Vijana Wanauliza. . .
Naweza Kutumiaje Rangi za Uso kwa Kufaa?
“JE UNATAKA kupaka rangi za uso kidogo?” Nina alishangaa kusikia mama yake akiuliza swali hilo. Miaka miwili mapema, alikuwa amenyimwa ruhusa kutumia rangi za uso. Lakini pindi hii ya pekee, karamu ya arusi ambayo wangehudhuria, mama yake aliamua kwamba ilikuwa wakati Nina ajifunze ustadi wa kike wa kupaka rangi za uso. “Nilikuwa na wasiwasi kidogo,” akumbuka Nina. “Sikujua jinsi ya kuzipaka vizuri. Kwa hiyo Mama alinipaka rangi ya mdomo na ya mashavu.”
Labda wazazi wako huona vivyo hivyo kwamba ingefaa upake rangi za uso.a Zinapotumiwa kwa kufaa—na kwa haba—rangi za uso zaweza kuongezea sura ya mtu. Lakini zinapotumiwa kwa makosa, zina matokeo yaliyo tofauti kabisa. “Wasichana wengine hupaka rangi za uso ikapendeza,” asema mvulana mtineja mmoja. “Lakini wasichana wengine hujipaka nyingi sana, zikawafanya waonekane vibaya sana.”
“Wanapopaka rangi yenye kung’aa sana, nayo ni yenye kung’aa kweli kweli,” aongeza msichana mtineja, “inawafanya waonekane kama mcheshi!” Waweza kutumiaje rangi za uso kwa njia ambayo itaongezea—wala siyo kupunguzia—sura yako?
Miongozo Kutoka kwa Neno la Mungu
Virembeshi si jambo jipya. Mabakuli au vibao vya kufanyiza rangi vilivyotimiza kusudi ambalo kwa ajabu ni la ki-siku-hizi, vimepatikana vikiwa vimefichika miongoni mwa magofu ya Kisraeli. Hivyo “vilikuwa vikitumiwa ili kutayarisha rangi kwa ajili ya uso” za wanawake Waisraeli. Kulingana na The Biblical Archaeologist, ya Februari 1955, “utumizi wa . . . virembeshi ulienea sana” hata katika nyakati za Biblia.—Ezekieli 23:40.
Leo, kiwanda cha virembeshi kinatumia dola milioni elfu mbili kila mwaka kwa kutangaza katika United States peke yake. Wakitumia wanawake wenye kuvutia sana kama mifano, wao huendeleza “sura,” ya kisasa inayoenea kutoka ile ya “kiasili” hadi ile isiyo ya kawaida. Wao hudai kwamba hiyo “sura”, yaweza kuwa yako ukinunua tu aina mbalimbali za virembeshi. Hata hivyo, ni wasichana wachache wanaoonekana kama wanawake wanaoonyesha mifano ya mitindo. Hata wanapoonekana hivyo, hiyo “sura” mpya yaweza kuwa ya kikale hata kabla kijiti kimoja cha rangi ya kupaka mdomoni hakijaisha.
Biblia inakusaidia uepuke kudhibitiwa na kubadilika-badilika kwa mtindo. Inasema hivi: “Msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.” (Warumi 12:2) Katika nyakati za Biblia, wanawake Wakristo wengine huenda walielekea kuvaa mavazi ya fahari na mitindo ya nywele yenye madoido yaliyopendwa na watu wengi wakati huo. Lakini mtume Paulo alishauri hivi: “Mimi nataka sana wanawake wajipambe wenyewe kwa mavazi yaliyotengenezwa vizuri, kwa kiasi na utimamu wa akili, wala si kwa mitindo ya kusuka nywele, wala dhahabu wala lulu wala vazi lenye thamani kubwa sana.”—1 Timotheo 2:9, NW.
Shauri la Paulo halikukatazi uonekane mwenye kuvutia. Linamaanisha tu kwamba sura yako yapaswa ‘kutengenezwa vizuri,’ au yenye kufaa, wala si ya fahari; yenye kiasi na akili timamu, wala si yenye kutazamisha au yenye mtindo wa kuchekesha. Neno la Kigiriki kwa “-a kiasi” huwa na wazo la kuwa na ‘staha kwa mawazo ya wengine,’ na unapaswa kuwa na staha hasa kwa mawazo ya wazazi wako. Kwa hiyo acheni tuone jinsi hilo laweza kuhusika na kupaka rangi za uso.
Kabla ya Kupaka Rangi za Uso
Kwa kuwa rangi za uso zapasa kuongezea sura yako, si kufanyiza kifuniko cha uso au maficho, ni jambo la kiakili kutunza sura yako ya kiasili na afya yako kwa ujumla kwanza. Kudumisha mlo kamili na kupumzika vya kutosha na kujizoeza kwa kawaida huenda kukaongezea zaidi kuvutia kwako hata kuliko rangi yoyote ya uso iwezavyo.
Jane Parks-McKay mwenye kutoa mashauri ya ustadi kuhusu urembo huhimiza wasichana wachanga “kuanza na mambo ya msingi—yaani, utunzaji wa uso wa kikawaida, wenye matokeo. . . . Watu wengi huelekea kutojali ngozi yao . . . [halafu] hufunika ngozi zao zisizovutia kwa virembeshi wakitumaini kwamba hilo litawafanya wapendeze.”
Rangi za uso hutumika kwa ubora zaidi kwenye uso uliotunzwa vizuri. Kitabu A Lifetime of Beauty chaeleza hivi: “Kusafisha ngozi ni kama kutayarisha ukuta ili kupaka rangi mpya: hata rangi iwe yenye kupendeza aje, kazi hiyo ya kupaka rangi itaonekana kuwa ovyo ikiwa kuna uchafu na alama zisizolaini chini-chini. Ngozi isiyosafishwa vizuri itaonekana isiyong’aa na yenye kupasuka-pasuka.”
Hivyo mstadi wa rangi za uso aliambia Amkeni! hivi: “Asubuhi, msichana aweza kunawa uso wake kwa kutumia dawa nzuri ya kusafisha uso. Aweza kufuata kwa kutumia dawa ya kusawazisha rangi ya uso na dawa ya kupa uso umaji-maji.”
Changanua Mahitaji yako
Sasa, tazama uso wako vizuri ukachanganue yaliyo mazuri na mabaya ya uso wako. Je! una macho machangamfu, ngozi iliyo laini kwa kadiri, au rangi ya uso yenye afya, iliyosawazika? Basi ni yamkini kwamba utahitaji rangi za uso kidogo au hutahitaji zozote. Kwa upande mwingine, labda ngozi yako ni yenye mafuta-mafuta sana (jambo la kawaida wakati wa miaka ya utineja) na inaelekea kuwa na chunusi. Au huenda una sehemu ya uso (kama vile vituguta) ambayo ungependa kutokeza hasa. Utumizi wenye busara wa rangi za uso huenda ukasaidia.
Katika nyakati za Biblia wanawake wengine walipaka rangi nyeusi machoni mwao ili kuonekana kana kwamba wana ‘macho makubwa.’ (Yeremia 4:30) Leo, rangi za kope, kalamu za macho, na rangi za umaji-maji za kupaka macho hutumiwa kupata matokeo hayo hayo. Krimu za uso za msingi na losheni zaweza kulainisha ngozi yenye mawaa. Rangi ya mashavu yaweza kutokeza vituguta vyako.
Vipi ikiwa unahitaji msaada ili kuchagua au kupaka rangi za uso? Kuna vitabu vinavyopatikana katika maktaba za umma viwezavyo kukusaidia. Lakini huenda ukataka shauri kwa mama yako au kwa rafiki mwenye umri mkubwa zaidi. Msichana mtineja anayeitwa Tina akumbuka hivi: “Mama alinipeleka tukanunue vitu akataka karani wa rangi za uso aone ni rangi gani ambazo ningepaswa kupaka.” Wenye kutoa mashauri ya ustadi kuhusu urembo katika maduka yenye sifa nzuri wanaweza kutoa mashauri juu ya rangi ambazo hufaa zaidi rangi yako ya ngozi na jinsi rangi za uso zaweza kupakwa vizuri zaidi. Lakini kwa sababu kazi yao ni kukuuzia bidhaa, jitahadhari usije ukanunue bidhaa usizohitaji kwa kweli. Na kwa sababu ya mahitaji yako ya kipekee ya mtindo-maisha wako wa Kikristo, utataka kuhakikisha kwamba hununui rangi ambazo zingefaa katika hali ya jioni ya kidesturi lakini zisingefaa shuleni au katika utendaji wa Kikristo.
Vidokezo vya Rangi za Uso
Mitindo ya rangi za uso hutofautiana katika bara moja hadi jingine. Lakini kanuni chache za ujumla zaweza kutaarifiwa:
Fikiria Aina ya Ngozi Yako. Kwa kuwa matineja wengi wana ngozi zenye mafuta-mafuta, ni yamkini kwamba ungetaka kutumia tu rangi za uso zisizo na mafuta zenye msingi wa maji. Hizo hazing’ai sana, kwa hiyo utaonekana kama huna rangi za uso nyingi. Wengi huona pia kwamba rangi za uso zenye mafuta huzidisha chunusi.
Soma Mibandiko. Linganisha viambato vya aina yenye bei ya chini pamoja na vile vya aina zenye bei ghali. Labda tofauti iliyopo kwa kweli ni bei na makasha tu. Kusoma mibandiko ni kwa maana hasa ikiwa unaathiriwa na rangi za uso.
Tumia Mwangaza Mwangavu. Ikiwa mwanga hautoshi, huenda ukapaka rangi za uso nyingi sana. Kwa kuwa rangi za uso zilizopakwa katika kuangaza kwa floresenti huenda zikaonekana zenye kuwaka sana juani, jaribu kupaka rangi zako za uso karibu na dirisha ili uweze kuona jinsi inavyoonekana katika mwangaza wa kiasili.
Tumia kwa Haba. Wingi wa hata kitu ambacho ni kizuri waweza kudhuru. (Linganisha Mithali 24:13; 25:27.) Ikiwa uso wako karibu ni kama inalia kwa sauti “rangi za uso!” umepaka nyingi mno au umepaka paka rangi ambazo zinawaka sana. Kupaka rangi za uso kupita kiasi kunashusha sifa za sura yako na huenda kukatoa wazo la makosa juu ya kanuni zako za kiadili. (Linganisha Ezekieli 23:36-42.) Basi tumia tu namna za rangi zilizo nzuri si zenye fahari. Jifunze njia za kupaka rangi za uso ili rangi ya mashavu isionekane kama rangi ya ukuta iliyo upande mmoja hadi mwingine wa uso wako au rangi ya macho isikufanye uonekane kama Rakuni (mnyama mdogo kama dubu mwenye miviringo myeusi inayozunguka macho yake).
Safisha Uso Wako Kamili. Kitabu A Lifetime of Beauty kinasema hivi: “Usiende kamwe kulala bila kuondoa kila alama ya rangi za uso . . . Kuzoea kulala na safu ya uchafu, takataka na seli za ngozi zilizokufa zikiwa zimeshikamana usoni mwako kutaacha ngozi yako ionekane yenye topetope na isiyong’aa.” Daktari wa ngozi mmoja hata hudai kwamba “una hatari ya kuambukizwa na kuwashwa ukishindwa kusafisha rangi zote za uso kila usiku kabla ya kulala.” Tumia kiyeyusho cha rangi za uso, kama vile krimu baridi, kusafisha uso wako.
“Uzuri ni ubatili,” yasema Mithali 31:30, na hata rangi za uso zilizopakwa kwa ustadi haziwezi kuficha mwelekeo mbaya au akili hafifu. Biblia inatukumbusha hivi: “Urembo wako haupasi kutokana na kujipamba kwa nje . . . Badala ya huo, unapasa kuwa ule wa utu wako wa ndani, ule urembo usiofifia wa roho nyororo na tulivu, ambayo ni yenye thamani kubwa machoni pa Mungu.”—1 Petro 3:3, 4, New International Version.
[Maelezo ya Chini]
a Ona makala “Kwa Nini Wazazi Wangu Hawaniruhusu Nipake Rangi za Uso?” inayotokea katika toleo la Amkeni! la Mei 22, 1990 katika Kiingereza.
[Sanduku katika ukurasa wa 14]
Hatari za Rangi za Uso
Mteteaji wanunuzi Elaine Brumberg aripoti hivi: “Kemikali na viambato vya virembeshi vingi vyaweza kupenya ngozi vikaingia mwili.” Viambato vinavyotumiwa kwa kawaida yanadhaniwa kuwa karsinojeni (vyenye kusababisha ugonjwa wa kansa).
Viambato vingine (kwa kawaida manukato na dawa za kuzuia vitu visioze) vinajulikana kusababisha kuathiriwa mbalimbali kutoka kujikuna-kuna hadi kupiga chafya. Ni kweli, bidhaa nyingine hudai kuwa hazisababishi kuathiriwa au kuwa “zimetahiniwa kama zinaathiri.” Lakini itikio la mwili wako kwa bidhaa fulani kunaweza kuhakikishwa tu kwa kujionea mwenyewe na kwa kuchunguza mibandiko kwa uangalifu.
Hatari nyingine yenye kuenea sana ni ambukizo ya kibakteria. Maskara (rangi ya macho ya umajimaji) yaweza kuwa mahali pa vitu vidogo sana venye uhai kuzaa vilivyopishwa hapo kutoka ukope au vidole kupitia chombo cha kupakia maskara. Hiyo yaweza kusababisha uambukizo ikiwa chombo cha kupakia maskara kinaruhusiwa kukwaruza jicho. Ambukizo ni tatizo hasa katika violezo vya dukani ambamo watu wengi wametia vidole vyao. Kwa hiyo wastadi wengine hudokeza kwamba uepuke kupaka violezo vya dukani usoni mwako
[Picha katika ukurasa wa 12]
Huenda mama yako akaweza kukufunza ustadi wa kupaka rangi za uso