Nondo au Kipepeo—Waweza Kuwatofautishaje?
JE! WAWEZA kuwatofautisha kwa mtazamo wa kwanza? Labda unatofautisha kipepeo kwa sababu ya rangi zake maridadi na mwendo wake unaoonekana kuwa haukomi—akipepea kutoka ua moja hadi jingine, akitua kidogo hapo, mabawa yake yakipiga-piga juu na chini, kisha aondoka kwa woga kwenda kwenye chanzo chake kingine cha mlo. Ni mtihani wa subira kama nini kwa mpiga-picha yeyote stadi! Kitu kingine cha kutofautisha ni vipembe vyembamba vya kupapasia vyenye miisho yenye nundu.
Lakini vipi juu ya nondo? Naam, hawa huwaoni sana wakati wa mchana. Wao hasa ni viumbe vya usiku. Rangi zao huwa nyeusi-nyeusi mara nyingi. Wana miili mikubwa, na vipembe vyao vya kupapasia vina manyoya mengi, jambo ambalo huwasaidia kutambua wa kike hata akiwa mbali sana. Aliyepigwa picha hapa ni nondo Polyphemus, anayepatikana kotekote katika United States. Kwa sababu ya madoa makubwa yanayofanana na macho katika mabawa yake ya nyuma, aliitwa jina la Jitu la hekaya la Kigiriki aliyekuwa na jicho moja na aliyeitwa Polyphemus. Upana wa mabawa yake waweza kutoka sentimeta 9 hadi 15, na huo ni mdogo kulinganisha na nondo wengine.
Kuna aina za vipepeo na nondo zaidi ya 112,000 zinazojulikana, kulingana na Grzimek’s Animal Life Encyclopedia. Mabawa yao “yamefunikwa juu na chini kwa magamba madogo sana . . . yanayotoa rangi zilizo nzuri ajabu na maridadi ambazo huonwa mara nyingi.” Kama vile mtaalamu yeyote wa vipepeo na nondo atakavyokuambia, hivi ni viumbe vinavyostaajabisha sana. Namna vilivyoumbwa, unamna-namna wavyo, na mabadiliko yavyo ya mwili ya ajabu huwafanya wafae kwa uchunguzi, si kwa maisha ya wakati huu tu, bali kwa maisha ya wakati wa milele!
[Picha katika ukurasa wa 25]
Nondo wa “Polyphemus” aliyepigwa picha katika Luverne, Alabama, U.S.A., aonyeshwa hapa kwa ukubwa wake halisi
Vipembe vyenye manyoya husaidia wa kiume kutafuta wa kike