Tujuayo Juu ya Jamii za Rangi Mbalimbali
YAPATA miaka 500 iliyopita Wazungu walipoanza safari za kuvumbua dunia, walishangaa wangekutana na watu wa aina gani. Kulikuwa na hekaya za majitu ambao wangeweza kutembea ndani ya bahari na kuvunja-vunja merikebu kwa mkono mmoja. Kulikuwa na hadithi za watu wenye vichwa kama mbwa wakipumua miali ya moto. Je, wangekutana na wale watu “wasiotaka urafiki” wa kihekaya waliokula nyama mbichi na ambao mdomo wao mkubwa wenye kuchomoza nje uliwapa kivuli kuwakinga na jua? Au wangeona watu wasio na midomo, walioishi kwa kunusa matofaa? Namna gani wale wenye masikio ya ukubwa wa kutosha kutumika kama mabawa, au wale waliosemwa kuwa hulala chali wakiwa chini ya kivuli cha wayo wao mmoja tu ulio mkubwa?
Watu walizipitia bahari, wakakwea milima, wakapenya misitu na kutembea majangwa wasione viumbe wageni. Badala yake, wavumbuzi walishangaa kuona watu walio kama wao wenyewe. Christopher Columbus aliandika hivi: “Katika visiwa hivi [West Indies] mpaka sasa sijaona madubwana yoyote ya kibinadamu, kama wengi walivyotarajia, bali sura nzuri zaonekana kati ya jamii zote za watu hawa. . . . Hivyo sijapata madubwana wala habari juu ya wowote, isipokuwa . . . jamii ya watu . . . walao mnofu wa kibinadamu . . . Wao hawana maumbo mabaya bali ni sawa na wengine.”
Kupanga Ainabinadamu Vikundi Vikundi
Hivyo, kwa safari za uvumbuzi wa dunia, zile tofauti za wanadamu ziliondolewa katika hadithi na hekaya za mizuka. Jamii za watu zingeweza kuonwa na kuchunguzwa. Baada ya muda, wanasayansi walijaribu kuwapanga vikundi vikundi.
Katika mwaka wa 1735 mtaalamu wa mimea Mswedi Carolus Linnaeus alichapisha kichapo Systema Naturae. Humo mwanadamu alipewa jina Homo sapiens, yaani “binadamu aliye mwenye hekima,” mtajo ambao mwandikaji mmoja alisema yawezekana ndiyo maelezo ya majivuno ya kishenzi zaidi yaliyopata kupewa kwa jamii yoyote ya vilivyo hai! Linnaeus aligawanya ainabinadamu katika vikundi vitano, alivyovieleza ifuatavyo:
WAAFRIKA: Weusi, watulivu tuli, wastarehevu. Nywele nyeusi, zenye visokoto; ngozi nyororo ya uangavu; pua pana; midomo minene; wajanja, wavivu, wazembe; hujipaka shahamu; huongozwa na tabia ya kigeugeu.
WAAMERIKA: Wenye rangi ya shaba nyekundu, wenye hasira ya haraka, wima; nywele nyeusi, wenye kunyooka, maungo manene; mianzi mipana ya pua; uso mkatili; ndevu haba; wakaidi, wenye kuridhika na mambo yao; hujichora mistari myembamba myekundu; hurekebishwa-rekebishwa na desturi.
WAESIA: Watu wa huzuni-huzuni, washikilia sana maoni; nywele nyeusi; macho meusi; wakali, wenye kiburi, watamani vya wengine; wenye kujifunika mavazi legelege; huongozwa na maoni.
WAZUNGU: Rangi nyepesi, wekundu, wenye maungo; nywele manjano, ya kahawia, yenye kutiririka; macho ya kibuluu; wanana, wachunguaji sana, wavumbuzi; wenye kujifunika mavazi ya kuwashika; huongozwa na sheria.
MTU WA MWITU: Mwenye miguu minne, bubu, mwenye nywele nyingi mwilini.
Angalia kwamba ingawa Linnaeus alipanga wanadamu kulingana na tabia za urithi (rangi ya ngozi, maumbile ya nywele, na kadhalika) pia alikadiria nyutu kwa maoni ya kuegemea upande mmoja. Linnaeus alidai kwamba Wazungu ni “wanana, wachunguaji sana, wavumbuzi,” hali akionyesha Waesia kuwa “wakali, wenye kiburi, watamani vya wengine” na Waafrika kuwa “wajanja, wavivu, wazembe”!
Lakini Linnaeus alikosea. Tabia hizo za nyutu hazina nafasi katika mipangilio ya ki-siku-hizi ya vikundi vikundi vya jamii za watu wa rangi mbalimbali, kwa vile utafiti wa kisayansi umeonyesha kwamba kuna tofauti za utu na kiwango cha akili kinacholingana, yaani, twapata sifa zile zile zilizo chanya na hasi katika jamii ya kila rangi ya watu.
Mara nyingi mifumo ya ki-siku-hizi hupanga wanadamu vikundi vitatu kwa msingi wa tofauti za umbo: (1) Wakaukasoidi, wenye ngozi laini na nywele za singa au za mawimbi; (2) Wamongoloidi, wenye ngozi ya kimanjano na makunyanzi machoni; na (3) Wanegroidi, wenye ngozi nyeusi na nywele kama sufi. Lakini si watu wote wanaofaana kabisa na kimojawapo vikundi hivi.
Kwa mfano, Wasani na Wakhoikhoi wa Afrika Kusini wana ngozi ya shaba nyekundu, nywele kama sufi, na sura ya Kimongoloidi. Wahindi wengine wana ngozi nyeusi lakini sura ya Kikaukasoidi. Waaustralia Waaborijini wana ngozi nyeusi lakini nywele zao za kisufi ni ndefu. Wamongolia wengine wana macho ya Kikaukasodi. Hakuna utofautisho wa wazi kabisa.
Matatizo haya yamefanya wengi wa wataalamu wa hali na tabia za jamii za watu wakate tamaa kufanya majaribio ya kuwapanga wanadamu vikundi vikundi, wakidai kwamba ule usemi “jamii ya rangi” hauna maana au thamani ya kisayansi.
Maazimio ya UNESCO
Pengine maazimio ya kisayansi yenye mamlaka kupita yote kuhusu jamii za rangi mbalimbali ni yale yaliyofanywa na kikundi cha wastadi waliokusanywa na UNESCO (Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni). Mikutano ilifanywa katika miaka ya 1950, 1951, 1964, na 1967 ambapo kikoa cha kimataifa cha wataalamu wa tabia na asili ya binadamu, wataalamu wa wanyama, madaktari, wataalamu wa maumbo ya mwili na wengine walifikia maazimio manne juu ya jamii za rangi mbalimbali. Azimio la mwisho lilikazia mambo matatu haya:
A “Wanadamu wote wanaoishi leo ni wa aina moja na walitoka shina moja.” Hilo lathibitishwa hata na mamlaka moja mashuhuri. Biblia husema: “Mungu aliumba kila taifa la wanadamu kutoka katika mmoja wakae juu ya uso wa nchi yote.”—Matendo 17:26.
Taarifa hiyo ya UNESCO inaendelea hivi:
B “Mgawanyo wa aina ya kibinadamu katika visehemu vya ‘rangi za kijamii’ kwa sehemu ni wa kawaida tu na kwa sehemu hauna kanuni na kwa vyovyote haumaanishi kuna walio wa madaraja ya juu kuliko wengine. . . .
C “Ufahamu wa kibayolojia hauturuhusu kutia dhana za ufanisi wa utamaduni katika tofauti za uwezo wa vipokeza-tabia. Tofauti za matimizo ya watu tofauti zapaswa kuhesabiwa kuwa zatokana na historia yao ya kitamaduni. Jamii za watu wa ulimwengu leo zaonekana kuwa na uwezo sawa wa kimaumbile wa kufikia kiwango chochote cha ustaarabu.”
Madhara ya Kubagua Jamii Kirangi
Hivyo basi hakuna msingi wa kuamini kwamba jamii ya rangi yoyote ni bora kuliko nyingine au ina haki ya kutawala nyingine. Lakini si sikuzote ambapo watu wametenda kupatana na uhakika huo. Fikiria, kwa mfano, biashara ya watumwa Waafrika.
Mataifa ya Ulaya yalipoanza kuunda milki za kikoloni, ilikuwa ni kwa faida yao ya kiuchumi kuwatumia wenyeji vibaya. Lakini hapa palikuwa na kitendo chenye kujipinganisha. Mamilioni ya Waafrika walikuwa wakikokotwa kutoka nyumba zao, wakitenganishwa na wapendwa wao, wakifungwa minyororo, wakipigwa viboko, wakichomwa chapa za kutambulisha wao ni mali ya nani, wakiuzwa kama wanyama, na kulazimishwa kufanya kazi bila mshahara mpaka siku walipokufa. Hilo lingewezaje kutetewa kiadili na mataifa yaliyodai kuwa Wakristo ambayo yalipaswa kuwapenda jirani zao kama wao wenyewe?—Luka 10:27.
Suluhisho walilochagua ni kushushia majeruhi wao hadhi ya kibinadamu. Hivi ndivyo alivyosababu mchunguzi mmoja wa tabia na asili ya kibinadamu, katika miaka ya 1840:
“Kama Wanegro na Waustralia si viumbe wenzetu na wa familia moja na sisi wenyewe bali watu wa kiwango cha chini, na ikiwa wajibu wetu kwao haungefikiriwa sana . . . katika yoyote ya amri chanya ambazo ndizo msingi wa maadili ya ulimwengu wa Kikristo, uhusiano wetu na makabila haya utaonekana si tofauti sana na ule ambao ungeweza kuwaziwa kuwako baina yetu na jamii ya orangutani [sokwe].”
Wale wenye kutafuta kuunga mkono wazo la kwamba watu wasio weupe walikuwa wanadamu wa hali ya chini walichukua nadharia ya mageuzi ya Darwin. Walitoa hoja ya kwamba watu wa kikoloni walikuwa kwenye daraja la chini kuliko weupe katika ngazi ya mageuzi. Wengine walidai kwamba wasio weupe ni matokeo ya mwendo tofauti wa mageuzi na wao si wanadamu kamili.
Wengine walinukuu Biblia wakipotosha maandiko yaunge mkono maoni yao ya ubaguzi wa jamii za rangi nyingine.Bila shaka, watu wengi hawakukubali kufikiri kwa namna hiyo. Utumwa umefutiliwa mbali katika mataifa mengi ya ulimwengu. Lakini ubaguzi, upendeleo na kufikiri kwamba jamii moja ni bora yameendelea na kuenea kwenye vikundi vya makabila vilivyodhaniwa na watu tu kuwa ni jamii za rangi nyingine. Profesa mmoja wa utaalamu wa wanyama alisema hivi: “Kwa kuwa ingeonekana kwamba kila mtu ana haki ya kujifanyizia jamii za rangi mbalimbali ili kutosheleza mawazo yake, wanasiasa, watetezi maalumu na wavumbuzi wa kawaida wamejiingiza katika kupanga wanadamu vikundi vikundi. Waliunda vibandiko vya uwongo kuhusu jamii za rangi za watu ili kudumisha heshima ‘ya kisayansi’ eti, juu ya mawazo na maoni yao ya ubaguzi wayapendayo sana.”
Miongozo ya Ujerumani ya Nazi ya kubagua jamii za rangi nyingine ni kielelezo kizuri. Ijapokuwa Adolf Hitler alitukuza jamii ya rangi ya Kiarya, kibayolojia hakuna kitu kama hicho. Haikuwako kamwe. Kuna Wayahudi wenye ngozi nyeupe-kimanjano na macho buluu katika Uswedi, Wayahudi weusi katika Ethiopia, na Wayahudi Wamongoloidi katika Uchina. Ijapokuwa hivyo, Wayahudi na wengine walikuwa majeruhi wa mwongozo wa ubaguzi wa jamii ya rangi nyinginezo. Mwongozo huo ulielekeza kwenye kambi za mateso, vyumba vya gesi, na mauaji ya Wayahudi milioni sita na wengine wengi, kama jamii za watu Waslavu kutoka Polandi na Urusi.
[Blabu katika ukurasa wa 5]
Utafiti wa kisayansi umeonyesha kwamba katika kila idadi ya watu, kuna unamna ule ule wa uelewevu wa akili
[Blabu katika ukurasa wa 6]
‘Wanasiasa, viongozi maalumu, na wavumbuzi wa kawaida wameunda vibandiko vya uwongo kuhusu jamii za rangi za watu ili kudumisha heshima “ya kisayansi” eti, juu ya mawazo na maoni yao ya ubaguzi wayapendayo sana’
[Picha katika ukurasa wa 7]
Kama ilani hizi zionyeshavyo, Waafrika walitangazwa na kuuzwa kama kwamba walikuwa mifugo