Tower Bridge Njia ya Kuingia London
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UINGEREZA
WAGENI ambao hawajawahi kutembelea Uingereza hulitambua. Kila mwaka maelfu ya watalii hulitembelea. Kila siku, wakaaji wa London hulivuka, bila kulizingatia wala kufikiria historia yake. Daraja la Tower Bridge ni mojawapo ya maeneo maarufu zaidi huko London.
Daraja hilo lina uhusiano na Mnara wa London ulio karibu, nalo si sawa na Daraja la London lililo mbali kidogo. Huko nyuma katika 1872, Bunge la Uingereza lilijadili mswada wa kuidhinisha ujenzi wa daraja kwenye Mto Thames. Licha ya kupingwa na gavana wa Mnara wa London, Bunge liliamua daraja lingine lijengwe, mradi umbo lake lipatane na lile la Mnara wa London. Daraja la Tower Bridge lilijengwa kufuatia uamuzi huo wa Bunge.
Katika karne ya 18 na 19, madaraja mengi yaliunganisha kingo za Mto Thames, nalo daraja maarufu zaidi lilikuwa lile la Old London Bridge. Kufikia 1750, daraja hilo lilikuwa hafifu. Pia lilikuwa jembamba sana hivi kwamba magari yalisongamana yalipokuwa yakivuka. Chini yake, meli kutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni zilishindania nafasi kwenye bandari iliyosongamana. Nyakati hizo, kulikuwa na meli nyingi sana bandarini hivi kwamba mtu angeweza kutembea kwa kilometa nyingi juu ya sitaha za meli zilizokuwa zimetia nanga.
Alipoombwa maoni na serikali ya Jiji la London, mchora-ramani aliyeitwa Horace Jones alipendekeza daraja la kushusha na kupandisha la mtindo wa Kigothi lijengwe umbali fulani kutoka kwenye Daraja la London. Daraja hilo lingeruhusu meli zinazoelekea bandari iliyokuwa magharibi mwa Mto Thames zipite. Kwa maoni ya wengi, daraja hilo lilikuwa na muundo wa pekee.
Muundo wa Pekee
Jones alikuwa ametembelea maeneo mengi, na madaraja madogo ya kushusha na kupandisha ya mifereji ya Uholanzi yalimpa wazo la kujenga daraja lenye sehemu mbili zinazoweza kuinuliwa ili kuruhusu mashua ndefu na meli zipite. Jones na wenzake walifaulu kujenga daraja la Tower Bridge kwa kutumia mbinu mpya za ufundi zilizohusisha kutumia vyuma na saruji.
Daraja la Tower Bridge lina minara miwili iliyounganishwa kwa juu na vijia viwili vya miguu vilivyo meta 34 juu ya barabara na meta 42 juu ya mto unapokuwa umefurika. Barabara zinazotoka kwenye kingo zote mbili huishia kwenye sehemu ya daraja ambayo haisogei. Sehemu mbili za daraja zinazobembea zina uzito wa tani 1,200, nazo hubembea na kuinuka kwa pembe ya digrii 86. Hata meli zinazoweza kubeba mizigo yenye uzito wa tani 10,000 zinaweza kupita salama chini ya daraja hilo.
Nguvu za Kuendesha Daraja
Nguvu za maji ndizo hasa zilitumiwa kuinua sehemu za daraja zinazobembea, kuendesha lifti, na pia kutoa ishara za kuelekeza magari. Naam, liliendeshwa kwa nguvu za maji! Na kulikuwa na nguvu za kutosha, nguvu nyingi kuliko ilivyohitajiwa.
Chini ya upande wa kusini wa daraja hilo kulikuwa na vifaa vinne vya kuchemshia maji ambavyo vilitumia makaa ya mawe. Vifaa hivyo, vilivyotoa shinikizo la kilo 5 hadi 6 kwa sentimeta 2 mraba, vilipiga pampu mbili kubwa sana. Pampu hizo nazo zilipiga maji kwa shinikizo la kilo 60 kwa sentimeta 2 mraba. Ili kudumisha kiasi cha nguvu zilizohitajiwa kuinua sehemu za daraja zinazobembea, vifaa sita vikubwa vya kuhifadhi maji yaliyoshinikizwa vilitumiwa. Kisha nguvu hizo zikatumiwa kuendesha injini nane zilizoendesha sehemu zinazobembea za daraja. Injini hizo zilipowashwa, sehemu zinazobembea za daraja ziliinuka zikining’inia kwenye mitaimbo yenye kipenyo cha sentimeta 50. Ilichukua dakika moja tu kuziinua hadi juu kabisa.
Kutembelea Daraja la Leo la Tower Bridge
Leo nguvu za umeme zinatumiwa badala ya nguvu za mvuke. Lakini kama ilivyokuwa zamani, daraja hilo linapofunguliwa magari yote husimama. Wanaotembea kwa miguu, watalii na wageni wengine hustaajabia kuona jinsi linavyofanya kazi.
King’ora kinalia, navyo vizuizi vinashushwa kufunga barabara, gari la mwisho linapita, na waelekezaji wanatoa ishara kwamba mambo yako shwari. Kimyakimya makomeo manne yanafunguka na sehemu zinazobembea za daraja zinafyatuka kwenda juu. Kisha macho yote yanaelekezwa mtoni. Iwe ni mashua, motaboti, au meli, watu wote wanaitazama inapopita. Dakika chache baadaye ishara inabadilika. Sehemu hizo za daraja zinashuka kasi na vizuizi vya barabara vinaondolewa. Waendeshaji wa baiskeli wanachomoka mbele ya magari ili wavuke kwanza. Sekunde kadhaa baadaye, daraja la Tower Bridge linatulia tuli hadi pale litakapoinuliwa tena.
Mgeni anayependezwa hufanya mengi kuliko kutazama tu mfululizo huo wa matukio unaorudiwa-rudiwa. Anajiunga na wengine kupanda lifti hadi kwenye mnara wa kaskazini ili kustaajabia vitu mbalimbali vilivyopangwa kwa utaratibu kuhusu historia ya daraja hilo. Vitu hivyo vinatia ndani vidude vinavyotumia umeme, navyo vimo katika maonyesho ya “Tower Bridge Experience.” Michoro ya wasanii inaonyesha kazi ngumu ya wahandisi na sherehe za ufunguzi wa daraja hilo. Picha zisizo laini zenye rangi ya kahawia na vibao vya maonyesho hufunua muundo wenye kupendeza na kustaajabisha wa Tower Bridge.
Vijia vya miguu vya daraja hilo vilivyo juu sana humwezesha mgeni kutazama mandhari inayopendeza ya London. Upande wa magharibi, anaweza kuona Kanisa Kuu la St. Paul na majengo ya benki ya mtaa wa biashara, na kule mbali, anaweza kuona mnara wa Ofisi ya Posta. Upande wa mashariki, mtu anaweza kutazamia kuona bandari, lakini sasa bandari iko mbali na eneo la jiji. Badala ya bandari, ataona Docklands, eneo maridadi lenye majengo mapya yaliyoundwa kwa ustadi. Naam, akiwa kwenye daraja hilo maarufu la London, anaweza kuona mandhari maridadi, yenye kuvutia, na yenye kupendeza sana.
Ukitembelea London, mbona usichunguze kwa makini daraja hilo la kale? Bila shaka ukifanya hivyo utavutiwa sana na kazi ngumu na ya kustaajabisha ya wahandisi wa daraja hilo.
[Picha katika ukurasa wa 16]
Mojawapo ya pampu mbili zilizopigwa kwa mvuke ambazo zilitumiwa kuendesha injini
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]
Copyright Tower Bridge Exhibition
[Picha katika ukurasa wa 16, 17]
Sehemu mbili zinazobembea za daraja zikiwa zimeinuliwa kufikia kiwango chake cha juu zaidi kwa muda unaopungua dakika moja
[Hisani]
©Alan Copson/Agency Jon Arnold Images/age fotostock
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]
© Brian Lawrence/SuperStock