Ni Nini Husababisha Tatizo Hilo?
“CHUMVI nyingi mno haifai kwa familia!” yule mama ajulisha. “Lakini chakula ni dufu sana na hakina ladha!” asisitiza binti-mkwe. Yeye adokoa chumvi kidogo na kuinyunyiza ndani wakati mama ageuzapo mgongo.
Huku kila mmoja akijaribu kufanya kivyake, wote wawili wajikuta wakila mlo usioonewa shangwe na yeyote kati yao. Lakini huenda matokeo yakawa mazito zaidi ya hayo. Mzozano wa wakwe huenda ukaongoza kwenye mapambano ya kiakili na kihisia-moyo ambayo hudumu kwa miaka mingi.
Kwa watu wengi, mgongano wa aina hii huonekana kuwa usioepukika. “Hata familia ionekane kuwa ikiambatana pamoja kwa njia nzuri kama nini, pasipo shaka patakuwa na mzozano kati ya mama na binti-mkwe wake,” aandika Dakt. Shigeta Saito, mwenyekiti wa Shirika la Japani la Hospitali ya Akili. Lakini tatizo si la Mashariki tu.
Mleta-habari wa Amkeni! katika Italia aripoti kwamba “ile desturi ya kufunga ndoa na kuhamia kuishi pamoja na wazazi wa ama bibi-arusi ama bwana-arusi imesababisha matatizo katika familia nyingi, na wake wengi wachanga huteseka kwa sababu ya mwelekeo wa mama-mkwe ambao mara nyingi huwa wa kusumbua-sumbua na kusema mambo kimamlaka.”
Katika nchi za Mashariki na Magharibi pia, karatasi-habari na magazeti yana safu nyingi za ushauri wa kibinafsi zinazoshughulikia migongano ya wakwe. Basi, ni nini huenda kikasababisha matatizo?
Nani Afanye Maamuzi?
Wakati wanawake wawili washirikipo jiko moja, mara nyingi suala huwa: Nani afanye maamuzi? “Mapendezi na njia zetu zatofautiana, nami nilibabaika kila wakati kutoafikiana kulipotokea,” asema mwanamke ambaye ameishi na mama-mkwe wake kwa miaka zaidi ya 12.
“Kwa miaka kumi ya kwanza, tulipambana juu ya vijambo,” akiri binti-mkwe mwingine. Huenda hali za kutoafikiana zikatokea kuhusu mambo duni kama jinsi ya kuangika shati katika kamba ya nguo. Hata ikiwa wanawake hao hawaishi katika nyumba ile ile, huenda hali ikawa yenye matata. Mama-mkwe mwenye kuzuru ambaye atoa maneno kama, “Mwanangu hapendi nyama yake ipikwe hivi,” huenda akatokeza hisia chungu muda wa maisha yote. Yote hayo yaonyesha kwamba tatizo hasa huwa ni kuamua nani afanye maamuzi gani na ayafanye kwa ajili ya nani.
Akielekeza kwenye suala hili, Takako Sodei, profesa msaidizi kwenye Chuo Kikuu cha Wanawake cha Ochanomizu kuhusiana na upambaji wa nyumbani asema hivi: “Kama mtu aishi pamoja na mwana au binti-mkwe au binti na mwana-mkwe, haiwezekani jamaa iruzuku wake wawili wenye kushindania udhibiti. Yahitajiwa kabisa kuwa na makao yaliyotengana au kurekebisha hali na kuacha mmoja awe ndiye mpambaji nyumba na yule mwingine mpambaji-nyumba-mdogo.” Ni lazima vizazi hivyo viwili vifikie mwafaka wa kiasi wenye kutegemea hali ya kimwili na ya kiakili ya aliye na umri mkubwa zaidi na ya ujuzi, au ukosefu wa ujuzi, wa aliye mchanga zaidi.
Lile Jambo la Faragha
Vizazi viwili au zaidi viishipo katika makao yale yale, ni lazima washiriki wa familia wadhabihu faragha yao kwa kadiri fulani. Hata hivyo, katika jambo hili kila mshiriki ataelekea kuwa na maoni tofauti. Huenda mume na mke wachanga wakawa na hamu sana ya faragha nyingi zaidi, hali walio wazee-wazee huenda wakaona kiu ya uandamani mwingi zaidi.
Kwa kielelezo, binti-mkwe anayeishi karibu na Tokyo alihisi kwamba mama-mkwe wake alivamia faragha yake na mumeye. Jinsi gani? Kwa kuziondoa nje nguo zake na za mumeye, kuzikunja, na kuziweka mahali pazipasapo. Yeye hakuona ikifaa mama-mkwe wake awafanyie mambo haya ya kibinafsi. Kwa upande mwingine, mama-mkwe wake, Tokiko, alisononeka wakati binti-mkwe wake, kwa kuweka nyumba katika hali maridadi, alitupa vitu ambavyo Tokiko alikuwa amevithamini sana kwa miaka mingi.
Uvamizi wa kuingilia faragha waweza kupita kiasi. Tom na mke wake, ambao waliomtunza mama mzee-mzee wa Tom, walifadhaishwa na kujidukiza-dukiza kwake usiku wa manane katika chumba chao cha kulala. Sababu yake? “Nilitaka kuona kama Tom yuko sawa,” akasema mama huyo. Tatizo hilo halikutatuliwa mpaka wakahamia nyumba yenye sakafu ya chini na ya ghorofani na mama huyo akakatazwa kuja kupanda juu.
Ingawa hivyo, katika familia nyingi matatizo huzidi wakati kizazi cha tatu kitokeapo.
Kushughulika na Watoto
Siku hizi, ni kawaida kwa mama kijana kutafuta ushauri wa kulea watoto katika vitabu mbalimbali. Kwa upande mwingine, nyanya, akiwa na ujuzi wake wa miaka mingi katika kulea watoto, huhisi kiasili kwamba yeye ndiye astahiliye kutoa ushauri. Hata hivyo, mara nyingi ushauri huo huonwa kuwa uchambuzi, na mgongano hutokea.
Takako alilazimika kushughulika na tatizo hili alipomtia nidhamu mwana wake mchanga. Mama na nyanya ya mume wake walienda mbio ndani ya chumba chake kumwachisha, wakipiga kelele hata kuliko mtoto huyo mwenye kulia. Kwa kuhisi ameogofywa, Takako aliacha kumtia nidhamu mwana wake. Baadaye, kwa kung’amua umaana wa kuandaa nidhamu, aliamua kurudia mazoezi hayo.—Mithali 23:13; Waebrania 12:11.
Mama mmoja aishiye katika Yokohama aling’ang’ana pia na mama-mkwe wake baada ya watoto kuzaliwa. Mama huyo aliudhika kwamba nyanya aliwapa watoto vionjo-onjo kati ya nyakati za kula hivi kwamba walikuwa wameshiba mno wasiweze kula vyakula vyao.
Akieleza juu ya tatizo hili, Dakt. Saito asema hivi: “[Akina babu na nyanya] huwapa wajukuu wao peremende na uhuru mwingi. Wao hukubalia matakwa ya ubinafsi ya watoto. Kwa ufupi, wao huharibu wajukuu wao bila kikomo.” Yeye ashauri kwamba mama vijana waeleze wazi kwamba hawatawaachia hata kidogo nafasi za kulea watoto.
Kushindania Kuonyeshwa Shauku
Katika mgongano huu kati ya mama-wakwe na mabinti-wakwe, kuna jambo fulani la kutotumia akili vizuri. “Kisaikolojia,” aeleza Dakt. Saito, “mama huhisi kwamba binti-mkwe wake amempokonya yeye mwanaye. Bila shaka, yeye hasemi wazo hilo kwa maneno, kwa kuwa ni utoto mno kufanya hivyo. Lakini, katika fikira ya ndani, wazo la kunyang’anywa shauku ya mwana wake lina mizizi ya kina kirefu ndani yake.” Tokeo huwa ni uhusiano wenye mgogoro, ikiwa si ushindani mkali wa moja kwa moja kati yao wawili.
Elekeo hili laonekana kuwa likizidi kwa kadiri ukubwa wa familia upunguavyo. Kukiwa na watoto wachache zaidi wa kutunza, mama huhisi ukaribu zaidi kwa mwanaye. Baada ya miaka mingi ya kuishi pamoja na mwanaye, mama huwa ajua sana mambo yampendezayo na yasiyompendeza. Ingawa bibi-arusi mpya ana hamu nyingi ya kumpendeza mume wake, hana maarifa haya ya kindani, angalau pale mwanzoni. Kwa hiyo huenda roho ya ushindani ikasitawi kwa urahisi, huku mama na binti-mkwe wakishindania kuonyeshwa shauku za mwanamume yule yule mmoja.
Badiliko Lenye Msiba
Katika siku za zamani katika Japani chini ya falsafa ya Konfyushasi, wakati migongano kama hiyo ya kifamilia ilipotukia, binti-mkwe alifukuzwa—kutalikiwa. Huo ukawa ndio mwisho wa jambo hilo. Hata hivyo, leo hali hiyo iko tofauti.
Tangu Vita ya Ulimwengu 2, kizazi cha walio wachanga kimechukua udhibiti wa gharama za familia, na kizazi cha wenye umri mkubwa zaidi kinapoteza uvutano na mamlaka yacho. Kidato kwa kidato, hali imebadilika. Sasa wazazi wazee-wazee wanaachwa peke yao katika hospitali na makao ya utunzaji. Ni msiba kama nini kuona shida hii katika jamii ambamo ilikuwa kawaida kuwastahi wazee-wazee!
Elekeo la kuwatupa wazee-wazee laweza kugeuzwaje? Je! kuna njia yoyote kwa wanawake wawili kukaa pamoja kwa amani chini ya paa ile ile?
[Picha katika ukurasa wa 7]
Mwafaka wa kiasi ni lazima ufikiwe juu ya mwenye kufanya maamuzi