Je! Unaweza Kutegemea Habari Unazopokea?
KATIKA Mei 10, 1927, chapa ya pekee ya gazeti la Ufaransa La Presse iliripoti kwamba mruko wa ndege wa kwanza kufanikiwa kuvuka Atlantiki bila kutua ulikuwa umefanywa na marubani wawili Wafaransa, Nungesser na Coli. Ukurasa wa kwanza ulionyesha picha za wanahewa hao wawili na pia habari ndefu juu ya kuwasili kwao katika New York. Lakini hadithi hiyo ilikuwa imetungwa. Kwa kweli, ndege hiyo ilikuwa imeangamia, na wanahewa hao wakafa.
Hata hivyo, ripoti za habari bandia ni za kawaida sana kuliko ambavyo labda watu wengi wanafikiri. Katika 1983 maandishi ya kisiri, yaliyodhaniwa kuwa ya Hitler, yalitangazwa katika magazeti muhimu ya kila juma, hasa katika Ufaransa na Ujerumani ya Magharibi. Ilikuja kugunduliwa yalikuwa bandia.
Vivyo hivyo, katika 1980 hadithi moja juu ya kijana mmoja mzoea madawa ya kulevya ilitangazwa katika Washington Post. Masimulizi hayo yalimshindia mwandishi huyo zawadi ya Pulitzer, ambayo ni tuzo la juu zaidi kwa mwandishi katika United States. Lakini baadaye hadithi hiyo ilifunuliwa kuwa ni ya kubuniwa, ya kutungwa. Kwa kusongwa na wapelelezi, mwandishi huyo wa kike alipeleka taarifa ya kujiuzulu, akisema: “Naomba msamaha gazeti la kwangu, kazi ya kwangu, halmashauri ya Pulitzer na watafutaji ukweli wote.”
Hata hivyo, mitungo ya habari, au ripoti bandia, sizo tu kizuizi pekee cha kuufikilia ukweli kuhusu yale yanayotukia ulimwenguni.
Uteuzi na Utoaji wa Habari
Mara nyingi waandishi wa habari na wahariri huteua habari zinazostaajabisha umma lakini huenda zikawa si zenye umaana wa kweli. Zenye kushtua au kuvutia ndizo hutangulizwa ili kuongeza mwenezo na umaarufu. Mabingwa wa ulimwengu wa utumbuizaji na wa michezo huonyeshwa, bila kujali wanawekea vijana kielelezo cha aina gani. Kwa hiyo mmoja wao akichukua mpenzi, akioa, au akifa, mara nyingi hizo ndizo habari.
Kwa ujumla habari za televisheni huonyesha mambo yanayovutia macho. Kiongozi wa shirika moja kubwa la utangazaji la televisheni, kama ilivyoripotiwa katika gazeti TV Guide, “alijulisha rasmi alitaka ‘vituko’ kwenye matangazo—vituko vyenye kusokota matumbo, vyenye kugutua ili kumvuta mtazamaji katika kila hadithi.” Kweli kweli, kuvutia watazamaji kwa kawaida huwa jambo linalohangaikiwa zaidi ya kuelimisha umma.
Njia ambayo matukio huonyeshwa huenda ikashindwa kufanya jambo lote lionekane lilivyo. Kwa kielelezo, nyongeza ya kila juma ya gazeti la Ufaransa la kila siku Le Monde ilieleza juu ya “kulipuka kwa televisheni tatu [katika Ufaransa] katika muda wa siku kumi na tano tu.” Ingawa hilo lilitangazwa kuwa jambo lisilo la kawaida, hesabu ya milipuko ya televisheni kwa kipindi hicho cha siku 15 kwa kweli ilikuwa ndogo zaidi ya ilivyo kawaida.
Pia, habari za maana huenda nyakati nyingine zikatolewa kwa kuegemea upande mmoja. Parade Magazine laripoti kwamba mara nyingi maofisa na wanasiasa “hupitisha udanganyifu wao kupitia vyombo vya habari, wakipotosha habari kwa kusudi la kuongoza kufikiri kwako. Wao hushughulika na mambo waliyoteua kuliko ukweli wote.”
Jambo hilo husumbua watangazaji wengi wa habari. Encyclopædia Universalis cha Kifaransa chataarifu hivi: “Tangu mwisho wa miaka ya 1980, vyombo vya habari vilivyo vya maana, na hasa televisheni, vimelaumiwa kutoka pande zote, na wataalamu na watu wa kawaida, na mtu aliye barabarani, na waheshimiwa, kwa yale yasemwayo na yale yanayoachwa bila kusemwa, kwa yasemwavyo na kwa utungaji wa madai mbalimbali.”
Mbadilishano usio na kizuizi wa habari kwa kiwango cha ulimwenguni pote ni tatizo pia nalo lilikuwa kichwa cha mjadala mkali kwenye UNESCO (Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi, na Utamaduni). Nchi zinazositawi zililalamika kwamba zilitajwa tu katika habari wakati misiba au matatizo makubwa ya kisiasa yalipotukia. Baada ya kusema kwamba mashirika fulani ya habari ya Magharibi huwa na habari nyingi zaidi kuhusu nchi zilizo katika kizio cha Kaskazini kuliko zinazohusu zile zilizo katika Kizio cha Kusini, makala moja katika gazeti la kila siku la Ufaransa Le Monde iliongeza hivi: “Hilo limezusha ukosefu mkubwa wa usawaziko unaohusu maoni ya umma katika nchi zenye maendeleo makubwa ya viwanda kwa kadiri ile ile kama katika nchi zinazositawi.”
Vikundi Vyenye Kuleta Msongo
Msongo ambao wenye matangazo ya biashara huweka juu ya wahariri wa habari huathiri zaidi habari ambazo umma hupokea. Katika miaka ya 1940 gazeti moja la U.S. lilipoteza matangazo ya biashara kutoka kwa waundaji piano lilipotangaza makala yenye kuonyesha faida za kutumia gitaa kuongoza waimbaji wenye kufuatisha. Makala moja ya mhariri ilitangazwa baadaye katika gazeti hilo ikisifu sana piano! Kwa hiyo, uchache wa makala zinazofunua hatari za kuvuta sigareti haupaswi kushangaza kwa sababu chanzo kikuu cha mapato ya magazeti mengi ni matangazo ya sigareti.
Msongo mwingine wahusisha wasomaji au watazamaji wenyewe. Raymond Castans, aliyekuwa mkurugenzi wa kituo kimoja cha redio ya Ufaransa chenye kupendwa na wengi, alieleza kwamba wasikilizaji kwa sehemu kubwa hawakutaka mabadiliko, kwa hiyo uangalifu ulipasa kuchukuliwa ili wasiudhike. Kwa hiyo, je! inashangaza kwamba katika nchi ambayo dini fulani ndiyo kubwa, mambo ya hakika yasiyopendeza kuihusu yamefunikwa au kupunguzwa uzito?
Pia misongo hutokezwa na vikundi au watu mmoja mmoja wenye kutaka mabadiliko makubwa wanaohisi kwamba maoni yao hayapewi uangalifu wa kutosha katika vyombo vya habari. Miaka michache iliyopita, maharamia waliomteka nyara Aldo Moro, aliyekuwa waziri mkuu wa Italia, walisisitiza kwamba madai yao yajulishwe kikamili kwenye televisheni, redio, na katika magazeti ya Italia. Vivyo hivyo, maharamia wanaoteka nyara ndege na kushika watu mateka huwa ndio habari kuu za TV na kwa njia hiyo kupata umaarufu wanaotaka.
Mara nyingine waleta habari hushtakiwa kuwa vibaraka, kuwa wanaendeleza mifumo na maoni ambayo yamekwisha imarishwa. Lakini je! twaweza kutazamia kiwanda kinachotafuta wasomaji au wasikilizaji wengi iwezekanavyo kisambaze mawazo na maoni yanayopingana na yale ya wengi wa watu kinachotumikia?
Tatizo linalohusiana ni kwamba katika nchi nyingi gharama zenye kupanda zimesababisha magazeti ya kila siku yaungane, hivyo kufanyiza kwa halisi “milki za vyombo vya habari” zikiwa mikononi mwa vikundi vidogo au hata mtu mmoja. Hesabu ya wamilikiji ikiendelea kupungua, hilo litapunguza utofauti-tofauti wa maoni yenye kutangazwa.
Uvutano juu ya Umma
Hakuna shaka kwamba vyombo vya habari vimechangia pia kuumbika kwa thamani za kijamii. Hilo hufanywa kwa kuonyesha kuwa vyenye kukubalika, viwango vya adili na mitindo ya maisha ambayo ingalikataliwa miaka michache tu iliyopita.
Kwa kielelezo, katika miaka ya mapema ya 1980, mwanamume mmoja wa makamo, mmoja wa Mashahidi wa Yehova, alikuwa na mazungumzo juu ya mwanaume na mwanamume kufanya ngono akiwa na baba yake, ambaye wakati huo aliishi si mbali kutoka San Fracisco, California. Mapema maishani mwake, baba huyo alikuwa amewasilisha kwa mwana wake maoni yake kwamba tabia ya mwanamume na mwanaume kufanya ngono ni ya kuchukiza. Lakini ndipo, miongo kadhaa baadaye, kwa kuvutwa na vyombo vya habari, baba huyo mwenye umri mkubwa akatetea ngono ya mwanamume na mwanamume kuwa mtindo mwingine wa maisha unaokubalika.
Encyclopedia of Sociology (Kifaransa) chashikilia maoni haya: “Redio na televisheni huenda . . . vikasitawisha sana mawazo mapya, kutia moyo mitindo mipya au yenye kuleta matata. Kwa sababu ya kutaka habari zenye kushtua, vyombo hivyo huzikuza tangu mwanzoni na kutilia chumvi umaana wazo.”
Ikiwa hatutaki thamani zetu ziumbwe na vyombo vya habari, twaweza kufanya nini? Twapaswa kufuata ushauri wenye hekima unaopatikana katika Biblia. Hii ni kwa sababu daima viwango na kanuni zayo zina thamani kwa jamii yoyote katika wakati wowote wa historia. Zaidi ya hayo, hutusaidia kuelewa jinsi lilivyo jambo la maana kufuata mtindo wa viwango vya Mungu na wala si mawazo yanayopendwa na walio wengi ya ulimwengu wa ki-siku-hizi.—Isaya 48:17; Warumi 12:2; Waefeso 4:22-24.
Kuongezea hayo, Maandiko hueleza upande wa maana wa habari ambazo kwa ujumla hukoswa kuonwa na vyombo vya habari. Acha tuchunguze upande huo katika makala inayofuata.
[Picha katika ukurasa wa 7]
Vyama vya wenye mawazo yasiyokubaliwa na walio wengi hupata umaarufu ambao vinataka
[Hisani]
Photo ANSA