Miaka 50 ya Jitihada Zilizoshindwa
“SISI WATU WA UMOJA WA MATAIFA TUMEAZIMIA kuokoa vizazi vifuatavyo kutokana na pigo la vita, ambalo mara mbili maishani mwetu limeleta huzuni kubwa kwa binadamu, na tuimarishe imani katika haki za msingi za kibinadamu, katika heshima na hadhi ya binadamu, katika usawa wa haki za wanaume na wanawake na za mataifa makubwa na madogo, . . .”—Utangulizi wa katiba ya Umoja wa Mataifa.
OKTOBA 24, 1995, yatia alama mwaka wa 50 wa Umoja wa Mataifa. Mataifa yote 185 yaliyo washirika wakati huu yanadumisha kanuni na miradi ya msingi ya tengenezo hilo kama ionyeshwavyo na katiba hiyo: kudumisha amani na usalama wa kimataifa; kukomesha matendo ya uchokozi yanayotisha amani ya ulimwengu; kutia moyo uhusiano wa kirafiki miongoni mwa mataifa; kulinda uhuru wa kimsingi wa watu wote bila ubaguzi wenye msingi wa kabila, jinsia, lugha, au dini; na kupata ushirika wa mataifa yote katika kutatua matatizo ya kifedha, kijamii, na ya kitamaduni.
Kwa miaka 50 shirika la Umoja wa Mataifa limefanya jitihada zilizo dhahiri kuleta amani na usalama ulimwenguni. Labda, huenda lilizuia vita ya ulimwengu ya tatu, na kuangamiza wanadamu kwa ujumla kupitia mabomu ya nyukilia hakujarudiwa. Umoja wa Mataifa umeandalia mamilioni ya watoto chakula na dawa. Umechangia kiwango cha afya kilichoboreka katika nchi nyingi, ukiandaa vitu kama, maji safi ya kunywa na chanjo dhidi ya maradhi hatari. Mamilioni ya wakimbizi wamepokea msaada.
Kwa uthamini wa matimizo yalo, shirika la Umoja wa Mataifa limepokea mara tano Tuzo ya Amani ya Nobeli. Hata hivyo, jambo la hakika lenye kuhuzunisha maishani ni kwamba bado tunaishi katika ulimwengu wenye vita.
Amani na Usalama—Miradi Isiyofikiwa
Baada ya jitihada ya miaka 50, amani na usalama bado ni miradi isiyofikiwa. Katika hotuba ya majuzi kwa Mkutano wa Watu Wote wa Umoja wa Mataifa, rais wa Marekani alieleza kukata tamaa kwake kwa kusema kwamba “karne hii iliyojaa tumaini na fursa na matimizo pia imekuwa kipindi cha uharibifu mwingi na cha kukatisha tamaa.”
Mwaka wa 1994 ulipomalizika, The New York Times lilisema: “Karibu vita au vita vidogo-vidogo 150 vinaendelea ambapo maelfu ya watu wanakufa—kulingana na makadirio mengi raia wengi kuliko wanajeshi wanakufa—na mamia ya maelfu wanakuwa wakimbizi.” Idara ya Umoja wa Mataifa ya Habari za Umma iliripoti kwamba tangu 1945 zaidi ya watu milioni 20 wamepoteza maisha yao katika mapambano ambamo silaha zimetumiwa. Madeleine Albright, balozi wa Marekani kwa Umoja wa Mataifa alionelea kwamba “sasa mapambano katika maeneo ni yenye ukatili zaidi kwa njia nyingi.” Kuvunja haki za binadamu na ubaguzi huripotiwa kila siku. Mataifa mengi yanavumiliana badala ya kupendana.
Bwana David Hannay, balozi wa Uingereza kwa Umoja wa Mataifa, alikubali kwamba, “kufikia miaka ya 1980, Umoja wa Mataifa umekuwa kama mshindwa mwenye nia nzuri.” Katibu-mkuu wa Umoja wa Mataifa, Boutros Boutros-Ghali, aliomboleza kwamba miongoni mwa Mataifa yaliyo washirika mna ubaridi na uchovu wenye kuendelea kuhusu mipango ya kudumisha amani. Alimalizia kwamba kwa washiriki walio wengi, “Umoja wa Mataifa si jambo kuu la kutangulizwa.”
Uvutano wa Vyombo vya Habari
Hata Umoja wa Mataifa uonekane kuwa wenye nguvu kadiri gani, mara nyingi jitihada zao zinazuiwa na siasa na vyombo vya habari. Umoja wa Mataifa hauna nguvu ukikosa kuungwa mkono na washiriki wao. Lakini bila kibali cha watu, washiriki wengi wa UM hawawezi kuunga mkono Umoja wa Mataifa. Kwa kielelezo, kulingana na The Wall Street Journal, “kule kushindwa kabisa [kusaidia] Somalia na Bosnia kumeshawishi Wamarekani wengi kwamba shirika hilo ni lenye kuharibu mali, lakini ni hatari hasa.” Halafu, huo mtazamo wa watu umeshawishi wanasiasa fulani Wamarekani wapendekeze kupunguza utegemezo wa kifedha kwa Umoja wa Mataifa.
Mashirika ya habari hayasiti kuchambua vikali Umoja wa Mataifa. Misemo kama vile “kutoweza kabisa,” “mzigo,” “bure,” na “kudhoofika” imetumiwa waziwazi kuelezea utendaji mbalimbali wa UM. The Washington Post National Weekly Edition majuzi lilisema kwamba “Umoja wa Mataifa ni shirika la kupiga-ubwana na lenye kutenda polepole linapojikakamua kujipatanisha na ulimwengu halisi.”
Gazeti jingine lilimnukuu Katibu-Mkuu Boutros Boutros-Ghali akieleza jinsi amekata tamaa kwa sababu ya machinjo ya Rwanda. Alisema: “Ni kushindwa si kwa Umoja wa Mataifa tu; ni kushindwa kwa jumuiya ya kimataifa. Na sisi sote tunahusika katika kushindwa huko.” Kituo cha habari za pekee za televisheni kijulikanacho sana kilieleza katika 1993 kwamba Umoja wa Mataifa “umeshindwa kumaliza tisho kubwa zaidi la amani—kuongezeka kwa silaha za nyukilia.” Programu hiyo ya televisheni ilisema kuhusu Umoja wa Mataifa kwamba “kwa miongo mingi umekuwa ni maneno matupu.”
Hisia hiyo ya kukata tamaa yenye kuenea inasumbua sana akili za wakuu wa Umoja wa Mataifa nayo yaongezea kufadhaika kwao. Hata hivyo, ijapokuwa mifadhaiko hiyo, katika mwaka wa 50 wa Umoja wa Mataifa, wengi wanaonekana kama wamerekebisha maoni na wanatumainia mwanzo mpya. Ingawa anakubali mapungukio ya Umoja wa Mataifa, Balozi Albright alirudia maneno ya wengi aliposema: “Ni lazima tuache kuzungumza juu ya yale tuliyofanya wakati uliopita, na twahitaji kuzungumza juu ya yale tutakayofanya wakati ujao.”
Ndiyo, ulimwengu unaelekea wapi? Je, ulimwengu usio na vita utakuwapo wakati wowote? Ikiwa ndivyo, Umoja wa Mataifa utakuwa na fungu gani? Zaidi ya hayo, ikiwa wewe ni mwenye kumhofu Mungu, unapaswa kuuliza, ‘Mungu atakuwa na fungu gani?’
[Sanduku katika ukurasa wa 4]
JITIHADA ZILIZOSHINDWA
Amani na usalama haziwezi kuwapo vikiwepo vita, umaskini, uhalifu, na ufisadi. Hivi majuzi Umoja wa Mataifa ulitoa makadirio yafuatayo.
Vita: “Kuhusu yale mapambano 82 ambamo silaha zilitumiwa kati ya 1989 na 1992, 79 yalikuwa ya wenyewe kwa wenyewe, mengi yakiwa ya kikabila; asilimia 90 ya waliojeruhiwa au kuuawa walikuwa raia.”—Idara ya Umoja wa Mataifa ya Habari za Umma (UNDPI)
Silaha: “ICRC [Chama cha Kimataifa cha Msalaba Mwekundu] chakadiria kwamba zaidi ya viwanda 95 katika nchi 48 vinafanyiza baruti kati ya milioni 5 na 10 kila mwaka za kulipua vifaa vya kijeshi.”—Tume ya Umoja wa Mataifa Inayoshughulikia Wakimbizi (UNHCR)
“Katika Afrika, kuna baruti za kutegwa ardhini karibu milioni 30 zilizotapakaa katika zaidi ya nchi 18.”—UNHCR
Umaskini: “Ulimwenguni pote, mtu mmoja kati ya kila watano—zaidi ya bilioni moja kwa ujumla—ni maskini kabisa, na kadiri ya milioni 13 hadi 18 wanakufa kila mwaka kutokana na visababu vinavyohusiana na umaskini.”—UNDPI
Uhalifu: “Uhalifu ulioripotiwa umeongezeka ulimwenguni kwa kadiri ya asilimia 5 kila mwaka tangu miaka ya 1980; katika Marekani pekee, kuna uhalifu milioni 35 unaofanywa kila mwaka.”—UNDPI
Ufisadi: “Ufisadi wa umma umekuwa kitu cha kawaida. Katika nchi fulani upunjaji wa fedha wakadiriwa kugharimu kiasi kinacholingana na asilimia 10 ya mapato yote ya nchi hizo kila mwaka.”—UNDPI