Tamaa Kubwa ya Kusafiri Angani
“NDEGE zote zimethibitisha haraka methali ya wakati wa ujana wetu isemayo, ‘Aliye juu mngojee chini.’”
Ndivyo ilivyoanza tahariri yenye kutilia shaka kwa kiasi fulani katika gazeti la The New York Times la Mei 25, 1908—kipindi kinachopungua miaka mitano baada ya ndugu wawili walioitwa Wright kufunga safari yao ya angani iliyo mashuhuri huko Kitty Hawk, North Carolina, Marekani. Bado wakitilia shaka mafanikio ya “mashine [mpya] zinazoruka” zilizokuwa zimeanza kutokea angani, mwandishi alifikiri kwamba “kwa kulinganishwa ni wachache kati yetu walio na tamaa ya kuelea hewani wakiwa juu sana kutoka duniani.” Ingawa ilikubali kwamba vizazi vya wakati ujao vyaweza kuwa na mwelekeo wa kukubali kusafiri kwa ndege, makala hiyo ilisisitiza kwamba “tamaa kubwa sana ya kutengeneza ndege za abiria za kusafiri masafa marefu . . . huenda isitimizwe kamwe.”
Utabiri huo ulikosea kama nini! Leo, abiria zaidi ya bilioni moja husafiri angani katika “ndege za kusafiri masafa marefu” kila mwaka. Ndiyo, katika karne moja, ndege zimebadilishwa kutoka kuwa vidude hafifu vya mbao na viunzi katika mwanzo wa karne ya 20 hadi kuwa ndege za kisasa zenye mitindo na zilizo na kompyuta, ambazo husafiri kilometa 10 juu ya dunia na kubeba mamia ya abiria hadi maeneo ya mbali sana zikiwa na hali nzuri zenye kustarehesha.
Maendeleo ya haraka ya ufundi wa vyombo vya anga katika karne ya 20 kwa kweli yamekuwa ya kipekee na yamebadili kwa kasi ulimwengu wetu. Kwa hakika, tamaa ya binadamu ya kuvumbua mambo ya anga yaweza kufuatiliwa zaidi ya miongo michache—au hata kupita karne chache zilizopita. Safari za angani za binadamu ni tamaa kubwa sana ambayo wanadamu wamekuwa nayo tangu nyakati za kale.
[Picha katika ukurasa wa 2, 3]
Ndege aina ya Lockheed SR-71 Blackbird, iliyo na mwendo wa kasi zaidi ulimwenguni, wa kilometa 3,600 kwa saa
[Picha katika ukurasa wa 3]
Ndege aina ya Boeing Stratoliner 307, karibu mwaka wa 1940, yenye kubeba abiria 33, na yenye mwendo wa kilometa 340 kwa saa
[Hisani]
Boeing Company Archives
[Picha katika ukurasa wa 3]
Ndege ya akina Wright iitwayo “Flyer,” ya 1903
[Hisani]
U.S. National Archives photo