Ni Nini Kimepata Maadili?
MAOFISA wa serikali. Wagombea viti vya kisiasa. Viongozi wa kidini. Tunatazamia watu kama hao kuwa vielelezo vya tabia nzuri. Ingawa hivyo, katika nyakati za hivi karibuni, watu wenye vyeo hivyo wamekuwa kwenye mstari wa mbele katika mfululizo wa kashfa zenye kushtusha. Tabia zao mbaya zimewaongoza kwenye maovu yote—kutoka uzinzi na kusema uwongo bila haya hadi mishughuliko isiyo halali ya kifedha na kula fedha za watu.
Kitabu The Death of Ethics in America chaomboleza hivi: “Huku mataifa yakishughulika na ule ugonjwa hatari . . . Ukosefu wa Kinga Mwilini, aina nyingine ya [Ukosefu wa Ushikamanifu Mwilini], unaonekana kuwa umeenea sana. Lakini bado haujatoa maombi mengi ya haraka ili utibiwe.” (Italiki ni zetu.) Gazeti Time ladai kwamba United States “inagaagaa katika tope la kiadili.”
Tope hilo la ufisadi wa kiadili halipatikani katika United States pekee. Katika nyakati za hivi karibuni India, Indonesia, Israeli, Japani, Uchina, Ufaransa, Ugiriki, na Ujerumani zimepatwa na kashfa zenye kuhusu watu mashuhuri. Na kwa hiyo isishangaze kwamba tabia zisizo za kiadili za viongozi wa jamii zinaonyesha tu ile tabia ya umma kwa ujumla. Waziri mkuu wa Thailand aliuita ufisadi katika nchi yake ‘ugonjwa usioweza kuponywa.’ Aliongezea kwamba jamii yote inaugua ugonjwa unaotokana na pupa na tabia za kijamii zilizoharibika.
Kwa kufaa watu hujiuliza: ‘Ni nini kinachosababisha kupotea huko kwa maadili duniani pote? Na la maana zaidi, maadili yanaelekea wapi?’
Wakati ‘Kuiba si Kuiba’
Katika Columbus, Ohio, U.S.A., mlango wa nyuma wa kilori cha ulinzi ulifunguka wazi, na mifuko miwili mikubwa ya fedha ikaanguka nje. Huku fedha zinazokadiriwa kuwa dola milioni mbili zilipokuwa zikipeperushwa na upepo na kutawanyika kwenye barabara kuu, makumi ya madereva walitoka mbio kwenye magari yao ili wajaze mifuko yao ya mavazi na mikoba yao kwa manoti. Madereva wengine waliwaita wengine kupitia redio za CB ili waungane nao katika wizi huo.
Sihi za serikali na zawadi ya asilimia 10 zilizotolewa kwa wale ambao wangerudisha angalau kiasi fulani cha fedha zilipuuzwa. Watu wengi waliona kwamba fedha hizo ni zao “kwa sababu waliziokota.” Ni kiasi kidogo sana cha fedha hizo kilichokuja kupatikana. Mtu mmoja hata alitetea wizi wake kwa kusema kwamba fedha hizo zilikuwa “zawadi kutoka kwa Mungu.” Ingawa hivyo, visa kama hivyo ni vingi. Wapita-njia walionyesha pupa ya aina iyo hiyo wakati fedha zilipomwagika kutoka kwenye magari yenye ulinzi katika San Francisco, Kalifornia, na katika Toronto, Kanada.
Jambo la kwamba watu ambao kwa kawaida ni wenye kufuatia haki na wanyoofu hushusha viwango vyao vya kawaida na kuiba linahangaisha. Angalau linaonyesha jinsi ambavyo ufafanuzi wa maadili unaojulikana na wengi umepotoshwa. Thomas Pogge, ambaye ni profesa msaidizi wa falsafa katika Chuo Kikuu cha Columbia katika New York, atoa hoja kwamba ingawa watu wengi huona kuwa ni vibaya kumwibia mtu, kwa njia fulani wao huona kuibia shirika si jambo baya sana.
Maadili ya Kingono Yanapotea
Mtazamo usiofaa wa maadili unaonekana katika utendaji wa kingono pia. Uchunguzi wa hivi karibuni ulionyesha kwamba kwa kushangaza wale wanaofanya uzinzi ndio watu ambao hukubaliwa kuwa wagombea vyeo vya kisiasa. Mwandikaji mmoja anapendekeza kwamba wapiga kura kama hao hawawezi kushutumu uzinzi mara moja kwa sababu wao wenyewe ‘wanajitahidi sana kufanya uzinzi.’
Kwa kweli, takwimu za hivi karibuni zafunua kwamba asilimia 31 ya watu wote waliooa na kuolewa katika United States wamepata kuwa na au kwa wakati huu wanaendelea kuwa na ngono nje ya ndoa. Waamerika wengi zaidi, asilimia 62, “hufikiri kwamba hakuna ubaya wowote wa kiadili” katika kufanya uzinzi. Maoni kuelekea ngono ya kabla ya ndoa pia ni ya uendekezaji vivyo hivyo. Uchunguzi mmoja katika 1969 ulionyesha kwamba wakati huo asilimia 68 ya Waamerika walipinga ngono ya kabla ya ndoa. Leo, ni asilimia 36 pekee wanaopinga. Katika miaka ya 1960, karibu nusu ya wanawake waliohojiwa walikuwa mabikira kufikia siku yao ya arusi. Leo, ni asilimia 20 tu ambao ni mabikira.
Ni Mambo Yapi Yaliyo ya Adili?
Kupotea kwa maadili kunaonekana pia katika biashara. Miongo miwili iliyopita, ni asilimia 39 tu ya wanafunzi waliotoka tu kuingia katika vyuo waliohojiwa ambao walifikiri kwamba “ufanisi wa kifedha ulikuwa wa umaana au wa muhimu.” Kufikia 1989 idadi hiyo iliongezeka maradufu kihalisi. Kwa wazi, vijana wengi hufikiria sana kupata fedha—kukiwa na matokeo mabaya sana ya kiadili.
Wakati wanafunzi wa sekondari 1,093 wa vidato vya juu walipohojiwa, asilimia 59 walisema kwamba wangekubali kushiriki katika shughuli ya kibiashara isiyo halali inayoweza kutokeza dola milioni kumi—hata kama watapata kifungo cha nje ya jela cha miezi sita! Na zaidi, asilimia 67 walisema kwamba wangeandika kwa njia yenye kudanganya kiasi cha fedha za akiba ya matumizi ya biashara; asilimia 66 walisema kwamba wangesema uwongo ili watimize miradi yao ya kibiashara. Hata hivyo, vijana wanafuata tu mwenendo wa kiadili uliowekwa na watu wazima. Wakati mameneja wa biashara 671 walipoombwa watoe maoni yao juu ya adili ya kazi, karibu robo yao walibisha kwamba adili nzuri inaweza kuzuia utafutaji wao wa kazi-maisha yenye mafanikio. Zaidi ya nusu wao walikiri kwamba walivunja sheria ili waweze kufanikiwa.
Vikijaribu kukomesha mwenendo huo wenye kusumbua, vyuo fulani hufundisha masomo ya adili. Lakini wengi wanatilia shaka kama jitihada hizo zinaweza kufaulu. “Sioni jinsi masomo ya adili yatakavyosaidia,” akasema mfanya biashara mmoja mashuhuri wa Kanada. “Wanafunzi wenye tabia nzuri hawatajifunza mambo mengi mapya, na wanafunzi ambao hata si washikamanifu wanaweza tu kutumia mambo mapya wanayojifunza katika kutafuta njia nyinginezo za kufanya matendo mengine yasiyo ya adili ambayo bila shaka wanaenda kufanya.”
Vivyo hivyo, mashirika mengi ya kibiashara yamefanyiza sheria rasmi za adili za kufuatwa. Hata hivyo, wataalam wanadai kwamba sheria kama hizo huwekwa tu na kwa kawaida hazifikiriwi sana—ila tu baada ya kashfa yenye kudhuru. Kwa kushangaza, uchunguzi wa hivi karibuni ulifunua kwamba mashirika ya kibiashara yenye sheria rasmi za adili zilizoandikwa yalikuwa na hatia ya tabia isiyo ya adili mara nyingi kuliko mashirika ya biashara ambayo hayakuwa na sheria zilizoandikwa!
Naam, kwa wazi maadili yanapotea katika pande zote za utendaji, na hakuna mtu yeyote anayeonekana anatambua yanaelekea wapi. Mkuu mmoja wa kibiashara asema hivi: “Zile ishara zilizotuonyesha mema na mabaya haziko tena. Polepole zimeharibiwa.” Ni kwa nini ishara kama hizo zimepotea? Ni nini kinachochukua mahali pazo? Masuala hayo yatachunguzwa katika makala zinazofuata.