Siku Moja Katika Maisha ya Kipepeo
IKIWA mambo unayofanya kila siku yaonekana kuwa yenye mkazo na magumu, fikiria juu ya kipepeo mwenye kufanya kazi kwa bidii. Mwanzoni huenda ukafikiri kwamba ratiba ya kazi ya kipepeo huwa kama likizo ya kindoto. Huku akiruka kutoka ua moja hadi jingine, akionja maji matamu ya ua hapa na pale, akiota jua kama apendavyo, kipepeo huonekana kuwa kielelezo bora zaidi cha mtindo wa maisha ya starehe nyingi.
Lakini katika ulimwengu wa wadudu, sikuzote mambo hayawi vile yanavyoonekana. Vipepeo ni viumbe wenye shughuli wanaofanya utumishi wa maana huku wakiharakisha mambo kila wakati. Acheni tujiunge na kipepeo katika siku ya kazi ya kawaida.
Kiamshakinywa cha Kuota Jua
Je! wewe huamka ukiwa dhaifu? Unyonge wa mapema asubuhi ni athari ya kawaida miongoni mwa vipepeo. Asubuhi fulani wanaketi tu—kihalisi. Tatizo lao ni halijoto ya mwili, inayobadilika kulingana na mazingira yao. Baada ya wao kutumia usiku wenye baridi wakiwa juu ya jani, damu yao ni baridi sana hivi kwamba hawawezi kusogea, licha ya kuruka. Kwa hiyo ni lazima wangojee hadi jua lichomoze.
Jua linapochomoza, kipepeo hufungua mabawa yake na kuyaweka yakikabili miali yalo yenye kutia joto. Upesi mabawa hayo yaliyopanuliwa, yakiwa kama vyombo vidogo vya kutwaa nishati ya jua, hupata joto linalohitajiwa, na huyoo aruka kipepeo. Lakini vipi ikiwa anga limetanda? Katika sehemu za baridi-baridi, inabidi vipepeo waendelee kukaa—bila kusogea juu ya tawi au ua linalofaa—hadi jua linapoangaza. Huo si uzembe. Inawabidi wafanye hivyo.
Ikiwa siku si yenye joto sana, kipepeo hutua mara kwa mara ili apate motisha zaidi kwa miale ya jua. Kama gari linalotiwa mafuta kwenye kituo cha petroli, yeye ahitaji kiasi chake cha nishati ya jua. Katika sehemu za kitropiki huenda kipepeo akahitaji kuota jua mapema asubuhi au baada ya mvua kunyesha. Kwa ujumla, kadiri hali-anga ilivyo baridi-baridi, ndivyo anavyotumia wakati mwingi zaidi akiota jua. Nishati yake ikiisha kurejeshwa, yeye huendelea na kazi anayohitaji kufanya.
‘Upendo kwa Manukato ya Kwanza’
Kazi ya maana zaidi ni kutafuta mwenzi. Akiwa na tazamio la kuishi muda usiopita majuma machache, hakuna wakati wa kupoteza. Na kupata mwenzi katika ulimwengu wa vipepeo si kazi rahisi—inahitaji subira na udumifu unaostahili sifa.
“Upendo kwa mtazamo wa kwanza” haujulikani miongoni mwa vipepeo. Wao waweza kuona tu umbali mdogo sana, na mara nyingi wao hudhania kimakosa kipepeo wa aina nyingine kuwa mmoja wao. Hilo hufanya kuwe na makimbizano mengi yanayofikia tamati wakati kipepeo mwenye kukimbiza anapong’amua hatimaye kwamba macho yake yalimdanganya.
Kufanya maisha yawe magumu hata zaidi, mara nyingi yule wa kike huwa hakubali. Yule wa kiume mwenye idili huruka bila kuacha akimzunguka yule wa kike, kwa mwendo wa kasi sana, akitumaini kwamba hatimaye atakubali. Lakini dansi hizo zenye kutazamisha za kipepeo huambulia patupu wakati yule wa kike anaporuka na kwenda zake, akiacha yule maskini wa kiume aendelee na jitihada za kutafuta mwenzi.
Kwa kushangaza, yule wa kike hasisimuliwi sana na rangi za kupendeza za yule wa kiume anayemwandama. Ingawa Darwin alidhania kijuu-juu kwamba rangi zenye kutokeza za vipepeo huandaa ‘fursa fulani ya mageuzi,’ hakujakuwa na ithibati yoyote ya hilo. Katika jaribio moja, wale wa kike wa aina ya Anartia amathea kutoka Amerika Kaskazini walijamiiana vizuri na wa kiume ambao mabawa yao ya rangi nyekundu-nyangavu na meusi yalikuwa yamepakwa rangi nyeusi kila mahali. Inaonekana kwamba kile cha maana sana ni kawaida ya kuruka kwa yule wa kiume, udumifu wake, na, zaidi ya yote, “manukato ya upendo” ya kipekee.
Manukato ya upendo hutia ndani marashi yenye kusisimua ambayo yule wa kiume hutumia ili kuvutia. Ni manukato yenye kulewesha, yaliyofanyizwa ili kuathiri wale wa kike wa aina yake. Wakati wa uchumba yeye hujaribu kumpaka hayo “manukato bora kabisa.” Ingawa hayo manukato si uhakikisho wa mafanikio, yana matokeo mema wakati yule wa kike mwenye nia anapopatikana.
Mwonjo wa Maji Matamu ya Maua
Ni lazima nishati yote iliyotumiwa katika jitihada hizo za kutafuta mwenzi irudishwe. Ndiyo sababu inayofanya vipepeo wapende maji matamu ya maua. Maua hutangaza chakula hicho chenye nishati nyingi kwa maumbo na rangi zayo zenye kuvutia. Anapotua juu ya ua, kipepeo hufyonza kwa ustadi maji matamu ya ua kwa mdomo wake mrefu ulio kama mrija, ambao yeye husukuma kwenye shina la ua hilo.
Huku akinywa maji hayo matamu, mdudu huyo hupakwa chavua juu ya mwili wake wenye nywele-nywele, hivyo akipeleka chavua kwa mwili wake hadi kwenye ua linalofuata analozuru. Wakati wa siku ya kazi ya kawaida, mamia ya maua hutiwa chavua. Hata hivyo, katika misitu ya tropiki, hakuna maua mengi. Vipepeo wa tropiki kwa kawaida hunywa nini?
Vipepeo wa tropiki hupenda mno kujishibisha kwa matunda yaliyooza. Matunda hayo yaliyoiva kupita kiasi yanayoanguka chini huwaandalia chanzo cha nishati yenye sukari-sukari.
Vipepeo pia hupenda chumvi. Mara nyingi wanaweza kupatikana wakifyonza unyevu wa chumvi-chumvi kwenye ardhi yenye unyevu au mara kwa mara jasho juu ya mkono wa binadamu mwenye kuvutiwa. Hata yule kipepeo jasiri wa rangi-moto ameonekana akifyonza machozi ya mamba.
Huku akijishughulisha kutafuta mwenzi, akitia chavua maua, na kujishibisha, ni lazima pia rafiki yetu mwenye mabawa awe chonjo kuona adui. Huenda akaonekana kuwa bila kinga, lakini ana njia kadhaa za kuepa asikamatwe.
Kuepa Hatari
Kipepeo maridadi anayeruka katika konde la majani angekuwa mlo wenye kuvutia wa ndege yeyote anayekula wadudu. Lakini mruko wa kipepeo usio na utaratibu, mara huku mara kule, hufanya kumkamata kuwe kugumu kweli. Ndege wengi huchoka baada ya kujaribu mara kadhaa. Hata ndege anapokamata kipepeo, huenda mdudu huyo akaweza kutoroka kwa kuacha sehemu ya bawa lake kwenye mdomo wa ndege.
Uwezo wa macho ni ulinzi mwingine. Ingawa vipepeo huona umbali mdogo, macho yao makubwa yana uwezo mkubwa wa kuona kitu kikisogea. Wao huruka mbali kwa dalili yoyote ya hatari, kama vile mtu yeyote ambaye amejaribu kupiga picha kipepeo anavyojua vizuri.
Vipepeo fulani wenye kuruka kwa mwendo wa polepole wana chombo kingine cha usalama—ladha yao mbaya. Hiyo husababishwa na mlo wao wa mimea yenye sumu walipokuwa viwavi. Mara akiisha kula kipepeo kama huyo, mara nyingi ndege ataepuka kipepeo mwingine. Mara nyingi vipepeo hao wenye ladha mbaya—kama vile kipepeo-mfalme—wana rangi zenye kutokeza, kionyo kinachoonekana ambacho yaonekana hukumbusha ndege wakae mbali.
Mwisho wa Safari
The World Book Encyclopedia chasema kwamba vipepeo wengi hawaishi muda unaozidi majuma machache, lakini kwamba jamii fulani zaweza kuishi kufikia miezi 18. Baadhi yao huwa hawatendi wakati wa miezi ya baridi ya kipupwe au wakati wa msimu mrefu wa kiangazi katika tropiki.
Lakini yajapokuwa maisha yao mafupi, vipepeo waweza kutimiza mambo yenye kushangaza. Karne iliyopita vipepeo-wafalme walivuka bahari Atlantiki kwa wingi na kusitawi katika Visiwa Kanari, mbali kutoka pwani ya Afrika. Msafiri mwingine mkubwa, kibibi-rangi-rangi, husafiri kwa ukawaida kutoka Afrika Kaskazini hadi Ulaya ya kaskazini katika musimu wa kiangazi.
Wakati wa muda mfupi wa maisha yao, vipepeo wasiochoka hufanya kazi ya maana wakitia chavua katika maua, vichaka, na miti ya matunda. Na zaidi ya hilo, kuwapo kwao huongeza uzuri na uvutio wa mashambani. Kiangazi hakiwezi kuwa kiangazi bila vipepeo.
[Picha katika ukurasa wa 16]
Kuota jua mapema asubuhi
[Picha katika ukurasa wa 17]
Kutoa maji matamu kutoka katika ua
[Picha katika ukurasa wa 18]
Kufyonza unyevu kutoka ardhini
[Hisani]
Hisani ya Buckfast Butterfly Farm