Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g92 8/8 kur. 4-6
  • Ni Utunzi Gani Ufaao kwa Walio Wagonjwa Mahututi?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Ni Utunzi Gani Ufaao kwa Walio Wagonjwa Mahututi?
  • Amkeni!—1992
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Masuluhisho Yaliyotokezwa
  • Aina Gani ya Utibabu au Utunzi?
  • Programu kwa Ajili ya Wagonjwa Mahututi—Lengo Ni Nini?
    Amkeni!—2011
  • Kuwafariji Watu Wenye Ugonjwa Usioweza Kupona
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2008
  • Msaada kwa Wanaokufa Katika Kizazi cha Kisasa
    Amkeni!—1992
  • Mpendwa Wako Anapokuwa na Ugonjwa Usiotibika
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova (Toleo la Watu wote)—2017
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1992
g92 8/8 kur. 4-6

Ni Utunzi Gani Ufaao kwa Walio Wagonjwa Mahututi?

KATIKA nyakati za hivi karibuni, njia ambayo watu wanashughulika na kifo na kufa imekuwa ikibadilika katika sehemu nyingi za ulimwengu.

Katika nyakati zilizopita matabibu walikubali kifo kuwa mwisho usioepukika wa utumishi wao kwa wagonjwa wengine—mwisho unaopaswa kuwa mtulivu, sana sana ukishughulikiwa nyumbani.

Hivi karibuni zaidi, tekinolojia na utibabu ukitiliwa mkazo, wafanyakazi wa kitiba wamekuja kuona kifo kuwa kutofaulu au ushinde. Kwa hiyo lengo la msingi la utabibu limekuwa lile la kuzuia kifo kwa njia zote. Pamoja na badiliko hilo kukatokezwa tekinolojia mpya kabisa ya kuendeleza watu wakiwa hai kwa muda mrefu zaidi kuliko vile ilivyowezekana hapo mbeleni.

Tekinolojia ya kitiba imefanya maendeleo yasiyoweza kupingwa katika nchi nyingi; hata hivyo, hiyo imetokeza wasiwasi mwingi. Daktari mmoja alieleza: “Matabibu wengi wamepoteza hazina iliyokuwa sehemu ya maana sana ya tiba, na hiyo ni ubinadamu. Utumizi wa mashine, ustadi na kufuata utaratibu kumetorosha moyoni wororo, huruma, sikitikio na hangaikio kuelekea mgonjwa. Utabibu sasa ni sayansi yenye ubaridi; uvutio wao ni wa kizazi kingine. Mtu anayekufa aweza kupata faraja kidogo sana kutoka kwa daktari afanyaye kazi kama mashine.”

Hayo ni maoni ya mtu mmoja tu, na kwa kweli si shtaka la kutoka kotekote kwa kazi ya tiba. Hata hivyo, labda umeona kwamba watu wengi wamekuza woga wa kuendelezwa kuwa hai kwa mashine.

Polepole maoni mengine yakaanza kusikiwa. Yalikuwa kwamba katika visa fulani watu wapaswa waachwe wafe kiasili, kwa heshima, bila kuendelezwa uhai na tekinolojia isiyo na hisi. Uchunguzi uliofanywa hivi karibuni wa gazeti la Time ulifunua kwamba zaidi ya robo tatu ya wale waliofikiwa walionelea kwamba daktari apaswa kuruhusiwa kukomesha utibabu unaoendeleza uhai kwa mgonjwa mahututi. Uchunguzi huo ulifikia mkataa huu: “Punde baada ya kukubali mambo yasiyoepukika, [watu] hutaka kufa kwa heshima, si wakiwa wamefungishwa kwenye aina-aina za mashine katika sehemu ya utunzaji wa wakati wote kama kwamba wao ni kiolezo kinachochunguzwa katika maabara.” Je! wewe wakubali hilo? Hayo yalinganaje na maoni yako kuhusu habari hiyo?

Masuluhisho Yaliyotokezwa

Ikitegemea utamaduni au aina ya maisha aliyokuwa nayo mtu, kuna tofauti kubwa katika njia za kushughulikia habari ya kifo na kufa. Walakini, watu katika nchi nyingi wanaonyesha upendezi ulioongezeka kwa hali ngumu za wagonjwa wasio na tumaini. Katika miaka michache iliyopita, wanamaadili, madaktari, na watu wote kwa ujumla wamechangia jitihada za kurekebisha utunzaji wa waliopatwa na msiba huo.

Kati ya njia nyingi zinazojaribiwa za kupambana na suala hili, moja inayotumiwa sana katika hospitali nyinginezo ni ile sera isemayo “Usihuishe,” (“Do Not Resuscitate,” au DNR.) Je! unajua hilo linatia ndani nini? Baada ya mazungumzo marefu pamoja na familia ya mgonjwa, na hasa pamoja na mgonjwa mwenyewe pia, mipango hususa inafanywa kimbele, na hiyo inaandikwa kwenye chati ya mgonjwa. Hiyo hukazia juu ya viwango vitakavyofikiwa katika jitihada za kurejeza kwenye uzima, au kuhuisha mgonjwa asiye na tumaini, iwapo hali yake inakuwa mbaya zaidi.

Karibu kila mtu atambua kuwa wazo la maana zaidi ya yote katika kufanya maamuzi magumu kama hayo lapasa kuwa “Mgonjwa angetaka nini kifanywe?” Hata hivyo, kile kinachofanya hilo liwe tatizo kubwa ni kwamba, mara nyingi mgonjwa huwa amezirai au kwa vyovyote hawezi kufanya maamuzi yafaayo ya kibinafsi. Hilo limefanya kuwe na hati inayoweza kuitwa wasia unaoishi. Imefanyizwa ili watu waweze kusema mahususi kimbele ni aina gani ya utabibu ambao wangetamani katika siku zao za mwisho. Kwa mfano, wasia kama huo waweza kusomeka hivi:

“Ikiwa ninakuwa katika hali isiyoponyeka au isiyoweza kubadilishwa itakayosababisha kifo changu katika muda mfupi sana, ni tamaa yangu kwamba maisha yangu yasirefushwe kwa kutumia njia za kuendeleza uhai. Ikiwa hali yangu ni mahututi na ninashindwa kushiriki katika kufanya maamuzi yanayohusu matibabu yangu, mimi ninaelekeza tabibu wangu anayenishughulikia akatize au kuacha kabisa utibabu mbalimbali utakaorefusha tu mwendo wa kufa na ambao si wa lazima katika kunistarehesha au kuniondolea uchungu.” Hati hizo zaweza hata kutaja mahususi aina ya matibabu ambayo mtu atataka au hatataka utumiwe katika hali mahututi.

Ingawa wasia hizo zinazoishi hazitambuliwi kisheria chini ya hali zote, zinatambuliwa mahali pengi. Watu waliokadiriwa kuwa milioni tano katika United States wameandika wasia za kitiba zinazoishi. Wenye mamlaka wengi katika bara hilo huona hilo kuwa njia bora zaidi ipatikanayo kuhakikisha kuwa matakwa ya mtu yanaheshimiwa na kufuatwa.

Aina Gani ya Utibabu au Utunzi?

Namna gani kuhusu utunzaji wenyewe wa wagonjwa mahututi? Labda ubuni wa maana zaidi ni ule uitwao malalo, unaozidi kutambuliwa ulimwenguni pote. “Malalo” ni nini hasa?

Badala ya kumaanisha mahali au jengo, malalo katika maana hii hurejezea kihalisi falsafa au programu ya utunzaji wa wagonjwa mahututi. Linatokana na neno la Kifaransa la kale linalomaanisha mahali pa kupumzika pa wahiji. Malalo hukazia shughuli za pamoja (madaktari, waaguzi, na wenye kujitolea) ambazo husaidia kuhakikisha kwamba mgonjwa mahututi anastareheshwa na kuwa bila uchungu, hasa akiwa nyumbani mwake mwenyewe.

Ingawa malalo mengine yanapatikana kwenye hospitali, mengi yayo yanajitegemea. Mengi hukaribisha msaada wa kijamii, kama vile waaguzi, wenye maakuli, wahubiri, na wenye kusugua viungo wanaozuru. Badala ya kuchukua hatua za kishujaa za kitiba, utunzaji wa malalo hukazia huruma ya kishujaa. Badala ya utibabu wa kila aina dhidi ya ugonjwa wa mgonjwa, hayo hukazia utibabu wa kila aina dhidi ya kutostarehe kwa mgonjwa. Daktari mmoja alisema: “Malalo sio utunzaji mdogo zaidi au ukosefu wa utunzi au utunzi wa hali ya chini. Ni aina nyingine tu ya utunzi iliyo tofauti kabisa.”

Wewe unaitikiaje wazo hilo? Je! mfikio huo ni ule unaoona wapaswa kuzungumziwa pamoja na wowote wa wapendwa wako ambao huenda wakatambulishwa kuwa wanakabili hali mahututi, na labda tabibu akitiwa ndani?

Hata ikiwa utunzi wa malalo huenda usipatikane katika eneo lako sasa, inawezekana kuwa utapatikana wakati ujao, kwani harakati ya malalo inakua ulimwenguni pote. Ingawa hapo mbeleni ulionwa kuwa jitihada dhidi ya maendeleo, utunzi wa malalo umeingia polepole kuwa kawaida ya utibabu, na sasa huonwa kuwa kibadala kinachokubalika kwa walio wagonjwa mahututi. Kupitia ustadi wazo, na hasa utumizi ufaao wa dawa za kuondoa maumivu, malalo yameleta maendeleo ya maana kwa utunzaji wa afya.

Katika barua kwa New England Journal of Medicine, Dakt. Gloria Werth alieleza kifo cha dada yake katika malalo: “Hakuna wakati ambao dawa, chakula, au kitu chochote kama maji kililazimishwa kwa dada yangu. Yeye alikuwa huru kula, kunywa, . . . au kutumia dawa kama alivyopenda . . . Lakini jambo bora zaidi kuhusu malalo ni kwamba kumbukumbu letu kuhusu kifo cha Virginia huruzuku na hufurahisha isivyo kawaida. Hilo laweza kusemwaje baada ya kifo katika sehemu ya utunzaji wa wakati wote?”

[Blabu katika ukurasa wa 5]

“Utabibu sasa ni sayansi yenye ubaridi; uvutio wao ni wa kizazi kingine. Mtu anayekufa aweza kupata faraja kidogo sana kutoka kwa daktari afanyaye kazi kama mashine”

[Blabu katika ukurasa wa 6]

Malalo hukazia utabibu wa kila aina dhidi ya kutostarehe kwa mgonjwa badala ya utabibu wa kila aina dhidi ya ugonjwa wenyewe

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki