Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g90 4/8 kur. 20-23
  • Fanya Ulaji Wako Uwe Salama

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Fanya Ulaji Wako Uwe Salama
  • Amkeni!—1990
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Nje ya Nyumba Yako
  • Mambo Saba Muhimu ya Kuhakikisha Chakula Ni Salama na Chenye Lishe
    Habari Zaidi
  • Jinsi ya Kuchagua Chakula Kisichodhuru Afya
    Amkeni!—2001
  • Jilinde na Ugonjwa Utokanao na Chakula
    Amkeni!—1995
  • Njia Sita za Kutunza Afya
    Amkeni!—2003
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1990
g90 4/8 kur. 20-23

Fanya Ulaji Wako Uwe Salama

BAKTERIA ambazo husababisha magonjwa yenye kuhusiana na chakula zina matakwa fulani kwa uhai—chakula, maji, hewa, ujotojoto, na wakati. Moja la mambo haya ya maana sana likiondolewa, ukuzi hukomeshwa au kuzuiliwa. Kwa hiyo kula kwa usalama humaanisha kwamba ni lazima chakula kitayarishwe chini ya hali zisizoruhusu ukuzi wa bakteria katika chakula au mweneo wa kuchafuliwa kwa chakula jikoni. Fikiria madokezo yanayofuata kwa ulaji salama, na uyatumie kwa hekima nyumbani mwako mahali ambapo yahitajiwa.

Nawa mikono, ikifaa zaidi ufanye hivyo kwa sabuni, kabla ya kushughulikia chakula. Hakikisha kufunga majeraha yoyote ya mkononi. Epuka kupiga chafya na kukohoa juu ya chakula, na ujizuie kugusa nywele zako au kupangusa pua unaposhughulikia chakula. Ikiwa utayarishaji wako wa chakula wakatizwa nawe wafanya mambo mengine, kama vile kutumia choo au kushughulika na wanyama, hakikisha kunawa mikono kabla ya kugusa chakula tena.

Osha chakula utakachotayarisha. Usitumie kamwe matunda na mboga mbichimbichi zilizotoka moja kwa moja kwenye soko au bustani yako mwenyewe bila kuziosha, hata kama zitapikwa. Maji yenye kutumiwa kwa kuziosha yapasa yawe safi. Ikiwa mboga fulani na matunda yasiyomenywa ngozi zitaliwa zikiwa mbichimbichi, sugua vyakula hivi (yafaa zaidi iwe kwa kutumia brashi ya kusafisha mboga) ili kuondoa uchafu na pia masalio ya dawa za kuua wadudu. Mboga zenye majani-majani, kama spinachi na letisi, zapasa pia kuoshwa kabisa kabisa ili kuondoa mchanga na udongo.

Ikiwa wewe waishi katika eneo la kitropiki (lenye joto) ambako vidudu vinyonyaji, kama vile chango (minyoo) wa matumbo na wa maini, hupatikana kwa wingi, hapo matunda na mboga zote mbichimbichi ambazo zitapakuliwa ziliwe zikiwa mbichi au zikiwa zimepikwa kidogo tu zapasa kuoshwa katika maji safi zikiwa zimeongezewa kiasi kidogo cha kiua-vijidudu. Haipokloraiti ni kiua-vijidudu chenye matokeo mazuri ambacho hutumiwa sana kuua vijidudu, nacho huuzwa kikiwa na chapa mbalimbali za majina ya watengenezaji. Kwa kawaida, kiasi kidogo huchanganywa na maji safi, halafu matunda na mboga zaingizwa ndani. Ndipo chakula hicho chaweza kuoshwa kwa maji safi yasiyotiwa kitu chochote kabla ya kuliwa.

Pika kabisa kabisa nyama yote, samaki, na kuku ili kuangamiza viini vyenye madhara. Nyama na kuku waliogandishwa kwa barafu zapasa kuachwa ziganduke barafu ile kabisa kabla ya kuzipika, ili joto liweze kupenya kuingia kwenye kitovu. Nguruwe huenda wakawa wameambukizwa chango wembamba wa matumbo, na wanadamu wenye kula nguruwe wasiopikwa vizuri huenda wakapatwa na chango hao ambao huongezeka sana na kujishikiza katika misuli. Katika nchi fulani fulani asilimia 10 ya nyama ya soseji ambayo huuzwa katika masoko makubwa ya majiji yasemwa kuwa yenye ambukizo la chango hao wa matumbo. Chango wa matumbo waweza kuuawa kwa kupikwa kabisa kabisa kwa kutumia moto mwingi, lakini njia nyingine za utayarishaji, kama vile uchomaji wa kutoa mafuta na kutumbukiza nyama ndani ya dawa ya kuua vimelea, haziwaui chango hao.

Huenda samaki na jamii ya pweza wakawa wana chango wengi wa maini au wa mapafu, nao watapitishwa waingie ndani ya mfumo wa kibinadamu ikiwa samaki hao hawapikwi kabisa kabisa. Kuwatia chumvi, kuwatumbukiza ndani ya dawa ya kuua vimelea au ndani ya divai ya mchele hakutoshi kuua vijidudu hivyo vinyonyaji. Ingawa samaki wabichi na jamii ya pweza kwa desturi huliwa katika tamaduni fulani, tahadhari yapasa kutumiwa ikiwa maji ya mahali penye kuhusika huwa yenye uchafuzi mbaya sana.

Maji yatokapo kwenye chanzo cha mashaka-mashaka, yapasa kuchemshwa kabla ya kunywewa, kwa angalau dakika 15 mahali ambako maji huwa yamechafuliwa vibaya sana. Katika maeneo fulani huenda maji ya kunywa yakatakaswa kwa kutiwa klorini, lakini hayapasi kutegemewa mahali ambako bakteria na vijidudu vinyonyaji hupatikana kwa wingi. Jambo bora zaidi ni kuyachemsha.

Katika nchi nyingi maji yaliyochafuliwa hueneza kipindupindu, ugonjwa wa kuingiwa na nyongo katika damu, homa ya kuhara, mharo mwingine wa bakteria tofauti kidogo, mharodamu uletwao na kijidudu basilusi, na mharodamu uletwao na amiba, miongoni mwa magonjwa mengine. Mahali fulani fulani hata maji ya majijini hayawezi kuchukuliwa eti ni salama tu. Maji yakiisha kuchemshwa, yaweke katika vyombo safi vyenye kufunikwa.

Katika maeneo fulani yapendekezwa pia maji yachujwe takataka zilizomo. Vichujio hupatikana vikiwa vimeshikamanishwa na mabomba ya maji au vikiwa peke yavyo, na maji humiminwa humo na kuruhusiwa yatonetone kupita ndani ya posilini isiyopakwa rangi ya mng’ao au ndani ya vitu vingine vya kuchujia. Kuchuja huondoa vitakataka na vichafuaji vyenye kuelea-elea majini, lakini kwa kawaida hakuondolei mbali bakteria zenye madhara. Hata hivyo, vichujio fulani vipya na vifaa vyenye kushikamanishwa na mabomba ya maji kwa uwazi huondoa bakteria zenye madhara, ingawa kwa kulinganishwa ni vya bei kubwa, na visipobadilishwa kwa ukawaida, hivyo vyenyewe vyaweza kuchafua maji. Vifaa vya ki-siku-hizi vya kuchujia maji hata viliwezesha wasafiri wa anga za juu wanywe mkojo wao wenyewe.

Ikiwa maziwa yako hayakutibiwa kwa mashine za joto la kuua vijidudu, ni jambo la hekima kuyaondolea vijidudu hivyo kwa kuyapasha joto. Dakt. Sucy Eapen aliye mstadi Mhindi wa mambo ya ulishaji aonya hivi: “Kuna hatari ya maziwa kuchafuliwa na mnyama mwenyewe, na muuza-maziwa na njia yake ya kuyashughulikia, na pia na vyombo vyenye kutumiwa kuwekea maziwa.”

Maziwa yapasa kupashwa joto kufikia digirii 160 Farenhaiti au juu zaidi na kuwekwa kwenye halijoto hiyo kwa angalau sekunde 15. Halafu yabaridishe (yapoeshe kwa baridi nyingi) haraka haraka ili yafikie ubaridi wa digirii 50 Farenhaiti au zaidi. Njia nyingine yahusisha ndani kupasha joto maziwa hayo kwa muda mrefu zaidi kwa halijoto za chini zaidi: digirii 145 hadi 151 Farenhaiti kwa dakika 30.

Zuia mainzi wawe mbali na chakula. Huenda mainzi wakawa wamebeba viini vibaya vyenye kusababisha homa ya kuhara, kipindupindu, mharodamu, homa ya vipele vyekundu na mchochota wa kooni, na ugonjwa wa difteria (wenye kufunga koo na kudhoofisha moyo). Wao waweza pia kueneza vairasi ya polio na mayai ya chango wa matumbo na vijidudu vinyonyaji. Njia bora zaidi ya kushughulika na mainzi nyumbani ni kuwazuia wasianguliane wawe wengi. Waweza kuchunguza hali yako mwenyewe na kuona kama takataka zahitaji kusafishwa. Vitu vya kuwekea takataka vyapaswa kufunikwa ifaavyo na kutiliwa dawa ya kuzuia maambukizo. Usiruhusu mtu yeyote atupe kifusi karibu na makao yako. Samadi yapasa kufunikwa au kuondolewa mbali ili mainzi wasianguliane humo wawe wengi.—Linganisha Kumbukumbu 23:13.

Kula chakula mara baada ya hicho kupikwa, hasa wakati wa halihewa yenye joto. Bakteria zenye madhara zitazidishana haraka. Ikiwa wataka kutayarisha chakula mapema na ukile baadaye, basi kibaridishe chakula hicho baada ya kukipika na ukipashe joto kabisa kabisa kabla ya kukipakua.

Chakula kilichopikwa chapasa kuwekwa kikiwa na joto la kutosha (zaidi ya digirii 140 Farenhaiti) au kikiwa baridi (chini ya digirii 50 Farenhaiti). Kiwango cha hatari—ambamo bakteria zitakua na kuzidishana—ni kile cha katikati ya hapo. Hii yamaanisha kwamba masalio hayapasi kuwekwa ikiwa hayawezi kubaridishwa. Ikiwa huna friji, pika chakula cha kutosha mlo mmoja tu. Katika mabara fulani mimea ya kuongeza ladha na vikoleza-chakula huwa mara nyingi vimechafuliwa vikiwa na bakteria. Kwa hiyo vitu hivyo vyapasa kuongezwa chakulani mwanzoni mwa upishi ili vitibiwe kwa kupata joto kamili.

Weka jiko lako likiwa safi. Hii yahusisha ndani vyombo vyako vya kupikia, nguo zako, na wewe. Ikiwa kwa kawaida wewe hupika na kutayarisha chakula sakafuni, fanya liwe zoea katika jamaa yako kuvua viatu vyenye kukanyaga maeneo ya barabarani kabla ya kuingia katika eneo la upishi. Viatu vyaweza kubeba magonjwa kwa kugusa mavi ya mnyama na mwanadamu na kuchafua chakula ambacho wewe wajitahidi sana kukitayarisha. Wanyama vipenzi na wanyama wenginewo wapasa kuzuiwa wawe mbali na maeneo ya kutayarishia chakula.

Osha vyombo vya kulia kwa kutumia maji yenye joto na sabuni. Ikiwa unaosha vyombo kadhaa vya kupikia, yamwage maji yawapo machafu na uyabadilishe kwa maji safi yenye joto na sabuni. Kausha vyombo vya kulia kwa kutumia vitambaa safi, au uviache vikaushwe na hewa katika eneo lililo mbali na mavumbi na wadudu.

Katika mabara mengi vyombo husuguliwa kwa majivu, vikasuzwa kwa maji, na kukaushwa katika jua. Hii huwa na matokeo ya kuridhisha mahali ambapo sabuni ni gharama kubwa ya kiuchumi, kwa kuwa yale majivu ya alkalini huua vijidudu visivyoonekana kwa macho, na joto la jua pamoja na mionzi yalo isiyoonekana kwa macho huzuia viini vyenye kuharibu afya.

Nje ya Nyumba Yako

Kwenye mikahawa au makusanyiko makubwa ambako chakula huwekwa mezani ili kila mtu ajipakulie, jaribu kuchagua vyakula ambavyo ama vyaonekana kuwa vyenye joto sana ama vyenye baridi sana. Ukiona kwamba chakula kimekaa katika chumba chenye halijoto ya kawaida kwa muda mrefu wakati wa halihewa yenye joto, huenda ikawa afadhali kukiepuka.

Kwa kuwa hugharimu pesa kuchemsha maji, mikahawa mingi katika mabara yanayositawi hayachemshi maji ya kunywa ambayo wateja huandaliwa, kwa hiyo ni salama zaidi kutoyanywa. Pia, epuka tomvu za matunda (jwisi) au vinywaji ambavyo huhitaji kuongezewa maji au barafu. Vinywaji vilivyohifadhiwa chupani au vinywaji vyenye joto huwa salama zaidi kwa ujumla.

Ikiwa chango na vidudu vingine vinyonyaji ni tatizo katika eneo, epuka saladi zote zilizo mbichi. Tena epuka mboga na matunda yasiyoweza kumenywa ngozi, hata kama ni yenye kushawishi kadiri gani. Yaelekea kwamba vyakula hivyo havikuoshwa ifaavyo au havikutiwa dawa ya kuua maambukizo. Katika mahali fulani fulani matunda na mboga nzuri kwa ubichi hukatwa na kuuzwa barabarani ili ziliwe na wenye haraka ya kula. Hizi zaweza hata kuwa si salama kuliwa.

Katika mabara mengi ya Mashariki, wauza-bidhaa barabarani huonekana kwa wingi, wakipakulia watu vitu mbalimbali vya kudondosha mate. Kabla ya kula chakula kwenye kibanda cha jinsi hiyo, angalia kama kimewekwa katika hali za afya. Je! chaonekana kuwa kichafu? Je! chakula hicho kimepikwa tayari na kimekaa hapo bila kufunikwa? Je! kuna uandalizi wa kuondolea mbali takataka, au takataka zimetapakaa mahali pote? Je! mwenye kutayarisha chakula hicho aonekana mchafu-mchafu na shaghala-baghala? Je! hapo karibu pana wanyama na mainzi wengi? Ikiwa jibu kwa lolote la maswali haya ni ndiyo, basi hapo wewe unaalika matatizo ukila chakula hapo.

Karibu kila mtu hufurahia sana kula chakula kilichotayarishwa vizuri, chenye ladha. Lakini tumia uamuzi mwema na uangalifu wakati unaposhughulikia na kuchagua chakula. Halafu ona shangwe ya ulaji ulio salama!

[Picha katika ukurasa wa 20]

Nawa mikono, ikifaa zaidi ufanye hivyo kwa sabuni, kabla ya kushughulikia chakula

[Picha katika ukurasa wa 21]

Pika kabisa kabisa nyama yote, samaki, na kuku ili kuangamiza viini vyenye madhara

[Picha katika ukurasa wa 21]

Maji kutoka chanzo chenye kutilika shaka yachemshwe

[Picha katika ukurasa wa 22]

Ikiwa maziwa hayakutiwa dawa, yachemshe

[Picha katika ukurasa wa 22]

Zuia mainzi yawe mbali na chakula

[Picha katika ukurasa wa 22]

Kilinde salama chakula chako kisichafuliwe

[Picha katika ukurasa wa 23]

Weka sahani na vyombo vikiwa safi

[Picha katika ukurasa wa 23]

Mara nyingi huwa kuna sababu nzuri ya kutilia shaka usalama wa chakula chenye kuuzwa na wauzaji wa barabarani

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki