Mfumaji wa Afrika Magharibi Akifanya Kazi
Na mleta habari za Amkeni! katika Liberia
KATIKA karne hii ya 20 yenye maarifa ya juu, ikiwa na viwanda vyayo vyenye kutokeza bidhaa nyingi sana kwa kutegemea kompyuta, inaburudisha kama nini kuona fundi akitokeza kazi ya kupendeza kwa njia ifananayo sana na ilivyokuwa katika nyakati za Biblia.
Siku moja nilipokuwa nikizuru Mustapha, nilimkuta akifanya kazi kwenye kitanda chake cha ufumaji. Nyakati za zamani, ufumaji ulikuwa sanaa ya siri, hivyo basi kulingana na pokeo la mahali, hakuna mtu angeweza kusimama nyuma ya mfumaji amtazame akifanya kazi. Mustapha alieleza kwamba miongoni mwa kabila la Mende, wakati mmoja wafumaji walikuwa wa familia moja katika milki ya chifu. Hata wakati huo, ni watu wachache tu walioujua utaratibu wa kufuata, na ni machifu wakuu peke yao wangekuwa na uwezo wa kuhudumiwa na mfumaji.
Chifu mkuu alipoajiri mfumaji, eneo fulani lilifyekwa katika msitu wa karibu, na ua ulioezekwa kwa makuti ukajengwa kuzungukia eneo hilo la kufumia. Ilikuwa imani ya kawaida kwamba roho fulani alimsaidia mfumaji katika utaratibu huo uliotatanika wa kufanyiza umbo la nguo, hivyo basi ua huo ulizuia mtu yeyote asiingie bila kumwonya mfumaji.
Mfumaji alikuwa akiajiriwa na chifu mkuu ili afanyize gbalee, yenye kanda kadhaa zilizoshonwa pamoja kufanyiza kipande kilicho kikubwa kidogo kuliko shuka ya kupamba kitanda. Mfumaji na familia yake, pamoja na msaidizi fulani, walikuwa wakienda wakakae kwenye boma la chifu huyo, ambako waliandaliwa kijumba na chakula cha kila siku. Mfumaji hakujiharakisha isivyofaa na ingeweza kumchukua hata mwaka mmoja kumaliza gbalee mbili. Ofisa wa serikali au mheshimiwa mwingine alipozuru, alipewa gbalee hiyo kuwa zawadi. Mfumaji hakulipwa kazi yake kwa pesa bali angeweza kupewa ng’ombe au msichana bikira.
Hata hivyo, wafumaji wa ki-siku-hizi, kama Mustapha, huendesha shughuli kibiashara. Mustapha hata alipata mkataba wa kuandaa vifaa vya kupamba Jumba la Mikutano ya Shirika la Umoja wa Afrika katika Monrovia. Kadiri biashara ya utalii inavyokua, kunakuwa na ukuzi wa soko la gauni, shati, shuka za kupamba vitanda, vikeka vya kuwekelea vitu, na bidhaa nyingine za kufumwa.
Chanzo cha Vifaa vya Msingi
Nilipata habari kwamba vifaa vyote vya msingi hupatikana katika eneo lile. Nyuzi hufanywa kutokana na pamba. Kuna namna mbili hasa, ile ya kichaka kifupi (nyeupe) na ile ya kichaka kirefu (ya kahawia). Ndipo pamba hiyo hutenganishwa kulingana na rangi—ya kahawia, ya kahawia-nyepesi, na nyeupe—na kuwekwa katika kinja (vikapu vya kuwekea akiba).
Nilialikwa nizuru mwanamke mmoja mzee, Siah, kuangalia hatua ambazo mfumaji hutayarishiwa pamba. Mwanamke huyo aliona fahari nyingi kuonyesha ujuzi wake.
Hatua ya kwanza ni kuziondoa mbegu kwenye pamba. Ili kufanya hivyo, pamba huwekwa juu ya bao kubwa, na kijiti cha mviringo au kipande cha chuma hupitishwa juu yalo kwa mwendo wa kuzunguka-zunguka. Kwa njia hiyo mbegu husongwa zikatoka kwenye pamba. Halafu vipande vya utembo wenye mbegu hutiwa katika vikapu kungojea hatua ile nyingine, ambayo ni kusafisha kwa kuchanua-chanua.
Kutazama hatua hii husisimua. Utembo wa pamba hukunjwa juu ya uzi wa upinde, ambao huchunwa-chunwa mara nyingi ili kuilegeza pamba. Hatimaye pamba hulainika. Halafu vipande vyenye ukubwa wa kiganja cha mkono huambuliwa, huchapwa-chapwa ziwe tambarare, na kuwekwa katika tabaka legelege katika vikapu, tayari kwa kusokotwa.
Hatua ifuatayo, kusokota, hufanywa sana-sana na wanawake. Hiyo yakumbusha juu ya pongezi ya Biblia juu ya mke hodari: “Hutia mikono yake katika kusokota [kwenye kijiti cha bonge la uzi, NW]; na mikono yake huishika pia.” (Mithali 31:19) Hiyo yaeleza kwa usahihi njia ambayo ingali yatumiwa leo, kama ionyeshwavyo na Siah.
Kwanza, ile pamba safi iliyochanuliwa yeye huifunga ikiwa legevu kuzungukia kijiti laini, kile kijiti cha bonge la uzi. Kwa kukiinua juu kijiti cha bonge la uzi katika mkono wake wa kushoto, mwanamke huyo huzivuta chini zile tembo (nyuzinyuzi) kwa mkono wake wa kulia, wakati ule ule akizipota ili ziwe uzi usio laini. Uzi huo hushikizwa kwenye pia, kisha husokotwa zaidi na ile pia inayozunguka kasi.
Kwa kuwa pamba ile huwa hasa nyeupe au ya kahawia, mimi nilishangaa ni jinsi gani zile rangi dhihirifu hupatikana. Basi, rangi nyekundu nyangavu hupatikana kwa kuchemsha gome la mti kamuwudi. Rangi ya manjano hutokana na mmea wa kinjano. Mzizi mmoja hutayarishwa kwa hatua zile zile ili kufanyiza rangi ya kahawia. Jivu la miti huongezewa ili kukwamisha rangi hizo.
Buluu nyangavu hupatikana kutokana na majani machanga mororo ya mnili. Majani hayo hukanyagwa-kanyagwa kwenye mkeka, halafu hukaushwa kwa jua kwa siku tatu au nne. Baadaye, hutiwa katika vikapu vya akiba bila kushindiliwa na kuangikwa chini ya vipenu vya nyumba. Baadaye vile vitakataka vya kutia rangi hutolewa katika vyombo hivyo na kuchanganywa na maji. Halafu huwekwa katika vyungu vilivyofunikwa, ambavyo vyaweza kuonwa vimesimama au vimefukiwa chini ya udongo katika ua au nyuma ya nyumba. Lile bonge la uzi huingizwa katika urangi huo kwa pindi za karibu siku moja moja, na namna mbalimbali za rangi hufanyizwa kulingana na mara ambazo limeingizwa.
Sanaa ya kufuma imetumiwa kwa karne nyingi kutokeza unamna-namna wa vitu ambavyo huongezea shangwe yetu maishani. Kujifunza mwenyewe mambo madogo-madogo ya hatua hizo kulinisisimua kweli kweli.