Mkubwa Zaidi na Mdogo Zaidi
“Usiue nondo wala kipepeo.”—WILLIAM BLAKE (1757-1827).
JE, UMEWAHI kutazama kipepeo akipepea? Ni nani ambaye hatasimama na kutazama umaridadi na wepesi wa mdudu huyo mwenye kupendeza ila tu mtu asiyejali kabisa viumbe? Nao wanapatikana kotekote ulimwenguni kwa ukubwa mbalimbali na maumbo mbalimbali hivi kwamba inasemekana kuna aina ya vipepeo baina ya 15,000 na 20,000!
Ni kipepeo yupi aliye mkubwa zaidi ambaye umewahi kumwona? Ikiwa unaishi Papua New Guinea, basi huenda umeona kipepeo mkubwa zaidi ulimwenguni—anayeitwa Queen Alexandra’s birdwing, mwenye mabawa yanayofikia sentimeta 28 yakipanuliwa kutoka mwisho mmoja hadi mwingine. Ikiwa unaishi Amerika ya Kaskazini au ya Kati, huenda umepata kumwona kipepeo aina ya Homerus swallowtail, mwenye mabawa yanayofikia sentimeta 15 yakiwa yamepanuliwa kutoka mwisho mmoja hadi mwingine. Kipepeo mkubwa zaidi katika Afrika ni African giant swallowtail, ambaye ana mabawa yanayofikia sentimeta 23 yakiwa yamepanuliwa kutoka mwisho mmoja hadi mwingine.
Vipi juu ya vipepeo wadogo zaidi? Wanapatikana wapi? Kitabu The Illustrated Encyclopedia of Butterflies, cha Dakt. John Feltwell, chasema kwamba “Pygmy blue wa Amerika Kaskazini . . . huenda ndiye kipepeo mdogo zaidi ulimwenguni, akiwa na mabawa yenye urefu wa milimeta 15-19 yakiwa yamepanuliwa kutoka mwisho mmoja hadi mwingine.” Kipepeo mdogo zaidi nchini Uingereza ni small blue, mwenye mabawa yanayofikia milimeta 24 yakiwa yamepanuliwa kutoka mwisho mmoja hadi mwingine.
Katika sehemu nyingi ulimwenguni, kuna majumba ya vipepeo ambako unaweza kutembea-tembea na vipepeo maridadi watue juu yako. Unaweza kujifunza mengi sana kuhusu uumbaji huu wenye kuvutia na mzunguko wa maisha yake, mabadiliko yake tokea yai dogo sana hadi kiwavi hadi mabuu hadi kipepeo mkomavu. Basi wakati mwingine uonapo kipepeo akipepea, simama, ukamtazame, ustaajabu. Utakuwa ukitazama mwujiza—awe kipepeo mkubwa au mdogo!
[Picha katika ukurasa wa 25, 25]
Kipepeo mkubwa zaidi na mdogo zaidi, “Queen Alexandra’s birdwing” na “pigmy blue” (ukubwa wao halisi)
[Hisani]
Vipepeo: Allyn Museum of Entomology, Florida Museum of Natural History