Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g93 3/8 kur. 15-19
  • Kufuga Kondoo Ndiyo Kazi Yetu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kufuga Kondoo Ndiyo Kazi Yetu
  • Amkeni!—1993
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Waongezeka na Kuwa Wengi
  • Malisho ya Wakati wa Kipupwe
  • Kutenda Tukiwa Wakunga
  • Kusaidia Katika Kukata Manyoya
  • Kuwaogesha
  • Maoni ya Mtu wa Jijini
  • Vita Dhidi ya Kupe na Minyoo
  • Mbwa Walio Muhimu Sana
  • Zuru Bara, Zuru Kondoo!
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1992
  • Maajabu ya Sufi
    Amkeni!—1992
  • Maisha ya Wachungaji wa Wales
    Amkeni!—2011
  • “Aliyepotea Nitamtafuta”
    Mrudie Yehova
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1993
g93 3/8 kur. 15-19

Kufuga Kondoo Ndiyo Kazi Yetu

JE! UMESHAPATA kuvaa vazi la sufu au kununua fungu la sufu? Je! ulipata kujiuliza sufu hiyo ilitoka wapi? Au ni nini kinachohusika katika kufuga kondoo wanaotoa sufu? Labda twaweza kukusaidia. Kwa nini? Kwa sababu, nikiwa na mke wangu Barbara, nina shamba kubwa la kondoo kule chini katika Kisiwa cha Kusini cha New Zealand.

Kondoo ni wanyama wenye kupendeza—watiifu, wepesi wa kutishwa, na mara nyingi wapumbavu kwa wazi. Na bado ninakumbuka kondoo-jike aliyedhibiti wanakondoo wake vizuri zaidi ya mama mwingineo katika kundi hilo. Wengine wangewapoteza wana wao, lakini si kondoo-jike huyo. Ni nini kilichokua cha pekee juu yake? Yeye alikuwa kipofu. Lakini alilipia upofu wake kwa hisi zake kali za kunusa na kusikia. Alijua kihususa mahali pa kupata wanakondoo wake. Ilikuwa furaha kuwatazama wakinyonya, mikia yao ikitikiswa-tikiswa kwa nguvu sana!

Nimeishi na kondoo kwa muda mrefu wa maisha yangu katika Kisiwa cha Kusini. Baba yangu amefuga kondoo kwa miaka 60. Sasa mbona ninasema “amefuga kondoo” na si “mchungaji”? Wazo la watu wengi juu ya mchungaji ni mtu anayechunga kikundi cha kondoo wenye kuhama-hama. Katika kisa chetu, tuna mashamba ya kufuga kondoo. Kondoo wetu hulishwa kwenye shamba moja lenye mpaka na kuhamishwa tu kutoka shamba moja, au uwanda, hadi mwingine. Badala ya makumi au mamia ya kondoo, tuna maelfu. Na bado, kwa kulinganishwa na mashamba ya New Zealand, shamba letu ni ndogo. Hata hivyo, kazi yetu ni ya kiwango kikubwa. Kwa hiyo kufuga kondoo wengi hivyo kunatia nini ndani?

Waongezeka na Kuwa Wengi

Kwa kuwa wafugaji wengine wa kondoo hufuga kwa ajili tu ya nyama, sisi hufuga kwa ajili ya sufu pamoja na nyama. Mara nyingi wenye kuzuru hushangaa kupata kwamba New Zealand ina kondoo milioni 70 hivi, hasa kutoka kwa aina 19 mbalimbali. Kondoo hawakutoka nchi yetu bali waliletwa kutoka nchi nyinginezo. Kondoo mkubwa wa aina ya merino, aliyetoka Extremadura, Uhispania, na Romney, Leicester, na wa aina nyinginezo kutoka Uingereza mara nyingi huletwa kupitia Australia.

Kondoo wetu ni wa aina ya Romney, walio warefu na wenye miili mikubwa, wakitoa sufu nzuri. Lakini kupata bidhaa hiyo ya mwisho hutia ndani kazi nyingi ya jasho na mpango. Kwanza, ni lazima tufuge kondoo wenye mazao, na hiyo inamaanisha aina bora ya wanyama. Mimi hununua kondoo-dume walio bora kila mwaka kuleta jumla ya 35, na katika Aprili wao hupelekwa kujamiiana na kondoo-jike. Katika kipindi cha majuma matatu, kondoo-dume watakuwa wamejamiiana na kondoo-jike wapatao 60 hadi 80 kila mmoja. Wakati wa kuzaa ni Septemba, na huo ndio wakati ambao Barbara nami hufurahia zaidi. Lakini sisi hujishughulishaje hadi Septemba?

Malisho ya Wakati wa Kipupwe

Huku katika Kizio cha Kusini, kipupwe chetu ni kuanzia Mei kuendelea. Wakati huo malisho hayajakua vizuri, hivyo sisi tunalazimika kupelekea kondoo malisho. Na ninasema “sisi” kwa kuwa Barbara hushughulika akinisaidia. Sisi hugawanya mashamba yetu, au uwanda, kwa waya ya umeme katika visehemu vyenye ukubwa wa karibu nusu hektari kila kimoja. Kuweka tu waya hizo ni kazi kubwa. Kwa nini sisi huhitaji kufanya hivyo? Kwa sababu kondoo watahamishwa kila siku kutoka sehemu moja ya malisho hadi nyingine, na inatubidi tuwapelekee ukoka mkavu na malisho mengine kwa gari-mkokoteni. “Malisho mengine” yaweza kumaanisha shayiri na kokwa, hasa kabla ya kuzaa wakati ambapo kondoo-jike huhitaji ulishaji wa ziada. Pia sisi hu-lisha kondoo wenye mwaka mmoja kwa aina ya tanipu (mboga). Na sisi hupata wapi aina hiyo ya tanipu? Tunawajibika kuikuza, jambo ambalo linamaanisha tunahusika pia na ukulima, si kufuga kondoo tu. Lakini ebu turudi kwenye kazi ya kufurahisha, ile ya kuzalisha.

Kutenda Tukiwa Wakunga

Septemba ifikapo, Barbara nami tunavuka malisho kwa pikipiki. La, hayo si mashindano. Ni njia yetu ya usafiri ya kufikia kondoo-jike wote wanaozaa. Sisi hujaribu kuzuru kondoo-jike wanaokaribia kuzaa mara nne au tano kwa siku ili kusaidia wowote wenye shida. Wengi wao huzaa bila matatizo, lakini bado tunawajibika kutia alama wanakondoo mapacha ili mmoja akitenganishwa, tuweze kumweka pamoja na pacha mwenzake.

Baadhi ya kondoo-jike huzaa kwa shida, na hapo pikipiki husaidia katika kuandaa msaada wa haraka. Kwa mfano, ikiwa mwanakondoo anazaliwa kichwa kikitoka kwanza bila miguu kutokeza, angeweza kujisakama. Kisha tunasaidia tukiwa wakunga na kusaidia kuzalisha. Kwa mtu ambaye hajazoea hayo, huenda akaona hiyo kuwa kazi chafu, lakini kwetu, kushuhudia uhai mpya ukija ni muujiza wa kila mwaka.

Kondoo-jike wengi huzaa mapacha. Hatimaye sisi huweka alama kwenye masikio kwa karibu wanakondoo-jike 500 wanaofugwa kwa ajili ya kuzaa. Hiyo hubainisha umri wao. Baada ya miezi mitatu au minne, madume na majike wanaobaki hupelekwa kwenye kiwanda cha nyama. Wajua, tuna maneno ya pekee ya kubainisha umri. Kondoo wa mwaka mmoja huitwa mwanakondoo na wa miaka miwili huitwa meno-mawili. Wajua, kondoo huota meno manane tu, mawili kwa mwaka. Kondoo-jike anapokuwa meno-mawili, yeye yuko tayari kujamiiana.

Tusisahau sababu kuu ya kufuga kondoo hao wote—kwa ajili ya manyoya yao ya thamani, sufu yao—jambo linalotuleta kwenye kipindi chenye mambo mengi ya kazi ya jasho kwelikweli.

Kusaidia Katika Kukata Manyoya

Ingawa mkata manyoya mzuri aweza kushughulikia kondoo wapatao 300 hadi 400 kwa siku, mimi siwezi hilo. Wastani wangu ni kama 150 kwa siku. Kondoo wengi hukatwa manyoya mara moja kwa mwaka, lakini wengine hukatwa mara mbili kwa mwaka, kama vile wanakondoo katika Oktoba na meno-mawili katika Machi. Ili kufanya ukataji manyoya uwe rahisi baadaye, sisi hukata mikia ya wanakondoo, jambo linalosaidia kuweka sehemu yao ya nyuma ikiwa safi.

Zamani, kukata manyoya kulikuwa kukifanywa kwa mabapa au makasi. Leo tuna makasi ya umeme, lakini bado kazi ni ngumu na hutaka ustadi maalum. Ikitegemea na jinsi unavyomshika kondoo, kazi yako yaweza kuwa rahisi zaidi au ngumu zaidi. Mimi huajiri wakataji wanaolipwa kulingana na hesabu ya kondoo wanaokata kila siku. Mara nyingi sisi hupata sufu kilo 4.5 hadi 5.5 kutoka kwa kila kondoo-jike.

Kazi inayofuata ni kutayarisha sufu iweze kusafirishwa kwa wauzaji wa sufu. Inatubidi tuipakie kabisa katika mitumba yenye uzito wa kilo 180. Lakini je, sisi hutoa sufu bora? Kuna upande mwingine wa kazi yetu ulio wa maana katika kupata sufu bora.

Kuwaogesha

Kondoo hupata kupe au chawa kutoka kwa wengine, na vimelea hao huwafanya wawashwe. Ghafula, kondoo wanatumia wakati wao wakijikuna kwenye ua badala ya kula. Kwa hiyo wanapunguza uzito na kuharibu sufu yao. Sisi huwezanaje na hilo? Sisi huwaogesha kwenye kemikali mara moja kwa mwaka. Huu pia ni wakati wa kazi nyingi, kama vile mgeni mwenye kuzuru malisho yangu alivyoona. Hivi ndivyo alivyoeleza yale aliyoona.

Maoni ya Mtu wa Jijini

“Nilipowasili mahali penyewe, maogesho yalikuwa yamekuwa yakiendelea kwa saa kadha. Kile nilichoona kwanza kwa macho yangu ya jijini yasiyozoezwa, ni mandhari ya pilikapilika. Wanaume walikuwa wakipaza sauti; mbwa walikuwa wakibweka. Baadhi ya kondoo walikuwa wakikohoa; wengine walikuwa wakihema. Mbwa walikuwa wakiruka kihalisi juu ya migongo ya kondoo wenye hofu ili kuenda mbele ya kikundi kuondoa msongamano. Hala-fu kidogo nikaona umaana wa yale yaliyokuwa yakiendelea.

“Mamia ya kondoo walikuwa katika nyanda walimowekwa, wakingoja zamu yao ili waongozwe, kama kumi kwa wakati mmoja, kwenye sehemu nyembamba. Hapo mfugaji-kondoo mmoja alikuwa akingoja kando ya kidimbwi kidogo cha mchanganyiko wa kemikali kilichofichwa kwa gunia ili kondoo wasikione. Punde tu kila mnyama alipomfikia mwanamume yule anayengoja, yeye aliwasukuma ghafula kwa magoti yake kupitia lile gunia na, chubwi! ndani ya umaji-maji ule wenye utusitusi. Itikio la kwanza la yule mnyama lilikuwa kujaribu kutoka nje, na alianza kuogelea kuelekea mahali pembamba pa kutokea. Hata hivyo, kwenye kila upande, kulikuwa wafanyakazi wengine wakingoja huku wakiwa na fito ndefu za kusukuma kondoo huyo chini ya kiogesho na hivyo kuhakikisha kwamba sufu yote, kuanzia utosi hadi kidole cha mguu, ilichovywa. Wanyama hao walipopanda kutoka kwa mchanganyiko wa kemikali, walikohoa-kohoa na kutematema na kujitikisa-tikisa kwa nguvu, wakirusha dawa hewani. Wengine walipokuwa tayari kuachiliwa kutoka kwa zizi la kutokea, waliruhusiwa kurudi malishoni, jambo ambalo wengi walifanya kwa furaha na utayari!”

Vita Dhidi ya Kupe na Minyoo

Inanivutia kusikia maelezo ya mtu wa nje juu ya yale tunayofanya. Huenda ukajiuliza ni mmumunyo gani wa kemikali tunatumia katika maogesho. Unaitwa Grenade, na Parethroidi ndiyo inayotumika, ikiwa na asilimia 5 ya Cyhalothrin, inayoua kupe au chawa. Vimelea hao si ndio tu adui wa asili ambaye kondoo wanao. Wao pia hupata minyoo wa matumboni na mapafuni, jambo linalomaanisha ni lazima tuwanyweshe kondoo dawa kwa ukawaida. Hilo latia ndani kuleta kondoo nyumbani kwenye viwanda. Tunawaweka kwenye vijia vyembamba, karibu mita 1.2 kwa upana, vinavyotoshea kondoo 50 hivi. Kisha wananyweshwa dawa kwa kulazimisha kupitia kwenye umio mchanganyiko wa kemikali unaoua minyoo. Sisi hubeba mfuko mgongoni wenye umaji-maji huo na hutumia tyubu na tundu ili kuitia kwa nguvu kupitia koo zao. Nyakati nyingine pia huwajibika kuwapa penisilini ili kuepuka kutiwa sumu.

Je! kondoo wetu hupata ugonjwa wa shuna (wa miguu na midomo)? La, kwa sababu ya udhibiti mkali wa wenye mamlaka wa uhamaji na kilimo kwenye bandari na wanja za ndege za New Zealand. Wageni wengi huudhika wanapowasili kwenye wanja zetu za ndege kupata kwamba chumba cha ndege lazima kipigwe dawa kabla ya wao kushuka. Lakini hiyo ni sababu mojawapo hatuna baadhi ya magonjwa yanayoathiri wanyama katika nchi nyinginezo.

Mbwa Walio Muhimu Sana

Hadithi yangu haingekuwa imekamilika bila kurejezea mbwa wetu wa kufuga kondoo. Tuna zaidi ya watano kwenye mashamba yetu na hutumia aina mbili za mbwa waliojamiiana wa aina ya kufuga kondoo. Tuna yule tunayemwita mbwa mbwekaji. Wao watabweka na kuelekeza kondoo kwa kukimbia juu ya migongo yao ili kufikia mahali panapofaa. Aina ile nyingine ni ile tuitayo mbwa-macho. Huyo atamwendea kondoo fulani na kumtazama jicho kwa jicho, akimtia wasiwasi kwa kutazama badala ya kubweka. Hakuna vile tungefanya kazi yetu bila wanyama hao waaminifu. Wao hufanya kazi kwa bidii hadi wanapoanguka kwa uchovu.

Kwa ufupi, huo ni muhtasari wa maisha yetu hapa Mossburn, New Zealand, tukitunza kondoo. Kwa hiyo ukinunua vazi zuri la sufu, toa fikira juu ya wafugaji kondoo ulimwenguni ambao wamewafuga wanyama hao kwa uangalifu ambao walitoa sufu hiyo.—Kama ilivyosimuliwa na Bruce Cournane.

[Picha katika ukurasa wa 16]

Kondoo wa aina kumi na tisa tofauti kwenye maonyesho katika

[Hisani]

Kondoo-dume wa Agrodome Jukwaani

[Picha katika ukurasa wa 18]

Juu: Kondoo wakiingia kwenye maogesho

Chini kulia: Kukata kondoo manyoya ni kazi ya jasho

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki