Jamii Ni Nini?
JAMII! Neno hilo lakukumbusha nini? Kwa watu fulani lamaanisha ubaguzi na uonevu. Kwa wengine lamaanisha chuki, ghasia zenye jeuri, na hata uuaji wa kimakusudi.
Kuanzia ghasia zenye jeuri za ubaguzi wa jamii katika United States hadi ubaguzi wa rangi katika Afrika Kusini, kuanzia vita miongoni mwa vikundi vya kikabila katika Ulaya Mashariki hadi mapigano katika sehemu kama Sri Lanka na Pakistan—jamii imekuwa kisababishi kikuu cha mateseko na uharibifu mkubwa sana wa kibinadamu.
Lakini ni kwa nini mambo yako hivyo? Hata katika nchi ambazo watu huonekana kuruhusu kila kitu kingine, ni kwa nini jamii ni suala kubwa hivyo? Ni nini kinachofanya jamii iwe kichochezi cha mvurugo mkubwa na ukosefu wa haki? Tukitaja kwa maneno machache, ni kwa nini watu wa jamii tofauti-tofauti hawawezi kupatana?
Ili kujibu maswali hayo, twahitaji kujua zaidi juu ya maana ya jamii na pia njia ambazo jamii mbalimbali zatofautiana. Ni lazima pia tuelewe fungu la historia katika mahusiano ya wakati wa sasa ya jamii. Lakini, ebu kwanza tuone jambo ambalo sayansi inaweza kutueleza kuhusu habari hii.
Tatizo la Kuainisha Wanadamu
Watu wanaoishi katika sehemu tofauti za ulimwengu wana hali za kimwili zenye kutofautiana. Hayo yatia ndani rangi ya ngozi, umbo la uso, namna za nywele, na kadhalika. Tofauti hizo za kimwili hutofautisha jamii moja kutoka jamii nyingine.
Hivyo, kwa kawaida watu husema juu ya weupe na weusi, wakirejezea rangi ya ngozi. Lakini watu husema pia juu ya watu wa Kihispania, Waesia, Waskandinavia, Wayahudi, na Warusi. Vitambulisho hivyo vya mwisho havirejezei sana hali za kimwili bali vyarejezea tofauti za kieneo, kitaifa, au za kitamaduni. Kwa hiyo, kwa watu wengi zaidi, jamii haitambuliwi tu na hali za kimwili bali pia na desturi, lugha, utamaduni, dini, na taifa.
Ingawa hivyo, waandikaji fulani wanaoandika juu ya jamii huepuka kutumia neno “jamii”; wao huweka neno hilo katika alama za kunukuu kila wakati neno hilo litokeapo. Wengine huepuka kabisa neno hilo na badala yalo kutumia maneno kama “watu wa kabila fulani,” “vikundi,” “wakazi,” na “aina mbalimbali.” Kwa nini? Ni kwa sababu neno “jamii,” kama linavyoeleweka kikawaida, limejawa na maana nyingi na matumizi mengi hivi kwamba kutumiwa kwalo, bila ufafanuzi unaofaa, mara nyingi hakutokezi wazi jambo linalozungumzwa.
Kwa wanabiolojia na wanthropolojia, jamii mara nyingi hufasiliwa kuwa “kikundi kidogo cha aina ambayo hurithi hali za kimwili ambazo zakitofautisha na aina iyo hiyo ya wale wakazi wengine.” Lakini swali ni hili, ni hali zipi za kimwili zinazoweza kutumiwa katika kufafanua vikundi tofauti miongoni mwa aina ya binadamu?
Mambo kama vile rangi ya ngozi, rangi na namna ya nywele, umbo la macho na pua, ukubwa wa ubongo, na aina ya damu yamedokezwa, lakini hakuna hata jambo moja kati ya hayo ambalo limefaulu kabisa katika kuainisha aina mbalimbali za binadamu. Hiyo ni kwa sababu hakuna kikundi cha asili cha watu ambacho washiriki wacho wote wafanana kwa mambo hayo yote.
Ebu fikiria rangi ya ngozi. Watu wengi wanaamini kwamba ainabinadamu yaweza kugawanywa katika jamii tano kwa rangi ya ngozi: weupe, weusi, wenye rangi ya kunde, wenye rangi ya manjano, na wekundu. Jamii ya weupe kwa kawaida huonwa kuwa ina ngozi nyeupe, nywele zenye rangi hafifu, na macho ya buluu. Lakini, kwa kweli, kuna tofauti kubwa ya rangi za nywele, rangi ya macho, na rangi ya ngozi miongoni mwa washiriki wa ile inayoitwa jamii ya weupe. Kitabu The Human Species charipoti hivi: “Si kwamba tu hakuna vikundi vya watu katika Ulaya leo ambavyo wengi wa washiriki wavyo ni wa aina moja; hakujapata kamwe kuwa na vikundi vya aina hiyo.”
Kwa kweli, ni vigumu kuainisha aina ya binadamu, kama vile kitabu The Kinds of Mankind kisemavyo: “Inaonekana yote tuwezayo kusema ni haya: ingawa si binadamu wote wanaofanana na binadamu wengine wote, na ingawa tunaweza kuona kwa wazi njia nyingi ambazo watu watofautiana, wanasayansi bado hawakubaliani kabisa juu ya ni aina ngapi za binadamu zilizopo. Hata hawajaamua ni kanuni zipi tunazoweza kutumia katika kuorodhesha watu kuwa wa jamii hii au ile. Wanasayansi wengine wangependa kuacha utafiti huo na kusema kwamba hilo ni tatizo gumu sana—kwamba hakuna suluhisho!”
Mambo hayo yote huenda yakaonekana kuwa ya kushangaza. Ingawa ni wazi kwamba wanasayansi hawatatiziki sana kuainisha wanyama na mimea katika jamii, aina, na aina ndogo-ndogo, ni kwa nini wanatatizika kuainisha ainabinadamu katika jamii mbalimbali?
“Ngano ya Binadamu Iliyo Hatari Zaidi”
Kulingana na mwanthropolojia Ashley Montagu, watu wengi wanaamini kwamba “hali za kimwili na tabia za kiakili zahusiana, kwamba tofauti za kimwili zahusiana na tofauti kubwa za uwezo wa kiakili, na kwamba tofauti hizo zaweza kupimwa na mitihani ya kukadiria akili na matimizo ya kitamaduni ya wakazi hao.”
Hivyo, wengi wanaamini kwamba kwa sababu jamii mbalimbali zina hali tofauti za kimwili, jamii fulani-fulani ni bora kwa weledi na nyingine ni duni. Hata hivyo, Montagu akuita kufikiri huko kuwa “ngano ya binadamu iliyo hatari zaidi.” Wastadi wengine wakubali hivyo.
Morton Klass na Hal Hellman waeleza hivi katika kitabu The Kinds of Mankind: “Ni kweli watu mmoja-mmoja watofautiana; katika vikundi vyote vya wakazi kuna watu wenye akili sana na kuna wapumbavu. Lakini, baada ya utafiti wote, wanachuo wenye kutegemeka hawajaona uthibitisho wanaoweza kukubali wa kuwapo kwa tofauti za jeni [chembe za urithi] kati ya vikundi-vikundi vya watu kwa habari ya weledi au uweza.”
Lakini, ni kwa nini wengi wanaendelea kuamini kwamba tofauti za nje za kimwili zamaanisha kwamba jamii zatofautiana kimsingi? Kwa kweli, ni jinsi gani jamii ikaja kuwa suala kubwa hivyo? Tutazungumzia mambo hayo katika makala inayofuata.