Daraja Lililoitwa Vasco Da Gama
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA URENO
MAGAZETI ya habari ya Ureno yalijaa habari—mojawapo ya madaraja marefu zaidi katika Ulaya lilikuwa limezinduliwa tu kwa milipuko ya fataki. Machi 29, 1998, ikawa siku ya kufungua rasmi Daraja la Vasco da Gama lenye urefu wa kilometa 17.2. Likipewa jina la mwabiri Mreno aliyegundua njia ya bahari kutoka Ulaya Magharibi hadi India katika karne ya 15, daraja hili jipya lafungua njia mpya za kuelekea sehemu za kaskazini mwa nchi hiyo zenye viwanda, hadi fuo nyeupe za kusini katika Algarve, na hata kuelekea Hispania.
Daraja hilo, ambalo ni namba tano kati ya madaraja marefu zaidi ulimwenguni, lavuka Mto Tagus kutoka jiji kuu la Ureno, Lisbon, hadi mji wa Montijo, kuelekea kusini. Sehemu yake ambayo imening’inia yenye urefu wa meta 826 huwezesha meli kupita meta 45 chini.
Mwanzo Wenye Shamrashamra
Sherehe za ufunguzi hasa zilianza kwa karamu za juma zima kabla ya mzinduo rasmi. Msisimko ukatanda kotekote siku ya Jumapili, Machi 22, wakati watu 15,000 walipoalikwa kwenye mlo wa asili ya Kireno wa mchuzi wa maharagwe. Watu hao wote wangelishwa wapi? Bila shaka, kwenye daraja jipya! Ilivutia kama nini kuona meza iliyotandazwa kwa zaidi ya kilometa tano za daraja! Mlo ulifana sana, na watu walithamini sana mpango huo.
Uhitaji Wenye Kuongezeka
Kwa nini daraja kama hilo lilihitajika? Tangu 1966, Lisbon limekuwa likitumia daraja linaloning’inia linaloitwa Aprili 25 lenye urefu wa meta 1,013. Wastani wa magari 130,000 yalikuwa yanalitumia kila siku. Je, unaweza kuwazia msongamano huo wakati wa shughuli nyingi na wakati wa miisho-juma? Lilikuwa jambo la kawaida kwa wasafiri kutumia muda wa saa moja hadi mbili kuvuka kati ya Lisbon na sehemu ya kusini ya Ureno. Basi kukawa na uhitaji wa kuwa na njia nyingine. Leni sita za hilo daraja jipya, zikiwa kilometa 13 hivi kuelekea kwenye mto, zimetuliza hali. Daraja hilo limeundwa kwa njia ya kwamba magari yafikapo 52,000 kwa siku, leni ya ziada yaweza kuongezwa kwenye kila upande. Inatarajiwa kwamba magari yataenda haraka kwa mwendo usiopita kilometa 100 kwa saa.
Kuvuka Daraja Hilo
Jiunge nasi tuingiapo kwenye daraja hili kutoka kusini, katika Montijo. Tukiacha nyuma bwawa, sasa tuko katika sehemu ya kilometa kumi ya Mto Tagus. Ni wakati wa kujaa kwa maji nasi tumezingirwa kabisa na maji. Sehemu za kandokando ambazo haziwezi kufanya uteleze pamoja na nguzo 1,500 zinazotegemeza daraja hilo zinafanya uhisi salama.
Sasa twafikia sehemu inayoning’inia ya daraja. Sehemu hiyo inategemezwa na kamba zilizonyooka zinazopitia juu ya minara miwili yenye kimo cha meta 150, zinazofanana na tanga za mashua. Misingi ya vyuma vyenye kutegemeza daraja hilo ilichimbwa tokea meta 50 hadi 65 chini. Kwa ajili ya usalama zaidi, daraja hilo lilijengwa listahimili pepo zenye nguvu zinazoweza kufikia kilometa 220 kwa saa na mitetemeko ambayo inashinda kwa mara nne na nusu tetemeko la dunia lililoharibu sehemu kubwa ya Lisbon mnamo 1755.
Tufikiapo mwisho wa Daraja la Vasco da Gama, ukingo wa kaskazini-mashariki wa Lisbon watokea ukiwa na michikichi. Tukitaka, tunaweza kuendelea na barabara hiyo kuu ambayo inaweza kutupeleka kaskazini ya nchi hiyo. Daraja hilo jipya lafanya iwezekane kusafiri katika barabara nzuri sana tokea Algarve katika sehemu ya kusini hadi mkoa wa Minho kule kaskazini, bila kung’ang’ana na magari mengi ya Lisbon!
Hatua za Usalama
Wakati wa kujenga daraja hilo, usalama ulitiliwa maanani. Kukwama tu kwa gari kwaweza kusababisha msongamano mkubwa. Lakini, kukiwa na kamera za vidio 87 zikiwa zimewekwa sehemu zifaazo kwenye daraja na vitongoji vyake, kasoro zote katika mwendo wa magari hupelekwa kwenye viwambo ambavyo viko kwenye kituo cha polisi na kituo cha kuongozea magari. Gari likisimama, king’ora hulia katika chumba kikuu.
Kwa kuongezea, jumla ya simu 36 za dharura zimewekwa kila baada ya meta 400 kwenye sehemu ya kilometa 17. Mfumo huo wa dharura unafanyaje kazi? Magari maalumu husafiri kwa ukawaida kwenye daraja hilo ili kushughulikia uhitaji wowote uwezao kutokea, kutia ndani kuzima moto au kuvuta magari.
Namna gani juu ya mabadiliko makubwa kwenye anga? Vituo viwili vya kupima hali ya hewa hupima mwendo, uzito, na zinakoelekea pepo na kuchunguza hali za hewa na barabara, vikibadili-badili mwendo wa magari kwa kulingana na hali za anga.
Umaridadi wa nguzo za daraja huonekana dhahiri zaidi wakati taa zake zinapowaka usiku, lina taa 1,200 za barabarani.
Magumu ya Kimazingira
Haikuwa rahisi kuamua mahali ambapo daraja jipya lingekuwa. Ni mambo yapi yaliyohusika?
Mahali hapo palitatiza sana kimazingira. Hiyo ni kwa sababu daraja hilo lavuka hifadhi ya asili ya ndege, kwenye mojawapo ya milango-mto mikubwa zaidi katika Ulaya Magharibi. Uchunguzi mwingi ulihitaji kufanywa ili kulinda mimea, samaki, ndege, vitu vya kale, ubora wa maji na hewa, na mamia ya ekari ya mashimo ya chumvi. Kwa nini mlango-mto wa Tagus huvutia viumbe? Ni mojawapo ya kanda zenye unyevu zilizo muhimu zaidi ya Ureno na Ulaya, ikifanya pawe mahali pafaapo pa kutagia mayai kwa ndege wenye kusafiri ambao hulindwa kimataifa, kama vile mlonjo, kiluwiluwi aina ya Kentish plover, na membe-mdogo. Wakati wa majira ya kipupwe na vuli, maelfu ya ndege hutumia bwawa hili la chumvi kujikinga na kujaa kwa maji.
Sehemu za kuzalisha samaki za muda mrefu zilikuwa lazima zifikiriwe. Hilo lilimaanisha kwamba tahadhari ilihitajiwa ili samaki wasisumbuliwe kwa kadiri iwezekanavyo. Samaki elfu tatu, hasa wayo na sea bass waliwekewa alama ili kuchunguza hali ya mahali pao pa kuzalia.
Kwa ghafula, mazingira hayo ya asili na manyamavu yameletwa karibu na jiji. Yataathiriwa kwa kadiri gani? Inatumainiwa kwamba hatua zinazochukuliwa ili kuhifadhi ukingo huu wa kusini wenye thamani zitalinda mali-asili za hifadhi hii kwa kadiri iwezekanavyo.
Kwa kweli Daraja la Vasco da Gama ni utimizo mkubwa sana wa uhandisi, umaridadi, na ulinganifu wa ujenzi. Kwa kweli Ureno yaweza kujivunia daraja lililoitwa kwa jina la Vasco da Gama!
[Ramani/Picha katika ukurasa wa 15]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
URENO
HISPANIA
[Ramani]
URENO
Lisbon
Montijo
Daraja la Vasco da Gama
[Hisani]
Courtesy of Lusoponte/Sonomage