Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g93 3/8 kur. 12-14
  • Mfanyakazi Mwenye Bidii wa Angani

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mfanyakazi Mwenye Bidii wa Angani
  • Amkeni!—1993
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Ilianzia Wapi?
  • Hiyo Hurukaje?
  • Kuokoa Wakati—Na Uhai!
  • Unajisikiaje Ukiruka kwa Helikopta?
  • Ndege Yenye Injini
    Amkeni!—2010
  • Kuongoza Ndege Kunukulindaje?
    Amkeni!—2008
  • Ndege Ziliwasilije?
    Amkeni!—1999
  • Kufanya Usafiri wa Ndege Uwe Salama Zaidi
    Amkeni!—2000
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1993
g93 3/8 kur. 12-14

Mfanyakazi Mwenye Bidii wa Angani

Na mleta habari za Amkeni! kutoka Afrika Kusini

“TULIKUWA tumekuwa tukisafiri angani kwa karibu saa mbili. Ghafula mzunguko wa injini ukaanza kupunguza mwendo—ishara ya kwanza ya tatizo la injini.a Nilianza mara hiyo kupanda juu, nikitumia mizunguko iliyobaki ili kwenda juu upesi iwezekanavyo kabla ya injini kusimama. Tulipofika juu kadiri tulivyoweza, mtambo wa klachi ulivunjika, ukitawanyika vipande-vipande hewani kila mahali.

“Mara hiyo nikaendesha helikopta kwa mwendo wa kushuka, mwendo wa kusonga mbele ukiwa uleule wa kilomita 90 hivi kwa saa. Tayari nilikuwa nimechunguza chini na tulikuwa tunaelekea kwenye mahali padogo palipo wazi palipokuwa rahisi kufikia.

“Niligeuza sehemu ya mbele iangalie juu tukiwa umbali wa mita 15 kutoka chini ili nipunguze mwendo wa ndege hiyo, na kisha tukatua, tukipiga breki karibu mita 1.5 kutoka kwenye ukingo wa donga [njia kavu ya mto].”

Yote hayo yalichukua dakika moja hivi. Ni kweli, helikopta zimeanguka zinapoelekea kutua kwa dharura, lakini kama vile inavyoweza kuonwa katika ono hilo la kweli, bado kuna tumaini ikiwa injini inaacha kufanya kazi. Rubani huyo alikamilisha kwa mafanikio mruko unaotia ndani kuzunguka kipekee—ambako huzoewa mara nyingi wakati wa mazoezi kwa ajili ya hali ya dharura kama hiyo.

Na bado, hata ingawa helikopta ni salama na yenye matumizi mengi, wengi bado hawajapata kamwe kuruka kwayo. Labda hata wewe hungependelea kusafiri kidogo kwa helikopta. Hata hivyo, huenda ukapendezwa kujifunza kuhusu mashine hizo za urukaji zisizo za kawaida.

Ilianzia Wapi?

Katika 1483, Leonardo da Vinci, alikuwa wa kwanza kubuni mashine yenye kuruka kwenda juu, akitumia majembe ili apae. Lakini, ole wake, wahandisi wa urukaji husema kwamba mashine hiyo aliyobuni haiwezi kuruka! Hata hivyo, urukaji wa kwenda juu umeendelea kuwavutia wavumbuzi. Ni hivi karibuni kwa kulinganisha ambapo hilo limetimizwa kwa mafanikio.

Ilikuwa katika 1923 kwamba Mhispania Juan de la Cierva, akiwa na umri wa miaka 27, aliporuka kwa ndege yake katika Getafe, Uhispania. Mashine aliyobuni iliendeleza nadharia ya heli-kopta mbele sana. Baadaye, mbuni aliyezaliwa Urusi, Igor Sikorsky, kuanzia kipindi cha 1939 hadi 1941, alifanya maendeleo makubwa ya helikopta kama ilivyo leo. Lakini siri ya kuruka hewani na mashine hiyo ilikuwa nini?

Hiyo Hurukaje?

Ndege ya kawaida yenye mabawa yaliyokazwa huruka hewani kwanza kwa kwenda mbio katika uwanja wa ndege. Inapofikia mwendo unaofaa, hewa inayopita juu ya ubawa hutokeza nguvu ya kutosha kushinda uzito wa ndege na kuinua ndege hewani. Hata hivyo, katika helikopta, mwinuko hutokezwa kwa kuzungusha majembe, yanayomithili mabawa. Hivyo, helikopta yaweza kuinuka bila kusonga mbele. Ili kufanya hivyo, ni lazima majembe yazunguke hewani katika pembe fulani, iitwayo pembe ya mashambulizi, ili kutokeza nguvu ya kutosha ya kuinua. Na rubani anaweza kubadili pembe ya mashambulizi, au mwinuko wa majembe kwa usukani uitwao wenzo wa mwinuko. Wakati mwinuko unaotokezwa na majembe unapita uzito wa helikopta, yaani, unapita nguvu ya uvutano wa dunia, helikopta itainuka. Kupunguza mwinuko hufanya mashine hiyo ishuke.

Helikopta yaweza kupelekwa mbele kutoka hali ya kutua hewani kwa kuinamisha diski ya majembe. Diski hiyo ni eneo linalowaziwa linalopitiwa na majembe wakati yanapozunguka. Diski ya majembe ikiinamishwa mbele, hewa hupitishwa si chini tu ili kuinua helikopta bali pia nyuma kidogo ili kuisukuma mbele. (Ona mchoro chini.) Hivyo, helikopta yaweza kusonga katika kila pande, kwa upogoupogo, hata kinyume-nyume, kwa kuinamisha tu diski ya vijembe katika upande unaotakiwa. Usukani unaofanya hayo hushikwa kwa mkono wa kulia wa rubani na huitwa kizingiti cha usukani, au kijiti cha mzunguko.

Kuna tatizo jingine ambalo lazima litatuliwe kabla ya kuruka kutoka ardhini—mwitikio wa urejeo unaosababishwa na majembe makuu. “Mwitikio wa urejeo” ni nini? Jiwazie ukijaribu kukaza parafujo kwa kibanuaparafujo kikubwa huku ukiwa umevaa viatu vyenye magurudumu. Unapokaza kibanuaparafujo upande mmoja, mwili wako utaelekea kugeuka katika upande ule mwingine. Hiyo ni kulingana na sheria ya sayansi ya mwendo kwamba kwa kila kitendo kuna itikio sawasawa na lililo kinyume. Kwa habari ya helikopta, injini inapoendesha majembe katika upande mmoja, ndege yenyewe huelekea kuzunguka katika upande ulio kinyume. Njia inayotumiwa sana ya kurekebisha hilo ni majembe ya kukinza urejeo, au jembe ndogo, linalowekwa kwenye mkia wa ndege. Kwa kutumia vikanyagio viwili vya kuendesha usukani, rubani aweza kuongeza au kupunguza msukumo wa kijembe cha mkiani na hivyo kuongoza nyendo za helikopta.

Usukani wa mwisho wa kufikiria ni mwendo. Ni lazima mizunguko ya injini iangaliwe wakati wote na rubani wakati anapotumia usukani, ikihitajika kubadilisha mwendo. Ni uangalifu huo wa kila mara wa kihesabia mizunguko uliomwonya rubani aliyeelezwa mwanzoni juu ya kushindwa kufanya kazi kwa injini hata kabla injini haijaacha kufanya kazi kabisa. Katika helikopta za kisasa zinazoendeshwa kwa gesi, sehemu kubwa ya kazi hiyo imepunguzwa kwa kutumiwa kwa mfumo wa kuonyesha mwendo wa injini.

Kuokoa Wakati—Na Uhai!

Helikopta zimeitwa kwa kufaa wafanyakazi wenye bidii wa angani. Katika Agosti 1979, kwa mfano, dhoruba kali iliharibu mashindano ya mashua ndogo ya kisiwa cha Uingereza cha Fastnet. Wanaume kumi na watano waliuawa katika ule ulioitwa “msiba mbaya zaidi katika historia ya uendeshaji mashua ndogo.” Tarakimu hiyo ingalikuwa mbaya zaidi isipokuwa ni ile kazi ya wafanyakazi wa helikopta. Katika uokoaji mmoja, rubani aliwajibika kutahadhari mawimbi yaliyo karibu na kuendesha ndege yake juu na chini ili kuepuka kupigwa nayo. Ripoti moja ya habari ilieleza hilo kuwa mchezo wa kuruka wa kufa na kupona kati ya mawimbi hatari yenye kina cha mita 13 [futi 40].”

Meli kubwa za mafuta zinazoabiri kuzunguka Cape of Good Hope ya kusini mwa Afrika zaweza kupokea ugavi mpya, vipuli, na hata kubadilisha wafanyakazi kwa helikopta, bila kuabiri bandarini. Lakini ni jambo gumu sana. Rubani huendesha helikopta hewani juu ya sehemu ya juu ya meli kwa kuenda sambamba na mwendo wa mbele wa meli uliopunguzwa. Kisha ni lazima aende sambamba na kuvingirika kwa meli ili atue polepole kadiri iwezekanavyo.

Unajisikiaje Ukiruka kwa Helikopta?

Kwa wale wanaopenda kuruka kwa ndege, njia mbalimbali za kuendeshwa kwa helikopta huandaa msisimko unaopita aina nyinginezo za usafiri wa hewa wenye injini. Ni ono lenye kuvutia kuweza kutua hewani, kusonga polepole nyuma au kwa upogoupogo au kuzunguka kwa digree 360 kutoka umbali wa nusu mita hivi kutoka chini. Kutokuwako mwendo wa mbele wakati wa kuruka hufanya helikopta ionekane kuwa salama zaidi kusafiria, na katika safari, upesi mtu huvutwa fikira na mandhari ya mashambani, hasa wakati wa kwenda kasi karibu na chini.

Hata hivyo rubani anayejifunza, atapata helikopta kuwa ngumu kuendesha hapo mwanzoni, kwa kuwa usukani huitikia upesi sana na helikopta haitulii sana kama ndege zenye mabawa yaliyokazwa. Mara mtu akiisha kuwa stadi, ni furaha kuiendesha na rahisi zaidi labda kuliko ndege kwa sababu ya stadi za kuruka na kutua zilizo rahisi zaidi.

Leo helikopta ni mashine iliyositawishwa kwa hali ya juu—mfanyakazi halisi mwenye bidii wa angani. Ni kweli, ikilinganishwa na baadhi ya uumbaji wa Yehova unaoruka, kama vile kereng’ende na ndege kivumi, inaweza kuonekana kuwa duni. Bado, hiyo ni mashine nzuri ajabu. Na sasa kwa kuwa unajua zaidi kidogo kuihusu, labda ungependa kupanda moja!

[Maelezo ya Chini]

a revs = revolutions

[Picha katika ukurasa wa 12]

Ubuni wa Leonardo da Vinci wa mashine ya kuruka kwenda juu

[Hisani]

Bibliothèque de l’Institut de France, Paris

[Picha katika ukurasa wa 12]

Usafiri katika uwanja wa ndege

[Picha katika ukurasa wa 13]

Uokoaji katika bahari kutoka hewani na RAF

[Hisani]

Kwa hisani ya Wizara ya Ulinzi, London

[Picha katika ukurasa wa 13]

Mara nyingi polisi hutumia helikopta

[Michoro/Picha katika ukurasa wa 13]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Kizingiti cha usukani huongoza pembe ya diski ya majembe, ambayo nayo huamua upande wa kuruka

Diski ya majembe

Helikopta ikitua hewani

Kuruka kinyume-nyume

Kuruka mbele

Wenzo wa mwinuko

Kizingiti cha uendeshaji

Vikanyagio vya usukani

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki