Jilinde na Ugonjwa Utokanao na Chakula
“SINGEWEZA hata kuondoka msalani kwa muda wa saa 12,” asema Becky. “Hayo maumivu ya tumbo yalikuwa makali mno. Nami nilikosa maji mwilini, ilinibidi kutiwa maji mwilini kupitia mishipa katika chumba cha dharura. Ilinichukua majuma mawili au matatu kurudia hali ya kawaida tena.”
Becky alisumishwa kwa chakula, ugonjwa utokanao na chakula. Kama ilivyo na majeruhi wengi, aliokoka. Lakini kumbukumbu la uguo lake kali lilibaki likiwa dhahiri. “Sikutambua kamwe kwamba kusumishwa kwa chakula kungeweza kukufanya uhisi mgonjwa sana,” yeye asema.
Maono kama hayo, na mengine mabaya zaidi, ni ya kawaida mno. Bakteria, virusi, vimelea, na protozoa nyingi hutisha kusumisha chakula chetu. Na ingawa baadhi ya aina fulani za magonjwa yatokanayo na chakula yamepungua miaka ya majuzi katika nchi zenye viwanda vingi, gazeti la World Health laripoti kwamba “[ugonjwa wa] salmonellois na mengineyo yamekataa katakata jitihada za kudhibitiwa.”
Visa vya kusumishwa kwa chakula ni vigumu kuvifuatilia kwa sababu visa vingi haviripotiwi. Dakt. Jane Koehler wa Vitovu vya Kudhibiti Maradhi vya Marekani alisema hivi: “Tunayoyajua kuhusu kusumishwa kwa chakula ni sehemu ndogo tu ya tatizo kubwa.”
Ni nini husababisha magonjwa yatokanayo na chakula? Huenda ukashangaa kujua kwamba mara nyingi tatizo huanza muda mrefu kabla ya chakula kufika sokoni.
Kilimo cha Kipuku
Karibu mbinu zote za kilimo za kisasa huhakikisha upitishwaji wa haraka wa pathojeni miongoni mwa mifugo. Kwa kielelezo, katika biashara ya ng’ombe katika Marekani, ndama kutoka mashamba yapatayo 900,000 huchangamana katika viwanda vya kuchinjia vichache kuliko mia moja. Kuchangamana huko kwaweza kusababisha msibiko wa shamba moja kuanzisha kipuku.
Isitoshe, Dakt. Edward L. Menning, mkurugenzi wa National Association of Federal Veterinarians, adai kwamba katika Marekani, “asilimia thelathini au zaidi ya chakula cha mifugo imesibikishwa kwa pathojeni.” Nyakati nyingine chakula cha mifugo huongezewa masazo ya kichinjio ili kuandaa protini za ziada—zoea ambalo laweza kusambaza salmonella na vijasumu vingine. Mifugo inapopewa vima vidogo vya viuavijasumu ili kuzidisha ukuzi, vijasumu vyaweza kuwa sugu kwa madawa. “Kielelezo kizuri ni salmonella, ambayo imekuwa sugu zaidi kwa viuavijasumu,” asema Dakt. Robert V. Tauxe wa Vitovu vya Kudhibiti Maradhi. “Twafikiri ni kwa sababu viuavijasumu hupatiwa wanyama wa kuliwa. Jambo hili huenda likahusu bakteria nyingine pia.”
Katika Marekani, ni asilimia ndogo tu ya kuku wana salmonella katika matumbo wakati wa kupelekwa kwenye kichinjio, lakini mwanamikrobiolojia Nelson Cox adai kwamba “asilimia hii huongezeka haraka kutoka asilimia ishirini hadi ishirini na tano wakati wa kusafirishwa.” Wakiwa wamesongamana katika vizimba vidogo, kuku waweza kuambukizwa kwa urahisi. Uchinjaji na utayarishaji wa kasi mno huongeza hatari. “Kufikia mwisho wa utayarishaji, hao kuku huwa wachafu kana kwamba wamechovywa ndani ya choo kichafu,” adai mwanamikrobiolojia Gerald Kuester. “Huenda wakawa walisafishwa, lakini vijasumu bado viko.”
Vivyo hivyo, utayarishaji wa nyama kwa kiwango kikubwa waweza kuwa hatari. “Vipakio vya chakula katika viwanda vya kisasa vya utayarishaji ni vikubwa sana hivi kwamba kipakio kimoja au viwili vilivyoambukizwa viingiapo vyaweza kusibikisha tani nyingi za vyakula ambavyo tayari vimetayarishwa,” yasema The Encyclopedia of Common Diseases. Kwa kielelezo, kipande cha nyama chenye dosari, chaweza kusibikisha kila mkate uliopachikwa nyama utokao kwa mtambo huohuo. Isitoshe, chakula kilichotayarishiwa mahali pamoja tu na kisha kusafirishwa hadi madukani na mikahawani huenda kielekee kisibikishwa ikiwa halijoto ifaayo haidumishwi wakati wa kusafirishwa.
Ni chakula kiasi gani sokoni ambacho chaelekea kuwa tisho? “Angalau asilimia 60 ya kila kitu kinachouzwa rejareja,” adai Dakt. Menning, akizungumza juu ya Marekani. Lakini unaweza kuchukua hatua za kujikinga kutokana na magonjwa yatokanayo na chakula, kwani gazeti FDA Consumer laonelea kwamba “asilimia 30 ya magonjwa ya aina hiyo hutokana na kushughulikia chakula kwa njia isiyofaa nyumbani.” Ni tahadhari zipi uwezazo kuchukua?
Kabla ya Kukinunua . . .
Soma Kibandiko. Viungo vyacho ni nini? Utahadhari ikiwa mayai ambayo hayajapikwa yametumiwa, kama vile katika mchuzi wa saladi au katika mayonnaise. Maziwa na jibini zapasa kuwa na kibandiko “pasteurized.” Tazama yale maonyo ya tarehe ya “usiuze baada ya” au “usitumie baada ya.” Usisadiki kwamba bidhaa zinazodai kuwa ni za asili ni lazima ziwe salama; huenda zikuhatarishe kwa hatari ambazo viongezwaji vimekusudiwa kuzuia.
Chunguza kwa makini chakula na kipakio chacho. Ikiwa chakula hakionekani kuwa cha karibuni, usikinunue. Kwa upande wa samaki, samaki mzima anapaswa kuwa na macho safi, mashavu mekundu, na harufu safi, na nyama yayo yapaswa kuwa safi na nyangavu, bila uvundo. Samaki wapaswa kuwa ama kwenye barafu au katika kibweta kilichojokofushwa. Samaki waliopikwa kimbele wakiwekwa pamoja na wabichi waweza kusibikishana. Isitoshe, mikebe na chupa zenye kuvuja, kufura, au zilizoharibika zaweza kusababisha ubotuli—kusumishwa kuliko haba lakini hatari ambako hushambulia mfumo wa neva.
Kabla ya Kukila . . .
Kipike kikamili. Hii ni mojapo kinga zilizo kuu zaidi dhidi ya ambukizo. “Zione bidhaa zote zitokanazo na wanyama kuwa zilizosibika, na ushughulike nazo inavyohitajika,” ashauri Dakt. Cohen. Mayai yapaswa kupikwa mpaka kiini pamoja na weupe wayo uwe thabiti, si wenye umajimaji. Kwa sababu bakteria yaweza kukua katika halijoto ya katikati ya digrii 4 Selsiasi na digrii 60 Selsiasi, nyama yapaswa kupikwa hivi kwamba halijoto yafikia digrii 71 Selsiasi, na ya kuku wapaswa kufikia digrii 82 Selsiasi.
Jizoeze upishi safi. Vyombo vyote vyapaswa kusafishwa kikamili baada ya kutumiwa. Ingawa wengine hudai kwamba vikatio vya mbao huzalishia bakteria, uchunguzi mmoja wadokeza kwamba hivyo huwa salama zaidi kuliko vikatio vya plastiki.a Iwe ni kikatio cha aina gani unachotumia chapasa kusafishwa kikamili kwa sabuni na maji moto. Wengine hudokeza kutumia kipararishaji pia. Nawa mikono baada ya kushika nyama na kuku mbichi, kwani chochote unachoshika chaweza kuwa kimesibika.
Tazama saa. Peleka nyumbani bidhaa ulizonunua haraka iwezekanavyo. Isitoshe, “bidhaa ziharibikazo haraka hazipaswi kuwa nje ya friji kwa zaidi ya muda wa saa mbili, iwe zimepikwa au ni mbichi,” asema mwanamlo Gail A. Levey. “Ikiwa halijoto nje ni zaidi ya digrii 90 [digrii 32 Selsiasi],” yeye aongezea, “punguza wakati huo kwa muda wa saa moja.”
Kabla ya Kukiweka . . .
Tumia vibweta vya kutosha. Gawanya vyakula moto kwenye vibweta vidogo ili viweze kupoa haraka katika friji. Acha nafasi katikati ya vibweta ili kwamba halijoto katika friji ama friza yako isizidi. Vibweta vyote vyapaswa kufunikwa ili kuzuia kusibikishana.
Chunguza friji yako. Halijoto ya friza haipaswi kuwa juu kupita digrii -18 Selsiasi, na ile ya friji yapasa kuwa chini ya digrii 4 Selsiasi. Ingawa nyama na nyama za kuku zaweza kuwekwa katika friza kwa miezi, zinaweza kuanza kuharibika katika friji kwa muda wa siku chache tu. Mayai yapasa kutumiwa mnamo majuma matatu. Ili kuepuka kupasuka na ili kuyaweka yakiwa baridi vyakutosha, ni vizuri zaidi ikiwa yataachwa katika katoni la awali na kuwekwa ndani ya friji badala ya kwenye trei ya mayai iliyo katika sehemu ya ndani ya mlango wa friji, ambapo ni mojapo mahali penye joto zaidi katika friji.
Licha ya tahadhari hizo zote zilizopo juu, ikiwa chakula chaonekana ama kunuka kwa njia yenye kutokeza mashaka, kitupe! Ingawa magonjwa yatokanayo na chakula mara nyingi huja na kutoweka bila madhara mabaya, katika visa vingine—hasa kwa watoto, wazee-wazee, na wale wenye kasoro za kinga mwilini—yaweza kuua.b
Ilikuwa mileani nyingi zilizopita kwamba Mungu alimwambia Noa hivi: “Wanyama wote, ndege wote, na samaki wote, . . . nakupa wote kuwa chakula.” (Mwanzo 9:2, 3, Today’s English Version) Utaratibu wa kuchinja na utayarishaji uliowekwa mahali pamoja tu kwa kuongezea usambazaji wa chakula kwa kiwango kikubwa huongeza hatari ya kuwa mgonjwa. Hivyo basi, fanya sehemu yako ukiwa mnunuzi. Uwe macho unaponunua, kupika, na kuweka chakula chako.
[Maelezo ya Chini]
b Iwapo utakuwa jeruhi wa ugonjwa utokanao na chakula, pata pumziko jingi, na unywe vinywaji kama vile maji ya matunda, supu, soda-maji. Dalili zikitokea za kuathiriwa kwa neva ama homa, kisunzi, kutapika, choo chenye damu, ama maumivu makali yakiendelea ama ukiwa katika kikundi cha waliohatarishwa zaidi, huenda ikawa afadhali kumwona daktari.
[Sanduku katika ukurasa wa 23]
Unapokula Ukiwa Mbali na Nyumbani
Tafrija. Tumia kihifadhi baridi kizuri kikiwa na barafu. Ingekuwa vema zaidi kukiweka katika mahali pa kuketi pa gari lako badala ya mahali pa mizigo. Kwenye tafrija hicho kihifadhi baridi chapaswa kuwekwa chini ya kivuli na kufunikwa. Viweke vyakula vyote vibichi kando na vyakula vingine. Kupika chakula nusu-nusu nyumbani na kisha kumalizia kukichoma baadaye hakupendekezwi, kwani kutokamilisha kupika chakula huchochea ukuzi wa bakteria.
Mikahawani. “Epuka mikahawa ambayo haionekani safi,” aonya Dakt. Jonathan Edlow. “Ikiwa eneo la kulia laonekana chafu, yaelekea jikoni ni kuchafu vilevile.” Regesha chakula chochote “moto” ambacho si moto kikweli au kisichopikwa kikamili. Nyama ya kuku ambayo ina wekundu-wekundu hivi haipaswi kuliwa. Mayai ya kukaangwa yapaswa kupikwa vizuri sehemu zote mbili. “Kadiri kiini kinavyokuwa chenye umajimaji, ndivyo hatari ilivyo kubwa zaidi,” laonya FDA Consumer.
Mikuo ya saladi. Kwa sababu wao huchanganya vyakula ambavyo huhitaji viwango tofauti vya kupika na vya ujokofushaji, mikuo ya saladi hufanyiza kile gazeti Newsweek hukiita “mahali pazuri pa kuzalishia bakteria.” Chunguza usafi wa mikuo ya saladi, na hakikisha kwamba chakula ambacho kinapasa kuwa baridi kimewekwa kwenye barafu. Hata mikuo ya saladi inapodumishwa vizuri, vijasumu vyaweza kupitishwa kutoka kwa mnunuzi mmoja hadi yule mwingine. Kama vile mwanamikrobiolojia Michael Pariza alivyosema: “Hujui ni nani alitumia mara ya mwisho kile kijiko cha mchuzi wa saladi.”
Vikusanyiko vya kijamii. Dakt. Edlow adokeza kwamba anapoandika chakula kwa ajili ya kujipakulia, mkaribishaji anapaswa “kuweka viwango vidogo vya chakula mezani na ugavi wa ziada ulio kwenye bakuli za kupakulia kurudisha kwenye friji au mekoni badala ya kuacha chakula kibaki pale kwa muda mrefu.” Weka vyakula baridi chini ya digrii 4 Selsiasi na vyakula moto zaidi ya digrii 60 Selsiasi. Nyama inayopikwa kwa matumizi ya baadaye yapasa kuwekwa kwenye friji mara moja na yapasa kubaki hivyo mpaka itakapokuwa tayari kusafirishwa. Kabla ya kuliwa, chakula chaweza kupashwa moto kikamili tena.
[Picha katika ukurasa wa 23]
Ikiwa hakionekani kuwa cha karibuni, usikinunue
[Picha katika ukurasa wa 22]
Je, jikoni ni safi katika mkahawa ambao unakula?