Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g93 4/8 kur. 20-23
  • Mamilioni Wanateseka—Je! Wanaweza Kusaidiwa?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mamilioni Wanateseka—Je! Wanaweza Kusaidiwa?
  • Amkeni!—1993
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Maoni Yametolewa Hadharani
  • Zoea Hilo Laendelea
  • Pokeo Linalotegemea Uwongo
  • Uhusiano na Dini
  • Je, Kutahiriwa Ni Ishara ya Kuwa Mtu Mzima?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2007
  • Jinsi Akina Mama Wanavyoshinda Magumu
    Amkeni!—2005
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1997
  • “Baada ya . . . Kutoelewana”
    “Kutoa Ushahidi Kamili” Kuhusu Ufalme wa Mungu
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1993
g93 4/8 kur. 20-23

Mamilioni Wanateseka—Je! Wanaweza Kusaidiwa?

Na mleta habari za Amkeni! kutoka Afrika

IKIWA ungekuwa na uwezo, je, ungeondoa kuteseka kwa binadamu? Bila shaka ungeondoa—ikiwa ungekuwa na uwezo! Uhalisi wa mambo ni kwamba hakuna binadamu aliye na uwezo wa kukomesha uchungu wote na maumivu ulimwenguni.

Na bado, labda una uwezo wa kusaidia kupunguza, na hata kuzuia, baadhi ya kuteseka kunakoendelea. Kwa mfano, inakadiriwa kwamba, katika nchi mbalimbali, makumi ya mamilioni ya wanawake wanapatwa na uchungu na maumivu mengi kwa sababu ya desturi ya zamani inayoshikiliwa sana. Kulingana na desturi hiyo, wazazi wenye makusudi mazuri hupanga binti yao akatwe sehemu ndogo au kubwa ya viungo vyake vya uzazi. Kunaitwa tohara ya wanawake.a Lakini wastadi wengi sasa wanakuita FGM (female genital mutilation, au kuchinjwa kwa sehemu za uzazi za wanawake), usemi unaoeleza kitendo hicho kwa usahihi zaidi.

Hosken Report juu ya FGM hutujulisha kwamba uchinjaji wa viungo vya uzazi ni zoea katika sehemu kubwa inayoenea kuanzia Afrika Mashariki hadi Afrika Magharibi na katika maeneo yaliyo karibu. Uchinjaji huo wa wanawake ulio na uchungu huleta matatizo ya afya na waweza kuleta kifo.

Maoni Yametolewa Hadharani

Haijakuwa rahisi kutoa maoni waziwazi dhidi ya zoea hilo. Gazeti la Kenya The Standard lilionyesha kwamba FGM “kwa sehemu kubwa umewekwa kwa siri. Imekuwa vigumu na nyakati nyingine hatari kwa wale wanawake au wanaume wanaotaka kukomesha upasuaji huo, kutoa maoni yao waziwazi dhidi ya zoea hilo. Mara nyingi wao huonwa kuwa wapinga-mapokeo, wapinga-familia, wapinga-dini, wapinga-utaifa, au kuwa wanakataa watu wao na utamaduni wao wenyewe.”

Gazeti hilohilo la Afrika lilieleza kwamba FGM “si ‘zoea la kitamaduni lisilo na dhara’ bali ni kisababishi kikuu cha kuharibiwa kabisa kimwili na kifo kwa wanawake na watoto wasichana . . . Huo huvunja haki ya kila mtoto msichana ya kukua kimwili kwa njia yenye afya na ya kawaida.”

Kotekote Afrika na katika mataifa yote, watu wengi zaidi wanatoa maoni yao katika jitihada ya kuwaelimisha watu juu ya zoea hilo. Zoea hilo huwatia uchungu na kuwajeruhi wasichana, hata tangu uchanga, na halina sababu za kitiba hata kidogo.

