Safari ya Basi ya Kwenda Katikati ya Australia
Na mleta habari za Amkeni! katika Australia
JE! UMEPATA kuabiri ukielekea chini katika mto uliojaa mamba? Je! umepata kufurahia kuimba mkiwa kikundi katika usiku unaongazwa na mwezi, mkiwa mamia ya kilometa kutoka kwenye makazi ya watu? Je! umepata kushiriki katika mikutano ya Kikristo huku gari likienda kwa mwendo wa kilometa 100 kwa saa? Maono kama hayo ni baadhi tu ya maono yaliyofurahiwa na mamia ya wajumbe kutoka sehemu mbalimbali waliosafiri kwa basi kwenda mkusanyiko wa wilaya wa Mashahidi wa Yehova katika Alice Springs iliyo katika ukavu wa katikati ya Australia.
“Neno ‘safari’ lilifaa,” akasema mjumbe mmoja, “kwa sababu tulilala nje katika mahema ya watu wawili-wawili. Kufikia wakati tulipowasili Alice Springs, tungeweza kusimamisha mahema yetu kwa muda unaopungua dakika tatu! Ilikuwa kama kutazama vidio yenye mwendo wa kasi sana: Mabasi yangesimama, na bustani tupu ingejazwa kwa ghafula na makumi ya mahema madogo-madogo.”
Karibu Kwenye “The Alice”
Alice Springs (wenyeji wanaiita “The Alice”) ni oasisi (eneo lenye maji jangwani) inayozungukwa na jangwa nyekundu. Ina idadi ya watu 23,000 na ipo kusini tu mwa sehemu ya katikati kabisa ya bara la Australia. Sasa ni mahali pa watalii panapokazia sana Waborijini ambao ni wenyeji wa awali wa Australia na sanaa yao aina ya pekee.
Hata hivyo, kwa Mashahidi, jambo kuu la safari hiyo yote lilikuwa ni mkusanyiko wa siku tatu wenyewe. Kwa baadhi yao, ilikuwa ni fursa yenye shangwe ya kukutana tena na wengine. Kikombe cha chai moto ni mojapo njia za kuonyesha ukaribishaji katika eneo hilo la mbali la Australia, na mkusanyiko uliendeleza desturi hiyo kwa kuandaa hema la viburudisho vya chai moto ya billy na aina fulani ya mkate. Chai ya billy ni chai tu inayochemshwa juu ya moto wazi wa nje katika birika inayoitwa billy ambayo huwa nyeusi kwa sababu ya moshi. Nyakati nyingine maji yanayochemka hukorogwa kwa kitawi cha mti eucalyptus, au kwa jina jingine mti gamu, wakati majani ya chai yanapowekwa ndani ya birika hiyo. Kitawi hicho kikiwekwa juu ya birika hiyo kinazuia moshi usiingie ndani ya chai.
Mkate ule ni aina fulani ya mkate sahili. Vitu vinavyohitajiwa pekee ni unga uliotiwa chachu pamoja na maji na chumvi. Ukiwa ungali moto, mkate huo unakatwa-katwa vipande vikubwa na kisha unapakwa siagi nyingi na shira (asali-bandia). Hema hilo la chai moto na mkate ilikuwa mojapo sehemu zilizopendwa zaidi na watu katika mahali pa mkusanyiko.
Kutumikia kwa Uaminifu Katika Upweke
Kundi la Alice Springs lina Mashahidi 72 na linashughulikia eneo la kilometa za mraba 200,000. Darwin ni karibu kilometa 1,800 kuelekea kaskazini, na Adelaide ni karibu kilometa 1,600 kuelekea kusini. Wajumbe waliozuru waliweza kujionea wenyewe jinsi kuishi katika eneo hilo la mbali ni jambo gumu kwa sababu ya umbali, joto la kudumu, mavumbi, na upweke.
Mfano mmoja unaotokeza ni mji wa Jabiru ambao una migodi ya urani. Kuna Shahidi mmoja tu anayeishi hapo, na yuko umbali wa kilometa 260 kutoka kundi lililo karibu zaidi. Na bado, upweke wake haujadhoofisha hali yake ya kiroho. Kuwapo kwake kwenye mkusanyiko kulikuwa kitia-moyo kwa wengine wengi. Pia, wanafunzi wa Biblia wanne walisafiri kutoka makazi ya mbali ya Waborijini ya Jilkmingan, katika ukingo wa Arnhem Land katika Eneo la Kaskazini nao walikuwa miongoni mwa wale 26 waliobatizwa katika mkusanyiko huo.
Wajumbe Waangaza Nuru Yao
Baada ya mkusanyiko, mabasi yote yalielekea kaskazini hadi sehemu ya juu kabisa ya bara la Australia. Jambo kuu la mkondo huu wa safari lilikuwa ni kuabiri kwa meli ndogo kwenda sehemu za juu kwenye maji safi ya Bonde la Katherine tukielekea Mbuga ya Kitaifa ya Kakadu inayojulikana sana. Hiyo iliwawezesha wasafiri waone kwa mara ya kwanza mamba wakiwa porini. Yapendeza, lakini yaogopesha kidogo! Kisha, baada ya usiku mzuri katika jiji kuu la Eneo la Kaskazini, Darwin, kituo kilichofuata cha safari hiyo kilikuwa Kituo cha Mataranka, ambacho kinajulikana sana kwa chemchemi zacho na vidimbwi vyacho vyenye maji safi yaliyo moto na ambavyo vimezingirwa na michikichi.
Hata hivyo, kuona vitu hakukuondolea mbali utendaji wa kiroho. Mabasi hayo yakawa Majumba ya Ufalme yenye kusonga. Andiko la Biblia na maelezo yaliyochapishwa yalizungumziwa kila siku, na mikutano ya kawaida ya kila juma ilifanywa mwendoni. Mmoja wa madereva wa mabasi hayo ambaye hakuwa Shahidi alivutiwa sana hivi kwamba, kwa nia yake mwenyewe, akanunua kamba ndefu ya umeme, kikuza sauti, na plagi za kuunganisha mfumo wa kuhutubia wa basi ili wale waliotoa maelezo wakati wa mazungumzo hayo wasikilizwe vizuri zaidi.
Wakati wa safari hiyo, msafiri mmoja mzee-mzee akawa mgonjwa sana hivi kwamba akahitaji kukimbizwa kwenye hospitali ya karibu. Rafiki mmoja alibaki naye, lakini mabasi yalilazimika kuendelea na safari. Siku mbili baadaye, baada ya kupata nafuu, yeye na mwandamani wake walihuzunika na kuvunjika moyo kwa kukosa sehemu iliyobaki ya safari. Lakini upendo wa Kikristo ulipunguza muda wa huzuni yao.
Mashahidi wawili wa huko ambao walikuwa marubani walisikia juu ya hali hiyo. Kisha mambo yakatendeka kwa kasi. Upesi wote wanne walikuwa angani katika ndege ndogo, wakielekea mji wa Port Augusta ili wafikie mabasi hayo. Mmoja wa wasafiri hao alisema kwa hisia moyo nyingi: “Tulijawa na upendo na uthamini kwa ajili ya udugu wa ajabu tuliokuwa sehemu yao!” Lakini mambo hayakuishia hapo. Ndege ilipofika, wajumbe wenzi zaidi ya kumi walijitolea kutoa michango ya kifedha ya kugharamia marubani hao! Dereva wa basi alivutiwa sana na wonyesho huo wa upendo wa kidugu, akisema kwamba hajapata kuona wonyesho kama huo kamwe.
“Nikifikiria majuma hayo matatu ya safari ya Alice Springs,” akasema mmoja wa wasafiri, “Ninaona ono hilo kuwa lenye kutia moyo sana na lenye kutia imani zaidi ambalo nimepata kuwa nalo. Jambo linalotokeza sana juu ya mengine yote ni roho ya umoja ambayo sisi sote tulifurahia. Haidhuru tungeenda wapi—hazina ya kweli ilikuwa muungano wetu wa akili na roho!”
[Ramani katika ukurasa wa 18]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Njia za safari hiyo kuelekea na kutoka mkusanyiko wa Alice Springs
Australia Magharibi
Eneo la Kaskazini
Queensland
New South Wales
Australia Kusini
Victoria
Tasmania
Darwin
Perth
Alice Springs
Brisbane
Sydney
Adelaide
Melbourne
Hobart
Uluru (Mwamba wa Ayers)
Port Augusta
Mbuga ya Kitaifa ya Kakadu
[Picha katika ukurasa wa 16, 17]
Waborijini walikuwa miongoni mwa wale waliongojea ubatizo kwenye mkusanyiko wa wilaya katika the Alice Springs
[Picha katika ukurasa wa 17]
Moto wa kambi pamoja na chai ya “billy” na mkate
[Picha katika ukurasa wa 17]
Mamba akiota jua katika Mbuga ya Kitaifa ya Kakadu
[Picha katika ukurasa wa 18]
Uluru (Mwamba wa Ayers) kilometa 470 kusini-magharibi mwa Alice Springs
Mandhari ya kawaida katika Mbuga ya Kitaifa ya Kakadu katika Eneo la Kaskazini