Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g92 3/8 kur. 3-4
  • Ni Nini Kinachotendeka Kwenye Umoja wa Mataifa?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Ni Nini Kinachotendeka Kwenye Umoja wa Mataifa?
  • Amkeni!—1992
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Ni Nini Kilicholeta Badiliko Hilo?
  • Kuwa na Maoni Halisi
  • Umoja wa Mataifa—Njia Bora Zaidi?
    Amkeni!—1992
  • Amani na Usalama Kutoka Chanzo Gani?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1985
  • Miaka 50 ya Jitihada Zilizoshindwa
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1995
  • Mipango ya Mwanadamu kwa Ajili ya Usalama wa Kimataifa
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1992
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1992
g92 3/8 kur. 3-4

Ni Nini Kinachotendeka Kwenye Umoja wa Mataifa?

JAMBO fulani linatendeka kwenye Umoja wa Mataifa. Matukio ya kugutusha yanatokea ambayo yataathiri wakati ujao wako. Viongozi wa ulimwengu wanatazamia mema mengi kuhusu matukio hayo. Fikiria maneno yao:

“Miaka arubaini na mitano tangu kuzaliwa kwao, baada ya kuwa usiotenda kwa muda mrefu, [Umoja wa Mataifa] unajifunua mbele ya macho yetu, na sasa unajitokeza kama hakimu wa kweli, ukijulisha wazi sheria na kujitahidi kuifikiliza.”—Rais François Mitterrand wa Ufaransa kwenye mkutano wa 45 wa Baraza Kuu la UM, Septemba 24, 1990.

Katika mkutano uu huu, Eduard Shevardnadze aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Kigeni wa Urusi alisema kwamba “mtu hawezi kukosa kuridhishwa na umoja usio na kifani wa Baraza la Usalama la [UM] . . . Misimamo iliyochukuliwa na washiriki wa Shirika la [Umoja wa Mataifa] inapatia Baraza la Usalama mamlaka ya kutafuta amani ya ulimwengu kwa kadiri itakavyohitajika.”

Siku chache baadaye, Rais George Bush wa United States alihutubia Baraza Kuu la UM. Mabadiliko aliyoona yalimsukuma kusema: “Tangu 1945 hatujaweza kuona uwezekano halisi wa kutumia Umoja wa Mataifa kama ulivyofanyizwa kuwa—kitovu cha usalama wa kimataifa kwa jumuiya nzima.” Alisema hayo kwa sababu “Umoja wa Mataifa uliitikia kwa umoja na kwa azimio lenye kuvutia isivyo kawaida” kuelekea hali ya hatari ya Ghuba ya Uajemi. “Kwa mara ya kwanza, Baraza la Usalama la U.M. linaanza kutenda kama lilivyofanyizwa ili kutenda.” Alisema pia kwamba: “Umoja wa Mataifa unaweza kusaidia kuleta siku mpya” ikiwa washiriki wake ‘wanaacha nyuma silaha hatari sana.’ Kwa kufanya hivyo, wanaweza kukamilisha “harakati yenye kuvutia isivyo kawaida kuelekea utengemano mpya wa ulimwengu na enzi ndefu ya amani.”

Bw. Guido de Marco, msimamizi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, alikuwa na matazamio mema kama hayo. Alitangaza hivi kwa uchangamfu: “Mwanzo wa mfumo mpya wenye msingi wa urafiki na ushirikiano kati ya serikali zenye nguvu uko karibu. . . . Matukio hayo yametia Shirika la Umoja wa Mataifa nguvu mpya.” Alisema kwamba “daraka la Baraza Kuu kama kitovu cha maana cha majadiliano ya kitaifa na makusudio, limesisitizwa tena katika njia ya kuvutia.” Kwa sababu hii, aliendelea kusema: “Ulimwengu haumo tena chini ya kivuli cha uwezekano wa Harmagedoni yenye kutokezwa na mashindano ya kimawazo.”

Yalikuwa nini “matukio hayo” yaliyokweza Umoja wa Mataifa kwenye hali hii iliyotumainiwa kwa muda mrefu ya ufanisi na uvutano? Ni nini kilichoanzisha matazamio mema hayo yaliyofanya watawala wa ulimwengu kusema kwa matumaini juu ya “utengemano mpya wa ulimwengu na enzi ndefu ya amani” bila hatari ya Harmagedoni ya kinyukilia?

Ni Nini Kilicholeta Badiliko Hilo?

“Mwisho wa vita baridi [katika Ulaya],” akajibu Katibu-Mkuu wa UM Javier Pérez de Cuéllar katika ripoti yake ya 1990 ya kazi ya Umoja wa Mataifa. Kwa miongo ya miaka hali hiyo ya wasiwasi “ilitokeza shuku za muda mrefu na hofu na kuleta mizozo ya ulimwengu.” Alisema kwamba “wazo la usalama [ambalo] limeanza kujitokeza ni lile hasa ambalo Umoja wa Mataifa umekuwa ukifasiri muda wote wa miaka.”

Naam, ilionekana kama kwamba hatimaye mataifa yalikuwa yakijifunza kwamba “tamaa kubwa ya usalama wa kijeshi hutokeza mashindano ya uundaji silaha yenye kujiendeleza daima, . . . huzuia majadiliano ya kisiasa, . . . na huongezea ukosefu wa usalama katika mataifa yote.” Mtazamo huu mpya ulitokeza nini?

Hali ya ushirikiano mchangamfu na kutumainiana ilianza kuenea katika mikutano ya wakuu wa zile serikali kubwa zaidi. Hali hii ilipoendelea kukua, hawakuona uhitaji wa kuwa na kadiri ile ile ya majeshi yenye silaha kali kutumika kama vizuizi katika sehemu za maana katika Ulaya. Ukuta wa Berlin ulianguka. Ujerumani iliunganika. Hesabu fulani ya nchi za Ulaya ya Mashariki zilianzisha serikali mpya mbalimbali, zikiwapa raia zao uhuru wasiokuwa wameufurahia hapo mbeleni. Mipaka iliyofungwa ilifunguliwa kwa utalii, mabadilishano ya tamaduni, uchumi, na biashara. Kwa upeo, Urusi na United States zilianza kusifu Umoja wa Mataifa na kutangaza juu ya uhitaji wa kuutumia kama mamlaka thabiti katika jitihada ya ulimwengu ya kutafuta amani na usalama.

Kuwa na Maoni Halisi

Je! wewe ulishangazwa na mabadiliko hayo ya ghafula? Je! ulianza kufikiri kwamba, hatimaye, amani na usalama uko karibu na kwamba Umoja wa Mataifa utakuwa na daraka kubwa katika kutimiza shabaha hizo? Kwa kufikiria yale ambayo yametendeka, matazamio mazuri hayo yanaeleweka. Hata hivyo, hekima na historia inatushurutisha kwamba tuwe na maoni halisi kuhusu uwezekano huo.

Angalia kile Bw. Pérez de Cuéllar alichosema katika ripoti yake: “Mara mbili katika karne hii, baada ya vita viwili vyenye uharibifu mkubwa, uwezekano wa kujenga utengemano wenye amani duniani pote haukufanikiwa kikamilifu.” Rais Bush alitumia karibu maneno hayo hayo katika hotuba yake kwa mkutano wa pamoja wa Baraza Kuu la U.S. mnamo Machi 6, 1991. “Mara mbili katika karne hii, ulimwengu wote ulisukwasukwa na vita. Mara mbili katika karne hii, kwa kuhofia vita tumaini lilijitokeza la amani ya kudumu. Mara mbili kabla ya hapo, matumaini hayo yalithibitika kuwa ndoto isiyowezekana, isiyoweza kufikiwa na binadamu.”

Waziri wa Mambo ya Serikali wa U.S. James Baker alisema kwa njia ya moja kwa moja zaidi alipokuwa akihutubia Baraza la Usalama la UM. Akiomba kuwe na azimio la UM la kutumia nguvu katika Ghuba ya Uajemi, alikumbusha wenzake kwamba “ombi [la Ethiopia la 1936] kwa Ushirika wa Mataifa halikusikilizwa. Jitihada za Ushirika za kusuluhisha visa vya ugomvi zilishindwa kisha fujo ya kimataifa na vita vikafuata.” Halafu Bw. Baker akasihi hivi: “Ni lazima tusiruhusu Umoja wa Mataifa uwe kama Ushirika wa Mataifa ulivyokuwa.”

Ushirika wa Mataifa ulikuwa nini? Kwa nini ulifanyizwa? Kwa nini ulishindwa? Majibu ya maswali hayo yatatuwezesha tuthamini yale mabadiliko yanayotendeka kwenye Umoja wa Mataifa.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki