Sura ya 14
Nguvu Juu ya Upepo na Mawimbi
UMEPATA kuwa katika dhoruba wakati upepo ulipokuwa ukivuma vikali sana?— Uliogopa?— Wakati kama huo ni vizuri kuangalia. Maana ungeweza kuumizwa na dhoruba mbaya.
Basi wakati upepo unaanza kuvuma vikali imekupasa ufanye nini, au unapoona umeme ukimeta-meta kutoka angani? Unaonaje? Jambo la hekima kufanya ni kuingia nyumbani. Usipoingia, upepo ungeweza kuangusha tawi la mti juu yako. Au umeme ungeweza kukupiga. Mamia ya watu wanauawa kila mwaka katika dhoruba.
Wewe na mimi hatuwezi kuzuia pepo zenye nguvu zisivume. Na hatuwezi kutuliza mawimbi makubwa ya bahari. Kweli, hapana mwanadamu aliye hai awezaye kufanya hili. Lakini ulijua kwamba mtu fulani aliishi duniani wakati mmoja aliyekuwa na nguvu juu ya upepo na mawimbi? Alikuwa Yesu, Mwalimu Mkuu. Ungependa kusikia aliyofanya?—
Siku moja jioni akiisha kufundisha karibu na Bahari ya Galilaya, aliwaambia wanafunzi wake hivi: “Na tuvuke mpaka ng’ambo.” Basi wakaingia katika chombo wakaanza kutweka matanga kuvuka ziwa.
Yesu alichoka sana. Mchana kutwa alikuwa amefanya kazi sana. Basi akaenda upande wa nyuma wa chombo akalala juu ya mto. Mara akapata usingizi mwingi.
Wanafunzi walikesha ili waongoze chombo. Kwa kitambo kila kitu kilikuwa sawa, lakini ndipo upepo wenye nguvu ukatokea. Ukavuma kwa nguvu zaidi, nayo mawimbi yakazidi kuwa makubwa zaidi. Mawimbi yalianza kuingia chomboni, nacho chombo kikaanza kujaa maji. Wanafunzi waliogopa kuzama.
Lakini Yesu hakuogopa. Alikuwa bado usingizini upande wa nyuma wa chombo. Mwisho, wanafunzi wakamwamsha, na kusema: ‘Mwalimu, Mwalimu, tuokoe; tu karibu kufa katika dhoruba hii.’
Hapo, Yesu akaamka akasema kwa upepo na mawimbi. “Nyamaza, utulie.” Mara hiyo upepo ukatulia. Ziwa likawa shwari.
Wanafunzi walishangaa. Walikuwa hawajaona jambo lo tote mfano wa hili. Wakaanza kusemezana: “Ni nani huyu basi hata anaamuru upepo na maji, navyo vyamtii?”—Marko 4:35-41; Luka 8:22-25.
Unajua Yesu ni nani?— Unajua anapata wapi nguvu yake kubwa? Isingaliwapasa wanafunzi waogope wakati Yesu alipokuwa nao, kwa sababu Yesu hakuwa mtu wa vivi hivi. Aliweza kufanya maajabu ambayo hapana mtu aliyeweza kufanya. Acha nikuambie juu ya jambo jingine ambapo alifanya siku moja juu ya bahari yenye dhoruba.
Ulikuwa wakati fulani uliofuata, siku nyingine. Ilipokuwa jioni Yesu aliwaambia wanafunzi wake waingie chomboni wamtangulie ng’ambo. Ndipo Yesu alipopanda mlimani akiwa peke yake. Palikuwa mahali pa kimya ambapo aliweza kusali kwa Baba yake, Yehova Mungu.
Wanafunzi wakaingia chomboni, wakaanza kutweka matanga kuvuka bahari. Lakini mara ukaanza upepo kuvuma. Ulivuma vikali zaidi. Sasa ulikuwa usiku.
Wanaume wakashusha matanga wakaanza kupiga makasia. Lakini wapi, kwa sababu upepo wenye nguvu ulikuwa ukiwapiga. Chombo kikaanza kwenda mrama katika mawimbi makuu, na yakiingia ndani. Wanaume wakafanya bidii kujaribu kufika pwani, lakini wapi.
Yesu alikuwa bado yuko peke yake mlimani. Alikuwa amekwenda huko kwa muda mrefu. Lakini sasa aliweza kuona kwamba wanafunzi wake walikuwa hatarini katika mawimbi makuu. Basi akatelemka toka mlimani mpaka kwenye ukingo wa bahari. Hakujitumbukiza majini na kuanza kuogelea, na hakutembea kwa miguu majini. Hapana, bali Yesu alianza kutembea juu ya bahari yenye dhoruba kama vile tungetembea juu ya majani mabichi.
Ingekuwaje ikiwa ungejaribu kutembea juu ya maji? Unajua?— Ungezama, na pengine kufa maji. Lakini Yesu alikuwa tofauti. Alikuwa na nguvu za pekee.
Yesu alitembea mwendo mrefu wapata maili tatu au nne kufika kwenye chombo. Hivyo ilikuwa wakati wa mapambazuko wakati wanafunzi walipomwona Yesu akija kwao juu ya maji. Lakini hawakuweza kuamini walichoona. Waliogofishwa sana, wakapiga yowe kwa woga.
Ndipo Yesu akasema kwao: “Jipeni moyo; ni mimi; msiogope.”
Mara Yesu alipoingia chomboni, upepo ukatulia. Tena wanafunzi walishangaa. Wakamsujudia Yesu, wakasema: “Hakika wewe u Mwana wa Mungu.”—Mathayo 14:23-33; Yohana 6:16-21.
Je! isingalikuwa vizuri sana kuishi wakati huo na kumwona Yesu akifanya mambo kama hayo?— Basi, tunaweza kuishi wakati Yesu atakapofanya mambo yaliyo ya ajabu sana.
Biblia inasema Mungu alimfanya Yesu Mtawala katika ufalme wa Mungu, na karibuni serikali yake peke yake ndiyo itatawala dunia hii. Hapana mtu atakayeishi wakati huo atakayeogopa dhoruba. Yesu atatumia nguvu yake juu ya upepo na mawimbi kwa baraka ya wote wanaomtii. Je! huo hautakuwa wakati mzuri sana kuishi ndani yake?—
(Maandiko mengine kuonyesha nguvu kuu ya Yesu kama ambaye Mungu anafanya Mtawala katika ufalme wa Mungu ni: Mathayo 28:18; Danieli 7:13, 14; Waefeso 1:20-22.)