Hisi Yetu ya Kunusa Inayobadilika-Badilika
HUCHOCHEA KUMBUKUMBU, HUONGEZA LADHA
NI HARUFU gani nzuri uipendayo? Swali hilo lilipoulizwa watu kadhaa, majibu yao yalikuwa yenye kusisimua. Bekoni inayokaangwa. Hewa ya chumvi ya bahari. Nguo zilizofuliwa zinazopepea kwenye upepo. Nyasi mbichi zilizokatwa. Viungo vikali vya chakula. Pumzi ya mbwa mdogo. Walipohojiwa zaidi ni kwa nini hizi zilikuwa harufu wazipendazo, wote walikuwa na sababu hususa, na kumbukumbu dhahiri walizokumbuka waliponusa harufu hizo nzuri mara ya kwanza. Mara nyingi kumbukumbu hizo zilikuwa za tangu utotoni.
Mwanamke mmoja akumbuka akilala kitandani mwake asubuhi, harufu nzuri ya bekoni iliyokuwa ikikaangwa ilipitia chumbani mwake, ikimwamsha aje kwenye kiamsha-kinywa na familia yake.
Louise, mwenye umri wa miaka 58, alisema kwamba harufu ya bahari humletea kumbukumbu za utotoni za wakati wa kiangazi kwenye pwani mwa Maine huko United States. “Uhuru tuliokuwa nao,” anasema, “tukikimbia na kucheza kwenye changarawe, tukitafuta samaki wa koa na kuzipika kwenye moto wa nje!”
Michele, mwenye umri wa miaka 72, akumbuka wakati alipokuwa mtoto akimsaidia mama yake kuanua nguo kutoka kwenye kamba ya nguo, akifunika uso wake na nguo alizobeba akizipeleka kwenye nyumba, huku akivuta ndani manukato safi, yenye kupendeza.
Harufu ya nyasi mabichi zilizokatwa zamkumbusha Jeremy miaka 55 iliyopita, siku za utoto wake katika shamba la Iowa, U.S.A., akiwa kwenye lori la kubeba nyasi mbichi zilizokatwa zikipelekwa kwenye ghala ili kuepuka mvua ambayo yeye na baba yake walihisi ikinukia kwa mbali.
“Viungo vikali vya chakula” lilikuwa itikio la Jessie mwenye umri wa miaka 76, ambaye alifunga macho yake na kusema juu ya familia yake iliyokuwa ikipika siagi ya tofaa (aina ya jamu yenye viungo vya chakula vingi inayotengenezwa United States) katika birika la chuma nje ya nyumba. Miaka sabini iliyopita, lakini bado alikuwa akikumbuka hayo.
Carol akumbuka mtoto mdogo wa mbwa aliyekuwa akimpakata pajani alipokuwa na umri wa miaka mitano na akumbuka harufu ya pumzi ya mbwa huyo mdogo. Aha, naam, harufu hiyo humpa hisia za joto chini ya jua kwenye ukumbi wa mbele akiwa amevaa nguo nyepesi.
Sasa, namna gani wewe? Je! harufu yoyote imewahi kukupendeza kama ilivyowapendeza wengine—zikiamsha kumbukumbu zako, zikichochea hisia zako? Je! umewahi kuburudishwa na mlima uliojawa na manukato ya msonobari au kuburudishwa na manukato ya upepo mzuri wa bahari? Au labda umejipata ukidondokwa mate kwa sababu ya kutamani chakula baada ya kunusa harufu nzuri katika duka la kuokea mikate. Mwanasayansi wa neva Gordon Shepherd alisema katika National Geographic: “Tunafikiri maisha zetu zimetawalwa na hisi yetu ya kuona, lakini kadiri wakati wa mlo wa usiku unavyokaribia, ndivyo unavyotambua zaidi jinsi hisi yako ya kunusa ilivyo yenye kupendeza maishani.”
Harufu ina athari ya ajabu kwa hisi yetu ya ladha. Huku tezi za ladha zikitofautisha ladha ya chumvi, kitu kitamu, chungu, na chachu, hisi yetu ya kunusa hupokea harufu nyinginezo ndogo-ndogo. Ikiwa tofaa na vitunguu vingekosa harufu, vingeweza kuwa na ladha sawa. Au, kwa mfano, ona jinsi kipande cha chokoleti kinavyopoteza ladha unapokila ukiziba pua yako.
Hebu weka akilini chakula chenye kuleta hamu—acha tuseme keki tamu. Harufu hiyo yenye kuvutia inapeperushwa kutoka kwayo kwa sababu inatoa vipande vidogo vyayo na kuvipeperusha hewani. Kisha unakuja hapo na pua yako yanusia manukato kwa kutamani. Inavuta hewa na kupeleka vipande hivyo kwenye mfumo wetu wa ajabu wa hisi ya kunusa.
Kwa habari zaidi juu ya mfumo wa kunusa, ona sanduku kwenye kurasa 24 na 25. Mambo mengi na utataniko wa hisi hiyo kwa kweli ni ya ajabu.
Harufu na Matokeo Yazo Kwako
Watengeneza manukato, wapishi wakuu, na watengenezaji divai wametambua kwa karne nyingi, uwezo wa harufu kushika akili na kufurahisha hisi. Leo, wanasaikolojia wa harufu na wastadi wa madawa wanajaribu kutumia uwezo wa kunusa katika njia mpya. Wakijaribia na manukato ya lili ya bonde hadi mchanganyiko wa tofaa na viungo vya upishi, wastadi wa harufu wameweka manukato kwenye shule, majengo ya ofisi, makao ya wagonjwa, na hata kwenye gari moshi la chini ya ardhi ili kuchunguza matokeo kwenye akili na tabia ya kibinadamu. Wanadai kwamba manukato fulani yanaweza kuwa na uvutano kwa hisia-moyo, zikiwafanya watu kuwa na urafiki, kuendeleza matokeo yao kazini, na hata kufanya akili yao iwe chonjo.
Kulingana na gazeti The Futurist, watu hupiga mstari kwenye klabu cha afya katika Tokyo, Japani, ili wapate “harufu nzuri ya mvinyo mkali” ya dakika 30 inayosemwa kuwa yenye kuondoa mkazo wa akili wa maisha ya mjini. Wanasayansi Wajapani wamejifunza pia juu ya matokeo ya hewa ya msitu kwa binadamu na wakapendekeza kwamba kutembea kwenye miti ni dawa ya mishipa iliyochoshwa. Harufu ya miti ya msonobari imepatikana kutuliza si mwili tu bali hasa akili.
Si harufu zote ziletazo afya; sivyo kamwe. Kinachomfurahisha mtu mmoja chaweza kumdhuru mwingine. Harufu kali, hata za marashi, zimejulikana kuleta pumu na mzio kwa watu fulani. Kisha, pia, kuna uvundo ambao kila mtu anakubali kwamba unaumiza—moshi wenye kudhuru utokao kwenye mabomba ya viwanda na mabomba ya kuondolea moshi ya magari, uvundo mbaya wa takataka na vidimbwi vya maji machafu, na mivuke kutoka kwa kemikali inayofukizwa inayotumiwa katika viwanda vingi.
Bila shaka kemikali hatari hupatikana kiasili kwenye mazingira yetu lakini hizo huyeyuka hewani hivi kwamba zisidhuru. Hata hivyo, kemikali hizo zinapokuwa nyingi sana, zinaweza kuharibu sana chembe za neva za kupumua. Kwa mfano, viyeyusho kama vile vinavyotumiwa kwenye rangi, pamoja na kemikali nyingine za viwanda, zimeorodheshwa na wataalamu kuwa hatari kwa mfumo wa kunusa. Kuna matatizo mengine ya kimwili ambayo yanaweza kudhoofisha au kuharibu hisi ya kunusa.
Je! Unaithamini Zawadi Hiyo?
Kwa kweli hisi ya kunusa inastahili kulindwa kutokana na vitisho hivyo iwezekanavyo. Kwa hivyo, fahamu hatari za kemikali zozote ambazo unapaswa kufanyia kazi, na uchukue hatua zozote zipaswazo ili kulinda mfumo wako wa kunusa. (Linganisha 2 Wakorintho 7:1.) Kwa upande ule mwingine, itakuwa vizuri kufikiria juu ya hisia za wengine. Usafi wa hali ya juu, kutia ndani nyumba zetu na miili yetu, waweza kusaidia kwa upande huu. Wengine wamechagua pia kuwa waangalifu zaidi na aina ya marashi wanayotumia—hasa wanapopanga kuwa karibu na wengine kwa muda mrefu, kama vile kwenye jumba la michezo au Jumba la Kusanyiko.—Linganisha Mathayo 7:12.
Ingawa hivyo, kwa ujumla, mfumo wa kunusa ni zawadi inayohitaji mambo machache ili kutunzwa. Hutuhitaji kufanya mambo machache katika kuutunza na kuulinda, lakini hutuletea upendezi mwingi kila siku katika maisha. Unapopokea zawadi inayokufurahisha, je, wewe hutamani kumshukuru mpaji? Mamilioni ya watu leo wanamshukuru Muumba kwa moyo wote kwa sababu ya njia ya ajabu ambayo mwili wa kibinadamu umeumbwa. (Linganisha Zaburi 139:14.) Tunaweza kutumaini kwamba shukrani na sifa nyingi zaidi kama hizo zitamwendea yeye na, kama dhabihu za Waisraeli wa kale, ziwe “harufu ipendezayo” kwa Muumba wetu mwenye upendo, na mkarimu.—Hesabu 15:3; Waebrania 13:15.
[Sanduku[Mchoro katika kurasa za 24 and 25]
Jinsi Hisi ya Kunusa Inavyofanya Kazi
Kwanza, Harufu Inatambuliwa
HARUFU huingilia puani unapopumua. Pia, unapomeza chakula, vipande husukumwa nyuma ya mdomo na kuingia kwenye mshipa wa pua. Hata hivyo, ni lazima hewa yenye harufu ipitie kwa “walinzi” kwanza. Neva za hisi hufunika mianzi ya pua (1), ambayo huchochea kupiga chafya zinapohisi kemikali kali au yenye kuwasha-washa. Neva hizi pia huleta upendezi kwa kuitikia harufu kali ya ladha nyinginezo.
Halafu, molekuli ya harufu husukumwa juu na mzunguko wa hewa ambao hutokea wakati mawimbi ya hewa ambayo huzunguka-zunguka upesi kupitia mifupa mitatu, iliyo kama mikunjo iliyobenuka iitwayo tabinate (2). Mkondo wa hewa, ukinyevushwa, na kufanywa joto, huchukua molekuli kwenye epitheliamu (3), mahali pa kwanza pa upokezi. Kikiwa kwenye kijia chembamba juu ya pua, kisehemu hiki kilicho na ukubwa wa ukucha wa kidole-gumba cha tishu kimejawa na karibu milioni kumi za selineva hisishi (4), kila kimoja yacho kikiwa kimejaa vivurumisho kadhaa vilivyo kama nywele, viitwavyo silia, vilivyo kwenye safu nyembamba ya ute. Ndivyo ilivyo na hisi ile epitheliamu ambayo inaweza kugundua miligramu 1/460,000,000 za marashi ya aina fulani katika pumzi moja ya hewa.
Lakini hasa jinsi harufu zinagunduliwa bado ni fumbo. Isitoshe, wanadamu wanaweza kutofautisha harufu 10,000. Na kuna zaidi ya vitu vyenye harufu 400,000 katika mazingira yetu, huku wanakemia wakitengeneza mpya daima. Kwa hiyo pua zetu zaweza kutofautishaje harufu hususa yoyote katika mfululizo wa harufu nyingi? Kwa kufaa, zaidi ya maelezo 20 tofauti yanajaribu kueleza fumbo hilo.
Hivi karibuni tu wanasayansi wamefanya maendeleo kuelekea kutatua sehemu ya fumbo hilo. Udhibitisho fulani ulipatikana 1991 kwamba kuna protini ndogo sana, ziitwazo vipokeza harufu, vilivyofumwa kupitia kiwamboseli katika silia. Kwa wazi vipokezi hivyo hujifunga kitofauti na aina tofauti za molekuli yenye harufu, hivyo vikitoa kila harufu zinavyotofautiana kama “alama za kidole.”
Pili, Harufu Inahamishwa
Ili kupitisha habari hii kwenye ubongo, habari za kielektroni na kemikali hupitishwa katika nuroni (4). Dakt. Lewis Thomas, mwandikaji insha wa sayansi, anaziita nuroni hizi ‘Maajabu ya tano ya ulimwengu wa sasa.’ Hizo ni neva seli ambazo hujirudufisha kila majuma kadhaa. Pia, hazina kizuizi cha ulinzi kati yazo na vichochezi, kama zifanyavyo nevanusishi ambazo hujibanza zikiwa zimelindwa kati ya jicho na sikio. Badala yake, nevanusishi hufikia kutoka kwa ubongo wenyewe na kuja moja kwa moja nje. Hivyo, pua ni mahali pa ubongo na mazingira.
Nuroni hizi zote zinaenda mahali pamoja: tunguu nusishi mbili (5) chini ya ubongo. Tunguu hizi ni vituo vikuu vya sehemu nyingine za ubongo. Ingawa hivyo, kwanza zinatoa habari nyingi ya kunusa, kutoa yote na kubakisha ile ya lazima, na kuipeleka.
Tatu, Harufu Yatambuliwa
Tunguu nusishi “zimefungwa” kwa njia yenye kutatanisha katika mfumo wa ubongo wa kuchochea hisia (6), seti yenye kupendeza ya vitu vilivyojipinda ambavyo huweka kumbukumbu na kutoa itikio la hisia. Hapa ndipo “ulimwengu baridi halisi unabadilishwa kuwa hisia zilizochemshwa za mwanadamu,” kulingana na kitabu The Human Body. Mfumo wa ubongo wa kuchochea hisia umefungana sana na hisi ya kunusa hivi kwamba ulikuwa ukiitwa ubongo-nusishi (rhinencephalon) inayomaanisha “pua ya ubongo.” Ungamanisho hilo la karibu kati ya pua na mfumo wa ubongo wa kuchochea hisia waweza kueleza ni kwa nini sisi huitikia kihisia na kukumbuka harufu zilizopita. Aha! Bekoni inayokaangwa! Nguo safi! Nyasi mbichi zilizokatwa! Pumzi ya mbwa mdogo!
Ikitegemea harufu iliyonuswa, mfumo wa ubongo wa kuchochea hisia huenda ukachochea hipothalasi (7), ambayo nayo yaweza kuelekeza kwenye tezi kuu ya ubongo, ile pitituari (8), kutoa hormoni mbalimbali—kwa mfano, hormoni zinazodhibiti hamu ya kula, au ngono. Basi, si ajabu kwamba harufu ya chakula yaweza kutufanya tuhisi njaa kwa ghafula au ile ya marashi yaweza kuonwa kuwa ya maana katika kuvutia kingono.
Mfumo wa ubongo wa kuchochea hisia pia hufika kwenye koteksi (9), ujirani wenye kuchunguza ubongo, wa akili ya juu. Hapa ndipo habari kutoka puani zaweza kulinganishwa na zinazokuja kutoka kwa hisi nyingine. Kama tokeo, unaweza kuchanganya habari hiyo ya harufu kali, sauti ya mwaliko, na moshi usioonekana vizuri ukining’inia hewani kumalizia kwa—moto!
Thalamasi (10) huwa na sehemu pia, labda kupatanisha kati ya sehemu tofauti kabisa, mfumo wa ubongo wa kuchochea “hisia-moyo” na koteksi ya “akili.” Koteksi nusishi (11) husaidia kutofautisha kati ya harufu zinazofanana. Vituo mbalimbali vya ubongo vyaweza pia kupeleka ujumbe kwenye vituo vya kutoa habari, zile tunguu nusishi. Kwa nini? Ili kwamba tunguu zibadilishe harufu, kisha kuzirudisha chini au kuzizima.
Huenda ikawa umetambua kuwa chakula hakinukii vizuri sana wakati ambapo umeshiba. Au je, umelazimika kunusa uvundo mkali, usioepukika ambao ulielekea kuisha polepole? Tunguu nusishi, zilijulishwa na ubongo, na kufanya mabadiliko hayo. Yanaweza kusaidiwa na seli pokezi kwenye silia ambazo zasemekana kuwa huchoka upesi. Hii ni sehemu yenye kusaidia, hasa unapokabili uvundo mbaya zaidi.
Ni mfumo wenye kutokeza kama nini, sivyo? Hata hivyo, tumegusia jambo hilo kifupi tu! Vitabu vizima vimetolewa kuhusu mfumo huu wenye kutatanisha na wa ajabu.
[Mchoro]
1
2
3
4
5
6
7
8
9
10
11
[Sanduku katika ukurasa wa 26]
Udhaifu wa Kutohisi Harufu
Mamilioni ya watu wana udhaifu wa kutohisi harufu. Manukato ya wakati wa masika au chakula chenye kujaa madoido hakiwavutii sana. Mwanamke mmoja alieleza kupoteza kwake hisi ya kunusa jinsi hii: “Sisi sote twajua juu ya upofu na kuwa kiziwi, na kwa kweli singebadili udhaifu wangu na matatizo hayo. Lakini twachukulia hivi-hivi harufu nzuri ya kahawa na ladha tamu ya machungwa hivi kwamba tukikosa hisi za kunusa na kuonja, ni kana kwamba tumesahau jinsi ya kupumua.”—gazeti Newsweek.
Matatizo ya kunusa yanaweza kuhatarisha maisha. Mwanamke anayeitwa Eva anaeleza: “Kwa kutoweza kunusia, nimekuwa mwangalifu sana. Ninaogopa kufikiri juu ya kipupwe kinapokuja, kwa sababu ni lazima nifunge madirisha yote na milango ya chumba changu. Bila hewa safi, ninaweza kushindwa kwa urahisi na harufu ya gesi ikiwa mwali mdogo unaoendelea kuwaka kwenye jiko ungezima.”
Ni nini ambacho kinasababisha udhaifu wa kutohisi harufu? Kukiwa na sababu nyingi, hizi tatu ni za kawaida: majeraha ya kichwa, ambukizo la virasi kwa mfumo wa juu wa kupumua, na ugonjwa wa kibweta. Ikiwa njia za neva zinaharibiwa, ikiwa epitheliamu inakosa hisi, au ikiwa hewa haiwezi kufikia epitheliamu kwa sababu ya kufungwa au kufura, hisi ya kunusa huisha. Vikitambua matatizo hayo kuwa makubwa, vituo vya kliniki ya uchunguzi wa ladha na kunusa vimeanzishwa.
Katika mahojiano, Dakt. Maxwell Mozell wa Kitovu cha Afya na Sayansi cha Chuo Kikuu cha New York katika Syracuse alieleza: “Tumekuwa na wagonjwa hapa ambao [wananusa uvundo ambao ni wao wenyewe tu wanahisi]. Wanahisi vitu vibaya sana. Mwanamke mmoja alihisi harufu ya samaki wakati wote. Hebu wazia kama kila dakika ya kila siku utahisi harufu ya samaki au mpira unaochomeka tu.” Baada ya kuteseka kwa miaka 11 na uvundo usiopendeza katika pua yake na baadaye mshuko wa moyo, mwanamke mmoja alipata kitulizo cha mara hiyo baada ya moja ya tunguu nusishi kutolewa kwa upasuaji.
[Picha katika ukurasa wa 23]
Pumzi ya mbwa mdogo
Bekoni inayokaangwa
Nyasi mbichi zilizokatwa