Kuutazama Ulimwengu
Spishi Zilizo Hatarini mwa Kutoweka
Katika Ujerumani Waziri wa Mazingira wa Serikali ya Muungano, Angela Merkel, alitaja hadharani hangaiko lake juu ya asilimia kubwa ya spishi zilizo hatarini mwa kutoweka katika nchi hiyo. Akitangaza kutolewa kwa kitabu kuhusu mazingira, kilichochapishwa na wizara hiyo, Merkel alifunua tarakimu fulani zenye kushtusha. Wataalamu wakadiria kuwa kati ya wanyama wenye uti wa mgongo waliopo Ujerumani, “asilimia 40 ya mamalia wote, asilimia 75 ya wanyama-watambaazi, asilimia 58 ya amfibia, asilimia 64 ya samaki wa maji matamu, na asilimia 39 ya ndege ni spishi zilizo hatarini mwa kutoweka,” laripoti gazeti Süddeutsche Zeitung. Mimea pia haiko katika hali nzuri, asilimia 26 za spishi zote zikiwa hatarini mwa kutoweka. Jitihada za hapo awali za kupunguza hatari kwa mazingira ya kiasili hayajawa na matokeo sana. Merkel alitoa mwito wa “mkakati mpya kwa ajili ya kukinga maumbile.”
Kuwalinda Watoto Dhidi ya Watekaji-Nyara
Wazazi katika Ujerumani wanaendelea kuwa na hangaiko kuhusu usalama wa watoto wao, hasa kwa sababu ya ongezeko la hivi karibuni la utekaji-nyara wa wasichana katika nchi hiyo. Kulingana na Nassauische Neue Presse, Julius Niebergall, mwanatiba katika Shirika la Ujerumani la Kuwalinda Watoto, alipendekeza hatua fulani za kutahadhari. Kwa kielelezo, wazazi wangeweza kuwaonyesha watoto wao sehemu fulani kwenye njia ya kwenda na kutoka shule—duka au nyumba—ambako waweza kutafuta msaada wakati wa dharura. Wachanga wapaswa pia kufunzwa kutozungumza na watu wasiowajua au kuwaruhusu wawaguse. Niebergall alitilia mkazo kwamba “watoto wapaswa kujifunza kwamba wanaweza kusema la,” hata kwa watu wazima. Hasa wakitishwa na mtu anayekusudia kuwa mtekaji-nyara, watoto wapaswa kuwaomba watu wazima wengine msaada. “Tafadhali nisaidie. Namwogopa mwanamume huyu,” ndivyo wapaswavyo kufunzwa kusema.
Abiria Wenye Jeuri
Kampuni za ndege za biashara zaripoti ongezeko kubwa la tabia yenye jeuri ya abiria wenye hasira. Wakikasirishwa na mambo kama kuchelewa kwa ndege na kupotea kwa mizigo, abiria “hutemea mate watumishi wa ndege, hutupa trei za chakula na wakati mwingine kuwapiga wafanyakazi. Mara kwa mara, wao hata huwashambulia marubani,” laripoti The New York Times. Maofisa wanahangaika hasa kuhusu mashambulizi kama hayo yakitukia katika ndege angani, kwani mashambulizi haya yaweza kutokeza aksidenti. Shirika moja la ndege huripoti karibu visa 100 vya matukano au mashambulizi ya kimwili kila mwezi. Gazeti Times lasema kuwa “abiria wasumbufu ni wa jinsia zote, wa jamii mbalimbali, wenye umri mbalimbali na ni wabaya hata wawe wameketi katika economy class, business class, au first class. Angalau mmoja kati ya kila watatu amekuwa akinywa pombe.”
Uchinjaji wa Sehemu za Uzazi za Wanawake Waendelea
Uchinjaji wa sehemu za uzazi za wanawake (FGM) waendelea kuwa tatizo katika nchi nyingi, hasa katika Afrika, kulingana na The Progress of Nations 1996, ambayo ni ripoti ya kila mwaka ichapishwayo na Umoja wa Mataifa. Ijapokuwa nchi kadhaa zimeweka sheria dhidi ya zoea hili katili, karibu wasichana milioni mbili huchinjwa sehemu za uzazi kila mwaka. Wahasiriwa hasa ni kati ya umri wa miaka 4 na 12. “Mbali na woga wa papo hapo na maumivu, matokeo yaweza kutia ndani kutokwa damu kwa muda mrefu, ambukizo, utasa, na kifo,” yasema ripoti hiyo. (Kwa habari zaidi kuhusu uchinjaji wa sehemu za uzazi za wanawake (FGM), ona toleo la Aprili 8, 1993, la Amkeni!, ukurasa wa 20-23.)
Mbwa Wasaidia Wenye Kifafa
Katika Uingereza mbwa wanazoezwa ili kuwatahadharisha wanaougua kifafa kwamba shambulio lakaribia. Hili lingempa mgonjwa wakati wa kutosha wa kujitayarishia shambulio hilo, laripoti The Times la London. “Likiwa tokeo la kumthawabisha mbwa kwa kubweka wakati wa shambulio,” aeleza meneja wa shirika linalojishughulisha na kuwazoeza mbwa wa kuwasaidia wasiojiweza, “ameweza kuzoea ishara na dalili zinazoonyeshwa na mgonjwa kabla tu ya kupatwa na shambulio. Akijua kwamba kuitikia hivyo kutatokeza thawabu, mbwa anakuwa makini sana kutambua dalili kama hizo.”
Mitazamo Mipya Katika Japani
Taasisi ya Vijana ya Japani hivi karibuni ilifanya uchunguzi kati ya wanafunzi 1,000 wa shule ya sekondari katika Japani, laripoti The Daily Yomiuri. Ukaguzi huo ulionyesha kwamba asilimia 65.2 ya wanafunzi hawaoni ubaya wa kukosa masomo. Karibu asilimia 80 wanahisi vivyo hivyo kuhusu kutotii walimu, na karibu asilimia 85 ya wanafunzi waona kwamba ni sawa kutotii wazazi. Kulingana na The Daily Yomiuri, uchunguzi huohuo ulionyesha kuwa asilimia 25.3 ya wasichana wanafikiri kwamba kujihusisha katika ukahaba wakiwa wangali shuleni kwapaswa kuwa chaguo la kibinafsi.
Mazoea Hatari ya Uendeshaji-Magari
● “Asilimia 50 ya vifo vyote vya barabarani katika Brazili vyasababishwa na kunywa pombe,” lataarifu gazeti la habari Gazeta do Povo la Curitiba, Brazili. Madereva walevi husababisha “zaidi ya vifo 26,000 kila mwaka.” Aksidenti hizi “mara nyingi hutokea katika safari fupifupi na katika halihewa nzuri.” Hata ingawa dereva mlevi aweza kuhisi akiwa na uhakika, uwezo wake wa kutenda haraka umepungua, hivyo akihatarisha usalama wake na wa wengine barabarani. Majaribio yaonyesha kwamba iwapo mtu amekunywa alkoholi, ni vigumu, na hata haiwezekani, kushughulikia hali zisizotarajiwa.” Kulingana na gazeti la habari hilo, kuondolewa kwa alkoholi katika mwili kwaweza kuchukua muda wa saa sita hadi nane na wala kahawa chungu wala kuoga kwa maji baridi hakuwezi kumsaidia dereva mlevi kuendesha gari kwa usalama.
● Kulingana na uchunguzi mmoja wa Uingereza, dereva wa kawaida hufanya makosa mazito 50 kwa juma moja. Kwa ujumla, madereva 300 waliochunguzwa walikiri kwamba hawakujali kwa angalau mara moja katika asilimia 98 ya safari zao, laripoti The Times la London. Moja kati ya safari mbili, wao walikasirika. Hatari ambayo madereva wengi hujasiria ni kwendesha gari kwa kasi, na zaidi ya nusu walisema kuwa walikuwa wamehusika katika aksidenti. Utafiti katika Toronto, Kanada, wapendekeza kuwa madereva wanaotumia simu garini wanapoendesha magari wana mwelekeo wa mara nne zaidi wa kusababisha aksidenti. Hatari ni kubwa zaidi katika dakika kumi za kwanza baada ya kuanza kuzungumza kwa simu, yaelekea kwa sababu dereva amekengeushwa na kuitikia kwake hupungua kwa kadiri iyo hiyo.
Upishi—Je, Ni Ustadi Unaofifia?
Kulingana na uchunguzi wa miezi 12 wa tabia za kula katika jimbo la Queensland la Australia, upishi waweza kuwa ustadi unaofifia. Gazeti The Courier Mail laripoti kuwa watu wengi wenye umri wa chini ya miaka 25 hawana stadi zinazohitajiwa ili kupika chakula chao wenyewe. Mhadhiri wa afya ya umma Margaret Wingett, mwanzilishi wa uchunguzi huo, alisema kuwa katika siku za zamani vijana—hasa wasichana—wangejifunza kupika ama nyumbani kutoka kwa mama zao ama shuleni. Lakini siku hizi yaonekana kwamba vijana wengi, kutia ndani wasichana, hawajui kupika na ni kama hawapendezwi kujifunza. Wengi hupendelea namna fulani ya chakula kilichopakiwa au vyakula vya kutengenezwa haraka. Wengine huamini kuwa tabia kama hizo za ulaji zaweza kuongoza kwenye ongezeko la msongo wa juu wa damu, ugonjwa wa kisukari, na maradhi ya moyo.
Majengo Yenye Nururishi
Kulingana na gazeti Asiaweek, “majengo 105 yaliyo na vyumba 1,249 yamechafuliwa” kwa unururifu kaskazini mwa Taiwan. Hii iligunduliwa na mfanyakazi mmoja wa kampuni ya umeme ambaye alikuwa akionyesha mwana wake jinsi kichunguza-mnururisho kifanyavyo kazi. Alipokuwa akichunguza kiasi cha mnururisho jikoni, alishtuka kuona indiketa ikionyesha kiwango cha hatari. Uchunguzi zaidi ulifanywa, ukihakikisha kuwa hilo jengo na majengo mengine yalikuwa yamechafuliwa. Majaribio yalionyesha kwamba mnururisho ulikuwa ukitokana na pao za chuma za kuimarisha jengo ambazo zilikuwa kwenye kuta. Wenye mamlaka hawakubaliani kuhusu jinsi unururifu ulivyoingia katika vyuma hivyo.
Vizuia-Wezi vya Hali ya Juu
Zile nukta ndogondogo, zilizopendwa sana wakati mmoja na wapelelezi kwa kupeleka jumbe za siri, zimetumika katika Uingereza ili kuzuia wizi. Hizo nukta, kila moja ikiwa na ukubwa usiozidi nukta ya kawaida, huwa na namba ya posta ya mwenye kuitumia mara 60 au 70 na zatumika kuwekea alama mali zinazoweza kuwavutia wezi. Gazeti The Times la London laripoti kuwa nukta hizo “huja zikiwa zimeelea katika kitu chenye kunata kwa nguvu ndani ya chupa ikiwa na burashi, inayofanana na kichupa cha rangi ya vidole. Kila chupa ina kufikia nukta ndogondogo 1,000 na mnunuzi aweza kupaka vitu vyake kama apendavyo kwa zile nukta.” Anyekusudia kuiba huonywa na kibandiko kionekanacho wazi na hawezi kuwa na hakika kamwe kuwa ameziondoa nukta zote zilizofichika. Hivyohivyo, chipu ya kompyuta, iliyotokezwa kutambulisha wapiganaji wa Vita ya Vietnam walioumizwa, sasa yatambulisha michoro, michongo, au fanicha. Ikikaribia kutoshana na chembe cha mchele, chipu hiyo inapoingizwa haiwezi kutambulika na hushikilia mambo makuu kama vile historia ya umiliki, ufafanuzi, na jina la mwenyewe, ambavyo vyaweza kusomwa kwa kutumia kisoma-maandishi. Habari hii yaweza kusaidia kutambulisha wenyewe halisi wa vitu vipatikanavyo vikiwa na wahalifu, lataarifu gazeti The Times.