Ndege Ziliwasilije?
WABUNI walifanikiwaje mwishowe kutokeza mashine zinazoruka angani zilizo nzito kuliko hewa? Walielekeza uangalifu wao kwa wasanii stadi wa safari za angani—ndege wanaopuruka. Katika mwaka wa 1889 mhandisi Mjerumani aliyeitwa Otto Lilienthal, akichochewa na mazoea ya koikoi ya kusafiri angani, alichapisha kitabu “Bird Flight as the Basis of Aviation.” Miaka miwili baadaye alijenga nyiririko yake ya kwanza iliyo sahili. Katika mwaka wa 1896, baada ya safari za angani 2,000 za nyiririko, Lilienthal alikufa alipokuwa akifanyia majaribio ndege ya bawa moja. Octave Chanute, mhandisi Mmarekani aliyezaliwa Ufaransa, alifanyia marekebisho muundo wa Lilienthal na kutokeza nyiririko ya injini mbili ambayo nayo ilipiga hatua kubwa katika kuunda mashine inayoruka angani iliyo nzito kuliko hewa.
Kisha akina Wright wakajitokeza. Orville na Wilbur Wright walikuwa na duka la baiskeli katika Dayton, Ohio, Marekani, nao walianza majaribio yao ya kwanza ya kunyiririka mwaka wa 1900, wakitegemea msingi uliowekwa na Lilienthal na Chanute. Akina Wright walifanya kazi polepole na kwa utaratibu kwa miaka mitatu iliyofuata, wakifunga safari za angani za majaribio mara kadhaa katika Kitty Hawk, North Carolina. Walitokeza miundo mipya inayotumia mashimo ya kupitishia upepo, na kwanza walitengeneza kwa kutumia sanduku la wanga. Katika safari yao ya kwanza ya angani kwa kutumia injini, walitengeneza injini yao wenyewe yenye silinda nne na nguvu-farasi 12 na kuipandisha kwenye bawa la chini la ndege mpya. Injini hiyo iliendesha rafadha mbili za mbao, moja katika kila upande wa usukani wa nyuma wa ndege.
Mnamo Desemba 14, 1903, ndege mpya iliyovumbuliwa na akina Wright ilipaa kutoka kwenye ubao wa kuipeperushia kwa mara ya kwanza—na kubaki hewani kwa sekunde tatu u nusu! Siku tatu baadaye ndugu hao walipaa wakitumia mashine hiyo tena. Hatimaye ilibaki hewani kwa karibu dakika moja na kusafiri umbali wa meta 260. Ndege hiyo ikafanikiwa.a
Kwa kushangaza, utimizo huo mkubwa haukuvutia uangalifu wowote wa ulimwengu. Hatimaye wakati The New York Times lilipochapisha habari kuhusu akina Wright katika Januari 1906, lilisema kwamba “mashine ya kuruka angani” ilikuwa imebuniwa kwa siri kubwa na kwamba ndugu hao walikuwa wamepata “mafanikio kidogo tu ya kusafiri angani” mwaka wa 1903. Kwa kweli, Orville alikuwa amempelekea baba yake telegramu usiku huohuo wa safari hiyo ya kihistoria, akimsihi aeleze vyombo vya habari. Hata hivyo, ni magazeti ya habari matatu tu huko Marekani yaliyojishughulisha kuchapisha habari hiyo wakati huo.
Je, Hakutakuwa na Ndege za Biashara?
Kwa ujumla ulimwengu ulikuwa na shaka kuhusu vyombo vya anga wakati vilipokuwa vikianza. Hata Chanute, mmojawapo wa waanzilishi wa vyombo vya anga alitabiri hivi mwaka wa 1910: “Kwa maoni ya wataalamu stadi ni kazi bure kutarajia kuwa na mashine zinazoruka angani za biashara. Sikuzote kutakuwako kipimo ambacho kitazuia kubeba abiria au shehena kupita kadiri fulani.”
Hata hivyo, ufundi wa vyombo vya anga ulisonga mbele upesi baada ya safari za kwanza za angani za akina Wright. Katika miaka mitano ndugu hao walikuwa wamejenga ndege yenye mabawa mawili kila upande inayobeba watu wawili ambayo ingeweza kufikia mwendo wa kilometa 71 kwa saa na kupaa kufikia mwinuko wa meta 43. Katika mwaka wa 1911 safari ya kwanza kuvuka bara la Marekani kwa ndege ilifanywa; safari hiyo kutoka New York hadi California ilichukua karibu siku 49! Wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Kwanza, mwendo wa ndege uliongezwa kutoka kilometa 100 kwa saa hadi kufikia kilometa 230 kwa saa. Pia upesi rekodi za mwinuko zilifikia meta 9,000.
Rekodi za vyombo vya anga ziliendelea kutangazwa katika vyombo vya habari katika miaka ya 1920. Maofisa wawili wa kijeshi Wamarekani walifunga safari ya kwanza bila kutua wakivuka Marekani mwaka wa 1923, nao walisafiri kutoka pwani moja hadi nyingine kwa muda unaopungua saa 27. Miaka minne baadaye Charles A. Lindbergh akawa maarufu mara moja kwa kusafiri kwa ndege bila kutua kutoka New York hadi Paris kwa muda wa saa 33 na dakika 20.
Wakati huohuo, mashirika machanga ya ndege yalikuwa yameanza kuvutia wateja. Kufikia mwisho wa mwaka wa 1939, safari za ndege zilikuwa zimefikia hatua ambapo mashirika ya ndege ya Marekani yalikuwa yakihudumia karibu abiria milioni tatu kila mwaka. Ndege ya kawaida ya miaka ya 1930, DC-3, ilibeba abiria 21 tu na kusafiri kwa mwendo wa kilometa 270 kwa saa; lakini baada ya Vita ya Ulimwengu ya Pili, ndege za biashara zikawa kubwa zaidi na zenye nguvu zaidi, zikisafiri kwa mwendo wa zaidi ya kilometa 480 kwa saa. Uingereza ilianzisha huduma za ndege yenye injini aina ya turbojet mwaka wa 1952. Na ndege kubwa-kubwa, kama vile Boeing 747 zinazoweza kubeba watu 400, ziliibuka mwaka wa 1970.
Mafanikio mengine yalipatikana mwaka wa 1976 wakati kikundi cha wahandisi Waingereza na Wafaransa walipotokeza ndege aina ya Concorde, yenye mabawa yanayoelekea nyuma iwezayo kubeba abiria 100 na kusafiri mwendo maradufu wa sauti—zaidi ya kilometa 2,300 kwa saa. Lakini gharama za juu za kudumisha ndege hiyo zimesababisha ndege hizo zisitumiwe sana kibiashara.
Kuuelekeza Ulimwengu
Hata ikiwa hujawahi kusafiri kwa ndege, yawezekana kwamba maisha yako yameelekezwa na mabadiliko haya ya haraka ya kitekinolojia. Ndege zinazobeba shehena husafiri na kuvuka tufe lote; mara nyingi chakula tunachokula, mavazi tunayovalia, na mashine tunazotumia kazini vimesafirishwa kwa ndege kutoka ng’ambo ya bahari au ng’ambo ya bara. Barua na vifurushi hupelekwa kutoka nchi moja hadi nyingine kwa njia ya ndege. Biashara hutegemea sana huduma za usafirishaji zinazofanywa na ndege ili kuendesha shughuli za kila siku. Bidhaa na huduma tunazopata na gharama tunazozilipia zote zimeathiriwa na uwezo wa mwanadamu wa kusafiri kwa ndege.
Pia vyombo vya anga vimechangia sana mabadiliko makubwa ya kijamii. Bila shaka, kwa sababu ya vyombo vya anga ulimwengu umekuwa mdogo sana. Kwa muda wa saa chache, unaweza kuwa karibu mahali popote ulimwenguni—ikiwa una uwezo wa kifedha. Habari husafiri haraka, ndivyo na watu.
Gharama ya Maendeleo
Lakini maendeleo hayo yametokeza gharama fulani. Ndege zinapozidi kuongezeka, wengine wanahofia anga inazidi kuwa hatari. Kila mwaka ndege za kibinafsi na za kibiashara zinazoanguka hupoteza uhai wa watu wengi. “Kukiwa na mkazo wa kushindana, mashirika mengi ya ndege yanapuuza hatua za ziada za usalama ambazo yalidumisha kwa ukawaida wakati ambapo abiria wangelipia gharama hizo za ziada,” lasema gazeti Fortune. Gazeti hilo laripoti kwamba Shirika la Serikali Linalosimamia Vyombo vya Anga, lenye daraka la kuhakikisha usalama wa ndege huko Marekani, “halina pesa za kutosha, halina wafanyakazi wa kutosha, na linasimamiwa vibaya.”
Wakati huohuo, idadi inayozidi kuongezeka ya wanamazingira wanashtushwa na ongezeko la uchafuzi wa hewa na wa kelele unaotokana na ndege nyingi sana. Kushughulika na mahangaiko kuhusu matatizo ya kelele ni “mojawapo ya masuala yanayosababisha mgawanyiko zaidi katika kusafirisha raia ulimwenguni,” likasema gazeti Aviation Week & Space Technology.
Matatizo haya yanaongezewa na uhakika wa kwamba ndege nyingi zinazidi kuchakaa: Katika mwaka wa 1990, ndege 1 kati ya 4 za Marekani zilipatikana kuwa zimedumu kwa zaidi ya miaka 20, na thuluthi moja zilikuwa zimetumiwa sana kupita “muda uliokusudiwa” kama ulivyopangwa hapo mwanzoni na mtengenezaji.
Hivyo, wahandisi wa usafiri wa anga sasa wanakabiliwa na magumu makubwa sana. Wanahitaji kubuni njia zilizo salama zaidi na zisizo ghali za kubebea abiria zaidi, kama vile gharama zinavyopanda na mahangaiko kuhusu mazingira yanavyoongezeka.
Tayari masuluhisho fulani ya kupunguza gharama yameanza kutokea. Jim Erickson, akiandika katika Asiaweek, asema kwamba kikundi cha wanasayansi wa anga wa Ufaransa na Uingereza kinapanga kutokeza ndege iwezayo kubeba kufikia abiria 300 na kusafiri mwendo maradufu wa sauti. Gharama na matumizi ya fueli kwa kila abiria zitakuwa chini. Na kufuatia hali ya msongamano wa ndege kwenye viwanja vingi vya ndege, watu fulani wamependekeza kutokezwa kwa helikopta kubwa za kubebea watu—kila moja ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 100. Wanaamini kwamba siku moja ndege hizi, zitaweza kushughulikia usafirishaji wa mwendo mfupi ambao sasa hufanywa na ndege za kawaida zenye mabawa.
Je, kweli helikopta kubwa sana na ndege zenye mwendo wa kasi sana zitatimiza mahitaji muhimu ya usafiri wa ndege katika miaka ijayo? Itajulikana baada ya muda kupita huku mwanadamu akijisukuma kufuatia ‘kufungua anga’ kwa safari zake.
[Maelezo ya Chini]
a Watu fulani wanadai kwamba mnamo mwaka wa 1901, Gustave Whitehead (Weisskopf), mhamiaji Mjerumani aliyeishi Connecticut, Marekani, pia aliendesha ndege aliyoibuni. Hata hivyo, hakuna picha za kuthibitisha dai hilo.
[Picha katika ukurasa wa 6]
Otto Lilienthal, karibu mwaka wa 1891
[Hisani]
Library of Congress/Corbis
[Picha katika ukurasa wa 6, 7]
Charles A. Lindbergh akiwasili London baada ya safari yake ya kuvuka Atlantiki hadi Paris, mwaka wa 1927
[Hisani]
Corbis-Bettmann
[Picha katika ukurasa wa 7]
Sopwith Camel, mwaka wa 1917
[Hisani]
Museum of Flight/Corbis
[Picha katika ukurasa wa 7]
DC-3, mwaka wa 1935
[Hisani]
[Picha katika ukurasa wa 7]
Photograph courtesy of Boeing Aircraft Company
[Picha katika ukurasa wa 7]
Boti inayoruka angani aina ya Sikorsky S-43, mwaka wa 1937
[Picha katika ukurasa wa 8]
Helikopta ya kuokoa uhai baharini
[Picha katika ukurasa wa 8]
Ndege aina ya acrobatic Pitts, Samson replica
[Picha katika ukurasa wa 8, 9]
Ndege aina ya Concorde ilianza safari zilizoratibiwa mwaka wa 1976
[Picha katika ukurasa wa 8, 9]
Ndege aina ya Airbus A300
[Picha katika ukurasa wa 9]
Baada ya kuingia tena angani, chombo cha angani huwa nyiririko ya mwendo wa kasi
[Picha katika ukurasa wa 9]
“Rutan VariEze,” 1978