Uchafuzi—Nani Huusababisha?
“KISIWA hiki ni mali ya serikali inayofanyiwa majaribio. Ardhi imechafuliwa kwa [ugonjwa wa] kimeta na ni hatari. Kutua ardhini kumekatazwa.”a Ishara hii iliyoangikwa katika bara la Uskochi upande mkabala wa Kisiwa Gruinard huwaonya watakao kukizuru wasifanye hivyo. Kwa miaka 47 iliyopita, tangu kuwe na mlipuko wa kujaribia silaha za kutumia viini hatari wakati wa vita ya ulimwengu ya pili, kisiwa hicho chenye upendezi kimechafuliwa na viini vya kimeta.
Kisiwa Gruinard ni kielelezo cha uchafuzi wa kupita kiasi. Lakini namna fulani za uchafuzi wa ardhi wa kadiri ndogo ni tatizo lililoenea kote na lenye kuongezeka.
Uchafuzi wa Ardhi Waongezeka
Kisababishi kimoja cha huu uchafuzi wa ardhi ni takataka. Kwa kielelezo, familia ya wastani ya Kiingereza ya washirika wanne, kulingana na The Times la London, hutupa kilo 51 za metali na kilo 41 za plastiki kila mwaka, “ambazo sehemu kubwa itazidi kuharibu sura ya barabara, kando za barabara, fuo na maeneo ya starehe.”
Gazeti la Kifaransa GEO liliripoti kwamba mahali pakubwa sana pa kutupia takataka huko Entressen nje ya Marseilles, Ufaransa, palirundamana pakafikia kimo cha meta 60 na kuvutia shakwe (ndege) 145,000. Kuweka ua wa waya yenye kuzungukia mahali hapo pa takataka hakukuzuia upepo usipeperushe karatasi na vifusi vya plastiki. Tokeo ni kwamba, wenye mamlaka wa huko walinunua kufikia hektari 30 za ardhi ya ukulima hapo kando kwa jaribio la kuzuia tatizo hilo la takataka.
Si ajabu sana kwamba katika kupanga mambo ya Mwaka wa Mazingira ya Ulaya—uliomalizika katika Machi 1988—Stanley Clinton Davis Kamishina wa EEC aliiona orodha ya matata ya uchafuzi kuwa “isiyo na mipaka.”b Hivyo basi, kampeni ilipangwa ya kutia moyo kutumia upya takataka kwa lengo la kufanya asilimia 80 ya zile tani 2,200,000,000 za takataka za Jumuiya kila mwaka zitumiwe kwa mafaa mengine.
Uchafuzi wenye kuletwa na takataka si kwa vyovyote wa Ulaya Magharibi tu. Sasa ni wa tufe lote. Kulingana na gazeti New Scientist, hata kumekuwa na uhitaji wa kusafisha lile bara la mbali la Antarctica. Wanasayansi watafiti wa Australia walikusanya zaidi ya tani 40 za visehemu vya mashine vilivyotupwa na vifaa vya kujengea vilivyokuwa vimetapakaa karibu na kituo chao. The New York Times (Desemba 19, 1989) laripoti kwamba Waamerika kwenye Kituo cha McMurdo, Antarctica, wanasafisha takataka ambazo zimerundamana kwa miaka 30, kutia na tingatinga ya kilo 35,000 iliyozama kina cha meta 24 katika maji.
Ndiyo, katika nchi kavu, uchafuzi na utiaji taka ni mwingi. Lakini namna gani maji ya dunia?
Maji Machafu—Hayafai kwa Uhai
“Mito ya Uingereza inakuwa michafu zaidi kwa mara ya kwanza katika muda wa zaidi ya robo karne,” likasema The Observer. “Kattegat [bahari iliyo kati ya Sweden na Denmark] inakufa. Kwa haraka sana inakuwa isiyoweza kutegemeza uhai wa samaki kwa sababu imechafuzwa sana na kumalizwa oksijeni,” liliripoti The Times la London. “Mito ya Poland inakuwa upesi-upesi mahali pa kutupia vinyesi na ni maendeleo kidogo yanayoonekana.”—The Guardian.
Novemba 1986 kulitukia msiba mkubwa wa uchafuzi ambao ulielezwa na Daily Telegraph la London kuwa “kunyang’anywa kwa Ulaya ya Magharibi mfereji wa maji ulio mkubwa zaidi na wenye kusaidia zaidi.” Moto mkali katika kiwanda cha kemikali katika Basel, Uswisi, ulifanya wazima-moto waje na kuzima mwako huo. Bila kukusudia, waliosha kuanzia tani 10 hadi 30 za kemikali na dawa za wadudu zikaingia katika Mto Rhine, na hiyo ikawa ni kama “[kuvuja kwa sumu ya] Chernobyl katika utumizi wa maji.” Tukio hilo lilitangazwa sana katika vichwa vya habari. Hata hivyo, jambo ambalo kwa ukawaida huwa haliripotiwi ni uhakika wa kwamba takataka zenye sumu hutupwa kwa ukawaida ndani ya Mto Rhine kwa kadiri isiyo ya kutazamisha jinsi hiyo.
Uchafuzi wa maji hauwi kwenye eneo lenye kuzunguka chanzo chayo tu. Kilometa nyingi mbali na hapo, athari zayo zaweza kuwa hatari. Mito ya Ulaya ambayo hutiririka kuingia katika Bahari ya Kaskazini husafirisha rangi, kemikali za kutia weupe katika dawa za meno, takataka zenye sumu, na mbolea kwa wingi sana hivi kwamba sasa Taasisi ya Kiholanzi ya Kuchunguza Uvuvi humsema samaki-ubapa wa Bahari ya Kaskazini kuwa asiyefaa kuliwa. Uchunguzi mbalimbali huonyesha kwamba asilimia 40 ya visamaki-ubapa vya maeneo yasiyo na maji ya kina kirefu vina magonjwa ya ngozi au vivimbe vya kansa.
Ni nani wa kulaumiwa kwa huo utiaji taka? Watu walio wengi hulaumu viwanda, ambavyo vina pupa nyingi mno ya kutaka faida kuliko kuhangaikia mazingira. Hata hivyo, wakulima pia wana hatia ya kuchafua vijito na mito karibu na bara lao. Utumiaji wao wenye kuongezeka wa virutubishaji vya naitreti waweza sasa kufanya maji yatolewayo katika majani ya kuwekwa akiba kwa ajili ya mifugo yawe na hatari ya kuua.
Pia watu mmoja mmoja hutumia mito kuwa mahali pa kutupia takataka. Mto Mersey, ulio na mahali pa kukusanyika maji mengi katika jimbo la kaskazini-magharibi la Uingereza, hudaiwa kuwa ndio mchafu zaidi katika Ulaya. “Sasa, wapumbavu tu au wasio na habari ndio wangeogelea katika Mersey,” ndivyo Daily Post la Liverpool lilivyoeleza, likiongezea hivi: “Mtu yeyote mwenye bahati mbaya sana ya kutumbukia katika mto huo atakuwa na uelekeo wa kupelekwa hospitali akiwa mgonjwa.”
Kinyesi kibichi pia ni sehemu kubwa ya vitu ambavyo huchafuza bahari. Bahari kandokando ya ufuo mmoja wenye kutembelewa nyakati za sikukuu katika Uingereza yaripotiwa kuwa ina kiasi chenye kulingana na “kikombe kimoja cha kinyesi kibichi katika kiogeo cha wastani cha nyumbani,” ambacho kimekizidi kiwango cha EEC kwa mara nne.
Halafu kuna hatari nyingine; hii huanguka kutoka angani.
Mvua ya Asidi—Tisho Lenye Kutia Wasiwasi
Wakati mmoja, watu katika Uingereza walikuwa wakifa kwa sababu ya kupumua hewa—au, tuseme, ukungu wa moshi. Leo, vifo kutokana na uchafuzi huo ni haba. Ukungu wa moshi wa London, ulioua watu wakadiriwao kuwa 4,000 katika 1952, si tisho tena. Vituo fulani vyenye kufanyiza nishati kwa kuchoma makaa-mawe ambavyo vilichangia kutokeza ukungu huo wa moshi vimehamishwa vikawa mashambani na kutiliwa mabomba ya moshi yenye kimo kirefu na, katika visa fulani, vikawa na visuguaji vya kuondoa asilimia kubwa ya gesi zilizo hatari kabisa.
Hata hivyo, jambo hilo halijakomesha uchafuzi wa halianga. Huenda ikawa kwamba mabomba marefu ya kuondolea moshi yamemaliza hatari hiyo kutoka kwenye eneo la pale pale. Lakini sasa, pepo zenye nguvu husafirisha vichafuzi hivyo sehemu za mbali—mara nyingi kwenye nchi nyinginezo. Tokeo ni kwamba, nchi za Skandinavia huteswa na uchafuzi wa Uingereza, na watu wengi hutaja Uingereza kuwa yule “Mzee Mchafu wa Ulaya.” Kwa njia kama hiyo, viwanda vya Magharibi-kati katika United States husababisha sehemu kubwa ya tatizo la mvua ya asidi katika Kanada.
Kwa miaka mingi, wanasayansi wamelaumu salfa dayoksaidi kuwa ndicho kilaumiwa kikuu cha uchafuzi wa hewa ambao husababisha mvua ya asidi. Katika 1985 Drew Lewis, mjumbe wa rais wa United States mwenye kushughulikia mashauri kati ya Kanada na Amerika kuhusu mvua ya asidi, alidai hivi: “Kusema kwamba salfeti hazisababishi mvua ya asidi ni sawa na kusema kwamba kuvuta sigareti hakusababishi kansa ya mapafu.” Yaonekana kwamba wakati ishikanapo na mvuke wa maji, salfa dayoksaidi hutokeza asidi yenye salfa ambayo huenda ikatia asidi katika mvua au kukusanyika katika vitone vya mawingu, hivyo ikiosha misitu ya miinuko ya ardhi kwa umajimaji hatari.
Wakati ile mvua ya asidi inyeshapo au, kwa ubaya zaidi, wakati asidi ya theluji iyeyukapo, udongo ulio chini huathiriwa. Wanasayansi Waswedi waliofanya marudio ya uchunguzi mmoja wa 1927 walikata shauri kwamba uasidi wa udongo wa misitu ulikuwa umeongezeka mara kumi, kwa kina cha sentimeta 70. Badiliko hili la kikemikali huathiri kwa uzito uwezo wa mmea kutwaa madini zilizo muhimu, kama vile kalisiamu na magineziamu.
Yote hayo huwa na tokeo gani juu ya binadamu? Yeye huteseka wakati maziwa na mito yenye umayamaya wa vitu hai huwa na asidi na kukosa uhai. Zaidi ya hilo, wanasayansi Wanorowei hukata shauri kutokana na uchunguzi wao kwamba uasidi wa maji ulioongezeka, uwe ni katika maziwa au udongo, huyeyusha aluminiamu. Hiyo hutokeza hatari halisi ya kiafya. Wanasayansi wameona “uhusiano wa wazi kati ya maongezeko ya vifo na ongezeko la kukolea kwa aluminiamu” katika maji. Hofu yaendelea kuwako juu ya uwezekano wa kwamba kuna uhusiano kati ya aluminiamu na ugonjwa wa Alzheimer na maradhi mengine ya wazee.
Ni kweli kwamba katika maeneo kama Mto Mersey wa Uingereza na Entressen wa Ufaransa ambamo takataka hutupwa, jitihada zimefanywa ili hali hiyo iwe na maendeleo. Hata hivyo, tatizo la namna hii haliondoki. Hutokea upya katika sehemu zote za ulimwengu. Lakini bado kuna aina nyingine ya uchafuzi—usioonekana.
Ozoni—Adui Asiyeonekana
Kuchoma masalio ya vitu vya aina ya fueli, iwe ni katika vituo vya kufanyiza nishati au katika tanuri za kinyumbani, hutokeza vichafuzi vingine kwa kuongezea salfa dayoksaidi. Hivyo ni kutia na oksaidi za naitrojeni na haidrokaboni zisizochomwa.
Sasa maoni ya kisayansi yanazidi kuzilaumu hizi oksaidi za naitrojeni kwa uchafuzi wa hewa. Zikiwa chini ya nuru ya jua, hizo husaidia kutokeza gesi hatari, ozoni. “Ozoni ndicho kichafuzi kibaya kabisa cha hewa kinachoathiri mimea katika U[nited] S[tates],” akataarifu David Tingey wa Shirika la Ulinzi wa Mazingira la United States. Alikadiria kwamba jambo hilo lilikuwa linagharimu nchi yake dola milioni 1,000 kwa mwaka katika 1986. Wakati huo hasara ya Ulaya ilionyeshwa kuwa dola milioni 400 kila mwaka.
Hivyo, ingawa mvua ya asidi inaua matiririko ya maji, watu wengi wahisi kwamba ozoni, ambayo yahusianishwa hasa na mioshi itokayo kwenye magari, ndiyo ya kulaumiwa zaidi ya mvua ya asidi kwa vifo vya miti. The Economist ilitaarifu hivi: “Miti [katika Ujeremani] inauawa mapema mno si na mvua ya asidi bali na ozoni. Ingawa pigo hilo la kifo laweza kuletwa na baridi kali, ukungu wa asidi au ugonjwa, ozoni ndiyo hufanya miti idhoofike kabisa.” Na linalotukia katika Ulaya ni kionyeshi tu cha hali zilizo katika kontinenti nyinginezo. “Miti katika bustani-starehe za kitaifa za Kalifornia inadhuriwa na uchafuzi wa hewa ambao huenda ukawa unatoka hata kule mbali Los Angeles,” likaripoti New Scientist.
Hata hivyo, kuna aina mbaya zaidi ya uchafuzi unaochafua dunia. Ni kisababishi cha msingi katika kuchafuza kihalisi bara, maji, na hewa ya sayari yetu.
Uchafuzi wa Kiadili
Ni rahisi kudanganywa na sura ya watu. Yesu Kristo alionyesha dhahiri sana kielezi cha jambo hilo. Akihutubia viongozi wa kidini wa siku yake, alisema hivi: “Ole wenu . . . kwa kuwa mmefanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, nayo kwa nje yaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa . . . uchafu wote.” (Mathayo 23:27) Ndiyo, huenda mtu akaonekana mstahifu sana, hata wa kuvutia, nje-nje, lakini huenda usemi na mwenendo wake ukafichua utu wake wa tabia potovu. Kwa kuhuzunisha, uchafuzi huo wa kiadili umeenea kwa mapana leo.
Uchafuzi wa kiadili ni kutia na utumizi mbaya wa dawa za kulevya, ambao umeenea kwa mapana kuliko wakati mwinginewo wote. Waimbaji mashuhuri, mabingwa waabudiwao kwa maonyesho yao ya jukwaani na sinemani, na hata wale ambao yaonekana ni wanabiashara wastahiwa, wamekuwa wenye matendo ya kashifa kwa sababu ya kutegemea kwao dawa za kulevya. Pia uchafuzi wa kiadili watia ndani ukosefu wa adili kingono, ambao waweza kuwa ndicho kisababishi cha familia zilizovunjika, talaka, utoaji mimba, na pia maongezeko makubwa sana ya magonjwa yaambukizwayo kingono, kutia na lile pigo lenye balaa kubwa la UKIMWI.
Kwenye mzizi wa huu uchafuzi wa kiadili kuna ubinafsi, ambao pia ndio ulioko kwenye mzizi wa kadiri kubwa ya uchafuzi wa kihalisi unaopiga ainabinadamu. Tereza Kliemann, mwenye kuhusika katika kutibu UKIMWI katika Mkoa wa São Paulo, Brazili, alitambulisha tatizo hilo: “Kuzuia [UKIMWI] kwamaanisha badiliko la mwenendo miongoni mwa vikundi vyenye elekeo la juu zaidi la kupatwa nao, na hilo ni jambo gumu.” Watu walio wengi sana hukazania kufanya lile ambalo wao hutaka kufanya, badala ya kufikiria jinsi vitendo vyao huathiri wengine. Tokeo ni kwamba, fasihi, vitumbuizo, na karibu utamaduni wote wa kibinadamu vimetatanishwa na uchafuzi wa kiadili.
Kwa watu wenye kufikiri, nyingi za jitihada za kisasa za kusafisha uchafu wa kimwili na wa kiadili zaonekana kuwa kisingizio tu. Basi, huenda wewe ukashangaa ukijiuliza kama kuna tumaini lolote lenye kutegemeka la kuwa na dunia iliyo safi kimwili na kiadili pia. Usife moyo. Biblia yatuambia kwamba mwisho wa uchafuzi u karibu!
[Maelezo ya Chini]
a Kimeta ni ugonjwa wa mifugo wa kuambukiza ambao husababisha vivimbe vya ngozi vyenye kutokeza vidonda au maambukizo ya mapafu katika binadamu.
b EEC yasimamia “European Economic Community,” au Soko la Kawaida.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]
Kibaya Kuliko Madhara ya Wakati
Baada ya miaka mingi ya kuachwa mahali wazi lipatwe na viharibu vya kiasili, jiwe hili la uso wa kuchongwa lilionyesha sura ya kufa tu. Matokeo ya ubabuzi wa hewa ni mabaya zaidi ya madhara ya wakati. Majengo ya zamani kotekote ulimwenguni hubabuliwa na mvua ya asidi ambayo huyaosha, kuanzia lile Jumba la Jiji katika Schenectady, United States, hadi yale majengo maarufu ya Venice, Italia. Majengo ya kumbukumbu ya Roma yaripotiwa kuwa huvunjika-vunjika kwa kuguswa tu. Parthenoni maarufu ya Ugiriki yaaminiwa kuwa iliharibika zaidi katika miaka 30 iliyopita kuliko katika 2,000 iliyotangulia. Mara nyingi uharibifu huo huongezewa na visababishi vya kimazingira ambavyo ni kutia ndani halijoto, upepo, na unyevu, na pia bakteria zinazoishi katika kuta za jengo. Kukiwa na matokeo hayo kwa vitu visivyo na uhai, tokeo la uchafuzi ni lazima liwe la kadiri gani juu ya viumbe hai?
[Picha]
Mchongo juu ya kathedro fulani katika London