Chakula Chako ni Salama Kadiri Gani?
JEAN aliudhika kupata kipande cha nyama aliyokuwa amenunua iwe ya chakula cha jioni ya Jumamosi kikiwa nyuma ya friji. Jamaa ilipokuwa imeenda kula nje usiku huo bila kutarajia, yeye alikuwa amesahau kuweka nyama hiyo katika sehemu yenye kugandisha vitu katika friji. Sasa siku nne zikawa zimepita.
Bila kutaka, alichomoa kifurushi hicho, akakifungua, na kuthibitisha kwamba hofu zake kukihusu zilikuwa za kweli, huku akitoa mpumuo wa kutamauka. Hata hivyo, yeye aliwaza hivi: ‘Labda harufu ile yenye kunuka kidogo itaisha kikipikwa kabisa kabisa.’ Hata hivyo, alipokuwa akipima uzito wa jambo hilo alikumbuka usemi mmoja wenye vina vyenye kupatana: ‘Ukikitilia shaka, kitupe ndani ya taka.’ Kwa kuondolea mbali nyama hiyo, Jean aliepusha jamaa yake na kasoro za afya ambazo zingeweza kutokana na kula chakula kisicho salama.
Lakini tatizo la chakula kisicho salama hutokeza hali zilizo nzito hata zaidi. Ugonjwa wenye kutokana na chakula kilichochafuliwa ni kisababishi kikubwa cha mteseko na kifo katika nchi zenye kusitawi. Mamilioni ya watu huathiriwa hata katika mabara yenye ufanisi. Kwa kielelezo, katika Uingereza visa zaidi ya elfu kumi vya chakula kugeuka kuwa sumu huripotiwa kila mwaka, na yawezekana kwamba vile ambavyo hasa hutukia ni mara mia moja zaidi ya hivyo. Lakini ni nini hufanya chakula kiwe si salama?
Kwa Nini Si Salama?
Huenda chakula kikawa si salama kwa sababu ya kuchafuliwa na bakteria (viini) vyenye madhara. Hiyo yaweza kutukia wakati kiwekeo chenye mboga zilizohifadhiwa kinyumbani kifunikwapo kwa njia isiyofaa, wakati majani-letisi katika saladi mbichimbichi yasipooshwa, wakati nyama iliyopikwa iachwapo kwa muda mrefu mno katika halijoto ya chumba cha kawaida, au wakati wenye kutayarisha chakula wakishughulikiapo kwa uzembe. Pia chakula chaweza kuchafuliwa na masalio ya dawa za kuua wadudu au kwa kugusana kiaksidenti pamoja na vitu vyenye madhara au sumu.
Wingi mkubwa wa chakula kisicho salama hupelekwa nje ya nchi na kuingizwa nchini kila siku. Wakati wa kipindi kimoja tu cha miezi mitatu ya kufanya hivyo, United States ilikataa chakula cha dola milioni 65 kuwa hakifai kuingizwa nchini. Ingawa hivyo, mabara mengi hayamo katika hali rahisi za kuweza kukataa chakula kisicho salama. Mara nyingi chakula hicho huuzwa na kuliwa.
Gazeti World Health laripoti kwamba “magonjwa yenye kuletwa na chakula hupatikana kwa wingi katika sehemu zote za ulimwengu, wala si miongoni mwa jamaa zenye umaskini tu.” Pia gazeti hilo lasema hivi: “Ugonjwa na ukosefu wa hali njema ambao huleta upungufu wa uchumi kwa sababu ya chakula kuchafuliwa hufanyiza moja la matatizo ya kiafya yenye kuenea kwa mapana zaidi katika ulimwengu wa sasa.”
Yakadiriwa kwamba watu wengi labda kufikia milioni 20 katika United States hupatwa kila mwaka na matatizo ya kula chakula kilichochafuliwa. Na katika Ulaya, magonjwa yenye kuletwa na chakula huonwa kuwa ndicho kisababishi cha pili chenye kufuata maambukizo ya umio wa pumzi katika kusababisha kifo. “Nchi zenye maendeleo ya viwandani zina mambo yenye kupendelewa zaidi na desturi zazo zenyewe ambazo huendeleza magonjwa yenye kuletwa na chakula,” asema mwanasayansi mmoja. “Moja la matatizo ya wazi zaidi ni kupendelea zaidi vipande vikubwa vya nyama, ambavyo mara nyingi huwa vimepikwa vikabaki vikiwa vibichi sana.”
Kula Nje
Kwa kawaida hakuna mtu hufikiria kwa uangalifu juu ya kula mlo mkuu katika mkahawa au kwenda kununua chakula cha haraka kwenye duka la upakuzi wa haraka. Mamia kwa maelfu ya milo hupakuliwa kila siku bila athari mbaya kwa wateja wa mikahawani. Hata hivyo, katika nchi zilizositawi, watu wameathiriwa na magonjwa mazito yenye kuletwa na chakula kutokana na kula mikahawani.
Kwa kielelezo, kwenye mkahawa mmoja kaskazini-magharibi mwa Ulaya watu zaidi ya 150 walitiwa sumu na chakula kilichoharibika baada ya mlo mkuu wa Krismasi. Baadaye ilipatwa kwamba mabata waliopikwa walikuwa wamekatwakatwa juu ya mbao zile zile za kukatia nyama ambazo zilitumiwa kutayarisha ndege wabichi wa kuchomwa. Bakteria-salmonella (viini vibaya) zilipatikana baadaye katika nyufa za mbao hizo.
Katika pindi moja ya kusafiri baharini kwa muda wa siku saba, asilimia 20 ya abiria walipatwa na ugonjwa wa kuhara. Sehemu ya jikoni katika meli yenyewe ilipatikana ikiwa na msongamano na uchafu, na nafasi isiyotosha ili kuweka akiba kwa njia salama. Chakula kiliachwa nje juu ya meza za upakuaji kwa vipindi virefu bila kuhifadhiwa katika mashine ya barafu, na masalio yalipakuliwa siku iliyofuata.
Ingawa chakula kisicho salama ni tatizo hata katika nchi zilizositawi, matokeo ni yenye msiba katika mabara yanayositawi.
Sehemu ya Maisha ya Kila Siku
Gazeti World Health laripoti kwamba katika maeneo mengi ya ulimwengu, mweneo mkubwa wa ukosefu wa chakula cha kuufaa mwili hautokani na ukosefu wa chakula tu “bali [hutokana na] kula chakula kilichochafuliwa, kisicho salama.” Hii huleta kuhara-hara na magonjwa mengine yenye kuambukiza.
“Katika 1980,” World Health ikaripoti, “kulikuwako visa milioni 750-1,000 vya mharo mkali katika watoto wa umri wa chini ya miaka mitano katika ulimwengu unaositawi (bila kutia ndani China). Karibu watoto milioni tano walikufa, kwa kadiri ya vifo kumi vya mharo kila dakika ya kila siku ya kila mwaka.” Lakini si watoto peke yao walio hatarini. Ripoti moja ya 1984 kuhusu “Fungu Lenye Kutimizwa na Usalama wa Chakula Katika Afya na Usitawi” iliarifu kwamba “sasa mharo wa wasafiri ni tukio ambalo limeenea kwa mapana, likaathiri karibu asilimia 20 hadi 50 ya wasafiri wote.”
Bila shaka kukosa maarifa kuhusu kanuni za afya zifaazo kufuatwa ndicho kisababishi cha kadiri kubwa ya magonjwa yenye kuletwa na chakula. Huenda chakula kikawa salama pale mwanzoni halafu kije kuchafuliwa na mlaji au mtu fulani wa katikati, kama vile mwenye duka au mpishi.
Vivyo hivyo, huenda imani za kitamaduni zikaongoza kwenye uchafuaji wa chakula. Kwa kielelezo, katika maeneo fulani ya Meksiko watu huamini kwamba mikono “iliyopata moto” kwa kushona nguo, kupiga pasi, kuoka vitu, na kadhalika, haipasi kuoshwa mara iyo hiyo. Yafikiriwa kwamba kuipasha baridi mapema mno kwa kuitilia maji kutasababisha baridi yabisi au mipindano ya misuli. Hivyo, huenda mwanamke mwenye mikono “iliyopata moto” akatumia choo halafu ageukie kutayarisha mlo wa jamaa bila kunawa mikono. Tokeo ni kwamba, bakteria zenye madhara huenezwa.
Kwa upande ule mwingine, tamaduni fulani zina mapokeo ambayo, yakifuatwa, husaidia kuzuia mweneo wa magonjwa yenye kuletwa na chakula. Katika nyumba nyingi katika India, ambako upishi hufanywa sakafuni, viatu vyenye kukanyaga maeneo ya barabarani huvuliwa kabla ya kuingia ndani ya nyumba, hasa jikoni. Pia, matunda humenywa ngozi kabla hayajaliwa. Nyama huliwa katika muda wa saa chache baada ya mnyama kuchinjwa. Na huenda milo ikaliwa ikiwa kwenye majani yaliyotoka kuoshwa sasa hivi badala ya kutiwa katika sahani.
Kulikabili Tatizo
Ni kwa kadiri gani mwanadamu anaukaribia mradi wa kuandalia watu wote chakula salama cha kiasi cha kutosha? Ikieleza juu ya tatizo hilo, ripoti moja ya Umoja wa Mataifa kuhusu usalama wa chakula ilisema hivi: “Katika miaka 40 iliyopita, matengenezo ya kimataifa yametokeza hesabu kubwa ya ripoti zenye kutaja vijambo vyote vya maana na ikaanzisha programu nyingi za kushughulika na suala hili. Na bado magonjwa yenye kuletwa na chakula yaendelea kuongezeka.”
Kitu ambacho chahitajiwa ili kukabiliana na tatizo hili ni kuelimisha watu kwa ujumla na akina mama hasa. Halafu watu mmoja mmoja waweza kuchukua hatua za tahadhari dhidi ya kuchafua chakula na waweza kudumisha tabia salama za kula kwa ajili yao wenyewe na jamaa zao. Makala inayofuata yaandaa madokezo fulani.
[Picha katika ukurasa wa 19]
Chakula chaweza kuwa salama eneo la kukitayarisha liwekwapo safi, kama vile katika nyumba hii katika India