Safari ya Baharini Yenye Kutokeza ya Vasco da Gama
Meli yapiga mwendo kwenye bahari yenye mawimbi ikiyapasua maji. Baada ya kukaa baharini kwa miezi kadhaa na kupatwa na magumu mengi, Vasco da Gama na mabaharia wenzake wanaelekea kuwa Wazungu wa kwanza kufika India kwa kusafiri baharini kuzunguka kusini mwa Afrika. Safari ya baharini kama hiyo ingekuwa ngumu hata ikiwa mtu angekuwa na ujuzi na vifaa vya kisasa vya kuabiri. Lakini lazima wale wanaume waliokuwa katika meli tatu ndogo za Da Gama, miaka 500 iliyopita, wawe waliona safari hiyo kuwa sawa na kwenda mwezini. Ni nini kilichomchochea mvumbuzi huyu Mreno mwenye ujasiri pamoja na watu wake kujasiria jambo hilo? Nayo safari yake iliuathirije ulimwengu?
KABLA ya kuzaliwa kwa Da Gama, safari yake ilikuwa imepangwa na Prince Henry Mreno, ambaye nyakati fulani huitwa Baharia (the Navigator). Chini ya uongozi wa Henry, safari na biashara za baharini za Wareno zilikuwa zimefana sana. Henry na wavumbuzi wengine waliosafiri baada yake waliona uvumbuzi, biashara, na dini kuwa mambo yaliyohusiana sana. Henry alikusudia kutajirisha Ureno na kuendeleza Ukatoliki. Alikuwa gavana wa Dini ya Kristo, dini kubwa zaidi ya kijeshi katika Ureno. Dini hiyo ilifadhiliwa na papa, na kwa kiasi kikubwa, gharama ya miradi ya Henry ililipwa na pesa zilizopatikana kutokana na dini hiyo. Kwa sababu hiyo, meli zake zote zilikuwa na msalaba mwekundu kwenye matanga yake.
Henry alipokufa mwaka wa 1460, Wareno walikuwa wamevumbua pwani ya magharibi ya Afrika hata kufikia kusini katika nchi ambayo siku hizi huitwa Sierra Leone. Mwaka wa 1488, Bartholomeu Dias alisafiri baharini kuzunguka mwisho wa Afrika. Kisha Mfalme John wa Pili akiwa na uhakika, akaagiza safari ya kwenda India ipangwe. Mfalme Manuel wa Kwanza, aliyetawala baada ya John, akaendeleza mipango hiyo. Wakati huo, vikolezo vya India vilipatikana Ulaya peke yake kupitia barani kutoka kwa wafanya-biashara Waitalia na Waarabu. Biashara kwenye Bahari ya Hindi ilifanywa hasa na wafanya-biashara Waislamu walio Waarabu. Manuel alijua kwamba kiongozi wa safari hiyo alipaswa kuwa “mtu aliyekuwa na ujasiri wa askari, ujanja wa mfanya-biashara, na busara ya balozi,” kama vile mwanahistoria mmoja alivyosema. Huenda ndiyo sababu iliyomfanya Manuel amchague Vasco da Gama.
Safari ya Baharini Isiyo na Kifani
Julai 8, 1497, wakiwa na bendera ya Dini ya Kristo, Da Gama na mabaharia wenzake 170 walipiga mwendo wakiwa wawili-wawili kuelekea kwenye meli zao mpya. Kasisi mmoja alimsamehe yeye na mabaharia wenzake dhambi zao wakiwa ufuoni. Iwapo yeyote kati yao angefia safarini, angekuwa amesamehewa dhambi zozote zile ambazo huenda akawa alifanya alipokuwa safarini. Yaonekana kwamba Da Gama alitarajia matata—alienda akiwa na mizinga ya kutosha pamoja na pinde, mishale, na mikuki mingi.
Da Gama aliamua kuepuka pepo na mawimbi makali ambayo Dias alikuwa amekabili miaka kumi mapema. Alipofika Sierra Leone, alielekeza meli zake kusini-magharibi mpaka akawa karibu zaidi na Brazili kuliko Afrika. Kisha pepo zilizokuwa zikivuma Kusini mwa Atlantiki zikamsukuma na kumrudisha Afrika karibu na Rasi ya Tumaini Jema. Hakuna rekodi iliyoko, inayoonyesha kwamba mtu mwingine yeyote alikuwa amesafiri kupitia njia hiyo hapo awali, lakini baadaye, meli zilizokuwa zikienda kwenye Rasi hiyo ziliipitia.
Akipita mahali ambapo Dias alikuwa amerudia, Da Gama alielekeza meli zake kwenye ufuo wa mashariki mwa Afrika. Msumbiji na Mombasa, masultani wenyeji walipanga njama ya kumwua Da Gama na mabaharia wenzake. Kwa hiyo Da Gama akasonga mbele kuelekea Malindi (kusini-mashariki mwa Kenya sasa). Hatimaye akiwa huko, alimkuta nahodha mwenye uzoefu aliyewaongoza kuvuka Bahari ya Hindi.
Magharibi na Mashariki Zakutana
Mei 20, 1948, baada ya kusafiri baharini kwa siku 23 tangu walipotoka Malindi, Vasco da Gama na mabaharia wenzake walitia nanga Calicut, India. Da Gama alimkuta zamorin, au mfalme Mhindi aliyekuwa akiishi katika utajiri na anasa nyingi. Baharia huyo alimweleza kwamba alikuwa na utume wa urafiki na kwamba yeye na watu wake walikuwa wakiwatafuta Wakristo. Mwanzoni hakutaja hata kidogo juu ya biashara ya vikolezo. Lakini wafanya-biashara ambao waliendesha biashara hiyo katika eneo hilo walitambua kwamba biashara zao zilikuwa hatarini nao wakamshauri mfalme awaharibu wadukizi hao. Walimwonya kwamba, ikiwa angefanya shughuli zozote na Wareno, angepoteza kila kitu. Akiwa ametaharuki kwa sababu ya shauri hilo, Mfalme alisitasita. Lakini hatimaye akampa Da Gama kile alichotaka—barua kwa mfalme wa Ureno ambayo ilisema kwamba mfalme wa India alikuwa amekubali kufanya biashara na mfalme.
Ulimwengu Uliobadilika
Da Gama alirejea Lisbon tarehe Septemba 8, 1499—akakaribishwa kama shujaa. Mara moja Mfalme Manuel akafanya mipango kwa ajili ya safari nyingine mbalimbali. Safari iliyofuata iliongozwa na Pedro Álvares Cabral, aliyeacha watu zaidi ya 70 huko Calicut ili kuendeleza masilahi ya Wareno. Lakini wafanya-biashara hao hawakuwa tayari kuvumilia kuingiliwa kwa biashara yao. Usiku mmoja kundi kubwa la watu liliua zaidi ya nusu ya watu hao. Da Gama aliporudi India akiongoza safari ya tatu, alilipiza kisasi, akashambulia Calicut kutoka kwenye meli zake 14 zilizokuwa na silaha za kutosha. Pia aliteka meli iliyokuwa ikirejea kutoka Mecca na kuichoma, akaua mamia ya wanaume, wanawake, na watoto. Ingawa walimwomba awarehemu, Da Gama aliwatazama bila huruma yoyote.
Wareno wakapata kuwa serikali yenye nguvu katika Bahari ya Hindi. Hatimaye, walifunga safari kadha wa kadha kwenda Malacca, China, Japani, na Moluccas (Visiwa vya Vikolezo). Waliamini kwamba watu waliokutana nao “hawakuongozwa na sheria ya Yesu Kristo” na kwa hiyo “walihukumiwa moto wa milele,” akaandika João de Barros, mchunguzi wa mambo wa karne ya 16. Kwa hiyo wavumbuzi hao walihisi wakiwa huru kutumia jeuri wakati wowote ule walipoona kwamba ilihitajiwa. Matendo hayo yasiyo ya Kikristo yaliufanya Ukristo uchukiwe sana katika Asia.
Matimizo ya Da Gama yalifungua njia ya baharini kati ya Ulaya na Asia. Kwa hiyo muhula mpya wa uvumbuzi ukaanza, ukitokeza dhana mpya miongoni mwa watu waliochangamana na wavumbuzi hao. “Hakuna yeyote kati ya watu hao,” aandika Profesa J. H. Parry, “ambaye hakuathiriwa na uvutano wa Ulaya, uwe wa kijamii, kidini, kibiashara, au kitekinolojia.” Kwa kiasi fulani, dhana za Magharibi zikipitia njia hizohizo, zilianza kuwa na uvutano mkubwa zaidi huko Ulaya. Hatimaye kubadilishana mawazo huko kukatokeza utamaduni mkubwa wa kibinadamu. Kwa kweli, vyovyote vile, ulimwengu wa leo ungali wahisi matokeo ya ile safari ya baharini yenye kutokeza ya Vasco da Gama.
[Ramani katika ukurasa wa 24, 25]
Njia aliyoipitia Vasco da Gama kwenye safari yake ya baharini ya kwanza
[Hisani]
Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.
[Picha katika ukurasa wa 26]
Mchoro wa mojawapo ya meli za Da Gama
[Hisani]
Cortesia da Academia das Ciências de Lisboa, Portugal
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 24]
Cortesia do Museu Nacional da Arte Antiga, Lisboa, Portugal, fotografia de Francisco Matias, Divisão de Documentação Fotográfica - IPM