Unaweza Kufanya Kusafiri kwa Ndege Kuwe Salama Zaidi
Na mleta habari za Amkeni! katika Finlandi
SIKU hizi, kusafiri kwa ndege ni njia ya haraka na ya kawaida. Pia huonwa kuwa mojawapo usafiri salama zaidi.
Usalama huo ni tokeo la jitihada zilizoazimiwa na za pamoja za wenye mamlaka na makampuni ya ndege kuondoa zile zinazoelekea kuwa hatari. Usalama unategemea mambo mbalimbali. Mashirika ya ndege huchangia kwa kuweka ndege zao katika hali nzuri kwa kuzichunguza na kuzirekebisha kwa ukawaida. Zaidi ya hiyo, mipango na maagizo mengi ya upakizi hufanywa kwa uangalifu katika kila safari. Mizigo, shehena, na barua huwekwa katika sehemu ya mizigo kulingana na maagizo hayo, na hesabu sahihi ya uzani na usawaziko hufanywa kwa kila safari. Je! ulipata kufikiri kuhusu matayarisho hayo yote yanayofanywa bila wewe kujua?
Lakini je! ni hayo tu ndiyo yanayohusika kwa habari ya usalama wa safari za ndege? La hasha! Kuna mambo mengine ya ziada ambayo wewe ukiwa abiria wa ndege waweza kuchangia moja kwa moja. Kwa njia gani? Je! ulijua kwamba unaweza kuhatirisha usalama bila wewe kujua? Au kwamba unaweza kudumisha usalama wa kawaida kwenye safari kwa kujua na kufuata kanuni fulani za msingi za usafiri wa ndege?
Mashirika ya Ndege na Usalama Wako
ICAO (Shirika la Kimataifa la Safari za Ndege za Abiria), lililo chini ya Umoja wa Mataifa, limefanya jitihada za kufanyia maendeleo usalama wa usafiri wa ndege, likifanya kazi na mashirika ya ndege ya kibiashara. IATA (Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Ndege) na ATA (Shirika la Amerika la Usafiri wa Ndege) yameshirikiana kwa karibu sana na ICAO kwa habari ya usalama. Yamechapisha maagizo na matakwa na kutayarisha vifaa na habari za mazoezi kwa manufaa ya washiriki wayo na umma kwa ujumla.
Kutokezwa kwa vifaa vipya na vile vya muungano wa kemikali, pamoja na vifaa vya kielektroni vinavyotumiwa na abiria, kumeongeza uwezekano wa hatari. Hilo pia limeongeza kiasi cha tahadhari za usalama na uhitaji wa kuwajulisha abiria.
Ni Hali Zipi za Hatari Zinazoweza Kutokea?
Matokeo ya msiba yangaliweza kutokea kutokana na hali zifuatazo:
(1) Kasha la mshiriki wa timu ya mchezo wa kuteleza juu ya theluji liliwaka moto likiwa kwenye mshipi wa kupandisha mizigo kabla halijapakiwa kwenye ndege. Lilipochunguzwa, ndani mlikuwa kiyeyushaji cha kuondoa nta kwenye vyuma vya kutelezea kwenye theluji. Kiyeyushaji hicho kilikuwa kimevuja. Pia ndani ya kasha mlikuwa na kifaa cha gesi cha kuwashia moto, na cheche iliyosababishwa na kutikiswa kwa kasha iliwasha moto vitu vilivyokuwemo. Jambo zuri ni kwamba yote hayo yalitukia chini na si kwenye sehemu ya mzigo ndani ya ndege meta 11,000 angani, jambo ambalo lingesababisha aksidenti mbaya sana.
(2) Kwa njia iyo hiyo, viberiti vya kawaida viliwaka kwenye kasha la abiria kwa sababu ya msuguo.
(3) Katika uwanja mmoja wa ndege, wafanyakazi walipata chupa ya gesi iliyovuja. Chupa hiyo ilikuwa inageuka upesi kuwa bomu iliyokawizwa kulipuka!
(4) Asidi iliyokuwa ikivuja kutoka kwa betri ya kigari cha kusukumwa chenye injini ilisababisha uharibifu mkubwa kwa ndege kwa ajili ya kutu. Ndege hiyo haikuruhusiwa kuruka kwa siku kadhaa ili isafishwe na kurekebishwa, jambo lililofanya kampuni ya ndege ipoteze fedha.
Vifaa Visivyopaswa Kusafirishwa kwa Ndege
Mashirika ya kimataifa yaliyotajwa juu huchapisha kijitabu cha mwongozo kinachoitwa Dangerous Goods Regulations, au Kanuni za Mizigo Hatari, kinachopatikana katika makampuni ya ndege na mashirika ya uchukuzi. Mengi ya masharti yacho hufanyiza sehemu ya sheria za kitaifa za usafiri wa ndege katika nchi mbalimbali. Masharti hayo hutia ndani kuorodheshwa kwa maelfu ya mizigo hatari pamoja na mielekezo yenye mambo mengi kuhusu upakizi na usafirishaji wa mizigo hiyo. Kuna vifaa na mizigo mingine ambayo hauruhusiwi hata kidogo kusafirisha kwa ndege. Isitoshe, kuna vifaa ambavyo haviwezi kusafirishwa vikiwa mzigo lakini vyaweza kukubaliwa kuwa shehena chini ya hali fulani. Kisha kuna vifaa—ingawa huonwa kuwa hatari—ambavyo kanuni za shirika hususa huenda zikakuruhusu kubeba kwa kiasi kidogo-kidogo, kwa mfano katika furushi la mkononi. Wakati wowote unapokosa uhakika, ni hekima kushauriana na shirika lako la ndege kabla ya safari.
Unaweza Kupata Wapi
Habari Inayohitajiwa?
Mashirika mengi ya ndege huchapisha kwenye majedwali yayo, vifaa hatari vinavyokatazwa. Pia tikiti yako ina orodha ya vifaa na mizigo ambayo hukatazwa. Isitoshe, kwenye mjadala wao uliofanywa katika 1989, mashirika ya ndege kotekote ulimwenguni yaliamua kuelekeza uangalifu wa umma kwenye mambo hatari ambayo watu wanaweza kufanya bila kujua. Mwanzoni mwa 1990, mashirika hayo yalianza kampeni iliyoelekezwa kwa wasafiri. Mabandiko yaliwekwa kwenye wanja za ndege na mashirika ya usafiri ili kujulisha umma kwamba vifaa hatari vingeorodheshwa kwenye kikaratasi ambacho wangepokea pamoja na tikiti zao.
Mizigo na Vifaa Hatari Vinatia Ndani Nini?
Kuna mizigo na vifaa vingi vinavyoonekana kuwa si hatari ambavyo katika hali fulani huenda vikawa hatari ndani ya ndege. Kwa mfano, wakati wa safari, mabadiliko ya joto na msongo wa hewa, waweza kusababisha kuvuja. Huenda vifaa fulani vikaonekana kuwa salama, lakini vinapogusana na vifaa vingine ambavyo kwa kawaida si hatari, huenda vikatokeza utendaji wa kikemikali. Hilo laweza kusababisha moto au mivuke ya sumu. Kwa hiyo, ni jambo la muhimu kwamba ujue kile unachopakia ndani ya kasha lako.
Kama ilivyotajwa mapema, vifaa vinavyokatazwa vinatia ndani viberiti vya kawaida na viwasha-sigareti. Unaruhusiwa kuvibeba vikiwa furushi la mkononi tu.
Usafirishaji wa aina zote za umaji-maji unaoweza kuwaka moto hauruhusiwi. Rangi, rangi ya sandarusi, na guluu zaweza pia kuwa hatari, sembuse viyeyushaji kama vile thina na asetoni.
Aina zote za gesi zinazoweza kuwaka moto, kama vile kiwasha-sigareti au mitungi ya gesi, hukatazwa zisipakiwe katika ndege.
Baruti, fataki, na vifaa vya kutoa ishara kwa moto wenye kung’aa hukatazwa pia kwa sababu ni hatari.
Labda umezoea kutumia aina nyingi ya kemikali na bidhaa za viwanda nyumbani mwako. Je! ulijua kwamba unaposafiri kwa ndege, huenda usiruhusiwe kusafiri na baadhi yavyo? Vifaa vinavyokatazwa vinatia ndani erosoli (bidhaa zilizoshindiliwa ndani ya mkebe kwa kani eneo), viuawadudu, vipararishaji, na kemikali za kusafisha nguo. Hizo zaweza kuleta kutu au ongezeko la oksijeni au kuharibu ndege au mizigo mingine iliyo karibu.
Vifaa vyenye sumaku vyaweza kuathiri utendaji wa mitambo ya ndege, na vifaa nururishi vyaweza kuleta uharibifu kwa mnururisho.
Huenda Ukaathiri Mfumo wa Uendeshaji wa Ndege!
Katika miaka michache iliyopita, huenda ikawa uliweza kufurahia kutumia aina nyingi za ubuni mpya katika uwanja wa elektroni. Redio, tepu-rekoda, kamera ndogo za vidio, kinanda cha CD, simu zinazobebeka, na kompyuta zinazobebeka, pamoja na vitu vya kuchezea vyenye kuendeshwa kielektroni kutoka mbali, vimependwa na wengi. Kwa kawaida, unaruhusiwa kupakia vifaa hivyo katika mzigo wako maadamu umeondoa betri. Kwa kuwa kanuni hutofautiana katika mashirika mbalimbali ya ndege, arifiana na shirika lako la usafiri kabla ya kupakia. Hata hivyo, ni kanuni ya ulimwenguni pote kwamba hupaswi kutumia aina hiyo ya vifaa wakati wa safari kwa kuwa vinaweza kuathiri mfumo wa uendeshaji wa ndege.
Kila abiria huruhusiwa kubeba kiasi kidogo cha dawa, virembeshi, na kileo kwa matumizi ya kibinafsi, na kwa kawaida erosoli kama vile umaji-maji wa kupulizia nywele na wa kudhibiti jasho zaweza kubebwa.
Je! Unadumisha Usalama Ndani ya Ndege?
Je! wewe hufuata kanuni hizo zote? Je! unajua daraka lako? Kabla ya kupakia kwa ajili ya safari yako ijayo, keti na usome kwa uangalifu kanuni za usafiri, hasa kanuni zinazohusiana na vifaa hatari. Kuhusu hilo, tumezungumzia kanuni za ujumla, lakini huenda kukawa na tofauti katika mashirika mbalimbali ya ndege.
Ikiwa huna uhakika kuhusu kifaa fulani, usisite kuuliza shirika lako la ndege ili kuhakikisha tu. Hivyo, unaweza kuepuka kuvunja kanuni bila kukusudia. Hivyo, unaepuka pia kujitia mwenyewe, abiria wenzako, na mali ya shirika la ndege katika hatari. Naam, unaweza kufanya kusafiri kwa ndege kuwe salama zaidi.
[Picha katika ukurasa wa 25]
Je! unaweza kutambua ni vifaa vipi kati ya hivi ambavyo havifai kuwa kwenye mzigo wako?