Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 2/8 kur. 24-27
  • Kuvuka Ukanda Mkuu wa Denmark

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuvuka Ukanda Mkuu wa Denmark
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Ng’ambo ya Ukanda Mkuu
  • Hali Yenye Kutatanisha ya Wapangaji
  • Daraja la Magharibi
  • Njia ya Chini kwa Chini Yenye Sehemu Mbili
  • Matatizo Waliyokabili
  • Daraja la Kuning’inizwa
  • Kuzinduliwa
  • Kinachomaanishwa na Kiungo Hicho
  • Madaraja—Hali Ingekuwaje Bila Madaraja?
    Amkeni!—1998
  • Daraja Lililoitwa Vasco Da Gama
    Amkeni!—1998
  • Tower Bridge Njia ya Kuingia London
    Amkeni!—2006
  • Barabara Ndefu Zaidi ya Chini ya Ardhi
    Amkeni!—2002
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 2/8 kur. 24-27

Kuvuka Ukanda Mkuu wa Denmark

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA DENMARK

TUNAPOTAZAMA Denmark kwenye ramani, tunaweza kuelewa kwa urahisi kwa nini raia wa Denmark wamekuwa mabaharia na wajenzi wa daraja kwa muda mrefu. Denmark ina visiwa 483 na peninsula inayojitokeza ndani ya bahari kutoka bara la Ulaya. Hivyo, sikuzote kusafiri kotekote katika Denmark kumehusisha kuvuka bahari.

Babu wa zamani wa Maharamia wa Skandinevia wa raia wa Denmark walijua namna ya kujenga meli zilizofaa kusafiri baharini. Na inaonekana kwamba kwa miaka mingi iliyopita, kila mji mdogo wa pwani ya Denmark umekuwa na huduma za feri zilizouunganisha na mji mwingine kwenye kisiwa jirani.

Ng’ambo ya Ukanda Mkuu

Hata hivyo, sikuzote kuvuka kwa meli kumekuwa jambo hatari. Iko hivyo unapovuka eneo pana la maji linalotenganisha visiwa viwili vikubwa zaidi vya Denmark, Sjælland na Fyn. Mlangobahari huu, Store Strait, unaenea kama ukanda mpana wa maji kutoka kaskazini hadi kusini; kwa sababu hiyo, mara nyingi unaitwa Ukanda Mkuu.

Ili kusafiri kati ya magharibi mwa Denmark na Sjælland, lilipo Copenhagen, jiji kuu la nchi, lazima uvuke Ukanda Mkuu. Zamani, hili lingemaanisha kutumia siku kadhaa ukisubiri pepo zibadili mkondo, dhoruba zitulie, au barafu ziyeyuke. Kuvuka kungechukua muda mrefu na kulikuwa hatari. Katika karne ya 16, kwa sababu ya barafu, kikundi cha kifalme kilikwama kwa muda wa juma moja kwenye kisiwa kidogo cha Sprogø, katikati ya kingo mbili.

Kwa hiyo, haishangazi kwamba wazo la kujenga daraja katika sehemu hii limewavutia raia wa Denmark kwa muda mrefu. Lakini je, daraja lolote lenye kujengwa na mwanadamu lingeweza kuvuka maji mengi yenye upana unaotoshana na Ukanda Mkuu? Lingehitaji kuwa na urefu wa kilometa 18, kutia ndani kisehemu kilichojengwa huko Sprogø. Lingefika mbali sana zaidi ya vile mtu awezavyo kuona kwa macho wakati wa halihewa ya kawaida—na ng’ambo ya bahari isiyozingirwa. Daraja la Golden Gate la San Francisco, ni lenye urefu unaopungua kilometa tatu.

Hali Yenye Kutatanisha ya Wapangaji

Kwa kweli, Bunge la Denmark lilianza kujadili suala la daraja hilo katika karne ya 19. Kwa miaka mingi iliyopita, wapangaji walihangaishwa na maswali kama haya: Je, tunataka daraja au njia ya chini kwa chini? Je, yapaswa kuunganisha magarimoshi, magari, au aina zote mbili za usafiri? Kuna ubaya gani wa kutumia feri tu?

Maelfu ya mipango ilifanywa, na maneno mengi sana yakanenwa. Usemi “mjadala wa Ukanda Mkuu” ukajulikana sana katika Denmark kukiwa na mazungumzo yasiyokoma. Lakini hatimaye, katika mwaka wa 1987, mkataa ulifikiwa. Makutano, yenye kuunganisha visiwa viwili vikubwa kwenye sehemu zao zinazokaribiana sana, yangekuwa kwa ajili ya magarimoshi na magari. Mradi huo ungehusisha madaraja mawili na njia ya chini kwa chini—muunganisho wenye umbali wa kilometa 18—pamoja uliitwa Kiungo cha Ukanda Mkuu.

Daraja la Magharibi

Kutoka kwenye kisiwa cha Fyn—mahali alipozaliwa mhadithiaji wa Denmark Hans Christian Andersen—muunganisho wa daraja la reli na la magari lililoimarishwa kwa saruji yenye chuma lilikuwa sehemu ya kwanza ya mradi huo. Lilikamilishwa Januari 1944, nalo linafanyiza nusu ya upande wa magharibi mwa kiungo hicho. Sasa ndilo daraja la Ulaya lililo refu zaidi linalounganisha reli na barabara. Likiwa na urefu wa meta 18 juu ya bahari, linaenea zaidi ya kilometa sita kuelekea upande wa mashariki kutoka Fyn hadi Sprogø.

Daraja hili la Magharibi, linalotegemezwa na mihimili iliyojengwa kwa saruji katika bahari, linafanyizwa kwa makumi ya visehemu kadhaa vya barabara ambavyo vingi vyake vina urefu wa meta 110. Visehemu hivi vilivyojengwa kwa saruji vilitengenezwa na kumaliziwa pwani. Lakini kila sehemu ilifikaje baharini na kuunganishwa na sehemu ya awali? Ili kutimiza hilo, mojawapo ya kreni kubwa zaidi ulimwenguni yenye kuelea ilitumiwa. Chombo hiki kikubwa sana cha kuinulia vitu kina urefu wa meta 90 na chaweza kuinua mzigo wenye uzito wa tani 7,100 na kuubeba hadi baharini. Uzito huo unazidi wa feri kubwa ya kubebea magari kwa kuongezea uzito wa magari 1,000!

Lakini kujenga njia mbili za reli na barabara kuu yenye sehemu nne za magari hadi kwenye kisiwa kidogo sana chenye mnara wa taa cha Sprogø hakukutosha. Kutoka hapo, ilihitaji kuunganishwa na sehemu mbili ambazo zingefuata za mradi huo. Ukingoni mwa Daraja la Magharibi, barabara hiyo hutengana na reli hiyo na kuelekea upande wa mashariki juu ya daraja jingine. Hata hivyo, reli huingia kwenye njia ya chini kwa chini yenye sehemu mbili na kuishia chini ya bahari.

Njia ya Chini kwa Chini Yenye Sehemu Mbili

Njia ya chini kwa chini, awamu ya pili ya mradi huo, ni mafanikio makubwa hasa. Njia za chini kwa chini mbili, kila moja ikiwa na kipenyo cha meta nane, zilijengwa kwa ajili ya magarimoshi. Hizo njia za chini kwa chini zilichimbwa ndani ya udongo, mawe, na matope ya maji kwa urefu wa kilometa 7.4. Na wajenzi wa njia ya chini kwa chini hawakuweza kukadiria kwa undani aina ya udongo ulio chini ya ardhi kabla ya kuanza kuchimba.

Hiyo njia ya chini kwa chini iko kati ya meta 10 na 40 chini ya bahari, ikitegemea mandhari iliyoko chini ya bahari—sehemu yenye kina zaidi ikiwa meta 75 chini ya usawa wa bahari. Kila moja ya mashine za kutoboa njia ya chini kwa chini zilizotumiwa ilikuwa na urefu wa meta zaidi ya 200, kutia ndani magarimoshi ya kuzitegemeza. Njia hizo za chini kwa chini zilizomalizika zimetandazwa kwa sehemu zilizopindwa 60,000 zilizotengenezwa kwa saruji, kila moja ikiwa na uzito upatao tani nane.

Wakianza kuchimba njia ya chini kwa chini kutoka sehemu zote mbili wakati huohuo, kwa ustadi wajenzi hao walifanikiwa kukutana katikati wakiachana kwa sentimeta nne. Lilikuwa tukio la pekee lililongojewa kwa muda mrefu wakati, katika Oktoba 15, 1994, Mkuu wa Denmark Joachim alipounganisha kirasmi nusu mbili za hiyo njia ya chini kwa chini kwa kuvuka kutoka mashine moja ya kutoboa hadi nyingine, ambayo ilikuwa ikichimba kuelekea ile ya kwanza. Kutoka Sprogø katikati ya Ukanda Mkuu, hizo njia mbili za chini kwa chini zilizokamilika sasa zinaelekea upande wa mashariki hadi pwani ya Sjælland. Tangu katikati ya mwaka wa 1997, magarimoshi huvuka kwa kasi Ukanda Mkuu yakiandaa huduma za kawaida.

Matatizo Waliyokabili

Maendeleo yalikuwa yamefanywa ya kuchimba njia ya chini kwa chini yenye sehemu mbili chini ya bahari wakati ambapo kwa ghafula wafanyakazi wote walikumbwa na ogofyo halisi—maji yalianza kuingia ndani ya hizo njia za chini kwa chini. Wajenzi wa njia ya chini kwa chini walitoroka, ingawa waliponea chupuchupu. Hata hivyo, mashimo mawili ya njia ya chini kwa chini, yalijaa maji ya bahari kabisa, na vifaa vingi vikapotezwa. Ni nini kilichokuwa kimetukia? Mashine zilifikia kijishimo cha maji ambacho hakikutazamiwa kilichokuwa chini ya bahari. Kama ambavyo ingetazamiwa, jambo hili lenye kufadhaisha lilipunguza mwendo wa mradi huo, na mbinu mpya ilihitaji kubuniwa ili kutatua tatizo hilo.

Kisha siku moja mlipuko wa moto ulizuka, na njia ya chini kwa chini ikajaa moshi upesi. Nyapara mmoja alieleza kwamba, “moshi huo ulikuwa mwingi sana hivi kwamba Pinocchio hangeweza kuona pua lake.” Wajenzi waliondoka katika sehemu hiyo, moto ukazimwa, na kazi ikasimamishwa mpaka chanzo cha moto kilipogunduliwa—mafuta ya haidroli yalikuwa yameshika moto. Tatizo hili na mengineyo yalifanya mradi wote ucheleweshwe mara kwa mara.

Daraja la Kuning’inizwa

Sehemu kuu ya tatu na yenye kufikia upeo ya Kiungo cha Ukanda Mkuu ni lile daraja maridadi la kuning’inizwa lenye urefu wa kilometa 6.8, la kuvusha magari. Daraja hilo latia ndani tao lenye urefu upatao kilometa 1.5, likilifanya kuwa mojawapo ya madaraja ya kuning’inizwa marefu zaidi ulimwenguni. Sehemu ya kati ya barabara iliyo upande huu wa mashariki mwa Kiungo cha Ukanda Mkuu imening’inizwa kwa urefu wa meta 67 juu ya bahari. Urefu huo ni wa lazima kwa sababu Ukanda Mkuu, ukiwa mojawapo ya njia ya majini yenye shughuli nyingi zaidi ulimwenguni, lazima iachwe ikiwa wazi kwa sababu ya meli.

Minara miwili mikubwa sana ya daraja hilo, au nguzo za chuma, kila moja ikiwa na urefu upatao meta 254, sasa ndiyo majengo marefu zaidi huko Denmark. Kwa kulinganisha, nguzo ya Statue of Liberty, katika New York Harbor, ina urefu wa meta 50 hivi, bila kutia ndani sehemu yake ya chini. Bila shaka, minara hii mikubwa sana katika bahari huhitaji msingi thabiti. Ili kuandaa hili, sehemu iliyo chini ya maji ilisawazishwa kwa uangalifu na kufunikwa kwa “mto” wa mawe ambao hutumika kama msingi wa kitundu cha kuzuia maji yasiingie, ambayo ni masanduku makubwa yaliyojengwa kwa saruji yanayotegemeza mnara. Kila moja ya vitundu hivyo vya kuzuia maji yasiingie kina urefu wa meta 78, upana wa meta 35 na urefu wa kwenda juu wa meta 19 na uzito wa tani 35,000.

Katika kujenga nguzo za chuma, jukwaa la kujengea la kipekee lenye kusongezwa lilitumiwa. Saruji ilimwagwa kwa sehemu—meta nne wima kila moja baada ya nyingine. Sehemu moja ilipomalizika, jukwaa hilo lilisongezwa juu, na meta 14 zaidi ziliongezewa juu yake. Ilichukua sehemu 58 kwenda juu ili kukamilisha kila mnara.

Sehemu yenye kuvutia sana ya daraja la kuning’inizwa ni kusokotwa kwa nyaya ngumu zinazotumiwa kulitegemeza. Nyaya hizi ni fungu lililopangwa vizuri la nyaya 169 zilizo ndogo zaidi, kila moja yake ikifanyizwa na nyaya 127 za feleji, kila moja ikiwa na kipenyo cha upana wa sehemu mbili kwa kumi ya inchi. Mafungu hayo mazito sana ya nyaya yalipandishwaje hewani? Hayakupandishwa! Badala yake, yaliunganishiwa mahali pa ujenzi. Kila waya ilifungiliwa kwenye kigari cha pekee kilichoivuta hadi kwenye sehemu ya juu ya mnara huo, chini kwenye upande mwingine, kisha juu ya mnara mwingine, na hatimaye chini kwenye msingi. Kila safari ilifanya waya hiyo iwe nene kidogo. Baada ya mwaka mmoja na visafari 20,000 vya vigari hivyo vyenye magurudumu, hatimaye waya hiyo ilikamilika.

Kuzinduliwa

Hatimaye, mnamo Juni 1998, sehemu zote za muunganisho huo zilikuwa tayari kufunguliwa rasmi. Kiungo cha Ukanda Mkuu kilikuwa shughuli thabiti na ghali kwa taifa dogo, na raia wa Denmark walifuatia ujenzi huo kwa upendezi. Kwa sababu hiyo kufunguliwa kulipangwa kuwe sherehe kwa wote waliotaka kushiriki.

Kabla ya madaraja hayo kuanza kutumiwa na magari, watu na waendesha baiskeli walipata fursa isiyoweza kurudiwa ya kuyavuka. Siku moja ya jua mnamo Juni, watu zaidi ya 250,000, kutia ndani wenye kutembea kwa miguu, watumiaji wa mbao za kuteleza, wenye kutumia rolasketi, na waendesha baiskeli, walimiminika kwenye ‘kijiji cha mzinduo’ kilichokuwa maridadi. Kilikuwa na vibanda vya kuuzia soseji katika mkate, majukwaa ya muziki, na maduka ya kuuzia vitu vya ukumbusho na nje kwenye daraja watu wangeweza kufurahia mandhari yenye kusisimua ya bahari na pwani.

Wakati wa sherehe hizo, malkia wa Denmark alisema kwamba neno “mjenzi wa daraja” ni mojawapo wa usemi mzuri zaidi unaoweza kutumiwa kuhusu mtu yeyote. Ndege za kijeshi zikiwa katika mpangilio zilivuka anga juu ya daraja. Wimbo mpya uliokuwa umetungwa “Bridge Cantata,” uliimbwa. Ulitia ndani saluti ya kuagana kutoka kwa moja ya feri za zamani. Ikiwa ni sehemu ya muziki, kiongozi alipoelekeza kifimbo chake kwenye kamera ya televisheni, feri iliyokuwa ikisubiri kilometa moja baharini ilipokea ishara hiyo na kuvumisha parapanda yake ya kutangaza hatari yenye sauti kubwa kusudi wote wapate kusikia.

Jioni baada ya mzinduo, feri nyingi kupita kiasi zilikusanyika chini ya daraja la kuning’inizwa na kuvumisha honi zao ikiwa ishara ya kuomboleza kwamba sasa zitaacha kutumiwa.

Kinachomaanishwa na Kiungo Hicho

Sasa kwa kuwa jitihada za maelfu ya wapangaji na wafanyakazi zimefikia kikomo, tokeo ni gani? Bila shaka, Denmark imejipatia uvutio wa wageni, kwa kuwa madaraja hayo yanavutia kikweli unapokuwa kwenye bara au baharini. Unapokuwa ndani ya gari, hutaweza kusahau pindi uvukapo daraja lililo kubwa sana hivi kwamba mara nyingi ni vigumu kuona mwisho mmoja au miisho yote miwili! Na, bila shaka, kuvuka sasa kunachukua muda mfupi kweli. Ingawa feri ilitumia muda unaozidi saa moja, sasa garimoshi huvuka kwa kasi kwa dakika saba tu!

Kiungo hicho tayari kinabadili mazoea fulani ya watu. Raia wengi zaidi wa Denmark wanazuru marafiki, wanafanya biashara, au wanaenda kujitumbuiza ng’ambo ya bahari. Ukuzi wa miji na wa biashara unaathiriwa kwa sababu sasa inawezekana kufanya kazi upande mmoja wa ukanda huo na uwe na nyumba upande ule mwingine. Na bidhaa zaweza kusafirishwa ng’ambo ya nchi haraka zaidi ya ilivyokuwa awali.

Lakini kitu fulani pia kimepotezwa. Feri zilizosafiri mara nyingi katika bahari hii ziliwakilisha utamaduni uliodumu kwa karne kadhaa, na wasafiri wengi walipendelea kipindi cha pumziko walichopata kwa kusafiri kwa feri. Mwanabiashara mmoja alilalamika akisema hivi, “nitazikumbuka feri hizo.” “Bahari na mashua kubwa huvutia. Mimi hufurahia kupigwa na upepo ninapokuwa kwenye sitaha.” Hata hivyo, hakuna shaka kwamba kiungo hicho kipya kitaunganisha sehemu mbalimbali za ufalme wa kisiwa cha Denmark na kurahisisha usafiri wa kwenda na kutoka kaskazini mwa Ulaya.

[Ramani katika ukurasa wa 25]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

DENMARK

FYN

SJÆLLAND

FYN

DARAJA LA MAGHARIBI

SPROGØ

NJIA YA CHINI KWA CHINI

DARAJA LA KUNING’INIZWA

SJÆLLAND

RELI

BARABARA KUU YA MAGARI

[Picha katika ukurasa wa 26]

Jioni ya mzinduo wa kukamilishwa kwa daraja la kuning’inizwa

[Hisani]

Nordfoto, Liselotte Sabroe

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki