Msiba wa Chile Waongoza Kwenye Upendo wa Kikristo
Na mleta habari za Amkeni! kutoka Chile
KASKAZINI MWA CHILE kunajulikana kwa Jangwa la Atakama lenye ukavu, na lenye eneo kubwa sana lisilokaliwa na watu ambalo huishilia kwenye upeo wa macho. Mvua huwa chache sana hivi kwamba kile watu wengi wanaweza kuita ukungu huitwa mvua katika eneo hilo lililo ukiwa kati ya Bahari ya Pasifiki na Milima ya Andes. Kwa sababu ya hali hizo za anga, nyumba nyingi hazitengenezwi kuweza kukabiliana na mvua, na hata mahali ambapo kuna mvua ya mara kwa mara—labda mara moja kwa kila miaka mitano—watu wengi hawashughuliki kamwe kuchunguza uwezekano wa paa yenye kuvuja hadi mvua inapokuja. Jambo hilo labda liliokoa maisha za watu wengi katika Antofagasta, jiji la wakazi 250,000 hivi.
Jumatatu usiku, Juni 17, 1991, watu wengi walikuwa wakijitayarisha kulala usiku, wakati mvua kubwa ilipoanza kunyesha. Paa za nyumba nyingi zilivuja maji, kwa hiyo badala ya kwenda kulala, watu walijaribu kurekebisha mivujo au kuzuia uharibifu—bila kung’amua kwamba jambo baya zaidi lilikuwa litukie katika muda wa saa chache.
Mapema asubuhi iliyofuata, miporomoko ya matope mikubwa mitatu, ikisukuma mamilioni ya tani za udongo kwa mwendo wa kilomita 32 kwa saa, ilisababisha vifo vya watu 85 hivi, ikajeruhi 700 hivi, na kuharibu au kubomoa nyumba za watu zaidi ya 30,000!
Maumivu Makali Katika Bahari ya Matope
Katika Antofagasta kuna makundi kumi ya Mashahidi wa Yehova, kukiwa na washiriki karibu 1,400, kwa hiyo kulikuwa na hangaiko la kweli kuhusu hali njema yao. Tulifurahi jinsi gani kusikia kwamba hakuna wowote waliopoteza uhai wao, ingawa dada mmoja alijeruhiwa vibaya alipofagiliwa mbali na matope hayo kwa umbali wa karibu kilomita tatu. Alipopatikana na waokoaji, walifikiri kuwa amekufa hadi muuguzi mmoja alipotambua kwamba anapumua na, alipomkaribia, akamsikia akiita “Jehová, Jehová.” Alikuwa amemeza kiasi kikubwa cha matope, kwa hiyo wakamkimbiza hospitali kumtibu kwa sababu ya maambukizo.
Katika Kundi la Oriente, asilimia 70 hivi ya familia walipoteza nyumba zao au zikaharibiwa vibaya. Familia nyingine katika Makundi ya Costanera na Corvallis pia waliharibiwa nyumba zao, kwa vile matope yalifikia urefu wa paa katika sehemu fulani au yakatiririka ndani ya nyumba, yakijaza vyumba kwa matope kufikia mita moja unusu. Katika nyumba moja mama na watoto wake wachanga wawili walielea juu ya bahari ya matope wakiwa kitandani mwao, matope hayo yakiwapeleka juu polepole hadi kwenye dari; waliokolewa wakati baba ya mwanamke huyo alipofaulu kuvunja dari. Wengine waliokuwa sehemu zenye usalama zaidi walihisi kwamba mwisho u karibu waliposikiliza mlio wa miporomoko ya matope yaking’oa kila kitu njiani na kusikia kilio cha maumivu makali katika giza la usiku.
Kitu Chenye Thamani Zaidi Kuliko Mali
Ingawa walipoteza mali zao nyingi, Mashahidi wameonyesha roho ya kutokeza. Shahidi mmoja alisema jinsi rafiki na wafanyakazi wenzake walivyoshangaa kuona hali yake ya furaha ijapokuwa alipoteza mali nyingi. Yeye aliwaambia kwamba kama mali zingewekwa kwa mpangilio wa alfabeti kulingana na umaana, zingekuwa katika nafasi ya herufi z. Yeye alikuwa mwenye furaha kuwa aliokoka na kuwa hai pamoja na familia yake nzima.
Mama mwingine, aliyeburutwa mbali kutoka kwa binti zake na akakaribia kupoteza wawili pamoja na maisha yake mwenyewe, alikuwa amemwomba Yehova kwa bidii kwamba ikiwa angerudi kwenye uhai mapema katika ufufuo, angependa kufanya kazi akiwa mpishi huku wengine wakifanya kazi ya kurudisha hali nzuri duniani! Yeye aliokoka, na unafikiri aliombwa atumikie wapi siku zilizofuata maporomoko hayo ya matope? Naam, jikoni iliyotengenezwa na Mashahidi ili kutayarisha mamia ya vyakula kwa Mashahidi wa Yehova na familia jirani waliokuwa wamepoteza makao yao!
Upendo wa Kikristo Katika Tendo
Mashahidi wenye upendo katika Kalama na Ikuikue walifanya mipango kupeleka mikate, maji, nguo, na vifaa vingine vya lazima hadi Antofagasta. Ofisi ya tawi ya Watch Tower Society ilipanga msaada pia, na upesi nguo, mablanketi, vitanda, vifaa vya jikoni, vyakula, na vifaa vingine vilianza kufika. Iligusa mioyo kama nini kuona kwamba vifaa vingi vilivyochangwa havikuwa vile vimetumiwa na masalio bali vifaa vipya kabisa! Upesi malori mawili ya Sosaiti na la tatu kutoka Rankagua yalikuwa njiani kuelekea Antofagasta, karibu kilomita 1,408 kwenda kaskazini, yakiwa na tani 14 za vitu. Ingawa habari ilipitishwa kwamba haikuhitajika tena kuchangia vifaa zaidi, vifaa viliendelea kufika. Kama tokeo, ilibidi kukodisha lori la ziada ili kubeba tani nyingine 16! Ugavi huo ulishirikiwa kwa ukarimu na majirani ambao si Mashahidi.
Ingawa nyumba ya familia moja ya Mashahidi ilikuwa katika moja ya sehemu zilizokumbwa vibaya sana, ilisalimika ikiwa katika hali nzuri. Upesi wao walionyesha upendo wao kwa jirani, wakipokea nyumbani mwao familia 9 za Mashahidi pamoja na majirani wengine 70 ambao hawakuwa Mashahidi, wengi wao wakifika wakiwa wamejawa na matope na bila nguo. Mashahidi hao walitoa nguo na mablanketi yote waliyokuwa nayo.
Wengi wametoa wakati, mali, na nishati zao kusaidia. Ingawa umekuwa msiba mkubwa kwa Chile, watu wa Yehova kwa mara nyingine walionyesha umoja na hangaiko lao la kidugu, michango ya kifedha ikipelekwa huko kutoka sehemu za mbali kama vile Teksas katika United States. Mtu mmoja alitoa muhtasari kuhusiana na majuma mawili ya kutoa misaada kwa waliopatwa na msiba katika Antofagasta hivi: “Hatujapata kamwe kuwa na mkusanyiko wa siku 13, kukiwa na drama nyingi halisi, wonyesho mwingi wa upendo, na kujitoa kwingi kwa wengine kama ilivyodhihirishwa wakati wa siku chache zilizopita.”