Sura 53
Mtawala Anayetamaniwa Mwenye Nguvu Zipitazo za Kibinadamu
WAKATI Yesu anapolisha maelfu kwa muujiza, watu wanastaajabu. “Hakika huyu ndiye nabii ambaye alikuwa aje ulimwenguni,” wao wanasema. Wanakata shauri si kwamba tu Yesu lazima awe ndiye nabii aliye mkuu kuliko Musa bali pia yeye angeweza kuwa mtawala wa kutamanika sana. Kwa hiyo, wanafanya mpango wamkamate na kumfanya mfalme.
Hata hivyo, Yesu anajua jambo ambalo watu hao wanapangia. Kwa hiyo anafanya haraka aepuke kuingizwa kwa nguvu katika cheo hicho. Yeye auaga umati huo na kulazimisha wanafunzi wake waingie katika mashua yao warudi kuelekea Kapernaumu. Kisha yeye anaingia mlimani peke yake ili kusali. Usiku huo Yesu anakuwa pale yeye peke yake kabisa.
Muda mfupi kabla ya mapambazuko Yesu anatazama kule nje akiwa mahali hapo palipoinuka na kuona mawimbi yakichafuliwa katika bahari na upepo wenye nguvu. Kwa mwangaza wa mwezi unaokaribia kuwa mpevu, kwa kuwa Sikukuu ya Kupitwa inakaribia, Yesu aiona mashua huku wanafunzi wake wakijitahidi sana kusonga mbele dhidi ya mawimbi yale. Wanaume hao wanapiga makasia kwa nguvu zao zote.
Kuona hivyo, Yesu anashuka mlimani na kuanza kutembea kuielekea mashua akipita juu ya mawimbi. Mashua imeenda umbali wa maili karibu tatu au nne hivi anapoifikia. Hata hivyo, yeye anaendelea mbele tu kana kwamba ataipita. Wanafunzi wanapomwona, wanapaaza sauti: “Ni mzuka!”
Kwa kufariji Yesu aitikia hivi: “Ni mimi; msiwe na woga.”
Lakini Petro anasema: “Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru mimi nikujie wewe juu ya maji haya.”
“Njoo!” Yesu anajibu.
Papo hapo, Petro anatoka mashuani, anatembea juu ya maji kumwelekea Yesu. Lakini anapotazama dhoruba ya upepo, Petro anaingiwa na woga, na anapoanza kuzama, anapaaza sauti hivi: “Bwana, niokoe!”
Akinyoosha mkono wake bila kukawia Yesu anamshika, akisema: “Wewe uliye na imani haba, mbona wewe umeliachia shaka nafasi?”
Baada ya Petro na Yesu kurudi ndani ya mashua, upepo ule unaacha kuvuma, na wanafunzi wanastaajabu. Lakini je! inawapasa kufanya hivyo? Kama wao wangaliifahamu “maana ya mikate ile” kwa kuthamini ule muujiza mkubwa ambao Yesu alifanya saa chache kabla ya hapo alipolisha maelfu kwa mikate mitano tu na samaki wawili wadogo, basi lisingalipasa kuonekana kana kwamba ni jambo la kustaajabisha sana kwamba yeye angeweza kutembea juu ya maji na kufanya upepo utulie. Hata hivyo, sasa wanafunzi wanamsujudia Yesu na kusema: “Kweli kweli wewe ni Mwana wa Mungu.”
Baada ya muda mfupi, wanafika Genesareti, uwanda wenye kupendeza wenye kutoa sana mazao ulio karibu na Kapernaumu. Hapo wanatia mashua nanga. Lakini wanapoenda pwani, watu wanamtambua Yesu na kwenda katika nchi yote inayozunguka eneo hilo, wakitafuta wale walio wagonjwa. Wanapoletwa wakiwa katika machela zao na kugusa tu upindo wa vazi la nje la Yesu, wanaponywa kabisa.
Wakati ule ule, umati ule ulioona ushahidi wa maelfu wakilishwa kimuujiza unagundua kwamba Yesu ameondoka. Kwa hiyo wakati mashua ndogo-ndogo zinapowasili kutoka Tiberia, wanazipanda na kutweka nanga kwenda Kapernaumu wakamtafute Yesu. Wanapompata, wanamuuliza: “Rabi, wewe ulifika hapa lini?” Yesu anawakemea kama vile tutakavyoona upesi. Yohana 6:14-25; Mathayo 14:22-36; Marko 6:45-56, NW.
▪ Baada ya Yesu kulisha maelfu kwa muujiza, watu wanataka kumfanya nini?
▪ Yesu anaona nini akiwa katika mlima ambako yeye amejitenga awe peke yake, naye ndipo anafanya nini?
▪ Kwa nini wanafunzi hawapaswi kustaajabu kuona mambo hayo?
▪ Kunatukia nini wafikapo ufuoni?