Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g92 4/8 kur. 18-19
  • Kwa Nini Pornografia Ni Hatari

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kwa Nini Pornografia Ni Hatari
  • Amkeni!—1992
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Je! Ni Kosa Kuamsha Tamaa?
  • Jinsi ya Kujiondoa Katika Kifungo Chayo
  • Madhara Yanayosababishwa na Ponografia
    Amkeni!—2003
  • Kwa Nini Ujiepushe na Ponografia?
    Vijana Huuliza
  • Ponografia
    Amkeni!—2013
  • Ponografia—Je, Ina Madhara?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2013
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1992
g92 4/8 kur. 18-19

Maoni ya Biblia

Kwa Nini Pornografia Ni Hatari

PORNOGRAFIA sasa haipatikani tu katika maduka ya vitabu vichafu na sinema za kingono. Inapatikana kila mahali. Katika nchi baada ya nchi, watu wa kawaida waweza kuiona katika magazeti, nyusipepa, vitabu, programu za TV, sinema, na video. Je! jambo lolote lenye mwenezo mkubwa kama huo laweza kweli kuwa hatari hivyo?

Hata hivyo, pornografia ni nini? Pornografia hufasiriwa kuwa “wonyesho wa tabia za uchu (kama katika picha au maandishi) unaokusudiwa kuamsha nyege.” Ufasiri huo ni wazi. Lakini ubishi hutokea kuhusu kuamua ni nini kiamshacho nyege na ni nini kisichoamsha. Ni kweli, kwa kiasi fulani, kile kifanyizacho pornografia ni katika jicho la mwenye kuona. Kwa maneno mengine, kile kiamshapo tamaa ya ngono kwa mtu mmoja huenda kisifanye hivyo kwa mwingine. Hata hivyo, uchunguzi wa hivi majuzi wa watu 5,000 katika Ujerumani ulivumbua kwamba kwa kiasi fulani, mambo ya kuamsha nyege huathiri karibu kila mtu, wanaume na wanawake pia.

Je! Ni Kosa Kuamsha Tamaa?

Kuamsha tamaa inayofaa—ya chochote kile—si jambo la hekima ikiwa hakuna njia ya kuitosheleza ifaavyo. Kwa mfano, ikiwa kimoja cha vyakula upendavyo zaidi hakipatikani, inaelekea hutaridhika ikiwa unaendelea kutazama picha zacho katika magazeti na vitabu. Kwa upande mwingine, ikiwa wewe—labda kwa sababu za kiafya—huruhusiwi kula chakula hicho, kushughulika nacho wakati wote inaelekea kutakuongoza uruke mipaka kwa njia hatari. Vivyo hivyo, mvutaji sigareti ambaye anajaribu kushinda tabia hiyo hataelekea zaidi kufanikiwa kwa kutumia wakati akitazama kwa uchu watu wengine wakivuta sigareti.

Kuhusiana na tamaa za kingono, katika oni la Kibiblia, furaha hutokana na kuzitosheleza vema katika mipaka ya ndoa yenye upendo. (1 Wakorintho 7:2-5; Waebrania 13:4) Basi ni kukosa hekima kama nini mseja kuamsha tamaa ambazo hawezi kuridhisha! Hilo huongoza kwenye hangaiko la akili tu au, lililo baya hata zaidi, kuzitosheleza kwa kugeukia punyeto au uasherati, na hivyo kukiuka sheria na kanuni za kimungu.—1 Wathesalonike 4:3-7.

Je! hilo lamaanisha kwamba pornografia si hatari ikiwa umeoa? La, sheria hizo za Kimaandiko kuhusu mwenendo hutumika kwa watu waliooana pia. Pia, pornografia huvutia tamaa za ubinafsi, kujaribu kuridhisha tamaa za kibinafsi, hali upendo hukazia kuridhisha mahitaji ya mwenzi. Pornografia huongoza kwenye ngono isiyofikiria mwingine na yenye ubinafsi, ambayo, hata katika uhusiano wa ndoa, hushusha heshima na hukosa upendo.—1 Wakorintho 13:5.

Badala ya kuimarisha upendo katika ndoa, pornografia huuua kwa kuushusha, na kuupotosha. Mahusiano ya kingono kama yanavyoonyeshwa katika pornografia ni ndoto mbaya kabisa kwa sababu hutoa habari za makosa na zenye madhara kuhusu mahusiano ya wenzi wa ndoa. Isitoshe, mahusiano halisi ya maisha huwa yanahusisha zaidi tu ya ngono; huwa yanategemea wororo, uchekeshano, uwasiliano, na kujali. Kwa kutofautisha, pornografia yaweza hata kuwa jambo la kutenganisha wenzi waliooana.

Pornografia hupunguza heshima ya wanadamu hadi kwenye kiwango cha wanyama wanaotenda kwa silika tu. Haitii moyo kuwa na kujidhibiti, tunda la roho ya Mungu. (Wagalatia 5:22, 23) Inaweza kusababisha ngono zilizopotoka. Hizi ni chache tu za sababu za Wakristo kuepuka pornografia.

Hivyo, shauri la Biblia la hekima ni: “Umfurahie mke wa ujana wako . . . Mbona unashangilia malaya, na kukikumbatia [kihalisi au vingine kwa pornografia] kifua cha mgeni?”—Mithali 5:15-20.

Hata hivyo, mtu anaweza kuepukaje au kujiondoaje katika kifungo cha pornografia?

Jinsi ya Kujiondoa Katika Kifungo Chayo

Ili kushinda uvutano wa pornografia, Biblia inashauri hivi: “Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya.” (Wakolosai 3:5) Hapa, neno “vifisheni” huonyesha wazi wazo la kupiga hadi kufa—si kukandamiza—kiungo chochote cha mwili ambacho kingetumika katika maovu hayo.

Hata hivyo, hilo lazima lieleweke katika maana ya mfano, si katika maana halisi. Haiwapasi Wakristo kuharibu miili yao. Ikiwa “tunaua” kwa uthabiti fikira zisizofaa za ngono, hatutashindwa na mvuto wa pornografia, hivyo tukitumia sehemu za miili yetu, kama vile macho, kwa njia mbaya. (Linganisha Mathayo 5:29, 30.) Hivyo, Biblia inashauri, kubadilisha tamaa mbaya kwa “mambo yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi,” halafu endelea ‘kuyatafakari hayo.’—Wafilipi 4:8.

Nini kingine chaweza kusaidia? Kuweka akilini—labda hata kuyakariri—mafungu ya Biblia, kama yale yafuatayo:

“Unigeuze macho yangu nisitazame visivyofaa.”—Zaburi 119:37.

“Kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho . . . havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia.”—1 Yohana 2:16.

“Kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa. Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti.”—Yakobo 1:14, 15.

Chochote kiwezacho kuanzisha mfuatano wa mambo hadi kwenye kifo chaweza kusemwa kuwa hatari kwa haki, na ndivyo hasa pornografia ilivyo! Kumbuka: “Yeye apandaye kwa mwili wake, katika mwili wake atavuna uharibifu; bali yeye apandaye kwa Roho, katika roho atavuna uzima wa milele.” Usiache pornografia ikupokonye uhai wa milele!—Wagalatia 6:8.

[Blabu katika ukurasa wa 19]

Badala ya kuimarisha upendo katika ndoa, pornografia huuua kwa kuushusha, na kuupotoa

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki