Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g93 2/22 kur. 22-24
  • Tamaa Ambazo Zilibadili Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Tamaa Ambazo Zilibadili Ulimwengu
  • Amkeni!—1993
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kupenda Viungo
  • Hali Zifaazo kwa Usitawi wa Viungo
  • Si Viungo vya Vyakula Tu
  • Zawadi Zilizofaa Mfalme
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2015
  • Wamishonari Wangesafiri Hadi Wapi Upande wa Mashariki?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2009
  • Safari ya Baharini Yenye Kutokeza ya Vasco da Gama
    Amkeni!—1999
  • “Tutakula nini?”
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2009
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1993
g93 2/22 kur. 22-24

Tamaa Ambazo Zilibadili Ulimwengu

Na mleta habari za Amkeni! katika India

KATIKA karne ya 13, Marco Polo aliviona kwa wingi. Christopher Columbus aliabiri ili akavipate lakini badala yake akagundua Ulimwengu Mpya. Katika karne ya 15, hatimaye Vasco da Gama alifika India kwa meli na akavileta kwa wanunuzi wenye hamu katika Ulaya. Kwelikweli, viungo (vya chakula) vilithaminiwa sana hivi kwamba watu walihatirisha maisha zao ili kuvipata!

Mabadiliko ya kisiasa yalipozuia njia za misafara ya barani, Vasco da Gama alitumia miaka miwili katika safari ya kilomita 39,000 kwenda na kurudi kuanzia Ureno kuzunguka ncha ya Afrika hadi India. Meli zake mbili ziliokoka safari hiyo, zikirudi na shehena ya viungo na vitu vingine vyenye thamani mara 60 ya gharama za safari hiyo! Lakini kufanikiwa kwa safari yake kulileta mzozano wa mataifa ya Ulaya. Katika karne tatu zilizofuata, Ureno, Uhispania, Ufaransa, Uholanzi, na Uingereza zilishindania udhibiti wa vyanzo vya viungo.

Historia ya viungo kama ilivyofanyiwa muhtasari na mwandishi mmoja, ni “hadithi yenye kusisimua, uvumbuzi, ushindi na ushindani mkali wa manowari.” Frederic Rosengarten, Jr., alisema katika The Book of Spices: “Viungo vilikuwa vya maana sana, kwa kweli vya lazima, kisiasa na kiuchumi pia, hivi kwamba wafalme walituma misafara ili wavitafute, wafanya biashara walihatirisha maisha na mali zao ili waviuze, vita vilipiganwa kwa ajili yavyo, idadi kubwa za watu wakatumikishwa, dunia yote ikavumbuliwa, na mabadiliko ya muda mrefu kama ule mvuvumko wa elimu uliletwa na ushindani mkali sana usiotulia.”

Waholanzi walipodhibiti biashara ya viungo, walipandisha bei ya nusu kilo ya pilipili manga kwa shilingi tano zaidi walipoiuzia Uingereza. Kikighadhabishwa na hilo, kikundi cha wafanya biashara wa London walikusanyika katika 1599 ili kuanzisha kampuni yao wenyewe ya biashara, ambayo baadaye ilikuja kuitwa East India Company. Hatimaye uvutano wa kampuni hiyo uliongoza kwenye utawala wa Uingereza wa zaidi ya miaka 300 katika India.

Ushindani mkali umetoweka, lakini tamaa ya viungo ya ulimwenguni pote huendelea. Na labda hakuna mahali pengine ambapo viungo hufurahiwa zaidi ya humu India.

Kupenda Viungo

Viungo na wapishi wa India hawatenganiki hivi kwamba mtu anaweza kusema kwamba nchi hiyo inapenda sana viungo. Ni nani kwa kweli, hajasikia juu ya mchuzi wenye viungo wa India—mlo uliochemshwa wa mboga, mayai, nyama nyekundu, samaki, au kuku wenye kukolezwa kwa unamna-namna wa viungo vitamu? Baadhi ya viungo hivyo huwa pia katika milo ya kumalizia chakula, ikithibitisha kwamba “-enye viungo” si sawa na “-enye pilipili.” Hata chai tamu yenye maziwa inayopendwa sana humu mara nyingi huongezewa utamu kwa iliki, karafuu, tangawizi kidogo, au mchanganyiko wa viungo. Kukiwa na hamu nyingi hivyo ya viungo, je inashangaza kwamba katika matumizi ya mtu mmoja mmoja yakisawazishwa, India ndiyo inayoongoza?

Hebu zuru jiko la mpishi Mhindi, nawe utaona viungo vya aina-aina katika unamna-namna wa rangi na sura. Miongoni mwavyo ni mbegu ndogo nyeusi za haradali; vijiti vinavyonukia, mdalasini ya hudhurungi; punje mbichi za iliki; manjano ya rangi dhahabu ye-nye kutokeza; tangawizi kijivujivu; na pilipili rangi nyekundu sana. Tofautisha unamna-namna huo na chupa moja ya bizari iliyo madukani katika nchi nyingi. Bila shaka, bizari ina mchanganyiko wa viungo mbalimbali, na ni ya muhimu. Lakini ni duni ikitumiwa badala ya mchanganyiko wa viungo—viitwavyo masalas—vinavyotumiwa India.

Masalas vya pekee vilivyotayarishwa huchanganywa kwa ajili ya vyakula tofauti, kutia ndani mboga, samaki, kuku, na nyama nyekundu. Lakini mara nyingi, kiungo kimoja kimoja huchanganywa wakati wa upishi, aina yavyo na kiasi kikitegemea mlo hususa. Mke wa nyumbani Mhindi aliye stadi ajua mpangilio hususa na wakati barabara ambapo kila kiungo chapaswa kuongezwa katika utaratibu wa upishi. Yeye aweza hata kutwaa ladha tofauti kutoka kwa kiungo kilekile kwa kukichoma, kukisaga, kukiweka kizima ndani ya mafuta moto, au kukichanganya na viungo vingine.

Mara nyingi wageni wanaoenda India hushangazwa na ule unamna-namna mwingi katika kutayarisha chakula. Kutia na tofauti kubwa ya wapishi wa India Kaskazini na India Kusini, tamaduni za kimkoa za nchi hiyo, kama vile Wabengali, Wagoa, Wagujarati, na Wapunjabi, wana matayarisho yao ya pekee. Itikadi za kidini pia huhusika katika ladha ya chakula. Hivyo, katika jimbo la Wagujarati, mtu huenda akawa na mlo wa mboga ulio desturi ya Wahindu, lakini katika sehemu ya kaskazini mwa India huenda akafurahia mlo wa nyama wa Mogul, kikumbusho cha siku za ushindi wa Waislamu. Kwa hiyo ukila katika usiku tofauti na familia za Kihindu, Kiislamu, Sikh, Jain, Parsi, na za Kikristo huenda usile mlo uleule.

Hali Zifaazo kwa Usitawi wa Viungo

Ingawa viungo husitawi katika dunia yote, India hutokeza zaidi ya nchi nyingineyo—zaidi ya aina 60 tofauti-tofauti. Na hiyo huuzia nchi za nje zaidi ya 160 viungo na bidhaa nzima-nzima za viungo au kwa namna ya poda. India Kusini huongoza katika utokezaji wa viungo nchini. Cochin, kwenye Bahari ya Uarabu, ambayo mara nyingi huitwa “Venice ya Mashariki” kwa sababu ya uzuri wayo na njia nyingi za maji, huandaa njia ya moja kwa moja kwenye viungo ambavyo vimesitawi kwa muda mrefu katika hali-hewa nzuri ya tropiki kando ya pwani ya Malabar.

Bandari ya Cochin imetumika kuwa soko la biashara ya kimataifa tangu nyakati za kale, kwa ajili ya Wafoinike, Wamisri, Waajemi, Wachina, Warumi, Wagiriki, na Waarabu. Kwa kupendeza, kitabu cha Biblia cha Ufunuo hutaja “wafanya biashara wa nchi” ambao biashara yao ilitia “kila chombo cha pembe . . . na mdalasini, na iliki [ya India, NW].”—Ufunuo 18:11-13.

Pilipili nyeusi, mashuhuri ikiwa “mfalme wa viungo,” ndiyo iliyotafutwa kwanza na wafanya biashara. Haikuwa tu kiungo cha chakula bali pia inahifadhi nyama na vyakula vingine vyenye kuharibika upesi. Kwa kuongeza viungo, vyakula ambavyo ama sivyo vingaliharibika na kuwa bure vingeweza kuhifadhiwa kwa mwaka mmoja au zaidi bila kuwekwa katika friji. Zaidi ya pilipili, wafanya biashara wa baadaye walitaka viungo vingine—iliki, giligilani, shamari, na uwatu, kutaja vichache tu.

Hata hivyo, viungo vyote vinavyositawi India havikutoka huko. Kwa mfano pilipili hoho ilitolewa Amerika Kusini. Dakt. C. V. Raman, mshindi wa tuzo la Nobeli wa India kwa ajili ya fizikia, wakati mmoja alisema kwamba ‘vyakula vyote si vitamu na haviliki bila pilipili.’ Wengi wenye malezi ya vyakula tofauti huenda wakapinga hilo. Lakini, kwa shukrani, ghala la dunia lilitiwa bidhaa za unamna-namna mwingi na Muumba mwenye upendo, akitosheleza mapendeleo mbalimbali yenye nguvu.

Si Viungo vya Vyakula Tu

Viungo vina historia yenye kuvutia. Biblia inaonyesha fungu la viungo katika mafuta, uvumba, na manukato ya kupaka. Inataja utumizi wa viungo katika mafuta matakatifu ya kupaka na katika uvumba uliotumiwa kwenye hekalu la Yehova katika Yerusalemu na husema juu ya viungo vikiongezwa katika divai. (Kutoka 30:23-25, 34-37; Wimbo Ulio Bora 8:2) Isitoshe, Biblia hufunua kwamba Wakristo wa mapema walinunua viungo ili kutayarisha mwili wa Yesu Kristo kwa ajili ya maziko.—Yohana 19:39, 40.

Huku India, vizazi vya wasichana Wahindi vimetumia mzizi wa rangi ya dhahabu yenye kutokeza ya mmea unaokaribiana na mtangawizi—manjano. Mchanganyiko wa manjano husuguliwa kwenye ngozi ili kusitawisha hali yayo. Leo, viwanda vya manukato na virembeshi hutumia mafuta kutoka kwa mbegu za pimento, kisibiti, mdalasini, namna ya mdalasini, karafuu, kungumanga, basibasi, halwaridi, na iliki katika mchanganyiko wa mafuta ya kufukiza na yasiyo ya kufukiza ili kufanyiza manukato mengi yenye kuvutia. Viungo hivyo pia huongezwa kwenye sabuni, poda za madini, mafuta ya kupaka baada ya kunyoa ndevu, marashi, viburudisha kinywa, na vitu vingine visivyohesabika.

Zaidi ya hiyo, viungo vimetumiwa kwa muda mrefu katika tiba. Miongoni mwa viungo vinavyopendekezwa na Ayurveda, sayansi ya tiba inayotolewa na maandishi ya Sanskrit ya Uhindu yaitwayo Vedas, ni tangawizi, mzizi-manjano, kitunguu saumu, iliki, pilipili, karafuu, na zafarani. Mtu anayezuru duka la dawa katika India leo bado atapata dawa ya mafuta ya mzizi-manjano kwa ajili ya majeraha na michomo, dawa ya meno yenye viungo 13, na bidhaa nyingine nyingi za viungo kwa ajili ya magonjwa mbalimbali.

Hivyo, pitio la historia ya viungo huonyesha kwamba bila viungo, mapendeleo ya chakula yangalikuwa tofauti, dawa haingekuwa ileile, na historia ingekuwa tofauti. Kwa kweli tamaa ya viungo ilikuwa na uvutano juu ya Ulimwengu wetu—katika njia nyingi.

[Picha katika ukurasa wa 23]

Kielelezo kidogo cha viungo vingi vinavyopendwa ulimwenguni pote

Mchuuzi wa barabarani akimpimia mteja viungo

Viungo vikingojea wanunuzi katika duka la Cochin

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki