Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g93 2/22 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1993
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Vitovu vya Dini ya Ulozi Katika Makaburi ya umma
  • Uuaji Waendelea
  • Ugonjwa na Kifo
  • Paka na Ndege
  • Michezo na Afya
  • “Jambo Lililo Kinyume Kuhusu Wingi”
  • Mafunzo Yasiyokusudiwa
  • Kutostahi Wale Waliozeeka
  • Biashara Nzuri
  • Kuwahofu Wagonjwa
  • Popoo na Kansa
  • Watengenezaji Stadi wa Pesa Bandia
  • Vifo vya Ugonjwa wa Pumu Vyaongezeka
  • Magonjwa ya Kuambukiza Katika Karne ya 20
    Amkeni!—1997
  • Kwa Nini Wanadamu Wanateseka?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2001
  • Je, Utafune Tambuu?
    Amkeni!—2012
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1992
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1993
g93 2/22 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Vitovu vya Dini ya Ulozi Katika Makaburi ya umma

Baraza la Jiji na meya wa São Paulo, Brazili, hivi karibuni walikubali utumizi wa nafasi iliyoko katika makaburi ya manispaa kuwa “vitovu vya dini ya ulozi,” bila malipo, kulingana na Jornal da Tarde. Wapinzani walizusha malalamiko dhidi ya vitovu hivyo, wakidai kwamba mafarakano ya Kiafrika na Brazili yatatumia makaburi hayo kutoa dhabihu za wanyama zenye kukirihisha. Vielelezo vya wanyama waliopatikana wametendwa vibaya, kukatwa-katwa, au kuuawa vilitia ndani mbwa wadogo waliozikwa wakiwa wangali hai ndani ya wanyama wakubwa zaidi na paka na mbwa waliong’olewa macho. Ofisa mmoja wa serikali alitaja kwamba mafarakano hayo hayakuja Brazili kivyayo lakini kwamba watumwa waliozoea kawaida hizo waliletwa kwa nguvu kutoka Afrika. Kwa sababu hiyo, yeye alimaanisha kwamba mafarakano ya dini ya ulozi yapaswa kuheshimiwa.

Uuaji Waendelea

Kulingana na JAMA (Journal of the American Medical Association), inakadiriwa kwamba wakati wa Vita ya Ulimwengu 1, asilimia isiyozidi 19 ya watu waliouawa katika vita walikuwa raia. Kufikia Vita ya Ulimwengu 2, karibu asilimia 50 ya wale waliouawa katika vita walikuwa raia. Tangu wakati huo, vita vipatavyo 150 vimepiganwa ulimwenguni kote. Kulingana na JAMA, “inakadiriwa kwamba zaidi ya asilimia 80 ya wale milioni 20 waliouawa na milioni 60 kujeruhiwa wamekuwa raia, wengi wao wakiwa watoto. Katika mwongo uliopita pekee, watoto wakadiriwao kuwa milioni 1.5 wameuawa na zaidi ya milioni 4 wakalemazwa na vita.”

Ugonjwa na Kifo

Ulimwenguni kote, watu wapatao milioni 50 hufa kila mwaka. Kati ya vifo hivyo, milioni 46.5 hushirikishwa moja kwa moja na ugonjwa, kulingana na WHO (Shirika la Afya Ulimwenguni). Magonjwa ya kuambukia na ya vimelea huua watu milioni 17.5 kila mwaka. Magonjwa ya moyo huua karibu milioni 12. Kansa huua zaidi ya milioni tano. Hiroshi Nakajima, mkurugenzi-mkuu wa WHO, alisema: “Msiba ni kwamba kuna angalau vifo milioni 20 kila mwaka ambavyo vingeweza kuzuiwa kukiwa na utunzaji wa afya uliositawishwa, kupatikana kwa madawa na chanjo muhimu, mtindo-maisha ufaao zaidi na elimu.”

Paka na Ndege

Watafiti wanakadiria kwamba katika Wisconsin, U.S.A., pekee, paka aweza kuua ndege zaidi ya milioni 19 kila mwaka. Uchunguzi katika Uingereza huonyesha kwamba paka milioni tano huua karibu ndege milioni 20 kila mwaka. Katika Australia, maofisa wa mji katika Sherbrooke Shire waliagiza wakazi wafungie wanyama-rafiki nyumbani wakati wa usiku, ukiukaji ukimtoza mtu faini ya dola 100, katika jitihada za kukomesha uuaji wa ndege wasiopatikana kwa urahisi. Katika United States, paka wapatao 35,000 huzaliwa kila siku. Lakini kama vile gazeti National Wildlife linavyoripoti, “uchunguzi wa Wisconsin ulipata kwamba asilimia 94 ya wenye paka walitaka ndege mwimbaji kwenye makao yao na asilimia 83 walitaka ndege wa kuwindwa, lakini ni asilimia 42 pekee waliotaka kupunguza hesabu ya paka ili kunufaisha jamii hiyo ya ndege.”

Michezo na Afya

Wastadi wanaonya kwamba kuulazimisha mwili kufanya tendo fulani kubwa usilozoea kwaweza kukufanya uwe mgonjwa. Gazeti The European liliripoti: “Utafiti wa wanasayansi wa tiba umefunua kwamba wanamichezo mashuhuri huelekea zaidi kupata maambukio ya virasi kama mafua, maumivu ya koo na ya mwili kuliko wengine.” Klaus Braumann, mshauri wa tiba wa timu ya Olimpiki ya Ujerumani, alihoji wanamichezo mashuhuri 481 wa Ujerumani. Kulingana na Süddeutsche Zeitung gazeti la kila siku, yeye alipata kwamba wao “huugua mafua kwenye midomo [vilengelenge visivyowasha] mara nne zaidi ya watu wa wastani.” Ingawa inakadiriwa kwamba katika Ujerumani karibu asilimia 10 ya watu wote huwa na mafua hayo mara kwa mara, asilimia 50 hivi ya wanamichezo mashuhuri hupatwa nayo. “Kila jitihada ya kimwili inayopita kiwango fulani yaweza kuudhoofisha mfumo wa kinga wa mwili,” akasema Heinz Liesen, stadi wa tiba ya michezo.

“Jambo Lililo Kinyume Kuhusu Wingi”

Kwenye mkutano wa hivi karibuni katika Geneva, Uswisi, mashirika mawili ya UM yalitangaza kwamba yataunganisha jitihada zayo katika “mojawapo hatua kubwa zaidi zilizopata kuchukuliwa dhidi ya utapiamlo [ukosefu wa ulishaji bora mwilini] wa ulimwenguni pote.” Gazeti la Paris la kila siku Le Monde laripoti kwamba Shirika la Chakula na Kilimo na Shirika la Afya Ulimwenguni yalisema kwamba yangechukua hatua ili kushinda kile yalichoita “jambo lililo kinyume kuhusu wingi.” Ingawa dunia hutokeza chakula cha kutosha kuweza kuridhisha mahitaji ya ulaji ya familia nzima ya kibinadamu, ugavi haugawanywi katika njia zinazopatana na mahitaji hayo. Katika Afrika, kila siku njaa hutisha maisha za watu milioni 40. Utapiamlo huathiri watoto milioni 192, na 40,000 yao hufa kila siku.

Mafunzo Yasiyokusudiwa

“Wazazi wanapovuta sigareti, inaelekea watoto wao watafuata mfano wao,” lasema gazeti la Paris Le Figaro. Uchunguzi wa hivi karibuni uliohusu vijana Wafaransa zaidi ya 10,000 kuanzia umri wa miaka 11 hadi 18 ulifunua kwamba karibu robo yao ni watumizi wa tumbaku kwa ukawaida—kumaanisha wao huvuta sigareti angalau mara moja kwa siku. Uchunguzi huo ulifunua kwamba miongoni mwa vijana wenye kuvuta sigareti, zaidi ya asilimia 50 wana baba wanaovuta sigareti. Pia ulionyesha kwamba karibu asilimia 72 ya vijana walio wavutaji wa kawaida hutamani kuacha kuvuta sigareti.

Kutostahi Wale Waliozeeka

Idadi ya watu wazee katika Esia inakua haraka sana. Katika Japani wengine wanatazamia idadi ya watu wenye miaka 65 na zaidi ikue kutoka milioni 15.5 iliopo hadi milioni 32 katika muda wa miaka 30 ijayo. Kulingana na Asiaweek, 1 kati ya kila Wajapani 4 atakuwa mzee kufikia mwaka 2020. “Wasingapore zaidi ya asilimia 9 wana umri wa miaka 60. Na kufikia mwisho wa karne hii, Wamaleya wapatao milioni 1.5 watastahili kuwa raia wenye umri mkubwa,” ikaongeza Asiaweek. Ongezeko hilo laja katika wakati ambapo desturi za zamani za kuwatunza na kuwastahi wazee zimepunguka. Henry Lim, wakili wa raia wenye umri mkubwa katika Singapore, alisema: “Kuna mwelekeo unaozidi kuongezeka wa kutoonyesha staha watu wazee.” Yeye aliongeza kwamba watu wachanga zaidi “hutumia wakati mwingi zaidi wakiwa na mbwa mdogo kuliko kuwa na wazazi wao.”

Biashara Nzuri

Katika Argentina, ripoti juu ya dhabihu za wanyama na wanadamu zimehangaisha watu. Kulingana na Clarín, kuna mafarakano 5,000 katika Argentina, mengi yayo yakitumia uasiliani-roho, Ushetani, na aina nyinginezo za uchawi. Utumizi wa mifano ni wenye maana miongoni mwa mafarakano hayo. Katika Buenos Aires ni kawaida kupata maduka yenye mifano ya Yesu Kristo na ya “watakatifu” Wakatoliki kwenye rafu zilezile na sanamu za mashetani. Mfano mmoja mashuhuri unaitwa “Lusifa, Kapteni Mkuu na aliye wa kutisha sana miongoni mwa miungu ya uovu.” Clarín lataja kwamba wafanyizaji wa mifano hiyo ya kishetani hugawanya mifano ya Katoliki pia. Mwenye duka mmoja alikiri kwamba uuzaji wa mifano ya Katoliki na mifano ya kishetani ni “biashara nzuri.”

Kuwahofu Wagonjwa

Huenda hofu ya kuambukizwa ugonjwa na wagonjwa wao kukawa kunaathiri sana tabia ya wafanyakazi wa afya, kulingana na New York Times. Madaktari wengi wanaogopa kuambukiwa UKIMWI au mchochota wa ini kwa kujidunga au kujikata ngozi yao kwa vifaa vya tiba bila kukusudia wanapowatibu wagonjwa. Kwa wazi hofu hiyo ina sababu. Uchunguzi uliofanywa katika hospitali ya Jiji la New York ulifunua kwamba karibu asilimia 60 ya madaktari wanaotibu wagonjwa wa kifua kikuu kwa ukawaida wameambukizwa ugonjwa huo wao wenyewe. Pia, kila mwaka wafanyakazi wa hospitali karibu 12,000 huambukizwa mchochota wa ini na wagonjwa. Tangu mweneo wa UKIMWI uanze, wafanyakazi wa hospitali karibu 47 katika United States wameambukizwa na ugonjwa huo na wagonjwa wao.

Popoo na Kansa

“Kutafuna au kutotafuna . . . hilo ndilo swali.” Swali hilo, linalohusu kutafuna popoo, lilizushwa katika Post-Courier, gazeti moja katika Papua New Guinea. Dakt. Barrie Milroy, mpasuaji maalum mwenye ustadi wa kutibu watafunaji wa popoo, alisema kwamba “inaonekana kwamba matatizo mawili makubwa katika Papua New Guinea ni maleria inayodumu na kansa ya mdomo, kansa hiyo ikihusishwa na utafunaji wa popoo.” Hata watoto wadogo wamo miongoni mwa watafunaji wa kawaida wa popoo. ‘Ikiwa mtu anatafuna popoo, swali si kama aweza kupata kansa, bali ni ataipata lini,’ akasema Dakt. Milroy. Aliongeza kwamba isipokuwa watu waache kutafuna popoo, “hawawezi kusaidiwa sana kitiba.”

Watengenezaji Stadi wa Pesa Bandia

“Ni Jambo moja pesa bandia kumpita mwenye duka au karani wa benki asiyeshuku. Lakini ni jambo tofauti kabisa kudanganya vifaa vya hali ya juu vya kuchunguza pesa kwenye Hazina ya Kitaifa,” lasema The Wall Street Journal. Na bado, mtu fulani amekuwa akitokeza noti za dola 100 pesa za U.S. zinazofanya hilohilo. Zinaitwa “nzuri isivyo kawaida,” noti hizo bandia zimekuwa zikitokea ghafula kote duniani. Ule mtindo mgumu wa kuchapia kwa kutumia chapa iliyoinuliwa, ile karatasi yenye msingi wa nguo pamoja na nyuzi nyekundu na buluu za kutambulisha, na ile rangi ya kipekee yenye sumaku, vyote hivyo vimeigwa kwa ustadi. Noti hizo bandia ni za ustadi sana hivi kwamba badala ya kufuata ule utaratibu wa kawaida wa kutoza benki kwa kupitisha noti hizo bandia, serikali ya U.S. inakubali hasara hiyo. Baadhi ya wakuu huhofia kwamba noti hizo bandia ni kazi ya kikundi cha maharamia au serikali fulani ya kigeni yenye uadui.

Vifo vya Ugonjwa wa Pumu Vyaongezeka

“Idadi ya watu wanaokufa kwa ugonjwa wa pumu [nchini Ujerumani] imeongezeka kwa kutazamisha,” likasema gazeti la kila siku Süddeutsche Zeitung. Kulingana na Shirika la Njia ya Kupumua la Ujerumani, mwaka 1991 watu zaidi ya 5,000 walikufa kwa sababu ya magonjwa ya kupumua katika nchi hiyo. Katika miaka ya katikati ya 1970, hesabu inayolingana ilikuwa karibu 2,000 kwa mwaka. Wenyeji wapatao milioni 20 wa Ujerumani wana magonjwa ya mizio, 1 kati ya 3 wana magonjwa ya mizio ya kupumua.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki