Vijana Wauliza . . .
Mwili Wangu Unapatwa na Nini?
MABADILIKO mazuri ajabu yameanza kutukia katika mwili wako.
Ingawa hivyo, sasa hivi huenda yakaonekana si mazuri ajabu hata kidogo. Huenda ukahisi umevurugika, mwenye aibu, au hata kuogopeshwa na linalokupata. “Mimi sikuwa tayari kamwe,” akasema msichana mmoja. “Nilifikiri, Jamani, sitaki jambo hili lianze kunipata sasa hivi.” Mvulana mmoja alisema hivi: “Sijui kama mimi ni mtu asiye wa kawaida au ni wa kawaida. Nina miaka 13 na mabadiliko yanatukia katika mwili wangu . . . Nahisi nikiwa tofauti kabisa na mpweke nyakati fulani nami naogopa sana kwamba mtu fulani atanicheka.”
Yaeleweka kwamba wewe pia ungeweza kuhisi hivyo. Unapita katika kile ambacho msichana mmoja tineja alikieleza wakati mmoja kuwa wakati ambapo “mwili [wake] ulianza kupatwa na kichaa.” Lakini kile ambacho huenda kikaonekana kama “kichaa” wakati ule ni utaratibu mzuri kweli kweli unaokubadili kutoka kuwa mtoto uwe mtu mzima. Huitwa ubalehe. Na ingawa jina hilo lasikika kuwa la kuogopesha, ubalehe si ugonjwa fulani, wala si wewe wa kwanza kupitia humo. Mama yako na baba yako walipatwa na jambo hilo. Labda wanashule wenzako na marafiki wengine wa umri wako wanalipitia. Tena uwe na uhakika kwamba, utaokoka.
Lakini ni nini hasa tukio hili la ajabu liupatalo mwili wako?
Utendaji wa Kemikali za Kubalehe
Biblia husema kwamba wakati fulani baada ya yeye kufika umri wa miaka 12, “Yesu akazidi kuendelea katika . . . kimo [ukuzi wa kimwili, NW].” (Luka 2:52) Ndiyo, hata Yesu Kristo alipitia ubalehe. Wakati wa ubalehe, utapatwa na kipindi cha ukuzi na usitawi wa kimwili. Ingawa hivyo, kisababishi cha ukuzi huu ni fumbo halisi, mwujiza! Twakumbushwa juu ya mfano mmoja wa Yesu ambamo alisema juu ya mwanamume aliyepanda mbegu fulani. Yesu alisema hivi: “Mbegu zinaota na kukua; yeye hajui inavyofanyika.” (Marko 4:27, NW) Vivyo hivyo, madaktari waweza kutupa muhtasari hivi hivi tu juu ya yatendekayo wakati wa ubalehe.
Mahali fulani kati ya umri wa karibu miaka 9 na 16, mtu huingia ghafula ndani ya ubalehe. (Umri huo hutofautiana mtu na mtu, na kwa kawaida wasichana huanza mwaka mmoja au miwili kabla.) Ubongo wako huanza mtendeshano wa kugutusha ambao huendelea mfululizo kwa kufungulia utendaji wa tezi ndogo sana juu ya kaakaa la kinywa chako iitwayo tezi-ubongo ya kuchochea ukuzi. Tezi hiyo huitikia kwa kufanyiza wajumbe wa kikemikali waitwao homoni. Wao huogelea wakipita katika mkondo wa damu yako na kuvipa viungo vyako vya uzazi ishara ya kuanza kufanyiza homoni nyingine zaidi. Makende ya mvulana hasa hutokeza homoni za kiume, kama vile testosteroni; mifuko ya mayai ya msichana, homoni za kike, kama vile estrojeni.
Homoni hizo, nazo, sasa huzipa ishara tezi na viungo vingine vianze kubadili sura yako.
Mabadiliko Ambayo Hupata Wasichana
Ikiwa wewe ni msichana, jambo la kwanza ambalo huenda ukaona ni ongezeko la kidato kwa kidato la ukubwa wa matiti yako. Homoni zako zimechochea tezi zako za umama zianze kukua. (Tezi hizo zenye kufanyiza maziwa huwapa akina mama uwezo wa kulisha watoto wao wachanga.) Homoni zako huchochea pia mfanyizo wa shahamu (mafuta), ambayo huyapa matiti yako umbo layo. Pia shahamu itawekwa kwenye viuno vyako, mapaja, na matako. Utaongezeka uzito na huenda ukapata ghafula ukuzi wa haraka.
Ingawa wasichana walio wengi hukaribisha mabadiliko haya ya kimwili, si wasichana wote huyakaribisha yote. Kwa kielelezo, nywele zilizo juu ya mikono yako, miguu, na makwapani huenda zikawa nene zaidi na nyeusi zaidi. Sasa, katika mabara fulani, huenda nywele hizo za mwili zikaonwa kuwa zisizo za kike au zisizofaa mtindo wa sasa. Bila kujali mitindo, hiyo ni ishara nzuri ya kwamba unakua kuingia katika uanauke.
Badiliko jingine lisilokaribishwa huenda likawa ni ule utendaji ulioongezeka wa tezi zako za jasho—utatoa jasho zaidi. Huenda harufu yenye kuandama ikakuaibisha. Lakini ukioga mara nyingi na kuvaa nguo safi, ni mara haba kuwa na matatizo mazito ya harufu. Pia vijana fulani huchagua kutumia marashi yawe ulinzi zaidi dhidi ya harufu.
Ukuzi mmoja wa kibinafsi sana wahusisha ukuzi wa nywele kuzunguka eneo lako la uzazi. Hizo huitwa mavuzi ya kinena. Ikiwa hukupashwa habari mapema, huenda ungeweza kuliona jambo hilo kuwa la kuogopesha kidogo. Lakini ni jambo la kikawaida kabisa wala si la kuaibikia kamwe.
Huenda pia ubalehe ukachochea kile ambacho The New Teenage Body Book ilikiita “hangaiko [la sura] lililo namba moja miongoni mwa matineja”—matatizo ya ngozi. Mara nyingi mabadiliko katika utendaji wa kemikali za mwili wako huwa na tokeo la kufanya ngozi iwe na mafuta zaidi. Chunusi na vipele vyeusi hutokea. (Kulingana na uchunguzi mmoja, matatizo ya vipelepele yalisumbua karibu asilimia 90 ya matineja wote waliochunguzwa!) Uzuri ni kwamba, kwa kawaida tatizo hilo laweza kudhibitiwa kwa kutunza ngozi vizuri.—Ona makala “Je! Siwezi Kufanya Jambo Fulani Kuhusu Vipele Vyangu?” iliyotokea katika toleo la Februari 22, 1987 la Amkeni! (Kiingereza).
Mabadiliko Ambayo Wavulana Hupata
Ikiwa wewe ni mvulana, matokeo ya kwanza ya ubalehe hayataonekana wazi kama ya msichana. Mfumo wako wa uzazi uanzapo kufanya kazi, viungo vyako vya uzazi huwa vikubwa kidato kwa kidato. Nywele huanza kukua kuzunguka sehemu zako za uzazi. Tena, hilo ni jambo la kawaida kabisa.
Wakati ule ule, huenda ukapata ukuzi wa ghafula. Shahamu na tishu za misuli zaongezeka kwenye mwili wako. Wapata kuwa mkubwa zaidi, imara zaidi, mabega yako yapanuka. Umbo la mwili linazidi kuacha kuonekana kama la mtoto na kuwa la kimwanamume zaidi.
Badiliko jingine la kupendeza lahusisha ukuzi wa nywele juu ya miguu yako, kifua, uso, makwapa. Hilo pia lachochewa na homoni ya testosteroni. Kitabu Changing Bodies, Changing Lives, cha Ruth Bell, hunukuu kijana mmoja akisema: “Nilipokuwa na miaka kumi na minne nilitembea-tembea karibu majuma mawili nikiwa na uchafu mweusi juu ya mdomo wangu wa juu. Niliendelea kujaribu kuuosha lakini ukakataa kuosheka. Halafu nikautazama kweli kweli nikaona kwamba ni masharubu.”
Ijapokuwa hivyo, nywele za mwili ubakizo ukiwa nazo hazina uhusiano wowote na jinsi ulivyo mwanamume kabambe; ni urithi tu. Ndiyo kusema, ikiwa baba yako ana kifua chenye nywele, yaelekea sana kwamba wewe pia utakuwa nacho. Ndivyo na nywele za uso. Ingawa hivyo, sana-sana ufikiapo miaka ya mwisho wa utineja au miaka ya mapema ya 20, ndipo utanyoa ndevu kwa ukawaida.
Hakika kutakuwako nyakati utakapoaibika. Wavulana pia hupata kwamba tezi zao za jasho huongezea utendaji wazo. Huenda ukalazimika kuhangaikia hasa usafi wako wa kibinafsi ili kuepuka matatizo ya harufu. Wewe pia huenda ukapatwa na vipelepele vya ghafula kwa sababu ya ngozi kuwa na mafuta mengi zaidi.
Wakati wa miaka yako ya katikati ya utineja, kikoromeo chako kitaongezeka ukubwa; nyuzi za sauti zitanenepa na kurefuka. Tokeo ni kwamba, sauti yako itaongezeka kina. Sauti za wavulana fulani hugeuka upesi sana kutoka nyembamba laini kuwa kati ya nyembamba na nzito. Lakini kwa wengine, sauti hubadilika kidato kwa kidato kwa kipindi cha majuma au miezi ambacho huonekana kuwa kirefu mno. Mahadhi nzuri za kina kirefu huvurugwa na sauti nyembamba za kuaibisha zilizo kali na zenye kuvunjika. Ingawa hivyo, starehe. Sauti yako italainika baada ya muda. Kwa sasa, ikiwa waweza kujicheka, hiyo yasaidia kupunguza aibu.
Ukuzi Ulio wa Maana Zaidi
Kukua ni jambo zuri la kusisimua! Kwaweza pia kuaibisha na kuogopesha. Jambo moja ni hakika: Huwezi kuharakisha wala kukawiza utaratibu wa ukuzi. Kwa hiyo badala ya kuyapokea kwa uhasama na hofu mabadiliko yaletwayo na ubalehe, yastaajabie, yakubali kwa neema—na kwa ucheshi. Ng’amua kwamba ubalehe si tokeo la mwisho bali ni awamu moja tu. Ile dhoruba ya ubalehe ituliapo, utaibuka ukiwa mwanamume au mwanamke aliye mtu mzima!
Ingawa hivyo, usisahau kamwe kwamba ukuzi wako ulio wa maana kabisa wahusisha, si kimo chako, umbo, wala maumbiko ya uso, bali ukuzi wako wa utu—kiakili, kihisia-moyo, na kiroho. Alisema hivi mtume Paulo: “Nilipokuwa mtoto mchanga, nalisema kama mtoto mchanga, nalifahamu kama mtoto mchanga, nalifikiri kama mtoto mchanga; tokea hapo nilipokuwa mtu mzima, nimeyabatilisha mambo ya kitoto.” (1 Wakorintho 13:11) Haitoshi kuonekana kama mtu mzima. Ni lazima kidato kwa kidato ujifunze kutenda, kusema, na kufikiri kama mtu mzima. Usihangaikie sana linaloupata mwili wako hivi kwamba usahau kumtunza “yule binadamu wa ndani.”—2 Wakorintho 4:16, The Jerusalem Bible.
Na bado, huenda pande fulani za ubalehe zikawa zenye kusononesha sana. Jinsi ya kushughulika nazo itakuwa ndiyo habari ya makala za wakati ujao.
[Picha katika ukurasa wa 27]
Ukuzi wa ghafula-ghafula hufupisha mno mikono ya koti