Kwa Nini Jamii ni Suala Kubwa Hivyo?
TANGU mwanzo wa historia iliyorekodiwa, wazo la “wao” na “sisi” limefikiriwa sana na watu. Wengi wamejisadikisha kwamba wao tu ndio watu timamu wenye njia zinazofaa za kufanya kila kitu. Hilo ndilo jambo wanasayansi wanaloita ethnosentristi, wazo la kwamba kikundi cha mtu mwenyewe na njia zacho ndicho kikundi cha pekee chenye maana.
Kwa kielelezo, Wagiriki wa kale waliwadharau “barbarians” (yaani, washenzi), neno walilotumia kwa mtu yeyote ambaye hakuwa Mgiriki. Neno “barbarian” lilitokana na njia ambayo lugha za kigeni zilisikika kwa masikio ya Wagiriki, kama maneno mengi ya kishenzi “bar-bar.” Wamisri wa kabla ya Wagiriki na Waroma wa baadaye pia walihisi kuwa bora kuliko vikundi vya watu vilivyokuwa tofauti na wao.
Kwa karne nyingi Wachina waliiita nchi yao Zhong Guo, au Ufalme wa Katikati, kwa sababu walisadiki kwamba Uchina ulikuwa kitovu cha ulimwengu kama si kitovu cha ulimwengu wote mzima. Baadaye, wakati wamishonari wa Ulaya wenye nywele nyekundu, macho ya kijani-kibichi, rangi ya ngozi nyekundu walipokuja Uchina, Wachina waliwaita “maibilisi wa kigeni.” Vivyo hivyo, wakati watu wa nchi za Mashariki walipofika Ulaya na Amerika ya Kaskazini kwa mara ya kwanza, macho yao yaliyoinama na zile desturi zao zilizoonwa kuwa za kiajabu-ajabu ziliwafanya wadhihakiwe na kushukiwa kwa urahisi.
Lakini, kuna jambo la maana la kufikiria, kama vile kitabu The Kinds of Mankind kinavyosema: “Ni rahisi kwa mtu kuamini ubora wa [jamii] yao; lakini kujaribu kuthibitisha ubora huo, kwa kutumia magunduzi ya kisayansi, ni jambo gumu sana.” Jitihada za kujaribu kuthibitisha kwamba jamii moja ni bora kuliko nyingine ni za karibuni tu. Mwanthropolojia Ashley Montagu aliandika kwamba “wazo la kuwapo kwa jamii za kiasili au kibiolojia za ainabinadamu ambazo zatofautiana kiakili na pia kimwili ni wazo ambalo halikuwako mpaka sehemu ya mwisho ya karne ya kumi na nane.”
Ni kwa nini suala la ubora wa jamii lilikuja kutokea sana wakati wa karne za 18 na 19?
Biashara ya Kununua na Kuuza Watumwa na Jamii
Sababu kubwa ni kwamba kufikia wakati huo biashara ya kununua na kuuza watumwa yenye faida ilikuwa imefikia upeo wayo, na mamia ya maelfu ya Wafrika walikuwa wakichukuliwa kwa nguvu na kulazimishwa kuwa watumwa katika Ulaya na zile bara za Amerika. Mara nyingi familia zilivunjwa, wanaume, wanawake, na watoto wakipelekwa katika sehemu tofauti za ulimwengu, wasionane tena kamwe. Wafanya biashara ya kununua na kuuza watumwa na wenye kumiliki watumwa, ambao wengi kati yao walidai kuwa Wakristo, wangewezaje kutetea matendo ya kinyama kama hayo?
Kwa kuendeleza maoni ya kwamba Wafrika weusi walikuwa duni kiasili. “Naelekea kushuku kwamba weusi wote, na kwa ujumla aina zote za watu kuwa duni kiasili kuliko weupe,” akaandika mwanafalsafa Mskochi wa karne ya 18 David Hume. Kwa kweli, Hume alidai kwamba mtu hangeweza kupata “uvumbuzi wowote wenye akili miongoni mwa [Weusi], hakuna usanii, hakuna sayansi.”
Hata hivyo, madai hayo yalikuwa yenye kosa. The World Book Encyclopedia (1973) chaeleza hivi: “Falme za Weusi zenye maendeleo sana zilikuwapo katika sehemu kadhaa za Afrika mamia ya miaka iliyopita. . . . Kati ya [miaka] 1200 na 1600, chuo kikuu cha Weusi na Waarabu kilisitawi katika Timbuktu katika Afrika Magharibi na kilijulikana sana kotekote Uhispania, Afrika Kaskazini, na Mashariki ya Kati.” Hata hivyo, wale waliohusika katika biashara ya kununua na kuuza watumwa walikubali upesi maoni ya wanafalsafa kama Hume kwamba weusi walikuwa jamii duni kulinganishwa na weupe, kwa kweli watu ambao hata hawakuwa binadamu kamili.
Dini na Jamii
Wafanya biashara ya kununua na kuuza watumwa waliungwa mkono sana na viongozi wa kidini kwa ajili ya maoni ya ubaguzi wa jamii. Mapema sana kama miaka ya 1450, sheria za mapapa wa Roma Katoliki ziliidhinisha kutiisha na kutia utumwani “wapagani” na “makafiri” ili kwamba “nafsi” zao zipate kuokolewa kwa ajili ya “Ufalme wa Mungu.” Wakiwa wamepokea baraka za kanisa, wavumbuzi wa nchi wa mapema kutoka Ulaya na wafanya biashara ya kununua na kuuza watumwa hawakuhisi hatia yoyote juu ya ukatili waliowatendea wenyeji.
“Katika miaka ya 1760, kama ilivyokuwa kwa miongo mingi iliyofuata, utumwa wa watu weusi uliidhinishwa na wanadini na wanatheolojia wa Katoliki, Anglikana, Lutheri, Presbiteri, na Reformed,” chasema kitabu Slavery and Human Progress. “Hakuna kanisa la kisasa au farakano lililokuwa limejaribu kukataza washiriki walo wasimiliki wala hata kushiriki katika biashara ya kununua na kuuza watumwa weusi.”
Ingawa baadhi ya makanisa yalikuwa yakizungumzia udugu wa ulimwenguni pote wa Kikristo, hayo nayo yalifundisha mafundisho yaliyoendeleza suala la ubaguzi wa kijamii. Kwa kielelezo, Encyclopaedia Judaica chaeleza kwamba “ilikuwa baada tu ya mizozano mirefu na mazungumzo ya kitheolojia kwamba Wahispania wakatambua kuwa jamii za wenyeji walizokuta Amerika ni watu waliojaliwa kupewa nafsi.”
Lililomaanishwa ni kwamba maadamu “nafsi” za watu wa jamii hizo za wenyeji ‘ziliokolewa’ kwa kugeuzwa kuingizwa katika Ukristo, basi si kitu walivyotendewa kimwili. Na suala lilipohusu hali ya weusi, viongozi wengi wa kidini walibisha kwamba haidhuru kwa sababu wao walilaaniwa na Mungu. Maandiko yalitumiwa vibaya kujaribu kuthibitisha jambo hilo. Makasisi Robert Jamieson, A. R. Fausset, na David Brown, katika kitabu chao cha maelezo ya Biblia, wakazia hivi: “Na alaaniwe Kanaani [Mwanzo 9:25]—hukumu hiyo imetimizwa kwa kuharibiwa kwa Wakanaani—kwa kushushwa hadhi kwa Misri, na utumwa wa Wafrika, wazao wa Hamu.”—Commentary, Critical and Explanatory, on the Whole Bible.
Fundisho la kwamba babu ya jamii ya weusi alilaaniwa halifundishwi katika Biblia hata kidogo. Ukweli ni kwamba jamii ya weusi ilitokana na Kushi, wala si na Kanaani. Katika karne ya 18, John Woolman alibisha kwamba kutumia laana hiyo ya Biblia katika kutetea kutia weusi utumwani, na hivyo kuwanyang’anya haki zao za asili, “ni dhana mbaya mno ambayo haipasi kuruhusiwa iingie katika akili ya mtu yeyote anayetaka kwa moyo mweupe kuongozwa na kanuni thabiti.”
Sayansi-Bandia na Jamii
Sayansi-bandia pia ilichangia jitihada ya kuunga mkono nadharia ya kwamba weusi ni jamii duni. Kitabu Essay on the Inequality of Races, kilichoandikwa na mwandikaji Mfaransa wa ka-rne ya 19, Joseph de Gobineau, kiliwekea msingi vitabu vingine kama hivyo ambavyo vingefuata. Katika kitabu hicho, Gobineau aligawanya ainabinadamu katika jamii tatu tofauti kuanzia na ile bora zaidi kuja chini: weupe, wenye rangi ya kimanjano, na weusi. Alidai kwamba sifa za pekee za kila jamii zilikuwa katika damu na kwa hiyo mchanganyiko wowote wa ndoa baina ya jamii tofauti ungetokeza mshuko wa ubora na kupoteza sifa bora.
Gobineau alibisha kwamba wakati mmoja kulikuwa na jamii bora halisi ya watu weupe, warefu, wenye nywele nyeupe na macho ya buluu ambao aliwaita Waaria. Alitoa hoja kwamba Waaria ndio walioleta katika India ustaarabu na lugha ya Sanskrit, na kwamba ni Waaria walioanzisha staarabu za Ugiriki na Roma za kale. Lakini kupitia ndoa baina yao na wenyeji waliokuwa duni, staarabu hizo ambazo wakati mmoja zilikuwa zenye utukufu zilipotea, pamoja na akili nyingi na sifa zilizo nzuri za jamii ya Waaria. Watu waliobaki bado wenye kukaribiana zaidi na Waaria halisi, akasisitiza Gobineau, wangeweza kupatikana katika kaskazini mwa Ulaya, yaani, miongoni mwa Wanordi na, kwa njia fulani, watu wa Kijerumani.
Mawazo ya msingi ya Gobineau—ile migawanyo mitatu ya jamii, uzao wa damu, jamii ya Waaria—hayakuwa kamwe na msingi wowote wa kisayansi, na yamekataliwa kabisa na jumuiya ya kisayansi leo. Hata hivyo, maoni hayo yalikubaliwa upesi na watu wengine. Miongoni mwa hao alikuwa Mwingereza, Houston Stewart Chamberlain, aliyependezwa sana na mawazo ya Gobineau hivi kwamba akaamua kuishi katika Ujerumani na kutetea wazo la kwamba ni kupitia Wajerumani tu ambapo kuna tumaini la kuhifadhi ubora wa jamii ya Waaria. Kwa wazi, maandishi ya Chamberlain yakaja kusomwa zaidi katika Ujerumani, na matokeo yalikuwa yenye kuchukiza.
Matokeo Yenye Kuchukiza ya Ubaguzi wa Kijamii
Katika kitabu chake Mein Kampf (Jitihada Yangu), Adolf Hitler alisisitiza kwamba jamii ya Kijerumani ilikuwa ndiyo jamii bora zaidi ya Kiaria iliyokusudiwa itawale ulimwengu. Hitler alihisi kwamba Wayahudi, aliowalaumu kuharibu uchumi wa Ujerumani, walikuwa kikwazo katika kusudi hilo tukufu. Hivyo, kuangamizwa kwa Wayahudi na vikundi vingine vidogo vya watu katika Ulaya kukafuata, tendo ambalo bila shaka lilikuwa moja kati ya vipindi vyenye huzuni zaidi katika historia ya binadamu. Hayo yalikuwa ndiyo matokeo yenye msiba ya mawazo ya ubaguzi wa kijamii, kutia ndani yale ya Gobineau na Chamberlain.
