Mahali Ambako Ng’ombe Hupuruka
PEPO kali za Visiwa Shetland zilikuja kujulikana ulimwenguni mnamo Januari 5, 1993. Zilichukua Braer, meli kubwa ya mafuta yenye urefu wa meta 243, na uzito wa tani 45,000, na kuigongesha kwenye sehemu hii ya mbali yenye miamba iliyo katika kaskazini mwa Skotlandi. Kwa juma moja tu upepo na mawimbi ya bahari yalikuwa yamevunja hiyo meli kubwa vipande-vipande.
Dhoruba za upepo mkali si jambo jipya kwa wakazi wa Shetland. Kile kikundi chenye karibu visiwa 100 vya mbali, ambavyo visiwa vinavyopungua 20 vinakaliwa, ndivyo hupatwa kwanza na dhoruba zenye baridi zinazokuja bila kuzuiwa kutoka ng’ambo ya bahari karibu na Aislandi.
Haishangazi kwamba wakazi wamezoea kuona mambo ya ajabu. Mtu mmoja aliyenukuliwa katika The Wall Street Journal, alisema hivi: “Labda kunapasa kuwe na ishara [za barabara] katika Shetland: Utahadhari kwa ng’ombe wanaopuruka.” Ng’ombe wa mtu mmoja anayemjua alikuwa amepeperushwa nje ya malisho miaka michache iliyopita. Mkazi mwingine, mwanasayansi, aliripoti kwamba aliona paka kipenzi chake “akipuruka” kufikia meta 5 katika upepo—bila shaka akianguka kwa miguu yake kila wakati. Madereva kwa kawaida hupakia magari vitu vizito, kama vile makaa-mawe, ili yasipeperushwe kutoka barabarani. Watu vilevile wamepata kupeperushwa hewani, wengine hata kuuawa. Upepo mmoja mkali, ulioua mwanamke mmoja, ulifikia mwendo usiothibitishwa rasmi wa kilometa 323 kwa saa—usiothibitishwa rasmi kwa sababu kipima nguvu ya upepo kilichotumiwa rasmi kilipeperushwa katika dhoruba iyo hiyo!