Kama Kisanamu Hicho Kingeweza Kusema!
“UWE mwangalifu!
Nisingependa kivunjike!” Jane huambia rafiki zake hivyo mara nyingi anaponionyesha kwa rafiki zake, hasa ikiwa mmoja wao athubutu kunigusa. Naam, mimi ni kitu cha thamani. Na ninajua kwamba wote wawili John na Jane wananithamini sana—wananishika kwa uangalifu sana. Lakini kwa kweli, siwezi kuvunjika kwa urahisi hivyo.
Nikitazama watu wenye kunistaajabia kupitia macho yangu yaliyorembeshwa sana, mimi hujichekea mara nyingi kwa ajili ya ile taratibu inayohitajika ili nitengenezwe. Hakuna mwanadamu anayeweza kustahimili hali hiyo ngumu sana! Ni masimulizi yanayopendeza sana.
Vianzo vya Tope-Tope
Udongo mweupe wa mfinyanzi, sehemu yangu kubwa, husagwa pamoja na aina ya jiwe gumu jeupe na mifupa ya mnyama iliyopashwa joto, na kuchanganywa na maji. Ni lazima kuwe na usawaziko mzuri. Sumaku-umeme huondoa vipande vyovyote vya chuma ambavyo huenda vikawa ndani ya umaji-maji huo mzito wenye rangi ya mtindi, au tope kama unavyoitwa kwa lugha ya biashara, baada ya hapo maji yanakamuliwa mpaka tope hilo lionekane kama kidonge cha plastiki.
Kisha tope linaingizwa katika mashine ya kufinyanga udongo, ambayo ni kama mashine ku-bwa sana ya kuchanganya, ili itiwe midukuo na kukandwa. Pampu ya kuvuta hewa hutoa hewa yote iliyomo ndani, ambayo yaweza kufanya udongo wangu upasuke wakati unapopashwa moto hatimaye katika tanuri.
Mbuni wangu ametengeneza kiolezo changu ambacho ni kikubwa zaidi ya vile nitakavyokuwa hatimaye kwa karibu asilimia 13. Na si ajabu! Mimi hufinyaa ninapopitishwa ndani ya tanuri mara tatu au nne katika halijoto inayoanzia sentigredi 800 hadi 1,200. Naam, bado kuna miezi mingi iliyo mbele ya kazi kabla niweze kutabasamu, ambalo ndilo jambo pekee niwezalo kufanya. Acha nikuambie zaidi.
Kuunganisha Vipande
Je! wafikiri kwamba ninamiminwa katika kalibu nikiwa kipande kimoja? Watu wengi hufikiri hivyo, lakini sivyo hata kidogo. Ninamiminwa katika kalibu nyingi za lipu zinazoondoa unyevu ili udongo wangu ushikamane vizuri. Mfinyanzi wangu anapofungua kalibu zake hatimaye, ninatokea, lakini nikiwa vipande-vipande—kichwa changu huku, mguu mmoja kule, rinda likiwa limewekwa sehemu nyingine kwa uangalifu. Ah, jinsi ninavyotamani niunganishwe!
Kwa mikono yenye uanana mwunganishi wangu anichukua. Ninafurahi kwamba ameona mikwaruzo ya kando iliyoachwa na kalibu. Aitoa kwa uangalifu, kutia na lile kunyanzi baya linalozunguka kichwa changu. Tayari ninahisi vizuri! Kwa ustadi mwingi aunganisha mikono yangu kwa mwili wangu, akihakikisha kwamba mfuko wa mkono wangu umewekwa mahali panapofaa. Kwa ustadi kama ule wa daktari mpasuaji, aniunganisha na kunishikanisha mpaka hakuna mtu anayeweza kutambua kwamba maisha yangu yalikuwa vipande vingi sana.
Sasa ninasimama ili nikauke. Kwa vile hakuna mipasuko inayoonekana, niko tayari kujaribiwa kwa moto. Tanuri inapashwa joto, nami ninaingizwa kwa uanana ndani yayo, nikiwa pamoja na visanamu vingine vingi.
Mapambo
Mkaguzi asema hivi juu yangu, “Bora kabisa!” Nimefaulu na sasa ninasimama kwenye mstari nipelekwe katika idara ya mapambo. Nitafunikwa kwa kioo kinachoitwa kwa kawaida king’arishaji, jambo linalomaanisha kwamba ni lazima nitumbukizwe katika pipa kubwa la kioo ambacho kimeyeyushwa. Kisha ninarudi tena katika tanuri nitoke humo niking’aa na kumetameta, nikiwa tayari kwa rangi zinazopakwa juu ya kioo hicho.
Ninapakwa kwa njia yangu pekee, na hiyo ndiyo sababu ya kwamba huwezi kupata miongoni mwetu visanamu viwili vinavyofanana kabisa. Inachukua mazoezi ya miaka mingi, na mwanamke mchanga atakayenipaka rangi asema kwamba ni lazima afanye hivyo kwa mwendo ule-ule lakini kwa haraka. Asipofanya hivyo, mistari yaweza kutokea katika sehemu ambazo rangi inakauka.
Je! wapenda macho yangu? Hayo ndiyo magumu zaidi kupaka rangi. Siku moja nilisikia mpakaji rangi mmoja akimweleza rafiki yake kwamba ni lazima aniweke imara kwenye benchi na avute pumzi nyingi ndani kisha asipumue mpaka amalize kupaka rangi macho, mboni za macho, na nyushi. Kupumua au kusonga kwa njia yoyote kwaweza kuharibu haraka sana mpako wa brashi, nilimsikia akisema.
Sasa nimevalishwa, na ninaitwa Autumn Breeze. Kwenye kikanyagio changu jina langu na la mfanyi wangu linapigwa muhuri—muhuri wa kibali, waweza kusema. Moto mwingine wa mwisho wa kuimarisha sura yangu nami niko tayari kwenda mahali popote ulimwenguni.
Kwa kweli, nilipelekwa katika soko la nyumbani nami nilikaa Uingereza, ambapo John aliniona. Ninafurahi kwamba aliniona. Jane, mke wake, alifurahi sana wakati John aliponitoa kwake kwa kuadhimisha mwaka wao wa 25 wa ndoa. Hapo ndipo nilipomsikia Jane akisema kwa mara ya kwanza: “Ah, ni lazima tuwe waangalifu! nisingefurahi kikivunjika!” Ni vizuri kujua kwamba niko salama katika mikono yao. Na ni vizuri sana kufurahisha—na kuthaminiwa.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]
“Autumn Breeze,” hisani ya Royal Doulton
[Picha katika ukurasa wa 26]
Mwunganishaji hushikanisha vile visehemu mbalimbali vya kisanamu katika kukitayarisha kwa ajili ya tanuri
Lile tope likimwagika kutoka kwa mashine ya kufinyanga hadi kwenye kalibu ya lipu
Kufungua kalibu za lipu
Baada ya kuwekwa kioo cha kung’arisha, kisanamu hicho kinapakwa rangi yacho pekee mara nyingi
Mambo madogo-madogo ya uso yanawekwa kwa uangalifu
[Hisani]
Picha zote: Hisani ya Royal Doulton