Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g91 10/8 kur. 16-21
  • Utunzaji wa Wazee-Wazee Tatizo Lenye Kukua

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Utunzaji wa Wazee-Wazee Tatizo Lenye Kukua
  • Amkeni!—1991
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Juhudi ya Kipekee Kutunza Walio Wako
  • Wakati Makao ya Utunzaji Yanapohitajiwa
  • “Wajibu Mzima wa Mwanadamu”
  • Wako Peke Yao Lakini Hawajasahauliwa
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2008
  • Familia ya Kikristo Huwasaidia Wazee-Wazee
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1993
  • Ni Daraka la Kikristo Kuwatunza Walio Wazee
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2004
  • Kuwaheshimu Wazazi Wetu Wazee-Wazee
    Siri ya Furaha ya Familia
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1991
g91 10/8 kur. 16-21

Utunzaji wa Wazee-Wazee Tatizo Lenye Kukua

HADITHI hii husemwa juu ya msichana mdogo aliyeuliza mama yake: “Kwa nini nyanya hula kwa kutumia bakuli ya mbao lakini sisi wengine wote hula kwa kutumia sahani zetu nzuri?” Mama yake akaeleza: “Mikono ya mama ni yenye kutetemeka-tetemeka na huenda akaangusha sahani zetu nzuri na kuzipasua, kwa hiyo yeye hutumia bakuli ya mbao badala yake.” Baada ya kufikiria jambo hilo kwa muda, yule msichana mdogo akauliza: “Basi utanihifadhia bakuli hiyo ya mbao ili uitumie nitakapokuwa mkubwa?” Mwono huu wa mambo yatakayokuja labda ulimshtua mama, hata kumbabaisha kidogo. Lakini alipowaza, labda ilimpa uhakika—msichana wake mdogo alikuwa anapanga kumtunza!

Mataraja ya wengi walio wazee-wazee si maangavu sana. Wao wamekuwa sehemu ya idadi ya watu yenye kukua kwa haraka sana katika sehemu nyingi za dunia. World Press Review la Agosti 1987 liliripoti kwamba watu milioni 600, asilimia 12 ya idadi ya watu duniani katika wakari huo, walikuwa na umri wa zaidi ya miaka 60 wakati huo.

Katika United States, watu wazee-wazee wanapita idadi ya matineja kwa mara ya kwanza kabisa. Mhariri wa sayansi wa gazeti moja la New York City aliripoti: “Waamerika milioni 30 sasa wana umri wa miaka 65 au zaidi—mmoja katika kila wanne wetu, zaidi ya wakati mwingine wowote, na: Idadi ya watu walio wazee inakua mara mbili zaidi ya idadi ya watu wale wengine . . . wastani wa mataraja ya urefu wa maisha ya Waamerika yalikuwa miaka 35 katika 1786. Kwa mtoto wa Kiamerika aliyezaliwa katika 1989, ni miaka 75.”

Katika Kanada idadi ya walio wazee-wazee kabisa, wa miaka 85 na zaidi, inatarajiwa iongezeke kwa mara tatu kufika mwisho wa karne hii.

Katika Ulaya miaka mia moja iliyopita, watu wazee-wazee walifanyiza asilimia 1 tu ya idadi yote ya watu. Leo idadi zao zimepanda kufika asilimia 17.

Ripoti moja kutoka kwa ofisi ya hesabu ya watu ya U.S. juu ya “Uzee katika nchi za ulimwengu wa tatu” ilisema. “Ongezeko la nne kwa tano ya watu wazee-wazee linatokea katika nchi za ulimwengu wa tatu.”

Miongo minne iliyopita matarajio ya urefu wa maisha ya watu wa Kichina yalikuwa kama miaka 35. Kufikia 1982, tarakimu hiyo iliruka ikafikia miaka 68. Leo, zaidi ya Wachina milioni 90 wanahesabiwa kuwa wazee, na inakadiriwa kwamba kufikia mwisho wa karne hii, tarakimu hiyo itapanda kufikia milioni 130, au asilimia 11 ya idadi ya watu.

