Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 11/8 kur. 10-13
  • Madaraja—Hali Ingekuwaje Bila Madaraja?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Madaraja—Hali Ingekuwaje Bila Madaraja?
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Madaraja ya Kale
  • Madaraja na Mahitaji Yetu Yenye Kubadilika
  • Aina za Madaraja
  • Tower Bridge Njia ya Kuingia London
    Amkeni!—2006
  • Kuvuka Ukanda Mkuu wa Denmark
    Amkeni!—1999
  • Daraja Lililoitwa Vasco Da Gama
    Amkeni!—1998
  • Daraja Lililojengwa Upya Mara Nyingi
    Amkeni!—2008
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 11/8 kur. 10-13

Madaraja—Hali Ingekuwaje Bila Madaraja?

“Ulisifu daraja lililokuvukisha.”—George Colman, mwandishi wa tamthilia Mwingereza wa karne ya 19.

NI LINI ulipovuka daraja kwa mara ya mwisho? Je, hata ulilifikiria? Mamilioni ya watu huvuka madaraja kila siku. Sisi huyachukulia madaraja kijuu-juu tu. Sisi huyapitia kwa miguu, kwa kutumia gari au kupitia chini yake, labda hata bila ya kuyafikiria. Lakini hali ingekuwaje bila madaraja?

Kwa maelfu ya miaka, kuwapo kwa madaraja ya aina mbalimbali kumewawezesha wanadamu na wanyama kuvuka mabonde ambayo hayangeweza kuvukika, yawe ni mto, ufa, au korongo. Ni vigumu kuwazia majiji fulani yakiwapo bila madaraja—Cairo, London, Moscow, New York, Sydney, na mengineyo mengi. Madaraja yana historia ya kale.

Madaraja ya Kale

Zaidi ya miaka 2,500 iliyopita, Malkia Nitocris wa Babiloni alijenga daraja la kuvuka Mto Frati. Kwa nini? Mwanahistoria Mgiriki Herodoto ajibu: “[Babiloni] liligawanyishwa mara mbili na mto. Chini ya wafalme wa awali, ikiwa mtu alitaka kuvuka mojawapo ya sehemu hizo mbili hadi nyingine, alilazimika kuvuka kwa mashua; jambo ambalo ni lazima lilisumbua sana.” Kwa kutumia mbao, matofali, na mawe kujengea na chuma na risasi kuwa kama sementi, Nitocris alijenga daraja juu ya mojawapo ya mito maarufu sana katika nyakati za kale.

Nyakati nyingine madaraja yamegeuza historia. Mfalme Dario Mkuu wa Uajemi alipoondoka kupigana na Waskithia, alitaka njia ya haraka zaidi iwezekanayo ya kufikia Ulaya kutoka Asia. Jambo hilo lilimaanisha kuongoza jeshi lake lenye wanaume 600,000 kuvuka Mlango-Bahari wa Bosporus. Ilikuwa hatari kuvuka mlango-bahari huo kwa mashua kwa sababu ya ukungu mwingi na mawimbi hatari, kwa hiyo Dario alizifunganisha pamoja mashua mpaka akafanyiza daraja lenye kuelea lenye urefu wa meta 900. Leo, huwezi kusumbuka sana kama alivyosumbuka Dario akivuka mlango-bahari huo. Unaweza kuvuka hapo kwa muda upunguao dakika mbili kwa gari ukitumia madaraja ya Bosporus jijini Istanbul, Uturuki.

Kama wewe ni mwanafunzi wa Biblia, huenda ukafikiria pindi ambapo ukosefu wa daraja ulibadili historia. Kumbuka yaliyotokea wakati Mfalme Nebukadneza wa Babiloni alipokizingira kisiwa kilichokuwa jiji la Tiro. Kwa miaka 13 alijaribu kuliteka jiji hilo, lakini hakufua dafu, sababu moja ikiwa kwamba hakukuwa na daraja lililounganisha kisiwa hicho na bara. (Ezekieli 29:17-20) Jiji hilo la kisiwa halikutekwa mpaka miaka mingine mia tatu iliyofuata, wakati ambapo Aleksanda Mkuu alipojenga barabara iliyoinuka juu ya bahari, iliyounganisha bara na kisiwa.

Kufikia karne ya kwanza, ‘barabara zote zilielekea Roma,’ lakini Waroma walihitaji madaraja na vilevile barabara ili kuunganisha milki hiyo pamoja. Wakitumia mawe yenye uzito wa tani nane hivi kila moja, wahandisi Waroma walijenga madaraja ya tao ambayo yalitengenezwa kwa ustadi sana hivi kwamba baadhi ya madaraja hayo yangalipo zaidi ya miaka elfu mbili tangu yajengwe. Mabomba yao vilevile yalikuwa madaraja.

Katika Enzi za Kati, nyakati nyingine madaraja yalitumika kama ngome. Mnamo 944 W.K., Wasakson walijenga daraja la mbao kuvuka Mto Thames kule London ili kukinza mashambulizi ya Wadenmark. Karibu miaka mia tatu baadaye, daraja hilo la mbao lilibadilishwa na daraja la Old London Bridge, ambalo limekuwa mashuhuri katika historia na katika mashairi ya watoto.

Kufikia wakati Malkia Elizabeth wa Kwanza alipoanza kutawala Uingereza, Old London Bridge halikuwa ngome tu ya mawe. Majengo yalikuwa yamejengwa kwenye daraja hilo. Maduka yalikuwa sehemu za chini. Na orofa za juu zikawa na nini? Hizo zikawa makao ya wafanyabiashara matajiri na hata ya washiriki wa makao ya kifalme. Daraja la Old London Bridge lilikuwa limekuwa kituo cha maisha ya kijamii cha London. Kodi zilizopatikana kutokana na nyumba hizo zilitumiwa kudumisha daraja hilo, na London Bridge hata likawa daraja la kutoza ada ya kuvuka!

Huku Wazungu wakishughulika kujenga madaraja kwa mawe, Wainka wa Amerika Kusini walikuwa wakiyatengeneza kwa kamba. Mfano mmoja maarufu wa daraja hilo ni lile San Luis Rey, ambalo lilivuka Mto Apurímac, nchini Peru. Wainka walitwaa nyuzi za mmea fulani na kuzisokota pamoja ili kufanyiza kamba nene kama mwili wa binadamu. Walizilaza kamba hizo kwenye majabali kisha wakazivusha juu ya mto. Baada ya kufunga kamba hizo kwenye pande zote za mto, wao walining’iniza vipande vya mbao ili kufanyiza daraja. Vikundi vya urekebishaji viliweka kamba mbili kila baada ya miaka miwili. Daraja hilo lilijengwa na kudumishwa vizuri sana hivi kwamba lilidumu kwa miaka mia tano!

Madaraja na Mahitaji Yetu Yenye Kubadilika

Ni lazima madaraja yaweze kustahimili matetemeko ya dunia, pepo zenye nguvu, na mabadiliko ya halijoto. Kama ambavyo tumeona, mpaka hivi karibuni wahandisi walikuwa wakitumia mbao, matofali, au mawe kujengea daraja. Magari yalipoanza kutumiwa kufikia mwisho wa karne ya 19, madaraja yaliyopo yalihitaji kuboreshwa na kupanuliwa ili kutoshea kuvuka kwa vitu vizito zaidi.

Kuvumbuliwa kwa magari-moshi pia kulichochea kujengwa kwa daraja na mtindo wa kulijenga. Mara nyingi reli zenye kutegemeka zaidi zilivuka mfereji mpana sana wa bahari au ufa wenye kina sana. Je, daraja lingeweza kujengwa ili kuvuka nafasi kama hiyo na kustahili uzito wenye kuongezeka daima wa mabehewa yaliyokuwa yakiongezwa? Kwa muda madaraja ya chuma yalitumika. Mojawapo ya madaraja maarufu zaidi mwanzoni-mwanzoni mwa karne ya 19 ni daraja linaloning’inia linalovuka Mlango-Bahari wa Menai katika North Wales, lililobuniwa na mhandisi wa Scotland Thomas Telford na kumalizika mnamo 1826. Lina urefu wa meta 176 na lingali linatumiwa! Lakini chuma huelekea kuvunjika-vunjika, na mara nyingi madaraja yalikosa kufanya kazi. Hatimaye, mwishoni-mwishoni mwa miaka ya 1800, feleji ilianza kutengenezwa. Feleji ikawa bora kujengea madaraja salama na marefu zaidi.

Aina za Madaraja

Kuna miundo mikuu saba ya madaraja. (Ona sanduku lililo juu.) Tutazungumzia aina mbili tu za daraja hapa.

Madaraja ya shikizowenza yana minara mikubwa miwili kwenye pande zote mbili za mto. Mihimili hushikanishwa kwenye kila mnara, kama ambavyo ubao wa kupigia mbizi hushikanishwa kwenye ukingo wa kidimbwi cha kuogelea. Ili kukamilisha daraja, mihimili huunganishwa katikati na boriti ngumu.

Mahali ambapo mto ni wenye msukosuko sana au ambapo sakafu ya mto ni nyororo sana, madaraja ya shikizowenza hupendelewa zaidi kwa sababu hayahitaji nguzo za kuchimbwa katikati ya mto. Kwa sababu ya uthabiti wake, madaraja ya shikizowenza yanafaa sana kuvushia vitu vizito kama vile magari-moshi.

Labda umepata kumwona mwanasarakasi akitembea kwenye kamba akiwa hewani. Je, ulitambua kwamba anatembea hasa kwenye daraja—daraja linaloning’inia? Baadhi ya madaraja yanayoning’inia ambayo yanatumiwa leo ni yenye utata sana kuliko kamba. Hayo yaweza kufanyizwa kwa kamba iliyofungwa pande zote mbili na kuning’iniziwa kikapu. Abiria aketi kwenye kikapu na kujisukuma kwenye nyaya zilizoegama kidogo mpaka afikapo upande mwingine. Ulimwenguni pote watu hutumia madaraja sahili ya kamba nyakati zote.

Bila shaka, huwezi kuwazia kamwe kuendesha gari kuvuka daraja lililofanyizwa kwa kamba. Baada ya kuvumbuliwa kwa minyororo ya vyuma na nyaya za feleji, iliwezekana kujenga madaraja yanayoning’inia ambayo yangeweza kustahimili vitu vizito. Kwa kawaida madaraja ya kisasa ambayo yananing’inia yana urefu wa meta 1,200 au zaidi. Madaraja yanayoning’inia hujengwa kwenye nguzo mbili za feleji, kila nguzo ikiutegemeza mnara. Kamba za feleji, zenye maelfu ya nyaya, hufungwa kwenye minara na kwenye barabara chini. Kamba hizo ndizo nguzo kuu zinazotegemeza uzito wa vitu vinavyovuka. Lijengwapo vizuri, daraja linaloning’inia ni mojawapo ya madaraja salama zaidi ulimwenguni.

Huenda zamani ulichukulia madaraja kijuu-juu tu. Lakini, wakati mwingine uvukapo daraja unalolijua, jiulize: ‘Najua nini kuhusu daraja hili? Lilijengwa lini?’ Lichunguze kwa makini. Je, hilo ni daraja la shikizowenza, linaloning’inia, au la aina nyingine? Kwa nini lilijengwa kwa muundo huu hasa?

Kisha, uvukapo, tazama chini, ujiulize, ‘Ningevukaje bila daraja hili?’

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 12]

MIUNDO YA MADARAJA

1. MADARAJA YA MHIMILI mara nyingi hutumiwa katika barabara kuu. Mihimili hulalia nguzo. Madaraja hayo yanaweza kuwa na urefu wa meta 300.

2. MADARAJA YA FARASI hutegemezwa na farasi zenye umbo la pembetatu. Madaraja hayo ambayo mara nyingi hutumiwa kwa reli, hutumiwa kuvuka mabonde yenye kina, mito na mengineyo.

3. Katika MADARAJA YA TAO kila sehemu kati ya mhimili hufanyiza utao. Hili ni mojawapo aina ya madaraja ya kale zaidi. Waroma walijenga aina hii ya utao katika mabomba yao na madaraja yao na kutumia mawe kufunga utao. Mengi yangalipo hadi leo.

4. MADARAJA YENYE KUTEGEMEZWA KWA KAMBA hufanana na madaraja yanayoning’inia ila tu kamba zimefungwa moja kwa moja kwenye minara.

5. MADARAJA YENYE KUSONGA yaweza kuinuliwa au kufunguliwa upande ili kuruhusu meli zipite. Mfano mzuri wa daraja la aina hii ni Tower Bridge ya London.

6. MADARAJA YA SHIKIZOWENZA yameelezwa katika makala hii.

7. MADARAJA YANAYONING’INIA yameelezwa katika makala hii.—World Book Encyclopedia, 1994.

[Chati katika ukurasa wa 13]

BAADHI YA MADARAJA MAARUFU

YANAYONING’INIA

Storebaelt Denmark meta 1,624

Brooklyn Marekani meta 486

Golden Gate Marekani meta 1,280

Jiangyin Yangtze China meta 1,385

SHIKIZOWENZA

Forth (sehemu mbili) Scotland meta 521

Quebec Kanada meta 549

Mto Mississippi Marekani meta 480

TAO ZA FELEJI

Sydney Harbour Australia meta 500

Birchenough Zimbabwe meta 329

ZENYE KUTEGEMEZWA KWA KAMBA

Pont de Normandie Ufaransa meta 856

Skarnsundet Norway meta 530

[Picha katika ukurasa wa 10]

Daraja la kisasa la mhimili likiwa juu ya daraja la kale la tao kule Almería, Hispania

[Picha katika ukurasa wa 13]

Brooklyn Bridge, New York, Marekani (linaloning’inia)

[Picha katika ukurasa wa 13]

Tower Bridge, London, Uingereza (lenye kusonga)

[Picha katika ukurasa wa 13]

Sydney Harbour Bridge, Australia (utao)

[Picha katika ukurasa wa 13]

Seto Ohashi, Japani (lenye kutegemezwa kwa kamba)

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki