Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g90 12/8 kur. 8-11
  • Kupata Shangwe ya Uhusiano Mchangamfu Kati ya Wakwe

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kupata Shangwe ya Uhusiano Mchangamfu Kati ya Wakwe
  • Amkeni!—1990
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kukitambua Kifungo Kipya
  • ‘Mwanamke Aliye na Hekima Kikweli’
  • Uwe Mwenye Kusamehe
  • ‘Upendo Haushindwi Kamwe’
  • Mke Anayependwa Sana
    Kufanya Maisha ya Jamaa Yako Yawe Yenye Furaha
  • Ni Nini Husababisha Tatizo Hilo?
    Amkeni!—1990
  • Faida Zenye Kudumu Kutokana na Kuifuata Biblia Kama Jamaa
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1975
  • Siri ya Kupata Maisha Yenye Furaha ya Jamaa
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1977
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1990
g90 12/8 kur. 8-11

Kupata Shangwe ya Uhusiano Mchangamfu Kati ya Wakwe

FUJIKO, binti-mkwe mwenye udhia mkali aliyetajwa katika makala ya ufunguzi, mwishowe alimsadikisha mume wake watoke katika nyumba ya wazazi wake waingie nyingine ya hapo karibu. Lakini mambo hayakupata nafuu sana. Wakwe zake waliendelea kuingilia mambo, na huzuni yake ikabakia. Halafu siku moja mgeni alimtembelea mwanamke huyo.

Ziara hiyo ilimwanzisha Fujiko katika mwendo uliotokeza badiliko la utu, na hiyo ikaleta nafuu katika uhusiano wake na wengine. Alianza kujifunza Biblia pamoja na Mashahidi wa Yehova. Baada ya muda, mwelekeo wake ulibadilika sana hivi kwamba baba-mkwe wake akataka kuhudhuria mafunzo hayo ajionee mwenyewe ‘ni dini ya aina gani iliyokuwa imebadili sana utu wake.’

Kukitambua Kifungo Kipya

Biblia hutoa picha yenye kueleweka wazi juu ya mpango wa ndoa ya Kimaandiko. Baada ya Mungu kuumba wanadamu wawili wa kwanza na kuwaleta pamoja, alianzisha kanuni inayofuata. “Mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.” (Mwanzo 2:24) Kwa hiyo ni lazima mume na mke hao waliofunga ndoa karibuni watambue kwamba wameingia katika kifungo kipya. Ni lazima sasa washikamane wakiwa kiungo kimoja chenye kujitegemea hata ingawa huenda wakaishi pamoja na wakwe zao.

Hata hivyo, kuacha baba na mama hakumaanishi kwamba watoto wafungapo ndoa waweza kugeuzia wazazi wao kisogo na kwamba hawahitaji tena kuwastahi na kuwaheshimu. “Usimdharau mama yako akiwa mzee,” Biblia yaonya kwa upole. (Mithali 23:22) Hata hivyo, ndoa ifanywapo, huwa kuna rekebisho katika mahusiano. Maadamu kila mshiriki wa familia akumbuka hilo vizuri, hao mume na mke vijana waweza kunufaika na ujuzi na hekima ya wazazi.

Timotheo, mwanamume kijana mwenye kusifika ambaye mtume Paulo alichukua katika safari zake za kimisionari, alilelewa na mama yake Myahudi, Eunike. Hata hivyo, kwa wazi Loisi nyanya yake alishiriki pia kufanyiza maisha yake. (2 Timotheo 1:5; 3:15) Hiyo si kusema kwamba akina nyanya wana haki ya kuingilia malezi ya watoto na kuweka viwango tofauti na vile vya wazazi. Kuna njia ifaayo ambayo kile kizazi chenye umri mkubwa zaidi chaweza kusaidia kile kichanga zaidi katika kulea watoto.—Tito 2:3-5.

‘Mwanamke Aliye na Hekima Kikweli’

Ikiwa vizazi viwili vitashirikiana katika suala lenye kutatiza sana kama hilo la kulea watoto, ni lazima vyote viwili vitende kwa hekima. “Mwanamke aliye na hekima [kikweli, NW] hujenga nyumba yake,” yasema mithali ya Biblia, “bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe.” (Mithali 14:1) Mwanamke awezaje kujenga nyumba yake? Tomiko asema kwamba kuwasiliana ndiko kulimsaidia kushona uhusiano wake na binti-mkwe wake, Fujiko. “Pasipo mashauri makusudi hubatilika,” yashauri Biblia.—Mithali 15:22.

Kuwasiliana hakumaanishi kuboboka mawazo yote yaliyo katika akili yako bila kufikiria hisia za wengine. Hapa ndipo hekima huingia. “Mtu mwenye hekima atasikiliza” wasemayo wengine. Nyakati fulani huenda wakwe zako wakawa na la kusema, lakini wao wasita kueleza maoni yao. Uwe mtambuzi, na ‘uteke mawazo yao.’ Halafu ‘tafakari’ kabla hujasema.—Mithali 1:5; 15:28; 20:5, NW.

Kupima wakati ufaao kusema jambo ni kwa maana sana. “Neno linenwalo wakati wa kufaa . . . ni kama machungwa katika vyano vya fedha,” yasema mithali moja ya Biblia. (Mithali 25:11) Tokiko na binti-mkwe wake wasema kwamba wao hungoja mpaka wakati ufaao kabla ya kueleza maoni yao ambayo huenda yakamkwaruza mwingine vibaya. “Mimi hujaribu kufikiri kabla ya kuongea nitakapo kumwonyesha jambo fulani binti-mkwe wangu,” asema Tokiko. “Mimi huweka mambo hayo akilini na kuyasema akiwa na hali nzuri ya moyoni na akiwa hana njaa. Waona, ni rahisi kuudhika ukiwa na njaa.”

Mwanamke mwenye hekima atajiepusha kusema mabaya juu ya wakwe zake. “Kama sisi ni akina mama-wakwe au mabinti-wakwe, twapaswa kujua kwamba ubaya wowote tusemao juu ya upande ule mwingine, mwishowe utajulikana kwao,” asema Sumie Tanaka, mwandikaji Mjapani aliyeishi pamoja na mama-mkwe wake kwa miaka 30. Bali, yeye atetea kusema mema juu ya wakwe kwa njia iliyo au isiyo ya moja kwa moja.

Ingawa hivyo, namna gani wakwe zako wasipoitikia jitihada zako?

Uwe Mwenye Kusamehe

Mara nyingi matatizo mazito kati ya wakwe hutokana na mambo ambayo hayangesababisha tatizo kama yangefanywa au kusemwa na mtu mwingine. Madhali sisi sote ni wasiokamilika na ‘hujikwaa katika kunena,’ huenda nyakati fulani ‘tukanena bila kufikiri, kama kuchoma kwa upanga.’ (Yakobo 3:2; Mithali 12:18) Hata hivyo, ni jambo la hekima kutoudhiwa na kila neno lisemwalo bila kufikiriwa.

Wale ambao wameshinda matatizo ya kiukwe wametii shauri hili la Biblia: “Mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake.” (Wakolosai 3:13) Ni kweli, huenda isiwe rahisi kuchukuliana na wakwe zako na kuwasamehe, hasa wakati kuna kisababishi cha lalamiko. Lakini kichocheo imara cha kufanya hivyo ni uhakikisho wa kwamba kwa njia hiyo sisi tutapokea msamaha kutoka kwa Mungu mwenyewe kwa makosa yetu.—Mathayo 6:14, 15.

Hata katika mabara ya Mashariki, ambako kimapokeo watu hufuata Ubuddha, Utao, Ukonfyushasi, na Ushinto, kuna wengi ambao wamejifunza Biblia wakaja kuuthamini ukweli juu ya Muumba aliye mwingi wa fadhili. Uthamini huo umewasaidia kushinda hisia za uchungu zilizoonekana kutoshindika.

‘Upendo Haushindwi Kamwe’

Uhusiano wa kiukwe ulio na furaha wahitaji msingi hakika. Kusaidia mkwe mzee au mgonjwa kwa sababu ya kuhisi ukiwa na wajibu tu wa kufanya hivyo huwa sikuzote hakufanyizi uhusiano bora. Haruko alijifunza hilo wakati mama-mkwe wake alipokuwa akifa kwa kansa. Alitumia sehemu kubwa ya siku yake akiwa hospitalini kumtunza mama-mkwe wake, na kuongezea hilo, alitunza familia yake mwenyewe. Alikuwa chini ya mkazo mwingi sana hivi kwamba hatimaye alipoteza kiasi kingi cha nywele yake.

Siku moja alipokuwa akikata kucha za mama-mkwe wake, aliukata mmoja hadi kwenye ngozi. “Wewe hunijali kabisa!” akang’aka mama-mkwe.

Kwa kushtushwa na maneno hayo yasiyo na uthamini, Haruko alishindwa kuzuia machozi. Halafu akang’amua kwamba maneno hayo yaliumiza sana kwa sababu kila jambo alilokuwa amekuwa akimfanyia mama-mkwe wake lilikuwa kwa sababu ya kuhisi wajibu tu. Aliamua kuacha kani yenye kumotisha utumishi wake iwe ile ya upendo. (Waefeso 5:1, 2) Hiyo ilimwezesha kushinda hisia zake za maumivu na ikarudisha uhusiano pamoja na mama-mkwe wake mpaka alipokufa.

Kweli kweli, upendo kama ufafanuliwavyo katika Biblia ndio ufunguo wa kutuliza mgombano wa kifamilia. Soma yale ambayo mtume Paulo alisema juu ya jambo hilo, na uone kama hutaafikiana nayo. “Upendo huvumilia, hufadhili,” akaandika. “Upendo hauhusudu [hauna wivu, NW]; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote.” Si ajabu Paulo aliongezea hivi: “Upendo haupungui neno wakati wo wote [haushindwi kamwe, NW].” (1 Wakorintho 13:4-8) Wewe waweza kusitawishaje upendo wa jinsi hiyo?

Biblia huorodhesha “upendo” kuwa sehemu ya “tunda” la roho ya Mungu. (Wagalatia 5:22, 23, NW) Hivyo, kuongezea jitihada zako mwenyewe, yahitajiwa kuwa na roho ya Mungu ndipo usitawishe aina hii ya upendo. Zaidi ya hilo, waweza kumwomba Yehova, Mungu wa Biblia, akusaidie uongeze upendo kama wake kwenye utu wako. (1 Yohana 4:8) Bila shaka, yote haya hutaka ujifunze juu yake kwa kutalii Neno lake, Biblia. Mashahidi wa Yehova watafurahi sana kukusaidia, kama walivyosaidia Fujiko na wengine wengi.

Utumiapo yale ujifunzayo kutokana na Biblia, utapata kwamba si uhusiano wako pamoja na Mungu tu utakaopata nafuu bali pia uhusiano wako na kila mtu akuzungukaye, kutia na wakwe zako. Utapata kile ambacho Biblia hukuahidi, yaani, “amani ya Mungu, ipitayo akili zote.”—Wafilipi 4:6, 7.

Fujiko na wengine waliotajwa katika makala hizi walikuja kuona shangwe ya jinsi hiyo—nawe pia waweza. Ndiyo, kwa kutegemea Yehova Mungu na kufuata shauri la Neno lake, Biblia, wewe pia waweza kujenga na kudumisha uhusiano mchangamfu pamoja na wakwe zako.

[Sanduku katika ukurasa wa 8, 9]

Mume—Mfanya-Amani au Mvunja-Amani?

Wakati vizazi viwili au vitatu viishipo chini ya paa moja, sehemu ya mume katika kudumisha amani ya familia haipasi kukosa kuangaliwa. Kwa habari ya mume halisi ambaye huepa daraka lake, Profesa Tohru Arichi wa Chuo Kikuu cha Kyushu, mtaalamu katika ujamii wa kifamilia, aandika hivi:

“Wakati mume na mke waishipo pamoja na [mama], mama huhisi mahitaji ya mwana wake, na bila kukusudia yeye humtunza mwana wake wakati yeye mama ahisipo mahitaji hayo. Mwana hukubali utunzaji huo bila msito wowote. Kama mwana angefikiria kidogo zaidi hali ya mke wake na kufikiria kidogo zaidi jinsi mama yake angehisi kama ni yeye daraka lake la utunzaji lingalikuwa likiingiliwa, tatizo hilo lingetatuliwa. Kwa kuhuzunisha, tena mara nyingi mno, mwana huwa hang’amui hivyo.”

Basi, mume awezaje kushiriki kwa bidii katika kuleta amani katika familia yake? Mitsuharu asema kwamba utumizi wake wa kanuni za Biblia ulisaidia familia yake. “Kifungo kilicho kati ya mama na mwana wake ni imara sana hata ingawa mwana amekua akawa mtu mzima,” yeye akiri, “hivyo basi ni lazima mwana afanye jitihada yenye ufahamu ili ‘amwache baba yake na mama yake na kuambatana na mkewe.’” Yeye alitumia kanuni hiyo kwa kuzungumza pamoja na mke wake tu mambo yanayohusu kutunza watoto na kuwalea, naye hakulinganisha mke wake na mama yake katika kazi za nyumbani. “Sasa,” yeye aendelea kusema, “sisi na wazazi wangu hustahiana. Kila mmoja wetu ajua ni wapi uchukivu utatokea kwa kuingilia mambo na ni wapi msaada na ushirikiano utathaminiwa.”

Kwa kuongezea ‘kuambatana na mkewe,’ ni lazima mume awe mpatanishi kati ya mama yake na mke wake. (Mwanzo 2:24) Yeye ahitaji kuwa msikilizaji mwema na kuwaacha wamimine mioyo yao. (Mithali 20:5) Mume mmoja, ambaye amejifunza kushughulikia hali kwa busara, kwanza hutafuta kujua hisia za mke wake. Halafu yeye huongea na mama yake juu ya masuala yahusikayo, mke wake akiwapo. Kwa kujitwalia sehemu yake hivyo akiwa mfanya amani, mwana aweza kusaidia kufanyiza mahusiano yenye kupendeza nyumbani kati ya wanawake hao wawili awapendao.

[Picha katika ukurasa wa 9]

Uwe msikivu na uwasiliane

[Picha katika ukurasa wa 10]

Upendo, si hisia ya wajibu, hujenga mahusiano mazuri

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki