Watangulizi wa Mapema wa Ufundi wa Vyombo vya Anga
“Kwa vile mimi ni rubani wa ndege, nilifurahia kikamili toleo la ‘Amkeni!’ la Machi 8, 1999 kuhusu kusafiri kwa ndege. Hata hivyo, nina swali moja. Kwa nini Alberto Santos-Dumont hakutajwa? Alikuwa miongoni mwa marubani wa mapema zaidi.” —C. B., Marekani.
MFULULIZO wa makala za Amkeni! la Machi 8, 1999, wenye kichwa “Kusafiri Kwa Ndege—Kulianzaje? Ni Salama Kadiri Gani?” uliandaa muhtasari wa historia ya ufundi wa vyombo vya anga. Ijapokuwa habari nyingi zilikazia mafanikio ya Wamarekani Wilbur na Orville Wright, ndugu hao wawili hawakuwa watu pekee waliofanyia vyombo vya anga majaribio karibu mwanzoni mwa karne. Wafikirie watangulizi wengine wachache wa ufundi wa vyombo vya anga.
• Alberto Santos-Dumont alizaliwa Julai 20, 1873, huko Minas Gerais, Brazili. Alipokuwa tineja, familia yao ilihamia Paris. Akiwa huko Santos-Dumont alisomea, fizikia, kemia, umekanika, na stima. Alikuwa na tamaa kubwa ya kusafiri kwa ndege, na kati ya 1898 na 1905, aliunda na kuendesha vyombo 11 vya anga.
Katika Oktoba 1906, Santos-Dumont hatimaye alitimiza mradi wake wa kuendesha chombo cha anga. Kwa kutofautishwa na baadhi ya ndege nyingine za mapema, ambazo zilihitaji kurushwa kwa manati, ndege ya Santos-Dumont, 14-bis, iliruka kwa kutegemea msukumo wake wenyewe. Safari ya angani ya Santos-Dumont ya meta 60 ndani ya 14-bis inaonwa kuwa safari ya kwanza ya angani iliyofanikiwa ya chombo cha anga huko Ulaya.
Katika mwaka uliofuata, Santos-Dumont alihuzunika kuona ndege hiyo ikiwa chombo cha uharibifu. Kwa kweli, inaripotiwa kwamba kwa sababu ya kukata tamaa kwa kuona ndege zikitumiwa vitani, alijiua mnamo mwaka wa 1932. Kwa vyovyote vile, Santos-Dumont anashiriki fungu thabiti katika historia ya ufundi wa vyombo vya anga.
• Gustave Whitehead alizaliwa huko Leutershausen, Ujerumani, Januari 1, 1874. Kwa sababu ya kupendezwa sana na ufundi wa vyombo vya anga, wanashule wenzake walimwita rubani. Alipofikisha umri wa miaka 13, Gustave alikuwa yatima, na ijapokuwa alihamia sehemu mbalimbali katika miaka iliyofuata, tamaa yake ya kusafiri kwa ndege haikudidimia kamwe. Kwa muda mfupi, Gustave mchanga alijifunza na rubani mashuhuri Mjerumani Otto Lilienthal. Kisha, mnamo mwaka wa 1894, akaenda kuishi Marekani.
Kama ilivyotajwa katika toleo la Amkeni! la Machi 8, 1999, wengine wanadai kwamba katika 1901, Whitehead alifanikiwa kufunga safari ya kwanza ya muda mrefu ulimwenguni kwa kutumia chombo cha anga. Hata hivyo, hakuna picha zinazothibitisha dai hilo. Kwa kushangaza, vyombo vya habari havikutambua mara moja umuhimu wa mafanikio ya mapema ya ufundi wa vyombo vya anga, hata wakati akina Wright walipofunga safari yao ya angani. Kwa kweli, kulingana na jarida Air Enthusiast, “ni kufikia mwaka wa 1910 ndipo umma ulipoanza kupendezwa kikweli na ‘tekinolojia [hiyo] mpya’ na watu wakaanza kuamini kwamba mwanadamu anaweza kusafiri angani.”
• Samuel Pierpont Langley, katibu wa shirika la Smithsonian Institution, huko Washington, D.C., alikuwa mwastronomia na mwanafizikia. Mnamo mwaka wa 1896 aliunda ndege inayoendeshwa na mvuke iliyosafiri bila rubani kwa umbali wa robo tatu ya maili kabla ya kuishiwa na mafuta.
Bila shaka, injini za mvuke ni nzito sana, na zilionwa kuwa zisizofaa kwa usafiri wa angani. Kwa hiyo msaidizi wa Langley, Charles M. Manly, aliunda injini yenye uzito wa kilogramu 57 ya nguvufarasi 53 ambayo ingefaa zaidi. Tokeo lilikuwa kuundwa kwa ndege bora zaidi, ambayo Langley aliiita Aerodrome. Katika Oktoba 7, 1903, Manly aliketi kwenye mitambo huku ndege ya Langley ikirushwa na manati kutoka kwenye mashua. Kisha ikatumbukia ndani ya Mto Potomac. Jitihada iliyofuatia miezi miwili baadaye haikufua dafu. Akiwa amekata tamaa, Langley aliacha mradi huo.
Hata hivyo, licha ya kukosa kufanikiwa, Langley alifanya maendeleo ya maana katika uwanja wa ufundi wa vyombo vya anga. Mnamo mwaka wa 1914, miaka minane baada ya kifo chake, mabadiliko kadhaa yalifanywa kwa Aerodrome, na ikaendeshwa kwa mafanikio huko Hammondsport, New York na Glenn H. Curtiss.
Hao ni baadhi ya watu wachache tu kati ya wengi walioongoza katika ufundi wa vyombo vya anga karibu mwanzoni mwa karne ya 20. Leo, mamia ya maelfu ya ndege zenye ukubwa mbalimbali hurembesha anga. Zote zimekuwapo na kufanikiwa kwa kiasi fulani kwa sababu ya watangulizi wa mapema wa ufundi wa vyombo vya anga.
[Picha katika ukurasa wa 19]
Alberto Santos-Dumont na ndege yake “14-bis”
[Hisani]
Culver Pictures
North Wind Picture Archives
[Picha katika ukurasa wa 20]
Gustave Whitehead akiwa na mfano wa chombo chake cha angani
[Hisani]
Flughistorische Forschungsgemeinschaft Gustav Weisskopf
[Picha katika ukurasa wa 20]
Samuel P. Langley na “Aerodrome” yake
[Hisani]
Dictionary of American Portraits/Dover
U.S. National Archives photo