Vijana Wauliza . . .
Namna Gani Kazi-Maisha za Kuwa Violezo vya Mapambo na Kufanya Mashindano ya Urembo?
“WAKATI wa kusafiri kwenda New York mwaka uliopita,” akakumbuka Amy mwenye umri wa miaka 12, “jamaa mwenye hoteli moja alimwambia mama yangu, ‘Wapaswa kuingiza binti yako katika shule ya violezo vya mapambo. . . . Yeye ana sura nzuri.’”
Imekuwa hivyo hivyo kwa vijana kadhaa wenye kuvutia. Racine mwenye umri wa miaka kumi na mitano alipokea simu kutoka kwa mwanamume aliyejaribu kufanya yeye na dada yake wa umri mdogo zaidi wapendezwe na kazi-maisha ya kuwa violezo vya mapambo. Mwanamke kijana wa kutoka Afrika Kusini aliombwa ashiriki katika shindano la urembo. Na matoleo hayo yenye pesa nyingi si kwa wasichana peke yao. Kijana Jonathan alipewa fursa ya kazi ya kuajiriwa awe kiolezo cha mapambo ya wanaume.
Ndiyo, kotekote ulimwenguni, wanaume na wanawake vijana na watoto wa umri wote wanaingizwa katika kazi-maisha za kuwa violezo vya mapambo, maonyesho ya urembo, na kadhalika. Katika United States pekee, yaripotiwa kwamba mamia ya maelfu ya mashindano ya urembo hufanywa kila mwaka. Washindi hupokea maelfu ya dola kwa pesa taslimu, zawadi, na tuzo za kupata uanachuo. Kwa wachache wateule, kushinda onyesho la urembo kumefanya wapate vitumbuizo vyenye faida ya kifedha na kazi-maisha za kuwa violezo vya mapambo.
Mwanamke mmoja kijana alitaarifu: “Maisha yangu yote nimetaka kuwa kiolezo cha mitindo—kuvaa mavazi ya kiolezo kwa ajili ya magazeti ya kwetu na maonyesho ya mitindo. Malipo hutofautiana kuanzia dola 25 hadi dola 100 kwa saa moja.” Ingawa hivyo, yaripotiwa kwamba violezo fulani walio mashuhuri huchuma mishahara ya kufikia dola 2,500 kwa siku! Basi, si ajabu kwamba vijana fulani Wakristo wameshawishwa kupata pesa taslimu kwa kutumia sura zao nzuri. Wewe ungeitikiaje ukitolewa fursa hiyo yenye kushawishi sana?
Urembo Waweza Kuwa na Manufaa
Ilisemwa juu ya Esta bikira Myahudi kwamba “alikuwa wa umbo mzuri na uso mwema.” (Esta 2:7) Kwa uhakika, hata ungeweza kusema kwamba alishiriki katika shindano la urembo la namna zote bila kujitolea yeye mwenyewe. Katika hali zipi? Malkia Mwajemi Vashti alikuwa ameondolewa cheoni kwa kutojitiisha. Ili kupata mtu afaaye badala yake, Mfalme Ahasuero alikusanya mabikira walio warembo zaidi kutoka milki yake. Katika kipindi cha miezi 12, alipanga wanawake vijana wawekwe katika ulaji maalumu na kukandwa mwili kwa ukawaida kwa mafuta ya zeri na manemane. Ndipo kwa zamu kila msichana akakadiriwa ubora wake. Na zamu ya Esta ilipofika, alichaguliwa awe malkia mpya!—Esta 1:12–2:17.
Ingawa hivyo, kwa nini Esta alishiriki? Je! yeye alikuwa mtafutaji wa utukufu ulio batili? Sivyo, Esta alikuwa akifuata mwelekezo wa Yehova, ambao aliutafuta-tafuta kupitia binamu yake aliye mtunzi mcha Mungu, Mordekai. (Esta 4:5-17) Mwanamume mwovu mwenye kuitwa Hamani alikuwa akipanga hila ya kuharibu watu wa Mungu, taifa la Israeli. Hilo ‘shindano la urembo’ lilimruhusu Yehova atumie maarifa kumwingiza Esta katika cheo cha umashuhuri ambamo angeweza kuvuruga hila hiyo. Hivyo sura nzuri ya Esta ikathibitika kuwa baraka kwa ajili ya watu wote wa Mungu!
Namna gani leo? Kwa wazi sura ya mtu silo jambo la maana kabisa maishani.a Hata hivyo, sura nzuri iandamanapo na kiasi na unyenyekevu yaweza kuwa sifa ya maana. Ingawa hivyo, je! hiyo yamaanisha kwamba kuwa violezo vya mapambo au kushiriki katika maonyesho ya urembo ni njia ya busara ya kutumia sifa hizo? Au kuna mambo ya kufikiria zaidi ya ule uvutio wa umaarufu, utukufu, au utajiri?
Nyuma ya Ule Umetimeti
Kuwa kiolezo cha mitindo kuna uvutio wa kadiri fulani. Nguo nzuri, vito vya bei, mshahara mzuri, fursa za kusafiri na kuonekana-onekana katika televisheni—yote haya ni mambo yenye kuvutia sana. Kwa kuongezea, mazoezi ya kuwa violezo yamesaidia wanawake wengi vijana watembee kwa madaha mazuri na kusema kwa uhakika na utulivu. Lakini zaidi ya ule uvutio, umetimeti, na mng’ao, kwaweza kuwako hatari halisi zenye kuotea Mkristo.
Si kwamba jambo lenyewe la kuwa kiolezo ni baya. Kadiri fulani ya kuwa kiolezo hutimiza kusudi nyofu: kufanya bidhaa ionekane yenye kuvutia. Hiyo ni sababu moja kwa nini mikono ya kupendeza hutumiwa kuonyesha mng’arisho wa kucha katika picha ya magazeti na matangazo ya biashara katika televisheni. Vivyo hivyo, wanaume na wanawake wenye maumbo mazuri hutumiwa kuonyesha nguo. Ikiwa nguo hizo ni za kiasi, huenda kusiwe na katao lolote kwa Mkristo kulipwa ili awe kiolezo chayo.
Hata hivyo, kuna matatizo mengi yenye kuhusika ndani ya kuwa kiolezo ambayo hayawi rahisi kuepukwa sikuzote. Kwa kielelezo, wewe ungeitikiaje kama ungeombwa uvae kitu fulani kisicho na kiasi au kisichowafaa Wakristo? Au ikiwa mpiga picha angetumia msongo fulani usioonekana wazi ili usimame kwa njia yenye kuchochea nyege au yenye kushawishi? Zaidi ya hilo, mtu hawezi kuwa na uhakika sikuzote jinsi picha zitakavyotumiwa. Kwa kielelezo, picha hizo zingeweza kutokea katika mazingira yenye kuunga mkono sikukuu za dini bandia au yenye mihusiko fulani ya kukosa adili.
Halafu kuna lile tokeo ambalo kazi-maisha ya jinsi hiyo ingeweza kuwa nalo juu ya utu wa mtu, kuendeleza ukuzi wa vitabia hasi. Mkazo wenye kuendelea juu ya sura ya mtu ya nje badala ya “utu wa moyoni usioonekana” umesababisha watu fulani walio violezo vya mitindo wawe bure kabisa. (1 Petro 3:4) Pia, kufanya kazi na nguo ghali, vito vyenye thamani, na vitu kama hivyo kwaweza kusababisha fikira za kufuatia vitu vya kimwili zitie mizizi.—1 Timotheo 6:10.
Kazi ya kuwa violezo vya mitindo ina sifa mbaya pia ya kufanya mtu awe wazi kwa watu mmoja mmoja, wa kiume na wa kike, ambao husisitiza juu ya kufanya mapenzi kingono kwa kubadilishana na kupandishwa cheo katika kazi-maisha. Kama vile mmoja aliyekuwa kiolezo cha mitindo alivyosema: “Kusema wazi, ni lazima ukubali kuingiliwa [kingono] ndipo ufaulu.” Zaidi ya hilo wengine hudai kwamba ugoni-jinsia-moja umeenea sana miongoni mwa violezo wa kiume. Ingawa huenda hilo lisiwe kweli sikuzote, huenda likawa ni tatizo zaidi katika kuwa kiolezo kuliko katika kazi nyinginezo.
Maonyesho ya Urembo
Mengi ya yaliyotangulia yaweza pia kusemwa juu ya maonyesho ya urembo. Hata hivyo, kwa kuongezea pia kuna ule msongo wa mashindano makali sana. Jambo hilo limesukuma washindani fulani kufikia hatua ya kuwaharibia mambo washindani wenzao. Kulingana na ripoti moja, “washindani fulani huwa wakitafuta sana ushindi hivi kwamba hawakosi kupaka rangi za midomoni juu ya nguo za kuogelea za washindani wenzao au kupaka madoa ya Kokakola katika gauni zao za jioni, eti ‘kiaksidenti.’”
Pia, wadhamini wa maonyesho ya urembo hutarajia wasichana wao wajitie kabisa katika wajibu wakiwa wawakilishi wao wa mauzo na mahusiano ya kiumma. Mara nyingi hiyo hutaka kufanya mikutano ya starehe pamoja na watu mpaka mapambazuko. Mwanamke mmoja kijana aliambiwa: “Mpenzi, wewe huchoki kamwe. Kumbuka hivyo tu. Wewe ndiwe wa kwanza kuwasili kwenye tafrija na ndiwe wa mwisho kuondoka.” Hata kusipotukia mengi mno, jambo hilo laweza kumweka kijana Mkristo katika hali ya kuwa na ushirika usiofaa na lingeweza hata kuongoza mtu ahusike kimahaba na mtu asiyeamini.—2 Wakorintho 6:14.
Mwisho, kuna ule uhakika wa kwamba mashindano ya urembo hupuuza ile kanuni ya Biblia kwenye Waroma 1:25, NW, ambayo hushutumu wale ‘waheshimuo mno na kuutolea utumishi mtakatifu uumbaji badala ya yule Mmoja aliyeumba.’ (Linganisha Matendo 12:21-23.) Kwa msingi huo pekee, ingefaa kijana Mkristo akatae kushiriki katika shindano la urembo hata ikiwa ni la kadiri ndogo shuleni.
Urembo wa Kweli Kweli
Vijana waliotajwa mapema kidogo walilazimika kupima uzito wa mambo haya ya uhakika katika kufanya maamuzi yao wenyewe. Ingawa jambo lenyewe tu la kufuatia kazi ya kuajiriwa ya kuwa kiolezo halingeweza kuwa kosa, Amy na Racine waliamua kutofanya hivyo. Vilevile Jonathan alikataa kazi ya kuajiriwa ya kuwa kiolezo wa kiume na sasa anatumikia kwenye makao makuu ya ulimwengu ya Mashahidi wa Yehova, akifuatia kazi-maisha katika huduma ya wakati wote. Lakini msichana mwingine wa kuvutia aliingia na kushinda mashindano mawili ya urembo. Leo, yeye hahudhurii kamwe mikutano ya Kikristo. Ni wa kweli kama nini usemi huu: “Chenye kuvutia sana na kirembo si chema sikuzote; lakini chema ni kirembo sikuzote.”
Twakumbushwa tena juu ya Esta. Kwa sababu ya urembo wake wa kimwili, yeye alitiwa katika mlolongo wa mfalme wa kutafuta mke. Hata hivyo, kiasi chake, ujitiisho, utiifu, na ukosefu wa pupa ndiyo mambo yaliyomfanya awe mrembo kweli kweli. (Esta 2:13, 15-17) Yeye aliweka kielelezo cha maneno ya Petro: “Kujipamba kwenu, kusiwe kujipamba kwa nje, yaani, kusuka nywele; na kujitia dhahabu, na kuvalia mavazi; bali kuwe utu wa moyoni usioonekana, katika mapambo yasiyoharibika; yaani, roho ya upole na utulivu, iliyo ya thamani kuu mbele za Mungu.” (1 Petro 3:3, 4) Hatimaye, kusitawisha sifa hizi za Kikristo kutakuja kuwa na pato kubwa ambalo lazidi kwa mbali thawabu za muda mfupi za urembo wa kimwili.
[Maelezo ya Chini]
a Ona makala, “Sura Ni ya Maana Kadiri Gani?” iliyo katika toleo la Awake! la Januari 8, 1986.
[Picha katika ukurasa wa 24]
Sifa za Kikristo ni zenye pato kubwa kuliko thawabu za muda mfupi za urembo wa kimwili