Hata hivyo, chukizo hilo halikutokea katika Ulaya pekee. Ng’ambo ya bahari katika ule ulioitwa ulimwengu mpya, mawazo kama hayo yasiyo na msingi yalileta mateso makubwa kwa vizazi vya watu wasio na hatia. Ingawa hatimaye watumwa wa Kiafrika waliachiliwa katika United States baada ya Vita ya Wenyewe kwa Wenyewe, sheria zilizozuia weusi wasiwe na mengi kati ya mapendeleo ambayo wakazi wengine walifurahia zilipitishwa. Kwa nini? Wakazi weupe walifikiria kwamba jamii ya weusi haikuwa na akili ya kutosha kuweza kushiriki katika kazi za jamii na za serikali.
Jinsi hisia hizo za ubaguzi zilivyoimarika yaonyeshwa na kesi moja iliyohusu sheria iliyokataza ndoa baina ya weupe na watu wa jamii nyingine. Sheria hiyo ilikataza ndoa kati ya weusi na weupe. Hakimu mmoja alisema hivi katika kuhukumu mume na mke waliovunja sheria hiyo: “Mungu Mwenye Uweza Wote aliziumba jamii zikiwa nyeupe, nyeusi, zenye rangi ya manjano, Kimalei, nyekundu, Naye akaziweka katika mabara tofauti, na kama isingalikuwa ni kwa ajili ya kuingiliana na mpango Wake, hakungalikuwa sababu kuwapo kwa ndoa hizo.”
Hakimu huyo alisema hayo, si katika karne ya 19 na si katika eneo la mashambani, bali katika 1958—na si umbali wa kilometa zenye kuzidi 100 kutoka kwenye Jumba la Kutungia sheria la U.S.! Kwa kweli, sheria zote zilizokataza ndoa za jamii tofauti hazikuondolewa mpaka 1967 wakati Mahakama Kuu Zaidi ya U.S. ilipozibatilisha.
Sheria hizo zenye kubagua—na vilevile ubaguzi katika shule, makanisa, na sehemu nyingine za umma na ubaguzi katika kuajiri na makao—zilileta mvurugo wa raia, mateto, na jeuri, mambo ambayo yamekuwa uhalisi wa maisha katika United States na sehemu nyingine nyingi. Hata mtu asipofikiria uharibifu wa uhai na mali, ule uchungu, chuki, na watu binafsi kushushiwa heshima na mateso ambayo yametokea yaweza tu kuwa aibu na fedheha ya ile inayoitwa eti jumuiya ya watu waliostaarabika.
Hivyo, ubaguzi wa kijamii umekuwa moja kati ya kani zenye kugawanya zaidi zinazokumba jumuiya ya kibinadamu. Kwa kweli, yafaa sisi sote tutafute yaliyo mioyoni mwetu, tukijiuliza hivi: Je! nakataa mafundisho yoyote yatangazayo jamii moja kuwa bora kuliko nyingine? Je! nimejitahidi kuondoa kabisa masalio yoyote yanayoweza kuwa yamebaki ndani yangu ya hisia ya ubora wa kijamii?
Pia yaafaa tujiulize hivi: Kuna tumaini gani kwamba uonevu wa kijamii na mzozano, ambao umeenea sana leo, utapata kuondolewa kabisa? Je! watu wa mataifa tofauti, lugha mbalimbali, na desturi zilizo tofauti waweza kuishi pamoja kwa amani?
[Picha katika ukurasa wa 7]
Weusi walionwa na weupe wengi kuwa si binadamu kamili.
[Hisani]
Imenakiliwa kutoka DESPOTISM—A Pictorial History of Tyranny
[Picha katika ukurasa wa 8]
Kambi za maangamizo za Nazi zilikuwa ni matokeo yenye msiba ya mawazo ya ubaguzi wa kijamii
[Hisani]
Picha ya U.S. National Archives