Juhudi ya Kipekee Kutunza Walio Wako

Kadiri tarakimu ya walio wazee-wazee inavyoongezeka duniani pote, swali lenye kutatanisha juu ya jinsi ya kuwatunza linakuwa lenye umaana sana. Katika nyakati za Biblia tatizo hilo halikuwa gumu hivyo. Walikuwa na familia zenye kuenea, ambapo watoto, wazazi, na babu na nyanya waliishi pamoja. Watoto na akina babu walichanganyika kukiwa na faida kwa kila mmoja, na wazazi wangeandaa mahitaji ya kimwili na waone kwamba utunzaji wowote wa kipekee uliohitajiwa na walio wazee katika nyumba ile ulifanywa upatikane. Familia kama hizo zenye kuenea zikiwa na utunzaji wa walio wazee bado ndio mtindo katika nchi fulani leo. (Kwa mfano, tafadhali ona sanduku lililo katika ukurasa wa 8.) Lakini hali si hiyo katika nchi zenye usitawi ambako duara ya familia inakuwa tu na wazazi na watoto. Wakati watoto wakuapo wakubwa na kuoa na kupata watoto wao wenyewe, mara nyingi wanapatwa na tatizo la kutunza wazazi wao ambao huwa wazee, wadhaifu, na mara nyingi wenye magonjwa ya kudumu.

Katika mfumo wa mambo huu wa sasa, kufanya hivyo kunaweza kuwa tatizo kubwa kweli kweli! Kwa jinsi isivyotamanika, chini ya hali za kiuchumi za leo, huenda ikawa lazima kwa wazazi wote kufanya kazi. Chakula ni ghali, kodi za nyumba ziko juu, hesabu ya vitakavyolipwa inaingia. Hata mishahara miwili inaweza kutoweka upesi. Ikiwa mwanamke wa nyumba hafanyi kazi nje, anaweza kuwa mwenye shughuli na watoto, ununuzi, usafi—wenyewe ukiwa kazi ya wakati wote. Hiyo si kusema kwamba mzazi mzee au wazazi, hawapaswi kutunzwa nyumbani. Kile kinachosemwa ni kwamba unaweza kuwa ni mgawo mgumu. Wazee wana maumivu yao, na taabu yao, na kwa uelewevu wakati mwingine wanaweza kulalamika na kuwa wenye kasirani, si wenye kupendeza wakati wote na wenye furaha. Hakuna yoyote ya haya yanayodokeza kwamba juhudi yenye bidii haipasi kufanywa ili kutunza mzazi mzee nyumbani.

Mara nyingi, jukumu linakalia mabegani mwa mabinti waliosalia. Uchunguzi baada ya uchunguzi umefunua kwamba ingawa wanaume huenda wakatoa msaada wa kifedha, kwa msingi ni wanawake huwa wanapeana utunzi wa kibinafsi kwa mikono. Wao hupika vyakula kwa ajili ya wazee—mara nyingi wakiwalisha kwa kijiko—wanawaosha na kuwavisha, wanawabadili mavazi, wanawapeleka kwa madaktari na hospitali, wanaona kwamba wamepata dawa zao. Mara nyingi wao ndio macho, masikio, na akili ya wazazi wao wazee. Kazi yao ni kubwa kweli kweli, na hiari yao ya kuifanya yajapokuwa magumu yake kweli kweli ni yenye sifa na kupendeza kwa Yehova Mungu.

Lile wazo kwamba watoto wengi wakubwa hupeleka wazazi wao wazee kwenye makao ya utunzaji watumie miaka yao inayopungua humo si la kweli, kulingana na Carl Eisdorfer, M.D., Ph.D., mkurugenzi wa Kitovu cha Ukuzi na Kuzeeka katika Chuo Kikuu cha Miami, Florida, U.S.A. “Uchunguzi mbalimbali umeonyesha kwamba utunzaji mwingi kwa wazee-wazee unaandaliwa na familia zao wenyewe,” yeye akasema.

Tarakimu zinaunga mkono dai lake. Katika United States, kwa mfano, asilimia 75 ya wale walionakiliwa walisema kwamba wangetaka wazazi wao, kama hawawezi tena kuishi peke yao, waishi nao. “Hii inathibitisha kwamba familia zinataka kutunza walio wao,” akasema Dkt. Eisdorfer. Na ripoti kutoka katika gazeti Ms. ilisema: “Ni asilimia 5 tu pekee yake ya wale wenye umri ya miaka zaidi ya 65 walio katika makao ya utunzaji katika wakati wowote ule kwa sababu wazee hao na watu wao wa ukoo wanapendelea utunzaji wa nyumbani kuliko ule wa makao ya utunzaji.

Kisa kinachofuata kinaonyesha jinsi wengine wanavyoweka jitihada katika kutunza mzazi aliye mzee. Ripoti hiyo imetoka kwa mwakilishi anyezuru wa Mashahidi wa Yehova anayetembelea makundi kotekote United States. Alieleza jinsi yeye na mke wake walivyoazimia kubaki wakiwa na mama yake mwenye umri wa miaka 83 kuliko kumweka katika makao ya utunzaji. “Mimi nilikumbuka msemo,” akasema, “kwamba mama mmoja angeweza kutunza watoto 11, lakini watoto 11 hawangeweza kutunza mama mmoja. Basi, sisi wawili tuliazimia kutunza mama mmoja mzee. Ingawa alikuwa katika kipindi cha mapema cha ugonjwa wa mfumo wa neva, alisafiri nasi katika trela.

“Mwanzoni alienda nasi tulipokuwa tukihubiri juu ya ujumbe wa ufalme mlango kwa mlango. Baadaye tulilazimika kumchukua kwa kigari cha kusukuma. Wenye nyumba walionekana kama wanathamini jinsi tulivyomtunza. Wakati mwingine angesema mambo ambayo hayakuwa sawa, lakini hatukumtia aibu kwa kumsahihisha. Bado yeye, hata hivyo, alikuwa mwenye ucheshi. Tulimtunza mpaka akafa, akiwa na umri wa miaka 90.

Wakati Makao ya Utunzaji Yanapohitajiwa

Karibu watu milioni 2 wazee-wazee wanaishi katika makao ya utunzaji katika United States. Katika hali nyingi, hata hivyo, si kule “kufungiwa kwa wazee ndani ya bohari bila huruma,” kama ambavyo wengine wamekuita kule kuweka kwao katika makao ya utunzaji. Bali, mara nyingi ndiyo njia pekee ya utunzaji wa kutosha kwa wale wasioweza kujitunza wenyewe. Katika hali nyingi, watoto wa wazazi wazee hawako katika hali ya kuwatunza wazazi wao, ambao wengi wao huenda wakawa wanaugua sana kwa ugonjwa wa neva au wamo kitandani kwa sababu ya ugonjwa mwingineo wenye kudhoofisha ambao wahitaji utunzaji wa kipekee wa saa zote. Katika hali kama hizo makao ya utunzaji huenda yakawa ndio tu sehemu inayoweza kutoa utunzaji huu wa mahitaji ya kipekee.

Mmisionari mmoja wa Watch Tower Society katika Sierra Leone, Afrika, alieleza juu ya uchungu mama yake aliona wakati alilazimika kumweka mamaye katika makao ya utunzaji: “Hivi majuzi mama yangu ambaye yuko Florida alimweka mama yake, Helen, katika makao ya utunzaji. Ulikuwa uamuzi ulio mzito sana kwake. Alikuwa amemtunza Helen kwa miaka minne, lakini sasa Helen alihitaji utunzaji wa wakati wote. Rafiki za mama yangu, familia, na wafanya kazi fulani wa kijamii na madaktari, wote waliunga mkono uamuzi wa kumweka Helen katika makao ya utunzaji, lakini bado ulikuwa ni uamuzi mgumu sana kufanya. Mama yangu alihisi kwamba kwa sababu mama yake alikuwa amemtunza yeye akiwa mtoto, sasa ilikuwa sawa kabisa kumtunza mama yake katika uzee wake—yale ‘malipo’ ambayo mtume Paulo alikuwa ameyazungumzia. Kama ilivyokuwa, hata hivyo, Helen alitunzwa vizuri zaidi katika makao ya utunzaji kuliko vile angetunzwa katika nyumba ya mama yangu.—1 Timotheo 5:4.