Idadi ya wale wanaolemazwa kabisa kwa uchungu na vifo vinavyoripotiwa vimeshtua maofisa wa afya na serikali za mataifa mengi. Hata inadokezwa kwamba huenda FGM ikawa na sehemu katika kuenezwa kwa UKIMWI barani Afrika. Na kwa sababu ya kuwasili kwa wahamaji kutoka Afrika na Mashariki ya Kati kwenda Australia, Kanada, Ulaya, na United States, uchinjaji huo wa wanawake unakuwa suala la afya ya umma katika hospitali fulani za Magharibi. Jambo lisilostahili kupuuzwa ni gharama za matibabu yanayoendelea kwa sababu ya matatizo ya kimwili na, katika visa vingi, matatizo ya kiakili.

Sheria zimetungwa na zinatungwa ili kukomesha desturi hiyo. Uingereza, Ufaransa, Italia, na Swedeni ni baadhi ya nchi za Ulaya ambako FGM si halali. The Globe and Mail la Kanada liliripoti kwamba FGM “umepigwa marufuku na halmashauri ya uelekezi inayosimamia madaktari wa Ontario.” Isitoshe, ilisemwa: “Ingawa sheria ya Kanada haitaji moja kwa moja tohara ya wanawake au kufungwa pamoja kwa kuta za nje za uke, maofisa wa serikali wamesema kwamba mazoea hayo yangeonwa kuwa aina ya kutenda vibaya watoto au mashambulizi yenye kudhuru.”

Hesabu fulani ya mashirika ya kimataifa kama vile Shirika la Afya Ulimwenguni yanapinga FGM. Hatua ya maana ilichukuliwa mnamo Septemba 1990, wakati viongozi wa ulimwengu, kutia na marais wa nchi za Afrika, kama vile Senegal, Uganda, na Zimbabwe, walipokutana jijini New York ili kutia sahihi Mkataba wa Kutetea Haki za Mtoto. Hati hiyo hushutumu tohara ya wanawake kuwa mateso na kutendwa vibaya kingono.

Gazeti Economist la London liliripoti: “Tohara ya wanawake—ambayo huitwa kwa usahihi zaidi uchinjaji wa viungo vya uzazi—inaendelea kuwa mojawapo mambo makuu yanayohofisha ya Afrika. Kulingana na ripoti ya Kikundi cha Kutetea Haki za Wachache kilicho London, . . . makumi ya mamilioni ya wasichana huathiriwa kila mwaka.”

Kichapo hicho kiliendelea kusema: “Upasuaji huo hutofautiana huku mwingine ukiwa na uchungu kidogo na mwingine ukiwa wenye kutia hofu, na waweza kutia ndani kuondolewa kwa kisimi na viungo vingine kwa visu, glasi zilizovunjika, na wembe—lakini mara nyingi dawa ya kugandiza haitumiwi. Unaweza kuongoza kwenye matatizo makubwa wakati wa hedhi, kufanya ngono na kujifungua, matatizo ya kiakili na hata kifo. . . . Zoea hilo huendelea kwa sababu ya hofu za kishirikina juu ya hali ya ngono ya mwanamke, tabia na imani yenye kosa kwamba huo ni usafi.”

Zoea Hilo Laendelea

Katika nchi moja ya Afrika ambako wanawake wengi wamepata tohara, sheria zilizotolewa katika 1947 hukataza aina ya uchinjaji ulio mbaya zaidi. Lakini zoea hilo bado huendelea. Kwa nini? Kwa sababu mamilioni ya watu wenye makusudi mazuri huendelea kuarifiwa vibaya na kudanganywa kuamini kwamba FGM inafaa. Kwa mfano, wanawake wazee wa vijiji huamini kwamba huo ni kwa manufaa ya msichana. Hiyo ndiyo sababu, kama ilivyoripotiwa na gazeti la Naijeria The Guardian, Kikundi cha Kutetea Haki za Wachache kilisema kwamba ni jambo linalohitajiwa “kubadili akili za wanawake wenye umri mkubwa wanaouchochea.”

