi wa Yehova walikuwa wakifanya mikutano, wangefanya msako. Ndugu Niyongira akumbuka: “Nilijenga jengo dogo lililounganishwa na nyumba yangu, ambamo tungeweza kufanyia mikutano kisiri. Tuliyatia machapisho yetu ndani ya mifuko ya plastiki, tukayazika na kuyafunika kwa makaa.”
Ingawa watu wengi walianza kukamatwa, Jean-Marie Mutezintare, aliyekuwa amebatizwa karibuni, alihudhuria Kusanyiko la kimataifa lenye kichwa “Washika-Ukamilifu” mjini Nairobi mnamo Desemba 1985. Alipokuwa akirudi, yeye pamoja na Isaie Sibomana, walichukua magazeti kutoka kwa akina ndugu magharibi mwa Uganda ili kuyapeleka Rwanda. Wakiwa mpakani, maofisa waliyaona magazeti hayo, wakawakamata na kuwafunga pingu ndugu hao, na kuwapeleka wakahojiwe na kukaa jela usiku huo wenye baridi. Baadaye, wakapelekwa katika gereza kuu mjini Kigali. Walikutana na akina ndugu na dada 140 hivi waliofurahi kupata ripoti kamili kuhusu kusanyiko mjini Nairobi. Bila shaka, mambo waliyosema yaliwatia moyo, na kuwaimarisha akina ndugu!
Akina ndugu waliokuwa gerezani walifanya mikutano na kufanya mipango kwa ajili ya utumishi. Mbali na kuhubiri, pia waliwafundisha baadhi ya wafungwa kujua kusoma na kuandika. Isitoshe, walijifunza Biblia pamoja na wenye kupendezwa na wakawasaidia wahubiri wapya kujitayarisha kwa ajili ya ubatizo. Baadhi yao walikuwa wanajifunza walipokamatwa, na wengine walijifunza kweli gerezani.
MWANGALIZI WA MZUNGUKO “AWATEMBELEA” WAFUNGWA WENZAKE
Ndugu mmoja anaeleza jinsi mambo yalivyokuwa katika gereza la Kigali mwaka wa 1986: “Ndugu wengi walikuwa humo. Tulifanya mkutano ili kuona jinsi ambavyo tungeweza kuwasaidia ndugu ambao hawakuwa gerezani. Tukaamua kuwaandika barua ya kuwatia moyo. Tukawaambia kwamba tutakapomaliza kuhubiri eneo letu la gerezani, tutarudi nyumbani. Tulimhubiria kila mtu gerezani na kuongoza mafunzo ya Biblia. Baadaye, tuliposikia kwamba mwangalizi wa mzunguko alikuwa anatembelea makutaniko yaliyo nje, sisi pia tulitamani kutembelewa, hivyo, tukasali kwa Yehova kuhusu jambo hilo. Muda mfupi baadaye, Ndugu Rwakabubu, aliyekuwa mwangalizi wa mzunguko, akakamatwa kwa mara ya pili. Kwa maoni yetu, kukamatwa kwake kulikuwa njia ya kututembelea akiwa mwangalizi wa mzunguko.”
Wakati huo wa mateso, ni ndugu mmoja tu aliyekana imani. Alipovaa beji ya kisiasa, wafungwa wasio Mashahidi walimpiga mateke na kumtukana wakimwita mwoga. Mke wake, aliyekuwa akijifunza Biblia, alimuuliza ni kwa nini hakuendelea kuwa mwaminifu. Baadaye, aliwaandikia mahakimu akiwaambia kwamba alifanya makosa na kwamba bado yeye ni Shahidi wa Yehova. Hata aliiandikia ofisi ya tawi ya Kenya kuomba msamaha. Sasa anamtumikia Yehova kwa uaminifu tena.
KAZI YA KUHUBIRI YAENDELEA NJE YA GEREZA
Waliokuwa huru waliendelea kuhubiri kwa bidii, wakiripoti kwa wastani saa 20 hivi kwa mwezi. Alfred Semali, aliyekuwa miongoni mwa waliokuwa huru, akumbuka: “Ijapokuwa sikuwahi kufungwa, nilitazamia kufungwa na nikajitayarisha kwa ajili ya hilo. Kwa kuwa Jumba la Ufalme lilifungwa, tulikutana katika vikundi vidogo na tukaendelea kuhubiri. Niliyatia magazeti ndani ya bahasha na kwenda mjini kana kwamba natafuta kazi, kisha nikatafuta fursa ya kuwaachia watu magazeti na kuzungumzia Biblia.
“Mnamo 1986 wengi wa ndugu zetu na watu wanaopendezwa walitiwa gerezani, hata wale waliokuwa wameanza tu kujifunza Biblia. Akina ndugu na hata wapya walikuwa imara kwa njia yenye kustaajabisha. Wakati huohuo, Mashahidi katika nchi nyingi walimwandikia rais wa Rwanda wakipinga jinsi Mashahidi walivyokuwa wakitendewa isivyo haki, na iliripotiwa katika redio kwamba alipokea mamia ya barua kila siku. Matokeo yalikuwa mazuri, kwa kuwa mwaka uliofuata ndugu na dada zetu na watu wenye kupendezwa waliachiliwa kwa amri ya rais. Tulijawa na shangwe.” Mara tu walipoachiliwa, wazee wakafanya mipango ya ubatizo mjini Kigali, watu 36 wakabatizwa, na 34 kati yao wakajiandikisha kuwa mapainia wasaidizi bila kukawia!
Mateso yalipokuwa makali zaidi mnamo 1986, kulikuwa na wastani wa wahubiri 435 walioripoti; kati yao, ndugu na dada 140 hivi walikuwa wamefungwa wakati fulani. Mashahidi hao walikuwa nguzo ya tengenezo la Yehova nchini Rwanda. Imani yao ilikuwa ‘imejaribiwa’ na walibaki imara katika kweli.—Yak. 1:3.
Hatimaye, baada ya miaka yenye misukosuko ya 1980, akina ndugu nchini Rwanda walipata ongezeko na amani ya kadiri. Hata hivyo, namna gani wakati ujao? Wengi waliikubali kweli. Je, wapya pia wangethibitika kuwa wanafunzi waliojengwa kwa vifaa visivyoshika moto? (1 Kor. 3:10-15) Je, imani yao ingeweza kushinda majaribu yaliyokuwa mbele? Acha tuone.
VITA NA MISUKOSUKO YA KISIASA
Kufikia 1990, kulikuwa na karibu wahubiri 1,000 wenye bidii nchini Rwanda. Hata hivyo, kulikuwa na msukosuko wa kisiasa, na mnamo Oktoba, majeshi ya Rwandan Patriotic Front (RPF) yalivamia eneo la kaskazini mwa Rwanda, kutoka nchi jirani ya Uganda.
Ferdinand Mugarura, ndugu jasiri aliyekuwa amefungwa katika pindi mbili tofauti kwa sababu ya imani yake, alikuwa anaishi Ruhengeri wakati wa uvamizi huo. Akumbuka hivi: “Chuki na ukabila vilienea. Hata hivyo, Mashahidi wa Yehova walidumisha msimamo wao wa kutojiingiza katika tofauti za kisiasa au chuki ya kijamii. Baadhi ya akina ndugu walilazimika kutoroka makwao na wengine kupoteza kazi zao kwa sababu ya kushikilia msimamo wao.”
Dada mmoja, mwenye watoto watatu ambaye ni mwalimu na mjane, alikataa kuwasaidia wanajeshi kifedha. Kwa sababu hiyo, mwalimu mkuu alimshtaki kwa wenye mamlaka wa kijeshi, akatupwa gerezani kwa mara ya pili, kwa kuwa aliwahi kufungwa katika miaka ya 1980. Majeshi yaliyopinga serikali yalipofika mji ambao dada huyo alikuwa amefungwa, gereza lilivunjwa na wafungwa wote wakatoroka. Lakini, badala ya kutoroka na wafungwa wengine, dada huyo alibaki gerezani. Majeshi hayo yalipoondoka, alikamatwa tena na kuhamishiwa gereza kuu la Kigali. Akiwa huko, alisali kwamba apate kujua tarehe ya Ukumbusho ili asikose kuhudhuria. Alishangaa sana baadaye alipoachiliwa siku ileile ya Ukumbusho! Kwa sababu ya msimamo wake wa kutounga mkono upande wowote, alipoteza nyumba na kazi yake, lakini akawa painia mwenye bidii.
Kwa sababu ya mataifa mengine kuingilia kati, uvamizi kutoka Uganda ulisitishwa kwa muda. Mnamo 1991, kulikuwa na jitihada za kuanzisha mfumo wa vyama vingi vya kisiasa nchini Rwanda. Vyama vingi vikubwa na vidogo vya kisiasa vilifanyizwa, vilivyotokeza kiburi cha ukabila na kimaeneo. Baadhi ya vyama hivyo vilikuwa na malengo yaliyoonwa kuwa yanafaa, lakini vingine vilikuwa vyenye fujo na vyenye msimamo mkali. Kwa mara ya kwanza, watu walivutiwa na msimamo wa Mashahidi wa Yehova wa kutounga mkono upande wowote. Kwa sababu hawakujihusisha katika mapambano ya kisiasa na ya kikabila, serikali na watu kwa ujumla hawakuona Mashahidi kuwa hatari.
Mnamo Septemba 1991, ndugu kutoka mataifa mbalimbali wakiambatana na ndugu Gaspard Rwakabubu na Tharcisse Seminega kutoka Rwanda, waliwatembelea mawaziri wakuu mjini Kigali. Ndugu hao walizungumza na Waziri mpya wa Haki, aliyewasikiliza kwa fadhili. Walimshukuru kwa hatua nzuri ambazo tayari zilikuwa zimefikiwa na kumwomba aendelee kuwasaidia ili wapate kutambuliwa kikamili kisheria.
Mnamo Januari 1992, kabla ya kutambuliwa kisheria, akina ndugu walifanya kusanyiko la wilaya mjini Kigali. Godfrey na Jennie Bint wanalikumbuka vizuri. “Tulikuwa tunatumika nchini Uganda wakati huo na tulishangaa kupata barua kutoka ofisi ya tawi ya Kenya, kutuomba twende Rwanda kwa majuma matatu kusaidia katika mipango ya kusanyiko na kurekodi drama. Ndugu walikuwa wakarimu sana, na kila siku tulialikwa kwa ajili ya mlo na familia tofauti-tofauti. Uwanja wa kibinafsi wa mpira ulikuwa umekodiwa, na tulipofika matayarisho yalikuwa yanaendelea. Wakati huo, tayari akina ndugu walikuwa wamefanya mipango ya kurekodi drama, na walifanikiwa licha ya vifaa vichache walivyokuwa navyo. Ingawa ndugu wengi kutoka kaskazini mwa nchi hawakupata vibali vya kusafiri, na mipaka ya Burundi na Uganda ilikuwa imefungwa, watu 2,079 walihudhuria siku ya Jumapili na 75 wakabatizwa.”
KUTAMBULIWA KISHERIA HATIMAYE!
Miezi michache baadaye, mnamo Aprili 13, 1992, kazi ya Mashahidi wa Yehova ikasajiliwa kisheria nchini Rwanda—na kwa mara ya kwanza! Huo ukawa mwisho wa pambano la muda mrefu la kutangaza habari njema chini ya marufuku, kusumbuliwa, na kufungwa. Akina ndugu walitazamia kipindi kipya cha ukuzi na upanuzi wa kitheokrasi.
Bila kukawia, Baraza Linaloongoza liliwatuma wamishonari nchini. Henk van Bussel ambaye awali alitumika katika Jamhuri ya Afrika ya Kati na Chad, na Godfrey na Jennie Bint, waliotumika Zaire (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo) na Uganda, walikuwa wamishonari wa kwanza kupata vibali vya kuishi nchini. Halmashauri ya Nchi ikawekwa rasmi kusimamia kazi ya kuhubiri.
Ndugu Bint asimulia mambo yalivyokuwa walipofika kwa mara ya kwanza pamoja na Henk van Bussel: “Punde si punde, tulipata nyumba nzuri kwa ajili ya makao ya wamishonari karibu sana na Jumba la Ufalme. Mara moja tukaanza kujifunza Kinyarwanda. Haikuwa rahisi, kama vile tu mapainia wa kwanza walivyogundua hapo awali katika mwaka wa 1970. Kitabu kimoja kilitoa shauri hili: ‘Herufi CW zikiwa pamoja zinatamkwa TCHKW!’ Pia, tunakumbuka kwamba dada aliyekuwa akitufundisha alisema, ‘Huwezi kamwe kutamka vizuri herufi “shy” katika neno “isi nshya” [dunia mpya] usipotabasamu!’”
Baadaye mwaka huo, kilele kipya cha wahubiri 1,665 kikafikiwa, na mnamo Januari 1993, kusanyiko lingine la wilaya likafanywa Kigali. Hudhurio lilikuwa 4,498, na 182 wakabatizwa. Kiala Mwango alikuwa mwakilishi kutoka ofisi ya tawi ya Kenya. Wakati huo, hakuna mtu angewazia kwamba ofisi ya tawi ingejengwa mwaka wa 2006 katika uwanja uliokuwa upande ule mwingine wa barabara kutoka kwa uwanja wa mpira ambamo tulifanyia kusanyiko.
Licha ya uvamizi mwingine kutoka kaskazini, kazi ya kuhubiri iliendelea kusonga mbele. Kufikia 1993, majeshi yaliyopinga serikali yalifika karibu sana na Kigali. Mipaka ya Uganda ilikuwa bado imefungwa, na milio ya bunduki ilisikika hadi milimani kutoka mjini. Karibu watu milioni moja walikuwa wamekimbia kutoka sehemu ya kaskazini ya nchi. Watu hao walitia ndani ndugu na dada 381 waliotunzwa na akina ndugu mjini Kigali au karibu na hapo. Hata hivyo, mazungumzo ya kusitisha vita yalifanywa mjini Arusha, Tanzania, eneo la amani likatengwa, nayo serikali ikakubali kushirikiana na majeshi yaliyoipinga na vyama fulani vya kisiasa, vikubwa na vidogo.
KUSANYIKO LA PEKEE SANA!
Kusanyiko la pekee la mwaka huo lilikuwa limepangiwa kufanywa katika Uwanja wa Michezo wa Kigali. Lakini, wenye mamlaka wa uwanja huo waliidhinisha pia mchezo wa kandanda ambao ungechezwa saa 9 jioni, siku hiyohiyo ya kusanyiko. Ndugu walihudhuria kipindi cha asubuhi, lakini kabla tu ya programu ya alasiri kuanza, mashabiki wa kandanda wakaanza kuwasili—nao polisi hawangeweza kuwazuia wasiingie. Meneja wa uwanja huo alisema kwamba mchezo huo ungemalizika saa 12 jioni. Hivyo, akina ndugu wakaondoka na kurudi saa 12 jioni ili kusikiliza sehemu iliyobaki ya programu.
Hilo lilisababisha wasiwasi kwa sababu kulikuwa na amri ya kutotembea nje usiku. Magari hayakuruhusiwa kusafiri baada ya saa 12 jioni, na watu hawakuruhusiwa kuwa nje baada ya saa 3 usiku. Hata hivyo, saa moja jioni hivi, ilitangazwa kupitia redio kwamba muda huo umeongezwa hadi saa 5 usiku. Isitoshe, kulikuwa na matatizo ya umeme. Kwa kuwa mipango ya kutumia uwanja huo ilivurugwa, meya wa Kigali alihakikisha akina ndugu wamepata umeme uwanjani. Hata alipanga wasafirishwe bila gharama yoyote baada ya programu. Hivyo, ndugu wakahudhuria programu yote ya kusanyiko. Wazia jinsi walivyofurahi kuona mabasi mengi yakiwasubiri nje ya uwanja baada ya programu!
Günter Reschke akumbuka kwamba alizuru Rwanda mwishoni mwa Septemba 1993. Anasema: “Ofisi ya tawi ya Kenya ilinituma Kigali ili nifundishe Shule ya Huduma ya Ufalme pamoja na Ndugu Rwakabubu. Wakati huo, kulikuwa na wazee 63 tu nchini Rwanda, ingawa idadi ya wahubiri ilikuwa imeongezeka hadi 1,881. Tayari kulikuwa na wasiwasi mwingi nchini, na tulisikia uvumi kuhusu mapigano katika eneo la kaskazini. Hakuna aliyetazamia wakati mgumu uliokuwa mbele, hata hivyo shule hiyo iliandaa chakula kwa wakati unaofaa. Imani ya wazee iliimarishwa na kuwasaidia kuwa wachungaji bora hasa wakati huo kwa kuwa vita vilikuwa vinakaribia.”
MIPANGO YA KUANZISHA OFISI
Mwishoni mwa Machi 1994, Leonard Ellis na mke wake, Nancy, kutoka Nairobi walikuja kuhudhuria makusanyiko ya pekee na kusaidia akina ndugu katika ofisi ya kutafsiri. Ofisi ya tawi mjini Nairobi ilikuwa imependekeza kwamba makao ya wamishonari na ofisi ya kutafsiri nchi Rwanda ziunganishwe. Mnamo Jumatatu, Aprili 4, watafsiri, Halmashauri ya Nchi, wamishonari, pamoja na Ndugu na Dada Ellis, walihudhuria Funzo la Mnara wa Mlinzi. Ulikuwa wakati wenye kusisimua—mwanzo wa upanuzi zaidi.
Baada ya kukamilisha kazi yao, Ndugu na Dada Ellis waliondoka kwa ndege iliyothibitika kuwa ya mwisho kutoka Kigali kwa muda wa miezi mingi. Alasiri iliyofuata, Ndugu Rwakabubu alipigia makao ya wamishonari simu na kuwaambia kwamba ubalozi wa Urusi umeacha kudai umiliki wa kiwanja ambacho tulikuwa tumetazamia kujenga ofisi. Huenda sasa kikapewa Mashahidi wa Yehova, hivyo, tulipaswa kukutana na maofisa wa Wizara ya Ardhi asubuhi iliyofuata, yaani, Alhamisi, Aprili 7. Mipango hiyo haikufanikiwa.
MAUAJI YA JAMII NZIMA-NZIMA YAANZA!
Jioni ya Aprili 6, ndege fulani ililipuliwa kwa kufyatuliwa risasi karibu na mji wa Kigali. Ilikuwa imebeba rais wa Rwanda na wa Burundi. Abiria wote walikufa. Watu wachache tu ndio waliojua jambo hilo; stesheni rasmi ya redio haikutoa tangazo lolote.
Wale wamishonari watatu, Ndugu na Dada Bint, na Henk hawatasahau kamwe siku zilizofuata. Ndugu Bint aeleza: “Tulipoamka asubuhi ya Aprili 7, tulisikia sauti za bunduki na milipuko ya mabomu ya mkononi. Haikushangaza kwani katika miezi iliyokuwa imepita hali ya kisiasa nchini ilikuwa yenye msukosuko sana. Hata hivyo, tulipokuwa tukitayarisha kiamsha-kinywa, tulipokea simu. Emmanuel Ngirente, aliyekuwa katika ofisi ya tafsiri, alituambia kwamba stesheni ya redio ya kitaifa ilikuwa imetangaza kifo cha marais wawili waliokuwa katika ndege iliyolipuliwa. Wizara ya Ulinzi ikawaonya watu mjini Kigali wasitoke nyumbani.
“Saa tatu asubuhi, tuliwasikia waporaji wakivunja nyumba ya jirani yetu. Wakaiba gari na kumuua mama mwenye nyumba.
“Punde si punde, askari na waporaji hao wakaja kwetu, wakaligonga lango la chuma na kupiga kengele. Tukakaa kimya. Kwa sababu fulani, hawakujaribu kuvunja lango bali waliondoka na kwenda kwa nyumba nyingine. Milio ya risasi na milipuko ilisikika kila mahali, kwa hiyo hatukuthubutu kuondoka. Milio ya bunduki ilisikika karibu na nyumba yetu, hivyo tukaenda kwenye sehemu iliyo katikati ya vyumba ili kukwepa risasi. Tulitambua kwamba hali haitabadilika karibuni, kwa hiyo, tukajaribu kuhifadhi chakula kwa kutayarisha mlo mmoja tu kwa siku. Siku iliyofuata, tulipokuwa tu tumemaliza kula chakula cha mchana na tunasikiliza habari za kimataifa kwenye redio, Henk akasema, ‘Ndio hao kwenye ua wetu!’
“Hatukuwa na wakati wa kupoteza. Tuliingia bafuni na kujifungia humo. Kisha, tukasali pamoja tukimwomba Yehova atusaidie tuvumilie chochote kitakachotokea. Kabla ya kumaliza kusali, tuliwasikia wanamgambo na waporaji wakivunja madirisha na milango. Baada ya dakika chache, walikuwa ndani, wakipiga kelele na kuvunja fanicha. Walikuwa waporaji 40 hivi—wanaume, wanawake, na watoto—pamoja na wanamgambo. Pia, tulisikia risasi zikifyatuliwa huku wakipigania vitu walivyopata.
“Baada ya muda huo ulioonekana kuwa mrefu sana—ingawa ilikuwa dakika 40 hivi—wakajaribu kufungua bafu. Kisha, kwa sababu mlango ulikuwa umefungwa kwa funguo, wakajaribu kuuvunja. Sasa tukatambua kwamba tunapaswa kujisalimisha. Wanaume hao walitenda kiwazimu na walikuwa wametumia dawa za kulevya. Wakatutisha kwa mapanga na visu. Jennie alimlilia Yehova kwa sauti. Mwanamume mmoja akatoa panga na kumpiga Henk shingoni kwa upande ulio bapa. Henk akaanguka bafuni. Kwa njia fulani, nilifanikiwa kupata pesa na kuwapa washambuliaji hao. Wakazipigania.
“Ghafula, tulimwona kijana mmoja akitukazia macho. Ingawa hatukumjua, alitutambua, labda kwa sababu ya kazi yetu ya kuhubiri. Akatusukuma ndani ya bafu na kutuambia tufunge mlango. Akasema kwamba angetuokoa.
“Kelele za waporaji ziliendelea kwa dakika 30 hivi, na hatimaye kukatulia. Baadaye, kijana huyo alirudi na kutuambia kwamba tunaweza kutoka nje. Akisisitiza kwamba tuondoke mara moja, alitusindikiza kutoka nyumbani. Hatukuchukua chochote. Tulishtuka kuona miili ya baadhi ya jirani zetu waliokuwa wameuawa. Washiriki wawili wa Walinzi wa Rais walitusindikiza hadi kwenye nyumba ya ofisa fulani wa jeshi iliyokuwa karibu. Kisha, ofisa huyo akatusindikiza hadi kwenye Hoteli ya Mille Collines, ambapo watu wengi walikuwa wamekimbilia. Hatimaye, mnamo Aprili 11, tukahamishiwa Kenya, baada ya kuhangaika kwa saa nyingi na kusafirishwa na wanajeshi kutoka mjini kupitia njia isiyo ya moja kwa moja hadi kwenye uwanja wa ndege. Tulifika kwenye eneo la mapokezi la Betheli ya Nairobi tukiwa wachafu. Henk, aliyekuwa ametenganishwa nasi wakati wa kuhamishwa, aliwasili saa kadhaa baadaye. Familia ya Betheli ilituhangaikia sana na kututia moyo.”
SALA YA MSICHANA MDOGO YAWAOKOA
Siku moja baada ya ndege iliyowaua marais wa Rwanda na Burundi kuanguka, askari sita wa serikali walienda kwa Ndugu Rwakabubu. Macho yao yalikuwa mekundu sana, walinuka pombe, na walijiendesha kwa njia iliyoonyesha kwamba walikuwa wametumia dawa za kulevya. Wakaamuru wapewe silaha. Ndugu Rwakabubu akawaambia kwamba yeye na familia yake ni Mashahidi wa Yehova na hivyo hawana silaha.
Askari hao walijua kwamba kwa sababu Mashahidi wa Yehova hawaungi mkono upande wowote, walikataa kuunga mkono serikali, na hawakuwasaidia wanajeshi kifedha. Hilo liliwakasirisha. Gaspard na Melanie Rwakabubu, si Watutsi, lakini wapiganaji wa Interahamwe waliwaua pia Wahutu ambao hawakuwa na msimamo mkali, hasa ikiwa walidhaniwa kuwa wanawahurumia Watutsi au jeshi lililopinga serikali.
Askari hao waliwapiga Gaspard na Melanie kwa vijiti na kuwapeleka pamoja na watoto wao watano katika chumba cha kulala. Wakaondoa mashuka kitandani na kuanza kuwafunika nayo. Baadhi yao walikuwa na makombora mikononi, hivyo ilikuwa wazi walitaka kuwaua. Gaspard akawauliza, “Tunaweza kusali tafadhali?”
Kwa dharau, askari mmoja alikataa ombi lao. Kisha, baada ya mazungumzo fulani askari hao wakakubali, lakini shingo upande. Wakawaambia “Sawa, tunawapa dakika mbili msali.”
Wakasali kimya-kimya, lakini Deborah Rwakabubu, aliyekuwa na umri wa miaka sita, akasali kwa sauti: “Yehova, watu hawa wanataka kutuua, lakini tutawarudiaje watu niliowahubiria na kuwaachia magazeti matano nikiwa na Baba? Wanasubiri tuwarudie na wanahitaji kujua kweli. Nakuahidi kwamba tusipouawa, nitakuwa mhubiri, nibatizwe, na kuwa painia! Yehova, tuokoe!”
Waliposikia sala hiyo, askari hao wakashangaa. Mwishowe, mmoja wao akasema: “Kwa sababu ya sala ya huyu msichana mdogo, hatutawaua. Wengine wakija, waambie kwamba tayari tumekuwa hapa.”b
HALI YAZIDI KUZOROTA
Pole kwa pole vita vilizidi kadiri majeshi yaliyopinga serikali (Rwandan Patriotic Front) yalivyozidi kukaribia mji wa Kigali. Hilo liliwachochea wapiganaji wa Interahamwe kuendeleza mauaji zaidi.
Kulikuwa na vizuizi vya barabarani kotekote mjini na katika makutano ya barabara. Vizuizi hivyo vilikuwa chini ya ulinzi wa wanajeshi na wapiganaji wa Interahamwe wenye silaha pamoja na wenyeji. Wanaume wote wenye nguvu pamoja na wapiganaji wa Interahamwe walilazimika kulinda vizuizi hivyo mchana na usiku. Kusudi la vizuizi hivyo lilikuwa kuwatambua na kuwaua Watutsi.
Kadiri mauaji yalivyoendelea kotekote nchini, ndivyo mamia ya maelfu ya wakaaji wa Rwanda walivyoacha makao yao. Wengi wao, kutia ndani Mashahidi wa Yehova, walitafuta usalama nchini Kongo na Tanzania.
KUKABILI VITA NA KIFO
Yafuatayo ni masimulizi ya ndugu na dada zetu wakati mauaji ya jamii nzima-nzima yalipoanza. Kumbuka kwamba Mashahidi wa Yehova nchini Rwanda walikuwa wamepitia majaribu makali yaliyoimarisha na kuboresha imani yao na kuwapa ujasiri katika miaka ya 1980. Imani yao iliwasaidia ‘kutokuwa sehemu ya ulimwengu’ kwa kutoshiriki katika uchaguzi, kutotumia silaha ili kujilinda, na kutojiingiza katika siasa. (Yoh. 15:19) Kwa sababu ya kutojihusisha katika mambo hayo, walikabili dhihaka, vifungo, mateso, na kifo. Hata hivyo, ujasiri wao uliwasaidia katika hali hizo zote. Mbali na kutojihusisha katika mauaji, sifa hizo zilizojaribiwa pamoja na upendo wao kwa Mungu na jirani, ziliwasaidia Mashahidi wa Yehova kuhatarisha uhai wao ili kuwalinda wenzao.
Kuna mambo mengi ambayo hayajatajwa. Ndugu wengi wangependa kusahau mambo hayo yenye kutisha, kwa kuwa hawatafuti kulipiza kisasi. Tunatumaini kwamba masimulizi haya ya imani yao yatatuchochea sote tuonyeshe kikamili upendo unaowatambulisha wanafunzi wa kweli wa Yesu Kristo.—Yoh. 13:34, 35.
KISA CHA JEAN NA CHANTAL
Jean de Dieu (John) Mugabo, ndugu mchangamfu na mwenye kujali, alianza kujifunza na Mashahidi wa Yehova mnamo 1982. Kabla ya kubatizwa katika mwaka wa 1984, alikuwa tayari amefungwa gerezani mara tatu kwa sababu ya msimamo wake kama Shahidi wa Yehova. Mke wake, Chantal, alibatizwa pia mwaka wa 1984, na wakafunga ndoa mwaka wa 1987. Mauaji ya jamii nzima-nzima yalipoanza, walikuwa na watoto watatu, wote wasichana. John na Chantal waliishi na kitinda-mimba wao mwenye umri wa miezi sita huku wale watoto wengine wakiishi na wazazi wa Chantal katika eneo lingine.
Siku ya kwanza ya mauaji, Aprili 7, 1994, askari na wapiganaji wa Interahamwe walianza kuvamia nyumba zote za Watutsi. John alikamatwa na kupigwa kwa marungu; lakini akafanikiwa kutoroka na kukimbilia Jumba la Ufalme lililo karibu akiwa pamoja na ndugu mwingine. Chantal naye, bila kujua kilichompata mumewe, alijaribu kuondoka mjini pamoja na mtoto wao mdogo ili kwenda kuungana na watoto wao wengine.
John asimulia mambo yaliyompata: “Jumba la Ufalme lilikuwa na dohani kubwa kwa maana jengo hilo lilikuwa duka la kuokea mikate hapo awali. Kwa juma moja, tulijificha katika Jumba la Ufalme lenyewe, na dada mmoja Mhutu alituletea chakula ilipokuwa salama kufanya hivyo. Baadaye, tulijificha kwenye paa, kati ya mabati na dari, ambapo kulikuwa na joto sana jua lilipowaka. Tulitaka sana kupata mahali pazuri zaidi pa kujificha, kwa hiyo tulibomoa sehemu fulani ya dohani hilo la matofali, tukaingia na kukaa huko kwa zaidi ya mwezi mmoja tukiwa tumechutama.
“Karibu na hapo, wapiganaji wa Interahamwe walikuwa wameweka kizuizi cha barabarani na mara nyingi waliingia ndani ya Jumba la Ufalme kuzungumza au kujikinga mvua. Tungewasikia wakiongea. Dada huyo aliendelea kutuletea chakula ilipowezekana. Wakati mwingine, nilihisi sitaweza kuvumilia tena, lakini tuliendelea kumwomba Yehova atusaidie kustahimili. Mwishowe, mnamo Mei 16, dada huyo alitujulisha kwamba wanajeshi wa Rwandan Patriotic Front wamechukua udhibiti wa eneo hilo la mji, na hivyo hakuna haja ya kujificha tena.”
Naye Chantal, mke wa John, alipatwa na nini? Anaeleza: “Nilifaulu kutoroka kutoka nyumbani pamoja na mtoto wetu mnamo Aprili 8. Nilikutana na Immaculée, ambaye kitambulisho chake kilionyesha kwamba yeye ni Mhutu, na Suzanne, ambaye ni Mtutsi. Tulitaka kufika Bugesera, mji ulio umbali wa kilomita 50, ambapo wazazi wangu waliishi pamoja na watoto wetu. Kwa kuwa tulisikia kwamba kuna vizuizi katika barabara zote za kuelekea nje ya mji, tuliamua kwenda kwenye kijiji kilicho karibu na mji wa Kigali, ambako Immaculée alikuwa na mtu wa ukoo aliyeitwa Gahizi, na ambaye pia alikuwa Shahidi wa Yehova. Gahizi, aliyekuwa Mhutu, alitukaribisha na licha ya vitisho kutoka kwa majirani, alifanya yote aliyoweza ili kutusaidia. Askari wa serikali na wapiganaji wa Interahamwe waliposikia kwamba Gahizi alikuwa anawalinda Watutsi, walimpiga risasi.
“Baada ya kumwua Gahizi, askari hao walitupeleka mtoni ili kutuua. Tukiwa na hofu nyingi, tulisubiri kuuawa. Ghafula, kukazuka bishano kali kati ya askari hao, na mmoja wao akasema: ‘Usiue wanawake. Tukiwaua, tutapatwa na mkosi. Huu ni wakati wa kuua wanaume tu.’ Baada ya hapo, André Twahirwa, mmoja wa ndugu waliokuwa wakitufuata na ambaye alikuwa amebatizwa juma lililotangulia, akatupeleka kwake nyumbani licha ya kukatazwa na majirani. Siku iliyofuata, akaandamana nasi hadi Kigali, ambapo alinuia kututafutia mahali salama pa kukaa. Alitusaidia kupita vizuizi kadhaa vya barabarani vilivyokuwa hatari sana. Immaculée alibeba mtoto wangu ili tukikamatwa, aweze kumwokoa. Mimi na Suzanne tulipasua vitambulisho vyetu ili tusigunduliwe.
“Katika kizuizi kimoja, Interahamwe walimgonga Immaculée na kusema, ‘Mbona unasafiri na Watutsi hawa?’ Mimi na Suzanne tulizuiwa tusipite. Hivyo Immaculée na André walitangulia hadi nyumbani kwa Ndugu Rwakabubu. André na ndugu wengine wawili, Simon na Mathias, walihatarisha uhai wao sana ili kutusaidia kupita kizuizi hicho cha mwisho na kunipeleka kwa Ndugu Rwakabubu, naye Suzanne akaenda kwa mmoja wa watu wake wa ukoo.
“Hata hivyo, ilikuwa hatari sana kwangu kuendelea kuishi kwa Ndugu Rwakabubu, hivyo, kwa shida nyingi, ndugu walinisaidia kwenda kwenye Jumba la Ufalme ambapo Mashahidi wengine walifichwa. Kufikia wakati huo, ndugu na dada kumi ambao ni Watutsi walikuwa wamejificha humo. Immaculée alikataa kuniacha. Alisema, ‘Wakikuua nami ninusurike, nitamwokoa mtoto wako.’”c
Wakati huo, Védaste Bimenyimana, ndugu aliyeishi karibu na ambaye alikuwa na mke Mtutsi, alikuwa tu amefaulu kupeleka familia yake mahali salama. Baadaye, akarudi kwenye Jumba la Ufalme kuwasaidia ndugu kukimbilia mahali salama. Inapendeza kwamba wote waliokoka.
Baada ya mauaji, John na Chantal walipata habari kwamba wazazi wao kutia ndani binti zao wawili wenye umri wa miaka miwili na mitano, ambao waliishi pamoja na wazazi hao, walikuwa wameuawa pamoja na watu wengine 100 wa ukoo. Walihisije baada ya kufiwa na watu wengi hivyo? “Mwanzoni, haikuwa rahisi kuvumilia,” asema Chantal. “Tulihisi tumekufa ganzi. Hakuna aliyewazia kwamba watu wengi hivyo wangekufa. Tuliacha yote mikononi mwa Yehova, tukiwa na tumaini la kuwaona watoto wetu tena wakati wa ufufuo.”
WAFICHWA KWA SIKU 75!
Tharcisse Seminega alibatizwa nchini Kongo mwaka wa 1983. Wakati wa mauaji alikuwa akiishi Butare, Rwanda, kilomita 120 hivi kutoka Kigali. Asema, “Baada ya ndege iliyombeba rais kuanguka huko Kigali, tulisikia kwamba amri ilitolewa ya kuwaua Watutsi wote. Ndugu wawili walijaribu kutusaidia tukimbilie Burundi, lakini wapiganaji wa Interahamwe walikuwa wanalinda barabara na vijia vyote.
“Tulikuwa wafungwa katika nyumba yetu wenyewe, na hatukujua twende wapi. Askari wanne walikuwa nje ya nyumba yetu na mmoja wao alisimama mita 180 kutoka nyumba yetu akiwa ametuelekezea bunduki ya rasharasha. Nilisali: ‘Ee Yehova, hatuwezi kufanya chochote ili kujiokoa. Ni wewe tu unayeweza kutusaidia!’ Jioni hiyo, ndugu fulani alikuja nyumbani akihofia kwamba tumeshakufa. Wanajeshi hao walimruhusu kuingia ndani ya nyumba na kukaa kwa dakika chache. Alifurahi sana kupata tuko hai, na akafanikiwa kwenda kwake na watoto wetu wawili. Kisha, akawajulisha ndugu wengine wawili, Justin Rwagatore na Joseph Nduwayezu, kwamba tulikuwa mafichoni na tulihitaji msaada. Wakaja usiku huo; na licha ya shida na hatari, wakatupeleka kwa Justin.
“Hatukukaa kwa Justin sana kwa sababu siku iliyofuata, watu walijua kwamba tumejificha huko. Siku hiyohiyo, mwanamume fulani anayeitwa Vincent alikuja kutuonya kuwa Interahamwe walikuwa wanajitayarisha kutuvamia na kutuua. Mwanamume huyo alikuwa amejifunza Biblia pamoja na Justin lakini hakuwa amechukua msimamo katika kweli. Vincent alipendekeza kwamba tujifiche kwanza katika kichaka kilichokuwa karibu na nyumba ya Justin. Kisha, usiku huo akatupeleka kwake. Alituficha katika kibanda cha mbuzi. Kibanda hicho kilikuwa cha matope, chenye sakafu ya udongo, paa la nyasi, na hakikuwa na dirisha.
“Siku zilionekana kuwa ndefu sana katika kibanda hicho kilichokuwa karibu na makutano ya barabara, na hatua chache tu kutoka soko lenye shughuli nyingi zaidi katika eneo hilo. Tungewasikia wapita-njia wakiongea kuhusu mambo waliyofanya siku hiyo, kutia ndani masimulizi yenye kutisha ya mauaji waliyotekeleza na mambo waliyopanga kufanya. Hofu yetu ilizidi, na tuliendelea kusali tusiuawe.
“Vincent alifanya yote aliyoweza ili kutuandalia mahitaji yetu. Tulikaa hapo kwa mwezi mmoja, na kuelekea mwishoni mwa mwezi wa Mei, mahali hapo pakawa hatari sana kwetu kwa sababu wapiganaji wa Interahamwe walikuwa wakikimbilia eneo hilo kutoka Kigali. Ndugu waliamua kutuhamisha hadi kwa ndugu mmoja aliyekuwa na chumba fulani cha chini ya ardhi ndani ya nyumba yake. Tayari alikuwa anawaficha ndugu watatu ndani ya chumba hicho. Tulitembea usiku kwa muda wa saa nne na nusu na safari hiyo ilikuwa hatari. Mvua kubwa ilinyesha, na kwa sababu hiyo wauaji hawakutuona.
“Maficho yetu mapya yalikuwa shimo lenye urefu wa mita 1.5 na mlango wa ubao. Ili kuingia shimoni, tuliteremka kwa ngazi, na kisha tukachutama na kutambaa kupitia mtaro fulani mpaka tulipofika kwenye sehemu wazi yenye ukubwa wa mita mbili mraba. Kulikuwa na harufu ya kuvu, na ni mwangaza kidogo tu uliotufikia kupitia ufa fulani. Tulikaa hapo pamoja na mke wangu Chantal, watoto wetu watano, na watu wengine watatu. Sote kumi tuliishi kwa woga ndani ya shimo hilo dogo kwa majuma sita. Hatukuthubutu kuwasha mshumaa, kwa kuwa mwangaza ungetusaliti. Hata hivyo, katika shida na kuteseka huko kwote, Yehova alitutegemeza. Ndugu walihatarisha maisha yao kuja kutuletea chakula, dawa, na kututia moyo. Wakati mwingine tuliwasha mshumaa mmoja wakati wa mchana ili kusoma Biblia, gazeti la Mnara wa Mlinzi, au andiko la siku.
“Kila hadithi ina mwisho wake,” Tharcisse aendelea kusema. “Hadithi hiyo ilifikia mwisho Julai 5, 1994. Vincent alitufahamisha kwamba jeshi lililokuwa linawafukuza wapiganaji wa Interahamwe lilikuwa limedhibiti eneo la Butare. Tulipotoka ndani ya chumba hicho cha chini ya ardhi, watu wengine hawakudhani sisi ni Wanyarwanda, tulikuwa tumegeuka rangi na kuwa weupe sana kwa sababu ya kukosa jua. Isitoshe, kwa muda fulani hatungeweza kuzungumza kwa sauti, tulinong’ona tu. Ilituchukua majuma kadhaa kurudia hali ya kawaida.
“Matukio hayo yote yalibadili sana maoni ya mke wangu, ambaye kwa miaka kumi alikataa kujifunza Biblia pamoja na Mashahidi wa Yehova. Lakini sasa, alianza kujifunza Biblia. Watu walipomwuliza kwa nini, alijibu: ‘Nilivutiwa na upendo tulioonyeshwa na akina ndugu na pia jinsi walivyojidhabihu ili kutuokoa. Pia, niliona mkono wenye nguvu wa Yehova, ambaye alituokoa kutoka kwa panga za wauaji.’ Alijiweka wakfu kwa Yehova na akabatizwa katika kusanyiko la kwanza baada ya vita.
“Tunawathamini sana akina ndugu na dada ambao walitusaidia kuokoka kupitia matendo yao na sala zao za kutoka moyoni. Tumejionea wenyewe upendo wao mkubwa unaotoka moyoni, na ambao unashinda tofauti za kijamii.”
KUMSAIDIA ALIYESAIDIA
Baadaye, Justin Rwagatore, mmoja wa akina ndugu waliosaidia familia ya Ndugu Seminega, alihitaji msaada. Mwaka wa 1986 alifungwa gerezani kwa sababu ya kutojiingiza katika siasa za serikali iliyokuwa mamlakani. Miaka kadhaa baada ya kuilinda familia ya Ndugu Seminega, Justin na ndugu wengine walikamatwa tena kwa sababu ya msimamo wao wa kutounga mkono upande wowote. Ndugu Seminega alikuwa mmoja wa ndugu walioenda kukutana na wenye mamlaka kuhusu msimamo wa Mashahidi wa Yehova wa kutojiingiza katika siasa. Aliwaeleza wenye mamlaka jinsi Justin alivyofanya mengi ili kuiokoa familia yake. Hivyo, ndugu wote wakaachiliwa.
Mfano mzuri wa ndugu zetu wakati wa mauaji uliwachochea wengine kuikubali kweli. Suzanne Lizinde, mwanamke Mkatoliki mwenye umri wa miaka 60 na kitu, aliona jinsi dini yake ilivyounga mkono mauaji hayo. Alichochewa kufanya maendeleo ya haraka alipoona mwenendo wa Mashahidi wa Yehova katika eneo la kwao wakati wa mauaji na pia upendo uliopo miongoni mwao. Suzanne alibatizwa Januari 1998 na hakuwahi kukosa mikutano hata kama alilazimika kutembea umbali wa kilomita 5 katika eneo lenye vilima. Pia, aliisaidia familia yake kujifunza kweli. Leo mwana wake mmoja ni mzee wa kutaniko, na mjukuu mmoja ni mtumishi wa huduma.
MAMIA YA MAELFU WATOROKA
Henk van Bussel, mmishonari aliyetumwa Rwanda mwaka wa 1992, alikimbilia Kenya mnamo Aprili 1994, na mara kwa mara alisafiri hadi Goma, mashariki mwa Kongo, ili kusaidia katika juhudi za kutoa misaada kwa wakimbizi wa Rwanda. Wakiwa upande wa Kongo, ndugu walitembea-tembea karibu na vivukio vya mpakani wakiwa wameshika machapisho ya Biblia na wakiimba nyimbo za Ufalme ili Mashahidi waliokuwa wakivuka kutoka Rwanda wawatambue.
Hofu ilitanda kila mahali. Huku vita kati ya vikosi vya serikali na Rwandan Patriotic Front vikiendelea, mamia ya watu walikimbilia nchi ya Kongo na Tanzania. Ndugu waliokimbilia mji wa Goma walikusanyika katika Jumba la Ufalme. Baadaye, kambi ya wakimbizi ilijengwa nje ya mji na ingetoshea zaidi ya watu 2,000—Mashahidi wa Yehova pekee, watoto wao, na watu wenye kupendezwa. Ndugu walianzisha kambi nyingine kama hizo katika maeneo mengine ya mashariki mwa Kongo.
Ijapokuwa watu waliokimbia walikuwa hasa Wahutu walioogopa adhabu, Mashahidi waliokimbia pamoja walikuwa Wahutu na Watutsi. Ilikuwa hatari sana kwa Watutsi kuvuka mpaka na kuingia Goma, kwa kuwa mauaji ya Watutsi yaliendelea. Wakati mmoja, iligharimu dola 100 za Marekani kumsafirisha ndugu mmoja Mtutsi nje ya nchi kisiri.
Wakiwa nchini Kongo, akina ndugu walitaka kukaa pamoja. Hawakutaka kushirikiana kwa vyovyote na Interahamwe, waliokuwa wanaendeleza utendaji wao katika kambi zilizoanzishwa na Umoja wa Mataifa. Isitoshe, wakimbizi wengi wasio Mashahidi waliiunga mkono serikali iliyokuwa inaondolewa mamlakani. Watu hao, na hasa Interahamwe, hawakuwapenda Mashahidi wa Yehova kwa kuwa Mashahidi hawakushirikiana nao. Akina ndugu walitaka kujitenga nao ili pia wawalinde ndugu zao Watutsi.
Wakimbizi hao wa Rwanda walihitaji msaada kwa kuwa waliacha vitu vyao vyote. Mashahidi wa Yehova kutoka Kenya, Kongo, Ubelgiji, Ufaransa, na Uswisi walisaidia kwa pesa, dawa, chakula, mavazi na pia madaktari na wauguzi. Mojawapo ya ndege za kwanza za msaada, ilibeba mahema mengi madogo kutoka ofisi ya tawi ya Ufaransa. Baadaye, ofisi ya tawi ya Ubelgiji ilituma mahema makubwa, ambayo yangetoshea familia nzima-nzima. Pia, vitanda vinavyoweza kubebwa kwa urahisi na vile vya kutiwa hewa ndani vilitumwa. Ofisi ya tawi ya Kenya nayo ilituma zaidi ya tani mbili za nguo na blanketi zaidi ya 2,000.
MLIPUKO WA KIPINDUPINDU
Baada ya kukimbia Rwanda, zaidi ya Mashahidi 1,000 na watu wenye kupendezwa waliishi katika Jumba la Ufalme la Goma na katika sehemu ya ardhi iliyopakana na Jumba hilo. Inasikitisha kwamba kwa sababu ya idadi kubwa ya wakimbizi kulitokea mlipuko wa maradhi ya kipindupindu mjini Goma. Upesi, ofisi ya tawi ya Kongo (Kinshasa) ilituma dawa, na Ndugu Van Bussel akapeleka makatoni 60 ya dawa kutoka Nairobi hadi Goma. Kwa muda, Jumba la Ufalme lilitumiwa kama hospitali, na jitihada zilifanywa ili kuwatenga wagonjwa. Loic Domalain na ndugu mwingine, wote wawili madaktari, pamoja na Aimable Habimana, daktari msaidizi kutoka Rwanda, walifanya kazi mfululizo. Pia, Ndugu Hamel kutoka Ufaransa alisaidia sana na vilevile ndugu na dada wengi wenye ujuzi wa kimatibabu walijitolea kuwatunza wagonjwa.
Licha ya jitihada kubwa za kuzuia ugonjwa huo, zaidi ya ndugu na watu wenye kupendezwa 150 waliathirika, na 40 hivi wakafa kabla ya ugonjwa huo wenye kufisha kukomeshwa. Baadaye, ndugu walikodi sehemu kubwa ya ardhi ambayo ingetumiwa kama kambi ya Mashahidi wa Yehova. Mamia ya mahema madogo-madogo yalisimamishwa, na hema moja kubwa kutoka Kenya lilitumiwa kama hospitali. Wafanyakazi wa afya kutoka Marekani walivutiwa na usafi na mpangilio walioona katika kambi hiyo.
Kufikia mapema Agosti 1994, halmashauri ya kutoa misaada mjini Goma ilikuwa ikiwatunza wakimbizi 2,274—Mashahidi, watoto, na watu wenye kupendezwa. Wakati huohuo, kulikuwa na ndugu wengine wakimbizi katika miji ya Bukavu na Uvira, iliyo mashariki mwa Kongo, na pia nchini Burundi. Wengine 230 walikuwa katika kambi moja ya wakimbizi nchini Tanzania.
Ndugu katika ofisi ya kutafsiri mjini Kigali walipolazimika kukimbilia Goma, walikodi nyumba ili kuendelea na kazi ya kutafsiri. Wakati wa vita akina ndugu walifaulu kuficha kompyuta na jenereta moja na wakazihamisha kutoka Kigali hadi Goma.
Mjini Goma, hamkuwa na huduma za simu wala za kutuma au kupokea barua. Hata hivyo, kwa msaada wa Mashahidi waliofanya kazi katika uwanja wa ndege, ndugu walituma makala walizotafsiri na pia barua nyingine kwa ndege kila juma kutoka Goma hadi Nairobi. Nayo ofisi ya tawi ya Kenya iliwatumia barua kupitia njia hiyohiyo.