Shahidi mwingine, anayefanya kazi katika makao makuu ya Mashahidi wa Yehova, alieleza juu ya shindano la baba yake na kansa. “Baba yangu alikuwa shahidi mwenye bidii kwa miaka zaidi ya 30. Kwa miaka tisa ya mwisho ya maisha yake, alikuwa na kansa. Mke wangu nami tulitumia likizo zetu pamoja naye na tukachukua likizo ndefu ili kuwa pamoja naye na kusaidia. Watu wa ukoo wengine walisaidia katika njia tofauti-tofauti. Lakini mwingi wa wakati huo, alitunzwa na mke wake na binti aliyeolewa aliyeishi katika ujirani. Pia alipata kutembelewa na washiriki wa kundi la Mashahidi alilokuwa ameshirikiana nalo. Miaka miwili ya mwisho, alikuwa anatembelea-tembelea hospitali, na alitumia miezi ya mwisho mitano katika makao ya utunzaji ambapo angepata utunzaji wa kipekee aliyohitaji.

“Uamuzi wa kumtoa nyumbani na kumpeleka kwa makao hayo ulikuwa wa kifamilia, yeye akishiriki. Aliamua kwamba utunzaji wake ulikuwa unakuwa mgumu zaidi, hata usiowezekana, kwa familia iliyokuwa nyumbani. ‘Itawauwa nyinyi nyote!’ akasema kwa nguvu. ‘Sasa ndio wakati wa kuenda kwenye makao hayo ya utunzaji. Vema kwenu vema kwangu.’

“Hivyo alienda. Kwa sehemu kubwa ya miaka tisa, familia ilikuwa imemtunza, na likiwa suluhisho la mwisho tu lililo baki ndipo tu alipoenda kwenye makao ya mweneo wa utunzi ili apate utunzi wa kipekee wa wakati wote aliyohitaji.”

Wakati, makao ya utunzaji yanapohitajiwa yakiwa suluhisho la mwisho kwa ajili ya utunzaji unaofaa, familia inapaswa kutafuta moja ambayo ni safi na yenye watunzaji wenye uwezo na wema. Kama inawezekana, panga kuwe na mwenye kumtembelea kila siku—mshiriki wa familia, mtu fulani kutoka kwenye kundi, angalau simu—ili kwamba mtu huyo mzee asihisi ameachwa, amesahauliwa, peke yake kabisa, na kufikiri kwamba hakuna anayejali. Wakati wengine katika makao hayo wanapotembelewa, na hakuna yeyote anayemtembelea mpendwa wenu—hilo laweza kuwa lenye kuvunja moyo sana. Hivyo jaribu kumwona mtu huyo kwa ukawaida. Tembelea mahali pamoja naye. Msikilize. Sali pamoja naye. Jambo hilo la mwisho ni la maana sana. Hata akiwa katika hali ya kuzirai, sali tu. Huwezi kujua ni kadiri gani anaweza kuwa anasikia jambo!

Wakati wa kufanya maamuzi kuhusu wazazi, jaribu kufanya hivyo pamoja nao badala ya kwa ajili yao. Waache wahisi kwamba bado wana uwezo juu ya maisha yao. Toa usaidizi unaohitajiwa kwa upendo wote na ustahimilivu wote pamoja na uelewevu kwa kadiri iwezekanavyo. Wakati huo ndio wa kulipa, kama matume Paulo alivyoandika, kile tunachowia wazazi wetu na wazazi wa wazazi wetu.

“Wajibu Mzima wa Mwanadamu”

Katika pirika pirika za ulimwengu wa leo, ni rahisi kwa walio wazee kusukumwa nyuma katika maisha. Sana sana, wachanga ambo ndio tu wanaingia kwenye mbio na wenye haraka kuendeleza maisha zao kufikiri kwamba wazee-wazee ni kizuizi, kwamba sasa hawana umaana wowote. Labda sisi sote tunapaswa kukomea hapo na kujiuliza: Ni nini hustahilisha uhai kuwa wa maana hata hivyo? Ni rahisi kwa walio wachanga kupunguza thamani ya wazee-wazee na kujiwekea thamani ya juu.

Hata hivyo, si watu wazee au wanyonge pekee, ambao huenda wakatoa mchango kidogo au wakakosa kutoa kwa kile ambacho huonekana kuwa cha maana. Mfalme Sulemani katika kitabu cha Mhubiri mara nyingi alirejezea matendo mengi ya watu kwa kawaida kuwa ubatili. Alizungumza juu ya vijana na nguvu zao za muda na akaonyesha jinsi kupita kwa miaka kungeumbua miili yao kama ambavyo kumefanya miili ya mamilioni wengine. Wote wanaisha wakiwa mavumbi na wanastahili kadirio hili: “Ubatili mtupu”! akasema Sulemani. “Mambo yote ni ubatili!”—Mhubiri 12:8.

Lakini yeye alisifu maneno ya wenye hekima na akajumlisha uchunguzi wake wa uhai kwa maneno haya: “Hii ndiyo jumla ya maneno; yote yamekwisha sikiwa; Mche Mungu, nawe uzishike amri zake, Maana kwa jumla ndiyo impasayo [wajibu mzima wa, NW] mtu. (Mhubiri 12:13) Hiyo ndiyo kanuni kwa maisha yenye maana, si jinsi ulivyo mchanga au mzee au ni jina gani wajifanyia katika ulimwengu huu wa anasa ambao unapitilia mbali.

Ili kuongoza mahusiano yetu ya kibinadamu, Yesu alitoa kanuni ya kuongoza ambayo imekuja kuitwa kanuni ya kidhahabu: “Nyakati zote tenda wengine jinsi ungetaka wengine wakutendee.” (Mathayo 7:12, The New English Bible) Ili kutumia kanuni hiyo, ni lazima tuweze kujiweka katika hali ya mtu yule mwingine, ili kuona jinsi tungetaka tutendewe kama tungekuwa katika hali yake. Kama tungekuwa wazee na wanyonge na katika uhitaji wa msaada, sisi tungependa tutendeweje na mmoja wa watoto wetu? Je! tutawalipa wazazi wetu kwa utunzaji wa miaka 20 na utegemezo waliotupa kwa wingi tulipokuwa hatuwezi kitu kama watoto kwa kuwatunza sasa wakati hawajiwezi katika umri wao wa uzee?

Tunapotazama wazazi wetu wazee katika uhitaji wao, labda tukifikiria utoto wetu na kukumbuka yote waliotufanyia tulipokuwa wachanga, watoto, tukitunzwa tulipokuwa wagonjwa, tukapewa chakula na kuvishwa nao, tukapelekwa nao kwenye tafrija zilizotupendeza sana. Halafu, kwa hangaiko la upendo kwa ajili ya hali njema yao, fikiria kilicho bora zaidi katika kutoa mahitaji yao.

Hiyo inaweza kuwa kufanya mipango inayohitajiwa kuwaweka nyumbani ikiwezekana. Kwa upande mwingine, mpango ulio bora kwa wote wanaohusika, kutia na wazazi wazee, ungekuwa ni makao ya utunzaji uliyoenea au ya uuguzi. Uamuzi wowote unaofanywa, unapaswa uheshimiwe na wengine. Kama ambavyo tunaambiwa: “Mbona wamhukumu ndugu yako? au wewe je! mbona wamdharau ndugu yako?” Na tena: “U nani wewe umhukumuye mtu mwingine?”—Warumi 14:10; Yakobo 4:12.

Chochote kile kiwezacho kufanikiwa katika kutunza wazazi wazee, kama wakiishi na watoto wao au katika makao ya utunzaji, ikiwa bado wana uwezo wao wa kufikiri, bado huenda wakawa na maisha yenye maana. Wanaweza kujifunza juu ya makusudi ya Yehova kwa ainabinadamu yote tiifu kuishi milele katika afya juu ya dunia-paradiso. Wanaweza kupata kazi-maisha mpya, yenye furaha na kuridhisha ya kumtumikia Muumba wao Yehova Mungu. Huu basi unakuwa wakati wenye kusudi zaidi na wenye furaha katika maisha zao. Wengine katika miaka yao iliyosonga, wakati ambapo wengine wamechoka na uhai wenyewe, wamekuja kujua juu ya ahadi za Yehova za uhai wa milele katika ulimwengu mpya wenye haki usio na mwisho na wamepata furaha mpya katika kuzungumza na wengine juu ya tumaini hilo.

Kwa kumalizia na kisa cha maana. Mwanamke mmoja kutoka Kalifornia, katika umri wa miaka 100, alijulishwa juu ya baraka hizi zilizoahidiwa, na muuguzi mmoja wa kike katika makao ya utunzaji, na katika umri wa ukomavu wa 102, alibatizwa akiwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova. Alimaliza maisha yake, si katika ‘ubatili wa ubatili’ wa mwisho kabisa, bali kwa kutimiza ‘wajibu wake mzima wa uhai,’ yaani, ‘kumcha Mungu na kushika amri zake.’

[Blabu katika ukurasa wa 18]

Imesemwa kwamba miaka mingi iliyopita mama mmoja angetunza watoto 11; sasa watoto 11 hawawezi kumtunza mama mmoja

[Sanduku katika ukurasa wa 20]

Kuonyesha Heshima kwa Kutunza Walio Wazee Wazee—Maelezo Kutoka Sehemu Mbalimbali za Ulimwengu

“Katika Afrika kuna maandalizi machache sana ya kiserikali au hata hakuna yoyote kwa ajili ya wazee wazee—hakuna makao ya utunzaji, utunzaji wa kutumia dawa au faida za Amana ya Kijamii, hakuna ujira. Watu wazee wanatunzwa na watoto wao.

“Sababu moja ya msingi kwa nini kuzaa watoto huwa jambo la maana kwa watu katika nchi zinazoendelea ni kwamba watoto wao watawatunza katika wakati ujao. Hata watu maskini watazaa watoto wengi, wakisababu kwamba kwa kadiri wanavyokuwa na wengi, ndivyo kulivyo na nafasi kwamba wengine hawatakufa na watawatunza.

“Ingawa viwango vinabadilika katika Afrika, kwa sehemu kubwa, familia zinachukua daraka la kutunza wazazi wao kwa uzito. Ikiwa hakuna watoto, washiriki wengine wa familia watawatunza. Mara nyingi wale wanaotoa utunzi wako katika hali dhaifu kifedha, lakini wanagawa kile walicho nacho.

“Njia nyingine ambayo watoto huwatunza wazazi wao ni kuwakopesha watoto wao wenyewe. Mara nyingi ni wajukuu ndio hufanya kazi nyumbani.

“Katika nchi zilizositawi, watu huishi muda mrefu kwa sababu ya maendeleo ya kitiba. Hali si hiyo katika nchi zinazositawi. Watu maskini hufa kwa sababu hawawezi kulipia gharama za msaada mdogo wa kitiba unaopatikana. Mithali moja inayosemwa katika Sierra Leone ni: ‘Hakuna mtu maskini aliye mgonjwa.’ Yaani, kwa sababu mtu maskini hana pesa za kulipia matibabu, yeye ama yuko mzima au amekufa.”—Robert Landis, mmisionari katika Afrika.

“Katika Meksiko watu wana heshima kubwa kwa wazazi wazee. Wazazi huishi peke yao katika nyumba zao wakati watoto wao wanapooa, lakini wazazi wao wanapozeeka na kuwa na uhitaji, watoto hoa wanawachukua katika nyumba zao na kuwatunza. Wao huhisi kwamba huu ni wajibu.

“Ni jambo la kawaida kuona babu na nyanya wakiishi katika nyumba ile ile pamoja na watoto wao na wajukuu. Wajukuu huwapenda na kuwaheshimu babu na nyanya zao. Familia iko karibu sana.

“Katika Meksiko makao ya wazee ni machache kwa sababu wana na mabinti hutunza walio wazee. Kama kuna wana kadhaa, wakati mwingine yule anayeoa mwisho anakaa nyumbani na kuishi na wazazi.”—Isha Aleman, kutoka Meksiko.

“Katika Korea sisi hufunzwa nyumbani na shuleni kuwaheshimu wazee. Katika familia yule mwana wa kwanza anapaswa awatunze wazazi wake wazee. Kama hawezi kuwategemeza, mwana mwingine au binti atafanya hivyo. Wenzi wengi wa ndoa huishi pamoja na wazazi wao wazee na kuwatunza. Wazazi hutarajia kuishi na watoto wao, na wao hupenda kuwaagiza na kutunza wajukuu wao. Huonwa kuwa jambo la aibu kwa wenzi wa ndoa wachanga kupeleka wazazi wao wazee kwenye makao ya utunzaji.

“Baba yangu ndiye aliyekuwa mvulana wa kwanza, na tuliishi na babu na nyanya zetu katika nyumba ile ile. Wakati wowote tulipoondoka nyumbani, tuliwajulisha mahali tulipokuwa tunaenda na wakati ambao tungerudi. Tuliporudi nyumbani, kwanza tulipitia kwenye chumba chao na kuwasalimu vichwa vyetu vikiwa vimeinamishwa chini na kuwajulisha kwamba tumerudi kwa sababu walihangaishwa na hali njema ya familia nzima.

“Tulipowapa kitu fulani, tulishika kitu hicho kwa mikono miwili. Ni jambo la kukosa staha kupitisha kitu kwa mkono mmoja kwa watu wa kuheshimiwa, kama vile wazazi, babu na nyanya, waalimu, au maofisa wa ngazi za juu wa utumishi wa umma. Tulipokuwa na chakula cha kipekee, tulipakulia babu zetu kwanza.

“Heshima kwa wazee haitolewi kwa washirika wa familia pekee lakini huenea kwa wazee wote. Kutoka shule ya msingi mpaka sekondari, kuna mafunzo ya maadili. Wakati wa kipindi hicho, tulijifunza kupitia hadhithi za kutungwa au hotuba jinsi ya kuheshimu na kustahi walio wazee.

“Wakati mtu mzee aingiapo chumba fulani, walio wachanga wanatazamiwa kusimama. Ikiwa aliye mchanga amekaa kwenye basi na mwanamume au mwanamke mzee anakosa kiti, basi ni jambo la kawaida kwa mchanga yule kupeana kiti chake. Kama mtu mzee anabeba inayoonekana kuwa sanduku nzito, unasimama kuuliza kama anahitaji msaada au la. Kama anasema ndiyo, unambebea sanduku lake mpaka mahali anakoenda.

“Kama vile Biblia ilivyotabiri, katika hizi siku za mwisho za mfumo wa mambo, kiwango cha adili kingezoroteka siku kwa siku. Korea haijaepuka mvuto huo. Bado, mwelekeo huu wa kuheshimu wazee unabaki kwenye mioyo ya Wakorea wengi.” (2 Timotheo 3:1-5)—Kay Kim, kutoka Korea.

[Picha katika ukurasa wa 19]

Kutembelea wazee-wazee ni muda unaotumiwa vema

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki