Kuutazama Ulimwengu
Volkeno Yapunguza Joto la Dunia
Mlima Pinatubo wenye volkeno wa Ufilipino ulipolipuka katika 1991, wanasayansi walitabiri kwamba sayari yetu ingepoa kidogo likiwa tokeo. Walikuwa sahihi, kama ilivyotukia. Volkeno hiyo ilirusha tani zipatazo milioni 20 za gesi sulfuri dioksaidi katika tabakastrato. Gesi hiyo ilifanyiza wingu kubwa mno lililofanyizwa kwa vitone vidogo sana vya sulfuri asidi nalo lilitandazwa tufeni kote na mikondo ya hewa ya juu yenye mwendo wa kasi kwa muda wa majuma machache. Vitone hivyo hutawanyika na kuzuia baadhi ya miali ya jua, hiyo ikitokeza halijoto iliyopoa kidogo kwenye ardhi iliyo chini. Kulingana na Science News, tangu mlipuko huo, sehemu za Kizio cha Kaskazini zimekuwa na mshuko wa zapata digrii moja Sentigredi katika wastani wa halijoto. Hata hivyo, tokeo hilo ni la muda na halipasi kuonwa kuwa ponyo la joto linaloongezeka hatua kwa hatua duniani. Mtaalam mmoja wa tabia ya dunia alitabiri kwamba mwelekeo huo wa kupoa uliotokezwa na volkeno hiyo utakwisha kufikia 1994.
Biashara ya Viungo ya Esia
“Ugavi na Uhitaji ndiyo sheria ya bara,” lasema gazeti Asiaweek kuhusu habari ya biashara ya viungo vya kibinadamu. Katika Hong Kong watu wapatao 600 walikuwa wakingojea kupandikizwa figo katika masika ya 1992, lakini ni 50 tu wao waliotarajia kupokea figo moja kufikia mwisho wa mwaka huo. Kwa hiyo, wengi husafiri kwenda nchi nyinginezo, kama vile India ambako mapandikizo yapatayo 6,000 ya figo hufanywa kila mwaka katika biashara ya dola milioni 20 kila mwaka. Mara nyingi wale maskini au waliopatwa na msiba wa kifedha wana nia ya kuuza figo moja, kwa kuwa kwa kawaida mtu aweza kuendelea kuishi akiwa na moja tu. Lakini Asiaweek huandika kwamba biashara ya viungo inajaa ufisadi. Baadhi ya wapaji wamepunjwa pesa zao na walanguzi wafisadi. Yaripotiwa kwamba mwanamume mmoja alilazwa hospitalini akiwa na tatizo ndogo la tumbo na mwishowe akatoka bila figo moja—ilikuwa imetolewa bila idhini yake!
Machinjo ya Wasio na Hatia
Angalau watoto 1,383 katika United States waliuawa kwa kutendea vibaya au kwa kutotunzwa katika 1991, yaripoti The Washington Post. Kadirio hilo la kiasi, lililotolewa na Halmashauri ya Taifa ya Uzuiaji wa Kutendwa Vibaya kwa Watoto, hujumlika kuwa kiasi chenye kuchukiza cha vifo vinne vyenye kuhusiana na kutendwa vibaya kila siku, ongezeko la asilimia 50 kupita miaka sita iliyopita. Visababishi vya ongezeko hutofautiana. Baadhi ya wataalam hulaumu hali za uchumi zinazozidi kuwa mbaya—kufutwa kazi, mapato ya chini, na ukosefu wa tumaini—vikisukuma watu waonyeshe kukatishwa tamaa kwao kwa kuwatendwa vibaya watoto hao walio hoi. Gazeti Post laandika kwamba ingawa visa kadhaa vilivyotangazwa sana vimehusu yaya waliotenda vibaya watoto walio katika kabidhi yao, “wataalam wajua kwamba sababu hasa ya idadi hiyo ya vifo kwa kawaida huwa ni za kinyumbani, kwa mama na baba, wapaswao kuwapenda zaidi watoto hao.”
Idadi Kubwa Mno ya Watu—Kwa Nini?
Kwa nini idadi kubwa mno ya watu huenea sana katika nchi maskini zaidi? Katika gazeti Visão, Paul Nogueira Neto, aliyekuwa hapo zamani waziri wa mazingira katika Brazili, huliweka jibu kwa nguvu sana: “Kuna hadithi isimuliwayo katika Brazili. Akiulizwa kwa nini ana watoto tisa, mwanamume husema, ‘Kwa sababu watatu hufa wakiwa wadogo; watatu huhamia São Paulo, Rio de Janeiro, au Brasília, na watatu hukaa hapa kututunza tuzeekapo.’ Mtoto ni usalama wa kijamii wa watu maskini.” Neto huongeza, kwa kuonya hivi: “Ni rahisi kuona ulimwenguni kote: Kuliko na umaskini kuna ongezeko kubwa la idadi ya watu. Na likiendelea, sayari itakuwa katika hatari ya kuangamia. Katika ulimwengu wenye maliasili kidogo, hatuwezi kuwa na usitawi usio na kikomo, isipokuwa uwe wa kiroho, kiadili, au kisayansi.”
Yesu Katika Vidio
Matengenezo mbalimbali katika Jumuiya ya Wakristo yanatenda mambo yenye kuchukiza katika jitihada zao za kushawishi vijana wajipatie kadiri fulani ya ujuzi wa Biblia. Mathalani, American Bible Society limetokeza namna ya vidio ya simulizi kwenye Marko 5:1-20 juu ya Yesu akiponya mwanamume mwenye kupagawa na roho waovu. The Miami Herald la Florida huripoti kwamba mtindo ni ule wa vidio ya muziki, ikiwa na mandhari za maandishi yenye mwendo wa kasi. Namna moja imeambatanishwa na muziki wa rapu, nyingine imeambatanishwa na nyimbo. Yesu ameonyeshwa akiwa amevaa T-shati na jaketi akipigana ngumi na mwanamume huyo aliyepagawa na roho waovu na ambaye hutokwa na mate kinywani na aliyevaa kofia ya besiboli. Vidio nyingine ya muziki, iitwayo Resurrection Rap, yaripotiwa kwamba humwonyesha Yesu akiwa kiongozi wa genge la barabarani!
Maji Hatari Sana
Vita iishapo, jambo gani lifanywe na risasi zote zisizotumiwa? Kulingana na gazeti la Kijerumani Hannoversche Allgemeine, baada ya Vita ya Ulimwengu 2, Mataifa Marafiki yalitokeza jibu rahisi, ingawa si la busara: Zitupeni ndani ya bahari. Gazeti hilo laripoti kwamba kati ya tani 700,000 na 1,500,000 za risasi kutoka Utawala wa Nazi zilitupwa kwenye sakafu ya bahari, baadaye risasi za Mataifa Marafiki zingajiunga nazo. Mahali pa kutupa palichaguliwa—lakini hapakurekodiwa hususa sana ni mahali gani—katika Bahari ya Kaskazini, Baltiki, na Skagerrak. Ingawa baadhi ya taka hii hatari ilichukuliwa katika miaka ya 1950, tani zipatazo 500,000 zazo zafikiriwa kuwa zinabaki. Sasa hangaiko linakua juu ya hatari zilizotokezwa na taka hii ya chini ya bahari. Wapiga-mbizi wa serikali wanachunguza baadhi ya mahali hapo na kujaribu kukadiria ni risasi nyingi kadiri gani zilizopo na ni zenye hatari kadiri gani. Baadhi ya vilipukaji hivyo vingali vinaweza kufanya kazi, na baadhi yavyo vinavuja sumu hatari, kama vile asidi ya risasi, hidrajiri, na TNT, ndani ya maji.
Majeraha ya Trampolini
Trampolini kwenye ua wa nyuma zinakuwa zenye kupendwa na watu wengi, lakini zinaweza kutokeza hatari, laripoti The Toronto Star la Kanada. Ingawa wengine huziona kuwa vitu vya kuchezea, uchunguzi wa miaka miwili uliofanywa na Takwimu za Kanada uligundua kwamba majeraha mabaya 324 ya trampolini yaliripotiwa nchini kote. “Watoto wa umri wote wamo hatarini na majeraha wanayopata huelekea kuwa mabaya zaidi ya majeraha mengi ya utotoni,” kulingana na Arlene Huhn wa Spor Baraza la Tiba ya Michezo la Alberta. Aksidenti nyingi hutukia wakati watu wanapokuwa wakipanda au kushuka kwenye trampolini au wanapojaribu kupinduka, aongeza Huhn. Wataalam hupendekeza kwamba wenyeji waweke trampolini katika eneo la peupe, kwamba washiriki michezo wavae viatu vyenye kushika sawasawa, na kwamba watumie tahadhari wanapopanda au kushuka. Ni mtu mmoja tu kwa wakati mmoja anayepaswa kutumia trampolini. Usimamizi ufaao ni wa maana.
Uvamizi wa Nyoka
Miaka yapata 30 iliyopita, tauni ilipiga kisiwa cha Mikronesia cha Guamu na kumaliza zilizo nyingi za spishi zacho za ndege wa msituni. Tauni hiyo haikuwa virasi au dawa ya kuua wadudu bali nyoka—yule nyoka wa rangi hudhurungi aishiye mitini. Yawezekana waliingizwa kisiwani na meli za jeshi la U.S. kutoka New Guinea, idadi ya nyoka huyo iliongezeka sana katika Guamu. Sasa kuna wengi kama 12,000 wa nyoka hao wenye sumu kidogo kwa kila kilometa ya mraba katika maeneo fulani. Yaripotiwa kwamba wao hujiviringisha juu ya nyua na waya za umeme, huvamia makao, huchomoka bila kutazamiwa kutoka mabomba ya kuchukulia maji machafu, na kushambulia wanyama wa nyumbani na hata watoto. Sasa wataalam wa mazingira katika Hawaii wanahangaika kwamba nyoka hao watafanya shambulio kama hilo huko. Hawaii haina nyoka wenyeji, lakini ina spishi nyingi za ndege wenye kuvutia sana na wasiopatikana sehemu nyingi ambao wangeweza kushambuliwa kwa urahisi na walaji ndege hao. Kufikia sasa nyoka hao wameonekana kwenye wanja za ndege za Hawaii—kwa wazi wakijificha katika elopleni zenye kuwasili kutoka Guamu.
Venice Yapigana na Magugubahari
Venice, lile jiji zuri liinukalo kutoka wangwa mmoja kaskazini mwa Italia, lakabili tatizo la uchafuzi lisilo la kawaida—magugubahari. Kwa sababu ya vilishaji vingi mno majini, wangwa huo hukuza kiasi chenye kushangaza cha tani 500,000 za magugubahari kila mwaka! Jambo gani lifanywe nayo? Katika jaribio la kwanza la ulimwengu la aina hiyo, ambalo gazeti Le Scienze huliita “fanikio halisi,” magugu hayo yanageuzwa kuwa karatasi. Wakitumia baadhi ya tani 40,000 hadi 60,000 za magugu yanayovunwa kutoka wangwa huo kila mwaka, wanasayansi wametokeza karatasi kwa njia ambayo inafaa zaidi mazingira kuliko kutokeza karatasi kutoka kwa karatasi zilizokwisha kutumiwa. Karatasi hiyo inafanana na, na kwa njia fulani ni bora kuliko, karatasi ifanyizwayo kwa selulosi. Na rangi yayo? Kijani yenye madoa ya kijivu—kama vile ingetazamiwa!
Je! Ni Kuonyesha Fadhili Kikweli?
Hivi karibuni gazeti Consumer Reports lilitaja shirika moja la kufadhili la kansa lililopeleka barua likiomba watu wakusanye upaji wa fedha kutoka kwa marafiki na majirani na kulipelekea. Ripoti hiyo ilisema kwamba, kufahamu maana ya yale maandishi madogo yaliyo nyuma ya barua hiyo hufunua mambo fulani yenye kupendeza. Mathalani, ingawa shirika hilo la kufadhili lilipata karibu dola milioni 2.5 za U.S. mwaka uliotangulia, kiasi kinachopungua senti moja kwa kila dola kwa kweli kilitumiwa kwa hazina ya utafiti wa kansa. “Zilizobaki zililipa mchangishaji pesa wa kulipwa, zikalipia gharama za kuchangisha pesa, zikasimamia hazina, zikalipia mashtaka ya mahakamani yaliyotokana na maombi ya pesa yenye kupotosha ya wakati uliopita, na yakalipia ‘elimu ya umma,’” likataarifu gazeti hilo. Linataja kielelezo cha elimu ya umma inayotajwa—shauri lisilopendeza na la ujumla sana juu ya kuzuia kansa, kama vile, “Weka mahali pako pa kazi pakiwa bila hatari za kansa.”
Lugha na Ubongo
Kulingana na Franco Fabbro, mchunguzi kwenye Chuo Kikuu cha Trieste katika Italia, kila lugha tuijuayo, au tuijuayo kwa sehemu, huwekwa katika eneo maalum la ubongo. Alifikiaje mkataa huo? Idadi fulani ya watu wasemao lugha nyingi waliokuwa wamepatwa na jeraha la ubongo na ambao hawakuweza kujieleza kisahihi katika lugha yao wenyewe walianza kunena kwa ufasaha katika lugha ya kigeni waliyofikiri walijua kijuujuu tu. Hilo ladokeza, lasema gazeti L’Espresso, “kwamba lugha ya mama huingilia zile nyingine, ikizizuia zisijieleze.”