Emmanuel Ngirente na watafsiri wengine wawili waliendea kufanya yote waliyoweza ijapokuwa hali zilikuwa ngumu. Hawakutafsiri makala zote za Mnara wa Mlinzi kwa sababu ya vita, lakini makala hizo zilitafsiriwa baadaye na kuchapishwa katika broshua za pekee ambazo ndugu walijifunza katika Funzo la Kitabu la Kutaniko.
MAISHA KATIKA KAMBI ZA WAKIMBIZI
Huku watu wengi wakikimbia kutoka Kigali, Francine, ambaye alikuwa amekimbia na kwenda Goma baada ya mume wake Ananie kuuawa, alihamishwa na kupelekwa katika kambi moja ya Mashahidi. Anasema hivi kuhusu maisha katika kambi: “Kila siku, akina ndugu na dada fulani walipewa mgawo wa kutayarisha chakula. Tulitayarisha uji wa mtama au mahindi kwa ajili ya kiamsha kinywa. Pia, tulipika chakula cha mchana. Baada ya kumaliza kazi, tulienda kuhubiri. Tuliwahubiria hasa watu wa familia zetu ambao si Mashahidi na pia watu walioishi nje ya kambi. Hata hivyo, baada ya muda, wapiganaji wa Interahamwe ambao walikuwa katika kambi nyingine, walikasirika kuona kwamba Mashahidi walikuwa katika kambi tofauti na wakimbizi wengine, na hilo likafanya hali ziwe hatari sana.”
Kufikia Novemba 1994, ilidhihirika wazi kwamba ni salama kwa ndugu kurudi Rwanda. Kwa kweli, ingefaa sana kurudi kwa sababu ya ukosefu wa usalama katika kambi za watu wasio Mashahidi zilizokuwa Kongo. Lakini ingekuwa vigumu kurudi. Interahamwe walinuia kujipanga tena na kuivamia Rwanda, na hivyo, mtu yeyote aliyerudi Rwanda kutoka Kongo alionwa kuwa msaliti.
Ndugu waliijulisha serikali ya Rwanda kwamba Mashahidi wa Yehova hawakuunga mkono vita wala kushiriki katika mauaji ya Watutsi, na walitaka kurudishwa Rwanda. Serikali iliwashauri wazungumze na Tume ya Umoja wa Mataifa Inayoshughulikia Wakimbizi (UNHCR), kwa kuwa ilikuwa na magari yanayoweza kutumiwa kuwarudisha nyumbani. Hata hivyo, kwa sababu Interahamwe wangewazuia kurudi Rwanda, ilibidi ndugu watumie maarifa.
Ndugu walitangaza kwamba kutakuwa na kusanyiko la pekee mjini Goma, na wakatayarisha mabango ya kusanyiko. Kisha wakawajulisha Mashahidi kisiri kuhusu mipango ya kurudishwa Rwanda. Ili kuepuka kutokeza shaka, ndugu waliagizwa kuacha vitu vyao vyote na kubeba tu Biblia zao na vitabu vya nyimbo kana kwamba wanaenda kusanyikoni.
Francine anakumbuka kwamba walitembea kwa saa kadhaa kisha wakapata malori yaliyowabeba hadi mpakani. Walipovuka mpaka na kuingia Rwanda, tume ya UNHCR iliwasafirisha mpaka Kigali na kisha kwenye maeneo ya nyumbani kwao. Hivyo, ndugu wengi, familia zao, na watu wenye kupendezwa walirudi Rwanda mnamo Desemba 1994. Gazeti moja la Ubelgiji, Le Soir, la Desemba 3, 1994, liliripoti: “Wakimbizi 1,500 wa Rwanda waliamua kuondoka Zaire [Kongo] kwa sababu walihofia usalama wao. Hao ni Mashahidi wa Yehova ambao walikuwa na kambi yao wenyewe karibu na kambi ya Katale. Mashahidi wa Yehova walinyanyaswa sana na serikali iliyopita kwa sababu walikataa kubeba silaha na kushiriki katika mikutano ya kisiasa.”
Baada ya kurudi Rwanda, Francine alifanikiwa kuhudhuria kusanyiko la wilaya mjini Nairobi. Akiwa amefarijiwa baada ya kifo cha mume wake na kuimarishwa na ushirika wa akina ndugu na dada, Francine alirudi kwenye ofisi ya kutafsiri ambayo ilikuwa imefunguliwa tena huko Kigali. Baadaye, aliolewa na Emmanuel Ngirente, na wanaendelea kutumika katika ofisi ya tawi.
Francine alikabilije hisia zake wakati wa vita? Asema: “Tulikuwa na jambo moja tu akilini wakati huo— lazima tuvumilie hadi mwisho. Tuliamua kutofikiria sana mambo mabaya yaliyokuwa yanaendelea. Nilifarijiwa na andiko la Habakuki 3:17-19, linaloongea kuhusu kupata shangwe wakati wa hali ngumu. Ndugu na dada walinitia moyo sana. Hata wengine waliniandikia barua. Hilo lilinisaidia kuwa na mtazamo unaofaa na wa kiroho. Nilikumbuka jinsi Shetani alivyo mjanja. Tukikazia fikira aina moja ya matatizo, huenda atunase kupitia aina nyingine. Tusipokaa macho, tunaweza kuwa dhaifu katika njia moja au nyingine.”
KURUDI RWANDA
Ndugu Van Bussel aliwasaidia sana ndugu waliorudi. Aeleza: “Mpango fulani ulianzishwa ili kusaidia ndugu waweze tena kukimu mahitaji ya familia zao, kutia ndani wale waliobaki nchini na kupoteza karibu kila kitu. Ndugu waliowekwa rasmi walitembelea kila kutaniko ili kujua mahitaji ya wahubiri. Familia na watu mmoja-mmoja walipewa msaada kulingana na uhitaji. Ndugu walielewa kwamba baada ya miezi mitatu, wangelazimika kujikimu wenyewe.”
Bila shaka, mahitaji ya kiroho ya akina ndugu yalizingatiwa. Watafsiri walirudi Kigali katika nyumba waliyoitumia kabla ya vita. Ndugu Van Bussel akumbuka kwamba nyumba waliyoitumia kama ofisi ilijaa matundu ya risasi lakini idadi kubwa ya vitabu vilivyokuwa kwenye depo bado vilikuwepo. Kwa miezi mingi baada ya hapo, walipata risasi ndani ya katoni za machapisho. Hata mmoja wa watafsiri alipata bomu la mkononi kwenye bustani! Mwaka uliofuata, Oktoba 1995 hivi, kikundi cha kutafsiri kilihamia jengo kubwa zaidi, na lenye kufaa zaidi lililokuwa katika sehemu nyingine ya mji. Jengo hilo la kukodi lilitumiwa kwa ajili ya ofisi na makazi mpaka ofisi mpya ya tawi ilipojengwa mwaka wa 2006.
“ILIKUWA KAMA WAKATI WA UFUFUO!”
Kufikia Desemba 1994, ndugu wengi walikuwa wamerudi kutoka Kongo kabla tu ya kusanyiko la wilaya. Kichwa cha kusanyiko hilo, “Hofu ya Kimungu,” kilifaa kabisa. Lilipangiwa kufanywa katika uwanja wa Jumba moja la Ufalme mjini Kigali. Ndugu kutoka Kenya, Ufaransa, na Uganda walihudhuria. Ijumaa asubuhi, ndugu walijaa katika uwanja wa jumba hilo. Dada mmoja akumbuka: “Iligusa moyo sana kuona ndugu na dada wakikumbatiana huku machozi yakiwatoka. Ilikuwa mara ya kwanza kuonana tangu vita vianze. Waliwaona marafiki ambao hawakudhani wako hai!” Mwingine alisema, “Ilikuwa kama wakati wa ufufuo!”
Günter Reschke alikuwa mmoja wa wahudhuriaji kutoka Kenya. Alisema: “Ilikuwa shangwe kama nini kuonana tena baada ya shida zote hizo na kuona watu waliokuwa wameokoka! Hata hivyo, kulikuwa na tatizo fulani. Wenye mamlaka walikuwa na wasiwasi walipoona umati jinsi hiyo umekusanyika pamoja. Mapema alasiri, askari wenye silaha walifika na kuvunjilia mbali kusanyiko hilo kwa kuhofia usalama. Tulilazimika kuondoka mara moja. Tulichukua muda fulani kuwatia moyo rafiki zetu lakini hatimaye ikabidi turudi Nairobi, tukiwa tumetamauka kwa sababu ndugu hawakusikiliza programu. Ingawa tulivunjika moyo, tulihisi kwamba tulifanya yote tuliyoweza kuwatia moyo ndugu waendelee kushikilia imani, na tuliondoka tukiwa na uhakika kwamba waliazimia kufanya hivyo.”
Kwa sababu kulikuwa na amani kwa kadiri fulani, watu wengi wenye asili ya Rwanda na ambao waliishi nje ya nchi waliamua kurudi. Wengine kati ya waliorudi walizaliwa nje ya nchi baada ya wazazi wao kukimbia wakati wa misukosuko ya kijamii na ya kisiasa mwishoni mwa miaka ya 1950 na mwanzoni mwa miaka 1960. Miongoni mwao kulikuwa na watu ambao walijifunza kweli katika nchi nyingine. Kwa mfano, James Munyaburanga na familia yake walijifunza kweli katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Kwa kuwa serikali mpya ya Rwanda iliwapa kazi watu wengi waliorudi nchini, Ndugu Munyaburanga alipata kazi pia. Hata hivyo, aliporudi Rwanda, alipingwa na kudhihakiwa na watu wa ukoo na wafanyakazi wenzake kwa sababu ya kuishi kulingana na kanuni za Kikristo. Mwishowe, aliomba kustaafu mapema na akawa painia wa kawaida. Sasa yeye ni mwakilishi wa kisheria wa Mashahidi wa Yehova nchini Rwanda.
Ngirabakunzi Mashariki alijifunza kweli akiwa mashariki mwa Kongo. Asema: “Kwa kuwa nilikuwa Mtutsi, nilibaguliwa kwa miaka mingi. Nilipoanza kushirikiana na Mashahidi wa Yehova, ilikuwa ni kama niko katika dunia nyingine! Ilikuwa kama muujiza kushirikiana na watu waliochukua mambo kwa uzito na kuishi kulingana na mambo waliyofundisha. Upendo wao ulionekana wazi zaidi wakati wa mauaji ya Watutsi mwaka wa 1994. Ndugu walituficha na kutulinda mimi na familia yangu. Nilialikwa Betheli mwaka wa 1998, ambapo ninatumika nikiwa na mke wangu, Emerance. Nangojea kwa hamu ulimwengu mpya, ambapo hakutakuwa na chuki ya kijamii na ubaguzi, na dunia itajaa watu wanaoliitia jina la Yehova na kuishi pamoja kwa amani.”
KAZI YA KUHUBIRI YAANZA KUSONGA MBELE TENA
Mnamo Machi 1994, kabla tu ya vita kuanza, kulikuwa na wahubiri 2,500 nchini Rwanda. Kufikia Mei 1995, kulikuwa na kilele kipya cha wahubiri 2,807, licha ya kwamba wengi sana waliuawa wakati wa mauaji. Watu wenye mioyo minyoofu walimiminika katika tengenezo la Yehova. Kwa mfano, dada mmoja painia wa pekee aliongoza zaidi ya mafunzo 22 ya Biblia, na bado alikuwa na orodha nyingine ya watu waliotaka kujifunza! Mwangalizi mmoja wa mzunguko alisema, “Vita viliwasaidia watu kutambua kwamba kufuatilia vitu vya kimwili ni kazi bure.”
Januari 1996, kulikuwa na Kusanyiko la Wilaya lenye kichwa “Wasifaji Wenye Shangwe.” Lilikuwa kusanyiko lenye shangwe kama nini! Kusanyiko hilo lilikuwa la kwanza la wilaya baada ya vita kwa kuwa lile lililotangulia lilifutiliwa mbali. Mtazamaji mmoja alisema, “Watu walikumbatiana huku wakitokwa na machozi, na ilivutia hasa kuona ndugu Wahutu na Watutsi wakikumbatiana.” Kilele cha hudhurio kilikuwa 4,424, na 285 wakabatizwa. Ndugu Reschke akumbuka: “Ilisisimua sana kusikia watakaobatizwa wakijibu kwa furaha ‘Yego!’ (ndiyo) walipoulizwa yale maswali mawili ya ubatizo. Walipanga foleni uwanjani wakisubiri kubatizwa, na mvua kubwa iliyonyesha ikawalowesha kabisa. Lakini hilo halikuwahangaisha. Ni kana kwamba walisema moyoni, ‘Si bado tutazamishwa ndani ya maji!’”
Henk van Bussel alirudi Rwanda; na Günter Reschke, aliyekuja kusaidia kuanzisha kazi upya, akapewa mgawo rasmi wa kutumika nchini Rwanda. Muda mfupi baadaye, Godfrey na Jennie Bint wakarudi Rwanda pia.
MWANA WAO ALIYEPOTEA APATIKANA!
Katika miaka iliyofuata baada ya vita, familia zilizokuwa zimetenganishwa ziliungana tena. Kwa mfano, mnamo 1994, vita vilipokuwa vimechacha huko Kigali, karibu watu wote walikimbia wakati mmoja. Katika vurugu hizo, Oreste Murinda alitenganishwa na mke wake na akakimbilia mji wa Gitarama pamoja na mwana wao mwenye umri wa miaka miwili na nusu. Oreste alipoenda kutafuta chakula, vita vilianza na akatenganishwa na mwanawe katika rabsha hizo.
Baada ya vita, Oreste na mke wake waliungana tena lakini hawakumpata mwana wao. Walikata kauli kwamba aliuawa. Lakini, zaidi ya miaka miwili baadaye, mwanamume fulani kutoka eneo la mashambani, na ambaye hakuwa Shahidi, alienda kufanya kazi mjini Kigali. Alikutana na ndugu fulani na akawatajia kwamba familia moja iliyoishi karibu naye huko Gisenyi, ilifiwa na watoto wao vitani lakini walikuwa wanatunza yatima fulani. Mtoto huyo alikumbuka jina la baba yake na alisema kwamba wazazi wake ni Mashahidi wa Yehova. Ndugu walilitambua jina hilo na wakawasiliana na Oreste na mke wake, ambao walimwonyesha mwanamume huyo picha za mwana wao. Ndiyo, mtoto huyo alikuwa wao! Mara moja Oreste akaenda kumchukua, na wazazi hao wakaunganishwa tena na mwana wao baada ya miaka miwili na nusu! Leo hii, mvulana huyo ni mhubiri aliyebatizwa.
Inafurahisha kwamba ndugu waliwatunza watoto wote ambao walifiwa na wazazi wao Mashahidi. Hakuna yeyote aliyewekwa katika makao ya watoto yatima. Nyakati nyingine ndugu walitunza watoto wa watu waliokuwa majirani wao au wa watu wa ukoo. Mume na mke fulani, ambao walikuwa na watoto wao kumi, walichukua mayatima wengine kumi.
ENEO LA KASKAZINI LAKUMBWA TENA NA UKOSEFU WA USALAMA
Kufikia mwishoni mwa mwaka wa 1996, vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Kongo vilifanya iwe vigumu sana kudumisha usalama katika kambi za wakimbizi, ambazo zilikuwa na watu zaidi ya milioni moja kutoka Rwanda. Mnamo Novemba, wakimbizi walilazimika ama kurudi Rwanda au kukimbilia ndani ya misitu ya mvua ya Kongo. Wengi wao walirudi, kutia ndani ndugu walioachwa na wengine mnamo Desemba 1994. Lilikuwa jambo lisilosahaulika kuona maelfu ya watu, wazee kwa vijana, wakitembea katika barabara za Kigali wakiwa wamevalia nguo chafu na mizigo vichwani. Kila mmoja wa wakimbizi hao alipaswa kurudi katika eneo la kwao ili kuandikishwa upya. Hilo lilitokeza ukosefu wa usalama kwa muda fulani.
Inasikitisha kwamba watu wengi wabaya walirudi pamoja na wakimbizi, kutia ndani wapiganaji fulani wa Interahamwe, ambao walijaribu kuendeleza vita katika eneo la kaskazini-magharibi mwa nchi. Hivyo, wanajeshi walitumwa huko kurudisha usalama. Wengi wa ndugu zetu waliishi katika eneo hilo, na ilikuwa vigumu sana kwao kudumisha msimamo wao kutounga mkono upande wowote. Zaidi ya wahubiri 100 waliuawa kati ya mwaka wa 1997 na 1998, na wengi wao waliuawa kwa sababu ya kushikilia msimamo huo wa Kikristo. Nyakati nyingine, eneo hilo lilikuwa hatari sana hivi kwamba waangalizi wa mzunguko hawakwenda huko kwa ukawaida.
WENZI WA NDOA WENYE UJASIRI
Théobald Munyampundu, na mke wake, Berancille, alikuwa mmoja wa waangalizi wa mzunguko wachache walioweza kuyatembelea makutaniko katika eneo hilo hatari. Walikuwa wamezoea hatari. Théobald alibatizwa mwaka wa 1984, na miaka miwili baadaye alikuwa mmoja wa ndugu na dada wengi waliofungwa gerezani na kupigwa sana. Yeye na mke wake walikuwa pia wamehatarisha uhai wao kwa kuficha wengine wakati wa mauaji ya Watutsi. Baada ya kumwokoa kijana mmoja tineja ambaye mama yake aliuawa wakati wa mauaji, walienda Tanzania. Huko, Théobald alitembelea kambi mbili za wakimbizi zilizokuwa Benaco na Karagwe ili kuwafariji akina ndugu, ingawa ilikuwa hatari sana kusafiri kati ya kambi hizo kwa sababu ya magaidi.
Waliporudi Rwanda, Théobald na mke wake walihatarisha uhai wao tena ili kuwatembelea Mashahidi katika eneo hatari la kaskazini-magharibi. Théobald alisema, “Wakati mwingine, makutaniko yalikuwa mbali. Kwa sababu ya ukosefu wa usalama hatungelala huko. Nakumbuka ziara fulani wakati wa majira ya mvua, ambapo tulitembea kwa saa nne kwenda kuwatembelea akina ndugu, na saa nne kurudi mahali tulikolala.”
Théobald alisema hivi kuhusu ndugu mmoja aliyekutana naye alipotembelea kikundi kimoja cha mbali katika eneo hilo: “Jean-Pierre ni kipofu, lakini nilishangaa kumwona akienda jukwaani kwa ajili ya usomaji wa Biblia wakati wa Shule ya Huduma ya Kitheokrasi, na kukariri sehemu yote, bila kukosea, na hata akizingatia alama za vituo! Alikuwa amemwomba ndugu fulani msomaji mzuri amsomee ili akariri maandiko hayo. Nilitiwa moyo sana na jitihada zake.”
Anapofikiria kuhusu maisha yake yenye shughuli nyingi na wakati mwingine yaliyokuwa hatarini, Théobald anasema: “Katika nyakati zote hizo ngumu, tulimtegemea Yehova na mara nyingi tulifikiria kuhusu maneno ya Waebrania 13:6: ‘Yehova ni msaidizi wangu; sitaogopa. Mwanadamu anaweza kunitenda nini?’” Baada ya kutumika kwa uaminifu katika kazi ya mzunguko na ya wilaya, yeye na mke wake wanaendelea na utumishi wa painia wa pekee licha ya matatizo ya afya.
MRADI WA UJENZI WA JUMBA LA KUSANYIKO
Idadi ya Mashahidi ilipoendelea kuongezeka, ilikuwa vigumu hata zaidi kupata mahali panapofaa kufanya makusanyiko ya wilaya mjini Kigali. Kwa mfano, mtaro wa maji-taka kutoka gereza lililokuwa karibu ulivuja, na hivyo kuwasumbua wahudhuriaji wakati wa Kusanyiko la Wilaya la “Wajumbe wa Amani ya Kimungu” lililofanywa katika uwanja fulani mnamo Desemba 1996. Ndugu walilalamika kuhusu harufu mbaya, na wazazi walihofia afya ya watoto wao. Kwa sababu ya hali hizo mbaya, Halmashauri ya Nchi iliamua kwa kauli moja kwamba, hawangefanya tena kusanyiko katika uwanja huo. Lakini makusanyiko ya wilaya yangefanyiwa wapi kwingine?
Wizara ya Ardhi ilikuwa imewapa ndugu wa mojawapo ya makutaniko mjini Kigali, kipande cha ardhi ili wajenge Jumba la Ufalme. Ardhi hiyo ilikuwa kubwa kuliko ilivyohitajiwa, na kama ndugu wangewasilisha ramani za ujenzi wa Jumba la Ufalme pekee, ni wazi kwamba wizara ingechukua sehemu ya ardhi hiyo na kumpa mwingine. Hivyo, walimtegemea Yehova na kupeleka ramani za Jumba la Ufalme na Jumba sahili la Kusanyiko, na pia wakaonyesha kwamba wangejenga Jumba lingine la Ufalme baadaye. Wenye mamlaka walikubali ramani hizo.
Ndugu walitayarisha ardhi na wakaweka ua. Mamia ya wajitoleaji walifyeka vichaka na kuchimba vyoo. Sasa walikuwa na uwanja wenye kupendeza, uliokuwa na mwinuko mdogo na uliofaa sana kwa ajili ya kusanyiko.
Miezi iliyofuata, ndugu walifanya makusanyiko mawili na mkutano wa pekee katika uwanja huo, lakini walilazimika kusukumana chini ya mahema na miavuli kwa sababu ya upepo mkali na mvua. Hivyo, wakawasiliana na Baraza Linaloongoza wakiomba kujenga Jumba la Kusanyiko lisilo na kuta.
Mnamo Machi 1998, Baraza Linaloongoza liliidhinisha ujenzi wa jumba hilo. Matayarisho yalianza mara moja. Katika kipindi chote cha ujenzi, familia nzima-nzima zilifanya kazi pamoja, wakichimba mashimo ya nguzo. Wote walifanya kazi bega kwa bega na kwa umoja. Mnamo Machi 6, 1999, Jean-Jules Guilloud kutoka ofisi ya tawi ya Uswisi alitoa hotuba ya kuwekwa wakfu jengo hilo zuri.
Kufikia mwaka wa 1999, hali ya usalama ilikuwa imerejea nchini kote. Februari mwaka huo, wamishonari wapya ambao ni wenzi wa ndoa, Ralph na Jennifer Jones, walipewa mgawo wa kutumika katika ofisi ya nchi ya Rwanda, na hivyo idadi ya Wanabetheli ikafikia 21.
Ndugu wawili kutoka Rwanda walikuwa wamehitimu Shule ya Mazoezi ya Kihuduma (sasa Shule ya Biblia ya Ndugu Waseja) huko Kinshasa, Kongo, umbali wa karibu kilomita 1,600. Hata hivyo, kwa sababu ya vita nchini Kongo, ilikuwa vigumu sana kwa ndugu kusafiri kutoka Rwanda hadi Kinshasa. Hivyo, Baraza Linaloongoza lilikubali Shule ya Mazoezi ya Kihuduma ifanywe mjini Kigali. Wanafunzi 28 wa darasa la kwanza kutoka Burundi, Kongo, na Rwanda walihitimu mnamo Desemba 2000.
Mnamo Mei 2000, Rwanda ikawa ofisi ya tawi, na muda mfupi baadaye, ndugu wakapata uwanja mzuri ambapo wangejenga ofisi ya tawi ili kushughulikia kazi iliyokuwa inaongezeka kwa kasi nchini Rwanda. Walinunua ardhi yenye ukubwa wa ekari 5 mnamo Aprili 2001. Ndugu wengi wa Kigali wanakumbuka kazi ngumu waliyofanya ya kufyeka kichaka katika ardhi hiyo iliyokuwa imeachwa ukiwa kwa miaka mingi.
VOLKANO YALIPUKA MASHARIKI MWA KONGO
Mnamo Januari 17, 2002, volkano ya Nyiragongo, kilomita 16 kutoka mji wa Goma, mashariki mwa Kongo, ililipuka na watu wengi katika eneo hilo walilazimika kukimbia. Wengi wa wahubiri 1,600 walioishi humo walivuka mpaka na kuingia Gisenyi, Rwanda, wakiwa pamoja na watoto wao na watu wenye kupendezwa. Huko, walielekezwa kwenye Majumba ya Ufalme yaliyo karibu.
Siku iliyofuata, ndugu wa ofisi ya tawi ya Rwanda waliwapelekea tani tatu za msaada kutia ndani chakula, blanketi na dawa. Upesi, vitu hivyo vilisambazwa kwa ndugu kwenye Majumba sita ya Ufalme yaliyo katika sehemu hiyo ya mpakani.
Kwa sababu za usalama, serikali ya Rwanda haikufurahia kuona wananchi wengi hivyo kutoka Kongo wakiishi kwenye Majumba ya Ufalme. Hivyo, wakasisitiza kwamba ndugu hao wapelekwe kwenye kambi za wakimbizi. Ndugu wa Halmashauri ya Tawi ya Rwanda walikutana mjini Goma pamoja na washiriki wawili wa Halmashauri ya Tawi ya Kongo na wazee wa makutaniko ya Goma, ili kuamua la kufanya. Ndugu kutoka Kongo walisisitiza kwamba hawakutaka wenzao wapelekwe kwenye kambi za wakimbizi. Walisema, “Mwaka wa 1994 tuliwatunza ndugu zaidi ya 2,000 wa Rwanda pamoja na familia zao na watu wenye kupendezwa, kwa hiyo, msiruhusu ndugu zetu waende kwenye kambi, acheni warudi Goma, na tutawatunza kama tulivyowatunza ndugu zetu kutoka Rwanda.”
Ndugu kutoka Kongo walifanya tendo la ukarimu na upendo walipowachukua watu wao wenyewe na kuishi nao badala ya kuwaacha wakae katika kambi zilizosimamiwa na watu ambao si Mashahidi. Basi, ndugu walirudi Goma pamoja na familia zao na wakaishi pamoja na Mashahidi wengine. Baada ya hapo, misaada zaidi, kutia ndani mahema ya plastiki, ilitumwa kutoka Ubelgiji, Ufaransa, na Uswisi. Ndugu hao walikaa Goma hadi walipojengewa nyumba.
MATUKIO MUHIMU YA KITHEOKRASI
Kuhusiana na ofisi mpya ya tawi, Ofisi ya Uhandisi ya Kimkoa nchini Afrika Kusini ilichora ramani za ujenzi, na mjenzi fulani wa Rwanda akaajiriwa kufanya kazi hiyo. Wajitoleaji wa kimataifa walisaidia, na Mashahidi wengi wa Rwanda walijitolea kusaidia kutengeneza bustani na kumalizia kazi nyinginezo. Licha ya matatizo fulani-fulani, familia ya Betheli ilihamia jengo hilo maridadi mwezi wa Machi 2006. Baadaye mwaka huo, Guy Pierce wa Baraza Linaloongoza pamoja na mke wake, alikuja kwa ajili ya programu ya pekee ya kuwekwa wakfu kwa jengo hilo mnamo Desemba 2, 2006. Ndugu 553, kutia ndani wajumbe 112 kutoka nchi 15, walihudhuria programu hiyo.
Jim na Rachel Holmes, kutoka Kanada, walifanya kazi katika mradi huo wa ujenzi. Walijua Lugha ya Ishara ya Marekani na walijitolea kufundisha Mwanabetheli yeyote aliyependezwa, Jumatatu baada ya Funzo la Mnara wa Mlinzi la familia ya Betheli. Wanabetheli sita walipendezwa na waliielewa lugha hiyo vizuri sana hivi kwamba kikundi cha lugha ya ishara kilianzishwa punde baadaye.
Kisha, mnamo Juni 2007, Kevin Rupp, mmishonari aliyehudhuria Shule ya Mazoezi ya Kihuduma nchini Uswisi, alikuja Rwanda kusaidia katika lugha ya ishara. Punde baadaye, wenzi wa ndoa wamishonari kutoka Kanada na ambao walifahamu lugha ya ishara waliwasili nchini Rwanda. Mnamo Julai 2008, ndugu walianzisha kutaniko la lugha ya ishara na muda mfupi baada ya hapo, vikundi vingi vilianzishwa.
Ndugu walifurahi kama nini wakati wa kusanyiko la wilaya la 2007, walipotangaziwa kutolewa kwa Tafsiri ya Ulimwengu Mpya ya Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo katika Kinyarwanda! Biblia nzima katika Kinyarwanda ilitafsiriwa na Muungano wa Vyama vya Biblia mwaka wa 1956. Ijapokuwa watafsiri hao walikuwa wanyoofu katika jitihada zao za kuitafsiri Biblia katika lugha ya kawaida, na hata wakatumia jina YEHOVA mara saba katika Maandiko ya Kiebrania, Tafsiri ya Ulimwengu Mpya inapatikana kwa urahisi kwa watu wote, na hasa wenye mapato madogo. Watafsiri walijitahidi sana na walishirikiana na Idara ya Huduma za Tafsiri jijini New York, ili kutokeza tafsiri hiyo sahihi na rahisi kusoma. Iligusa moyo sana kuona watoto wengi katika Jumba la Ufalme wakiwa na nakala zao za Biblia hiyo na wakiinua mkono kwa hamu ili wasome andiko wakati wa mikutano!
MATATIZO YA KUTOUNGA MKONO UPANDE WOWOTE YAZUKA TENA
Ingawa ndugu zetu wamefurahia uhuru wa ibada tangu walipoandikishwa kisheria mwaka wa 1992, bado wanaendelea kupata matatizo yanayohusiana na msimamo wa Kikristo wa kutounga mkono upande wowote. Katika miaka 15 iliyopita, mamia ya ndugu wamekamatwa kwa sababu hawashiriki kushika doria za usiku zinazosimamiwa kijeshi. Hata hivyo, ndugu walipofanya mkutano na waziri wa serikali, wenye mamlaka waliwaruhusu ndugu wafanye kazi ya badala.
Katika miaka ya karibuni walimu 215 wa shule wamepoteza kazi zao kwa sababu ya kukataa kuhudhuria semina zinazohusisha mambo ya siasa. Baadaye, watoto 118 walifukuzwa shuleni kwa sababu ya kukataa kuimba wimbo wa taifa. Wawakilishi wa ofisi ya tawi walienda kwa wenye mamlaka kueleza msimamo wetu, na baada ya miezi mingi, wengi wa watoto waliofukuzwa waliruhusiwa kurudi shuleni. Wakirejelea historia, ndugu hao walisema kwamba mnamo 1986, Mashahidi wa Yehova walifungwa gerezani kwa sababu ya msimamo wao wa kutounga mkono upande wowote, na msimamo huohuo ndio uliowafanya wasishiriki katika mauaji ya jamii nzima-nzima mwaka wa 1994.—Yoh. 17:16.
Mashahidi wa Yehova hutii sheria za serikali na wanadumisha msimamo wa kutounga mkono upande wowote chini ya serikali yoyote ile. Kwa mfano, mnamo 1986, François-Xavier Hakizimana alifungwa gerezani kwa miezi 18 kwa sababu ya msimamo wake wa kutounga mkono upande wowote. Serikali ilipobadilishwa baada ya mauaji, alifungwa gerezani tena mwaka wa 1997 na 1998 kwa sababu hiyohiyo. Mifano ya watu kama hao inaonyesha kwamba Mashahidi wa Yehova hushikilia msimamo wao nyakati zote na si kwa sababu wanaipinga serikali fulani. Msimamo wa Kikristo wa kutounga mkono upande wowote unategemea kanuni za Maandiko.
Kando na matatizo hayo yanayoendelea, ndugu wanafurahia uhuru wa kufanya mikutano, makusanyiko, na pia kuhubiri na kufanya mikutano katika magereza mengi, ambapo wafungwa wengi wameikubali kweli. Isitoshe, katika mwaka wa utumishi wa 2009 watu wa Yehova nchini Rwanda, walishinda kesi sita za mahakamani.
WAKATI UJAO MWANGAVU
Simulizi kuhusu Rwanda haliwezi kukamilika bila kutaja kifupi mafanikio yenye kustaajabisha katika programu ya ujenzi wa Majumba ya Ufalme. Tangu mpango mpya wa kujenga Majumba ya Ufalme katika nchi zisizo na uwezo mkubwa wa kifedha uanzishwe mwaka wa 1999, Majumba ya Ufalme 290 yasiyo ghali lakini yenye kuvutia yamejengwa na wajitoleaji.
Kwa kuwa wahubiri wa kutaniko huwaunga mkono sana ndugu hao wajitoleaji, majumba mengi hujengwa kwa miezi mitatu tu. Kwa kuwa Majumba ya Ufalme hujengwa kwa kasi sana, watazamaji hushangaa, na hilo hutokeza fursa za kutoa ushahidi. Kando na Jumba la Kusanyiko mjini Kigali, ndugu wamejenga majumba mengine kumi madogo yasiyo na kuta, hivyo kuwawezesha wahubiri kuhudhuria makusanyiko pasipo na uhitaji wa kutembea kwa muda mrefu katika nchi hii yenye milima na mabonde. Vilevile, ndugu wamejenga Majumba ya Ufalme manne yanayoweza kupanuliwa na hivyo inawezekana kufanya makusanyiko katika majumba hayo.
Miezi michache ya kwanza kila mwaka, makutaniko yote hushiriki kwa bidii kuhubiri katika maeneo yasiyogawiwa mtu au yasiyohubiriwa kwa ukawaida. Nyakati nyingine, wahubiri husafiri mbali na kwa gharama yao wenyewe ili kuhubiri maeneo hayo. Mapainia wa pekee wa muda hutumwa kwa miezi mitatu katika maeneo yaliyo mbali zaidi. Hilo hutokeza vikundi vipya ambavyo baadaye huwa makutaniko. Kwa mfano, katika kampeni iliyoanza Januari hadi Machi 2010, mamia ya mafunzo ya Biblia yalianzishwa na vikundi tisa vipya vikaanzishwa. Isitoshe, katika kipindi hichohicho, mapainia wa pekee 30 wa muda walianzisha vikundi vipya 15.
TUKIO LINGINE MUHIMU NCHINI RWANDA
Katika Kusanyiko la Wilaya “Endeleeni Kukesha!” la mwaka wa 2009, ndugu nchini Rwanda walifurahi kusikia kutolewa kwa kitabu kipya cha nyimbo na kusikiliza baadhi ya nyimbo hizo zikiimbwa katika Kinyarwanda. Kitabu hicho kilitafsiriwa kwa wakati, na ndugu wakapokea nakala zao kwa wakati ili wajiunge na ndugu wenzao ulimwenguni pote walipoanza kukitumia mikutanoni mnamo Januari 2010.
Ni wazi kwamba baada ya kutolewa kwa Tafsiri ya Ulimwengu Mpya ya Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo katika Kinyarwanda mnamo 2007, kila mtu aliwaza ni wakati gani Biblia nzima ingetafsiriwa katika Kinyarwanda. Makusanyiko ya wilaya ya 2010 yalipokaribia, ilitangazwa kwamba Guy Pierce, mshiriki wa Baraza Linaloongoza angetembelea Rwanda wakati wa kusanyiko la Kigali mwezi wa Agosti. Kusanyiko hilo lingefanywa katika uwanja wa michezo uliokuwa karibu na ofisi ya tawi. Watu walisisimka na kujawa na furaha wakati Ndugu Pierce alipotangaza kutolewa kwa tafsiri nzima ya Biblia Takatifu—Tafsiri ya Ulimwengu Mpya katika Kinyarwanda! Wahudhuriaji wote 7,149 walipokea nakala ya Biblia hiyo mpya. Siku ya Jumapili, ndugu kutoka maeneo mengine ya Rwanda walihudhuria, na hivyo hudhurio likafikia 11,355. Wakati wa kusanyiko, askari waliokuwa wakitembea nje ya uwanja huo waliomba nakala za Biblia hiyo, na wakapewa nakala 180. Pia, meya wa mji wa Kigali, mkuu wa polisi, na wenye mamlaka katika Wizara ya Michezo walifurahi sana kupokea nakala zao.
Kazi ya kuhubiri habari njema nchini Rwanda ilianza mwaka 1970, kukiwa na wahubiri watatu. Sasa kuna wahubiri 20,000 hivi nchini. Wanaongoza mafunzo ya Biblia karibu 50,000 kila mwezi. Mnamo Aprili 2011, watu 87,010 walihudhuria Ukumbusho. Ndugu wa Rwanda wanajulikana kwa bidii yao katika utumishi. Asilimia 25 hivi ya wahubiri wako katika utumishi fulani wa wakati wote na hao wengine wanatumia wastani wa saa 20 kila mwezi katika utumishi. Ndugu zetu wanafanya kazi kwa bidii pamoja na “Bwana wa mavuno” katika shamba hili lenye rutuba, bila nia ya kupunguza bidii yao. Huku Yehova akiendelea kubariki kazi, tunasubiri kwa hamu kuona ni watu wangapi zaidi watamiminika katika mlima wa Yehova wa ibada ya kweli katika Nchi hii ya Milima Elfu.—Mt. 9:38; Mika 4:1, 2.
[Maelezo ya Chini]
a Kwa kawaida huitwa Kongo au Kongo (Kinshasa) ili kuitofautisha na nchi jirani ya Kongo (Brazzaville). Katika masimulizi haya, tutatumia jina Kongo.
b Deborah alifanya maendeleo na kuwa mhubiri, akabatizwa akiwa na umri wa miaka kumi, na sasa yeye ni painia wa kawaida pamoja na mama yake.
c Mtoto huyo sasa ni dada aliyebatizwa.
[Blabu katika ukurasa wa 178]
Aliwaambia wasikilizaji wake wajihadhari na Mashahidi wa Yehova
[Blabu katika ukurasa wa 181]
Walisalimiana kwa kusema “Komera!” yaani, “Jipe moyo!”
[Blabu katika ukurasa wa 218]
“Ee Yehova, hatuwezi kufanya chochote ili kujiokoa. Ni wewe tu unayeweza kutusaidia!”
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 166]
Maelezo Mafupi Kuhusu Rwanda
Nchi
Rwanda ina ukubwa wa kilomita 177 tu kutoka kaskazini hadi kusini na kilomita 233 kutoka mashariki hadi magharibi. Nchi hii inakadiriwa kuwa na watu 11,000,000. Hata hivyo, hiyo ni idadi kubwa sana kwa nchi ndogo hivyo. Mji mkuu ni Kigali.
Watu
Wakaaji ni Wahutu, Watutsi, Watwa, Wahindi na Wazungu. Zaidi ya nusu ya idadi ya watu nchini Rwanda ni Wakatoliki zaidi ya robo moja ni Waprotestanti, kutia ndani Waadventisti wengi. Hao wengine ni Waislamu na watu wa imani nyinginezo.
Lugha
Lugha rasmi ni Kinyarwanda, Kiingereza, na Kifaransa. Wanatumia lugha ya Kiswahili katika mawasiliano wanapofanya biashara na watu wa nchi jirani.
Kazi
Wanyarwanda wengi ni wakulima. Kwa sababu mashamba mengi hayana rutuba, wengi hukuza chakula cha kutosha familia zao tu. Mimea inayokuzwa ni pareto—mmea unaotumiwa kutengeneza dawa za kuua wadudu—chai, na vilevile kahawa, ambayo huuzwa nje ya nchi kwa wingi.
Chakula
Vyakula vya msingi vinatia ndani viazi, ndizi, na maharagwe.
Hali ya hewa
Kuna hali nzuri ya hewa licha ya kwamba Rwanda iko karibu na ikweta. Hali ya joto katika maeneo ya nyanda za juu yaliyo ndani zaidi ni wastani wa nyuzi 21 Selsiasi, na inapata mvua ya kadiri kila mwaka.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 185]
“Yehova Atatukimbiza!”
EMMANUEL NGIRENTE
ALIZALIWA 1955
ALIBATIZWA 1982
MAELEZO MAFUPI KUMHUSU Mshiriki wa Halmashauri ya Tawi ya Rwanda na mwangalizi wa Idara ya Tafsiri.
◼ MWAKA wa 1989, nilikuwa painia mashariki mwa Rwanda. Kisha, mwishoni mwa mwaka huo, nikapewa mgawo katika ofisi ya kutafsiri. Nilishtuka na kuhisi sistahili, kwa sababu sikuwa na uzoefu wowote katika kazi ya kutafsiri. Hata hivyo, nilianza kutafsiri machapisho matatu. Tulikodi nyumba na tukatafuta kamusi kadhaa. Nyakati nyingine nilitafsiri usiku kucha, huku nikinywa kahawa ili nibaki macho.
Jeshi la wavamizi liliposhambulia mnamo Oktoba 1990, watu fulani walidhani Mashahidi wa Yehova wana ushirikiano na majeshi hayo. Walinda usalama walianza kufanya uchunguzi. Kwa sababu nilitafsiri nikiwa nyumbani, nilionekana kama mtu asiyeajiriwa, kwa hiyo walitaka kujua ni kazi gani niliyokuwa nikifanya. Siku moja ambayo sikutarajia, walifanya msako. Nilikuwa nimepiga chapa usiku kucha na ilipofika saa kumi na moja asubuhi, nikaamua kulala. Ghafula, nikaamshwa ili niende kufanya kazi ya jumuiya.
Nikiwa huko, wenye mamlaka waliipekua-pekua nyumba yangu. Niliporudi, jirani zangu walinieleza kuwa askari na diwani fulani walikuwa hapo kwa saa moja wakisoma machapisho niliyotafsiri, ambayo yalitumia jina Yehova tena na tena. Mwishowe, walisema: “Acheni tuondoke hapa. La sivyo, Yehova atatukimbiza!”
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 194]
Katika Muda wa Siku 100, Watu Milioni Moja Walikufa
“Mauaji ya 1994 nchini Rwanda ni mfano ulio wazi wa mauaji ya jamii nzima-nzima katika historia ya sasa. Kuanzia mapema mwezi wa Aprili 1994 hadi katikati ya mwezi wa Julai 1994, Wahutu nchini Rwanda waliamua kuliangamiza kabisa kabila la Watutsi lenye watu wachache. Utawala mkali wa Wahutu, ukihofia kupoteza mamlaka yao walipokabili maandamano ya kidemokrasia na vita vya wenyewe kwa wenyewe, ulipanga kuwaua watu wote waliowaona kuwa tisho kwa mamlaka yao, yaani, Wahutu wenye usawaziko na vilevile Watutsi. Mauaji hayo yalifikia mwisho wakati waasi Watutsi walipoimiliki nchi na wenye mamlaka wa serikali iliyoendeleza mauaji wakakimbilia nchi nyingine. Kwa kipindi cha siku mia moja tu, watu wapatao milioni moja, walikufa katika mauaji hayo na pia vitani. Hiyo ndiyo idadi kubwa zaidi ya watu waliouawa kwa muda mfupi sana katika historia iliyorekodiwa.”—Encyclopedia of Genocide and Crimes Against Humanity.
Mashahidi wa Yehova 400 hivi waliuawa, kutia ndani Wahutu ambao waliuawa kwa sababu ya kuwalinda ndugu na dada zao Watutsi. Hakuna Shahidi aliyeuawa na mwamini mwenzake.
[Picha]
Wakimbizi waondoka Rwanda
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 197]
“Vyumba vya Kifo”
“Waliopanga mauaji ya jamii nzima-nzima waliwadanganya makumi ya maelfu ya Watutsi kwamba wakikimbilia makanisani, watapata ulinzi; kisha wanamgambo na majeshi ya Wahutu wakawaangamiza wote waliotafuta kimbilio kwa kuwafyatulia risasi na kurusha maguruneti ndani ya makanisa, na majengo ya shule. Halafu wakaja na mapanga, miundu na visu na kuwaua wale walionusurika. . . . Hata hivyo, kando na kuacha majengo yao yatumiwe kama vyumba vya kifo, makanisa yalihusika zaidi katika mauaji. Katika jamii nyingine, viongozi wa kidini, walimu wa dini, na wafanyakazi wengine wa kanisa walifahamu wenyeji vizuri na hivyo wakasaidia kuwatambulisha Watutsi ili wauawe. Katika visa vingine, wafanyakazi wa kanisa walihusika moja kwa moja katika mauaji.”—Christianity and Genocide in Rwanda.
“Shutuma kuu dhidi ya Kanisa [Katoliki] ni kwamba liliacha kuwapendelea Watutsi wenye ufanisi na likaunga mkono mapinduzi ya Wahutu yaliyomwezesha Habyarimana apate mamlaka katika nchi hiyo yenye Wahutu wengi. Kuhusiana na mauaji ya jamii nzima-nzima, wachambuzi wanadai pia kwamba Kanisa lilihusika moja kwa moja kwa sababu lilichochea chuki, likawaficha wauaji, na likakosa kuwalinda watu waliotafuta ulinzi makanisani. Pia, kuna watu ambao wanaamini kwamba, kwa kuwa Kanisa hutoa mwongozo wa kiroho kwa walio wengi nchini Rwanda, linapaswa kulaumiwa kwa kutochukua hatua zote zilizopo ili kukomesha mauaji.”—Encyclopedia of Genocide and Crimes Against Humanity.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 201-203]
“Kwa Nini Tumuue Mtu Anayetetewa na Kila Mtu?”
JEAN-MARIE MUTEZINTARE
ALIZALIWA 1959
ALIBATIZWA 1985
MAELEZO MAFUPI KUMHUSU Ndugu mwaminifu mwenye tabasamu changamfu anayefanya kazi ya ujenzi, na ambaye alifungwa gerezani kwa miezi nane mnamo 1986, muda mfupi baada ya kubatizwa. Alimwoa Jeanne mwaka wa 1993, na sasa ni mwenyekiti wa Halmashauri ya Jumba la Kusanyiko la Kigali.
◼ MNAMO Aprili 7, mimi na mke wangu Jeanne, pamoja na Jemima, binti yetu mwenye umri wa mwezi mmoja, tuliamshwa kwa ghafula na mlio wa bunduki. Mwanzoni, tulifikiri ni tatizo la kisiasa tu, lakini punde baadaye, tukapata habari kuwa wapiganaji wa Interahamwe walikuwa wameanza kuua Watutsi. Kwa sababu sisi ni Watutsi, hatukuthubutu kutoka nje. Tulimsihi Yehova atusaidie tujue la kufanya. Wakati huohuo, ndugu watatu wajasiri ambao ni Wahutu—Athanase, Charles, na Emmanuel—walihatarisha uhai wao ili kutuletea chakula.
Kwa mwezi mmoja hivi, mimi na mke wangu tulilazimika kujificha katika nyumba tofauti-tofauti za akina ndugu. Mauaji ya Watutsi yalipopamba moto, wapiganaji hao walikuja na visu, mikuki, na mapanga hadi mahali nilipokuwa nimejificha. Niliwaona wakija, nikakimbia haraka iwezekanavyo kujificha kichakani, lakini wakanipata. Nikiwa nimezingirwa na wanaume wenye silaha, niliwasihi wasiniue na kuwaambia kwamba mimi ni Shahidi wa Yehova, lakini wakasema, “Wewe ni mwasi!” Wakanipiga teke nikaanguka, kisha wakanipiga kwa rungu na sehemu ya nyuma ya bunduki. Kufikia wakati huo umati ulikuwa tayari umekusanyika. Katika umati huo, kulikuwa na mtu ambaye nilikuwa nimemhubiria. Alipaaza sauti kwa ujasiri, “Mhurumieni!” Kisha, Charles, mmoja wa ndugu Wahutu akawasili. Waliponiona chini, huku nikitokwa na damu, mke wa Charles na watoto wake wakaanza kulia. Wakiwa na wasiwasi, wauaji hao wakaniacha, huku wakisema, “Kwa nini tumuue mtu anayetetewa na kila mtu?” Charles alinirudisha nyumbani kwake ili anitunze. Wanajeshi hao walituonya kwamba iwapo ningetoroka, wangemuua Charles badala yangu.
Yote hayo yakiendelea, nilikuwa nimetenganishwa na Jeanne na mtoto wetu. Katika shambulizi lenye kutisha, yeye pia alikuwa amepigwa na kuponea chupuchupu. Baadaye, alipokea habari kuwa nimeuawa. Hata aliambiwa atafute shuka za kuufunga mwili wangu.
Tulitokwa na machozi ya furaha tulipoungana tena katika nyumba ya Athanase. Hata hivyo, hatukutazamia kuwa hai siku iliyofuata. Ilikuwa siku nyingine yenye kutia hofu, inayotisha, huku tukijificha katika sehemu mbalimbali. Nakumbuka nikimsihi Yehova: “Jana ulitusaidia. Tafadhali tusaidie tena. Tungependa kumlea mtoto wetu na kuendelea kukutumikia!” Ilipokaribia jioni, ndugu watatu Wahutu walihatarisha uhai wao ili kutusaidia tukiwa Watutsi 30 hivi, kupita vizuizi hatari vya barabarani hadi mahali salama. Sita kati ya Watutsi hao, waliikubali kweli.
Baadaye tulipata habari kwamba Charles na watu aliokuwa nao waliendelea kuwasaidia wengine lakini wapiganaji wa Interahamwe walikasirika sana walipogundua kuwa akina ndugu waliwasaidia Watutsi kutoroka. Hatimaye, walimkamata Charles na mhubiri Mhutu aliyeitwa Leonard. Mke wa Charles aliwasikia wakisema, “Lazima mfe kwa sababu mmewasaidia Watutsi kutoroka.” Kisha wakawaua. Jambo hilo linatukumbusha maneno ya Yesu: “Hakuna aliye na upendo mkuu kuliko huu, kwamba mtu aitoe nafsi yake kwa ajili ya rafiki zake.”—Yoh. 15:13.
Kabla ya vita, wakati mimi na Jeanne tulipokuwa tunapanga kufunga ndoa, tuliamua kwamba mmoja wetu angekuwa painia. Lakini, baada ya vita, kwa sababu wengi wa watu wetu wa ukoo walikuwa wameuawa, tulilea mayatima sita, ingawa tulikuwa na watoto wetu wawili. Licha ya hayo, Jeanne alianza utumishi wa painia baada ya vita na ameufanya kwa miaka 12. Pia, mayatima hao sita—ambao wazazi wao hawakuwa Mashahidi wa Yehova—sasa wamebatizwa wote. Wavulana watatu ni watumishi wa huduma, na mmoja kati ya wasichana anatumika Betheli pamoja na mume wake. Kwa sasa tuna watoto wanne, na wasichana wawili wa kwanza wamebatizwa.
[Picha]
Ndugu na Dada Mutezintare na watoto wao wawili pamoja na mayatima watano
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 204, 205]
“Kweli Ilitusaidia Kudumisha Usawaziko”
Valerie Musabyimana na Angeline Musabwe ni dada wa kimwili. Walilewa katika familia inayofuata sana mafundisho ya Kanisa Katoliki, na baba yao alikuwa mwenyekiti wa halmashauri moja ya parokia. Kwa miaka minne, Valerie alisomea kuwa mtawa wa kike. Hata hivyo, kwa sababu ya kutamaushwa na mwenendo wa kasisi fulani, aliacha masomo hayo mwaka wa 1974. Baadaye, alijifunza Biblia pamoja na Mashahidi wa Yehova, akabatizwa, na akaanza upainia mnamo 1979. Dada yake mdogo, Angeline, pia alijifunza Biblia na akabatizwa. Dada hao wawili sasa ni mapainia wa pekee na wamewasaidia wengi kujifunza kweli.
Angeline na Valerie waliishi Kigali wakati wa mauaji ya jamii nzima-nzima na walificha watu tisa katika nyumba yao, kutia ndani wanawake wawili wajawazito, ambao mume wa mmoja wao alikuwa ameuawa. Baada ya muda fulani, mwanamke huyo alijifungua. Kwa sababu ilikuwa hatari sana kuondoka nyumbani, dada hao walimsaidia kujifungua. Majirani walipojua jambo hilo, wakawaletea chakula na maji.
Wapiganaji wa Interahamwe walipojua kuwa Angeline na Valerie walikuwa wanaficha Watutsi, walisema: “Tumekuja kumuua huyo Shahidi wa Yehova Mtutsi.” Hata hivyo, kwa sababu nyumba waliyokuwa wamekodi ilikuwa ya mwanajeshi, wauaji hao waliogopa kuingia.d Hakuna mtu ndani ya nyumba hiyo aliyeuawa.
Mwishowe, vita vilipozidi na risasi zikaendelea kufyatuliwa mfululizo, iliwabidi Angeline na Valerie waondoke eneo hilo. Wakiwa pamoja na Mashahidi wengine wakakimbilia Goma, ambapo walikaribishwa kwa uchangamfu na ndugu Wakongomani. Waliendelea kuhubiri na kuongoza mafunzo mengi ya Biblia.
Walikabilije hisia hizo zenye kuhuzunisha baada ya mauaji hayo? Valerie alisema hivi kwa huzuni: “Watu wengi niliosaidia kujifunza kweli waliuawa, kutia ndani Eugène Ntabana na familia yake. Kweli ilitusaidia kudumisha usawaziko. Tunajua kwamba Yehova atawahukumu watenda-maovu.”
[Maelezo ya Chini]
d Baada ya vita, mwenye nyumba hiyo alianza kujifunza Biblia. Ingawa alikufa, mke na watoto wake walijifunza wakawa Mashahidi.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 206, 207]
Walikuwa Tayari Kufa kwa Ajili Yetu
ALFRED SEMALI
ALIZALIWA 1964
ALIBATIZWA 1981
MAELEZO MAFUPI KUMHUSU Aliishi katika vitongoji vya Kigali pamoja na mke wake, Georgette. Alfred, ni baba na mume mwenye upendo, na sasa ni mshiriki wa Halmashauri ya Uhusiano na Hospitali mjini Kigali.
◼ MAUAJI ya jamii nzima-nzima yalipoanza, Athanase, ndugu Mhutu aliyeishi karibu nasi, alitutahadharisha, “Wanawaua Watutsi wote na watawaua ninyi pia.” Alisisitiza twende kwake. Kabla ya vita, alikuwa amechimba shimo la mita 3.5 hivi na akaamua kutuficha humo. Nilikuwa wa kwanza kuingia humo kwa kutumia ngazi aliyotengeneza. Athanase alifanya mpango ili tupate chakula na magodoro. Wakati huohuo, mauaji yaliendelea kotekote.
Ingawa majirani walishuku kwamba tulikuwa tunajificha huko na wakatishia kuteketeza nyumba yake, Athanase na familia yake waliendelea kutuficha. Ni wazi kwamba walikuwa tayari kufa kwa ajili yetu.
Vita vilipochacha, familia ya Athanase ikajiunga nasi ndani ya shimo, hivyo idadi yetu ikafikia watu 16. Tulikuwa katika giza tititi kwa sababu hatukuthubutu kutumia mwangaza wowote. Kila siku, sote tulipata kipimo cha kijiko kimoja cha mchele ulioloweshwa ndani ya maji yenye sukari. Baada ya siku kumi, hata chakula hicho kiliisha. Kufikia siku ya 13, tulikuwa na njaa kali! Tungefanya nini? Tukiwa juu ya ngazi, tulitazama nje na kutambua kwamba kuna mabadiliko hata ingawa hatukuona vizuri. Tuliona wanajeshi wakiwa wamevalia sare tofauti. Kwa kuwa familia ya Athanase walinipa ulinzi, niliona ni zamu yangu kujidhabihu. Niliamua kutoka pamoja na kijana wa Athanase ili kutafuta chakula. Kwanza sote tulisali.
Baada ya dakika 30 hivi, tulipata habari kuwa chama cha Rwandan Patriotic Front kilikuwa kinadhibiti eneo hilo. Wanajeshi fulani walitufuata. Niliwaonyesha mahali tulipokuwa tukijificha. Hawakuamini hadi pale ndugu na dada walipoanza kutoka shimoni, mmoja baada ya mwingine. Georgette anasema hatasahau kamwe tukio hilo: “Tulitoka tukiwa wachafu; kwa majuma matatu hivi tulikaa shimoni bila kuoga au hata kufua nguo.”
Wanajeshi hao walishangaa kwamba watu wa makabila yote mawili walikaa pamoja katika shimo hilo. “Sisi ni Mashahidi wa Yehova na hatuna ubaguzi wowote,” nikawaeleza. Walishangaa na kusema, “Wape chakula na sukari watu hawa waliotoka shimoni!” Halafu wakatupeleka katika nyumba fulani ambapo watu 100 hivi walikuwa wamepewa makao kwa muda. Baada ya hapo, dada fulani alisisitiza kwamba sote 16 tuishi na familia yake.
Tunashukuru kwamba tuko hai. Hata hivyo, ndugu na dada yangu na familia zao—ambao wote ni Mashahidi wa Yehova—waliuawa, kama vile wengine wengi. Tunasikitika walikufa, lakini pia tunajua kwamba ‘wakati na tukio lisilotazamiwa hutupata sote.’ Georgette anaeleza tunavyohisi: “Ndugu na dada wengi waliuawa, na wengine walipitia hali ngumu na zenye kutisha wakikimbia na kujificha. Hata hivyo, tuliimarisha uhusiano wetu pamoja na Yehova kupitia sala, na tukaona kuwa mkono wake ni wenye nguvu. Tulipata faraja kupitia msaada aliotuandalia kwa wakati unaofaa kupitia tengenezo lake, hivyo tunamshukuru sana. Yehova alitubariki kwelikweli.”—Mhu. 9:11.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 208, 209]
Yehova Alitusaidia Katika Nyakati Hizo Zenye Kutisha
ALBERT BAHATI
ALIZALIWA 1958
ALIBATIZWA 1980
MAELEZO MAFUPI KUMHUSU Mzee wa kutaniko, ameoa, na ana watoto watatu. Mke wake na binti yake mkubwa ni mapainia wa kawaida. Kijana wake ni mtumishi wa huduma. Albert, ndugu mnyamavu ambaye ni Mhutu, alipoanza kuhudhuria mikutano mwaka wa 1977, kulikuwa na wahubiri wapatao 70 tu nchini Rwanda. Mwaka wa 1988 alifungwa gerezani na kupigwa. Alipokataa kuvaa beji ya chama cha kisiasa, jirani ambaye awali alikuwa mwanajeshi alimdunga na kuingiza pini ya beji ndani ya ngozi yake na kusema kwa dharau: “Sasa umevaa beji!”
◼ BAADA ya kifo cha rais, ndugu kadhaa, watu wa ukoo, na majirani, walikimbilia kwangu. Hata hivyo, nilikuwa na wasiwasi kuhusu Goretti na Suzanne, dada wawili Watutsi, ambao hawakuwa pamoja nasi. Ijapokuwa ilikuwa hatari sana, nilienda kuwatafuta. Ingawa watu walikuwa wakikimbia, nilimwona Goretti na watoto wake na kuwapeleka nyumbani, kwa sababu nilijua kuna kizuizi katika barabara waliyofuata, na bila shaka wangeuawa.
Baada ya siku chache, Suzanne, akiwa pamoja na wengine watano, walifaulu kujiunga nasi. Tukawa zaidi ya watu 20 nyumbani, na sote tulikuwa katika hatari kubwa.
Katika angalau pindi tatu, wapiganaji wa Interahamwe walikuja nyumbani. Pindi moja walimwona mke wangu, Vestine, kupitia dirishani na wakamwita atoke nje. Yeye ni Mtutsi. Nilisimama kati ya wauaji hao na mke wangu na kuwaambia: “Ikiwa mtamuua, niueni kwanza!” Baada ya mazungumzo mafupi, wakamwambia arudi ndani. Mmoja wao akasema, “Sitaki kuua mwanamke; nataka kuua mwanamume.” Kisha wakamkazia macho ndugu ya mke wangu. Walipomtoa nje, nilijitupa mbele ya kijana huyo na kuwasihi, “Ikiwa mnamwogopa Mungu, tafadhali mwacheni!”
“Sifanyi kazi ya Mungu,” mmoja wao alinijibu kwa hasira, huku akinigonga kwa kiwiko. Hata hivyo, alipunguza hasira, na kuniambia: “Endeni basi! Mchukue!” Kwa hiyo, shemeji yangu akanusurika.
Baada ya mwezi mmoja hivi, ndugu wawili walikuja kutafuta chakula. Kwa sababu nilikuwa na maharagwe, niliwapa kidogo, lakini nilipokuwa nikiwasindikiza ili kuwaonyesha njia iliyo salama waliyopaswa kufuata, nikasikia mlio wa bunduki na kupoteza fahamu. Ganda la risasi lilinigonga jicho. Jirani alinipeleka hospitalini, lakini kwa sababu ya majeraha niliyopata, jicho hilo lilipoteza uwezo wa kuona. Isitoshe, sikuweza kurudi nyumbani. Wakati huohuo, vita vilipozidi, ikawa hatari sana kwa yeyote aliyekuwa kwangu kuendelea kukaa humo, kwa hiyo wakakimbilia nyumba za ndugu wengine ambao walihatarisha uhai wao ili kuwalinda hadi Juni 1994. Sikuweza kuungana tena na mke wangu na familia yangu hadi mwezi wa Oktoba. Namshukuru Yehova kwa kunisaidia mimi na familia yangu kuvumilia nyakati hizo zenye kutisha.
[Picha]
Albert Bahati pamoja na familia yake na wengine aliowaficha
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 210-212]
“Njia Ndiyo Hii”
GASPARD NIYONGIRA
ALIZALIWA 1954
ALIBATIZWA 1978
MAELEZO MAFUPI KUMHUSU Mteteaji wa kweli asiye na woga, anayependa kutabasamu, na mwenye mtazamo mzuri. Gaspard ameoa, ana mabinti watatu, na sasa ni mshiriki wa Halmashauri ya Tawi ya Rwanda.
◼ BAADA ya milio ya risasi kuanza kusikiwa asubuhi na mapema mnamo Aprili 7, niliona nyumba 15 hivi za Watutsi, kutia ndani nyumba mbili za ndugu zetu, zikiteketea. Je, nyumba yetu pia ingeteketezwa? Karibu nirukwe na akili kwa kuhofia kile kingempata mke wangu, ambaye ni Mtutsi, na watoto wetu wawili.
Sikujua jambo la kufanya. Kulikuwa na mvurugo na hali ya wasiwasi, vilevile kulikuwa na uvumi na ripoti za uwongo. Niliona kwamba mke na watoto wangu wangekuwa salama wakienda kwa ndugu mmoja aliyeishi karibu, kisha baadaye nijiunge nao. Ilipokuwa salama kwangu kwenda huko, niligundua kwamba mke wangu alilazimika kukimbilia jengo kubwa la shule. Alasiri hiyo, jirani alikuja na kuniambia, “Watutsi wote wanaojificha katika shule hiyo watauawa!” Mara moja nilikimbia hadi shuleni, nikampata mke wangu na watoto wangu, na nikawakusanya karibu watu 20—kutia ndani akina ndugu na dada—na kuwaambia waende makwao. Tulipokuwa tukiondoka, tuliona wanajeshi wakiwaelekeza watu kutoka mjini hadi mahali ambapo waliwaua zaidi ya Watutsi 2,000.
Wakati huohuo, mke wa jirani fulani alijifungua akiwa katika shule hiyo. Wapiganaji wa Interahamwe waliporusha gruneti ndani ya shule hiyo, mume wake alikimbia na mtoto huyo aliyezaliwa. Katika vurugu hiyo, mwanamke huyo alikimbilia upande mwingine. Ingawa mwanamume huyo alikuwa Mtutsi, alifaulu kupita vizuizi vya barabarani kwa sababu ya mtoto aliyekuwa mikononi mwake, na akakimbia hadi nyumbani mwetu. Aliniomba nijaribu kumtafutia mtoto wake maziwa. Nilipoenda kumtafutia maziwa, bila kukusudia nilijipata kwenye kizuizi cha barabara kilichosimamiwa na wanajeshi. Wakifikiri kwamba naunga mkono Watutsi kwa sababu nilikuwa nikitafuta maziwa kwa ajili ya mtoto Mtutsi, wakasema, “Tumuue!” Mmoja wao alinigonga kwa kutumia upande wa nyuma wa bunduki, na nikapoteza fahamu, huku nikitokwa na damu usoni na puani. Wakifikiri kwamba nimekufa, wakanikokota hadi nyuma ya nyumba iliyokuwa karibu.
Jirani fulani alinitambua na kuniambia, “Lazima uondoke, au watarudi kukumaliza.” Alinisaidia kurudi nyumbani.
Ingawa niliumia, kisa hiki kilikuwa ulinzi kwangu. Kwa sababu watu walijua kuwa mimi ni dereva, watu watano walikuja kesho yake kunishurutisha niwe dereva wa mkuu wa jeshi. Walipoona majeraha yangu, hawakusisitiza, wala kunilazimisha nishike doria pamoja na wapiganaji wa Interahamwe.
Kisha siku za hofu, wasiwasi, na njaa zikafuata. Wakati huo, mwanamke fulani Mtutsi akakimbilia kwangu akiwa na watoto wake wawili wadogo. Tulimficha katika kabati iliyokuwa jikoni kisha tukaweka watoto wake pamoja na wangu katika chumba kingine. Jeshi la Rwandan Patriotic Front (RPF), lililokuwa likipinga serikali, lilipokaribia zaidi na habari zikaenea kuwa wapiganaji wa Interahamwe walianza kuua Wahutu waliokuwa na wake Watutsi, familia yetu nzima ikawa tayari kukimbia tena. Lakini eneo letu tayari lilikuwa chini ya RPF, kwa hiyo Watutsi hawakuwa hatarini. Hata hivyo, sasa mimi ndiye niliyekabili hatari ya kuuawa.
Kisha nikaandamana na kundi la majirani wetu hadi kwenye kizuizi cha barabarani kilichosimamiwa na wanajeshi wa RPF. Waliponiona mimi, Mhutu, nikiwa na bendeji kichwani, walifikiri kuwa mimi ni mmoja wa wapiganaji wa Interahamwe. Walipaza sauti na kusema: “Kati yenu kuna wauaji na waporaji, na bado mnaomba msaada! Nani kati yenu alificha au kuwalinda Watutsi?” Nikawaonyesha mwanamke na watoto ambao nilikuwa nimewaficha. Waliwachukua watoto na kuwaweka upande mmoja, kisha wakawauliza, “Mtu huyu mwenye bendeji kichwani ni nani?” Wakajibu, “Yeye si mmoja wa Interahamwe; yeye ni Shahidi wa Yehova na ni mtu mzuri.” Nilikuwa nimemwokoa mwanamke Mtutsi na watoto wake wawili, na sasa walikuwa wananiokoa.
Wakiwa wameridhika na majibu hayo, wanajeshi hao walitupeleka katika kambi moja iliyokuwa kilomita 20 kutoka Kigali, ambapo watu 16,000 walionusurika walikuwa wamekusanyika. Huko tulikutana na ndugu na dada 60 kutoka makutaniko 14 tofauti-tofauti. Tulipanga mikutano; watu 96 walihudhuria mkutano wa kwanza! Hata hivyo, kilikuwa kipindi kigumu, kwa sababu tulipata ripoti kuhusu marafiki ambao waliuawa na akina dada waliobakwa. Ni mimi tu niliyekuwa mzee wa kutaniko, na ndugu na dada wengi walihitaji kitulizo na msaada wa Maandiko. Nilisikiliza mambo yenye kuhuzunisha yaliyowakumba na nikawatia moyo kuwa Yehova anawapenda na anaelewa uchungu walio nao.
Mwishowe, mnamo tarehe 10 mwezi wa Julai, baada ya majuma mengi yenye kutia hofu, tulirudi nyumbani. Nakumbuka kwamba katika nyakati hizo za hofu na hatari, mara nyingi nilifikiria kuhusu wimbo wenye kichwa “Njia Ndiyo Hii.” Maneno ya wimbo huo yalinitia moyo sana: “La hatugeuki tumeishika, kwa njia ya Mungu twasonga mbele.”
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 223, 224]
Mtu Fulani Aliniita
HENK VAN BUSSEL
ALIZALIWA 1957
ALIBATIZWA 1976
MAELEZO MAFUPI KUMHUSU Alitumika katika Betheli ya Uholanzi kabla ya kuhudhuria Shule ya Gileadi mwaka wa 1984. Alipata mgawo wa kwenda Jamhuri ya Afrika ya Kati, kisha Chad, na baadaye Rwanda mnamo Septemba 1992. Sasa, yeye na mke wake Berthe, wanatumika katika ofisi ya tawi ya Rwanda.
◼ KUTANIKO la Kigali Sud ndilo la kwanza nililoshirikiana nalo nchini Rwanda. Kutaniko hilo lilikuwa na watoto wengi. Ndugu na dada walikuwa wachangamfu na wakarimu. Mwaka wa 1992, kulikuwa na makutaniko machache tu nchini na kulikuwa na wahubiri 1,500 hivi. Wenye mamlaka walitushuku, kwa hiyo mara kwa mara, askari walikatiza kazi yetu ya kuhubiri ili kuangalia vitambulisho vyetu.
Mauaji ya jamii nzima-nzima yalipoanza, nililazimika kuondoka Rwanda. Lakini punde tu baada ya hapo, niliombwa niwasaidie wakimbizi waliokuwa mashariki mwa Kongo. Nilisafiri kutoka Nairobi hadi Goma, mji ulio karibu na mpaka wa Rwanda. Sikuwa na habari zozote ila jina la mzee mmoja tu, na kwa sababu ilikuwa mara yangu ya kwanza kufika huko, sikujua ningempata jinsi gani. Hata hivyo, nilipofika, nilimuuliza dereva wa teksi iliyonibeba ikiwa anamfahamu. Alizungumza na madereva wengine na hata kabla ya dakika thelathini kuisha, nilikuwa nimesimama mlangoni mwa mzee huyo. Ndugu wawili wa Halmashauri ya Nchi ya Rwanda walifaulu kuvuka mpaka na kuingia Goma, na nikawapa pesa nilizopokea kutoka kwa ofisi ya tawi ya Kenya ili wawasaidie ndugu nchini Rwanda.
Mara ya pili nilipoenda Goma kutoka Nairobi, nakumbuka nikitembea hadi kwenye mpaka wa Rwanda. Ingawa haikuwa mbali, nilitumia muda mrefu kwa sababu ya wakimbizi wengi niliopishana nao wakitoka Rwanda.
Bila kutarajia, mtu fulani aliniita: “Ndugu Henk! Ndugu Henk!” Nilipotazama upande ambao sauti hiyo ilitoka, nilimwona Alphonsine, msichana mwenye umri wa miaka 14 hivi, kutoka kutaniko nililokuwa nikishirikiana nalo mjini Kigali. Alphonsine alikuwa ametenganishwa na mama yake. Tulikaa pamoja katika umati huo mkubwa, na kisha nikampeleka kwenye Jumba la Ufalme ambapo ndugu na dada wengi wakimbizi walikusanyika. Familia moja kutoka Kongo walimtunza, na baada ya hapo dada mmoja mkimbizi kutoka kutaniko la kwao alimwandalia mahitaji yake. Mwishowe, Alphonsine aliungana na mama yake mjini Kigali.
[Picha]
Henk na mke wake Berthe
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 235, 236]
Yehova Amefanya Mambo Makuu ya Ajabu!
GÜNTER RESCHKE
ALIZALIWA 1937
ALIBATIZWA 1953
MAELEZO MAFUPI KUMHUSU Alianza upainia 1958 na akahudhuria darasa la 43 la Shule ya Gileadi. Tangu 1967, ametumika nchini Gabon, Jamhuri ya Afrika ya Kati, na Kenya na ametembelea nchi nyingine kadhaa akiwa mwangalizi anayesafiri. Kwa sasa, ni mshiriki wa Halmashauri ya Tawi ya Rwanda.
◼ NILIENDA Rwanda kwa mara ya kwanza mwaka wa 1980 baada ya kuombwa na ofisi ya Kenya kwenda huko kufanya kazi ya wilaya. Wakati huo, kulikuwa na makutaniko saba tu na wahubiri 127 nchini Rwanda. Pia nilikuwa mmoja wa walimu wawili katika darasa la kwanza la Shule ya Utumishi wa Painia kufanywa nchini. Wengi wa mapainia 22 katika darasa hilo bado wangali katika utumishi wa wakati wote. Nilirudi Kenya nikiwa na kumbukumbu nzuri ya bidii ya akina ndugu katika huduma na jinsi walivyoithamini kweli.
Mwaka wa 1996, nilipokea barua kutoka ofisi ya tawi ya Kenya, iliyoniomba nihamie Rwanda. Nilikuwa nimeishi Kenya kwa miaka 18, na niliipenda nchi hiyo. Nilipofika Rwanda, bado kulikuwa na msukosuko. Mara kwa mara tulisikia milio ya risasi usiku. Lakini, muda mfupi baadaye nilianza kufurahia mgawo wangu, hasa nilipoona baraka za Yehova katika kazi yake.
Maeneo ya kusanyiko yalikuwa ya hali ya chini. Hata hivyo, mara nyingi ndugu waliketi kwenye sakafu au juu ya mawe bila kulalamika. Vidimbwi vya ubatizo vilikuwa mashimo makubwa yaliyochimbwa ardhini, na kutandazwa chandarua cha plastiki. Makusanyiko kama hayo bado yanafanywa katika sehemu nyingi za vijijini, lakini kadiri ambavyo muda umepita, majumba yasiyo na kuta yamejengwa kutia ndani Majumba machache ya Ufalme yanayoweza kupanuliwa.
Ndugu walikuwa wenye bidii katika kutangaza habari njema. Mikutano mjini Kigali ilianza mapema sana mwishoni mwa juma. Baadaye, wahubiri walishiriki utumishi hadi usiku.
Nyakati zote nilitenga wakati ili kuwa pamoja na wachanga makutanikoni, ambao baadaye wangechukua madaraka zaidi. Inapendeza kama nini kuona wengi wakisimama imara, hivyo wakithibitisha kwamba licha ya umri wao mdogo, walikuwa na uhusiano wa karibu pamoja na Yehova!
Kwa mfano, katika eneo la kusini, Luc mwenye umri wa miaka 11, alipokuwa darasani aliambiwa aimbe wimbo wa taifa. Kwa heshima, aliomba aruhusiwe kuimba moja ya nyimbo zetu za Ufalme badala ya wimbo wa taifa. Mwalimu alimruhusu, na wote wakapiga makofi alipomaliza kuimba. Kwa kuwa alijua mfuatano wa sauti ya wimbo huo, na hata maneno yake, ni wazi kuwa Luc alifurahia kumsifu Muumba wake. Jambo hilo na mengine mengi yalinitia moyo. Nilikutana pia na dada mmoja ambaye alikuwa amefungwa gerezani miaka kadhaa mapema kwa sababu ya kuhubiri habari njema. Alipokuwa gerezani alijifungua mwana na kumwita “Shikama Hodari” (linalomaanisha “kubaki imara”). Shikama ameishi kupatana na jina lake. Hivi majuzi alihudhuria Shule ya Biblia ya Ndugu Waseja na anatumika akiwa mtumishi wa huduma na painia wa pekee.
Kwa miaka mingi ambayo ndugu zetu nchini Rwanda walikabili hali ngumu sana—kutia ndani kupigwa marufuku, vita vya wenyewe kwa wenyewe, na mauaji ya jamii nzima-nzima—nimeguswa moyo nyakati zote na bidii yao katika utumishi na uaminifu wao, na ni pendeleo kubwa kutumikia pamoja nao. Pia, sikuzote niliona baraka za Yehova, ulinzi wake na utegemezo wake, na hivyo nimemkaribia zaidi. Kwa kweli, Yehova amefanya mambo makuu, ya ajabu!—Zab. 136:4.
[Chati/Picha katika ukurasa wa 254, 255]
MFUATANO WA MATUKIO—Rwanda
1970
1970 Ripoti ya kwanza ya wahubiri.
1975 Familia ya kwanza ya Wanyarwanda yarudi kutoka Congo.
1976 Kijitabu “Habari Njema Hizi za Ufalme” chachapishwa katika Kinyarwanda.
1978 Gazeti la Mnara wa Mlinzi la kila mwezi lachapishwa katika Kinyarwanda.
1980
1982 Kazi ya kuhubiri yapigwa marufuku; ndugu wenye madaraka wafungwa gerezani.
1986 Asilimia 33 ya wahubiri wote wafungwa gerezani.
1990
1990 Vita vyaanza kaskazini mwa nchi.
1992 Kusanyiko la Wilaya lafanywa kwa mara ya kwanza nchini Rwanda.
Kazi yaandikishwa kisheria.
Wamishonari wafika.
1994 Mauaji ya Watutsi.
1996 Wamishonari warudi.
Idara ya Utumishi yaanzishwa.
1998 Gazeti la Mnara wa Mlinzi katika Kinyarwanda lachapishwa sambamba na toleo la Kiingereza.
1999 Jumba la Kusanyiko lisilo na kuta mjini Kigali lawekwa wakfu.
2000
2000 Ofisi ya tawi yaanzishwa.
Dawati la Ujenzi wa Majumba ya Ufalme laanzishwa
2001 Uwanja kwa ajili ya ujenzi wa ofisi mpya ya tawi wapatikana.
2006 Ofisi mpya ya tawi yawekwa wakfu.
2007 Tafsiri ya Ulimwengu Mpya ya Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo yatolewa katika Kinyarwanda.
2010
2010 Chapa nzima ya Biblia Takatifu—Tafsiri ya Ulimwengu Mpya yatolewa katika Kinyarwanda.
[Grafu/Picha katika ukurasa wa 234]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Jumla ya Wahubiri
Jumla ya Mapainia
20,000
15,000
10,000
5,000
1985 1990 1995 2000 2005 2010
[Ramani katika ukurasa wa 167]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
UGANDA
JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA KONGO
Volkano ya Nyiragongo
Bukavu
Goma
BURUNDI
TANZANIA
RWANDA
KIGALI
MIL. YA VIRUNGA
Volkano ya Karisimbi
Ruhengeri (sasa Musanze)
Gisenyi (sasa Rubavu)
Ziwa Kivu
Kanombe
Masaka
Gitarama (sasa Muhanga)
Bugesera
Nyabisindu (sasa Nyanza)
Save
Butare (sasa Huye)
Ikweta
[Picha katika ukurasa wa 164, 165]
Kuvua samaki katika Ziwa Kivu
[Picha katika ukurasa wa 169]
Oden na Enea Mwaisoba
[Picha katika ukurasa wa 170]
Gaspard Rwakabubu akiwa na binti yake Deborah na mkewe, Melanie
[Picha katika ukurasa wa 171]
Habari Njema Hizi za Ufalme katika Kinyarwanda
[Picha katika ukurasa wa 172]
Justin Rwagatore
[Picha katika ukurasa wa 172]
Ferdinand Mugarura
[Picha katika ukurasa wa 173]
Wale watatu waliobatizwa mwaka wa 1976: Leopold Harerimana, Pierre Twagirayezu, na Emmanuel Bazatsinda
[Picha katika ukurasa wa 174]
Machapisho katika Kinyarwanda
[Picha katika ukurasa wa 179]
Phocas Hakizumwami
[Picha katika ukurasa wa 180]
Palatin Nsanzurwimo pamoja na mke wake (kulia) na watoto
[Picha katika ukurasa wa 181]
Odette Mukandekezi
[Picha katika ukurasa wa 182]
Henry Ssenyonga juu ya pikipiki yake
[Picha katika ukurasa wa 188]
Hati ya usajili, Aprili 13, 1992
[Picha katika ukurasa wa 190]
Ndugu waondoa jukwaa kuwapa nafasi wachezaji wa kandanda
[Picha katika ukurasa wa 192]
Leonard na Nancy Ellis (katikati) wakiwa na familia ya Rwakabubu na ya Sombe
[Picha katika ukurasa wa 193]
Mabaki ya ndege iliyoanguka karibu na mji wa Kigali
[Picha katika ukurasa wa 199]
“Hatukujiendesha kama ndugu,” maandishi kwenye jengo la Kanisa Katoliki huko Kibuye (sasa Karongi)
[Picha katika ukurasa wa 214]
Kuanzia kushoto kuelekea kulia: (nyuma) André Twahirwa, Jean de Dieu, Immaculée, Chantal (na mtoto), Suzanne; (mbele) watoto wa Mugabo: Jean-Luc na Agapé
[Picha katika ukurasa wa 216]
Védaste Bimenyimana akiongoza funzo la Biblia
[Picha katika ukurasa wa 217]
Tharcisse Seminega na mke wake, Chantal
[Picha katika ukurasa wa 218]
Tharcisse na Justin karibu na kibanda ambamo Tharcisse na familia yake walifichwa kwa mwezi mmoja
[Picha katika ukurasa wa 226]
Juu: Kambi ya wakimbizi ya Mashahidi kutoka Rwanda; chini: kambi ya wakimbizi Mashahidi na watu wengine
Goma, Kongo
Benaco, Tanzania
[Picha katika ukurasa wa 229]
Jumba la Ufalme lilitumiwa kama hospitali
[Picha katika ukurasa wa 238]
Oreste pamoja na familia yake, 1996
[Picha katika ukurasa wa 240]
Théobald na Berancille Munyampundu
[Picha katika ukurasa wa 241]
Ndugu na dada Watutsi na Wahutu wakitayarisha uwanja kwa ajili ya ujenzi wa Jumba la Kusanyiko
[Picha katika ukurasa wa 242]
Jumba la Kusanyiko lisilo na kuta, Kigali, 2006
[Picha katika ukurasa wa 243]
Shule ya Mazoezi ya Kihuduma, Kigali, 2008
[Picha katika ukurasa wa 246]
Sehemu ya lugha ya ishara katika kusanyiko la pekee mjini Gisenyi, 2011
[Picha katika ukurasa wa 248]
François-Xavier Hakizimana
[Picha katika ukurasa wa 252, 253]
Ndugu na dada wakifanya kazi pamoja na “Bwana wa mavuno” katika shamba hili lenye rutuba bila nia ya kupunguza bidii yao