Utawala wa Kibinadamu Wapimwa Katika Mizani
Sehemu ya 9: Utawala wa Kibinadamu Wafikia Upeo Wao!
Mifumo ya kisiasa ya mataifa yote: milki, mashirika, miungano ya kirafiki, au urafiki unaofanyizwa kati ya mataifa kwa muda mfupi au kwa kudumu katika kufuatia miradi ile ile inayopita mipaka ya kitaifa, mamlaka, au mapendezi.
SIKU ya Oktoba 5, 539 K.W.K., ilipata jiji la Babuloni likiwa katika sherehe. Maofisa wa serikali elfu moja wa vyeo vya juu zaidi walikuwa wamekubali mwaliko wa jioni kutoka kwa Mfalme Belshaza. Wajapotishwa na majeshi ya Umedi na Uajemi, waliokuwa wakizingira jiji, Belshaza na wanasiasa wenzake hawakutishwa. Kwa vile, kuta za jiji hazingeweza kupitika. Hakukuwa na sababu yoyote ya kuhofu wakati huo.
Kisha, bila onyo, sherehe hizo zilipokuwa zikiendelea, vidole vya mkono wa mtu usio na mwili vilianza kuandika maneno ya kuogofya kwenye ukuta wa jumba la kifalme: MENE, MENE, TEKELI, na PERESI. Magoti ya mfalme yakaanza kutetemeka, naye akabadilika sura.—Danieli 5:5, 6, 25.
Danieli, Mwisraeli na mwabudu wa Mungu ambaye Belshaza na wenzi wake wa serikali walidharau, aliitwa ili aeleze maandishi hayo. “Na tafsiri ya maneno haya ni hii; “Danieli akaanza, “MENE, Mungu ameuhesabu ufalme wako na kuukomesha. TEKELI, umepimwa katika mizani nawe umeonekana kuwa umepunguka. PERESI, ufalme wako umegawanyika, nao wamepewa Waamedi na Waajemi.” Kwa wazi unabii huo haukutabiri mazuri. Kwa kutimizwa, “usiku uo huo Belshaza, mfalme wa Wakaldayo, akauawa.”—Danieli 5:26-28, 30.
Kwa usiku mmoja, aina moja ya utawala wa kibinadamu ulibadilishwa na mwingine! Kwa kufikiria msukosuko wa kisiasa unaofanana na huo katika Ulaya Mashariki, twaweza kujiuliza kama yaliyompata Belshaza yanaweza kuwa na umaana katika siku zetu. Je, matukio hayo yaliweza kuwa ishara ya mambo yatakayotokea kwa utawala wa kibinadamu wote? Tuna kila sababu ya kufikiria jambo hilo kwa uzito, kwa sababu “staarabu nzima nzima huangamia,” asema profesa Jacques Barzun wa Chuo Kikuu cha Columbia, akiongezea hivi: “Miisho yenye kushtua ya Ugiriki na Rumi si hekaya.”
Binadamu wamebuni kila aina ya serikali iwezayo kuwaziwa. Baada ya maelfu ya miaka ya kujaribia, matokeo yamekuwa nini? Je, utawala wa kibinadamu umekuwa wenye kuridhisha? Je! utawala wa kibinadamu unaweza kuandaa masuluhisho kwa matatizo ya kibinadamu yanayoongezeka?
Ahadi, Ahadi!
Jibu linatolewa kwa sehemu na Bakul Rajni Patel, mkurugenzi wa kitovu cha utafiti ulio maarufu katika Bombay, India. Akishtaki wanasiasa kwa “unafiki kamili,” mwanamke huyo asema: “Ni jambo la kawaida katika India na mataifa mengine ya Ulimwengu wa Tatu, kuona viongozi wakisimama jukwaani na kusema kwa maneno ya madoido yasiyo na maana juu ya ‘ukuzi’ na ‘maendeleo.’ Ukuzi na maendeleo gani? Tunadanganya nani? Ni kwa kuangalia tu takwimu za kutisha zinazohusu mataifa ya Ulimwengu wa Tatu: watoto 40,000 hufa kila siku kutokana na maradhi yanayoweza kuzuiliwa.” Mwanamke huyo aongezea kwamba angalau watoto milioni 80 hawana chakula cha kufaa mwili au huenda kulala wakiwa na njaa kila usiku.
‘Lakini hebu ngoja kidogo,’ huenda ukateta. ‘Angalau wape sifa wanasiasa kwa kujaribu. Aina fulani ya serikali inahitajika ikiwa matatizo mazito yanayokabili ulimwengu yatatatuliwa.’ Hiyo ni kweli, lakini swali ni: serikali hiyo yapaswa iwe imefanyizwa na mwanadamu au na Mungu?
Usitupilie mbali swali hilo kwa kuliona kuwa la ujinga, ukiwazia, kama vile wengi huwazia, kwamba Mungu huchagua kutojiingiza. Papa John Paul 2 kwa wazi pia afikiria kwamba Mungu ameacha binadamu wajitawale wenyewe kwa kadiri ile wawezavyo, kwa vile alipokuwa akizuru Kenya miaka kumi iliyopita, alisema hivi: “Mwito wa ushindani mkuu kwa Mkristo ni ule wa maisha ya kisiasa.” Yeye aliendelea kusema: “Raia wana haki na wajibu wa kushiriki kisiasa katika taifa. . ..Ingekuwa ni kosa kufikiri kwamba Mkristo mmoja mmoja hapaswi kujiingiza katika maeneo kama hayo ya maisha.”
Binadamu, wakifuatia nadharia hiyo, na mara nyingi wakiungwa mkono na dini, wametafuta serikali kamilifu kwa muda mrefu. Kila aina mpya ya serikali huja na ahadi zenye uzuri ajabu. Lakini hata ahadi zilizo bora zaidi huchukiza zisipotimizwa. (Ona “Ahadi Mbalimbali kwa Kulinganisha na Mambo ya Hakika” katika ukurasa wa 13) Kwa wazi basi, binadamu hawajapata serikali inayofaa.
Kujitwika Pamoja
Je! mwanasayansi wa nyukilia Harold Urey alikuwa na suluhisho? Yeye alibisha kwamba “hakuna suluhisho lenye kufaa kwa matatizo ya ulimwengu isipokuwa hatimaye kuwe na serikali ya ulimwenguni pote yenye uwezo wa kuweka sheria duniani pote.” Lakini si kila mtu ana uhakika kamili kwamba suluhisho hilo linaweza kufanya kazi. Katika muda uliopita, ushirikiano wenye kufaulu kati ya wanachama wa mashirika ya kimataifa ulikuwa hauwezekani. Hebu ona mfano mmoja wenye kutokeza.
Baada ya Vita ya Ulimwengu ya 1, katika Januari 16, 1920, shirika la kimataifa, liitwalo Ushirika wa Mataifa, ulisimamishwa, mataifa 42 yakiwa wanachama. Badala ya kufanyizwa uwe serikali ya ulimwengu, ulikusudiwa uwe bunge la dunia, ukifanyizwa uendeleze umoja wa ulimwenguni, hasa kwa kutatua magomvi ya mataifa yanayojitawala, na hivyo kuzuia vita. Kufikia 1934, mataifa wanachama yalikuwa yameongezeka kuwa 58.
Hata hivyo, Ushirika huo ulifanyizwa kwa msingi usio imara. “Vita ya Ulimwengu 1 ilimalizika huku kukiwa na matazamio mazuri, lakini kuvunjika moyo ndiko kulikofuatia,” yaeleza The Columbia History of the World. “Matumaini yaliyowekewa ule Ushirika wa Mataifa yakawa ndoto tu.”
Katika Septemba 1, 1939, Vita ya Ulimwengu 2 ikaanza, ikiingiza Ushirika huo katika hali ya kutotenda. Ingawa haukuvunjwa rasmi hadi Aprili 18, 1946, ulikufa kwa nia yote na makusudi, ukiwa “tineja,” hata bila kufikia umri wa miaka 20. Kabla ya kusahauliwa kwalo, tayari mahali palo palikuwa pamechukuliwa na shirika lingine la kimataifa, Umoja wa Mataifa, uliofanyizwa Oktoba 24, 1945, ukiwa na mataifa 51 wanachama. Jaribio hilo la kujitwika upya liliendeleaje?
Jaribio la Pili
Watu wengine husema kwamba Ushirika huo haukufaulu kwa sababu ulikuwa na kasoro katika muundo. Oni lingine halilaumu Ushirika huo ila linalaumu serikali moja moja ambazo hazikupendelea kuupa ule Ushirika utegemezo unaofaa. Bila shaka kuna ukweli katika maoni hayo mawili. Kwa vyovyote vile, waanzilishi wa Umoja wa Mataifa walijaribu kujifunza kutokana na uhafifu wa ule Ushirika na kurekebisha udhaifu mbalimbali ulioonyeshwa na ule Ushirika.
Mwandikaji R. Baldwin ataja Umoja wa Mataifa kuwa “bora kushinda ule Ushirika wa zamani katika uwezo wake wa kufanyiza utaratibu wa amani ya ulimwenguni, ushirikiano, sheria, na haki za kibinadamu.” Kwa kweli, baadhi ya mashirika yalo yanayoshughulika na mambo hususa, yakiwemo miongoni mwayo WHO (Shirika la Afya Ulimwenguni), UNICEF (Hazina ya Umoja wa Mataifa kwa Watoto), na FAO (Shirika la Chakula Ulimwenguni), yamefuatia miradi mizuri na kufaulu kadiri fulani. Tena unaoelekea kuonyesha kwamba usemi wa Baldwin ni sahihi ni ule uhakika wa kwamba Umoja wa Mataifa umekuwa ukitenda kwa miaka 45, zaidi ya mara mbili kushinda ule Ushirika wa zamani.
Timizo kuu la Umoja wa Mataifa lilikuwa ni katika kuharakisha kukomeshwa kwa ukoloni, angalau ukiufanya ukoloni uwe “na taratibu mzuri kidogo kuliko vile ungalikuwa,” hilo ni kulingana na mwandishi wa gazeti Richard Ivor. Pia adai kwamba shirika hilo “lilisaidia kupunguza vita baridi vikawa vita vya maneno matupu.” Naye asifu “kigezo cha kufanya kazi kwa ushirika” ambacho Umoja wa Mataifa ulishiriki kufanyiza.
Bila shaka, wengine hubisha kwamba tisho la vita ya nyukilia lilifanya mengi kushinda Umoja wa Mataifa katika kuzuia Vita Baridi. Badala ya kuweka ahadi inayofanyiza jina lake, yaani kuunganisha mataifa, ukweli ni kwamba shirika hilo kwa upande mkubwa halijafanya lolote ila tu kuwa kama mtu wa kati, likijaribu kuzuia mataifa yasiyosikilizana yasivamiane. Na hata katika hali hiyo ya kuwa mwamuzi, halijafanikiwa sikuzote. Kama aelezavyo mwandishi Baldwin, kama ulivyo na ule Ushirika wa zamani, “Umoja wa Mataifa hauna uwezo wa kufanya mambo mengi zaidi ya yale yanayoruhusiwa na taifa linaloshtakiwa.”
Utegemezo huu wa moyo nusu nusu kwa upande wa wanachama wa UM wakati mwingine huonyeshwa kwa kutopendelea kwa wanachama kutoa pesa za kuendeleza shirika hilo. Kwa mfano, United states, ilikataa kutoa malipo yake kwa Shirika la Chakula Ulimwenguni kwa sababu ya maazimio yaliyoonekana kwamba yanachambua Israeli na kupendelea Palestina. Baadaye, United States ikiwa mtegemezaji mkubwa wa UM kifedha ilikubali kulipa kiasi cha kutoshea tu kuhifadhi uanachama wake lakini iliacha theluthi mbili ya deni yake bila kulipwa.
Aliyekuwa naibu mkurugenzi wa UNICEF, Varindra Tarzie Vittachi, aliandika katika 1988 kwamba akataa “kujiunga na harakati ya kushutumu” ya wale wanaopinga Umoja wa Mataifa. Ingawa ajiita “mchambuzi mwaminifu,” yeye akiri kwamba mashambulizi mengi yanafanywa na watu wasemao kwamba “Umoja wa Mataifa ni ‘nuru iliyokataa kuwaka,’ haujatenda kulingana na viwango vyake vya juu, kwamba umeshindwa kutekeleza kazi yao ya kuhifadhi amani na kwamba kukiwa na mashirika ya kuleta maendeleo yanayofanya vizuri, mengi hayajathibitisha ni kwa sababu gani yalifanyizwa.”
Udhaifu mkubwa zaidi wa Umoja wa Mataifa wafunuliwa na mwandishi Ivor, aandikapo hivi: “UM hata uweze kufanya nini kinginecho, hautaondoa dhambi. Ingawa unaweza kufanya kutenda makosa ya kimataifa kuwe kugumu na utafanya mtenda makosa alipie makosa yake. Lakini haujafaulu bado kugeuza mioyo na akili za ama viongozi wa nchi au wananchi.”— Italiki ni zetu.
Hivyo, upungufu wa Umoja wa Mataifa ndio upungufu ule ule wa aina zote za utawala wa kibinadamu. Hakuna ile iwezayo kutia ndani ya mioyo ya watu upendo wa mema usio na ubinafsi, kuchukia mabaya, na heshima kwa mamlaka, mambo ambayo ni ya lazima kwa mafanikio. Fikiria ni matatizo mangapi ya tufeni pote yangeweza kutatuliwa ikiwa watu wangekuwa na nia ya kuongozwa na viwango vya uadilifu! Kwa mfano, ripoti moja ya habari inayohusu uchafuzi katika Australia, yasema kwamba tatizo hilo lipo “si kwa sababu kwamba watu hawajui wanalofanya, bali kwa sababu ya mielekeo ya mioyo.” Ikiita pupa kuwa sababu kuu ya uchafuzi, makala hiyo yasema kwamba “mwongozo wa serikali umeongezea matatizo hayo ya uchafuzi.”
Wanadamu wasiokamilika hawawezi kamwe kufanyiza serikali kamilifu. Kama vile alivyotaja mwandikaji Thomas Carlyle katika 1843: “Kila serikali mwishowe hufananisha watu wake, katika hekima yao na upumbavu wao.” Ni nani awezaye kubishana na hoja yenye akili kama hiyo?
‘Kuvunjwa Vipande Vipande!’
Upeo wa utawala wa kibinadamu umefikiwa sasa, katika karne hii ya 20. Serikali za kibinadamu zimefanya mapatano ya pamoja yenye hila, yasiyo na haya na yenye kuasi dhidi ya utawala wa kimungu ambayo hayajapata kuwepo. (Linganisha Isaya 8:11-13.) Zimefanya hivyo, si mara moja tu, bali mara mbili, kwanza wakifanyiza ule Ushirika wa Mataifa na baadaye Umoja wa Mataifa. Ufunuo 13:14, 15 huiita mifanyizo hiyo “mfano wa hayawani-mwitu.” Jina hilo linafaa kwa sababu ni mfano wa mfumo wote wa kisiasa wa kibinadamu duniani. Kama hayawani-mwitu halisi, visehemu vya mfumo huo wa kisiasa vimevamia wakaaji wa dunia na kusababisha madhara yasiyoelezeka.
Ule Ushirika ulikwisha kwa msiba katika 1939. Mwisho uo huo wangojea Umoja wa Mataifa kwa utimizo wa unabii huu wa Biblia: “Jikazeni viuno, nanyi mtavunjwa vipande vipande; jikazeni viuno, nanyi mtavunjwa vipande vipande. Fanyeni shauri pamoja, nalo litabatilika!”— Isaya 8:9, 10.
Ni lini ambapo kuvunjwa-vunjwa kwa mwisho kwa “mfano wa hayawani-mwitu,” pamoja na kifananishi chake mfumo wa utawala wa kibinadamu, kutatokea? Ni lini ambapo Yehova ataumaliza utawala wa kibinadamu unaopinga enzi kuu yake? Biblia haitoi tarehe kamili, lakini unabii wa Biblia pamoja na matukio ya ulimwengu yasema: ‘Karibuni sana.’—Luka 21:25-32.
Mwandiko uliopo ukutani upo uonekane na wale wanaotaka kuuona. Kama vile kwa kweli Ufalme wa Belshaza ulipimwa katika mizani na kupatikana umepungukiwa, kwa hakika ndivyo ilivyo na utawala wa kibinadamu ambao umehukumiwa na kupatikana umepungukiwa. Utawala wa kibinadamu huachilia ufisadi wa kisiasa, huchochea vita, huendeleza unafiki na ubinafsi wa kila aina na huwa haushughuliki kuandalia wafuasi wao makao ya kufaa, chakula, shule, na utunzaji wa afya.
Utawala wa kibinadamu utowekapo, utatoweka kana kwamba ni kwa usiku mmoja. Upo leo, kesho katoweka—ubadilishwe na Ufalme wa Mungu, hatimaye serikali kamilifu!
[Sanduku katika ukurasa wa 13]
Ahadi Mbalimbali kwa Kulinganisha na Mambo ya Hakika
Serikali za Uanarki huahidi uhuru kamili usio na mipaka; ukweli wa mambo ni kwamba pasipo na serikali hakuna sheria au kanuni ambazo watu mmoja mmoja wanaweza kufuata kwa manufaa ya wao kwa wao; uhuru usio na mipaka husababisha ghasia.
Serikali za Umonarki huahidi udhibiti na umoja chini ya utawala wa kiongozi mmoja; ukweli wa mambo ni kwamba watawala wa kibinadamu, wakiwa na maarifa kidogo, wakipungukiwa na kutokamilika pamoja na udhaifu mbalimbali, labda hata wakiongozwa na tamaa mbaya, wenyewe hufa; kwa hiyo udhibiti na umoja wowote ule hautadumu.
Serikali za Aristokrasi huahidi kuandaa watawala bora zaidi; ukweli ni kwamba wanatawala kwa sababu wana mali, wametokana na ukoo fulani, au wana mamlaka, lakini si lazima iwe kwa sababu ya kwamba wana hekima, muono wa ndani, au upendo na kuhangaikia wengine; mtawala asiyestahili wa monarki hubadilishwa tu na watawala wengi walio bora wa aristokrasi.
Serikali za Demokrasi huahidi kwamba watu wote wanaweza kuamua jambo kwa manufaa ya wote; ukweli wa mambo ni kwamba wananchi hukosa maarifa na nia nzuri inayohitajika ili kufanya maamuzi mazuri kila wakati kwa manufaa ya wote; Plato aliieleza demokrasi kuwa “aina ya serikali yenye kupendeza, ikijawa na mambo mengi ya kuchagua na ukosefu wa utaratibu, na kutoa aina fulani ya usawa, kwa wenye usawa na wasio na usawa.”
Serikali za Autokrasi huahidi kutimiza mambo na tena kwa uharaka sana; ukweli ni kwamba, kama anavyoandika mwandishi wa gazeti Otto Friedrich, “hata watu wenye nia bora kabisa, wanapoingia katika uwanja wa mamlaka ya kisiasa, hujikabili na uhitaji wa kuongoza mambo ambayo kwa hali ya kawaida, wangeyaita yasiyo ya adili”; hivyo waautokrasi “wema” hugeuka kuwa wenye kutafuta mamlaka walio tayari kudhabihu mahitaji ya wananchi wao kwa sababu ya tamaa ya kibinafsi au faida yao.
Serikali za Kifashisti huahidi kuongoza uchumi kwa wema wa wote; ukweli ni kwamba wao hufanya hivyo bila kufanikiwa sana na kwa kudhabihu uhuru wa kibinafsi; kwa kutukuza vita na utaifa, hizo hufanyiza majitu ya kisiasa kama Italia chini ya Mussolini na Ujerumani chini ya Hitler.
Serikali za Kikomunisti huahidi kutengeneza serikali kamilifu isiyoweza kupatikana, isiyo na tabaka za jamii huku wananchi wakifurahia usawa kamili mbele ya sheria; ukweli wa mambo ni kwamba tabaka za jamii na ubaguzi bado upo na kwamba wanasiasa wafisadi hunyonya mtu wa kawaida; matokeo yamekuwa ni wengi kukataa wazo la ukomunisti huku zikitishwa kuvunjwa na harakati za kutukuza utaifa na zile za kujitenga.
[Sanduku katika ukurasa wa 13]
Kuhusu Umoja wa Mataifa
◼Kufikia sasa UM una wanachama 160. Nchi ziwezazo kutajwa ambazo si wanachama ni zile Korea mbili na Uswisi; Watu wa Uswisi walipoombwa maoni yao katika Machi 1986 kuhusu kujiunga na UM walipinga wazo hilo kwa kiasi cha 3 kwa 1.
◼Mbali na shirika lenyewe, UM unaendesha mashirika ya kipekee mengine 55, matengenezo ya kipekee, tume za kupigania haki za kibinadamu, na hatua za kuhifadhi amani.
◼Kila taifa ambalo ni mwanachama wa UM huwa na kura moja katika Baraza la UM, na huku Uchina ambayo ina watu wengi zaidi, ina wananchi 22,000 kwa kila mmoja wa mwananchi wa taifa ambalo lina watu wachache zaidi, St. Kitts na Nevis.
◼Mwaka wa Amani ya Kimataifa wa Umoja wa Mataifa ulipokuwa ukiadhimishwa katika 1986, kulikuwa na vita 37 vya kutumia silaha, zaidi ya wakati mwingine wowote tokea mwisho wa Vita ya Ulimwengu ya 2.
◼Kwa mataifa yote yaliyo wanachama wa UM, asilimia 37 ya hayo yana wananchi wachache zaidi kushinda lile “taifa” lenye umoja la kimataifa la Mashahidi wa Yehova; asilimia 59 ya wanachama hao wana wananchi wachache kushinda wale waliohudhuria mwadhimisho wa Ukumbusho wa kifo cha Yesu mwaka jana.
[Picha katika ukurasa wa 14]
Kumekuwa ni kupita uwezo wa wanadamu wasiokamilika kuandaa serikali kamilifu.
Ushirika wa Mataifa
Umoja wa Mataifa