Gazeti Nursing Times lilitoa sababu kwa njia hiyohiyo: “Elimu ndiyo njia pekee ambayo unaweza kukinza kikweli tohara ya wanawake.” Na baadaye, jarida hilohilo lilisema: “Tatizo hilo lote laweza kuondolewa tu kwa kujulisha juu ya hatari, na kuelimisha wanaume, pamoja na wanawake.” Mbona wanaume waelimishwe pia? Kwa sababu baba wengi hulipia gharama za upasuaji ili waoze binti zao kwa wanaume ambao wanataka tu wanawake waliotahiriwa.

Sababu nyingine ya uchinjaji huo kuendelea linahusu pesa. The American Journal of Nursing lasema: “Tohara ni chanzo muhimu cha mapato kwa wale wanaofanya upasuaji huo; kwa hiyo, watu hao wana faida za kibinafsi katika kuendeleza zoea hilo.” Si wanawake wenye umri mkubwa wanaolipwa tu ili kufanya upasuaji huo bali pia wakunga na vinyozi. Wauguzi na madaktari katika baadhi ya kliniki za tiba watajaribu pia kuepusha wasichana na baadhi ya hatari na mshtuko unaoletwa na upasuaji usio safi. Hata hivyo, hata iwe ni nani anayeufanya, bado huo ni uchinjaji.

Katika visa fulani wanawake wazima hufanyiwa upasuaji huo tena na tena katika miaka yao yote ya kujifungua. The New York Times International lilisema kwamba “wanawake wengi hutahiriwa tena na tena kwa uchungu kwa kukatwa sehemu iliyotahiriwa na kushonwa tena sehemu hiyo kila baada ya kujifungua. Kovu (majeraha yaliyopona) ya tohara hufunguliwa kwa kukatwa kabla ya kujifungua na kushonwa pamoja baadaye. Hilo husababisha kutokwa damu nyingi, huzidisha wakati wa kujifungua na huongeza hatari ya kuharibika akili kwa kitoto.”

Gazeti New Scientist liliripoti kwamba “wasichana wengi wadogo huvuja damu hadi kufa kwa sababu ya kukatwa ateri ya viungo vya uzazi (pudendal) au ateri ya kisimi. Wengine hufa kwa sababu ya mshtuko wa wakati wa upasuaji kwa sababu hakuna ajuaye jinsi ya kuwahuisha na hospitali iko mbali sana, au wale wanaohusika husita kutafuta msaada kwa sababu wanaona aibu kwa upasuaji uliofanywa vibaya.”

Na bado, zoea hilo huendelea. Ripoti za FGM huendelea kutokea katika magazeti ya Afrika na Ulaya. Jarida moja la Afrika hivi karibuni liliripoti kwamba “wadhulumiwa wengi wa uchinjaji wa viungo vya uzazi vya wanawake ni watoto na wasichana. Ingawa wazazi hutahiri binti zao wakiamini kwamba inafaa na inahitajiwa, upasuaji huo na matokeo yao yaweza kulinganishwa na mateso.” Kulingana na gazeti la London The Independent (Julai 7, 1992), uchunguzi wa hivi karibuni ulifunua kwamba “zoea hilo lilienea sana katika Uingereza kuliko vile ilivyokuwa imeaminiwa.” Katika Uingereza wasichana zaidi ya 10,000, “wengi wao wakiwa na umri wa miaka minane au chini, wanakadiriwa kuwa wamo katika hatari ya tohara ya wanawake.”

Pokeo Linalotegemea Uwongo

Wengine huamini uwongo wa kwamba viungo vya uzazi vya wanawake si safi na lazima vitakaswe kwa kuvikatilia mbali. Wanafikiri kwamba ni wanaume tu ambao wana haki ya kufurahia raha ya ngono. Pia inaaminiwa kwamba FGM husitawisha uwezo wa kuzaa, huzuia ukosefu wa adili kingono, na huongeza nafasi za msichana kuolewa. “Kwa kinyume,” lasema gazeti Time, “hali ya kutoamshwa kingono au kutozaa inayoletwa na uchinjaji huo hufanya waume wengi wakatae wake zao.”

Washiriki wa kongamano la hivi karibuni la Halmashauri ya Nchi za Afrika lililofanyiwa Lagos, Naijeria, hawakuamini kwamba tohara ya wanawake yaweza kuzuia wanawake wasiwe wakosefu wa adili na walisema kwamba mazoezi ya mapema juu ya adili ni ya manufaa zaidi. Matendo yasiyofaa yaweza kuzuiwa kwa elimu, si kwa kuchinja. Ili kutoa kielezi: Je! twapaswa kukata mikono ya watoto ili wasije kuwa wevi? Au tukate ndimi zao ili wasiseme mambo mabaya kamwe?

Mume na mke Wanaijeria walikataa kumtahiri binti yao. Hilo lilimkasirisha mama ya mume, aliyehisi kwamba mtoto huyo angekuja kuwa mkosefu wa adili. Lakini kwa malezi mazuri ya kiadili, msichana huyo aliendelea kuwa safi. Kwa kutofautisha, watoto wengine waliojulikana na familia hiyo, ambao wazazi wao hawakutumia wakati kutia adili njema ndani yao, walikuja kuwa wakosefu wa adili sana hata ingawa walikuwa wametahiriwa. Sasa nyanya huyo amesadikishwa kwamba jambo la maana si kutahiriwa au kutokutahiriwa, bali ni kukaza kikiki akilini sheria za adili za Mungu ndani ya watoto.

Ikiwa twawapenda mabinti zetu, tutafikiri kwa uzito juu ya matokeo mabaya ya FGM kwa maisha zao na tusichochee au kuendeleza zoea hilo kwa njia yoyote. Hilo litahitaji ujasiri kwa sababu katika maeneo fulani, kuna hofu kuu ya kukazwa na jamii ili mtu apatane na pokeo hilo.

Uhusiano na Dini

Historia ya uchinjaji wa wanawake ni yenye kuelimisha. Zoea hilo limefanywa kwa karne nyingi na hata liko dhahiri katika maiti zilizohifadhiwa za Misri ya kale. Jarida Plastic and Reconstructive Surgery lasema: “Tohara ya wanawake ilizoewa katika Misri ya kale na inahusiana na itikadi ya Kifarao katika miungu yenye jinsia zote mbili.” Hata leo, jina la aina ya uchinjaji ulio mbaya zaidi ni tohara ya Kifarao.

Katika sehemu fulani, sherehe za kale za kidini zinahusika na FGM. Mwafrika mwenye kuheshimika alieleza kwamba sherehe moja hususa huonwa kuwa tendo la kuwasiliana na mungu wa wazazi wa kale, ambaye anaombwa ulinzi ili asaidie wasichana wapitie upasuaji wenyewe na wakati uleule kuwapatia hekima ya mababu zao.—Linganisha 2 Wakorintho 6:14-18.

Si vigumu kuelewa kwa nini Wakristo wa kweli wanaoishi katika nchi ambako FGM huzoewa hawafuati pokeo hilo. Hakuna lolote katika Biblia ambalo hata linadokeza uhitaji wa kufanyia wanawake machinjo hayo ya upasuaji. Ni wazi kwamba Muumba alikusudia mwanamke aweze kufurahia raha ya ngono katika mpango wa ndoa. Uchinjaji wa viungo vya uzazi vya wanawake haupatani na kanuni za upendo, huruma, na utumizi wa kiasi unaohimizwa katika Maandiko Matakatifu.—Waefeso 5:28, 29; Wafilipi 4:5.

Jambo la maana zaidi, Mungu wa upendo, Yehova, huhuzunishwa na uchinjaji huo usio wa akili na mateso yanayotokea kwa mamilioni ya wanawake na wasichana wadogo. Jinsi tunavyofurahi kwamba ameahidi ulimwengu mpya ambamo hakuna mmoja atakayeteseka!—Ufunuo 21:3, 4.

[Maelezo ya Chini]

a Ona makala “Kutahiriwa kwa Wanawake—Mbona Kunafanywa?” katika toleo la Amkeni! la Julai 1986.

[Sanduku katika ukurasa wa 21]

Namna Gani Kuhusu Tohara ya Wanaume?

Huenda wengine wakazusha swali, Je! si tohara ya wanaume ni uchinjaji wa mwili pia? Biblia husema kwamba wakati mmoja Mungu alifanya tohara ya wanaume iwe ya lazima. Baadaye, kwa kuanzishwa kwa kundi la Kikristo, kutahiriwa hakukuwa kwa lazima tena, ingawa hakukukatazwa. Kunaachiwa uamuzi wa mtu binafsi ikiwa atatahiriwa au wana wake watatahiriwa au la.

Leo, tohara ya wanaume inazoewa katika mahali pengi. Ni kweli, upasuaji huo unatia ndani kuondolewa kwa nyama. Lakini upasuaji huo haulingani kwa njia yoyote ya FGM. Kwa kawaida, wanaume hawapatwi na matokeo mabaya baada ya kutahiriwa. Kwa kutofautisha, utendaji wa kawaida wa wanawake, kama vile hedhi, ngono, kujifungua, na kukojoa, mara nyingi huandamana na uchungu mwingi wa maisha yote kwa sababu ya FGM. Pia, matatizo makubwa ya kujifungua yamesababisha kulemaa vibaya kwa mtoto na hata kifo cha watoto wengi.

Ni wanaume wangapi wangependa wao wenyewe au wana wao wachinjwe uume wao hivi kwamba wakose hisi yote wakati wa ngono na wawe na uchungu na matatizo ya afya wakati wote katika muda wa maisha yao? Kwa wazi, hakuna ulinganisho kati ya tohara ya wanaume na FGM.

[Sanduku katika ukurasa wa 23]

Msichana Mwafrika Atoa Maoni

‘Nilikuwa mwenye miaka minane nilipotahiriwa. Sasa nina miaka 11, lakini bado ninakumbuka upasuaji huo vizuri sana. Mimi huhuzunika hata ninapofikiria juu ya huo, na nyakati nyingine ninapata ndoto mbaya sana. Siku nyingi mimi huwa mtu mwenye furaha, lakini ninapofikiria upasuaji huo, ninaanza kuhisi nimedhoofika sana.

‘Nilikuwa na furaha kwelikweli niliposikia juu ya tohara kwa mara ya kwanza. Familia na watu wa ukoo wetu wangenipa zawadi nyingi. Sikujua upasuaji wa tohara ni nini, na sikufikiri kwamba ungekuwa wa uchungu.

‘Msisimko wangu ukatoweka. Nikaanza kulia na nikaogopa kwelikweli. Kulikuwa na wanawake wanne walionishika mikono na miguu. Mwanamke mmoja alifunika mdomo wangu kwa mkono wake. Nilijaribu kujiondoa, lakini walikuwa wenye nguvu kunishinda na wakanilazimisha nilale chini tena. Ulikuwa uchungu wee.

‘Kisu kiliponikata, damu ilienea kila mahali. Sikujua kamwe kwamba jambo fulani laweza kutia uchungu hivyo. Baadaye walifunika jeraha hilo kwa mchanganyiko wa mayai na sukari. Kisha wakafunga miguu yangu pamoja. Nilichukuliwa hadi kwenye gari. Nililia hadi tulipofika kwenye kijiji.’—Dondoo lililochukuliwa kutoka gazeti la The Standard la Kenya.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 20]

WHO/OXFAM

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki