Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g93 9/22 kur. 24-27
  • Vipandaji vya Kifumbo vya Pepo za Kimbingu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Vipandaji vya Kifumbo vya Pepo za Kimbingu
  • Amkeni!—1993
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Tunaweza Kuziona Wapi, na Zinafananaje?
  • Je! Waweza Kweli Kuzisikia?
  • Uvutio Wenye Kudumu
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—2010
  • Sayari Yenye Uhai Tele
    Uhai—Ulitokana na Muumba?
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—1994
  • Safari ya Kupendeza Sana Baharini
    Amkeni!—2003
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1993
g93 9/22 kur. 24-27

Vipandaji vya Kifumbo vya Pepo za Kimbingu

“Ni nani ila Mungu awezaye kutunga mandhari hizo zisizo na mwisho zenye utukufu hivyo? Ni nani ila Mungu awezaye kuzitokeza, akipaka mbingu rangi kwa wonyesho mzuri ajabu?”

NI NINI kilichoamsha hisi hiyo ya kumcha Mungu ndani ya Charles F. Hall, mvumbua Aktiki wa karne ya 19? Ni mmoja wa utendaji wa kiajabu wa asili unaoonekana kwa macho ya kibinadamu, aurora borealis—unaoitwa kwa kawaida nuru za kaskazini.

Uvutio kwa nuru hizo za kimbingu waenda nyuma mpaka karne ya nne K.W.K., wakati ambapo mwanafalsafa Mgiriki Aristotle alipoandika nadharia yake juu ya tukio hilo la ajabu. Hata hivyo, haikuwa mpaka 1621, kwamba mwanasayansi na mwanahisabati Mfaransa Pierre Gassendi alianzisha mtajo “aurora borealis” (au, pambazuko la kaskazini) kama tunavyoyatumia sasa. Aurora lilikuwa jina la kijimungu-kike cha mapambazuko cha Waroma chenye kidole cha rangi ya waridi katika ngano za kale. Alikuwa pia mama ya upepo, upepo wa kaskazi ukiitwa Boreas.

Ni nini husababisha aurora? Je! inawezekana kwamba hiyo husababishwa na miale ya jua inayoangaza kutoka kwenye vipande vidogo vya barafu angani? Au kuangazwa kwa nuru ya jua kutoka kwenye vilima vya barafu? Au milipuko inayotokezwa na mgongano wa hewa joto na hewa baridi? Hakuna mmo-ja wa utendaji huo unaoisababisha. Uchunguzi wa hali ya juu wa kisayansi wahusianisha utendaji huo wa kiajabu kati ya utendaji wa moja kwa moja wa jua na uvutano wa nguvu za ugasumaku wa dunia.

Aurora yenye ajabu huanza umbali wa kilometa milioni 150, kwenye kiini cha mfumo wetu wa jua. Milipuko ya kinyukilia ambayo hutokea kwenye jua na ndani ya jua hurusha gesi nyingi sana katika anga kwa mwendo unaokadiriwa na wengine kufikia kilometa 4,000,000 kwa saa. Pepo hizo za jua zenye nguvu, zikibeba mikondo ya vipande vyenye kani nyingi, zaweza kufika katika anga la nje ya dunia kwa muda wa saa 24 hadi 48. Zinapoingia katika sehemu za nje za uvutano wa kisumaki wa dunia, vipande vingi vyenye kani nyingi hunaswa na kuvutwa kuelekea ncha za dunia. Kisha zinagongana na molekuli za nitrojeni na atomu za oksijeni, zikizichochea na kutendesha wonyesho wa nuru. Utendaji uo huo hutokea unapowasha taa za neoni.

Nyakati nyingine huonekana kana kwamba wonyesho wa aurora hukaribia kufika ardhini. Hata hivyo, utendaji huo wa kiajabu hutendeka tu katikati ya kilometa 100 na 1,000 juu ya dunia. Migongano ya karibu hutokeza rangi za kimanjano na kijani, ilhali migongano ya mbali hutokeza rangi nyekundu na buluu. Wonyesho mwingine huwa mkubwa—kutokea kilometa 3 hadi 5 na kuwa zaidi ya kilometa 160 kuelekea juu—kihalisi ukifikia umbali wa maelfu ya kilometa.

Tunaweza Kuziona Wapi, na Zinafananaje?

Kwa ubaya, ni asilimia kidogo sana ya wakazi wa dunia watakaopata kuona aurora maishani mwao. Haijulikani kabisa kwa watu wanaoishi katika nchi za tropiki. Hata hivyo, kama unaishi katika sehemu ya kusini ya Greenland, Aisilandi, sehemu za kaskazini za Norway, au kaskazini mwa Alaska, aurora hucheza mara nyingi kama usiku 240 kwa mwaka. Kaskazini mwa Siberia na Kanada ya kati huziona karibu usiku 100 kwa mwaka, ilhali wakazi wa kusini mwa Alaska waziona kwa karibu masiku 5 kwa mwaka. Meksiko ya kati yaweza kuona wonyesho mara moja kwa mwongo mmoja. Katika Kizio cha Kusini, nuru hizo zenye kucheza, zikiitwa aurora australis, hutoa wonyesho wao hasa kwa sili, nyangumi, na penguini kwa kuwa hakuna watu huko. Hata hivyo, New Zealand, sehemu za Australia, na Argentina ziko ndani ya eneo la aurora lisilokaliwa na watu wengi na hivyo huona wonyesho huo wa kimbingu.

Anga la usiku lenye kutakata huandaa mandhari bora kabisa kwa wonyesho unaobadilika-badilika wa umbo la pazia, mizingo ya duara, na maporomoko ya maji yanayoenda kama wimbi na kuyumba-yumba kuvuka mbingu. Ukanda usioonekana kwa macho, unaozunguka ncha za kisumaku za kaskazini na kusini, mahali fulani kati ya latitudo za digrii 55 na 75, huonekana kuwa mahali ambapo nuru hizo huonekana kuangaza zaidi. Mvumbuzi wa ncha za dunia William H. Hooper akiri hivi: “Lugha itajaribu bila kufanikiwa kufafanua hali zake mbalimbali zenye uzuri wa ajabu; hakuna kalamu wala pensili iwezayo kuandika rangi zayo za kubadilika-badilika, uangavu wayo, na utukufu wayo.”

Je! Waweza Kweli Kuzisikia?

Ingawa wanasayansi hawajakataa uwezekano wa kutokezwa kwa sauti kutokana na wonyesho wa aurora, haijulikani vizuri jinsi msukosuko wa kutambuliwa waweza kutokea kwenye wonyesho wenyewe. Tukio hilo la ajabu hutukia mbali sana kutoka duniani. Sauti huchukua karibu sekunde tatu kusafiri kilometa, kwa hiyo kelele ingeonekana ikija baada ya mmweko halisi.

Kwa kupendeza, wakati wa aurora moja nyangavu, mtu mmoja alifungwa macho, na “kwa karibu kila mmweko mwangavu wa nuru ya aurora, alisema kwa sauti, ‘Hamwisikii?’” Mwastronomia mmoja asiye stadi alisema hivi: “Ilisikika kama selofane na mvuke. Ilikuwa mojapo nyakati zenye hofu ya kicho maishani mwangu.” Mkazi wa Inuit kutoka Fort Chimo, Ungava, Kanada, aliulizwa asimulie kile alichosikia katika usiku mmoja uliotakata alipokuwa akienda nyumbani pamoja mbwa zake. “Hizo [aurora] zilitoa sauti ya whoo-o-o-sh, whish- whoo-o-o-sh, kama hiyo. Haukuwa upepo. Usiku ulikuwa mwanana sana. . . . Na mbwa waliogopa. Walitawanyika kila upande, waliogopa sana.”

Je! sauti hizo ni za kuwaziwa tu—sauti zinazotokea akilini? Watu fulani hufikiri hivyo. Hata hivyo, mwanasayansi William Petrie katika kitabu chake Keoeeit—The Story of the Aurora Borealis atoa maelezo yanayoweza kutokea. Yeye atoa sababu hivi: “Swichi ya taa yenye kasoro yaweza kufanyiza sauti ndogo nyembamba au sauti ya kutatarika wakati kani za umeme zinapotoka nje badala ya kufuata njia ya kawaida ndani ya swichi. Na kwa sababu wonyesho wa aurora ni tokeo la vipande vyenye umeme kuingia katika anga, mtu anaweza kutazamia hali za umeme karibu na uso wa dunia zibadilike. Hivi karibuni, imetambulika kwamba hali hubadilika sana, matokeo yakiwa kwamba kani za umeme ‘huenda’ nje ya uso wa dunia, na kwa kufanya hivyo, inawezekana kwamba hutoa sauti ndogo.”

Ni yenye nguvu kadiri gani? Jarida Aurora Borealis—The Amazing Northern Lights la Alaska Geographic linalotokea mara nne kwa mwaka na lililotangazwa katika 1979, laripoti kwamba “nguvu za umeme zinazohusika na kani za aurora ni nyingi sana, karibu kipimo cha wati bilioni 1,000, au kwa mwaka mmoja saa za kilowati bilioni 9,000—inayoshinda matumizi ya sasa ya mwaka mmoja ya U.S., ambayo ni chini kidogo ya saa za kilowati bilioni 1,000!” Aurora hutoa mawimbi yanayoitwa kelele ya redio inayoweza kunaswa na mapokezi ya redio lakini bila kusikiwa na wanadamu. Kwa uzuri anga-iono hutukinga kutokana na kelele hiyo, kwa hiyo twaweza kutumia redio bila kusumbuliwa na kelele za aurora.

Dhoruba kali za aurora zimepata kukatiza njia ya mawasiliano za kibiashara. Katika pindi moja milio ya simu isiyo ya adabu ilihitilafiana na muziki mzuri uliokuwa ukitangazwa na kituo cha redio. Pindi moja mabomba ya Trans-Alaska Pipeline yalipata kuwa na kani za umeme zenye kipimo cha ampea 100 kwa sababu ya aurora. Hata mifumo ya rada imepata kudanganywa ikaripoti mashambulizi ya makombora ya kinyukilia. Wonyesho mmoja mkubwa sana juu ya Amerika Kaskazini katika 1941 unaripotiwa kuwa uliwaamsha shakwe katika ufuko wa Toronto, Kanada.

Uvutio Wenye Kudumu

Edward Ellis, mjasiri na mwandikaji wa karne ya 19, alilazimika kusema haya kwa kuona aurora borealis: “Namsikitikia mtu asemaye, ‘Hakuna Mungu,’ au asiyeweza kuguswa kwa kina kabisa cha nafsi yake kwa maonyesho hayo yenye nguvu nyingi ajabu.” Kushuhudia vipandaji hivyo vya kifumbo vya pepo za kimbingu kwa mara ya kwanza hutokeza mawazo ya sifa bora mno, kama ajabu ya kutisha! bora ajabu! yenye fahari! Tukio hilo huvutia sana hivi kwamba watu kutoka sehemu za mbali kama Japani hukodisha ndege za kwenda Yellowknife, Maeneo ya Kaskazini-Magharibi, Kanada, ili kuona tu nuru za kaskazini. Mkazi mmoja wa hapo alisema hivi juu ya kikundi kama hicho: “Wengine wao walilia baadaye, walifikiri ilikuwa nzuri mno.”

Kwa kweli, ni kazi ya Mbuni Mkuu wetu iwezayo kugusa hisia zetu kwa njia nzuri sana kama hiyo. Ni kama vile mtunga-zaburi alivyosukumwa kuandika: “Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu; na anga laitangaza kazi ya mikono yake.”—Zaburi 19:1.

[Sanduku katika ukurasa wa 26]

Aurora Borealis Hekaya na Shirikina

Kwa vizazi vingi tamaduni za kaskazini ziliamini aurora kuwa:

“Tochi zilizoshikwa mikononi mwa roho ili kuelekeza nafsi za wale waliotoka tu kufa kwenye furaha na utele”

“Roho za wafu zikicheza mpira na kichwa cha mnyama walrasi”

“Ishara mbaya ya vita na ugonjwa wa kipuku”

“Mizuka ya maadui wao waliouawa”

Ishara ya kwamba “hali-hewa ingebadilika iwe mbaya zaidi”

“Mioto ambayo waganga wakuu na mashujaa wa vita . . . walichemsha polepole maadui wao waliokufa katika vyungu vikubwa sana”

“Nyoka anayetoa mnururisho akicheza angani”

“Roho za watoto waliokufa wakati wa kuzaliwa”

“Zenye kusaidia katika kutibu maradhi ya moyo”

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]

Picha ya NASA

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki